Archive for the ‘Uncategorized’ Category

MUNGU ANATAFUTA MTU WA KUSIMAMA MAHALI PALIPOBOMOKA APATENGENEZE

March 22, 2015

 Na: Patrick Sanga

2

Biblia katika kitabu cha Ezekieli 22:30 inasema ‘Nami NIKATAFUTA MTU miongoni mwao, ATAKAYELITENGENEZA BOMA, na KUSIMAMA mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu’. Ukisoma fungu zima katika kitabu cha Ezekieli 22:23-31, utaona kwamba uasi uliolifikisha taifa katika hali hii ulitokana na mambo manne;

Moja kulikuwa na fitina ya manabii ambapo walitwaa kwa nguvu mali za watu, walitoa nabii za uongo na kufunika dhambi. Pili ni dhambi ya makuhani ambapo walihalifu sheria ya Mungu, kunajisi hekalu la Mungu na kutofundisha watu kweli juu ya masuala mbalimbali ya kiroho.  Tatu ni dhambi ya watawala ambapo walimwaga damu, kujipatia faida zisizo halali na kuharibu roho za watu. Na mwisho (nne) ni dhambi ya watu wa nchi ambapo walifanya udhalimu, unyang’anyi, jeuri na uonevu juu ya maskini na wageni.

Kwa nini ilimlazimu Mungu atafute MTU kwanza na si kupiga moja kwa moja licha ya uovu mkuu kiasi hiki?. Hili ndilo swali ambalo nilikuwa nikijiuliza mara kwa mara kila ninaposoma andiko hili. Katika kuendelea kujifunza na kutafakari ndipo BWANA akanionyesha jambao lifuatalo kama jibu la swali hili muhimu.

Katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana 5:10 imeandikwa ‘ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi’. Naam andiko hili linatujulisha kwamba, Mungu kwa hiari yake ameweka utaratibu kwamba mtu mwenye mwili awe kuhani na mfame juu ya nchi, na kwa hiyo KIMSINGI maamuzi ya mwisho juu ya nini kifanyike juu ya nchi/familia/kanisa yapo kwa mtu akitokea kwenye nafasi ya Mfalme na kuhani kwa Mungu wake.

3

Tuone mfano wa Musa, kitabu cha Kutoka sura ya 32 kinaeleza uamuzi wa wana wa Israeli kutengeneza ndama kama mungu wao baada ya Musa kukawia kushuka kutoka mlimani, naam walifanya hivyo na jambo hilo likawa chukizo kubwa kwa Mungu. Ndipo Mungu akamwambia Musa katika Kutoka 32:10 akisema ‘Basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao…’ Je umeaona maneno haya “Basi sasa niache”?. Maneno haya kwenye tafsiri za kingereza yameandikwa ‘Let me alone, don’t try to stop me, do not get in my way’.

Maneno haya yanatuonyesha kwamba, Musa kama Mfalme na Kuhani alikuwa ndiyo mwenye mamlaka na watu wa eneo lake na hivyo ilimbidi Mungu kuwasiliana naye kwanza kabla ya kutekeleza uamuzi wake. Hivyo basi ndiyo maana wakati wa nabii Ezekieli, Mungu alitafuta mtu, Ili mtu kutoka kwenye nafasi ya Mfalme na Kuhani asimame mahali palipobomoka kupatengeneza.

Naam, hata sasa, Mungu anatafuta mtu mwenye kusimama mahala palipobomoka ili kupatengeneza. Yapo maeneo mengi katika nchi, kanisa, familia, ndoa, koo nk ambayo yameharibika na hayana budi kutengenezwa. Je ni mtu wa namna gani Mungu anamtafuta?

  • MWENYE KUDUMU KULITUNZA NENO LAKE NA KUTOKULIKANA JINA LAKE Katika Ufunuo wa Yohana 3:8 imeandikwa ‘Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu’. Mungu anatafuta mtu ambaye ANADUMU KULITUNZA NENO LAKE NA KUTOKULIKANA JINA LAKE bila kujali anapita katika mazingira ya namna gani. Naam mtu mwenye kutenda haya yupo tayari kusimama na kutengeneza mahali palipobomoka (Wafilipi 4:11-13 na Matendo ya Mitume 4:9-19).

