Archive for April 2015

MAMBO YA KUMSAIDIA KIJANA ALIYEOKOKA AISHI MAISHA YENYE USHUHUDA MZURI

April 16, 2015

AuthorsNa: Patrick S. Sanga

 

Mtume Paulo katika waraka wake kwa Timotheo anamwambia hivi, ‘Mtu awaye yote ASIUDHARAU ujana wako, bali uwe KIELELEZO kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi. JITUNZE nafsi yako, na mafundisho yako. DUMU katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo UTAJIOKOA NAFSI YAKO NA WALE WAKUSIKIAO PIA’ (1Timotheo 4:12 & 14).

Sentensi hizi zinatuonyesha kwamba kijana yeyote ambaye amefanya uamuzi wa kuokoka, kwa hakika amefanya maamuzi ambayo yanamtaka amaanishe katika kumfuata kwake Yesu au kuuishi wakovu wake. Pamoja na kumpa Yesu maisha yake ni lazima kijana afanye maamuzi ya kuishi maisha ya kudumu kumpendeza Mungu kwa kuzikubali gharama zinazohusiana na wokovu aliouchagua na si kuishi maisha yenye kupelekea jina la BWANA kutukanwa kama ilivyo kwa baadhi ya vijana wengi leo.

Ukisoma mstari huu wa 1Timotheo 4:14 kwenye toleo la kiingereza la ESV unasemaKeep a close watch on yourself and on the teaching. Persist in this, for by so doing you will save both yourself and your hearers’. Kwa mujibu wa dictionary ya kigiriki na kiebrania neno ‘save’ lina maana ya kuweka huru (deliver), kulinda (protect), kuponya (heal), kutunza (preserve), kuokoa (save). Jambo muhimu ambalo Mtume Paulo alikuwa akilisisitiza hapa ni hili; jambo muhimu si tu kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wako, bali kila mwamini ana kazi kubwa ya kufanya ili KUULINDA NA KUUTUNZA WOKOVU WAKE.

Moja ya changamoto kubwa sana ambazo zinawakabili vijana wengi waliokoka leo ni kuipenda dunia. Kuipenda dunia kumekuwa tanzi kwa vijana wengi na kwa sababu ya kuipenda dunia; (a) Mahusiano ya vijana wengi na Mungu wao yameharibika (b) Maisha ya vijana wengi yamekosa uelekeo (c) Kutokana na uovu wao jina la Bwana Yesu limekuwa likitukanwa.

4

Katika kile kitabu cha 1Yohana 2:16 ni dhahiri kwamba dunia imejaa TAMAA YA MWILI, TAMAA YA MACHO NA KISHA KIBURI CHA UZIMA. Tamaa ina nguvu ya kuvuta pamoja na kudanganya, naam inamuingiza mtu kwenye jaribu. Hii ina maana tamaa ni mlango, naam mlango huu unapaswa kufungwa mapema usikupoteze. Hebu tujifunze kutokana na anguko la mfalme Daudi na mke wa Bathssheba (Samweli 11:1-2). Tunaona anguko la Daudi lilisaabishwa na kumpa Ibilisi nafasi kwa kutokwenda vitani. Mkristo akipoa katika kuvipiga vita vya kiroho inakuwa rahisi kwake kuanguka dhambini             (Yakobo 1:14-15), naam kumbuka kwamba siku zote tamaa inalenga kumfurahisha mtu binafsi (self-pleasing) bila kujali matokeo yake.

Hivyo katika nyakati tulizonazo sasa suala la kuipenda dunia ni lazima litafutiwe ufumbuzi wa kudumu miongoni mwa vijana wetu. Ujumbe huu mfupi unalenga kueleza kwa namna gani kuipenda dunia kumekuwa tanzi kwa vijana na nini vijana wafanye ili kuikabili na kuishinda changamoto husika.

Pia katika waraka 2Timotheo 2:15 Mtume Paulo anaendelea kumwambia kijana Timotheo Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli’.

Pengine kila mmoja wetu atafakari maisha yake kwa kuhusianisha na maelekezo ya Paulo kwa Timotheo. Naomba jiulize na kujijibu kwa uaminifu kwamba mosi, je, ujana wako wako unaheshimika au unadharauliwa? Pili, je, kwa waamini wenzako umekuwa kielelezo cha kweli kwa habari ya imani, upendo, usafi, usemi na mwenendo au la?

