Archive for March 2009

NAMNA UNAVYOWAZA NI PICHA YA NAMNA UTAKAVYOISHI.

March 28, 2009

 

Na: Sanga P.S

Waraka wa Machi.

Zaburi 36:4

Huwaza maovu kitandani pake, hujiweka katika njia mbaya; ubaya hauchukii’.

Aina ya maisha/mapito anayoishi au kupita mtu ni matokeo ya mawazo yake. Mawazo ya mtu ndiyo yanayoamua maisha ya mtu yaweje.

 

Jifunze yafuatayo kutoka katika msatri huu wa Zaburi hii ya 36.

 

Ø      Kumbe kwa kuwaza maovu mtu anajiweka katika njia mbaya.

Ø      Hii ina maana mtu anatumia mawazo yake mwenyewe kujiweka kwenye njia mbaya.

Ø      Mtu huyu yuko katika njia mabaya kwa sababu anawaza maovu. Hii ina maana mtu huyuhuyu kama akiwaza mawazo mazuri/mema atajiweka katika njia bora/njema na nzuri.

Ø      Mtu huyu atafanikiwa ikiwa atawaza kufanikiwa na atafeli ikiwa atawaza kufeli.

Ø      Kwa hiyo mpaka hapa tunagundua kwamba kumbe mawazo yake yanatueleza hali au matokeo ya maisha yake yatakavyokuwa.

 

Je mpendwa wangu, kiroho, kihuduma, kijamii, kibiashara, kiuchumi , kikazi nk uko katika hali/njia/mfumo gani wa maisha, ni mzuri au ni mfumo mbaya. Kama ni mbaya angalia jinsi unavyowaza kuhusu hilo eneo. Ulivyo kwenye hilo eneo kibiblia ni matokeo ya ulivyowaza nafsini mwako. Kama huoni kufanikiwa kwenye biashara/kazi/kiuchumi ina maana umewaza au uliwaza kutokufanikiwa. Na hata kama unawaza kufanikiwa basi hauwazi sawasawa na ahadi za Mungu katika maisha yako.

 

Hasara ya kuwaza vibaya ni kujiweka katika njia mbaya, yaani unajitengenezea mazingira mbaya, mazingira ya kutokufanikiwa katika maisha yako kwa ujumla. Ili neno la Mungu liweze kutenda yale yote ambayo limetumwa na Mungu kuyatenda kwenye maisha yako kwa uaminifu ni lazima kwanza na wewe ujifunze kuwaza in a positive way.

 

Yaani kuwaza sawaswa na ahadi au na neno la Mungu kwenye maisha yako. Kinyume chake haliwezi kutimia na hivyo utakuwa umempa Ibilisi nafasi kutekeleza mapenzi yake juu yako.

 

Jifunze kuwa makini na unavyowaza juu ya mambo mbalimbali unayokutana nayo kila siku. Hakikisha hauwazi kinyume na ahadi za Mungu kwenye maisha yako.

 

Neema ya Kristo iwe nawe.

MWANAMKE, JIFUNZE KUSIMAMA KWENYE NAFASI YAKO KAMA MLINZI.

March 28, 2009

 

Na : Mwalimu Sanga P.S

 

Yeremia 31:22” hata lini utatanga tanga , Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya duniani, mwanamke atamlinda mwanaume”.

Soma pia habari hii yote katika Isaya 32:9-17

 

Ule mstari wa tisa unasema “Inukeni enyi wanawake wenye raha, sikieni sauti yangu; enyi binti za watu wasiokuwa na uangalifu,tegeni masikio yenu msikie sauti yangu”.

 

Moja ya majukumu makubwa ambayo Mungu amemkabdihi mwanamke ni jukumu la ulinzi kwa mwamamumue yoyote na si mumewe tu kama wengi wanavodhani au kufikiri. Kwa maana hili andiko linawahusu wanwake haijalishi wameolewa au la, ni binti au mjane linamhusu.

