MUNGU ANATAFUTA MTU WA KUSIMAMA MAHALI PALIPOBOMOKA APATENGENEZE

 Na: Patrick Sanga

2

Biblia katika kitabu cha Ezekieli 22:30 inasema ‘Nami NIKATAFUTA MTU miongoni mwao, ATAKAYELITENGENEZA BOMA, na KUSIMAMA mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu’. Ukisoma fungu zima katika kitabu cha Ezekieli 22:23-31, utaona kwamba uasi uliolifikisha taifa katika hali hii ulitokana na mambo manne;

Moja kulikuwa na fitina ya manabii ambapo walitwaa kwa nguvu mali za watu, walitoa nabii za uongo na kufunika dhambi. Pili ni dhambi ya makuhani ambapo walihalifu sheria ya Mungu, kunajisi hekalu la Mungu na kutofundisha watu kweli juu ya masuala mbalimbali ya kiroho.  Tatu ni dhambi ya watawala ambapo walimwaga damu, kujipatia faida zisizo halali na kuharibu roho za watu. Na mwisho (nne) ni dhambi ya watu wa nchi ambapo walifanya udhalimu, unyang’anyi, jeuri na uonevu juu ya maskini na wageni.

Kwa nini ilimlazimu Mungu atafute MTU kwanza na si kupiga moja kwa moja licha ya uovu mkuu kiasi hiki?. Hili ndilo swali ambalo nilikuwa nikijiuliza mara kwa mara kila ninaposoma andiko hili. Katika kuendelea kujifunza na kutafakari ndipo BWANA akanionyesha jambao lifuatalo kama jibu la swali hili muhimu.

Katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana 5:10 imeandikwa ‘ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi’. Naam andiko hili linatujulisha kwamba, Mungu kwa hiari yake ameweka utaratibu kwamba mtu mwenye mwili awe kuhani na mfame juu ya nchi, na kwa hiyo KIMSINGI maamuzi ya mwisho juu ya nini kifanyike juu ya nchi/familia/kanisa yapo kwa mtu akitokea kwenye nafasi ya Mfalme na kuhani kwa Mungu wake.

3

Tuone mfano wa Musa, kitabu cha Kutoka sura ya 32 kinaeleza uamuzi wa wana wa Israeli kutengeneza ndama kama mungu wao baada ya Musa kukawia kushuka kutoka mlimani, naam walifanya hivyo na jambo hilo likawa chukizo kubwa kwa Mungu. Ndipo Mungu akamwambia Musa katika Kutoka 32:10 akisema ‘Basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao…’ Je umeaona maneno haya “Basi sasa niache”?. Maneno haya kwenye tafsiri za kingereza yameandikwa ‘Let me alone, don’t try to stop me, do not get in my way’.

Maneno haya yanatuonyesha kwamba, Musa kama Mfalme na Kuhani alikuwa ndiyo mwenye mamlaka na watu wa eneo lake na hivyo ilimbidi Mungu kuwasiliana naye kwanza kabla ya kutekeleza uamuzi wake. Hivyo basi ndiyo maana wakati wa nabii Ezekieli, Mungu alitafuta mtu, Ili mtu kutoka kwenye nafasi ya Mfalme na Kuhani asimame mahali palipobomoka kupatengeneza.

Naam, hata sasa, Mungu anatafuta mtu mwenye kusimama mahala palipobomoka ili kupatengeneza. Yapo maeneo mengi katika nchi, kanisa, familia, ndoa, koo nk ambayo yameharibika na hayana budi kutengenezwa. Je ni mtu wa namna gani Mungu anamtafuta?

  • MWENYE KUDUMU KULITUNZA NENO LAKE NA KUTOKULIKANA JINA LAKE Katika Ufunuo wa Yohana 3:8 imeandikwa ‘Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu’. Mungu anatafuta mtu ambaye ANADUMU KULITUNZA NENO LAKE NA KUTOKULIKANA JINA LAKE bila kujali anapita katika mazingira ya namna gani. Naam mtu mwenye kutenda haya yupo tayari kusimama na kutengeneza mahali palipobomoka (Wafilipi 4:11-13 na Matendo ya Mitume 4:9-19).