DSCF0028

Binafsi  nimekuwa nikijiuliza ni kwa namna gani kijana atahakikisha kwamba (a) Ujana wake haudharauliwi (b) Anakuwa kielelezo kwa waamini wenzake (c) Anathibitisha kwamba kweli amekubaliwa na Mungu. Naam katika kusoma na kutafakari neno la Mungu nimejifunza kwamba zifuatazo ni njia ambazo zitatusaidia sisi vijana wa leo kuifikia kweli hii ya neno la Mungu.

 • Kijana adumu katika kuomba na kusoma (kutafakari + kulitenda) neno la Mungu

Katika Zaburi 119:9 & 11 Biblia inasema ‘Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii AKILIFUATA neno lako’. Pia kwenye ule mstari wa 11 inasema ‘moyoni mwangu nimeliweka neno lako, NISIJE NIKAKUTENDA DHAMBI’.

Naam katika Mathayo 26:41 imeandikwa ‘Kesheni, mwombe, MSIJE mkaingia majaribuni; roho I radhi, lakini mwili ni dhaifu’. Yohana 17:17 inasema ‘uwatakase kwa ile kweli ;neno lako ndiyo kweli. Mambo haya mawili yanapaswa kwenda kwa pamoja nakijana akidumu katika kuomba na kusoma neno la Mungu ushindi ni lazima.

 • Kijana asimpe Ibilisi nafasi.

Kijana anapaswa kujiuepusha na mazingira yenye kumfanya aiepende na kuifuatisha namna ya dunia hii. Katika kitabu cha 1Wakorinto 6:12 imeandikwa ‘Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote VIFAAVYO; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya UWEZO wa kitu chochote’.  Ni vizuri ukahakikisha kwamba ufahamu wako hautawaliwi na mambo yasiyo ya msingi (non-essentials of life) – Je ufahamu wako umetawaliwa ni nini?

Hii ndiyo sababu iliyomfanya Paulo awaambie Waefeso ‘Wala msimpe Ibilisi nafasi’ (Waefeso 4:27) na pia awaambie Warumi “Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili hata kuwasha tamaa zake’. Toleo la KJV linasema ‘But put ye on the Lord Jesus Christ, and MAKE NOT PROVISION for the flesh, to fulfill the lusts thereof’.  Na toleo la ESV linasema ‘But put on the Lord Jesus Christ, AND MAKE NO PROVISION FOR THE FLESH, TO GRATIFY ITS DESIRES’ (Warumi 13:14)Je hivi leo ni kwa namna gani vijana wanaungalia mwili na kumpa Ibilisi nafasi? – Mitandao ya kijamii, kuangalia na kusoma vitu vichafu, hasira, mawazo, mazingira.

Mfano wa Vijana

 • Kijana azikimbie tamaa za ujanani

Katika 2Timotheo 2:22 imeandikwa ‘LAKINI ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi’. Kijana anawezaje kuzikimbia tama za ujanani? Hebu tuangalie mfano wa Yusufu. Ushindi wa Yusufu dhidi ya mke wa Uria (Mwanzo 39:2-9). Hii ni habari ya kijana Yusufu ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa mali za Potifa.

Pamoja na ushawishi aliokutana nao Yusufu alijibu kwamba ‘Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?’ Mwanzo 39:12 inasema ‘huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake akakimbia akatoka nje. Ili kuzikimbia tamaa za ujanani kijana anapswa (a) ajiepushe na mazingira/marafiki wabaya (Mithali 1:10 & 1Wakorinto 15:33) (b) Ajitenge na uovu (Mithali 16:17, Zaburi 1:1).

Ni muhimu ukakumbuka kwamba hukupewa mwili kwa ajili ya zinaa maana miili yenu ni ni viungo vya Kristo na tena hekalu la Roho Mtakatifu (1 Wakorinto 6:15 & 19), tena yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye (1 Wakorinto 6:17) maana tena imeandikwa ‘Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili’ (1Wakorinto 6:13b). Tena imeandikwa ‘Lakini uasherati USITAJWE kwenu kamwe, wala uchafu wowote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu’   (Waefeso 5:3).

 • Kijana ajifunze kuenenda kwa roho na si kwa mwili

Katika wagalatia 5:16 imeandikwa ‘Basi nasema ENENDENI KWA ROHO, wala HAMTATIMIZA kamwe TAMAA ZA MWILI. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayoyataka’.

Je kuenenda kwa Roho ndio kukoje?

Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, ATAWAONGOZA awatie kwenye kweli yote (Yohana 16:13) na pia imeandikwa ‘kwa kuwa wote WANAOONGOZWA na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu’ (Warumi 8:14). Kuenenda kwa Roho ina maana ya kuishi kwa kufuata utaratibu/uongozi wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yako (Warumi 8:2).

Naam kadri unavyokuwa mtiifu kufuata utaratibu wake ndivyo unavyokuwa mbali na sheria ya dhambi na mauti ambayo ni mwili. Kumbuka imeandikwa ‘kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waiufuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa nia mwili ni mauti bali nia ya roho ni uzima na amani (Warumi 8:5-6) na pia Wafilipi 4:8.

2

Naam imeandikwa ‘Kila mmoja wenu ajue KUUWEZA MWILI wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama mataifa wasiomjua Mungu. Maana Mungu HAKUTUITIA UCHAFU, bali tuwe katika utakaso’ (1Thesalonike 4:4-5, 7). Ni jambo la ajabu sana kwamba kwamba tumepewa fursa ya kuiweza miili yetu. Ndio tunapaswa kuuweza mwili kwa maana ya kuudhibiti kwa kuuongoza na kuufanya ufuate nia ya roho.

Kijana mwenzangu kama umechagua kumpa Yesu maisha yako kwa njia ya wokovu,  nakusihi na kukushauri zingatia haya ili kuwa na maisha yenye kielelezo na ushuhuda mzuri maana imeandikwa  ‘Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa’ (2Petro 2:20-21).

Neema ya Kristo iwe nanyi, na tuzidi kuombeana.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA.

 

NAMNA YA KUSIKIA NA KUIELEWA SAUTI YA MUNGU ILI IKUSAIDIE KATIKA KUFANYA MAAMUZI (Sehemu ya 2)

April 8, 2015

Na: Patrick Sanga

1

Mada: Mambo mhumu kujua kuhusu sauti ya Mungu

Katika sehemu ya kwanza ya ujumbe huu niliandika kuhusu mambo matatu ambayo ni kujenga mahusiano na Roho Mtakatifu, kuongeza ufahamu wako kuhusu alama za mawasilano na tatu ujue namna ya kutofautisha sauti ya Mungu na isiyo ya Mungu. Ili kusoma sehemu ya kwanza bonyeza link hii  https://sanga.wordpress.com/2015/04/02/namna-ya-kusikia-na-kuielewa-sauti-ya-mungu-ili-ikusaide-katika-kufanya-maamuzi-sehemu-ya-1/ Sasa fuatana nami tuendelee na mabo mengine muhimu kujua:

 • Vifahamu vikwazo vinavyopelekea kutokusikia sauti ya Mungu

Biblia imeainisha vikwazo kadhaa vyenye kupelekea mtu kutokuisika sauti ya Mungu. Vikwazo hivyo ni pamoja na moja kutenda dhambi au kuishi maisha ya dhambi (Isaya 59: 1-2), pili kukosa uaminifu (Hesabu 12:7-8, 1 Samweli 2:35). Biblia katika Isaya 59: 1-2 inasema ‘Lakini maovu yenu, yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia’ Pia katika Hesabu 12:7-8 imeandikwa ‘Sivyo ilivyo kwa mtumshi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si mafumbo.

2

 • Ongeza ufahamu wako kuhusu njia anazotumia Mungu kuzungumza

Ni dhahiri kwamba zipo njia mbalimbali ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu. Namna Mungu anavyosema na huyu sivyo atakavyosema namtu mwingine. Tofauti hizi zipo tegemeana na mahusainao yaliyopo kati ya Mtu na Mungu na pia ngazi ya kiroho aliyonayo mtu katika ulimwengu wa roho. Hivyo ni muhimu sana kuwa na uelewa wa hizi njia mbalimbali ili kuelewa mazingira yake na hivyo kutafuta kumsika Mungu kupitia njia hizo ili kudumisha mahusiano na mawasiliano yako na Mungu. Katika sehemu ya tatu ya somo hili nitaanza kufundisha njia husika hivyo naamini ufahamu wako utaongezeka.

 • Unahitaji kufahamu umuhimu wa Mungu kuzungumza/kusema nawe

5

Zipo sababu nyingi za Mungu kuzungumza na wanadamu laikini kubwa yenye kuzibeba zote ni ile iliyoandikwa katika Zaburi 32:8 kwamba ‘Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama’. Ni muhimu ukakumbuka kwamba kwa mujibu wa Wayumi 8:28 umeitwa ili kulitumika kusudi la Mungu katika siku zako. Ili uweze kulitumika ipasavyo sharti akuongoze katika njia sahihi. Naam njia mojawapo ya kukuongoza na kukufundisha ni kwa yeye kusema na wewe.

Lengo lake katika kusema na wewe ni kukuongoza katika njia sahihi kwa kukuondoa kwenye makusudi ambayo yapo nje na mapenzi yake kwenye maisha yako maana imeandikwa ‘Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam hata mara ya pili ajapokuwa mtu hajali, ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi’ (Ayubu 33:14, 17).

 • Ongeza ufahamu wako kuhusu ulimwengu wa roho

Mambo yote yanayotokea katika ulimwengu wa mwili yameanzia katika uilimwengu wa roho, naam maamuzi ya kile ambacho hutokea katika ulimwengu wa mwili hufanyika katika ulimwengu wa roho. Zaidi hata mapambano (vita vya kiroho) yote aliyoanayo mwamini katika kulitumikia kusudi la Mungu hufanyika katika ulimwengu wa roho.

Hivyo kuwa na ufahamu wa ulimwengu wa roho hususani namna ya kuishi na  kuwasiliana katika ulimwengu huo ni muhimu sana kwa mwamini mwenye kutafuta kujua na kuisikia sauti/mawazo ya Mungu katika maisha yake kwa kuwa Mungu ni roho kama alivyo na Shetani pia. (Rejea 2 Wafalme 6:8-17 na Waefeso 6:10-12).

3

Mpenzi msomaji usiruhusu yale unayoyapitia au yale ambayo watu /mazingira yanasema juu yako yabadilishe au kuongoza maisha yako, bali tafuta kuijua na kuielewa sauti ya Mungu kwenye maisha yako. Na ndiyo maana somo hili limekuja ili kukusaidia kufika mahala ambapo utaweza kuyatenda mapenzi kamili ya Mungu kwenye maisha yako.

Baada ya kuwa tumeangalia mambo haya saba ambayo ni muhimu kujua kuhusiana na sauti ya Mungu, katika sehemu ya tatu nitaanza kuandika kuhusu njia mbalimbali ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu. Somo litaendelea….

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA.

 

NAMNA YA KUSIKIA NA KUIELEWA SAUTI YA MUNGU ILI IKUSAIDE KATIKA KUFANYA MAAMUZI (Sehemu ya 1)

April 2, 2015

Na: Patrick Sanga

1

Salaam katika jina la Yesu Kristo na heri ya Pasaka mpenzi msomaji.

Je ni kweli Mungu anazungumza na mwanadamu hata sasa? Hili ni moja ya swali ambalo watu wengi wamekuwa wakijiuliza na kukosa majibu muafaka kwani baadhi yao hawaamini kwamba ni kawaida ya Mungu kuzungumza na wanadamu. Kama ilivyokuwa katika agano la kale, agano jipya, naam hata sasa, Mungu ni yeye yule jana na leo na hata milele. Hivyo ni kusudio la ujumbe huu kuongeza ufahamu wako ili uweze kujua ni kwa namna gani Mungu huzungumza na mwanadamu na kisha nini ufanye ili kumuelewa Mungu anapozungumza. Naam fuatana name sasa katika mfululizo huu…

Kwa nini Mungu azungumze/aseme na mwanadamu? – mtu anahitaji kusikia sauti ya Mungu ili; (a) aishi sawasawa na kusudi au mapenzi ya Mungu awapo hapa duniani      (b) kujenga na kudumisha mahusiano/mawasiliano mazuri kati yake na Mungu (c) kuona kama Mungu aonavyo na hivyo kutafsiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni (Rejea Zaburi 32:8, 1Samweli 3:1 na Isaya 55:8).

Mambo mhumu kujua kuhusu sauti ya Mungu

Yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu ya kukusaidia kuijua, kuisikia na kuielewa sauti ya Mungu, nawe hunabudi kuyafahamu na kuyatenda;

 • Jenga na kudumisha mahusiano mazuri na Roho Mtakatifu – Ni vizuri ukafahamu kwamba Roho Mtakatifu yupo duniani sasa akiliongoza kanisa katika kuyatenda mapenzi ya Mungu. Hivyo uwepo wa mahusiano mazuri kati yako na Roho Mtakatifu ndio ufunguo wa mawasilaino mazuri kati yako na Mungu. Biblia katika 1Wakorinto 2:10 inasema ‘Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu… vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu’. Andiko hili linatuonyesha nafasi ya Roho Mtakatifu katika kutusaidia kuisikia sauti ya Mungu. Hivyo jenga na kudumisha uhusiano wako na yeye, itakusaidia sana katika kiujua na kuisikia sauti ya Mungu.

Roho Mtakatifu

 • Ongeza ufahamu wa viashiria (signal) vya mawasiliano kati yako na Mungu                              Ufahamu wa viashiria (signal) za mawasiliano kati yako na Mungu ni wa lazima ili kusikia na kuielewa sauti ya Mungu. Zipo alama mbalimbali kwa kila mwamini ambazo Mungu hutumia katika kusema naye. Biblia katika 1Samweli 3:9 inasema   ‘… Enenda, kalale, itakauwa AKIKUITA, utasema, Nena, BWANA; kwa kuwa mtumishi wako anasikia…’ Jambo ninalotaka ulijue hapa ni kwamba Mungu ana njia nyingi za KUITA, naam anaweza kukuita kwa sauti itokayo kinywani pake au KWA NJIA KUKULETEA ALAMA/VIASHIRIA VYENYE KUKUFANYA UJUE MUNGU ANANIITA. Kama ilivyo kwa jinsi ya kibinadamu anayekuita si lazima aongee, anaweza kutumia alama za mikono au hata maandishi nk, kukuita. Katika kukuita kwa njia ya viashiria/alama Mungu anaweza kuleta nguvu/msisimuko/ubaridi/maumivu fulani kwenye sehemu ya mwili wako au huzuni moyoni mwako kama ishara/kiashiria cha uwepo wake juu yako na hivyo KUTAFUTA/KUTAKA USIKIVU WAKO ILI ASEME NAWE. Hivyo ni lazima uwe na ufahamu na utafute kujua kuhusu alama/namna ya kwako ambayo Mungu hutumia kutafuta usikivu wako.

 

 • Ni lazima ujue kutofautisha sauti ya Mungu na sauti nyingine                                                                           Hili ni muhimu sana kwako kulielewa ili usije ukaipuuza sauti ya Mungu kwa kudhani ni mawazo yako au ni ya Shetani au usije ukatekeleza jambo ukiamini kwamba Mungu amesema nawe kumbe Shetani ndiye alisema nawe. Katika             1 Samweli 3:7 imeandikwa ‘Basi Samweli alikuwa hamjui BWANA bado, na neno la BWANA lilikuwa bado halijafunuliwa kwake’. Andiko hili linatuonyesha makosa aliyofanya kijana Samweli katika kuielewa sauti ya Mungu akiichanganya na babu yake Kuhani Eli. Ni muhimu ukaelewa kwamba Mungu anaweza kusema na wewe hata kama uko katikati ya mkutano wa watu wenye kelele nyingi sana. Hii ni kwa sababu Mungu hatumii mdomo kusema nasi bali anatumia moyo wako kuzungumza. Moyo ndio kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya mtu na Mungu.

2

Ukisoma katika Matendo ya Mitume 12:22 Biblia inasema ‘Watu wakapiga kelele, wakasema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya Mwanadamu’. Kauli hii ya watu ilikuja baada ya Mfalme Herode kuhutubia watu na kutoa maneno makuu. Watu waliamini kwamba ile ilikuwa sauti ya Mungu, kumbe sivyo na matokeo yake Herode alipigwa na Mungu akafa. Tahadhari, kuna wakati mtu/watu/watumishi wanaweza kunena mambo makubwa na watu wakadhani Mungu wa kweli anasema ndani yao, kumbe ni mungu wa dunia hii. Na ndio maana ni muhimu wewe binafsi uongeze ufahamu wako katika kuijua, kuisikia na kuielewa sauti ya Mungu, ili hata mwanadamu akinena unajua kwamba hili limetoka kwa Mungu wa kweli au vinginevyo.

Naam zipo sauti mbalimbali ambazo zote zinalenga kupambana/kuharibu kusudi la Mungu ndani ya mtu, zipo sauti za wanadamu (wazazi, walezi, mwenza wa ndoa, viongozi wa kiroho), ipo sauti ya Shetani kupitia majeshi ya pepo wabaya nk. Ni lazima mwanadamu amjue sana Mungu kiasi cha kuweza kutofautisha sauti hizi. Na namna pekee ya kutofautisha sauti hizi na ile ya Mungu ni kuwa na ufahamu mkubwa wa neno la Mungu kwani Mungu hawezi kukuagiza kutenda jambo lililo kinyume na neno lake.

Photo 3

Katika sehemu inayofuata nitakuonyesha mambo mengine kadhaa kujua na kuyaelewa kabla sijaanza sasa kuandika kuhusu njia ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu. Maombi yako ni muhimu sana.

Kwa mara nyingine heri ya Pasaka na amani ya Kristo iwe nawe. Tutaendelea na sehemu ya pili…

Utukufu na heshima vina wewe Yesu! Wastahili BWANA.