 

Si wanawake wengi wanaoifahamu siri hii juu yao. Imeandikwa ya kwamba Mungu ameumba jambo jipya, mwanamke atamlinda mwanaume. Hii ina maana ulinzi wa mwanaume uko kwa mwanamke. Hii inaashiria kumbe Mungu ameweka neno la ulinzi wa mwanaume kwa mwanamke.

 

Hebu tuangalie mifano kadhaa ndani ya Biblia;

 

*      Kuzaliwa kwa Musa, Kutoka 2;1-10.

Tunaona wazi kabisa mama wa Musa alivyomlinda mwanae akijua ndani yake kuna kusudi limebebwa.

*      Kuzaliwa, kukua na ndoa ya yakobo, Mwanzo 25:21-28, 27:1-4, 5, 6, 11-13, 17, 46.

Siri ya kusudi la Mungu hapa duniani kupitia Yakobo aliiweka kwa mamaye. Alimweleza maana ya vita iliyokuwa ikiendelea tumboni mwake alipokuwa mjamzito. Rebeka alihakikisha kusudi la Mungu juu ya watoto atakaowazaa linatimia, kwa sababu alijua Yakobo ndiye taifa kuu alihakikisha hilo linatimia na pia alihakikisha Yakobo haoi nje ya mpango wa Mungu kwa maana ya kuoa mataifa.

*      Kuzaliwa na maisha ya Samson, waamuzi 13:2-5, 12-15.

Siri ya nini Mungu amekiweka kwa Samson na kwa nini anamleta duniani, pamoja na namna mtoto huyo anavyotakiwa kulelewa aliiweka kwa mamaye Samson na si baba yake, Mzee Manoa. Sasa ukisoma utaona jinsi huyu mama alivyosimama kwenye nafasi yake ki ulinzi mpaka Samson alipoanza wajibu wake uliomleta duniani.

*      Zaidi unaweza ukajifunza pia kupitia kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Siri ya kitu gani kitazaliwa, Malaika aliileta kwa Mariam, akijua ni jukumu lake kulinda hiyo siri mpaka utimilifu wake. Soma Mathayo 1:18-25.

 

Hata leo wanawake wanatakiwa kusimama kwenye nafasi zao za ulinzi kwa ajili ya watoto wao, vijana wao, waume zao, ndugu zao waume nk. Kwa lugha nyepesi ni shauri la Bwana kwamba kila mwanamke amlinde mwanamume anayetoka katika tumbo lake, mumuwe kama ameolewa nk ili kuhakikisha kusudi la Mungu linatimia.

 

Kosa la hawa wanawake/mabinti katika siku za nabii Isaya ni kujisahau, kufurahia starehe na kutokuwa waangalifu katika kufuatilia maagizo ya Mungu kuhusu ulinzi wa watoto, vijana, na waume zao nk.

 

Kibiblia ni utaratibu wa Mungu kumpa kila mwanamke taarifa juu ya mtoto atayemzaa, juu ya mume ambaye atamuoa lengo ikiwa ni kumsaidia ajipange ki-ulinzi.

 

Mwanamke hakikisha unasimama vema kwenye nafasi yako ya ulinzi kwa mwanamume. Kama utasiamama vizuri kwenye nafasi yako ya ulinzi basi uwe na uhakika umeubariki moyo wa Mungu na kwa sababu hiyo umepelekea uponyaji kwenye familia yako, jamii yako, taifa lako na uchumi wako binafsi lakini na ule wa taifa pia.

 

Kazi kubwa ya Shetani ni kuwafanya wanawake waliokoka  duniani wajisahau, wasiwe waangalifu na hivyo wasifuatilie maagizo ambayo Bwana Mungu ameweka ndani yao kuhusu waume zao, vijana, watoto na ndugu zao wa kiume ili  kusudi la Mungu lisifanikiwe. Sasa wewe usikubali shetani akuzidi maarifa, weka neno hili kwenye matendo utaona wazo la Mungu linatimia kwa kuwa MWANAMKE AMESIMAMA KWENYE NAFASI YAKE YA ULINZI.

 

Bwana na akubariki.

 

MOYO WAKO UNASEMA NINI?

March 28, 2009

 

 

 

 

Na: Sanga P.S

 

Zaburi ya 14:1 “Mpumbavu amesema moyoni, hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, hakuna atendaye mema”.

 

Zaburi 14:1 b,c ni matokeo ya kauli ya kipengele a. Kwa sababu mtu huyu ambaye ni mpumbavu ameshasema moyoni mwake kwamba hakuna Mungu, hivyo suala la kutenda dhambi kwake  ni kawaida.

 

Ukisoma pia  Zaburi 36:1 Biblia inasema  Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake, hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake’. Sikiliza mtu huyu hawezi kuwa na hofu ya Mungu kwa sababu tayari moyoni mwake ameshasema hakuna Mungu.

Kwa nini inakuwa hivi? Ni kwa sababu awazavyo nafsini mwake ndivyo alivyo na pia ni kwa sababu maamuzi yake ndiyo yanaamua maisha yake. Soma Zaburi 36:4 na Mithali 23:7a.

 

Mpumbavu ni mtu anayejua kitu au kweli halafu anafanya maksudi kuvunja hiyo sheria au kukiuka hiyo kweli.

Je, nawe msomaji wangu unapopita kwenye hali ngumu kiuchumi, moyo wako unaema nini?

Unapojaribiwa, unapoachwa, unapochelewa kuoa/kuolewa, kuzaa, kupata kazi moyo wako unasema nini?, unapowekwa na Mungu kwenye nafasi ya uongozi, unapobarikiwa, unapokosewa na ndugu yako, je moyo wako unasema nini?.

 

Katika mazingira yoyote unayopita lolote utakalolisema moyoni lina matokeo yake, yanaweza kuwa ni mazuri au mabaya tegemeana na ulivyosema.

 

Lolote utakalolinena moyoni mwako kinyume na ahadi za Mungu juu yako, hii ina maana na wewe umesema hakuna Mungu katika hilo. Kwa lugha nyepesi umekataa wazo au msaada wa Mungu kwenye hilo unalolipitia hadi ukasema hakuna Mungu. Na ukisema hakuna Mungu tegemea kutopata msaada wa Mungu bali kuonewa zaidi na utawala wa Shetani.

 

Tuangalie mifano kadhaa kwenye Biblia;

*      Mwanamke aliyetokwa na damu kwa miaka 12, Mathayo 9:20-22

*      Anania na safira , Matendo 5:1-4.

*      Yuda Iskariote, Yohana 13:2

*      Mikali binti Sauli, mke wa Daudi, 2samweli 6; 16, 20-23.

Katika hii mifano yote hawa watu hawakusema kwa vinywa vyao, bali ni mawazo/kusema kwa mioyo yao.

Na ndiyo maana Yeremia 17:9 inasema;

 

Moyo huwa mdanganyifu sana kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha, nani awezaye kuujua? Mimi Bwana , nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.

 

Jifunze kuwa makini na namna unavyosema moyoni mwako, ukihakikisha unasema sawasawa na ahadi/mapenzi ya Mungu kwenye maisha yako.

 

Bwana Mungu akubariki.

UPONYAJI WA NAFSI ILIYOINAMA.

March 28, 2009

 

Na: Patrick Sanga

 

Mithali 12:25a “Uzito katika moyo wa mtu huunamisha”

 

Mwanadamu anapita katika vipindi/mazingira tofauti tofauti kwenye maisha yake.Mazingira hayo yanaweza yakamsababishia nafsi yake kuinama au kufuarahi. Biblia inasema uzito wa moyo wa mtu huuinamisha , kwa lugha nyingine moyo wa mtu huinama kwa sababu ya uzito uliomo ndani yake.

Maana yake nini? Uzito kwenye moyo inawakilisha  hali ya mtu kuchoka moyoni, kukata tamaa moyoni, kuhuzunika, kufadhaika, kuugua, kukosa amani moyoni nk.

 

Chanzo chake nini?

 

* Kuchelewa kwa kilichotarajiwa, Mithali 13:12.

Kuwa na matarajio ya mambo mabalimbali kutoka kwa Mungu ni kawaida ya mwanadamu.Tarajio linapochelewa moyo wa mtu unainama, mfano kuchelewa kuolewa/kuoa, kuzaa, kupata kazi, kupoana nk.

* Hatari/hofu ya kifo, Matahyo 26:37-38.

Ukisoma habari hii utaona jinsi Yesu mwenyewe alivyougua na kusononeka kwa sababu ya kifo kilichokuwa kinamkabili. Hata leo watu wengi nafsi zao zimeinama kwa sababu ya hofu ya kifo kupitia magonjwa ukimwi na uchawi pia.

 

* Hali mbaya kiuchumi, dhiki nk 2Wafalme 4:1

Hii imekuwa ni changamoto kwa watu wengi sana na limepelekea watu wengi kuona kama wokovu ni mgumu sana.

 

* Dhambi

Mtu anapofanya dhambi anakuwa amempa Ibilisi nafasi kutawala maisha yake. Dhambi pia inaondoa furaha rohoni.

 

* Maneno ya kuvunja moyo toka kwa watu wengine. Zaburi 42:2-3

Katika hali ya kawaida maneno ya fitina, uzushi, kuaibisha nk yanaumiza sana watu wanapokusema. Huu ni mfano wa Onesmo katika Filemoni ule mstari wa kumi na moja.

 

Nini cha kufanya?

 

Jifunze kujitamkia maneno yanayolenga kuinua nafsi yako.

Neno jema/zuri ni uponyaji wa nafsi iliyoinama, linaleta furaha kwenye nafsi hiyo.

 

 Hebu tuangalie mfano wa mwimbaji wa zaburi ya 42.

 

Ukisoma hii Zaburi utagundua huyu mwimbaji wa Zaburi nafsi yake iliinama kwa sababu ya maneno ya kuumiza watu waliyokuwa wanayasema dhidi yake. Na chanzo cha kauli hizo hakijatajwa, lakini huenda ni kwa sababu alitenda dhambi. Lakini siri ya ushindi kutoka kwenye mazingira ya kifo ilikuwa ni kujitamkia maneno yenye kujenga na kurejesha afya ya nafsi yake. Mstari wa tano katika sura hii unasema ‘nafsi yangu kwa nini kuinama,na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; kwa maana nitakuja kumsifu, aliye afya ya uso wangu, na Mungu wangu”

 

Ndani ya Biblia kuna ahadi na mistari mingi sana ambayo waweza kuitumia ili kuinua nafsi yako au hata ya mtu mwingine ikiwa imeinama kutokana na mazingira anayoyapitia kwa wakati huo. Mistari ifuatayo itakusaidia sana kurejesha nafsi mahali pake, hakikisha unaisoma yote na ukiweza kuiandika mahali ili kila wakati uwe unaitamkia nafsi yako.

 

Mithali 11:8, 26:2c, 28:20, 28:13b, 24:16a.

Isaya49:15-16, 24-26, 43:25, 50:8, 54:7-10

Zaburi 34:4, 19, 89:33-34

Mhubiri 3:8

 

Baada ya kusoma anza kuiambia nafsi yako kama mwimbaji wa zaburi alivyiambia nafsi yake akisema nafsi yangu usiiname kwa sababu….., sasa tegemeana na kilichosababisha nafsi yako iiname tamka neno ambalo linavunja ile fikra iliyopelekea nafsi yako kuinama. Mfano kama ni hatari ya kifo, Iambie nafsi yangu usiiname kwa kuwa  Kila silaha itayofanyika juu yangu haitafanikiwa…. Isaya 54;17 nk. Weka neno hili kwenye matendo utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.

 

Mungu wangu akulinde na kukuponya nafsi yako.