Archive for the ‘Ndoa’ Category

JE, UNAJUA HIYO NDOA UNAYOTAKA KUINGIA INAKUPELEKA WAPI?

June 16, 2017

Na: Patrick Sanga

Mtumishi, ninachohitaji sasa ni mume tu, umri unazidi kwenda na nimeomba ila sioni nikijibiwa, waliojitokeza kutaka kunioa hawamaanishi na sasa nimechoka kusubiri. Hivyo kuanzia sasa mwanaume yoyote atakayekuja haijalishi ameokoka au hajaokoka na hata akiwa mpagani nitakubali kuolewa naye ili na mimi niwe na mume. Hivi ndivyo dada Agnes (siyo jina lake halisi) alivyonieleza baada ya kunipigia simu.

Kimsingi kila ninapotafakari changamoto zilizoko kwenye ndoa, hususani ndoa ambazo zilifungwa bila wahusika kumpa Mungu nafasi awaongoze kupata wenza sahihi, huwa napata mzigo wa kuwaombea vijana (kiume/kike), Mungu awape uvumilivu na kuwaongoza ili wasiingie kwenye ndoa kinyume na mapenzi yake juu yao.

Najua hata sasa wapo vijana wengi wanaopitia changamoto inayofanana na ile ya Agnes. Vijana ambao wamekuwa wakiwaza kukubali kuoa au kuolewa na mtu yoyote atakayekuja bila kujali kwamba mwenza husika ni wa mapenzi ya Mungu au la, na zaidi bila kujua ndoa wanayotaka kuingia itawapeleka wapi.

Hoja ya dada Agnes ilinifanya nitafakari kwa upana sana juu ya pito lake, kisha nikamshauri mambo kadhaa ya kufikiri kabla ya kuchukua uamuzi wake alioukusudia. Ujumbe huu unakuja ili kusaidia kubadilisha mtazamo wako na kukuongoza katika njia ya Bwana unapokutana na changamoto ya aina hii, tafadhali jifunze na kuzingatia mambo yafuatayo;

Huhitaji kuoa yoyote au kuolewa na yoyote – ukisoma Biblia yako vizuri utagundua kwamba mbele za Mungu wewe ni mtu wa thamani na upo duniani kwa kusudi maalum ufalme wake. Hii ina maanisha hauhitaji kupata mwenza yoyote, bali unahitaji kupata mwenza sahihi kwako kati ya wengi waliopo, naam, mwenza ambaye ni wa mapenzi ya Mungu kwako (Zaburi 8:4-6, Yeremia 29:11)

Kinadharia mtu yoyote anaweza kuwa mwenza wako, lakini kinafasi na utumishi wa kusudi la Mungu uliloitiwa, si kila mtu anafaa kuwa mume wako au mke wako, yuko mmoja aliyewazidi wote, ndiye aliyekusudiwa kwa ajili ya nafasi hiyo. Naam kwa Mungu, suala la nani atakuwa mwenza wako wa maisha ni kipaumbele, yeye hutaka kuona unampa nafasi akuongoze kumpata mwenza ambaye kwa huyo mtalitumikia vema kusudi lake (Warumi 8:27, Mithali 19:14, Zaburi 32:8).

Ndoa ni wito unaoleta wajibu na changamoto – kuingia kwenye ndoa ni kuingia kwenye majukumu ambayo yanahitaji uwe na mwenza sahihi mtakayesaidiana naye katika kuyakabili na kuyatatua. Ndoa inafungua milango ya majukumu na changamoto mbalimbali ambazo zinaongeza zile ulizokuwa nazo kabla ya kuoa au kuolewa (Mwanzo 2:20).

Baadhi ya majukumu na changamoto utakazokutana nazo ni za kifamilia, kiuchumi, kimakazi, kihuduma, kikazi, kijamii, kimahusiano na watu wengine nk, naam changamoto ambazo kama huna mwenza sahihi mwenye uwezo wa  kukuvumilia na kuchukuliana nawe katika mapungufu yako, changamoto hizo zitawafikisheni pabaya.

Shetani hupambana kuhakikisha watu wanaoana kinyume na mapenzi ya Mungu – Ndoa inayofungwa katika mapenzi ya Mungu ni pigo kwenye ufalme wa giza maana kupitia ndoa za aina hiyo makusudi ya Mungu hutimilizwa endapo wanandoa hao watasimama kwenye njia ya Bwana. Shetani kwa kujua hilo hupambana kuhakikisha watu wanaoana kinyume na mapenzi ya Mungu kwenye maisha yao.

Sasa jiulize unapofika mahali ukasema yoyote atakayekuja nitamkubali, unajuaje kwamba huyo atakayekuja ni wazo la ufalme wa giza au la? Kumbuka haji kama mbwa mbwitu bali atakuja akiwa amevaa vazi la kondoo. Naam usitafute mwenza wa maisha kwa akili zako au usiwaze kutaka kuoa au kuolewa na yeyote atakayekuja maana itakugharimu sana.

Ndoa hiyo itakupeleka wapi – Kumbuka ndoa ni wito unaokutaka kuwaacha baba na mama yako na kisha kuanzisha maisha mapya (Mwanzo 2:24). Sasa jiulize hiyo ndoa unayotaka kuingia itakupeleka wapi? Je ni maisha ya furaha au majuto? Usisahau kwamba ni mke au mume mmoja tu na hakuna fursa ya kuoa au kuolewa tena hadi kifo kiwatenganishe (Soma biblia vizuri huku ukimuuliza Roho Mtakatifu pale usipoelewa, usidanganywe na wale wanaotafsiri maandiko kwa matakwa yao binafsi).

Tafadhali jiulize, kwenye hiyo ndoa unayotaka kuingia utaishi kwa amani au la? Je unajua mtaishi na huyo mtu kwa muda gani? Je unajua kwamba ndoa inaweza kukuondoa kabisa kwa Mungu hata kukufanya uache huduma/wokovu wako na kuishia pabaya? Je unajua kwamba ndoa ni wito wa mapungufu? Je utaweza kuyabeba mapungufu ya mtu ambaye unataka kufunga naye ndoa bila kujua ni wa mapenzi ya Mungu au la? Wewe unayafahamu mapungufu yako binafsi, je unafikiri huyo mwenza wako ataweza kuchukuliana na mapungufu yako kama si wa mapenzi ya Mungu kwako?

Ni maombi yangu, ujumbe huu ukufikirishe kutafuta uongozi wa Mungu kuhusu mwenza sahihi kwako na si kuamua unavyotaka. Suala sio kuitwa mke au mume wa fulani, ni heri kuchelewa kuoa au kuolewa, kuliko kuingia kwenye ndoa ambayo itakuwa ni tanzi na maumivu kwako. Kumbuka wewe ni thamani, usikubali kuoa yeyote au kuolewa na mwanaume yoyote bali yule wa mapenzi ya Mungu kwako (Asomaye na afahahamu).

 ‘Utukufu na Heshima vina wewe Yesu, Wastahili BWANA’

UHURU WAKO KATIKA KUMTUMIKIA MUNGU, UNATEGEMEA UHUSIANO WAKO NA MWENZI WAKO

December 22, 2011

Na: Patrick Sanga

Biblia katika kitabu cha Mwanzo 2:18 inasema ‘Bwana Mungu akasema, si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye’. Ni kusudi na mpango wa Mungu watu waoe na kuoana. Hii ni kwa sababu kufanikiwa kwa kusudi la Mungu duniani kunategemea ndoa au wanandoa pia. Naam kwa Mungu ni muhimu sana kujua nani anakuwa mwenzi wako wa maisha tegemeana na kusudi lake la kukuumba.

Tunapoenda kufunga mwaka nimesikia ndani kuweka ujumbe huu kwenye blog hii nikiamini utawafaa wengi. Jambo la msingi ambalo nataka ulipate ni kuhusu uhusiano uliopo kati ya ‘uhuru’ wa kumtumikia Mungu na ndoa yako. Pengine si wengi wanaojua umuhimu wa mahusiano mzuri baina yao kama wanandoa na kumtumikia Mungu. Naam ndiyo maana kuna ujumbe huu kwa ajili yako.

Watumishi wengi katika nyakati za leo hawajawapa heshima na nafasi ambayo wenzi wao wanaistahili. Baadhi ya wanaume wameona kupata mke ni sehemu ya kukamilisha sifa za utumishi wao kama wanandoa bila kujua kwa nini ameunganishwa na huyo mwenzi wake. Wengine wamekuwa wakiwapuuza wake au waume zao na bado madhabahuni wanalihubiri neno. Na kuna baadhi yao hawana upendo kwa wake zao, wake nao  si watiifu kwa waume zao, ni watu wa kugombana, wenye uchungu ndani yao nk, naam bila kutengeneza au kumaliza tofauti zao hizo  utawakuta madhabahuni wakihudumu kwa raha kabisa. Je, jambo hili ni sahihi kweli? Je ni jambo la kumpendeza Bwana?

Fahamu kwamba ‘uhuru wako katika kumtumikia Mungu kwenye nafasi aliyokupa katika mwili wake, ipo kwa mwenzi wako wa maisha’. Ilikuwa Desemba 28, 2010, Bwana Yesu aliponifundisha jambo hili. Naam uhuru wako wa kumtumikia Mungu upo kwa mke/mume wako. Hivyo kama mahusiano yako na mwenzi wako si mazuri huwezi kutumika katika mapenzi yake. Naam uhuru wa wewe kusikia na kupokea kutoka kwa Mungu unategemea sana mahusiano yako na mwenzi wako.

Nilipofuatilia tafsiri ya neno hili uhuru (freedom) niligundua zipo tafsiri nyingi lakini nikachukua hizi tatu kwa kuwa zinaendana na ujumbe huu.  Tafsiri moja wapo ya ‘Oxford dictionary’ inasema uhuru ina maana ya ‘special privilege or right of access’.  Na tafsiri ya neno hilo kutoka katika ‘Encarta dictionary’ ni ‘right to use or occupy a space’ na pia tafsiri nyingine ni ‘ease of movement’.

Naam mahusiano yako na mwenzi wako yanapokwa mazuri jambo hili linakupa haki, kibali, nafasi na mpenyo wa kumtumika Mungu katika kiwango alichokusudia na zaidi katika mapenzi yake. Jambo hili linakupa mpenyo wa kusikia, kuhoji na kusemezana na Mungu juu ya kile ambacho anataka uwafundishe watoto wake ama ukiwa madhabahuni, au kwa njia ya kuandika, kushuhudia nk. Naam kwa hiyo mahusiano mazuri kati yako na mwenzi wako ni ufunguo wa wewe kumtumika Mungu.

Si hivyo tu bali mahusiano yako na mwenza wako yanapokuwa mazuri utapata wepesi wa kutembea na kutumika katika kusudi la Mungu. Naam ndivyo unavyopata haki ya kutumia kila ambacho Mungu ameweka ndani yako kwa utukufu wake, naam ndivyo unavyokuwa na nguvu ya utawala kwenye nafasi na eneo lako la utumishi katika ulimwengu wa roho.

Biblia inasema katika 1Petro 3:7 ‘Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe’.

Naamini umeona kile kipengele cha mwisho kinavyosema. Hii ina maana kama mwanaume atashindwa kukaa na mke wake kwa akili na kumpa heshima, maombi yake yatazuiliwa. Sasa fikiri mwanaume huyu ni mtumishi yaani Mchungaji, Mwalimu, Nabii nk nini kitatokea kwa wale anaowachunga au kuwahudumia? Naam mahusiano yako na mwenzi wako ni ya maana sana kama unataka kutumika katika mapenzi ya Mungu. Mahusiano mazuri baina yenu yanaleta mawasiliano mazuri baina yako kama Mtumishi na Mungu wako. Hivyo msingi wa mawasiliano mazuri na Mungu wako, upo kwa mwenzi wako.

Ni vizuri ukafahamu kwamba bila kuwa na mahusinao mazuri na mwenzi wako wa maisha, utumishi wako ni bure. Naam uhuru wako katika kumtumika Mungu unategemea uhusiano wako na mwenzi wako. Si rahisi kwa Mungu kusema na wewe kama mahusiano yako na mwenzi wako si mazuri, matokeo yake utawasikizisha/hubiri/fundisha watu mawazo yako na pengine ya adui, zaidi utahudumu kwa mazoea bila uwepo wa Bwana, au chini ya kiwango cha upako uliokusudiwa, tena ni kwa sababu Mungu anawaonea huruma watu wake.

Jifunze kufanya tathimini ya mahusiano yako na mwenzi wako mara kwa mara, na kuhakikisha unayaboresha, naam jambo hili ni muhimu sana kwenu binafsi na zaidi kwa Mungu ili kupata uhuru wa kusikia kutoka kwake kila wakati kwa ajili yenu na  wale ambao amekupa kuwahudumia.

Nakutakia utumishi mwema katika nafasi yako pamoja na mwenzi wako, mwenzi wako ni wa muhimu sana, mpe nafasi yake, utaona mabadiliko kwenye utumishi wako.

UPONYAJI WA NDOA ZETU

October 28, 2011

 Na: Patrick Sanga

Siku moja mama Allen (hili siyo jina lake halisi) alianza kunishirikisha mambo ya ndoa yake yanavyomtesa. Akaniambia mwanangu hizi ndoa tunapenda tu kuingia bila kujua kilichomo ndani yake. Hivi unavyoniona sina hamu kabisa ya ndoa, maana maisha tunayoishi (ingawa kwa nje watu wanaona tuko pamoja), lakini ukweli ni maisha ya taabu na majuto karibu kila siku.

Tabia ya mume wangu imefika mahali haivumiliki. Nikamuuliza tatizo ni nini hasa? Akasema ni fedha, elimu yake na kutoka nje ya ndoa. Fedha ya mume wangu wanaijua wazazi wake na si wazazi wangu, kwani mara kwa mara yeye hutuma fedha kwa wazazi wake. Inaniuma maana natamani hata mie  wazazi wangu niwatumie fedha pia.

 Mume wangu ni kweli Mungu kamjalia kuwa na elimu ya kutosha, lakini elimu yake imekuwa dharau kwangu nisiye ana elimu kama yake. Maana hunisema kwa sababu ya elimu yangu ndogo, kazi yangu na mshahara wangu mdogo ukilinganisha na wake.  Kubwa na baya Baba Allen sio mwaminifu katika ndoa, sina amani na hasa ukizingatia ugonjwa huu wa ukimwi, nina mashaka makubwa sana ndani yangu.

Nikamuuliza umefanya jitihada gani ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizi za ndoa yako? Akajibu akasema nimeamua kuishi naye kwa kuzikubali tofauti zetu (agree to differ). Kwa lugha nyingine nimekubali kuishi na hali hii, kwamba haya ndiyo maisha yangu ya ndoa chini ya jua. Hivyo imefika mahali sina jingine la kufanya ila kukubali kwamba mwenzangu yuko vile na mimi niko hivi, tutendelea kuishi kwa kutofautina hadi kifi kitutenganishe, kwani jitihada za kujaribu kurekebisha mambo haya zimekwama.

Baada ya kusikia maelezo haya niliumia sana, nikamshauri mambo kadhaa ya kufanya ili kuiponya ndoa yake. Lengo langu la msingi katika kuandika habari za mama Allen ni kujaribu kukufukirisha mwanandoa mwenzangu mambo kadhaa yatakayokusaidia kuiponya ndoa yako pia;

  • Jambo la kwanza – Ndoa ni wito wa upungufu na hivyo suala la uvumilivu ni la lazima.

Si watu wengi wanaojua kwamba ndoa ni wito wa mapungufu pia. Maandiko yanasema ‘ Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja’ (Mwanzo 2:24).

Ni dhahiri kwamba watu wanapooana wanakuwa wametoka katika asili na malezi (background) tofauti hasa kutokana na mazingira waliyokulia. Ile tu kwamba huyu anatoka katika familia hii na huyu ile, fahamu kwamba lazima kutakuwa na tofauti kadhaa katika ndoa hiyo. Naam tofauti zenu ndiyo sehemu ya  mapungufu kwenu kama  wanandoa. kwa sababu wewe ungependa mwenzako awe hivi na yeye kuna vitu ambavyo angependa vibadilike kwako.

Na wala usije ukajiona wewe upo kamili, naam kwa upande wako unaweza kuwa sawa lakini kwa mwenzako, hauko kamili. Ni vizuri ukafahamu kwamba unapoingia kwenye ndoa, utakabilana na mapungufu ya mwenzi wako. Kwa sababu hii suala la uvumilivu, kuchukuliana, kusameheana kwa wanandoa ni la msingi ili kufikia mahala pa kutengeneza tabia au mfumo mpya wa ndoa yenu.

  • Jambo la pili – Haijalishi mwenzi wako anatabia mbaya kiasi gani, Yesu anaweza kumbadilisha.

Jambo la pili ambalo nimeoana vema kusisitiza ni kwamba wewe mama au baba ambaye ndoa yako ipo kwenye misukosuko kama ya mama Allen pengine na kuzidi, usifike mahala pa kukata tamaa na kuamua kuishi kwa kuzikubali tofauti zenu kama sehemu ya maisha. Kwa kufanya hivyo utakuwa unamzuia Roho Mtakatifu kukusaidia kuiponya ndoa yako. Ni lazima kwanza ubadili fikra zako na mtazamo wako kwamba, kwa Mungu hakuna lisilowezekana na hivyo haya si maisha yangu ya ndoa ninayostahili kuyaishi.

Kwa Mungu sisi tu watoto wake. Hakuna Baba mwenye kufurahia kuona maisha ya ndoa ya watoto wake yanakuwa ya majuto. Mungu alipoleta wazo la ndoa ilikuwa ni kwa ajili ya kusudi la ufalme wake na kuwa furaha kwa watoto wake na si majuto. Nasikitika kusema leo, ndoa nyingi zimekuwa ni majuto na si kile Mungu alikiona wakati wa uumbaji hata akasema, kila kitu nilichokifanya ni chema sana (Mwanzo 1:31).

Kwa kilio kilichopo kwenye ndoa hivi sasa ni dhahiri kwamba kuna mahali kama wanandoa tumekosea na kumpa Iblisi nafasi (Waefeso 4:27) hata ameleta majuto kiasi hiki. Ushauri wangu ni kwamba ni vema kila mwanandoa akasimama kwenye nafasi zake (Mwanaume kama kichwa na Mwanamke kama Mlinzi na Msaidizi nk) kwa pamoja tumpinge Shetani naye atatukimbia. Endapo mwenzi wako hayuko tayari kwa hili au hamjui Mungu wako, basi wewe mwenye kujua siri hii kama anza, maana kwa Mungu mtu mmoja natosha kuleta uponyaji wa Taifa, je si zaidi ndoa yako? Naam usikate tamaa, Mungu wetu, ni MUNGU ASYESHINDWA.

 

Bwana Mungu na akusaidie katika kuzikabili changamoto za ndoa yako.

NAJUTA KWA NINI NILIKUBALI KUOLEWA?

August 24, 2011

Na: Patrick Sanga

Baada ya mwaka mmoja wa ndoa, Merian asema anajuta kwa nini alikubali kuolewa. Merian na Joseph (haya siyo majina yao halisi) ni mtu na mumewe. Nikiwa katika Mkoa wao kikazi, niliamua kuwatembela wanandoa hawa. Merian alinipokea na kunikaribisha ndani kwa furaha sana. Tukaanza kuongea nami nikamuuliza, Joseph yupo? Akaniambia bado hajarudi kutoka kazini, hata hivyo kaniambia yupo njiani anakuja.

Tukaanza kuzungumuza mambo kadha wa kadha na kisha nikamuuliza mnaendeleaje na ndoa yenu changa? Baada ya kuwa nimemuliza swali hili akacheka na kisha akaanza kwa kusema, nyie maisha haya ya ndoa yaacheni tu, kwa kweli najuta kwa nini nilikubali kuolewa? Kauli hii ilinishtua sana kwa sababu kwanza sikuitegemea na pia ndoa hii ilikuwa ndio imetoka kutimiza mwaka  wa kwanza tu.

Kwa haraka kabla hajaendelea nikamzuia asiseme hayo maneno tena, maana nilijua kadri anavyosema ndivyo anavyozidi kuumba uharibifu kwenye ndoa yake. Akaniambia usinizuie, si umeuliza tunaendeleaje, subiri nimalize kukuelezea. Ndipo akaanza kuniambia kile kilichompelekea kusema anajuta kwa nini alikubali kuolewa (Kwa ufupi ni changamoto ambazo kwa ujumla naweza kusema za kawaida, hata hivyo sitaweza kuziandika hapa kwa sababu maalum).

Katika maelezo yake Merian aliniambia, vijana wengi sana walinifuata ili kunioa, mie nikawakataa, natamani ningeolewa na yoyote kati ya wale wengine, lakini si hapa nilipo na laiti likitokea lolote sasa (kwa maana ya mwenzake kufa) sitakubali kuolewa tena.

Mpenzi msomaji sijui kama unakiona ninachokushirikisha kupitia maisha ya wanandoa wenzetu hawa. Kumbuka ni mwaka mmoja tu wa ndoa, na leo tunashuhudia Merian akijutia maamuzi yake ya kuolewa na Joseph. Licha ya kwamba ni mwaka wa kwanza tu, lakini wawili hawa wameokoka pia.

Maelezo ya dada Merian yaliniletea maswali matano (5) ndani yangu ambayo ndiyo ninayotaka tujifunze kutoka kwake;

Swali la kwanza; Je! Merian, alijua nini maana ya ndoa kabla ya kuolewa?

Swali la pili: Je, Merian alijua aina ya maamuzi anayotaka kufanya kabla ya kuolewa?

Swali la tatu: Je, Merian alimuhusisha Mungu kabla ya kuolewa ili ampate mwenzi sahihi wa kuishi naye?

Swali la nne: Je, Merian alikuwa amejiandaa/andaliwa kifikra kuishi kama mke?

Swali la tano: Je, mpaka sasa, Merian anajua wajibu wake ni nini kwenye ndoa?

Kutokana na maswali haya niliwaza mambo matatu ambayo, nafikiri kama vijana wangefahamu yatawasaidia katika ndoa zao;

  • Moja, ni vema vijana wajifunze kumshirikisha Mungu awaongoze kupata mwenzi sahihi wa maisha, kabla hawajaingia kwenye hizo ndoa. 
  • Mbili, ni vema vijana wakajifunza kufikiri kimapana kabla ya kuingia kwenye ndoa. Swali la msingi katika kufungua tafakuri hii, ni kwa nini mtu aoe au kuolewa? Ni swali fupi lakini kama wewe ni mtu ambaye hufikiri kimapana swali hili litakujengea msingi mzuri wa baadaye. Naam kile kitabu cha 1 Wakorinto sura nzima ya saba kikuongoze katika tafakuri hii.
  • Tatu, ni vema vijana wangefunzwa/kuandaliwa vya kutosha kuhusu ndoa na hasa wajibu uliopo mbele yao. Endapo kama Serikali inawasomesha watumishi wake kwa lengo la kuwaongezea uwezo na maarifa ya kutekeleza majukumu yao, basi ifike mahali kanisa, wazazi, viongozi wa vijana nk makundi haya yaone umuhimu wa kuwaandaa vijana wao kuyakabili maisha ya ndoa.

Watu wengi hufikiri chanzo cha matatizo kwenye ndoa zao ni Shetani. Ndio hii ni sababu moja, lakini sababu nyingine kubwa, ni watu wengi kukosa ufahamu wa masuala ya ndoa kabla na baada ya kuingia kwenye hizo ndoa. Naam wakati watu wanasema Shetani anaangamiza ndoa zetu, Mungu anasema, ndoa za watoto wangu zinaangamizwa kwa kukosa maarifa (Hosea 4:6).

Ni imani yangu kwamba, kama mambo haya yatazingatiwa, sehemu kubwa ya changamoto ambazo wanandoa wanapitia, zingepata ufumbuzi wa haraka. Natoa wito kwa wadau mbalimbali wa masuala ya ndoa na hasa Wachungaji, Walimu na Viongozi wa makundi ya kiroho, kuanzisha utaratibu wa kuwa na mafunzo maalum kuhusu ndoa, kwa vijana ambao wameweka wazi dhamira zao za kuingia kwenye maisha ya ndoa.

Ni vema pia, hata kwa wale ambao wako ndani ya ndoa, wakawekewa utaratibu wa kuwa na mafunzo ya mara kwa mara, maana kwa mtazamo wangu ndoa ni shule ambayo, wahusika wanapaswa kuongeza (kujifunza) ufahamu wao kila siku, ili kulitumikia vema kusudi la Mungu. 

Bwana Yesu na utusaidie watoto wako, Amen!

JIFUNZE KUFIKIRI KABLA HUJACHUKUA UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA

April 9, 2011

Na: Patrick Samson Sanga

Nawasalimu kwa jina la Yesu . Leo katika nyanja hii ya vijana, nimeona ni vema tukashirikishana kuhusu suala la ‘kufikiri kabla ya kuoa au kuolewa’.

Siku moja katika kusoma Biblia nilikutana na mstari ufuatao, nakusahuri uusome kwa umakini. Biblia katika 1Wakorinto 7:8-9 inasema “Lakini nawaambia wale, wasiooa bado na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo, lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa”.

Baada ya kuusoma mstari huu niliingia katika tafakuri nzito sana ambayo mwishowe ilinipeleka kuandaa somo hili, kwamba ni vema ukafikiri vizuri kabla ya kuchuka uamuzi wa kuoa au kuolewa.

Unajua malezi, dini, madhehebu yetu, wazazi, mila na desturi vinachangia kwa kiwango kikubwa sana kuhusu utaratibu wa kuanzia mtu kupata mke au mume mpaka watakapofunga ndoa. Kila kundi lina mfumo na utaratibu wake ambao lingependa vijana waufuate ili kuhakikisha wanaoa na kuolewa kwa kile ambacho kila kundi linaona na kuamini kwamba huo ndio uataratibu mzuri kufuatwa. 

Namshukuru Mungu kwa kuwa nami nimeoa, ingawa vitu vingi sana Bwana alikuwa ananifundisha vinavyohusu ndoa hata kabla sijaoa. Nakubaliana na dhana kwamba ili uweze kuwa Mwalimu mzuri kwenye nyanja fulani basi ni lazima au ni vema wewe mwenyewe ukawa umepitia kwanza kwenye nyanja hiyo. Lengo ikiwa sio tu ufundishe ‘theory’ bali pia utufundishe na uzoefu wako binafsi kwenye eneo hilo. Licha ya kukubaliana na dhana hii, kwangu binafsi haikuwa hivyo, maana kuna mambo mengi ambayo, Bwana Yesu, alikuwa ananifundisha yanayohusu ndoa hata kabla sijaoa.

Kwa kifupi ndoa ni shule au darasa ambalo wanandoa wanatakiwa kukaa chini na kujifunza kila siku namna ya kuishi humo ndani ili kuweza kuishi maisha ambayo Mungu amewakusudia.

Kutokana na mifumo ya baadhi ya makanisa yetu, si vijana wengi ambao wanafundishwa kwa undani kuhusu maamuzi haya makubwa. Wengi wao wameingia kimwili na kujikuta wakijutia na kulaumu kwa nini nilimuoa au kuolewa na huyu kijana. Nasema haya kwa kuwa nimekutana na wanandoa wengi wa aina hii, na nataka nikuambie kama Biblia ingetoa mwanya wa wanandoa kuachana na kuoa au kuolewa na mtu mwingine, wapendwa wengi sana walioko kwenye ndoa wangefanya hivyo na wengine wasingekubali kuolewa au kuoa tena.

Unajua kwa nini?

Ni kwa sababu si vijana wengi wenye ufahamu wa kutosha juu ya aina ya maamuzi wanayotaka kuyachukua. Kwa hiyo katika somo hili nimeona vema niandike mambo manne ya msingi ambayo naamini yataongeza na kupanua ufahamu wako ili kukusaidia kufikiri kwanza kabla ya kufanya maamuzi haya makubwa;

  • Si kila ndoa inayofungwa imeunganishwa na Mungu, kwa kuwa ndoa ni kiungo cha muhimu kwa Mungu na Shetani pia.

Kuanzia mwaka 2005, Mungu alinipa kibali cha kuanza kufundisha na pia kushauri  juu ya mambo kadhaa kuhusu wanandoa. Tangu wakati huo hadi sasa nimekutana na baadhi ya wanandoa ambao wanajuta kwa nini walikubali kuoa au kuolewa. Wanaishi kwenye ndoa kwa sababu tu ya watoto na pia kwa hofu kwamba endapo kama wataachana jamii na watu wanaowazunguka hawatawaelewa.

Ni vizuri ukafahamu kwamba si kila ndoa inayofungwa ni ya mapenzi ya Mungu, hata kama imefungwa kanisani. Biblia inaposema kilichounganishwa na Mungu, mwanadamu asikitenganishe, katika nafasi ya kwanza maana yake iwe ndoa ambayo Mungu ndiyo aliyehusika katika kuanzisha mahusiano na kuwaongoza hao watu kuishi pamoja. Wakati Mungu anatafuta kuhakikisha watu wake wanaoana katika mapenzi yake na Shetani naye anapambana kuhakikisha watu wanaoana katika hila (mapenzi) zake.

Shetani amefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana kuvuruga wanandoa wengi na kuwafanya waishi maisha tofauti na yale ambayo Mungu aliwakusudia. Ni kwa sababu hii ndio maana Paulo aliwaambia Wakorinto ‘Lakini nawaambia wale, wasiooa bado na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo, lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa’. Paulo aliona shida, maudhi ya wandugu walioko kwenye ndoa tokana na migogoro aliyokuwa akikutana nayo.

Fahamu kwamba ni furaha kubwa kwenye ufalme wa giza mtu anapooa au kuolewa kinyume cha mapenzi ya Mungu. Hii ni kwa sababu Shetani anajua akifanikiwa kukushawishi ukaoa kinyume na mapenzi ya Mungu, ameharibu ‘future’ yako na kile ambacho Mungu alikusudia ukifanye hapa duniani. Kumbuka suala sio kuoa au kuolewa tu, bali ni kuingia kwenye ndoa ambayo itakuwezesha kulitumika shauri la Bwana katika kizazi chako. Hivyo kabla hujaamua nani uishi naye hakikisha unamshirikisha Mungu akuongoze kumpata mwenzi sahihi.

  • Unapaswa kuoa au kulewa katika mapenzi ya Mungu

Naam kuoa au kuolewa katika mapenzi ya Mungu ni changamoto nyingine kubwa kwa vijana wa kizazi cha leo. Naam hili ni eneo ambalo Mungu yupo makini sana kufuatilia nani atakuwa mwenzi wako wa maisha. Na upande wa pili nao, Shetani anapigana kwa juhudi kubwa ili kuvuruga kusudi la Mungu kupitia mtu au watu.

Ni vizuri ukafahamu kwamba unapotaka kufanya maamuzi ya kutaka kuoa au kuolewa, Shetani naye ataleta mawazo (mapenzi) yake ndani yako juu ya nani anafaa zaidi  kuwa mwenzi wako maisha. Lengo lake ni kuhakikisha anakuunganisha na mtu ambaye anajua kwa huyo atakumaliza kiroho na kihuduma kabisa. Suala sio kuwazuia msiende kanisani, bali ni kuhakikisha kile ambacho ungefanya kwa kuwa na mtu sahihi hakifanikiwi. Ukitaka kujua ukweli wa jambo hili, muulize Mchungaji wako, kesi nyingi anazokutana nazo kanisani kwake zinahusu nini, naamini atakujibu kimapana. Ni jukumu lako kuwa makini kufuatilia unatii wazo la nani, Mungu au Shetani?  

  • Vigezo vya kimwili ni silaha kubwa ya uharibifu

Vigezo vya kimwili ni moja ya silaha kubwa ambazo Shetani anazitumia kuwavuruga watu wengi waweze kuoa au kuolewa nje ya mapenzi ya Mungu kwao. Jifunze kufukiri na kutafsiri mambo au makusudi kama Mungu anavyotazama na kutafsiri. Na uwezo wa kufanya hili utaupata kwenye neno lake tu. Kwako mwanaume Mungu anapokupa mke anakupa Mlinzi na msaidizi. Na kwa mwanamke Mungu anakuwa amekupa kichwa. Ni muhimu sana kuchunga ni msaidizi, mlinzi au kichwa gani unataka kiunganishwe na maisha yako kwa njia ya ndoa.

  • Ndoa ni wajibu mkubwa

Ndani ya ndoa kuna wajibu mkubwa sana unaokusubiri kama baba au mama. Ndani ya ndoa muda na uhuru wako unabanwa na mwenzi wako. Ndoa inabana pia muda wa kuwa na Mungu wako. Na kwa wengi kwa kutaka kuwapendeza zaidi waume au wake zao, wamefarakana na Mungu, kwa sababu wamewapa waume au wake zao hata nafasi na muda wa Mungu kwenye maisha yao.

Usiingie ndani ya ndoa kwa fikra za uapnde mmoja. Naam ndoa ni wito wa mapungufu na uvumilivu ambao ni lazima uwe tayari kuchukuliana na mwenzi wako katika mapungufu yake. Kuna vitu hamtaweza kufanana na kwa sababu ya mapungufu yaliyopo kwa kila mmoja  unapaswa kutafakari kuhusu majukumu yanayokuja kwako kama mwanandoa, hekima na busara katika kuzikabili changamoto za ndoa, kama vile kuzaa au kutokuzaa, kutokujiweza katika masuala ya unyumba, matumizi ya fedha, tabia za mwenzi wako nk.

Haya ni mambo ya kuhakikisha unayaombea mapema ili kujenga msingi imara utakapoingia kwenye ndoa yako. Lakini nikutie moyo kwamba endapo utaoa au kuolewa katika mapenzi ya Mungu, yeye ni mwaminifu, atakuunganisha na mtu ambaye katika changamoto mtakazokutana nazo hazitawakwamisha wala kuwafanya mjute. Bali endapo Shetani ndiye ataongoza maamuzi yako, ni majuto makubwa sana (asomaye na afahamu).

Mungu akubariki, naamini ujumbe huu umeongezea mambo ya kutafakari na kuzingatia kabla ya kufanya uamuzi wa kuoa au kuolewa.