 

  • MTU MWAMINIFU TENA MWENYE AKILI – Matahyo 24:45 inasema ‘Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo’. Hivyo Mungu anatafuta mtu MWAMINIFU katika kutekeleza wajibu/wito/kusudi alilompa hapa duniani (Waruni 8:28). Naam si tu kutekeleza wajibu husika bali zaidi autekeleze kwa nyakati (majira) za Mungu na si kama atakavyo yeye (mtu). Je, umepewa kufanya nini hapa duniani? Je umekuwa mwamnifu katika hilo ulilopewa? Mungu amekupa nafasi zipi katika mwili wa Kristo (kanisa)? Katika nafasi hizo, je umekuwa mwaminifu?

 

  • ALIYE TAYARI KUJIFUNZA NA KUBADILIKA – Katika Ezekieli 23:11 imeandikwa    ‘Na umbu lake, Oholiba, akayaona hayo walakini alizidi kuharibika kuliko yeye, kwa kupendelea kwake, na kwa uzinzi wake, uliokuwa mwingi kuliko uzinzi wa umbu lake’. Hivyo Mungu ANATAFUTA mtu ambaye YUKO TAYARI KUJIFUNZA NA KUBADILIKA kutokana na makosa ya wengine waliomtangulia au waliotangulia. Kutoka 32:9 inasema ‘… Mimi nimewaona watu hawa, na tazama ni watu wenye SHINGO NGUMU’. Tukumbuke kwamba katika Waebrania 10:26 imeandikwa ‘Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi’. Mtu asiye tayari kubadilika hawezi kusimama mahali palipobomoka apatengeneze.

 

  • MWENYE KUMPENDA MUNGU – Katika Warumi 8:28 imeandikwa ‘Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake’. Hivyo Mungu anatafuta mtu ANAYEMPENDA kwa moyo wake wote, akili zake zote, roho yake yote na nguvu zake zote. Je unampenda Mungu kwa kiwango gani?. Na mtu mwenye kumpenda Mungu huzishika ammri zake na hujibiidisha katika kutaka kmujua zaidi Mungu (Ayubu 22:21). Ni vizuri ukafahamu kwamba mtu mwenye kumpenda na kumjua sana Mungu; ni mnyenyekevu, mtunzaji siri, mwenye kusamehe, hadharau wengine na wala hawezi kufurahia mapungufu au kufeli kwa wengine bali atafanya kila awezalo kuwasaidia.

7

Mkumbuke BWANA wetu Yesu Kristo jinsi alivyotupenda ingawa hatukustahili (Yohana 3:16). Kutokana na upendo wake alichukua uamuzi wa kusimama mahali palipobomoka na kupatengeneza ili kurejesha tena uhusiano ulioharibika kati ya mtu na Mungu kwa sababu ya dhambi.  

Hitimisho

Mpenzi msomaj, Je Mungu anaweza kukuamini kiasi cha kukushirikisha agano lake na mawazo yake? Rejea (1 Wakorinto 2:9). Hata sasa Mungu anatafuta mtu mwenye kusimama mahala palipobomoka ili kupatengeneza. Je Mungu anapokutafuta na kukupima katika maeneo haya tuliyojifunza anaona nini ndani yako? Uharibifu au uponyaji? maamuzi ya mwisho kuhusu nchi yako, kanisa lako, ndoa yako, watoto wako, ukoo wako, wazazi wako nk yapo kwako kutoka kwenye nafasi ya mfalme na kuhani kwa mungu. Hivyo Kumbuka siku zote kusimama mahali palipobomoka kama kuhani na mfalme upatengeneze, ili Mungu akitaka kupiga akute umesha simamama mahali husika unaendelea na matengenezo.

 

Neema ya BWANA wetu Yesu Kristo iwe nanyi.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu.

 

USIKUBALI KUFA KIFO CHA KIPUMBAVU.

