Archive for August 2009

UNATEKELEZA WAZO LA NANI UNAPOKUWA NDANI YA JARIBU?

August 24, 2009

 Na. Sanga, P.S 

Andiko la msingi ni Matahayo 27:11-20. 

Mpenzi msomaji ninakusalimu katika jina la Bwana Yesu. Katika mwezi huu nataka nikuulize swali hili nalo ni ‘je unaruhusu/unatekeleza wazo la nani unapokuwa ndani ya jaribu?

Katika andiko letu hapo juu ukisoma utakutana na habari ya Pilato, Yesu, Baraba na wayaudi waliotaka Yesu asulubiwe. Labda nieleze kidogo kwa faida ya wale ambao hawajasoma eneo hili kwenye Biblia. Huu ulikuwa ni wakati Yesu yuko mbele za Pilato akisubiri hukumu yake ya mwisho. Kimsingi Pilato hakuwa tayari kumsulubisha Yesu kwani alionywa na Mungu kupitia mkewe kwamba mtu huyu ni wa haki na kwa hiyo akaamua kutaka kwa jinsi ya kibinadamu kumsaidia asisulubiwe.

Katika majira ya Pasaka ilikuwa ni desturi ya Pilato kumfungulia na kumuacha huru mfungwa mmoja. Pilato huku akijua jinsi watu walivyomchukia mfungwa aliyeitwa Baraba aliwauliza je niwafungulie nani Baraba au Yesu? Baraba alikuwa ni mfungwa hatari  na alifahamika kwa sifa ya uuaji na ujambazi. Baada ya swali hilo Mafarisayo wakaanza kuwashawishi watu kwa kuwaeleza kwamba kubalini afunguliwe Baraba bali Yesu Mnazareti asulubiwe.  Mwishowe ushawishi ule ukakubalika na watu wakataka afunguliwe Baraba na hivyo wakapewa Baraba.

Nilipokuwa nikitafakari habari hii ndipo lilinijia swali hili kwenye ufahamu wangu “unapokuwa kwenye jaribu unaruhusu wazo la nani kwenye maisha yako”? Je la Mungu au la Shetani? Kumbuka jaribu ni lile linalomweka mtu kwenye njia panda katika kufanya maamuzi.   Naamini wewe ni shahidi wa maisha yako, mara kadhaa huenda umejikuta kwenye jaribu kikazi, kimasomo, kindoa, kibiashara, kihuduma, kimahusiano, kijamii, kutoolewa, kutozaa nk. Na kwa ujumla siku zote mtu anapokuwa kwenye jaribu watu wa kumshauri namna ya kukabiliana na changamoto/jaribu husika huwa hawakosekani.

Kila mtu huwa anakuwa na mtazamo wake wa kukushauri tegemeana na aina ya jaribu ulilonalo. Licha ya mawazo kutoka kwa watu lakini pia ndani yako huwa yanakuja mawazo tofauti tofauti ya namna ya kukabiliana na jaribu unalolipitia. Katika mawazo hayo yanayokuja yapo ambayo ni ya kutoka kwa Mungu, Shetani au wanadamu. Na siku zote wazo bora kutekeleza na la kukutoa kwenye jaribu ulilonalo ni wazo la Mungu. 

Swali kwako mpenzi msomaji ni “je unapokuwa kwenye jaribu huwa unaruhusu/unatekeleza wazo la nani”, wazo la Mungu au la shetani?

Siku moja nikiwa nimelala nilisikia sauti karibu mara tatu ikiniambia usipokuwa na wazo jipya huwezi kutoka mahali ulipo”. Kitu cha ajabu nilipoamka niliendelea kuisema hii sentensi karibu siku nzima iliyofuata. Mungu aliileta kauli hii kwani wakati huo kuna jaribu liliniweka kwenye   njia panda. Kwa jinsi ya kibinadamu sikuona ufumbuzi mzuri, na mawazo yaliyokuja yasingeweza kunitoa kabisa kwenye jaribu husika na mengine yangesababisha tatizo/jaribu kuwa kubwa zaidi.

Hivyo Roho Mtakatifu aliponiletea wazo hili nilielewa nini maana yake kwangu. Ndipo nikaanza kutafuta wazo la Mungu la kunivusha kutoka kwenye jaribu husika kwa maombi na kwa kutafakari neno lake  huku nikipima ushauri ninaoupata kutoka kwa watu. Baadae nikapata wazo bora katika Roho Mtakatifu. Nilipolitekeleza niliona mlango uliofunguliwa kwa ajili yangu na nikavuka hapo.

Labda niseme kila wazo lina ushawishi wake maalum, kwa hiyo ni jukumu lako kufikiri vizuri kabla hujachukua maamuzi ya wazo gani ulitekeleze. Wayaudi walishawishiwa na Mafarisayo kukubali afunguliwe Baraba, mtu ambaye alikuwa ni jambazi na muuaji. Na ukiitazama dhana hii kwa mfumo wa mawazo, ina maana walikubali wazo ambalo ni uharibifu na mauti kwenye kizazi chao.  

Zingatia yafutayo ili kutekeleza wazo la Mungu;

Kwanza kumbuka katika Yeremia 29:11, Mungu anayo mawazo mazuri ya kukufanikisha kwa ajili yako. Kwa hiyo ni jukumu lako kuyatafuta.

 • Jifunze kutafuta na kujua lipi/yapi ni mawazo ya Mungu juu ya jaribu linalokukabili.
 • Tafuta wazo la Mungu kwa kuomba, kutafakari neno, kutafuta ushauri kwa watu wengine unaosukumwa kuwaendea, kusoma vitabu, kusikiliza mafundisho nk tegemeana na aina ya jaribu/changamoto unayoipitia wakati huo.
 • Hakikisha unapima kwanza wazo lolote ambalo unalipata, na kipimo chako kiwe neno la Mungu. Angalia kama wazo hilo halipingani na neno la Mungu basi unaweza kulitekeleza.
 • Ukishalijua wazo la Mungu, haijalishi kibinadamu kulitekeleza lina athari gani, maadamu una uhakika kwamba ni la Mungu wewe litekeleze utaona mlango wa kukutoa kwenye jaribu ukijitokeza.
 • Wafilipi 4:6 inatugiza kutokujisumbua kwa jambo lolote, bali tusali, tuombe na kumjulisha Mungu haja zetu pamoja na kumshukuru. Je, unajua ni kwa nini? Hii ni kwa sababu hata ukijisumbua kiasi gani bila kuwa na wazo la Mungu huwezi kutoka mahali ulipo. Kwa hiyo mweleze haja zako naye atakupa mawazo yake nawe utavuka.

Barikiwa sana mpendwa wangu.

NINI CHA KUFANYA MUNGU ANAPOWEKA MSUKUMO WA KUOMBA NDANI YAKO? (Part 2)

August 20, 2009

 Na: Sanga,P.S.

 Agosti 2009.

Kumbuka lengo la ujumbe huu ni kukusaidia ili maombi yako yawe ni maombi yenye matokeo mazuri. Maana kama ni kuomba huenda umeomba sana lakini huoni matokeo ya maombi yako. Na suala si kuomba tu, unaweza ukaomba kwa muda mrefu na kufunga lakini kama hatuoni matokeo ya maombi yako haitusadii kwa lolote na haikusaidii pia kwa lolote. Mambo yafuatayo yatakusaidia kuboresha maombi yako ili yawe na matokeo mazuri zaidi, fuatana nami katika sehemu hii ya pili;

 Namna ya kuomba kwa kuzingatia mfumo wa kuombea unachokiombea;

1 Yohana 5:14 “… Kama tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake”. Je Kuomba huku kukoje au ni kwa namna gani?

 • Kuomba kwa uongozi wake (Roho Mtakatifu),i.e kwa kuzingatia maagizo yake. Waefeso 6:18 “Pray in the Spirit”.
 • Kuomba kwa kuzingatia upako wa Mungu ulioko juu yako.
 • Kuomba kwa imani katika Jina la Yesu (Yohana 14:13, 16:23, Matendo 3:16).
 • Kuomba wakati moyo wako haukuhukumu (1Yohana 3:21-22).
 • Kuomba kwa kujenga hoja zenye nguvu.
 • Kuomba kwa juhudi na bila kukata tamaa, (Luka 18:1).
 • Kuomba kwa kuzingatia muda unaotumia kuliombea jambo husika. Na linapokuja suala la muda kuna tafsiri mbili. Moja unaomba kwa muda gani i.e kwa dakika au masaa mangapi?, mbili unaomba wakati gani yaani saa ile unaposikia msukumo wa kuomba au kwa wakati unaotaka wewe?, (Luka 18:1-8, Matendo ya Mitume 12:1).

 Hata hivyo suala sio kuomba tu, bali katika maombi yako zingatia yafuatayo;

 • Kwa nini uombe, unaombaje, na unaombea wapi?
 • Unaomba kwa muda gani?
 • Katika na kutoka nafasi ipi? yaani kama nani?
 • Ukiwa na ufahamu kiasi gani juu ya suala unaloliombea?
 • Ukiwa na ufahamu kiasi gani juu ya maandiko yanayohusu suala unaliliombea?
 • Ukilenga nini katika kuomba kwako?
 • Unaomba ukiwa katika hali gani kiroho?
 • Je unaomba huku ndani yako unaona nini? (Marko 8:22-26).
 • Omba kwa sala zote i.e kukiri, kuungama,kufunga,kusifu nk. (Waefeso 6:18).

 Bwana Mungu akubariki, naamini dondoo hizi chache za mwisho zinakamilisha somo hili la “nini cha kufanya Munguanapoweka msukumo wa kuomba ndani yako?” swali aliloniuliza kiongozi wa kiroho wa mkoa wa Lindi.

 Weka kwenye matendo na jifunze kujiuliza maswali hayo kabla hujaomba naamini utaona mabadiliko kwenye maombi yako.

 Neema ya Kristo ikulinde.