Archive for the ‘Maswali na majibu’ Category

NIFANYE NINI ILI KUSHINDA TAMAA ZA MWILI?

November 11, 2011

Na: Patrick Sanga

Septemba mwaka huu, Mwanafunzi mmoja wa shule ya Sekondari alinitembelea nyumbani kwangu hapa Dodoma. Alipofika nilimkaribisha ndani nikajua amekuja kunisalimia tu. Baada ya muda akaniambia kaka Sanga nina swali nahitaji msaada wako sana. Tukatoka nje mahala penye utulivu ndipo akaniambia tamaa za mwili kwa maana ya uasherati/zinaaa zinanitesa nifanye nini ili kushinda? Jambo hili linanitesa kiasi kwamba nahisi kama vile sijaokoka kutokana na vita niliyonayo katika fahamu zangu na mwilini mwangu?

Kwa kuwa vijana wengi wamekuwa wakiuliza swali hili kwa namna tofauti tofauti na kwa njia mbalimbali, nimeona ni vema nikaliweka somo hili kwenye ‘blog’ hii  kwa kuwa tunao vijana wengi ambao changamoto hii inawakabili pia. Naam yafuatayao ni mambo ya msingi kuzingatia ili kijana aweze kuwa na ushindi dhidi ya tamaa za  mwili (dhambi) nk.

 • Kwa kutii na kulifuata neno la Mungu

Biblia katika Zaburi 119:9 inasema ‘Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako’. Ukisoma Mstari huu katika tafsiri ya Biblia ya Kiingereza ya GNB unasema How can young people keep their lives pure? By obeying your commands’. Mtazamo wa tafsiri hii ya kiingerza ni kujaribu kutafuta ufumbuzi wa namna ambayo vijana wanaweza kuishi maisha ya utakatifu na yenye ushuhuda. Inawezekana mwandishi huyu wa Zaburi aliona namna vijana wanavyohangaika katika eneo hili, ndipo ikabidi amuulize Mungu, ni jinsi gani kijana aisafishe njia/au anaweza kusihi maisha ya utakatifu? Kipengele cha pili kinatupa jibu la swali la kwanza kwamba ni kwa kutii, akilifuata neno lako.

Naam hii ina maana ni lazima kwanza kijana achukua hatue  ya kuliweka neno la Mungu moyoni mwake kwa wingi, maana hawezi kutii neno ambalo halimo ndani yake au hajalisoma na kulitafakari. Zaburi 119:11 inasema ‘Moyoni mwangu nimeleiweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi’. Maana yake ni kwamba, kama kijana atajijengea tabia ya kuhakikisha analiweka neno la Bwana moyoni mwake kwa kulitafakari kila siku, kwa vyovyote vile lazima atakuwa na ushindi dhidi ya tamaa za mwili na kazi zote za Shetani. Naam usiishie tu kuliweka moyoni mwako bali fuatilia sauti ya neno uliloliweka ndani yako, ukaiitii.

 • Kuacha michezo ya mapenzi na kuwa makini na nini unatazama/unasikia.

Michezo ya mapenzi (foreplay) ni maalumu kwa ajili ya wanandoa. Kwa bahati mbaya vijana wetu nao sasa wamekuwa wakifanya mambo haya ambayo kimsingi si yao. Michezo ya mapenzi ni sehemu ya vitendo vyvyote ambavyo hupelekea ashiki ya kufanya tendo la ndoa hii ni pamoja na kushikana shikana/kugusana maeneo mbalimbali ya mwili na pia kunyonyana ndimi.

Zaidi Katika dunia ya sasa Shetani ametumia teknolojia iliyopo kuteka fikra za vijana wengi. Vijana wengi kupitia simu, computer, video nk wanaangalia picha chafu za ngono na kusoma jumbe za aina hiyo kitu ambacho kinaharibu fahamu zao bila wao kujua. Na kwa kufanya hivyo wanakuwa wanayachochea mapenzi na kuamsha tamaa zao za mwili. Naam mambo haya ni hatari tena kinyume na mapenzi ya Mungu. Na kwa bahati mbaya vijana wetu tena waliokoka baadhi yao bado wamefungwa katika kufanya mambo haya.

Katika kile kitabu cha Wimbo Ulio Bora 2:7 Biblia inasema ‘Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe’. Kulingana na mstari huu tunajua kwamba, kumbe mapenzi yanaweza kuchochewa na kuamshwa, naam na hili ni jambo hatari sana kama litafanywa na wahusika ambao si wanandoa kwa maana ya (foreplay) hata kama wana kiroho cha iana gani.

Jambo la msingi kuepuka hapa ni kuwa kwenye mazingira ambayo yanaweza yakawashawishi kufanya mambo haya. Vijana ambao si wanandoa kutembeleana mahali wanaposihi kwa maana ya eneo ambalo wako pekee yao, au kwenda guest na  maeneo yote ya namna hii eti kwa lengo la kupanga mipango yenu. Fahamu kwamba kitendo cha vijana wawili ambao si wanandoa kukaa katika mazingira ya aina hii ni kumpa Iblisi nafasi ya kuwamaliza, naam kijana uwe makini usifanye ujinga huu, Shetani asije akakumaliza.

 • Kuenenda kwa Roho.

Mtume Paulo alikutana na kesi ya aina hii kwa wandugu wa kanisa la Galatia. Moja ya ufumbuzi juu ya suala hili aliwataka waenende kwa Roho ili wasisitimize kamwe taamaa za mwili. Wagalatia 5:16 ‘Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili’. Kuenenda kwa Roho ndio kukoje? Ni kuishi/kuenenda kwa kufuata utaratibu/uongozi wa Roho Mtakatifu maishani mwako (Zaburi 32:8). Jambo la msingi ni kuwa mtiifu kwa Roho Mtakatifu, naam atakusaidia kushinda dhambi kama alivyomsaidia Bwana Yesu alipokuwa hapa duniani.

 • Kujitenga na marafiki/makundi mabaya

Zaburi 1;1 inasema ‘Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki; Wala hakusiamama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha’. Jiulize muda wako mwingi unautumia kwa kufanya nini? Na kama ni marafiki ni marafiki wa aina gani?  Siku zote wale unaokuwa nao karibu wanachangia sana kujenga (kushape) mfumo wa maisha yako. Biblia katika 1 Wakorinto 15:33 inatuambia ‘Msindanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema’. Naam kama utakuwa na marafiki wabaya basi tegemea na mazungumzo yao yatakuwa mabaya na hivyo tegemea na wewe kuwa na tabia mbaya. Jambo la msingi ni kujitenga nao usiende katika shauri lao, wala njia yao na pia kuketi katika baraza yao.

Mtume Paulo akizungumza na kijana wake Paulo alimwambia hivi ‘Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi’ 1 Timotheo 4:12. Wazo ninalotaka ulipate hapa ni kwamba kama Paulo angejua kwamba vijana hawawezi kuishi maisha ya utakatifu na yenye ushuhuda katika dunia hii, asingemwambia Timotheo afanye haya. Basi kwa kuwa alijua inawezekana, ndiyo maana Roho Mtakatifu alimwongoza kuandika haya ili kumwagiza Timotheo na sisi vijana wa leo katika jambo hili. Naam uwe kielelezo katika shule, chuo, kanisa, kazini nk ili Mungu aone sababu ya kuendelea kukutumia kwa utukufu wake.

Neema ya Mungu iwe nanyi

 

 

KWA NINI IMANI YA MWANAMKE MKANANAYO ILIONEKANA KUWA KUBWA?

June 12, 2011

Na: Patrick Sanga

Nakusalimu kwa jina la Bwana, amani na iwe kwako.

Katika Mathayo 15:21-28 maandiko yanasema “Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akamsujudia, akisema, Bwana, unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yaka tangu saa ile

Katika zamu hii  nimeona vema kujibu swali jingine linalohusu imani ya mwanamke Mkakanayo.  Huyu Mama alikuwa mwenyeji wa nchi ya Kanaani ambayo ilikuwa karibu na pwani ya Bahari ya kati kutoka Sidoni. Kwa bahati nzuri Yesu alikuwa amekwenda katika miji ya Tiro na Sidoni kihuduma, ndipo akakutana na mama huyu ambaye alikuwa anahitaji msaada wa Yesu apate kumponya bintiye.

Haikuwa jambo rahisi kwa Yesu kuachilia uponyaji uende kwa yule binti. Lakini baada ya mvutano wa muda mrefu, Yesu alimwambia yule mama ‘Imani yako ni kubwa, na iwe kwako kama utakavyo’. Sasa swali la msingi ninalotaka kujibu ili nasi tupate kujifunza ni hili; kwa nini imani ya yule mama ilionekana kuwa kubwa kiasi cha kuamua uponyaji utoke kwa Yesu na kwenda kwa binti yake na kumponya saa ile ile?

Yafuatayo ni mambo matatu yaliyompelekea Yesu kusema, Mama, imani yako ni kubwa;

 • Kutokukata tamaa/kuchoka.

Kwa mara ya kwanza yule mama alipoeleza hitaji lake kwa Yesu, maandiko yanasema Yesu hakujibu neno. Na kwa hiyo tunaweza kusema, Yesu hakusikiliza wala kujali maombi ya yule mama. Naam mwitikio huu wa Yesu haukumvunja moyo yule mama akaendelea kuomba tena kwa kupiga kelele ili Yesu amsaidie.

 • Aliyapuuza/hakujali maneno ya wanafunzi na wale walifuatana na Yesu.

Kwa kadri yule mama alivyooendelea kumsihi Yesu amponye mwanaye, ilifika mahali wanafunzi wa Yesu waliona anapiga kelele. Hivyo wakamsihi Yesu amfukuze  ili asiendelee kuwapigia kelele. Sijui kama unaliona jambo hili kwa upana wake. Huyu mama ana  hitaji katika nyumba yake, anajieleza kwa Yesu, Yesu ana nyamaza, kama vile haitoshi Wanafunzi wa Yesu wanasema anapiga kelele. Sasa kilichomsaidia yule mama ni kupuuzia kauli zote zenye kumvunja moyo, yeye alitaka kusikia kutoka kwa Yesu na si wanadamu. Kwa hiyo hakuruhusu maneno yao yamvunje moyo/yaweke mpaka kwa kile anachoamini.

 • Alikuwa na ufahamu wa masuala ya kiroho(imani).

Ukweli huu tunaupata baada ya kuona majibu ya huyu mama pale, Yesu, alipomwambia; kwanza hakutumwa kwa watu wa taifa (kabila) lake na pili kumponya bintiye ni sawa na kuwatupia mbwa chakula cha watoto. Katika hali ya kibinadamu majibu ya Yesu na wanafunzi wake kwa huyu mama, yalitosha kumfanya huyu mama kukata tamaa na ikibidi kumtukana Yesu na wanafunzi wake pia. Lakini mwanamke huyu wa ajabu hakufanya hivyo.

Ile kuendelea kuomba kwa unyenyekevu kwa Bwana amponye bintiye na pia kujibu kwamba hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao, ilidhihirisha kwamba ni lazima huyu mama, ingawa alikuwa Mkaanani kuna namna alikuwa ana ufahamu wa mambo ya imani katika Kristo (neno la Mungu). Kwa hiyo hakikumsumbua watu (Yesu) wanasema nini, ndani yake alikuwa na ufahamu na imani kwamba hakuna jambo la kumshinda Bwana, na hivyo ndani yake akazidisha uhakika kwamba bintiye atapona tu.   

Naam ile kusema hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao, kauli hili ilimfanya Yesu kuachilia uponyaji kwenda kwa binti yake saa ile ile na ndipo akasema, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo.

Sijui kama umeliona jambo hili mpenzi msomaji, imani ya yule mama ili kuwa kubwa kiasi cha kutenda kwa kadri ya matakwa yake kuhusu binti yake. Ni imani iliyoje kutoka kwa mwanamke wa pande za Kaanani, mahali ambako kwa mujibu wa Yesu hapakuwa kipaumbele chake kuwafikia/kuwasaidia. Naam imani ya huyu mama ilivuka fikra na mipaka hiyo na kumfanya Yesu kuachilia uponyaji kawa kdari ya matakwa na muda anaotaka yule mama (Such a wonderful faith).

Tunajifunza nini?

Naam hata leo kuna sababu kubwa tatu zinazofanya watu washindwe kupokea majibu ya mahitaji yao au yale wanayoamini kwamba Mungu atawafanyia;

 • Kukata tamaa

Utasikia mtu anasema huu ni mwaka wa tatu, tano au saba namuomba Mungu sioni majibu, nimechoka, bora kwenda kwa waganga wa kienyeji au kuacha wokovu. Haajalishi kwa jinsi ya kibinadamu majibu yako yamechelewa kwa kiasi gani, usikate tamaa. Si lengo la Yesu kukutesa au kukuhuzunisha maana, Bwana hapendi kuwatesa wala kuwahuzunisha wanadamu (Maombolezo3:33). Hivyo usikubali kukata tamaa kwa sababu iwayo yote, mruhusu Yesu akusaidie, usijaribu kutegemea akilia zako. Zidisha imani yako kwake, atafanya tu, mpendwa.

 • Maneno ya kusikia

Kwa mujibu wa Yakobo 3:1-12 Ulimi ni kiungo kidogo lakini chenye madhara makubwa. Ulimi ni moto, uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti na hakuna awezaye kuufuga. Kwa huo twamuhimidi Bwana na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mafano wa Mungu nk. Jambo ninalotaka kusisitiza hapa ni kwamba usikubali maneno ya kusikia yakakusababishia ugonjwa wa nafsi yako na hivyo kuharibu imani yako. Kazi ya kinywa ni kusema, huwezi kuzuia watu wasiseme, ila unaweza kuzuia wanayosema kama ni mabaya yasitimie kwenye maisha yako. Naam ni kwa kutumia damu ya Yesu kuyafuta na kwa kutumia neno la Mungu kuumba kile unachotaka.

 • Kukosa ufahamu wa neno la Mungu kuhusu imani

Maandiko yanasema neno la Kristo likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote… (Wakolosai 3:16). Kwa nini likae kwa wingi? Mwimbaji wa Zaburi anajibu ni kwa sababu neno la Mungu ni taa ya miguu yetu, mwanga wa njia zetu(Zab 119:105). Hivyo litakusaidia kushinda vikwazo vya imani yako, maana kila imani sharti ijaribiwe. Yesu mwenyewe alijaribiwa alipokuwa jangwani lakini kwa sababu ya ufahamu wa neno la Mungu alimshinda Shetani. Hakikisha unakuwa na nidhamu ya kujisomea neno la Mungu kila leo.

Kwa sababu imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo, tena bayana ya yale yasiyoonekana (Waebrania 11:1), tunaweza kusema kwamba ukubwa wa imani ya huyu Mama ulitokana na uhakika aliokuwa nao kwamba Yesu atamponya mwanawe licha ya upinzani aliokutana nao kuhusu imani yake. Si tu kwamba yule mama alikuwa ana amini Yesu atamponya bintiye, bali yeye alishaona kwa imani kwamba Yesu amemponya mwanawe na hivyo alikuwa anang’ang’ania utimilifu wa kile alichoona kwa imani. Naam alikiona alichokiamini, hivyo alikijua anachokiamini, akakipata alichokiona.

Naam hakikisha unaongeza imani yako kila siku, ili ifikie na kuzidi ile ya Mwanamke Mkananayo na hivyo iweze kuamua majibu kwa kadri ya matakwa na muda wako kutoka kwa Yesu.

Mungu akubariki.

NITAMTAMBUAJE MKE AMBAYE MUNGU AMENIANDALIA?

March 14, 2011

Na:Patrick Sanga

Swali
Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu Sanga.
Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa ajili yenu kwa huduma mnayoitoa ambayo imekuwa msaada katika maisha yangu kama mkristo na kama mwanajamii. Mungu awabariki sana.

Pili naomba msaada wa maarifa juu ya namna ya kumtambua mke ambaye Mungu ameniandalia. Nimefanya maombi ya kumuomba Mungu mke mwema tangu septemba 2008 hadi sasa lakini bado sijapokea majibu ya maombi yangu. Ninaamini ninasumbuliwa na tatizo la upokeaji wa majibu ya maombi yangu jambo ambalo linahatarisha ustawi wangu kiroho.

Naomba kwa manufaa ya wengine pia ambao wana tatizo kama langu utupatie majibu hayo kwenye kipengele cha maswali na majibu. Ninaomba pia kwa ajili yangu na wengine ambao ninaweza kuwafikia unisaidie majibu hayo kupitia email address yangu hapo juu. Asante sana na Mungu awatimizieni haja za mioyo yenu na kuimarisha huduma yenu ili watu wengi zaidi waimarike kiroho.

 Lucas

 Majibu;

Hello Lucas, tunakusalimu kwa jina la Bwana, ahsante kutuombea, kututia moyo na kwa swali lako ambalo naamini majibu yake yatawafaa wengi kama ulivyoshauri katika swali lako.

Kaka Lucas swali lako ni pana sana na ‘it is more personal’ kimajibu, lakini namshukuru Roho Mtakatifu anayeweza kutupa majibu ya kutufaa .Katika swali lako nimegundua mambo mawili ya msingi ambayo natakiwa kuyatolea ufafanuzi, moja ni namna unavyoweza kumtambua mke ambaye Mungu amekuandalia na pili namna bora ya kuomba yenye kuleta matokeo.

Katika kujibu maswali haya mawili nitazungumzia mambo manne yafuatayo ambayo naamini baada ya kuwa umeyasoma haya utapata ufahamu wa kukusaidia katika kufanya maamuzi hayo yanayokukabili;

Jambo la kwanza; Mungu hatumii njia au mfumo wa aina moja katika kukujulisha wewe mwenzi wa maisha yako (Isaya 55:8).

Oktoba 2006 naliandika kitabu kuhusu Njia kumi za Kibiblia zitakazokusaidia kumjua na kumpata mwenzi wako wa maisha. Katika ukursa wa nne wa kitabu hicho ndipo nilipoandika wazo hili hapo juu, kwamba, Mungu hatumii njia au mfumo wa aina moja katika kumjulisha mtu mwenzi wake wa maisha.

Nimeona hata sasa nianze na msingi huu na hii ni kwa sababu vijana wengi hujaribu kuuliza wanandoa waliotangulia kwamba waliwapataje wenzi wao wa maisha kwa dhana ya uongozi wa Mungu? Kutokana na majibu ambayo vijana hao hupewa wengi humuomba Mungu na wanasubiri, Mungu aseme nao kwa njia ile aliyotumia kusema na mtu mwingine.

Kibiblia wazo hili siyo sahihi kwani, Mungu ana njia nyingi sana za kusema na watu wake katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na nani atakuwa mwenzi wako wa maisha. Kwa mtu mmoja Mungu anaweza akasema naye kwa ndoto, mwingine kwa sauti yake, na mwingine kwa maono, mwingine kwa mafunuo, mwingine kwa amani ya Kristo, mwingine kwa kutumia watumishi/wachungaji nk

Jambo ninalojaribu kukuonyesha hapa ndugu Lucas ni kwamba ‘Mungu ana namna yake ya kukusaidia kumtambua mwenzi wako wa maisha, ambayo si lazima ifanane na ya mtu mwingine’. Na mara nyingi namna/njia hiyo haitofautiani sana na ile ambayo Mungu hutumia kusema nawe katika mambo mbalimbali. Hivyo tafuta kujua njia ambayo Mungu huwa anatumia kusema na wewe katika mambo mbalilmbali, naam kwa hiyo aweza kusema na wewe hata kuhusu mwenzi wako.

Jambo la pili; Jenga na kuboresha mahusiano yako na Roho Mtakatifu

Roho Mtakatifu ndiye aliyepewa jukumu la kuwa Msaidizi wako hapa duniani katika kufanya maamuzi mbalimbali. Watu wengi leo wanakwama au wanajikuta wamefanya maamuzi mabaya kwa kosa la kutokumshirikisha Roho Mtakatifu awasaidie. Mwambie Roho Mtakatifu nahitaji mwenzi(Mke), nisaidie kumtambua yupi ni wa kwangu, naomba uongozi wako. Roho Mtakatifu kwa hakika atakuongoza katika njia sahihi (Zaburi 32:8). Jambo la msingi ni kwa wewe kuboresha mahusiano yako na yake ili kuruhusu mawasilano mazuri kati yenu. Kumbuka mawasilano hutegemea mahusiano. Na jambo la msingi katika kuboresha mahusiano ni utakatifu na kutenga muda wa kuzungumza naye kwa njia ya maombi na neno.

 Jambo la tatu; Jifunze kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie kuhusu mwenzi wa maisha yako.

Hili ni jambo lingine la msingi kuzingatia. Endapo umeamua kufuata au kutafuta kumjua mwenzi wako kutoka kwa Bwana, basi ni vema ukaruhusu mapenzi yake juu yako yatimie. Wengi huenda mbele za Bwana wakimuuliza jambo hili lakini anapoleta wazo/jibu lake juu ya nani anafaa, wengi wakishamtazama huyo muhusika kimwili na kwa vigezo vyao humkataa na kusema si Mungu. Ni vizuri ukafahamu kwamba, kama Mungu ndiye aliyemleta mtu wa kwanza kwako na wewe kwa sababu zako binafsi ukasema huyu si wa kutoka kwa Bwana, maana yake umemzuia  Mungu asikusaidie kwenye hilo eneo, na hivyo usitegemee kusikia tena kutoka kwake, labda mpaka ujue kosa lako na kuomba toba.

Kumbuka usimuombe Mungu akujulishe mwenzi wako wa maisha wakati moyoni mwako tayari kuna mtu au watu ambao umeshadhamiria kutaka mmoja wao awe mwenzi wako, Mungu hawezi kusema hapo. Ikiwa unataka Mungu ahusike mpe asilimia mia moja hatafanya makosa kama Mwandamu.

Jambo la nne; Jifunze kuomba kimaswali

Najiribu kufikiri kwa nini umeomba tangu Septemba 2008 hadi sasa Mungu asijibu? Kwa ufahamu nilionao katika Kristo nina hakika yeye alisha-kujibu ila wewe ndiyo hukuelewa kwamba alijibu. Nina uhakika huo kwa sababu mtu amwendeaye Mungu kutaka kujua jambo, Mungu humjibu mtu huyo ili kumsaidia asipotee katika jambo hilo.

Naamini shida ipo kwako, huenda jibu ulilokuwa unataka wewe ni kuambiwa fulani ndiye mwenzi wako, kumbe kwa Mungu huenda alikuwa anasema huu si muda wake endelea kuomba maana kwa kila jambo kuna majira yake. Zaidi huenda shida iko kwenye namna unavyoomba na namna unavyopokea, au kuelewa Mungu anapoleta jibu.

Ili kuweza kupata ufumbuzi juu ya jambo hili jifunze kutumia mfumo wa maswali katika maombi yako, naamini utaona matokeo yake. Jifunze kuyatengeneza maombi yako kimaswali, omba huku ukitaka kujua/ukitafuta ufumbuzi wa lile unaloliombea kwa Mungu.

Jambo la msingi katika maombi haya ni kuwa na muda wa utulivu wa kuhojiana na kusemezana na Mungu wako. Kama vile ambavyo unaweza kuongea kwa simu na rafiki yako na mkasikilizana na kujibizana, ndivyo Mungu anavyotaka tujifunze kuwasilama naye. Unaeleza haja yako kwa swali na unampa muda na yeye akujibu. Najua kama hukuwa na mazoea ya kutumia mfumo huu, unapoanza itakusumbua, lakini endelea kufanya hivyo utona matokeo yake. Ili kupata ufahamu zaidi juu ya maombi soma link zifuatazo;https://sanga.wordpress.com/2006/10/23/mafundisho-ya-neno-la-mungu/ na pia https://sanga.wordpress.com/2009/10/29/jifunze-kuomba-kimaswali-3/

Ingawa swali  lilikuwa ni pana, naamini Roho Mtakatifu ameniongoza kujibu kwa namna ambayo kwako Lucas na  hata msomaji mwingine mwenye changamoto kama hii, mtakuwa mmepata ufahamu wa kusaidia. Kama umefuatilia kwa makini katika majibu yangu sijeleza moja kwa moja ni kwa namna gani utamjua mwenza wako, ila nimeelezea mazingira mbalimbali ambayo ukiyazingatia itakuwa ni rahisi kwako kumjua mwenzi wako wa maisha. Kupata ufahamu juu ya njia za Kibilia za kumjua na kumpata mwenzi, wasiliana nami nitakutumia kitabu bado nina nakala chache naamini kitakusaidia pia.  

Mungu akubariki, tuzidi kuombeana.

USHAURI KWA WAJANE

February 16, 2011

Na:Patrick Sanga

Mpenzi msomaji katika category hii ya “maswali na majibu” huwa naandaa masomo yanayolenga kujibu maswali ya wasomaji mbalimbali wa blog hii kama yanavyoulizwa na wasomaji husika kwa njia mbalimbali. Mwezi huu nimeona ni vema nikajibu swali lililoulizwa na dada L  kuhusu wajane. Majibu yangu hayakuzuii wewe msomaji mwingine kuongezea majibu yako juu ya maswali wanayouliza wasomaji mbalimbali.

Swali; Ahsante mtumishi kwa masomo yako mazuri. Mimi nakiri kuwa yamenipa uamsho mkubwa. Naomba niulize, unatushauri nini sisi tulio wajane tena vijana? Mimi ni mjane tokea mwaka 2004. Nina miaka 39 na watoto wawili wakike, naomba uniombee sana Mtumishi. Dada L     

Jibu; Hello dada L na kwa wajane wengine, nawasalimu kwa jina la Bwana Yesu. Pole sana kwa kumpoteza mwenzi wako wa maisha tokea mwaka 2004. Bwana akuwezeshe na kukutia nguvu katika hali yako ya sasa.

Paulo alipokuwa akimfundisha Timotheo kwa habari ya makundi mbalimbali ambayo atapaswa kuyaongoza likiwemo kundi la Wajane alimwambia maneno yafuatayo katika ile 1Timotheo 5.

(3)Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli, (5)Basi yeye aliye mjane kwelikweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku, (6)Basi yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai, (11)Bali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao, maana wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa, (13) Usiwe mvivu, epuka kuwa mchongezi na mdadisi, usinene maneno yasiyokupasa, (14)Basi, napenda wajane ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani, ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu, (15)Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka na kumfuata Shetani. Nakushauri pata muda usome kuanzia msitari wa kwanza hadi wa kumi na sita.

Mtume Paulo alipokuwa akiongea na wandugu wa Korinto kuhusu Wajane pia, aslisema hivi;

1Wakorinto 7:8-9 “Lakini nawaambia wale, wasiooa bado na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilvyo, lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa”.

Baada ya kuangalia maandiko hayo hapo juu nashauri mambo yafuatayo kwako na wajane wote na hasa wale ambao bado ni vijana;

 • Weka tumaini lako kwa Mungu

Katika hali ya kawaida na kibindanamu kuna namna mwenzi wako alikuwa msaidizi mkubwa kwako juu ya mambo mbalimbali pamoja na kuangalia na kutunza familia yenu kwa ujumla. Punde mmoja wenu anapoondoka mambo mengi hubadilika tena kwa kuharibika. Hii ni kwa sababu wajane wengi huwa wanakuwa waliweka matumaini yao kwa mwenzi wake, kwa hiyo kitendo cha mwenzi wake kuondoka anafikiri huo ndio mwisho wa maisha yake mazuri na    ya furaha hapa duniani. Fikra hiyo si sahihi, wewe weka tumaini lako kwa Bwana ukijua yeye ndiye mume wa Wajane na Baba wa yatima, mtetezi aliye hai, hatashindwa kukulisha wala kuwatunza wanao.(Isaya 54:5)

 • Endelea kuishi maisha ya utakatifu

Kuondokewa na mumeo isiwe sababu ya wewe kupunguza jitihada yako katika kumtafuta na kumpendeza Bwana. Endelea kudumu katika maombi na sala mchana na usiku, jizuie nafsi yako kutenda dhambi na zaidi chunga sana matumizi ya kinywa chako. Tumia kinywa chako katika mambo yenye kuleta utukufu kwa Mungu na  sio kusengenya, kuchonganisha na mambo yanayofanana na hayo.

 • Ni vema ukaolewa kama huwezi kujizuia kutenda dhambi.

Mtume Paulo kwa Wakorinto alitoa ushauri kwamba ni vema Wajane waamue kutoolewa au kuoa tena. Lakini kwa Timotheo anamwambia, napenda wajane ambao si vijana waolewe, tena wazae watoe na wawe na madaraka ya nyumbani.

Usije ukafikiri Paulo alijichanganya, hapana. Ushauri wa Wakorinto ulitokana na namna ambavyo Paulo aliona ndoa nyingi zikisababisha watu kumokosea na kumkosa Kristo. Paulo alikutana na watu ambao walijuta kwa nini waliamua kuoa au kuolewa na ndio maana akashauri kwamba basi ni vema kuto oa au kuolewa kama mtu ataweza kujizuia asiwakwe na tamaa na kisha kuanguka dhambini.

Biblia inasema ‘Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe’ (1 Wakorintho7:2).

Hivyo kutokana na umri wako binafsi ningeshauri ni vema ukafikiri na ukachukua uamuzi wa kuolewa tena. Maana ni heri ukaolewa kuliko kushindwa kujizuia nafsi yako ukajikuta unaingia katika dhambi na fedheha. Kama unafikiri unaweza ukaishi katika hali hiyo ya sasa ni bora zaidi, lakini Kibiblia maadam mwenzi wako alifariki uko huru kuolewa tena(Warumi 7:1-3). Kama ukichukua uamuzi wa kuolewa basi usiharakishe, bali muombe Mungu akuongoze na akuunganishe na mtu ambaye atakufaa na zaidi atawapenda watoto wako.

 • Watumie wajane kwelikweli(Wazee)

Pia ni vema ukawatafuta akina mama ambao wamekutangulia katika hali hiyo ya ujane na wameshuhudiwa katika Bwana kuwa waaminifu. Watumie hao  kuomba ushauri kwao, naamini watakushauri vema pia katika Bwana.

 • Endelea kuwa mwaminifu kwa Mungu

Naam mwisho nakushauri endelea kuwa mwaminifu kwa Mungu na Mungu atakuwa mwaminifu kwako. (Zaburi 18:25-26).

 Mungu akubariki naamini ujumbe utakusaidia katika safari hii tuliyo nayo. Bwana akulinde na kukutunza na watoto wako wazuri.

 

UNATEKELEZA WAZO LA NANI UNAPOKUWA NDANI YA JARIBU?

August 24, 2009

 Na. Sanga, P.S 

Andiko la msingi ni Matahayo 27:11-20. 

Mpenzi msomaji ninakusalimu katika jina la Bwana Yesu. Katika mwezi huu nataka nikuulize swali hili nalo ni ‘je unaruhusu/unatekeleza wazo la nani unapokuwa ndani ya jaribu?

Katika andiko letu hapo juu ukisoma utakutana na habari ya Pilato, Yesu, Baraba na wayaudi waliotaka Yesu asulubiwe. Labda nieleze kidogo kwa faida ya wale ambao hawajasoma eneo hili kwenye Biblia. Huu ulikuwa ni wakati Yesu yuko mbele za Pilato akisubiri hukumu yake ya mwisho. Kimsingi Pilato hakuwa tayari kumsulubisha Yesu kwani alionywa na Mungu kupitia mkewe kwamba mtu huyu ni wa haki na kwa hiyo akaamua kutaka kwa jinsi ya kibinadamu kumsaidia asisulubiwe.

Katika majira ya Pasaka ilikuwa ni desturi ya Pilato kumfungulia na kumuacha huru mfungwa mmoja. Pilato huku akijua jinsi watu walivyomchukia mfungwa aliyeitwa Baraba aliwauliza je niwafungulie nani Baraba au Yesu? Baraba alikuwa ni mfungwa hatari  na alifahamika kwa sifa ya uuaji na ujambazi. Baada ya swali hilo Mafarisayo wakaanza kuwashawishi watu kwa kuwaeleza kwamba kubalini afunguliwe Baraba bali Yesu Mnazareti asulubiwe.  Mwishowe ushawishi ule ukakubalika na watu wakataka afunguliwe Baraba na hivyo wakapewa Baraba.

Nilipokuwa nikitafakari habari hii ndipo lilinijia swali hili kwenye ufahamu wangu “unapokuwa kwenye jaribu unaruhusu wazo la nani kwenye maisha yako”? Je la Mungu au la Shetani? Kumbuka jaribu ni lile linalomweka mtu kwenye njia panda katika kufanya maamuzi.   Naamini wewe ni shahidi wa maisha yako, mara kadhaa huenda umejikuta kwenye jaribu kikazi, kimasomo, kindoa, kibiashara, kihuduma, kimahusiano, kijamii, kutoolewa, kutozaa nk. Na kwa ujumla siku zote mtu anapokuwa kwenye jaribu watu wa kumshauri namna ya kukabiliana na changamoto/jaribu husika huwa hawakosekani.

Kila mtu huwa anakuwa na mtazamo wake wa kukushauri tegemeana na aina ya jaribu ulilonalo. Licha ya mawazo kutoka kwa watu lakini pia ndani yako huwa yanakuja mawazo tofauti tofauti ya namna ya kukabiliana na jaribu unalolipitia. Katika mawazo hayo yanayokuja yapo ambayo ni ya kutoka kwa Mungu, Shetani au wanadamu. Na siku zote wazo bora kutekeleza na la kukutoa kwenye jaribu ulilonalo ni wazo la Mungu. 

Swali kwako mpenzi msomaji ni “je unapokuwa kwenye jaribu huwa unaruhusu/unatekeleza wazo la nani”, wazo la Mungu au la shetani?

Siku moja nikiwa nimelala nilisikia sauti karibu mara tatu ikiniambia usipokuwa na wazo jipya huwezi kutoka mahali ulipo”. Kitu cha ajabu nilipoamka niliendelea kuisema hii sentensi karibu siku nzima iliyofuata. Mungu aliileta kauli hii kwani wakati huo kuna jaribu liliniweka kwenye   njia panda. Kwa jinsi ya kibinadamu sikuona ufumbuzi mzuri, na mawazo yaliyokuja yasingeweza kunitoa kabisa kwenye jaribu husika na mengine yangesababisha tatizo/jaribu kuwa kubwa zaidi.

Hivyo Roho Mtakatifu aliponiletea wazo hili nilielewa nini maana yake kwangu. Ndipo nikaanza kutafuta wazo la Mungu la kunivusha kutoka kwenye jaribu husika kwa maombi na kwa kutafakari neno lake  huku nikipima ushauri ninaoupata kutoka kwa watu. Baadae nikapata wazo bora katika Roho Mtakatifu. Nilipolitekeleza niliona mlango uliofunguliwa kwa ajili yangu na nikavuka hapo.

Labda niseme kila wazo lina ushawishi wake maalum, kwa hiyo ni jukumu lako kufikiri vizuri kabla hujachukua maamuzi ya wazo gani ulitekeleze. Wayaudi walishawishiwa na Mafarisayo kukubali afunguliwe Baraba, mtu ambaye alikuwa ni jambazi na muuaji. Na ukiitazama dhana hii kwa mfumo wa mawazo, ina maana walikubali wazo ambalo ni uharibifu na mauti kwenye kizazi chao.  

Zingatia yafutayo ili kutekeleza wazo la Mungu;

Kwanza kumbuka katika Yeremia 29:11, Mungu anayo mawazo mazuri ya kukufanikisha kwa ajili yako. Kwa hiyo ni jukumu lako kuyatafuta.

 • Jifunze kutafuta na kujua lipi/yapi ni mawazo ya Mungu juu ya jaribu linalokukabili.
 • Tafuta wazo la Mungu kwa kuomba, kutafakari neno, kutafuta ushauri kwa watu wengine unaosukumwa kuwaendea, kusoma vitabu, kusikiliza mafundisho nk tegemeana na aina ya jaribu/changamoto unayoipitia wakati huo.
 • Hakikisha unapima kwanza wazo lolote ambalo unalipata, na kipimo chako kiwe neno la Mungu. Angalia kama wazo hilo halipingani na neno la Mungu basi unaweza kulitekeleza.
 • Ukishalijua wazo la Mungu, haijalishi kibinadamu kulitekeleza lina athari gani, maadamu una uhakika kwamba ni la Mungu wewe litekeleze utaona mlango wa kukutoa kwenye jaribu ukijitokeza.
 • Wafilipi 4:6 inatugiza kutokujisumbua kwa jambo lolote, bali tusali, tuombe na kumjulisha Mungu haja zetu pamoja na kumshukuru. Je, unajua ni kwa nini? Hii ni kwa sababu hata ukijisumbua kiasi gani bila kuwa na wazo la Mungu huwezi kutoka mahali ulipo. Kwa hiyo mweleze haja zako naye atakupa mawazo yake nawe utavuka.

Barikiwa sana mpendwa wangu.