March 26, 2008

 Na: Patrick Samson Sanga.
 Waraka wa Machi.

2Samweli 2:31-34 na Zaburi 14:1 ‘Mpumbavu amesema moyoni, mwake hakuna Mungu…..’ Mpenzi msomaji naamini unaendelea vema kwa ujumla kimwili na kiroho. Katika mwezi huu nataka niseme nawe juu ya kifo cha kipumbavu.

Mpumbavu ni nani? Kibiblia ni mtu yoyote aliyekataa kuwa na ufahamu au elimu ya Mungu ndani yake. Mtu aliyekataa uwepo wa Mungu au kuwa na Mungu maishani mwake.

Hivyo basi kifo cha mpumbavu ni kifo cha mtu ambaye moyoni mwake amesema hakuna Mungu.Mauti inayomkuta mtu ambaye amekana elimu au ufahamu au uwepo wa Mungu katika maisha yake. Mauti inayommkuta mtu kabla hajakubali uwepo wa Mugu katika maisha yake. Kifo kinachomkuta mtu ambaye hajampa Mungu nafasi ya utawala moyoni mwake.

Tujifunze kwa Abneri. 2Samweli 2:22-39 ukisoma vema hapa utaona habari za shujaa mmoja aliyeitwa Abneri. Kwa kifupi Abneri alikuwa;
Kiongozi wa majeshi ya Sauli, mpinzani mkubwa wa Daudi, baadaye alipelekea Daudi kuitawala Israeli yote, Alimwua Asaheli shujaa wa Daudi ndugu yake Yoabu, kiongozi wa majeshi wa Daudi. Na mwishowe Yoabu ndiye aliyemwua Abneri ili kulipiza kisasi cha kifo cha nduguye.
Sasa baada ya kifo cha Abneri, ndipo Daudi akamlilia Abneri akasema, ilimpasaje Abneri kufa afavyo mpumbavu?, mikono yako haikufungwa wala miguu yako haikutiwa pingu; aangukavyo mtu mbele ya wana wa uovu, ndivyo ulivyoanguka.

Ukiendelea kusoma habari hii utaona kwamba siku ile Daudi alikataa kula akimliilia Abneri, akisema hamjui ya kuwa mkuu mmoja, naye ni mtu mkubwa ameanguka leo katika Israeli?

Je kwa mazingira ya leo, mtu anawezaje kufa kifo cha kipumbavu?Unaposhindwa kutumia fursa zilizopo kuiponya nafsi yako matokeo yake ni kifo cha kipumbavu. Abneri hakufungwa mikono wala miguu lakini aliuawa. Daudi alikuwa akimuuliza Abneri kwa nini usitumie mikono na miguu yako kuiponya roho yako? .

Katika Zaburi 14;1 TUMEONA MPUMBAVU NI MTU YULE AMBAYE MOYONI MWAKE AMESEMA HAKUNA MUNGU, kwa lugha nyepesi amekataa kuwa na Mungu moyoni mwake na kwa sababu hiyo amekataa uongozi wa Mugu katika maisha yake.

Kibiblia mtu wa namna hii anapokufa anaenda kuzimu na si paradiso au mahali pema peponi. Kumbe kwa lugha nyepesi mtu ambaye anakufa katika dhambi zake wakati fursa ya kuzitubu au kuziacha kabisa ilikuwepo ndiye anakuwa amekufa kifop cha kipumbavu.

Mpango wa Mungu ni kukuokoa kutoka katika dhambi ili usije ukafa kifo cha kipumbavu na ukaenda kuzimu kwenye mateso makali. Yohana 3:16 inasema ‘kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipoteee bali awe na uzima wa miele.

Neno ‘asipotee’ linawakilisha kifo cha kipumbavu . Mungu alimtoa Yesu ili wewe usife kifo cha Kipumbavu, kifo cha bila kumpa Mungu nafasi katika maisha yako.

Hivyo basi, Yesu ni fursa ya wewe kuitumia ili usife kifo cha kipumbavu. Kwa nini ufe katika dhambi yako, wakati Yesu yupo tayari kuiokoa nafsi yako isiangamizwe? Je ndugu yangu itakufaa nini kuupata ulimwengu wote na mali zake zote huku ukiaangamiza nafsi yako mwenyewe?

Abneri alishindwa kutumia mikono na miguu yake kama fursa iliyokuwa mbele yake kwa wakti ule, akafa kifo cha kipumbavu. Usiwe kama Abneri itumie fursa ya kuja kwa Yesu vema, fanya maamuzi ya kumwamini kama Bwana na mwokozi wako.

Baba yangu, mama yangu, kaka yangu, dada yangu, na rafiki yangu nakuomba kwa jina la Bwana usikubali kufa kifo cha kipumbavu, usikubali mauti ikukute kabla hujampa nafasi Yesu ya kutawala maisha yako. Mshahara wa dhambi ni mauti na baada ya kifo ni hukumu, je utakuwa mgeni wa nani siku ile?

Mungu ameniongoza nikuandikie ujumbe huu maana yeye hafurahii kifo cha mwenye dhambi, kwa sababu mtu anapokufa katika dhambi yake anatengwa na Mungu milele kwa sababu hakuna kuokoka baada ya kufa, ni hukumu tu tena ya kutisha. Siku ya kufa kwako ndiyo mwisho wa dunia kwako.

Usikubali kufa kifo cha kipumbavu , maana mpumbavu amesema hakuna Mungu katika moyo wake, bali wewe moyoni mwako mpe Mungu nafasi katika Jina la Yesu atawale maisha yako

Ikiwa umeguswa na ujumbe huu na unataka kuokoka bonyeza category ya wokovu utapata maelekezo ya nini cha kufanya.

Neema ya kristo iwe nawe.

KWA NINI VIJANA WENGI HAWAJAKA KWENYE NAFASI ZAO KI-MUNGU?

September 16, 2006

Na : Patrick Sanga.

Iyohana 2:14

 Kila kundi katika kanisa, jamii na hata nchi Mungu amelipa nafasi na wajibu wake maalumu wa kutekeleza. Pia Mungu anao mtazamo wake binafsi na matarajio yake kwa hayo  makundi

mbali mbali ndani ya nchi. Vijana, watoto, wababa, wazee, wanawake, viongozi wote / yote yana mtazamo wake mbele za Mungu. Ukimuuliza Mungu  nini mtazamo  wako  kwa vijana, atakujibu  soma vizuri IYohana 2:14 maana  yake Mungu anawatazama vijana kama watu wenye nguvu, watu ambao neno la Mungu linakaa ndani yao na pia wamemshinda mwovu.

 Sasa  ukirudi  mazingira  halisi unaona kwa  asilimia kubwa vijana wengi hawako kwenye nafasi ambazo Mungu aliwakusudia. Lengo la somo hili ni :-         Kueleza sababu za kwa nini  vijana wengi hawajakaa  katika nafasi zao.         Kumweleza kijana mambo ya kujiepusha nayo ili  aweze kukaa kwenye nafasi yake.         Kumpa kijana maarifa yatakayomsaidia kurejea kwenye nafasi yake na ili aweze kutekeleza matarajio ya Mungu kwake. Zaidi ujumbe huu umekusudia kulenga na kuelewesha vijana waliokoka, nazungumza  na vijana waliookoka maana hawa ndio ambao Mungu amewatamkia maneno haya au kuwa namtazamo huu juu yao. Zipo sababu  nyingi lakini hizi zifuatazo ni za msingi na zimesababisha wengi kuishi maisha nje ya kusudi la Mungu na kufa bila kutekeleza matarajio ya Mungu  kwao sababu hizo ni:-

         Moja vijana wengi hawajajazwa nguvu za Roho Mtakatifu.

 Biblia inasema katika matendo ya Mitume 1:8 kwamba “lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajia  juu yenu Roho  Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika  Yerusalemu, na katika uyahudi wote, na samaria, na hata mwisho wa nchi”. Hivyo vijana wengi hawajakaa katika nafasi zao  kwasababu wengi wa vijana leo makanisani  hawajajazwa nguvu za Roho Mtakatifu si kwamba  Mungu hataki kuwajaza lakini shida ipo kwa vijana wenyewe wengine kutotaka kujazwa nguvu hizo, lakini wengine hawajui nini wafanye wajazwe  nguvu za Roho  Mtakatifu  na wengine wanajua lakini hawana kiu ya kujazwa nguvu hizo.

         Pili vijana wengi hawajui namna ya kuenenda kwa Roho .

Paulo kwa warumi anasema” kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” Warumi 8:14 na pia kwa wagatia  anasema” Basi nasema  enendeni kwa Roho hamtatimiza kamwe   tamaa za mwili “Gal 5:16.         Kuna  wengi waliojazwa lakini si wote wanaoenenda au wanaoishi wa Roho. Vijana wengi Mungu amewapa  vitu vizuri  sana ndani yao lakini kwa sababu ya kukosa utiifu na kutoenenda kwa  Roho wameshindwa kusimama kwenye nafasi zao.    

Tatu  vijana wengi wameshindwa kushirikiana  na upako wa Mungu uliodhihirishwa kwao.

Hili ni tatizo kubwa kwa  kweli, Mara nyingi Mungu  amekuwa akiwapa upako, nguvu au uweza wa kufanya mambo  mbalimbali vijana. Sasa si vijana wote  wanaojua  namna  ya kushirikiana  na  huo upako ambao Mungu aliwapa kwa jambo fulani  Mfano, Mungu anaweza akampa kijana upako wa kuomba lakini  kijana  huyo badala ya kuomba yeye anaangalia  mpira, au ni mwanafunzi anatakiwa kusoma na Mungu ameleta upako  huo  sasa yeye anaenda kuomba mambo huwa hayakai hivyo. Upako lazima utumike kwa kusudi  lile  uliotumiwa. Upako wowote unaokuja kwako unakuja kwa kusudi maalumu. 

Nne Kukosa maarifa ya Mungu.

Mungu anasema katika Hosea 4:6 kila kipengele cha kwanza  watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa na pia katika Zaburi 119:9 anasema “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii akilifuata neno lake”. Sasa kwa sababu  nazungumza na vijana naweza nikaweka mistari huu hivi “Vijana wangu wanaagamizwa kwa kukosa maarifa. Maarifa yanayozungumzia hapa ni mafundisho ya neno la Mungu.

Vijana wengi wako  tayari kuangalia mechi mbili mfululizo kuanzia saa nne kasoro usiku hadi saa  nane kwa masaa ya Kitanzania, lakini hawako tayari kusoma Biblia kwa saa moja, wako tayari kuangalia “Movie” za kinigeria, au za kizungu hata masaa matatu (3) lakini si kuangalia na kusikiliza mafundisho ya Neno la Mungu. Na Biblia inasema Apendaye mafundisho hupenda maarifa. Sasa kwa vile vijana wengi hawapendi mafundisho ndiyo maana hawako kwenye kusudi la Mungu. 

Tano, vijana wengi bado wanaipenda dunia,

Mzee Yohana katika 1Yohana 2:15” Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia, mtu akiipena dunia kumpenda Baba  hakupo ndani yake”. Na pia  Daudi anasema katika Zaburi  1:1 Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki wala  kusimama katika njia ya wakosaji wala     hakuketi barazani pa wenye mzaha.Ni vijana wachache sana katika  kanisa la leo ambao wako tayari kujikana nafsi zao kwa ajili ya Mungu wengi wanapenda kupoteza muda kwa habari  zisizo za Msingi, wengi wanapenda mzaha na utani, ni vijana wachache  ambao wanaweza kuacha kuangalia mchezo kwenye TV, au  akakataa kwenda kutembea ufukweni kwa lengo  la kuomba, au kusoma Neno, ninachojaribu kusema hapa ni hiki, najua kila jambo lina wakati wake, lakini ni vijana wachache sana waliojizuia katika mambo ya mwili kwa ajili ya kufanya yaliyo mapenzi ya Mungu.

Sita, Vijana wengi hawajazivaa silaha za vita.

 Waefeso 6:11 Vaeni Silaha zote za Mungu, mpate kuzipinga hila  za shetani.Viajana wengi wameshindwa kumshinda mwovu kwa sababu hawazajivaa silaha za vita. Wengine hawajui silaha za vita ni zipi? Lakini wengine wanajua lakini hawajazivaa. Ile sura ya sita ya waefeso 6:10-18 Paulo anazungumzia silaha za vita, ambazo ni kwlei, haki, amani, Imani, wokovu na Neno la Mungu. Sasa hizi ni silaha na kama ni silaha zina namna zinavyovaliwa na namna zinavyotumika. Sasa si vijana wote waliozivaa silaha, wengi hawasomi neno la Mungu, hawatendi haki, wengi wana imani ya maneno isiyo ya  Matendo.

Saba, Vijana wengi wanaishi bila kuwa na malengo katika maisha yao / maono.

Mithali 29:18. Inasema “Pasipo maono watu huacha kujizuia bali ana heri mtu yule aishikaye sheria”. Hivi leo  ukiwauliza vijana wengi kwamba una maono au hasa malengo gani katika maisha yako? Asilimia kubwa watakujibu  sina malengo  yeyote  yale.Wakati huo huo hakuna aliyeumbwa kwa bahati mbaya Yeremia  29 :12. Kwa kila mtu Mungu analokusudi maalum la kumuumba na pia anayo malengo na mikakati ya kumpa huyu mtu atekeleze katika maisha yake. Sasa kwa sababu vijana wengi  hawana na hawajajua  hayo malengo ndio maana wanafanya  kila kinachotokea mbele yao bila kujua  kama ni kusudi la Mungu.

    Naamini  baada ya kuwa umesoma ujumbe huu umepata maarifa ya kukusaidia kukaa katika nafasi yako kama kijana kwa sababu umeshajua sababu za kuktokukaa kwenye nafasi yako.

 

KWA NINI MUNGU ANATAKA TUENENDE KWA ROHO?

September 16, 2006

Na; Patrick Sanga.

 Ukisoma katika warumi 8:14 Biblia inasema “kwa kuwa wote wanaoongozwa  na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” na pia Paulo kwa wagalatia anasema” Basi nasema Enendeni kwa Roho,wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili Wagalatia  5:16. 

Hapa tunaona jinsi Paulo anavyosisitiza kwa makanisa ya Rumi na korinto kuhusu suala zima la kuongozwa  na Roho  Mtakatifu. Anawaambia warumi kwa  kuwa wote wanaongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana  wa Mungu maana yake haijalishi  ana umri gani, ni wa dhehebu gani, jinsia gani maadamu anaongozwa  na Roho wa Mungu huyo ni mwana wa Mungu na bado anawaagiza wagalatia akisema Basi nasema  enendeni   kwa Roho………….. anaposema enendeni maana  yake  mkiongozwa  na Roho, au mkimfuata  Roho katika yale anayowaagiza. Maneno haya yanaonyesha  zipo sababu za msingi  kwa nini tunatakiwa kuongozwa  na Roho  sasa hapa sizungumzii kazi za Roho mtakatifu najua zipo kazi nyingi anazozifanya Roho Mtakatifu lakini mimi nazumgumzia sababu za kuongozwa  na Roho Mtakatifu, ambaye ndio agano jipya la Mungu kwetu (Yeremia 31:31) katika hiyo Yeremia Neno linasema “Angalia siku zinakuja asema Bwana nitakapofanya  agano jipya na nyumba ya Israel. Sasa ukiendelea kusoma mistari inayofuata utaona anazungumzia habari za kutia sheria yake katika mioyo ya watu.

Sasa hili ndilo agano jipya la Mungu pamoja na wanadamu. Sasa usipojua kwa nini unatakiwa kuongozwa na Roho na siyo akili zako, au mazoea, au taratibu za kwako n.k. hautajua umuhimu wa kuongozwa na Roho Mtakatifu na pili hautaona sababu za kuongoza na Roho Mtakatifu. Sasa  lengo la ujumbe huu ni kukufundisha sababu za msingi  za kwa nini unatakiwa kuongozwa na Roho Mtakatifu na siyo akili  zako au mawazo yako. Sasa baada ya utangulizi huo mfupi na tuangalie sababu hizo za msingi. 

Moja,

Ili tusizitimize tamaa za mwili wagalatia 5:16

“Basi nasema enendeni kwa Roho , wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.Tunatakiwa tuenende kwa Roho ili tusizitimize tamaa za mwili. Siku zote mwili na Roho ni maadui nia ya mwili ni mauti na nia ya Roho ni uzima na amani (Warumi  8:7). Maana  yake siku zote mwili utakuongoza kufanya mambo ambayo mwisho wake ni mauti ya kiroho na  hata kimwili pia.

Utakuongoza katika  tamaa zake, sasa usipoongozwa na Roho huwezi  kujizuia kutekeleza tamaa za mwili na kwa sababu hiyo wewe si mwana wa Mungu   na mtu wa namna  hii hataingia mbinguni kamwe.  Katika 1Wakorinto 6:9-10 anasema “Au  hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme  wa Mungu? Msidanyanyike, waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala  waabudu  sanamu, wala wazinzi, wala  wafiraji, wala walawiti, wala walevi, wala watamanio, wala walevi wala   watukanaji, wala wanyang’anyi.Sasa utakapoongozwa na Roho Mtakatifu utaratibu wake utakuacha huru mbali  na hayo mambo ya mwili au nia ya mwili na utakuongoza katika uzima  na amani  na kulitenda tunda la Roho ambalo  ni upendo, furaha, amani, uvumilivu utu wema  , fadhii, uaminifu, upole na kiasi “Wagalatia 5:22-23”.

 Mbili,

Ili tupate kuyaelewa mafumbo ya Mungu  na kuyafasiri mambo ya Rohoni kwa maneno ya Rohoni.

1Wakorinto 2:10 inasema “ Lakini  Mungu  ametufunulia  sisi kwa Roho, maana Roho huchunguza yote hasa mafumbo ya Mungu” na ule mstari wa 13 unasema “ Nayo twayanena , si kwa maneno yanayofundishwa  kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa  na Roho, tukiyafasiri mambo ya Rohoni  kwa maneno  ya Rohoni. Hapa najua walio  wachungaji, walimu  wa neno la Mungu au viongozi wa vikundi mbalimbali vya kiroho watanielewa zaidi.

sikiliza Roho Mtakatifu ndiye mwenye uwezo wa kuchunguza kilichopo kwenye ufahamu wa Mungu kuhusu wewe, ndoa yako, kanisa lako, biashara yako, masomo yako, nchi  yako n.k. sasa akishachunguza ndiyo anakujulisha maana wewe ulikuwa hujui. Pia Roho Mtakatifu ndiye  anayekusaidia kuyanena, kuyafundisha au kuyafafanua maneno ya Mungu kwa  watu wake,  anaposema kuyafasiri  maana yake kuyafundisha mambo ya Rohoni kwa jinsi / namna ya Rohoni.

 Hivyo kama  wewe ni kiongozi au mwalimu wa neno  la  Mungu, ukiongozwa na Roho, yeye atakuongoza / atakusaidia kuwafundisha hao watu neno la Mungu kwa jinsi  ya Rohoni yaani kwa mfumo wa Rohoni kulingana na watu ulio nao, maana yeye ndio mtunzi wa hilo Neno,soma mwenyewe 2Petro 2:21” maana  unabii haukuletwa popote kwa mapenzi  ya mwanadamu, bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

Tatu,

 

Ili   tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu na kuyapokea mambo ya Roho na Mungu .

Iwakorinto 2:12 inasema “Lakini sisi hatukupokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa  na Mungu” na ule wa 14 unasema “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei  mambo ya Roho wa Mungu maana kwake huyo ni upuuzi, wala hawezi kuyafahamu kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya Rohoni. Unapoongozwa  na Roho Mtakatifu ndipo anapokusaidia kujijua wewe mwenyewe vizuri. Anaposema  upate kuyajua yale ambayo Mungu amekupa katika maisha yako.Roho mtakatifu atakusaidia kujua aina ya vipawa  ulivyonavyo, karama za Rohoni ulizonazo, huduma ulizonazo kama umeitwa huko, atakusaidia kujua vizuri unaweza kufanya  nini na nini  huwezi, kipi ufanye  na kipi usifanye, atakusaidia kujua baraka zako za kiroho  na kimwili pia. Kwa kifupi  atakusidia kulijua kusudi   la Mungu katika maisha yako na vipi ufanye ili uweze kulifikia hilo kusudi na zaidi  atakupa upako/ nguvu za kuweza kuyapokea yale yote anayo kuagiza ili uweze kulifikia kusudi lake kwako na kuzirithi baraka zako maana katika zaburi 32:8  anasema “Nitakufundisha  na kukuonyesha njia utakayoienda nitakushauri, Jicho langu likikutazama”.

 Nne,

Ili atusidie kuomba yale tunayotakiwa kuyaomba kwa wakati huo.

Warumi 8:26” kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua   kusikoweza kutamkwa”. Udhaifu unaozumgumziwa ni wa namna  mbili moja si rahisi kwa jinsi  ya  mwili kuomba kwa muda mrefu kwa sababu mwili ni dhaifu na pili udhaifu tulionao ni kushindwa kuomba jinsi inavyotupasa kuomba.

 Sasa  tunapoongozwa na Roho, maana yake moja anatusidia tuweze kuomba na zaidi anatufundisha namna ya kuomba  na kutuongoza  yapi tuyaombee kwa wakati huo  au kipindi hicho. Mfano wewe unaweza ukawa unaomba upako wa Roho Mtakatifu katika huduma na yeye  Roho Mtakatifu, anajua kwamba  ameshakutia mafuta  na shida uliyonayo ni kutokujua namna ya kushirikiana na upako wake ulio juu yako. Hivyo yeye atakuongoza kuomba kwa habari ya kushirikiana  na upako aliouweka juu yako. Kwa  kifupi yeye kwa sababu ndiye mwenye maisha yako atakuongoza siku zote kuomba yale unayotakiwa kuyaomba kwa majira hayo iwe kuhusu masomo, ndoa, kanisa, nchi n.k.

Tano,

Ili atuongoze katika kufanya maamuzi.

 2Wakorinto 3:17  Basi Bwana ndiye Roho, walakini alipo Roho  wa Bwana, hapo ndipo penye  uhuru”  pia ukisoma warumi 8:1-2 inasema  “sasa, basi hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu, kwa sababu sheria ya Roho wa uzima  ule ulio katika kristo Yesu imeniacha huru, mbali  na sheria ya dhambi na mauti”  kufanya maamuzi ni sehemu  ya maisha ya mwanadamu. Yapo  maamuzi  mengi sana  ambayo mwanadamu anatakiwa kufanya na hawezi kukwepa kuyafanya.

Sasa Mungu kwa kulijua  hilo ametupatia Roho Mtakatifu ili atusaidie katika kufanya  maamuzi. Roho Mtakatifu anapokuwa Bwana   kwako, yaani  mtawala, kiongozi ndipo anapokupa uhuru juu ya kufanya maamuzi katika maisha yako. Maana yake ulikuwa hujui nifanye nini? Niamueje ? Sasa yeye anakuletea uhuru ndani wa  kufanya jambo ambalo anajua ni la mafaniko  kwako. Kumbuka siku zote nia ya Roho ni uzima na amani.

 Huenda ziko sababu nyingi ni kwa nini unatakiwa uenende  kwa Roho, lakini hizi tano ndizo Mungu alizonipa tuweze kushirikiana kujifunza. Ni imani yangu kwamba utakapoamua kutaka na kupenda kuongozwa na Roho ndipo utakapoona Mungu akijifunua kwako .

 

Tuendelee  Kuombeana