 

  • MTU MWAMINIFU TENA MWENYE AKILI – Matahyo 24:45 inasema ‘Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo’. Hivyo Mungu anatafuta mtu MWAMINIFU katika kutekeleza wajibu/wito/kusudi alilompa hapa duniani (Waruni 8:28). Naam si tu kutekeleza wajibu husika bali zaidi autekeleze kwa nyakati (majira) za Mungu na si kama atakavyo yeye (mtu). Je, umepewa kufanya nini hapa duniani? Je umekuwa mwamnifu katika hilo ulilopewa? Mungu amekupa nafasi zipi katika mwili wa Kristo (kanisa)? Katika nafasi hizo, je umekuwa mwaminifu?

 

  • ALIYE TAYARI KUJIFUNZA NA KUBADILIKA – Katika Ezekieli 23:11 imeandikwa    ‘Na umbu lake, Oholiba, akayaona hayo walakini alizidi kuharibika kuliko yeye, kwa kupendelea kwake, na kwa uzinzi wake, uliokuwa mwingi kuliko uzinzi wa umbu lake’. Hivyo Mungu ANATAFUTA mtu ambaye YUKO TAYARI KUJIFUNZA NA KUBADILIKA kutokana na makosa ya wengine waliomtangulia au waliotangulia. Kutoka 32:9 inasema ‘… Mimi nimewaona watu hawa, na tazama ni watu wenye SHINGO NGUMU’. Tukumbuke kwamba katika Waebrania 10:26 imeandikwa ‘Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi’. Mtu asiye tayari kubadilika hawezi kusimama mahali palipobomoka apatengeneze.

 

  • MWENYE KUMPENDA MUNGU – Katika Warumi 8:28 imeandikwa ‘Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake’. Hivyo Mungu anatafuta mtu ANAYEMPENDA kwa moyo wake wote, akili zake zote, roho yake yote na nguvu zake zote. Je unampenda Mungu kwa kiwango gani?. Na mtu mwenye kumpenda Mungu huzishika ammri zake na hujibiidisha katika kutaka kmujua zaidi Mungu (Ayubu 22:21). Ni vizuri ukafahamu kwamba mtu mwenye kumpenda na kumjua sana Mungu; ni mnyenyekevu, mtunzaji siri, mwenye kusamehe, hadharau wengine na wala hawezi kufurahia mapungufu au kufeli kwa wengine bali atafanya kila awezalo kuwasaidia.

7

Mkumbuke BWANA wetu Yesu Kristo jinsi alivyotupenda ingawa hatukustahili (Yohana 3:16). Kutokana na upendo wake alichukua uamuzi wa kusimama mahali palipobomoka na kupatengeneza ili kurejesha tena uhusiano ulioharibika kati ya mtu na Mungu kwa sababu ya dhambi.  

Hitimisho

Mpenzi msomaj, Je Mungu anaweza kukuamini kiasi cha kukushirikisha agano lake na mawazo yake? Rejea (1 Wakorinto 2:9). Hata sasa Mungu anatafuta mtu mwenye kusimama mahala palipobomoka ili kupatengeneza. Je Mungu anapokutafuta na kukupima katika maeneo haya tuliyojifunza anaona nini ndani yako? Uharibifu au uponyaji? maamuzi ya mwisho kuhusu nchi yako, kanisa lako, ndoa yako, watoto wako, ukoo wako, wazazi wako nk yapo kwako kutoka kwenye nafasi ya mfalme na kuhani kwa mungu. Hivyo Kumbuka siku zote kusimama mahali palipobomoka kama kuhani na mfalme upatengeneze, ili Mungu akitaka kupiga akute umesha simamama mahali husika unaendelea na matengenezo.

 

Neema ya BWANA wetu Yesu Kristo iwe nanyi.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu.

 

20 comments

  1. Napenda sana kuutafuta uso wa bwana…nimefurahi sana endelea kutufundisha zaidi;ili tuweze kusimama kwenye nafasi zetu.

    Like

  2. Mtumishi wa Mungu ubarikiwe mno..
    nabarikiwa sana na masomo unayoyaandika…Hakika Mungu azidi kukutumia na kuinua huduma yako maradufu ili uzidi kuwa msaada na kuinua misingi ya vizazi vingi.

    Like

Leave a comment