Archive for September 2014

NAMNA YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA UJANA (Sehemu ya mwisho)

September 26, 2014

Na: Patrick Sanga

c

Katika sehemu ya kwanza tuliangalia changamoto kubwa tano ambazo zimekuwa zikiwakabili vijana na hivyo kuathiri uhusiano wao na Mungu. Ili kusoma sehemu ya kwanza kwa wewe ambaye hukusoma bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2014/09/07/namna-ya-kukabiliana-na-changamoto-za-ujana-sehemu-ya-1/ Katika sehemu hii ya pili na ya mwisho nitaeleza mbinu za kumsaidia kijana kuzikabili na kuzishinda changamoto tulizoziangalia awali. Naam fuatana name sasa tuendelee…

Biblia katika Mithali 1:4 inasema ‘Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na hadhari. Pengine huu ni msatri wa ujumla wenye lengo la kumsaidia kijana awe mwenye tahadhari, mwangalifu, na ajifunze kufikiri kibiblia na kuchukua tahadhari kubwa kabla kabla ya kutenda, naam huku akitumia vema maarifa apatayo kuzishinda changamoto zenye kumkabili kila siku. Zifuatazo ni baadhi ya mbinu zitakazomsaidia kijana kuzikabili changamoto mbalimbali;

  • Kijana atafute kujua nini kusudi la Mungu kumleta duniani

1

 

Wafilipi 2:13 inasema ‘Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema’. Tambua kwamba kabla hujazaliwa alikujua na akakuwekea kusudi lake unalopaswa kuliishi, maana umeumbwa ili uyatende mapenzi (kusudi) ya Mungu hapa duniani. Naam ufahamu wa kusudi la Mungu kwako utakusaidi kuishi kwa malengo na hivyo kukuepusha na kuifuatisha namna ya dunia hii.

Katika Warumi 12:2 imeandikwa ‘Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza na ukamilifu’. Kijana mwenye kujua wajibu wake duniani katika kulitumikia kusudi la Mungu atajizuia na kujiepusha na makundi mabaya, kuipenda dunia, atatumia vizuri fursa ya teknolojia kwa utukufu wa Mungu na kuwa na matumizi mazuri ya muda.

Kijana huyu atatumia muda na nguvu zake ipasavyo katika kufanya kazi zenye kumsaidia kujikimu kimaisha ikiwa ameajiriwa au amejiajiri, na ambaye anasoma atazingatia masomo kwa sababu anajua anakokwenda, hivyo hataruhusu mambo ya kipuuzi yaharibu ndoto yake (Waefeso 5:15-17 na Mhubiri 12:1). Hivyo ni jukumu lako kumuuliza Mungu ili upate kujua kwa nini upo duniani. Hata hivyo, wokovu, ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu, kuomba kimaswali na vipawa ulivyopewa ni funguo muhimu za kukusaidia kuelewa kusudi la Mungu kwako.

  • Kijana ajifunze kuishi kwa imani

2

 

Waebrania 10:38 inasema ‘Lakini mwenye haki ataishi kwa imani; Naye akisi-sita, roho yangu haina furaha naye’. Pia katika 1 Yohana 2:14 imeandikwa ‘Nimewaandikia, ninyi vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi, mmemshinda yule mwovu’. Ili aweze kuishi kwa imani ni lazima kijana adumu kuongeza ufahamu wa neno la Mungu na kulitenda. Kwa kuwa chanzo cha imani ni kusikia na kusika huja kwa neno la Kristo (Warumi 10:17).

Neno la Mungu likikaa kwa wingi litaumba imani kubwa ndani yake ambayo itamsaidia kushinda kila changamoto zinazolenga kumuondoa kwenye imani husika. Maarifa yatokanayo na neno la Kristo yatamjengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kuzikabili changamoto za ujana. Naam kuishi kwa imani kutamsiaida kijana kudumu kuwa mwaminifu na kudumu kumpenda Mungu bila kuifuatisha namna ya dunia hii na tamaa zake (Mitahli 12:1a, 1 Timotheo 4:13 – 16, Ayubu 22:19 na Waefeso 5:6).

  • Kijana ajifunze kuenenda kwa roho

3

Kuenenda kwa roho ni wito wa Mungu kwa vijana leo ili waweze kuzishinda changamoto za ujanani. Biblia katika wagalatia 5:16 inasema ‘Basi nasema enendeni kwa roho, wala hamtatimiza kamwe tamaa za mwili’. Kuenenda kwa roho ni kumpa nafasi Roho Mtakatifu ya kuongoza maisha yako sawasawa na mapenzi ya Mungu kwako.

