RUHUSU MAPENZI YA MUNGU YATIMIE KUHUSU MWENZI WA MAISHA YAKO.

 Na: Sanga P.S.

Najua yumkini upo njia panda kwa habari ya kuoa au kuolewa. Si kwa sababu hakuna mtu wa kuoa au kukuoa, bali ni kwa sababu kila anayekuja ni tofauti kabisa na kile ambacho wewe unapenda na unafikiri pia ni mapenzi ya Mungu iwe utakavyo. Huenda kibinadamu kuna sifa/vigezo ambavyo ulijiwekea vya mtu ambaye ungependa kumuoa au kuolewa naye, lakini kila unapoomba unaona mtu anayekuja ni tofauti kabisa na vile ulivyotaka wewe. Na unapoomba zaidi kumhoji Mungu anakuhakikishia kwamba huyohuyo ndiye mtu wa mapenzi yake.

Hukuishia hapo umeshirikisha na wapendwa wenzako au hata watumishi wengine wameomba nao wamethibitisha huyo ndiye mtu wa mapenzi ya Mungu kwako. Kila unapojitahidi kufikiri kumwacha unakosa amani. Mimi ninakushauri inapofika mahali kama hapo we ruhusu tu mapenzi ya Mungu yatimie kwako. Zipo sababu nne za msingi  zinazonifanya nikushauri hivyo;

  • Mapenzi ya Mungu ndio utimilifu wa kusudi lake kukuleta wewe duniani.

Haukuja duniani kwa sababu ni kawaida ya wanadamu kuzaa, bali ni kwa sababu ni Mungu alikusudia wewe uzaliwe.Hii ina maana lipo kusudi la Mungu kukuleta duniani. Na ili kusudi lake liweze kufikiwa ni lazima ujifunze kuishi maisha ya mapenzi yake. Uishi ili kutimiza mapenzi yake hapa duniani.

Ni mapenzi ya Mungu pia kuhakikisha unaoa/kuolewa na mtu ambaye anajua mtasaidiana katika kutekeleza makusudi yake hapa duniani. Kwa hiyo si suala la kuoa au kuolewa unavyotaka, bali ni kuoa au kuolewa kwa mapenzi yake.

  • Mapenzi ya Mungu si lazima yakubaliane/yaendane na ya kwako.

Ni muhimu ujue kwamba mapenzi ya Mungu si lazima yaendane na ya kwako. Na hii ni kwa sababu mawazo yako si mawazo yake na njia zake si njia zako (Isaya 55:8). Jua kabisa mapenzi ya Mungu si lazima yakupendeze, yakufurahishe au yalinde heshima yako.

  • Kuna nyakati ambazo mapenzi ya Mungu kuyapokea ni machungu, yanaliza, yanafadhaisha, yanaogopesha.

Katika kuyakubali au kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie wakati mwingine     yanaweza kuwa machungu, kukufadhaisha, kukuliza, kukuumiza, kukuogopesha au hata kukuabisha kwa jinsi ya kibinadamu.

  • Mapenzi ya Mungu yanalenga kuleta heshima na utukufu kwake.

Ingawaje yanaumiza, kufadhaisha au hata kuaibisha kwa jinsi ya kibidamu /kiheshima/kimahusiano/kijamii /kiuchumi nk. Na hata kama  kwako yana athari kiasi gani uwe na uhakika mapenzi ya Mungu yanalenga kuleta heshima na utukufu kwake, hii ina maana HAYO NDIYO MAPENZI YAKE na si ya KWAKO. Tunapoomba kusema mapenzi yako (Mungu) yatimizwe ina maana mapenzi/matakwa ya kwetu (wanadamu) yasitimie.

Hebu tuangalie mifano kadhaa ndani ya Biblia;

Mfano wa Yakobo Mwanzo 29:15-31.

Hii ni habari ya Yakobo alipokwenda Harani kwa Labani nduguye. Labani alikuwa na binti wawili, mkubwa aliitwa Lea na mdogo aliitwa Raheli amabye alikuwa na uso na umbilie zuri. Raheli ndiye ambaye Yakobo alimpenda na alikubali kutumika kwa miaka saba ili apate kumuoa. Baada ya miaka saba, Yakobo alipewa Lea ambaye hakumpenda kama mke bali alimpenda Raheli. Ingawa zilipopita siku saba ndipo alipopewa na Raheli kama mke wa pili.

Nikuulize swali, je Yakobo angeambiwa atumike miaka saba kwa ajili ya kumpata Lea, angekubali? Je unafikiri ni kwa nini Mungu aliruhusu Yakobo  mtumishi wake kufanyiwa hili? Sababu kubwa ni hii, ilikuwa ni mpango/mapenzi ya Mungu Yakobo amuoe na Lea pia. Hii ni kwa sababu ya umuhimu wa watoto aliowazaa ukihusianisha na uzao/ukoo wa Bwana wetu Yesu Kristo. Namaanisha kupitia Lea, Yakobo alizaa naye watoto wane, mmoja wao aliitwa  Yuda. Ukifuatilia ukoo wa Yesu Kristo utalikuta jina la Yuda linajitokeza (Mathayo 1:2). Kwa hiyo japo Yakobo hakumpenda Lea kabisa lakini Mungu alitaka na akajua kupitia wao atazaliwa Yuda ambaye ni kiungo muhimu katika uzao wa Yesu Kristo.

Mfano wa nabii Hosea – Hosea 1:1-4

Mstari wa pili unasema ‘… Bwana alimwambia Hosea enenda ukatwae mke wa uzinzi…’ Ukisoma hii habari yote utaona jinsi Mungu alivyomwagiza Hosea kwenda kuoa mawanamke mzinzi na aliyekubuhu kwenye dhambi hii. Sasa kwa jinsi ya kibinadamu haikuwa rahisi kulikubali. Lakini kwa sababu ilikuwa ni jambo la MAPENZI YA MUNGU ili mlazimu akubaliane nalo hata kama yeye hakutaka. Na ukiendelea kusoma sura za mbele utaona fundisho na uponyaji ambao ulitokea kwa watu wa taifa la nabii Hosea kutokana na utiifu wake katika mapenzi ya Mungu.

 Mfano wa nabii Samweli – 1Samwel 16:1-13.

Hii ni habari inayoelezea agizo la Mungu kwa Samweli kwenda kwenye nyumba ya Yese kumtia mmoja wa watoto wake mafuta kuwa mfalme wa Israel baada ya Mfalme Sauli kuasi. Yese alikuwa na jumla ya wana nane wa kiume, Mkubwa  wao aliitwa Eliabu na mdogo aliitwa Daudi. Sasa Samweli alipofika kwa Yese, Yese aliwaita watoto wake wote isipokuwa Daudi aliyekuwa anachunga kondoo wa babaye, akaanza kuwapitisha kwa Samweli ili amtie mafuta yule ambaye ndio mfalme.

Alipopita mtoto wa kwanza, nabii Samweli akasema moyoni mwake Yakini masihi wa Bwana yupo hapa mbele yake, kwa lugha nyepesi alisema yamkini huyu ndiye Mfalme ninayepaswa kumtia mafuta. Je Mungu alimjibu nini alipowaza hivyo moyoni mwake. Mungu alimwambia ‘usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama mwanadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo’. Mwishowe walipita watoto wote saba na Bwana akawakataa, hadi alipofika Daudi aliyetiwa mafuta.

Jifunze yafuatayo kutoka kwenye mifano hii mitatu;

  • Upo duniani sasa kwa ridhaa/ruhusa/mapenzi ya Mungu.
  • Na kama upo kwa ridhaa yake, ni lazima uishi kwa uongozi wake (Zab 32:8).
  • Thamani ya maisha yako ipo katika kuyatenda mapenzi ya Mungu.
  • Ni kipaumbele (priority) cha Mungu kujua nani atakuwa ni mkeo au mumeo. Sio suala la kuoa au kuolewa unayotaka wewe.
  • Mtazamo wako kuhusu mkeo au mumeo sio mtazamo wa Mungu. Ndoa yoyote anayo iunganisha Mungu ameshaiangalia mpaka mwisho wake.
  • Hivyo anapokupa mtu wa aina fulani, hata kama haendani na vigezo vyako, kumbuka lengo lake sio kukukomoa au kukuhuzunisha bali ni kuhakikisha anachotaka/mapenzi yake na si ya kwako yanatimia.
  • Smweli na Yakobo walitaka kukosea kwa sababu ya maumbile na mvuto wa sura kwa nje. Angalia sababu kama hizi zisikufanye ukaharibu mahusiano yako na Mungu na hivyo kukwamisha makusudi yake duniani.
  • Japo lilikuwa ni jambo gumu kwa Hosea kulikubali kibinadamu, yeye alitii na akabarikiwa kwa kulitumikia shauri la Bwana katika kizazi chake.
  • Ni mfano wa mfinyanzi na vyombo alivyovifanya. Mfinyazi ndiye anayejua sababu na matumizi ya chombo alichokifanya. Kazi yake huyu mfinyazi ni kuhakikisha lengo la ubunifu/uumbaji wake linafikiwa.
  • Na Mungu ndivyo alivyo, yeye ndiye aliyekufanya na anajua unachotakiwa kufanya hapa dunani, kazi yake ni kuhakikisha anakuongoza na kukuweka kwenye mazingira ya kusudi lake kupitia wewe kufanikiwa. Sasa mazingira au uongozi huo ni pamoja na kuhakikisha unaoa au kuolewa na mtu wa mapenzi yake.
  • Mtu wa mapenzi yake anaweza akawa tofauti na ulivyokuwa unataka. Ndugu yangu inapofika uko mahali kama hapa “the only option/alternative ni kuruhusu mapenzi yake yatimie na si kulazimisha yako kutimia”. This means there is no an option or alternative, you cannot escape it (Je unakumbuka habari za Yona, au Yesu pale Gethesemane?). Let his will be made in your life i.e.   Totally submit yourself to his will.
  • Usipokubali wakati una hakika hayo ni mapenzi ya Mungu kwako maana yake umeasi, ukiasi unatafuta matakwa yako na si yake. Mungu hata kulazimisha kuyatii mapenzi yake ila atakushauri kwa njia mbalimbali na mojawapo na mafundisho kama haya. Ukikataa ushauri wake ujue huko unakoenda yeye/uwepo wake hauko pamoja na wewe. Je unajua gharama ya kukosea au kutokutii mapenzi ya Mungu katika hili? Waulize wanandoa waliokosea ndio utajua madhara yake.
  • Naamini ujumbe huu umekuongezea maarifa na ufahamu wa kukusaidia katika kufanya maamuzi. Zaidi ni imani yangu kwamba kama ukijua hakika haya ni mapenzi ya Mungu kuhusu mwenzi wako basi utahakikisha yanatimia. Haijalishi hayuko unavyotaka, ndugu zako, ukoo wako, kanisa au hata Mchungaji wako hawamtaki, kama unahakika ni mtu wa mapenzi ya Mungu mpendwa nakushauri RUHUSU MAPENZI YA MUNGU YATIMIE, KINYUME CHA HAPO NI MAJUTO.
  • “Asomaye na afahamu, msukumo ambao nimeupata kuhusu kuandika ujumbe huu haukuwa mdogo, ni kama nilikuwa naambiwa hakikisha ujumbe huu unakamilika haraka iwezekanavyo ili kuwapa maarifa haya watu wangu”.

 Mwenye sikio na asikie lile ambalo Roho wa Yesu anasema na kanisa. Amen.

19 comments

  1. Bwana asifiwe sana!nimara ya kwanza kuingia hii blog,lakini nimekuta msg ambayo imenigusa sana,yaani kama ulikuwa kwenye mawazo yangu.Mungu ni mwema na umenifariji sana!BWANA WETU YESU ATUKUZWE!!!.

    Like

  2. Bwana wetu YESU KRISTO ASIFIWE SANA MI NAAMINI KAMA MUNGU ANATAKA KUKUFIKISHIA UJUMBE LAZIMA UKUPATE TU IWE KWA KUKUONYA KWA KUKUBARIKI KWA KUKUFUNDISHA HUWEZI KUJIFICHA NA USO WA MUNGU.ASANTE MUNGU WETU KWA KUTUFUNDISHA.

    Like

  3. Shalom,

    Ni ujumbe mzuri wenye kufundisha na kuelimisha, Mungu azidi kukutumia, ila ongeza bidii ya kutangaza hii brog maana haijulikani kabisaa, mwenyewe nimeipata ktk pita pita kwenye mitandao.

    Huu ujumbe ulioandika ni kweli mtupu mi nina mifano mingi sana ya wapendwa walioamua kufuata matakwa yao na kuacha ya Mungu, Pia ya waliotii ya Mungu na matunda yake wanayaona.

    Tusinga’ang’anie tu kuangalia sura, kazi ,elimu, n,k tuangalie Mungu anataka nini Hasa kwa Watumishi na yeyote anaeona ana nia ya Kumtumikia Mungu. Kama una nia ya dhati ya kumtumikia Mungu na haujaingia kwenye ndoa, basi yaruhusu mapenzi ya Mungu yatimie, hata kama upo kwenye uchumba na umegundua sio mpango wa mungu nakushauri uvunnje.

    Kufanya huduma na mwezako ambaye sio mpango wa Mungu utakuwa umebeba donda ngugu, wengi wanalia.,wengi walikuwa na huduma nzuri sana baada ya kuingia katika ndoa na huduma zimekufa, sasa jiulize Mungu anakupa mwenza wa kuuwa huduma, maana tunaambiwa utumishi wetu ni mapaka kristo akija, sasa wenzetu walipo oa au kuolewa na kwaya wakaacha, maombi wakaacha, mikesha wameacha na huduma nyingi. hebu jiulize ??

    Tutafanya huduma mpaka yesu atukute shambani, ndiyo huduma zitaishia hapo, sio huduma iishie na ndoa, tuwe waangalifu

    ubarikiwe mtumisha kwa huduma njema.

    Like

  4. Bwana wetu Yesu Kristo asifiwe. Ujumbe huu wa ndugu yetu Sanga ni muhimu sana kwa kila anayetaka kuingia kwenye ndoa yenye baraka, iliyojaa furaha na amani. Tatizo kubwa la mwanadamu anaangalia mambo kwa nje na harusu mapenzi ya Mungu yatizwe kwenye kila kitu anachotaka kukifanya, ingawa kila siku mwanadamu huyu huomba mapenzi ya Mungu yatimie kupitia ile sala aliyotufundisha Bwana wetu Yesu Kristo. Hakika sala hiyo imekuwa ya kukariri tu na watu hawachukui nafasi au hawatilii umuhimu wa kuitafakari kwa undani kwa nini Yesu alitaka tujue umuhimu ya mapenzi ya Mungu kutimizwa kwanza kwetu kabla ya mambo mengine, (Mathayo 6:9……). Yote hiyo alitaka kusudi lake la kutuleta sisi hapa dunia lipewe kipaumbele cha kwanza, na kumbuka siku zote kusudi limefungwa na muda (the purpose of God is timed or time framed), hivyo tusicheze nalo kabisa. Unahitaji kujua kwa uhakika kipindi hiki Mungu ana kusudi gani na wewe ili ulitimize kikamilifu. Yapo mengi sana ya kuzungumza kuhusu ujumbe huu lakini naomba niishie hapo ili na wengine watoe comment zao. Bwana Yesu aliye mfalme wa amani awabariki wote na Roho Mtakatifu azidi kutupa ufahamu wa kulijua kusudi la Mungu kila wakati kwenye maisha yetu.

    Like

  5. God bless you ma dear bro, hakika nimefurahishwa sana na ujumbe huu mzuri ambao kwa hakika unatufanya vijana kama sisi ambao bado hatujafikia ngazi/daraja hilo la ndoa kuendelea kujidhatiti na kujipanga vizuri huku tukimtanguliza Mungu kwani yeye pekee ndiye anayetujua vyema
    kaka mimi napenda kukutia moyo kwamba kazi yako ni njema na MUNGU wangu wa mbinguni azidi kukuwezesha na kukupa mafunuo zaidi kwaajili ya kazi yake.
    jipe moyo mkuu BWANA yu pamoja nawe. UBARIKIWE

    Robert

    Like

    • Mungu akubariki sana kaka kwa ujumbe mzuri sana ambao umeutoa kwa vijana ambao bado hatujaolewa, kweli tutaomba Mungu atuongoze katika mapenzi yake katika kutafuta mwenzi. UBARIKIWE

      Like

  6. Shalam

    BWANA WETU YESU KRISTO APEWE SIFA! HAKIKA VIJANA TUJIHADHARI NA MAPENZI YETU KATIKA UCHUMBA BADALA YA KUTIMIZA MAPENZI YA MUNGU. MUNGU AKUBARIKI MTUMISHI KWA MAFUNZO HAYA UTAFIKIRI ULIKUWA NAMI: HAKIKA ROHO WA BWANA ANAKUTUMIA MTUMISHI MUNGU AKUBARIKI SANA.

    IWENI MAKINI VIJANA WENZANGU AMBAO MPO KWENYE SAFARI HII YA KUPATA WENZA WA MAISHA MWENZENU SASA NIPO KWENYE REHEMA SIPENDI NANYI MLIPE GHARAMA KAMA MIMI NAYO LIPA MKIJUA MPANGO WA MUNGU ACHENI UTIMIE: TUOMBEANE AMENI.

    Like

  7. Shaloom, mapendo Mungu ana makusudi nawe hivyo usiwe mwepesi wa kukata tamaa. OMBA Kila wakati naye hatakuacha. Ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, bisheni nanyi mtafunguliwa.

    Like

  8. Bwana wetu Yesu asifiwe. nimebarikiwa na ujumbe wako Mungu aendelee kukutumia kutoa lile lililo kusudi lake kwa vijana na watu wazima hata watoto Mungu akubariki

    Like

  9. ulichokisema ni cha kweli,Lakini kabla ya kufika mbali na huyo mwenzi wako,wahusika watambue kuwa nguvu ya asili,(baraka,au laana)Ina nguvu ya kuendeleza au kuvunja ndoa,Nikiwa na maana kuwa kama upande wa mwanaume au mwanamke kuna mwenendo wa kuachana au kusaritiana sana au watu kuchukuana na kuishi pamoja kabla ya kupata baraka za wazazi ua kanisa/msikiti.Basi hata wewe mwanamke/mume ipo siku utaachwa kama usipochukua hatua ya kuvunja laana za koo juu ya roho za maangamizi ya mahusiano mema.maombi ya nguvu ni lazima yafanyike ili kulinda huo uhusiano,yaani uliza vizuri historia za mahusiano upande wa mwenzi wako,kumbuka laana ni vizazi vinne vya wamchukiao MUNGU,sasa hujui nani huko kwenu aliwahi kumchukia MUNGU,pia vunja roho za kutofunga ndoa huko kwenu.

    Like

  10. bwana yesu asifiwe mtumishi wa mungu, ujumbe wako umenitia moyo sana katika maisha yangu ukizingatia niko katika kipindi kigumu sana cha mahusiano na mturajiwa wangu katika ndoa.nilichojifunza hakuna haja ya kulazimisha kama mungu amepanga ipo siku na mimi nitapata mtu mungu aliyenipangia.
    kama ni yeye aminikimbia kwa mtazamo wa wanadamu basi namwachia mungu atanionyesha njia ya kufanya.

    mungu akubariki sana mtumishi uzidi kutufundisha kadri mungu anavyokufunulia.

    Like

  11. Amen mtumishi wa bwana nimejifunza mengi na naomba Mwenyezi Mungu anisamehe kwa yote na naachilia mapenzi yake yafanyike katika maisha yangu.Barikiwa mtumishi

    Like

Leave a comment