UFAHAMU WA KAZI ZA ROHO MTAKATIFU

Na: Patrick Sanga

Ufahamu kuhusu Roho Mtakatifu na kuwa na ushirika na Roho Mtakatifu ni masuala ya lazima kwa mwamini yoyote kama anataka kuishi maisha sawasawa na kusudi la Mungu hapa duniani. Kupitia ujumbe huu naandika kwa habari ya kazi za Roho Mtakatifu ili uweze kuona maeneo au mazingira ambayo unahitaji kumpa nafasi yeye kama Msaidizi akusaidie na kukuonyesha njia uipasayo kuiendea. Lengo la kukufundisha kuhusu kazi zake ni kukuonyesha maeneo ya kiusaidizi ambayo unapaswa kumruhusu, kushirikiana naye na kumtumia akusaidie.

Roho Mtakatifuni Mungu, mwenye nguvu zote, maarifa yote na anayepatikana kila mahali. Yeye anayo nafsi na ameamua kuishi ndani ya mwili wa mwanadamu kwa lengo la kuwa Msaidizi wa mwanadamu kwenye ulimwengu huu wa mwili, ili kumsaidia kuishi katika mapenzi ya Mungu.

Katika Yohana 14:16-18imeandikwa “… Nami nitamwomba baba naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu”.

Mungu ameweka utaratibu kwamba mwanadamu awe mtawala kwenye ulimwengu wa mwili kwa mwili wa damu na nyama. Hivyo, ili kufanikisha makusudi yake kwenye ulimwengu huu wa mwili, Mungu analazimika kumtumia mwanadamu. Ndio, Mungu, anafanya hilo kwa kuingia kwenye mwili wa mtu na kufanya makao yake hapo kupitia Roho Mtakatifu.

Nafasi hiyo inamfanya Roho Mtakatifu kuwa kiungo, tena nguzo muhimu sana kwa ajili ya kazi na makusudi ya ufalme wa nuru kutimia duniani. Hivyo basi,  kuwa na ufahamu wa kazi zake ni suala la lazima kwa kanisa ili liweze kusimama kwenye nafasi yake ipasavyo chini ya jua.

Zifuatazo ni baadhi ya kazi za Roho Mtakatifu ambazo zimeainishwa ndani ya Biblia, karibu sasa tuendelee kujifunza:  

Kufundisha – Yeye niMwalimu, kufundisha ni jukumu lake kuu na ndio maana hivi sasa yeye yupo duniani pamoja nasi ili atufundishie njia ya Mungu. Kufeli au kushindwa kwa mwanadamu kunatokana na mambo mawil nayo ni ujinga na kiburi. Ndio, kutojua kwamba tuna Mwalimu tumruhusu atufundishe na pili ni kutokutii yale anayotuelekeza kutenda (Yohana 14:26).

Kukumbusha – Yeye ni mkumbushaji, kwa kawaida sio rahisi ufahamu wa mwanadamu kushika na kutunza kumbukumbu za mambo yote tunayojifunza au kuagizwa. Sasa katika yale ambayo ni elimu ya ufalme wa mbinguni  na lolote lililo katika mapenzi yake, Roho Mtakatifu ana wajibu wa kutukumbusha ili tusipotee bali tufanye maamuzi sahihi na kuwa na tumaini la kusonga mbele (Yohana 14:26).

Kuongoza – Yeye ni kiongozi, yeye ndiye mwenye kulijua shauri la kuwepo kwetu duniani na njia ya kuiendea, hivyo ana wajibu wa kutuongoza kwenye njia ya kweli yote. Naam, ni ajabu kuona wanadamu wanaenda kwa mwili na kwa akili zao wakati yupo Kiongozi aliye tayari kuwaongoza katika njia sahihi (Warumi 8:14, Yohana 16:13).

Kutuombea – Yeye ni muombezi, licha ya kwamba yeye hutusaidia kuomba kwa sababu hatujui kuomba itupasavyo, jambo muhimu ni kwamba yeye HUTUOMBEA sisi kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Pale tunapofikiri tupo hai kwa sababu tunastahili, ukweli ni kwamba kuna mwombezi anaugua na kulia kila siku juu yetu tupate neema ya kutengeneza njia zetu na kuishi katika mapenzi ya Mungu (Warumi 8:26).

Kufunua mambo, siri au mafumbo – Yeye ni mfunuaji wa mambo, mafumbo au siri za Mungu. Yeye ndiye amepewa heshima na nafasi ya kuchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu na hivyo pekee ndiye mwenye uwezo wa kutufunulia mafumbo na siri za Mungu. Kwake hakuna gumu au siri iliyofichika, mpe nafasi, si tu atakufunulia mambo ya wanadamu bali muhumu zaidi ni yale aliyo nayo Mungu kwa ajili yako chini ya jua, naam mapenzi yake kwako (1Wakorinto 2:10).

Kutia au kuwapa nguvu watu wake watende kazi yake – Roho Mtakatifu huachilia mafuta, upako, neema juu ya watoto wake kwa lengo la kuwatia nguvu ili kutekeleza maagizo na kufanya kazi ya Mungu sambamba na kuzikabili na kushinda changamoto zote ambazo kwa jinsi ya kibinadamu wasingeweza (Matendo ya Mitume1:8, 10:38).

Kutoa au kupasha habari za mambo yajayo – Yeye ni mtoa habari, naam yeye ndiye autangazaye mwisho tangu mwanzo. Daima yeye yupo tayari kutupasha au kutujulisha habari za mambo yajayo kwenye kila eneo la maisha yetu hususani pale tunapokuwa tunatembea katika kusudi la kuitwa kwetu chini ya jua (Yohana 16:13).

Msemaji wa mambo ya Mungu – Ndiyo yeye ndiye Msemaji sahihi wa mambo ya Mungu kwa usahihi, utoshelevu na ukamilifu wake. Pale tunapokuwa njia panda, basi wa kumuuliza ni Roho Mtakatifu. Vivyo hivyo yeye ndiye mwenye uwezo wa kutuwezesha na kutuongoza kunena mambo yaliyotoka kwa Mungu yakaleta wokovu na uponyaji uliokusudiwa kwa watu tofauti na pale tunapotumia akili, ujuzi au hekima zetu (Yohana 15:26, 2 Petro 1:21).

Mtetezi wetu na mfunuaji wa yale tutakayosema – Daima tunapita katika changamoto nyingi, hata hivyo Mungu ametupa Roho Mtakatifu atusaidie, atusemee, atutetee na kutufunulia hata jinsi ya kujieleza pale tunapokuwa kwenye mazingira tata au mbele za baraza kwa sababu ya kulitumikia kusudi lake. Ndio, maadam unamtumikia kwa uaminifu usiangaike kujitetea, mpe nafasi akusaidie (Marko 13:11).

Kuuhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, haki na hukumu – Katika hali ya kawaida yapo mambo ambayo watu wengi husema hawajui ikiwa ni sahihi au sio sahihi kuyafanya. Sasa kazi mojawapo ya Roho Mtakatifu ni kutuhakikishia, kutuonyesha, kutujulisha kilicho sahihi na kisicho sahihi, haki na uovu na kwa kwamba katika hayo kuna hukumu. Hivyo mwanadamu hatakuwa na la kujitetea endapo atafia dhambini, hivyo mpe nafasi Roho Mtakatifu akusaidie (Yohana 16:8).

Hitimisho – Mpendwa msomaji, kupitia ujumbe huu nimekuonyesha nafasi na kazi za Roho Mtakatifu kwako. Kazi hizi za Roho Mtakatifu zinatufikisha mahali pa kujua kwamba jukumu lake kubwa ni kuwa Msaidizi wa mwanadamu kwenye kila nyanja au eneo ambalo Mungu alijua mwanadamu atahitaji msaada wake.

Ukweli ni kwamba, BWANA hategemei kuona mwanadamu anakwama au kufeli kwenye eneo lolote katika kulitumikia kusudi la Mungu awapo chini ya jua. Hivyo ni jukumu lako kuboresha uhusiano wako na Roho Mtakatifu na kumpa nafasi akusaidie. Ndio, ni jukumu lako kushirikiana naye na kumpa nafasi akusaidie ndivyo utakavyofanikiwa katika mambo yote, naam tukiishi kwa roho na tuenende kwa Roho.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili Bwana wangu.

Nawe ukaniambia… Utaiinua Misingi ya Vizazi Vingi… (Isaya 58:12)

2 comments

Leave a comment