Katika kuenenda kwa roho, siku zote, kijana anapaswa kutafakari mambo yoyote yaliyo ya kweli, ya haki, safi, yenye kupendeza, yenye sifa njema na yenye kupendeza      (Rejea Wafilipi 4:8 na Warumi 8:5). Ukweli ni kwamba kijana hawezi kuzikwepa kabisa changamoto za mwili kwa sababu mwili ni sehemu ya maisha na siku zote mwili hutamani ukipingana na roho (Yohana 3:6 na Wagalatia 5:16). Hivyo ni lazima kijana ajifunze kuenenda kwa roho ili asizitimize tamaa za mwili. Ili kusoma ujumbe wa namna ya kuenenda kwa Roho bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2007/02/06/roho-mtakatifu-2/ mahali ambapo nimeandika kwa upana jambo hili.

  • Kijana ajifunze kuruhusu mapenzi ya Mungu yatime kuhusu mwenzi wa maisha.

4

 

Najua vijana wengi sana wamejiwekea vigezo vya wenza ambao wangependa waje kuishi nao kama wanandoa. Ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya vigezo vyao ni vya kimwili na ni kinyume na mapenzi ya Mungu kwenye maisha yao. Fahamu kwamba licha ya wewe kuwa na vigezo vya mtu unayefikiri anafaa kuwa mwenza wako na Mungu naye naye ana vigezo vya mtu anayejua anayekufaa. Naam suala la nani atakuwa mwenza wako kwa Mungu ni kipaumbele muhimu sana na ndiyo maana unapaswa kumshirikisha kwa asilimia zote ili akuongoze kufanya maamuzi sahihi (Mithali 19:14, Isaya 55:8, Mithali 16:1 na Yeremia 29:11).

Ni muhimu kijana awe makini kuhusu maamuzi anayofanya katika kitafuta mwenzi wa maisha ili yasije kuharibu kusudi la Mungu juu yake. Kijana anapaswa kujiepusha na makosa mbalimbali katika kutafuta mwenza ikiwa ni pamoja na; Kutokumshirikisha Mungu katika kutafuta mwenzi wa maisha, kufanya maamuzi ya mwenzi wake atakuwa nani ndipo aanze kuomba, Kuficha dhambi, kuwa na vigezo binafsi visivyo sahihi, na kufanya maamuzi kabla ya wakati.

Naam kuhusu vijana walioko kwenye ndoa, ni muhimu vijana hao wakajua kwamba ndoa ni wito wa mapungufu na kwamba hakuna isiyo na mapungufu, hivyo katika ndoa suala muhimu ni kila mmoja kusimama vema kwenye nafasi yake na kuchukuliana katika mapungufu yenu huku mkilenga kutafuta na kutenda makusudi ya Mungu ya kuwaunganisha.

Changamoto ni sehemu ya maisha kwa vijana, na madam tupo katika dunia hii, hakuna namna kijana atishi bila kuzikabili changamoto husika, naam jambo muhimu kijana ni kuwa makini na maisha yake akijua nafasi yake katika ufalme wa Mungu ili adumu kuyatenda mapenzi ya Mungu katika siku zake. Ni imani yangu kwamba somo hili limekuongezea maarifa katika kuzikabili na kuzishinda changamoto mbalimbali za ujanani.

Mungu wangu na akubariki na kukusaidia maana ndiye aliyeniambia ‘…utaiinua misingi ya vizazi vingi…’ (Isaya 58:12)

Utukufu na heshima vina wewe Yesu! Wastahili BWANA.

NAMNA YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA UJANA (Sehemu ya 1)

September 7, 2014

1Na: Patrick Sanga

Shalom, neno changamoto linaweza kuwa na maana kadhaa, katika somo hili nimefafanua changamoto kama ushindani au mashindano baina ya pande mbili au zaidi, kila upande ukidai uhalali wa kile unachokiamini na hivyo kushawishi upande wa pili ukubaliane na kukifuata kile unachokiamini. Kutoka kwenye dhana ya vita vya kiroho (Waefeso 6:10), Shetani kama mfalme wa giza ndiye mwenye kuzileta changamoto mbalimbali dhidi ya wana wa Mungu kwa nia ya kuwaondoa kwenye nafasi zao za ki-Mungu na hivyo kuwatumia kufanikisha makusudi yake ya ufalme wa giza na mwishowe kuwaharibu kabisa. Zifuatazo ni sehemu ya changamoto kubwa zenye kuwakabili vijana;

  •  Kuipenda dunia (1Yohana 2:15 -16).

Ule mstari wa 15 unasema ‘Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia, Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake’. Sisi sote leo tu mashahidi juu ya nama ambavyo vijana wengi, wanavyovutwa na nguvu ya dhambi inayotenda kazi duniani kupitia taama ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima. Shetani kwa kutumia mambo hayo amewafanya wengi sana kuipenda na kuifuatisha namna ya dunia hii, wasijue kwamba nia ya mwili ni mauti na wale waufutao mwili hawawezi kumpendeza Mungu (Warumi 8:5-6)

  •  Kufanya maamuzi muhimu yahusuyo maisha

4

Vijana wengi wapo katika rika ambalo wanahaja ya kuoa au kuolewa na wengine bado wanasoma katika nagzi mbalimbali. Katika nyakati za sasa imeakuwa ni changamoto kubwa sana kwa kijana kumpata mwenza shaihi wa maisha sambamba na kujua nini asome ambacho kina uhusiano mkubwa na wito wa kusudi la Mungu katika maisha yake. Tambau kwamba (a) Mungu anapokupa fursa ya kusoma, si suala la kusoma bali kusoma kitu ambacho kipo connected na future ambayo Mungu amakuandalia (b) si kila mwanamume/mwanamke anafaa kuwa mwenza wako wa maisha. Naam ile kwamba wako wengi ambao wangetamani kuishi na wewe kama mke au mume ni ishara kwamba wengi wao si wenza sahihi wa kuishi na wewe. Katika kutafuta na kupata mwenza wa maisha vijana wengi leo wanatumia akili zao bila kumshirikisha Mungu ipasavyo, wasijue kwamba ndoa isiyounganishwa na Mungu, ni kikwazo kikubwa katika kulitumikia shauri la BWANA Mungu wao.

  • Kuishi kwa amani katika ndoa 

Wanandoa

Hii inahusu wale ambao walishaoana. Kwa zaidi ya miaka saba katika kufundisha na kuandika masuala yahusuyo mahusiano ya wanandoa nimejifunza na kuthibitisha kwamba ndoa nyingi za vijana zina matatizo makubwa kuliko wengi wanavyofikiri juu ya ndoa hizo ambazo wanaamini ni changa. Binafsi nimeshuhudia ndoa nyingi ambazo ni chini ya miaka mitano lakini wanandoa husika hawalali kitanda kimoja tena, hawaaminiani tena, hawapeani unyumba tena nk. Naam kuishi vema na mwenza limekuwa gumu sana kwa wanandoa wengi ambao ni vijana na baadhi yao wanajuta kwa nini walioa au kuolewa.

  • Matumizi ya teknolojia (mtandao)

2

Kijana mwenzetu Danieli alionyeshwa kwamba katika siku za mwisho maarifa yataongezeka sana, jambo ambalo ni dhahiri katika kizazi chetu bila shaka. Sote tu mashahidi juu ya namna vijana wanavyotumikishwa na nguvu ya matumizi mabaya ya mitandao mbalimbali ya kijamii. Sote tunaona namna vijana wengi wanavyotumia muda mwingi kusoma na kuangalia vitu visivyofaa kwenye mtandao na mbaya zaidi tunaona ni kawaida. Kadri kijana anavyaongalia vitu vichafu ndivyo anavyoyachochea nguvu ya dhambi na kutenda mabaya ndani yake, naam ndivyo anavyoingiza roho chafu za kila namna ndani yake.

  • Kijana na maisha/uchumi

Hali ngumu ya kiuchumi inaleta ushawishi kwa vijana kujiingiza kwenye mambo ambayo yanaharibu mahusiano yake na Mungu. Naam wapo ambao imefika mahala wameamua kuingia kwenye biashara haramu za madawa ya kulevya, zinaa, uasherati, kutamani kuishi maisha ya kuiga, na mbaya zaidi hata wale ambao wanakiri kumpokea Yesu nao wanaishi maisha ambayo hayana ushuhuda makazini mwao, mtaani mwao nk hususani linapokuja suala zima la uaminifu, mahusiano na fedha.

Pengine zipo changamoto nyingine, lakini hizi tano nilizoziandika ndizo ambazo nimeona umuhimu wake zaidi kuzifundisha kwa kuwa zina athari kubwa sana sit u kwa vijana wenyewe bali zaidi kwenye ufalme wa Mungu wetu. Katika sehemu ya pili nitaanza kwa kukuonyesha ni kwa namna gani kijana anaweza kuazikabili changamo husika.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA!