Archive for the ‘Mafundisho mbalimbali’ Category

NAMNA UNAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI YA MLINZI KWENYE ULIMWENGU WA ROHO KUFANYA MAOMBI YENYE MATOKEO MAZURI (Sehemu ya 2)

August 5, 2017

Na: Patrick Sanga

Mada: Mambo muhimu kujua na kuzingatia kwa Mlinzi ili maombi yake yawe na mafanikio.

Shalom, katika sehemu ya kwanza tuliangalia tafsiri ya kuwa Mlinzi katika ulimwengu wa roho, ili kusoma sehemu hiyo tafadhali bonyeza link hii  https://sanga.wordpress.com/2017/07/05/namna-unavyoweza-kutumia-nafasi-ya-mlinzi-kwenye-ulimwengu-wa-roho-kufanya-maombi-yenye-matokeo-mazuri-zaidi-sehemu-ya-1/ Kuanzia sehemu hii ya pili kwa neema ya Mungu nitaanza kuandika kuhusu Mambo muhimu kujua na kuzingatia kwa Mlinzi ili maombi yake yawe na mafanikio. Naam fuatana nami tuendelee…

Jambo la kwanza: Jifunze kuutunza utakatifu wako

Biblia katika Mambo ya Walawi 20:26 inasema Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi Bwana ni mtakatifu nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu’. Pia katika 1Petro 1:15 imeandikwa ‘bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; Zaidi katika Waefeso 5:8 imeandikwa ‘Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru’.

Kuwa mtakatifu ni kuishi au kuenenda katika utaratibu wa yeye aliyekuita alivyo. Mlinzi anapaswa aishi maisha ya kutojichafua kwa kujitenga na uovu, asiwe mtu wa maneno mengi na wala asimpe adui nafasi itakayomwondolea utakatifu wake ili kuruhusu mawasiliano mazuri kati yake na Mungu na maombi yake yaweze kujibiwa.

Katika Isaya 59:1-2 Biblia inasema ‘lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia’. Katika Isaya 1:15 imeandikwa ‘Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, MWOMBAPO MAOMBI MENGI, sitasikia; mikono yenu imejaa damu’. Hii ni kutuonyesha kwamba dhambi ni chukizo kubwa mbele za Mungu kiasi cha kumfanya Mungu akatae kusikia na hivyo kujibu maombi (Yohana 9:31).

Mungu anajua kwamba ikiwa watu wake watajifunza kuishi kwa kuongozwa na Roho, agizo la utakatifu linatekelezeka (Wagalatia 5:16-17, 1Yohana 3:3-10), naam katika uaminifu wake BWANA hawezi kutoa maelekezo ambayo hayatekelezeki vinginevyo hakuna atakayemuona (Waebrania 12:14). Swali muhimu ni je kwa nini bado watoto wake wanatenda dhambi? – ni kwa sababu bado hawajamjua jinsi alivyo Mtakatifu, ndiyo maana imeandikwa ‘Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua’ (1Yohana 3:6).

Hivyo lazima watoto wa Mungu wajilinde (kwa kutompa adui nafasi) na kujiepusha wasimtende Mungu wao dhambi, na mwovu hatawagusa (1Yohana 5:18), ikiwa wanataka kuona matokeo mazuri ya maombi yao. Hatuna sababu ya kuomba maombi mengi ambayo tunajua kwamba kwa mujibu wa neno la Mungu hayasikilizwi na hayatajibiwa, tunahitaji kuhakikisha muda wote tunaenenda kama wana wa nuru.

Rejea  Pigo la wana wa Haruni Nadabu na Abihu (Mambo ya Walawi 10:1-11). Katika kitabu cha Kutoka 19:12 imeandikwa Makuhani nao, wamkaribiao Bwana, na wajitakase, Bwana asije akawafurikia’ (Ona pia Isaya 52:11). Neno hili Bwana alilisema lakini watoto wa Haruni hawakulizingatia. Dhambi ya vijana hawa ilipelekea kifo chao wakiwa madhabahuni.

Hili linatufundisha kwamba hali ya muombaji ina nafasi kubwa sana katika kuamua matokeo ya maombi yake. Je, mwombaji anastahili na ujasiri wa kusimama na kuomba mbele za Mungu au la?. Kumbuka utakatifu unaruhusu mawasiliano kati yako na Mungu, wakati dhambi inakata mawasiliano husika. (1Yohana 3:21-22, Waebrania 4:16)

Hata hivyo pamoja na wana Haruni kufa walivyokuwa Haruni na wanawe waliosalia waliagizwa kutotoka nje ya hema ya kukutania na kwenda kushiriki maombolezo, ispokuwa ndugu zao. Hili linatufundisha kwamba haijalishi Mlinzi atakutana na changamoto gani, hatakiwi kuruhusu changamoto hizo zimuondoe kwenye nafasi yake na kuathiri wajibu wake tokana na umuhimu wa nafasi yake na upako ulio juu yake.

Mlinzi anapaswa kuwa mtu wa toba na kujitakasa akihakikisha anatunza mavazi yake yasichafuke (kuwa mtakatifu). Jambo hili litamsaidia kila aombapo ASIHUKUMIWE moyoni na hivyo kuwa na UJASIRI wa kusimama mbele za BWANA na kupata mpenyo unaostahili  kuwasilisha hoja za watu wake.

Somo litaendelea…

Utukufu na Heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA.

NAMNA UNAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI YA MLINZI KWENYE ULIMWENGU WA ROHO KUFANYA MAOMBI YENYE MATOKEO MAZURI ZAIDI (Sehemu ya 1)

July 5, 2017

Na: Patrick Sanga

 

Mada: Tafsiri ya kuwa Mlinzi katika ulimwengu wa roho

Shalom, tunapoanza mwezi huu wa Julai 2017, nimeona ni vema kuanza pia mfululizo wa somo hili muhimu ambalo naamini si tu litabadilisha maisha yako bali litabadilisha na kuomba kwako. Lengo la somo hili ni (a) kuongeza ufahamu wako kuhusu nafasi ya Mlinzi kama Mwombaji (Mwombezi) na mwisho ni (b) Kuboresha mfumo wako wa kuomba uwe na matokeo mazuri zaidi.

Mambo mengi mabaya yanayotokea leo ni matokeo ya walinzi kutojua na kutofanya wajibu wao ipasavyo kwenye nafasi zao katika ulimwengu wa roho. Ukisoma Biblia utaona Mwanadamu amepewa nafasi ya kuwa ‘Mlinzi’ katika nyanja mbalimbali za maisha ili kufanikisha makusudi ya Mungu hapa duniani. Rejea ya Ufunuo wa Yohana 5:10 inatufanya tujue kwamba kila aliyeokoka ni Mlinzi, kinachotutofautisha ni nafasi au maeneo ya ulinzi ambayo tumepewa kuwajibika.

Suala la kuweka ‘walinzi’ katika maeneo mbalimbali ni utaratibu ambao Mungu ameuweka na unatoa uhalali na fursa ya pekee kwa pande zote kuwa karibu kimawasiliano. Naam, kufanikiwa kwa kusudi lake duniani kunategemea nidhamu na utiifu wa ‘walinzi’ wake kwenye nafasi alizowaweka.

Biblia katika Ezekieli 33:7 inasema ‘Basi, wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli, basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu’. Pia ukienda kwenye Isaya 62:6-7 imeandikwa ‘Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Eee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani’.

Maandiko haya yanatufanya tujue kwamba yako makusudi au mambo ambayo Mungu anahitaji kufanya juu ya nchi, miji, kanisa, ofisi, ndoa, mtu au watu nk. Naam ili kuyafanikisha anahitaji ‘Mlinzi au Walinzi’ atakaowatumia kufanikisha makusudi yake. Swali muhimu kujiuliza ni, Je, Mungu anaposema nimekuweka kuwa ‘MLINZI’ wa eneo fulani maana yake nini? Naam katika ulimwengu wa roho, unapowekwa kuwa Mlinzi wa eneo fulani maana yake ni;

  • Umewekwa kuwa Kiongozi wa eneo husika (Waebrania 13:17, Ufunuo 5:10)

Kuwa Mlinzi wa eneo fulani katika ulimwengu wa roho ni kuwa kiongozi wa eneo husika katika mambo au masula mbalimbali ya eneo lako la ulinzi. Huu ni wajibu wa kufanya maamuzi kwa niaba ya watu wa eneo lako sambamba na kuleta ufumbuzi wa changamoto zenye kuwakabaili.

Kumbuka mlinzi ndiye mwenye uwezo wa kuona jambo lolote linalotaka kuja kwenye eneo lake na ki-nafasi ana uwezo wa kuruhusu litokee au kuzuia lisitokee. Ikiwa ni jambo ambalo halina budi kutokea basi anayo fursa ya kuwaonya watu wake wajipange kukabiliana na jambo husika (Wimbo Ulio Bora 3:3, 2Samweli 12:14-19).

  • Umewekwa kuwa Mwonyaji wa eneo lako la ulinzi (Ezekieli 33:1-9)

Daima Shetani hupambana kuhakikisha watoto wa Mungu, wanaishi nje ya mapenzi ya Mungu kwenye maisha yako, yeye huja ili aibe na kuchinja na kuharibu. Hivyo ili watoto wa Mungu waweze kuepushwa na mabaya hayo, wanahitaji Mlinzi ambaye anajukumu la kuwaonya watu wa eneo lake kadri naye anavyopokea maonyo husika toka kwa Mungu. Naam, haya ni maonyo ambayo yana gharama kubwa kwa kila upande kama yatapuuzwa (Eze 3:26-27)

  • Umewekwa kuwa Mtoa taarifa wa eneo lako la ulinzi (Isa 21:6, 11 & Yer 6:17)

Siku zote taarifa inalenga kumpa mtu ufahamu wa nini kipo au kinakuja na hivyo kuwa fursa ya kujiandaa kukabiliana na jambo husika. Mwanadamu kama mlinzi una nafasi kubwa ya kutoa taarifa za msingi kwa watu wa eneo lako ili zifanyiwe kazi kwa wakati. Naam kadri Mungu anavyokupa taarifa za eneo lako nawe fanya hima kuzitoa kwa nyakati zilizoamriwa ili kufanikisha malengo.

  • Umewekwa kuwa Mshauri wa Mungu kwenye eneo lako la ulinzi

Mlinzi katika ulimwengu wa roho ni mshauri wa Mungu wa masuala ya kiroho kwenye eneo lake. Naam kwa nafasi hii Mlinzi anaweza kwenda mbele za Mungu na kuzungumza naye juu ya kile ambacho anataka kifanyike au kisifanyike kwenye eneo lake au kwa watu wa eneo lake (Kutoka 32:9-14)

Kutoka 39:10 inasema BWANA akamwambia Musa ‘Basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize… Je umeliona lile neno linalosema‘niache’. Kitendo cha Mungu kumwambia Musa ‘basi sasa niache’ kinatuonyesha kwamba,si tu Musa alikuwa kiongozi wa wana wa Israeli, bali, zaidi alikuwa ‘MLINZI wao’ na kwa sababu hiyo hakuna ambaye angeweza kufanya jambo juu yao bila ridhaa yake. Nafasi yako kama mlinzi ina thamani kubwa sana hivyo itumie ipasavyo kwa manufaa yako na watu wa eneo lako binafsi kama Musa alivyoitumia.

  • Umewekwa kuwa Mwombaji wa eneo lako la ulinzi (Isaya 62:6)

Kuomba ni wajibu mkubwa zaidi ambao Mlinzi amepewa kwenye eneo lake la ulinzi, wajibu huu ndio unaowezesha majukumu yake mengine kufanyika ipasavyo. Mlinzi wa eneo anapswa kujua sababu na makusudi ya yeye kuwa mlinzi kwenye eneo husika ndipo atakuwa kwenye nafasi ya kudumu kuomba, ili kuhakikisha yale ambayo Mungu anayo moyoni mwake, kuhusu eneo lake la ulinzi yanatimia. Huu ni wajibu unaokutaka kuomba na kufikiri kama Mlinzi wa eneo husika tena bila kukata tamaa (Luka 18:1).

Ndugu zangu, nafasi ya ulinzi katika ulimwengu wa roho, ni nafasi ya pekee sana ambayo Mungu ametupa watoto wake. Haya matano ndio majukumu ambayo Mlinzi anapaswa kuyafanya kutokana na nafasi yake. Hata hivyo kwa kuwa somo hili linahusu maombi, kuanzia sehemu ya pili ya ujumbe huu nitaaingia ndani kufundisha kuhusu nafasi ya mlinzi kama  mwombaji wa eneo lake la ulinzi. Naam binafsi nimejifunza kwamba kufanikiwa kwa kusudi la Mungu hapa duniani si tu kunategemea utiifu wa watu wake ,bali zaidi, kunategemea namna Walinzi aliowaweka wanavyozitumia nafasi zao katika ulimwengu wa roho na hivyo kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwenye ulimwengu wa mwili. Fuatilia mfululizo wa somo hili, utaelewa siri iliyoko ndani ya ujumbe huu muhimu kwa nyakati tulizonazo.

Tutaendelea na sehemu ya pili …

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, Wastahili BWANA.

FAHAMU UMUHIMU WA NAFASI YA MTU AU WATU WENGINE KWENYE MAISHA YAKO KIBIBLIA (Sehemu ya mwisho)

May 13, 2017

Na: Patrick Sanga

Mada: Maisha ya Musa kama mfano wa kusisitiza umuhimu wa watu wengine kwenye maisha yako

Katika sehemu ya pili niliandika kuhusu makundi muhimu kuyaombea kama watu ambao wameunganishwa kwenye maisha yako. Ili kusoma sehemu hiyo tafadhali bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2017/04/20/fahamu-umuhimu-wa-nafasi-ya-mtu-au-watu-wengine-kwenye-maisha-yako-kibiblia-sehemu-ya-pili/ Ndani ya Biblia kumejaa fafanuzi (mifano) nyingi zinazoeleza dhana hii kwa upana hivyo ni jukumu lako kujifunza ili kuongeza ufahamu wako. Katika sehemu hii ya mwisho nitakuonyesha mfano mmoja tu wa maisha ya Musa ili kukujengea msingi mzuri wa somo hili na kufuatilia mifano mingine. Naam fuatana nami sasa tuendelee;

Katika viongozi wa kiroho waliopata changamoto kubwa za wale waliwaongoza, hakika  Musa ni mmoja wao. Siku moja, Mungu alimwambia Musa … Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu basi sasa NIACHE, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu (Kutoka 32:9-10). Mpenzi msomaji, umeona namna Mungu alivyokuwa amefikia mahali pa kukasirika hata kukukusudia kuangamiza taifa zima, kwa sababu ya uovu na uasi wao?   

Pamoja na kusudio hilo umeshawahi kujiuliza kwa nini hakuwaangamiza moja kwa moja hadi atake ushauri au kibali kutoka kwa Musa? Hiki ndicho nilichokisisitiza katika sehemu ya kwanza ya somo hili, kwamba wapo watu ambao wameunganishwa kwenye kusudi la maisha yako na hivyo wanahusika kwa namana moja au nyingine na maisha yako.  Kitendo cha Mungu kumwambia Musa SASA NIACHE NIWAANGAMIZE, ina maana asingeangamiza hadi kwa ridhaa ya Musa, naam Musa ndiye alikuwa na uamuzi wa kukubali au kukataa.

 

Je unajua Musa alimjibuje Mungu? Biblia inasema hivi  ‘Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema, Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? GEUKA KATIKA HASIRA YAKO KALI, UGHAIRI UOVU HUU ULIO NAO JUU YA WATU WAKO. Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele. Na Bwana AKAUGHAIRI ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake’ (Kutoka 32:11-14).

Je umeona ushauri wa Musa kwa Mungu kiasi cha kugeuza nia ya BWANA kwa watu wake? Ushauri huu wa Musa kwa Mungu unatufanya tujue kwamba kwa hakika Musa alikuwa ni kiongozi wa kipekee sana. Kupitia mfano huu yafuatayo ni mambo ambayo natamani ujifunze;

  • Musa alijua kwamba yeye ndiye aliyepewa jukumu la kuwatoa wana wa Israeli, Misri na kuwaingiza kanani, sio wakafie jangwani. Naam na hata kama ingebidi kufa sio kufia katika zamu yake. Hii ni kwa sababu katika ulimwengu wa roho, Musa alikuwa Mlinzi wa wana wa Israeli na kwamba kama kiongozi wao alikuwa anawajibika kwa lolote linalohusua uwepo wao na maisha yao.
  • Musa alikuwa na jitihada binafsi ya kumuomba Mungu hata akaweza kupata ufunuo wa kumshauri Mungu vema. Hivyo hata viongozi wetu leo wanahitaji maombi yako sana ili Mungu anaposema nao kuhusu wewe wajue namna ya kutoa ushauri sahihi. Nasikitika kwamba watu wengi leo wamerudi nyuma na wengine kufa kiroho na kimwili pia, kwa sababu vioingozi au wale waliounganishwa nao hawako kwenye nafasi zao.
  • Viongozi wa kiroho, kutoka kwenye nafasi ya kuwa walinzi, ni washauri wa Mungu katika mambo yahusuyo wale waliounganishwa kwao, lakini pia ni washauri wa mwanadamu katika mambo yahusuyo mawazo ya Mungu juu yao. Ndiyo maana unahitajika kuwaombea viongozi wako wa kiroho au yeyote aliyeunganishwa kwenye maisha yako, wapate mafunuo sahihi kuhusu maisha yako na hivyo kukushauri ipasavyo.
  • Viongozi wa kiroho wanaweza kuleta laana au Baraka kwenye maisha yako. Je unamkumbuka Haruni ndugu yake Musa aliyekuwa kuhani wa wana wa Israeli. Kuhani huyu ki-nafasi ndiyo chanzo cha ghadhabu hii kubwa aliyokuwa nayo Mungu. Biblia inaeleza kwamba Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata. Haruni akawaambia, Zivunjeni pete za dhahabu zilizo katika masikio ya wake zenu, na wana wenu, na binti zenu, mkaniletee’ (Kutoa 32:1-2). Je, ni kwa nini Haruni alikubali haraka ombi lao, asiwaambie mnipe muda niulize kwa Mungu kuhusu huyu Musa aliyechelewa huko Mlimani au hata asiwaambie nipeni walu siku tatu niende huko Mlimani nijue kinachoendelea bali akawakubalia katika wazo lao ovu? Kama kuhani alikuwa na nafasi muhimu ya kuzuia laana na mabaya yasiwajie wana wa Israeli, lakini kwa sababu alikubali wazo lao, alileta laana juu yao bila wao kujua na ndio maana Musa alimwambia akisema ‘…Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao?’ (Kutoka 32:21).

Ndio maana nasisitiza, jifunze kuwaombea wale wote ambao wameunganishwa na kusudi la maisha yako ili wawajibike ipasavyo kwenye nafasi zao huku wakilenga kuyatenda na kutii mapenzi ya Mungu ili usije ukaingia kwenye laana kwa sababu yao kama ambavyo viongozi au watumishi mbalimbali walivyoleta laana kwenye familia zao, jamaa zao na hata taifa kwa kushindwa kuyatii na kutenda mapenzi ya Mungu.

Mwisho, inawezekana wewe ni sehemu ya wale ambao unahusika kwa namna moja au nyingine na maisha ya wengine. Ujumbe huu ukusaidie kujua kwamba, licha ya kuwa wale ambao unahusika kwao, wana wajibu wa kukuombea, nafasi yako ni tofauti sana na yao na hivyo una wajibika kukaa vizuri kwenye nafasi yako, kuwa na muda wa kutosha wa kuhoji na kusikia kutoka kwa Mungu na kufanyia kazi kwa nidhamu yale ambayo Mungu anakuonyesha kuhusu wale ambao wapo chini ya sauti au mamlaka yako kiroho (Isaya 42:20).

Naam ningweza kuandika na mifano mingine kadhaa juu ya jambo hili, naamini mfano huu umetoa mwanga uliokusudiwa juu ya jambo hili. Kumbuka lengo la somo hili ilikuwa ni kukuonyesha umuhimu wa nafasi ya mtu au watu wengine kwenye maisha yako ili ujue namana ya kuhusiana nao na zaidi ujifunze kuwaombea kwenye maeneo mbalimbali kama nilivyofundisha kuanzia sehemu ya kwanza. Naam, hakikisha unadumu katika kuwaombea watu hao muhimu kwenye maisha yako (Waefeso 6:18-19)

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, Wastahili BWANA.

FAHAMU UMUHIMU WA NAFASI YA MTU AU WATU WENGINE KWENYE MAISHA YAKO KIBIBLIA (Sehemu ya pili)

April 20, 2017

Na: Patrick Sanga

Mada: Makundi muhimu kuyaombea kama watu ambao wameunganishwa kwenye maisha yako

Katika sehemu ya kwanza ya ujumbe huu naliandika kuhusu mambo ya msingi kuwaombea wale ambao wameunganishwa kwenye kusdi la maisha yako. Ili kusoma sehemu hiyo ya kwanza tafadhali bonyeza link hiihttps://sanga.wordpress.com/2017/03/09/fahamu-umuhimu-wa-nafasi-ya-mtu-au-watu-wengine-kwenye-maisha-yako-kibiblia-sehemu-ya-kwanza/ . Katika sehemu hii ya pili nitakuonyesha baadhi ya makundi muhimu kuyaombea kama watu ambao wameunganishwa kwenye maisha yako. Naam fuatana nami sasa tuendelee;

Viongozi wa kiroho – Katika Waebrania 13:17 imeandikwa Watiini wenye KUWAONGOZA, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi’. Je umeliona neno wenye ‘kuwaongoza’, hii ina maana hili ni kundi muhimu sana kulitii na zaidi kuliombea, kwa kuwa viongozi hawa wanahusika si tu na maisha yako ya sasa bali na yale ya baadae (future/destiny) yako.

Unapaswa kuwaombea viongozi hawa wafanye wajibu wao kwa uaminfu, wakidumu kukuombea na kukufundisha mafundisho sahihi ya neno la Mungu ili ufanikiwe hapa duniani na kisha kuurithi uzima wa milele, ukikumbuka kwamba mtu anapokufa ndipo anaanza maisha mapya ya umilele. Ndio maana mzee Samweli (Nabii)  katika 1Samweli 12:23 anasema ‘Walakini mimi, hasha! Nisimtende Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka’.

Viongozi wa Taasisi/Serikali/watumishi wenzako – Baada ya kifo cha Musa, Mungu alimwambia hivi Joshua Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa’ (Joshua 1:6). Naam, ni vizuri ukafahamu kwamba viongozi wa Serikali, Taasisi au Kampuni unayofanyia kazi wanahusika na mafanikio yako kwa namna mbalimbali. Hata kama huwapendi, elewa kwamba kibiblia Mungu ndio kawaweka au karidhia wao wawe kwenye hizo nafasi. Hivyo ni jukumu lako kuwaombea ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo, kwa sababu kufanikiwa au kufeli kwao kutakugusa na wewe.

Pia wafanyakazi au watumishi wenzako kwa namna moja au nyingine ni watu muhimu sana kwako hata kama umewazidi cheo, elimu, uwezo nk. Jambo muhimu ni kwamba maadam ni watu unafanya nao kazi Ofisi au kampuni moja unapaswa kuwaombea kwa kuwa Mungu anaweza kutumia mtu yoyote hata ambaye hukumtegemea kukupeleka kwenye hatua nyingine ya mafanikio.

 Mwenza wako wa maisha – Biblia katika Waefeso 5:22,25 Biblia inasema Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake’.  Ikiwa una mweza (mume au mke), basi elewa kwamba kibiblia mwenza wako ana nafasi kubwa sana katika kuamua aina au hatma ya maisha yako kiroho, kiuchumi, kihuduma, kimwili na wito wa kusudi la Mungu kwako. Hakikisha unaomba sana kwa ajili ya mwenza wako, ili akae vizuri kwenye nafasi yake na kufanya wajibu wake ipasavyo.

Kibiblia zipo nafasi ambazo kila mmoja amepewa, ambapo mke ametwa kuwa mlinzi, msaidizi, mjenzi, mshauri na mleta kibali kwa mumewe huku pamoja na nafasi nyingine mume ameitwa kuwa kichwa cha mkewe. Naam unamuhitaji mwenza wako ili msaidiane katika kulea watoto, kujenga familia yenu na kumtumika Mungu wenu kwa pamoja. Umeshawahi kufikiri maisha bila mwenza wako au watoto/walezi yatakuwaje? Mara nyingi thamani ya mtu huwa inaonekana akishafariki, naam ujumbe huu ukusaidie kuona thamani yake aangali hai.

Familia, ndugu, walezi wako – watoto, ndugu zako au wazazi/walezi wako ni kundi jingine muhimu sana ambalo hunabudi kuliombea ipasavyo ili kufanikiwa pia katika maisha yako. Ukisoma Biblia utaona namna ambavyo ndugu, jamaa, watoto au walezi walivyohusika ama kujenga au kuharibu maisha ya wale ambao walihusiana nao kwa namna moja au nyingine.

Watoto, ndugu, wazazi, walezi na jamaa zako kibiblia kuna mambo ambayo wamewekewa ya kukusaidia wewe kuvuka hatua moja kwenda nyingine na ndio maana ni muhimu sana kuwaombea ili wafanyike malango yaw ewe kupenya kufikia kusudi la Mungu kwenye maisha yako.

Kumbuka licha ya kwamba watoto umezaa wewe, ni wa Mungu kwa kusudi lake, hivyo unapaswa kuwalea kwa namna ambayo wataenda katika njia sahihi kwenye maisha yao. Haijalishi kwa jinsi ya kibinadamu tabia au mwendndo wao si mzuri usikate tamaa, dumu kuwaombea maana Mungu ana kazi ya kufanya duniani kupitia wao. (Rejea pia Mithali 13:24, Mithali 22:6, Mithali 19:18, Mithali 29:17, Waefeso 6:1-4).

Kanisa la Kristo duniani (Waamini wenzako) – kanisa linapaswa katambua kwamba sisi tu viungo katika mwili wa Kristo, na kila kiungo (mtu) kina umuhimu kwa nafasi yake. Biblia katika 1Wakorinto 12:12-30 imeeleza kwa upana sana kuhusu dhana hii, hata hivyo kwenye mstari wa ishirini na tano imeandikwa ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe’.

Ndio, ili mwili uweze kufanya kazi ipasavyo sharti na viungo vitunzane. Kanisa hatupaswi kugombana, kuchafuana nk bali tudumu kuombeana, kuchukuliana na kuonyana ili kila kiungo kikae katika utaratibu unaofaa na kufanya kazi yake ipasavyo.

Maadui na Marafiki zako – Biblia katika Mathayo 5:43-44 inasema Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi’. Licha ya kwamba kwa mtazamo wa kibinadamu maadui ni wabaya lakini kwa mtazamo wa neno la Mungu, maadui ni kundi muhimu na hivyo unapaswa kuliombea kwa sababu maadui wanakusaidia kumjua Mungu kupitia changamoto (hila) zao kwako.

Hata hivyo ni kweli kwamba wapo maadui ambao uwepo wao ni changamoto kwako katika kutimiza kusudi la Mungu jukumu lako sio kuwaombea wafe maana kisasi ni cha BWANA, bali omba Mungu akuokoe na hila (mabaya) zao zote, na zaidi wafike mahali pa kumjua Mungu wako kwa sababu mosi, Mungu hafurahii kifo cha mwenye dhambi na pili mtu ambaye ni adui wako leo, kesho anaweza kuwa wa msaada mkubwa kwako katika kulitumika kusudi la Mungu kwenye maisha yako.   

Kuhusu marafiki, kumbuka hawa ndio watu wako wa karibu zaidi kwa kila jambo na changamoto unazopitia, basi hakikisha unawaombea ili urafiki wenu udumu kuwa wa kweli kama ilivyokuwa kwa Yonathani na Daudi, na zaidi mwombe Mungu akusaidie kupata marafiki ambao ni sahihi kwa ajili yako kwa kila ngazi ya maisha yako.

Mpenzi msomaji haya ni baadhi ya makundi muhimu sana kuyajua na kuyombea pia. Ndio, ni lazima ujifunze kuwaombea watu hawa wawe na utiifu katika yale ambayo Mungu ameweka moyoni mwao wayatende kwa ajili yako ukijua kwamba kutii kwao ndiko kufanikiwa kwako na kutokutii kwao ni kufeli kwako. Kutokuwaombea kunatoa nafasi kwa Shetani kupenya na kuwafanya hao watu wasahau kabisa wajibu wao kukuhusu wewe na zaidi hata baadhi yao wageuke na kuwa adui zako. Kumbuka hawa na watu ambao BWANA amewaweka wawe fursa ya kufanikiwa kwako.

Tutaendelea na sehemu ya tatu …

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, Wastahili BWANA.

NAMNA YA KUSIKIA NA KUIELEWA SAUTI YA MUNGU ILI IKUSAIDE KATIKA KUFANYA MAAMUZI (Sehemu ya mwisho)

March 28, 2017

Na: Patrick Sanga

Mada – mambo ya kukusaidia kuelewa sauti ya Mungu ili kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yako

Katika sehemu ya tano ya somo hili tuliangalia njia sita ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu, ili kusoma sehemu hiyo bonyeza hapa https://sanga.wordpress.com/2017/03/16/877/ Katika sehemu hii ya sita na ya mwisho kwa somo hili nitafundisha mambo ya kukusaidia kuelewa sauti ya Mungu na hivyo kuweza kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yako.

Jambo muhimu si tu kusikia sauti ya Mungu, bali zaidi kuelewa kile anachosema . Uelewa wa sauti ya Mungu (ujumbe uliokusudiwa) imekuwa ni changamoto kwa watu wengi. Nimewasikia watu wakisema nimemwomba Mungu kwa muda mrefu lakini hajawahi kujibu au kusema nami. Naam, huwezi kumwomba Mungu aliye hai asikujibu, daima yeye huwajibu na kusema na watoto wake. Changamoto iliyopo kwa watu wengi ni kushindwa kuelewa pale Mungu anaposema nao, kiasi cha kuamini bado hawajajibiwa.

Siku za mwanzo nilipokuwa najifunza jambo hili, kufuatia wingi wa mafunuo yaliyonijia kupitia neno, maono, mazingira, ndoto, sauti nk, nilipata tabu sana, mosi kutofautisha ikiwa mafunuo hayo yalikuwa kutoka kwa Mungu au la? na pili ikiwa yalikuwa kwa ajili yangu binafsi au watu wengine nk?. Kutokana na kukosa ufahamu wa kutosha, mara nyingi nilikuwa mtu wa kutubu, kukemea au kuomba maombi mengi ambayo sehemu kubwa yake hayakuwa sahihi kwani yalihusu mimi na familia yangu tu.

Niliendelea hivyo kwa muda mrefu sana bila kujua kwamba nilikuwa nakosea, hadi pale Bwana, aliponifundisha kwamba, pamoja na kuendelea kusema kwa ajili yangu binafsi, kwa kuzingatia nafasi yangu na kusudi lake kupitia maisha yangu, mara nyingi atasema nami ajili ya watu wake ili niwaombee, kuwaonya na kuwafundisha. Bwana akaendelea kunifundiha kwamba, hata hivyo nionapo jambo lolote napaswa kutafuta kwanza maelekezo sahihi kutoka kwake’.

Naam, katika sehemu hii ya mwisho nitaandika mambo matano ya kukusaidia kuelewa sauti ya Mungu na kukuwezesha kufanya maamuzi sahihi;

Moja, jifunze kufuatilia ili kuelewa kile Mungu anasema nawe – Ukisoma Ayubu 33:14 imeandikwa ‘Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu HAJALI’. Ukienda kwenye Isaya 42:20 imeandikwa Unaona mambo mengi, lakini HUYATII MOYONI; masikio yake ya wazi, lakini hasikii’. Mistari hii inatufanya tujue kwamba, Mungu anaposema, lengo lake ni kutaka watu wake wathamini, waelewe na kuufanyia kazi ujumbe aliowapa, na si kupuuza.

 

Watu wengi Mungu anaposema nao, mosi hawana nidhamu ya kufuatilia ili kuelewa kile walichoona au kusikia na baadhi yao hata ujumbe huo ukijirudia bado hawajali hadi pale madhara yawapatapo ndipo hujuta na kukumbuka yale Mungu aliwaonya. Hivyo ni jukumu lako kuhakikisha unafuatilia hadi uelewe kile Mungu alichosema nawe maana yeye ndiye anayejua kinachokuja mbele yako na mwenye kuona usiyoyaona wewe. Naam jifunze kutopuuza ujumbe wowote ambao Mungu anauleta kwenye maisha yako kupitia njia mbalimbali.

Mbili, sauti ya Mungu inaendana na nyakati alizoziamuru juu yako – ukisoma katika Mhubiri 3:1 Biblia inasema ‘Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu’. Ile kusema kwa kila jambo kuna majira yake ina maana kwa kila majira kuna maelekezo yake pia. Naam kila majira yanakuja na maelekezo yake mahususi ya kufanyiwa kazi, jambo linalomaanisha ndani ya kila nyakati kuna sauti ya Mungu yenye kutoa maelekezo mahususi.

 

Ni vizuri ukaelewa kwamba Mungu anaposema amekujibu si kukupatia kile ambacho wewe ulikuwa unategemea kukipata kwa jinsi ya kibinadamu. Uwepo (uhalisia) wa kile ulichoomba ni hatua ya mwisho ya jibu lako, na kabla ya hapo, nyakati zinakutaka (demand) ufanye mambo fulani ambayo yameunganishwa na nyakati hizo ndipo uweze kupata ulichoomba. Uhalisia wa kile ulichoomba ni matokeo ya mchakato (process) wa ushirikiano kati yako na nyakati zilizoamriwa juu yako ambazo ndizo zilizobeba mambo au majibu au kusudi linalopaswa kutokea.

Tatu, unahitaji muda, utulivu na usikivu ili kuelewa kile Mungu amesema – katika Yeremia 23:18 imeandikwa Maana, ni nani aliyesimama katika baraza la Bwana, hata akalifahamu neno lake na kulisikia? Ni nani aliyelitia moyoni neno langu, na kulisikia?’ Siku zote Mungu hutafuta  utulivu na usikivu wa mwanandamu ili aweze kusema naye.

Hata hivyo moja ya gharama kubwa ya kumsikia na kumuelewa Mungu anaposema ambayo wengi wameshindwa kuilipa ni kutenga muda wa kuwa barazani pa Bwana wao (Yesu) ili aseme nao. Ndio mwanadamu anahitaji kuwa na muda na mazingira ya utulivu kama njia ya kumsaidia kufuatilia na kuelewa zaidi kile mbacho Mungu alisema naye kupitia ndoto, malaika, maono, sauti ya waziwazi, neno lake nk.

Nne, jifunze kuandika yale Mungu anasema nawe – mara nyingi Mungu husema nasi kwa habari ya mambo yajayo na anaposema kuna nyakati inakuwa si rahisi pia kuelewa kwa wakati huo. Hivyo hakikisha katika yale ambayo Mungu anasema nawe unayaandika ikiwa ni ndoto, neno, sauti au maono nk.

Kuandika kutakusaidia; (a) kufanya rejea ya yale Mungu amekuwa akisema nawe (b) kuendelea kuomba utimilifu wake ikiwa ni mambo mema au kutotokea ikiwa ni mambo mabaya (c) kuwa onyo kwako na hivyo kukuongezea umakini katika mahusiano yako na baadhi ya watu au vitu tegemeana na uliyoyona.

Tano, kuwa makini na sauti nyingine – ukirejea Yeremia 23:16 Biblia inasema Bwana wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha Bwana’. Hapa nisisitize kuhusu wale ambao hawataki kulipa gharama kumtafuta Mungu bali daima wanategemea kusikia kutoka kwa wanadamu.

Ni kweli kwamba Mungu husema kupitia wanadamu (watumishi wa kiroho), ingawa changamoto ni kwamba baadhi ya watumishi hawa si wa ufalme wa nuru, hata kama wanataja jina la Yeu, naam wamevaa ngozi ya kondoo lakini ndani ni mbwa mwitu. Kumbuka Shetani naye ana uwezo wa kusema na wanadamu kupitia njia mbalimbali. Hivyo ni muhimu sana kuwa na uelewa wa kutosha wa njia za Mungu ili ikusaidie kutofautisha na sauti ya Mungu na sauti nyingine.

Tamati – Mungu anaposema na mwanadamu kwa njia yoyote ile lengo lake ni kumsaidia mtu aishi katika njia sahihi ya kusudi lake (Zaburi 32:8). Kusikia na kuielewa sauti ya Mungu ni somo muhimu kwa mwamini kujua na kufuatilia mara kwa mara ili kuishi maisha yenye kuleta thamani kwenye maisha yake. Naamini ujumbe huu kuanzia sehemu ya kwanza hadi hii ya mwisho zitakuwa zimeweka msingi mzuri wa kuanzia.

Neema ya Bwana wetu, Yesu Kristo iwe nawe.

Utukufu na heshima, vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu.