Archive for the ‘Nyaraka’ Category

NGUVU YA ULIMI (MANENO) KATIKA KUAMUA HATMA YA MAISHA YAKO (Sehemu ya mwisho)

February 18, 2017

Na: Patrick Sanga

8y

Mada: Mambo muhimu kujua kuhusu matumizi ya kinywa

Katika sehemu ya kwanza nilikuonyesha mistari mbalimbali kutoka kwenye Biblia inavyozungumza kwa habari ya ulimi ili upate kujua nguvu ya ulimi ilivyo na athari zake. Ili kusoma sehemu ya kwanza tafadhali bonyeza link ifuatayo https://sanga.wordpress.com/2017/01/31/nguvu-ya-maneno-katika-kuamua-hatma-ya-maisha-yako-sehemu-ya-kwanza/

Katika sehemu hii ya pili na ya mwisho nitafundisha mambo muhimu kuzingatia na kujua kwa habari ya matumizi ya ulimi (kinywa) ili kuweka hatma nzuri ya maisha yako kwa sababu maneno yako yana nguvu ya kuathiri maisha yako ya sasa na baadaye pia.

3

 • Jifunze kuzuia ulimi wako usinene mabaya – Mtume Petro anatueleza kwamba Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila’ (1Petro 3:10). Ikiwa unataka kuwa na maisha yenye furaha na amani (siku njema) basi chunga sana unayoyasema. Ukiruhusu kinywa chako kunena mabaya na kutunga hila usitegemee kuwa na amani ya kweli, maana utaishi kwa maneno hayo. Daima usiakiache kinywa chako kinene mabaya wala kutunga hila kwa kuwa mtu azuiaye kinywa chake kunena mabaya, huilinda nafsi yake na taabu (Rejea Mithali 21:23 & Zaburi 50:19). Kumbuka unaponena mabaya juu ya mwingine, kama mtu huyo hana Yesu aliye hai wa kumuongoza kusamehe, basi ujue ndani yake unaamsha roho ya kisasi na uharibifu. Wapo pepo ambao kazi yao ni kufuatilia nini mtu anajinenea au kunena juu ya mwingine hususani yale ambayo ni mabaya, na kazi yao kufuatilia maneno hayo kuhakikisha kwamba yanatimia au yanatokea.

r

 • Jizuie kunena unapokuwa na hasira – Katika Waefeso 4: 26 imeandikwa Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka’. Mara nyingi kwenye jambo hili watu wengi wameshindwa kujizuia, na ukitaka ujue yaujazayo moyo wa mtu au mtu anakuwazia nini subiri azungumze habari zako au mambo yako akiwa amekasirika.  Hasira ni mlango ambao adui anautumia sana kuharibu maisha ya watu wengi na hasa wanandoa kwa sababu ya yale ambayo kila mmoja aliyanena akiwa na hasira na uchungu juu ya mwenzake. Biblia inatuambia kunyamaza ni hekima, hivyo jifunze kunyamaza. Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu’ (Mithali 17:28).

 

 • Jifunze kulinda kinywa chako – ukienda kwenye Mithali 13:3 Biblia inasema ‘Yeye alindaye kinywa chake hulinda nafsi yake, bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu’. Naam watu wengi hawajui kwamba kadri unavyosema maneno mabaya, ya uongo, kusengenya au kusingiza au kuchafua nk, ndivyo wanavyojitengenezea mazingira ya uharibifu kwenye maisha yao binafsi na si tu kwa wale ambao wanawaelekezea maneno husika.Katika Mithali 21:23 imeandikwa ‘Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu’. Hii ni kwa sababu maneno unayoyanena unayaumba au kuyaandika na kwa jinsi hiyo maneno hayo yana nguvu ya kuongoza na kuathiri hisia, nia na maamuzi (matendo) yako.

s

 • Jifunze kuwa mtu wa maneno machache – Biblia inatuambia ‘Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili’ (Mithali 10:19). Naam sio lazima kusema kila neno linalokujia jifunze kunyamaza na kuzuia maneno yako, maana azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa. Ingawa Yakobo anatuambia ulimi haufugiki, lakini kwa mujibu wa (Mithali 17:27a) mtu anaweza kuzuia maneno yake na hiki ndicho alichomaanisha Mzee Yakobo mwenyewe pale aliposema iweni wepesi wa kusikia na si wepesi wa kusema (Yakobo 1:19).
 • Jifunze kufikiri kabla hujanena – Katika Mithali 12:18 imeandikwa ‘Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; Bali ulimi wa mwenye haki ni afya. Naamini umeshawahi kupitia mazingira ambayo unajutia maneno uliyoyanena. Mara nyingi majuto hayo ni matokeo ya kunena bila kufikiri. Hii ina maana kabla ya kusema, jifunze kufikiri kwanza athari ya unachotaka kusema kwa mtu au watu unaotaka kusema nao. Katika kufanikisha hili mwimbaji wa Zaburi akasema Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu’ (Zaburi 141:3).

Photo 3

 • Jaza neno la Mungu moyoni mwako (Yoshua 1:8) – Hii ni kwa sababu yale yaujazayo moyo wa mtu ndiyo yamtokayo. Hivyo ili kusaidia kinywa chako kutoa maneno yenye kujenga sharti neno la Mungu likae kwa wingi moyoni. Hatutegemei mtu aliyejaa neno la Mungu atukane watu, kulaani, kusengenya nk. Katika Yakobo 3:9-10 imeandikwa ‘Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo’. Naam ile kusema haifai mambo hayo kuwa hivyo ni ishara kwamba hatupaswi kutumia vinywa vyetu kunena mabaya na kutunga hila wakati tunatumia pia ulimi huo huo kumtukuza Mungu.

8

Katika kumalizia ujumbe huu sina budi kusema mwanadamu hana budi kuwa makini sana na kinywa chake. Maisha ya mtu yanachangiwa kwa sehemu kubwa na maneno yake, akiutumia vizuri ulimi wake  ataishi vizuri na akiutumia vibaya mabaya yatakuwa haki yake. Naamini ujumbe huu mfupi umekuongezea ufahamu wa kutosha mosi kuhusu Biblia inasema nini juu ya ulimi na pili namna ya kukitumia kinywa chako vizuri ili kuamua hatma nzuri ya maisha yako.

‘Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa’ (Zaburi 35:28)

Utukufu na Heshima vina wewe Yesu wangu, wastahili BWANA.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, iwe nanyi.

NGUVU YA MANENO KATIKA KUAMUA HATMA YA MAISHA YAKO (Sehemu ya kwanza)

January 31, 2017

Na: Patrick Sanga

Waraka wa Januauri 2017

1a

Mpenzi Msomaji heri ya mwaka mpya wa 2017.

Changamoto nyingi ambazo watu wengi wanazipitia leo ni matokeo ya maneno ambayo wamekuwa wakiyanena bila kujua athari yake kwenye maisha yao binafsi, familia zao, kazi na hatma (future) yao. Kuna watu wengi sana ambao haki zao zimeibiwa, wengine wamefungwa, wamepoteza kazi zao, wapendwa wao au kuonewa kwa namna nyingi yote haya yakiwa yamesababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya ulimi (kinywa).

Kutokana na ukweli kwamba watu wengi hawajui athari za kutumia kinywa vibaya, nimeona vema kuandaa somo hili ili, mosi kuonyesha kile ambacho Biblia inasema kuhusu ulimi na pili kufundisha mambo ya msingi kujua kuhusu matumizi ya ulimi ili kusaidia watu kuepukana na athari (mauti) mbaya ziletazwo na ulimi. Fuatana nami sasa tuangalie kile ambacho Biblia inasema kuhusu ulimi katika sehemu hii ya kwanza:

Katika Mithali 18:21 Biblia inasema Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake’.  Katika andiko hli ni dhahiri kwamba matokeo (athari) ya maneno yanaweza kuwa mazuri au mabaya kutegemeana na maneno yanayotoka kwenye kinywa cha mtu husika. Naam ni kawaida ya watu kusema lakini sio wengi wanajua kwamba, ulimi ingawa ni kiungo kidogo kimebeba uzima na mauti, tegemeana na mtu anavyoutumia.

8y

Kwenye Waraka wa Yakobo imeandikwa hivi ‘Maana twajikwaa sisi sote katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika KUNENA, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye KUUZUIA na mwili wake wote kama kwa lijamu’ (Yakobo 3:2). Neno twajikwaa, kwenye toleo la kiingereza la KJV limeandikwa ‘offend’ ambapo tafsiri yake hai-ishii kuonyesha maneno yanayosemwa yana athari kwa mtu binafsi tu, bali pia athari hiyo inapelekea kumizwa kwa mtu au watu wengine.

Mzee Yakobo anaendelea kuonya askisema ‘Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio UUTIAO MWILI WOTE UNAJISI, huuwasha moto mfululizo wa maumbile, nao huwasha moto na jehanum. Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti’ (Yakobo 3:6&8). Mpenzi msomaji je umeona jinsi ulimi wa mtu ulivyo na nguvu ya ajabu. Biblia inauita ulimi kuwa ni moto, uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti na ndio unaoleta unajisi kwenye mwili wote wa mtu.

4d

Je mpenzi msomaji wewe unakitumiaje kinywa chako, fahamu wapo wanadamu wanaotumia vinywa vyao kwa hila, furaha yao ni kuona wengine wakiharibikiwa na si kufanikiwa. Zaburi inasema ‘Ulimi wako watunga madhara, Kama wembe mkali, Ewe mwenye hila Umependa mabaya kuliko mema, Na uongo kuliko kusema kweli. Umependa maneno yote ya kupoteza watu, Ewe ulimi wenye hila’ (Zaburi 52:2-4). Pia katika Warumi 3:13-14 imeandikwa Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira i chini ya midomo yao. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu’ Naam ole wako ulimi unaokazana kutunga hila, kuachilia laana, kusema uongo na kupoteza watu, maana mabaya yaliyopandwa yatakurudia.

Je tuufafanishe ulimi na kitu gani sisi wa kizazi cha leo?, naam ni zaidi ya kimbunga, kwa kuwa maneno yanaishi kizazi hata kizazi. Ndio maana leo vita haviishi baina ya familia, makabila, makanisa, mataifa nk, kwa sababu maneno ambayo yalinenwa nyakati hizo na watangulizi (wazee) wetu kuhusu watu wa upande ya pili iwe ni kwa haki au kwa hila athari zake zinaendelea kutugusa hadi leo.

Ukienda kwenye Zaburi 45:1 Biblia inatuambia Moyo wangu umefurika kwa neno jema, Mimi nasema niliyomfanyizia mfalme; ulimi wangu ni KALAMU ya mwandishi mstadi’. Hapa Mwandishi ameufananisha ulimi na kalamu, na hii ni kuonyesha kwamba kila unapotamka maneno ujue unaumba au unaandika kile unachokisema na hivyo ni muhimu sana kufikiri kabla hujasema jambo lolote, ili kwa kinywa chako usiandike ujumbe ambao utakuletea madhara makubwa.

8

Mpenzi msomaji kumbuka kwamba tabu nyingi ambazo wanadamu wanazipata leo ni matokeo ya matumizi mabaya ya vinywa vyao. Jambo muhimu kuelewa ni kwamba mtu anapotumia kinywa chake kusema maneno mabaya, ya uongo na yenye hila dhidi ya mwingine si tu anaumba hayo mabaya kwa huyo mtu, bali yeye binafsi anajiletea madhara makubwa pia. Naam, yale mtu anayanena kwa kinywa chake yana nguvu kubwa ya kuathiri vibaya maisha yake ya sasa na ya baadaye sambamba na uzao wake.

 Neema ya Kristo iwe nanyi, nitaendelea na sehemu ya pili……..

 Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu.

NAMNA SHETANI ANAVYOTUMIA ROHO YA USAHULIFU KUHARIBU MAISHA YA WAAMINI

December 9, 2016

Na: Patrick Sanga

1

Shalom, katika waraka huu wa Desemba 2016 nimeona ni vema kukumbusha juu ya jambo hili ambalo si wengi wanalijua ili uweze kuwa makini katika utendaji wa neno la Mungu na hivyo kupokea kilichokusudiwa kwenye kila hatua ya maisha yako. Tafadhali rejea andiko la somo, Luka 8:4-15, kwenye  ule mstari wa 12 imeandikwa ‘Wale wa karibu na njia ndio wasikiao, KISHA HUJA IBILISI AKALIONDOA HILO NENO MIOYONI MWAO, wasije wkaliamini na kuokoka’.

Ni vizuri ukafahamu kwamba ni kazi ya Shetani kupofusha/kuondoa amri na maagizo ya Mungu kwenye fahamu/mioyo ya watu ili wasiyatende na hivyo kuwafanya WASAHAU wajibu wao na kisha kuleta athari mbalimbali kwenye maisha yao, ambapo Shetani  hutumia roho ya usahulifu ili kufanikisha jambo hili. Yafuatayo ni maeneo muhimu ambayo Shetani huyalenga katika kutekeleza jukumu hili muhimu kwa ufalme wa giza.

 • Kuwafanya watu wasahau nafasi zao katika mwili wa Kristo

Shetani kwa kufahamu umuhimu na athari ya waamini kusimama kwenye nafasi zao kama viungo kwenye mwili wa Kristo, anatumia kila njia kuhakikisha anawasaulisha watu nafasi zao na hivyo kushindwa kutekeleza wajibu wa nafasi zao. Kumbuka mtu anaposhindwa kusimama kwenye nafasi yake katika ulimwengu wa roho, si tu atashindwa kutekeleza majukumu ya nafasi yake bali zaidi atapoteza na thamani yake kwenye ufalme wa Mungu.

2a

Moja ya nafasi muhimu ni ile ya mtu kuwa Mlinzi katika ulimwengu wa roho. Biblia katika Isaya 62:6 na Ezekiel 33:7 inatujulisha kwamba mtu ameitwa au amewekwa na Mungu kuwa mlinzi wa maeneo mbalimbali. Mlinzi ni nafasi inayomtaka mhusika afanye kazi hiyo kama Muombaji, Muonyaji, Muonaji, Mtoa taarifa na mwisho Mshauri wa Mungu kuhusu eneo lake la ulinzi. Naam, kwa kuwa Shetani amendoa neno la ulinzi kwa waamini wengi, hivi leo walinzi wengi ni vipofu na hawako kwenye nafasi zao (Isaya 56:10).

 • Kuwafanya wasahau wajibu wa kuvipiga vita vya kiroho (Waefeso 6:10-12).

Katika fungu hilo Biblia inasema ‘Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. VAENI SILAHA ZOTE ZA MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho’

7

Kupitia roho ya usahulifu, Shetani amewafanya watu wasikumbuke kwamba kwa  kila sekunde wako vitani, tena vita ambayo ni endelevu, na kwa maana hiyo waamini wengi hawajazivaa silaha zote za Mungu na ndiyo maana wanaonewa na kuangamizwa. Kupitia roho hii amewafanya waamini wengi kuishi maisha yao kama wa mataifa ambao wanabaki kulalamika juu ya yale yanayowatokea, badala ya kusimama imara na kuvipiga vita vya kiroho.

 • Kuwafanya wasau kuwaza sawasawa na neno la Mungu

Katika Yoshua 1:8 imeandikwa ‘Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana’.

Watu wengi wanawaza kinyume cha ahadi/neno la Mungu kwenye maisha yao na kwa njia hiyo wanajikuta wanakiri mabaya juu yao na hivyo kuishia pabaya. Shetani amewafanya waamini kuwaza kama wa mataifa kwenye kila changamoto wanazokutana nazo, hata wamesahu kwamba neno la BWANA ni taa ya miguu yao.

4

Shetani anajua akifanikiwa kukufanya uwaze nje ya neno la Mungu, atakuwa amefanikiwa kukamata maamuzi yako na hivyo kuongoza maisha yako kwenye kusudi lake la uharibifu. Naam usikubali kunaswa na hila hii ya ufalme wa giza, hakikisha neno la Mungu linaongoza kuwaza kwako na maamuzi yako diama.

 • Kuwafanya washindwe kutumia vizuri fursa wanazopewa na Mungu

Katika Mathayo 11:20-21 imeandikwa ‘Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu haikutubu. Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenuingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu’. Tafadhali soma pia Mathayo 23:37 uone Yesu anavyousikitikia Yerusalemu kwa kutozipokea fursa walizopewa.

Shetani amewafanya waamini wengi washindwe kuelewa sababu za msingi za kwa nini Mungu amewapa nafasi walizonazo katika ulimwengu wa mwili, kwa mfano uongozi (kiroho/kijamii/kisiasa nk), elimu, biashara, miradi mbalimbali, familia, huduma nk. Kwa jinsi hiyo hata fursa za ufalme wa Mungu kujengwa na kuendelezwa zinapokuja ili wahusika wazitumie, kwa kutokea kwenye nafasi zao wanashindwa kwani wamesahau kwa nini wapo walipo na wako walivyo.

2b

Naam badala yake Shetani ameingiza roho za majivuno, kiburi, dharau, uchoyo na kupenda fedha kwa waamini kiasi kwamba hata fedha ambazo Mungu anawapa wanafikiri ni kwa ajili yao tu na familia zao, wameshau kwamba Mungu anawapa nguvu za kupata utajiri ili kulifanya imara agano lake.

Mpenzi msomaji ningeweza kuendelea kuandika na kuandika na kuandika, lakini katika ujumbe huu nimeona ni vema kukuonyesha baadhi ya maeneo yaliyobomoka ambayo hapana budi kuyatengeneza. Tafadhali hakikisha kwamba upo kwenye nafasi yako, unadumu kuvipiga vita vizuri vya kiroho, unadumu kuwaza sawasawa na neno la Mungu na kisha unatumia kila fursa inayokuja kwa lengo la kuendeleza ufalme wa Mungu. Kumbuka siku zote tupo vitani, roho ya usahulifu ni moja ya roho ambazo unatakiwa kupambana nayo kila siku ili kuhakikisha unaelewa na kukitenda kila kilicho cha Mungu kwenye maisha yako.

Neema ya Kristo iwe nawe.

USIPOKUWA NA WAZO JIPYA HUWEZI KUTOKA MAHALI ULIPO

October 5, 2016

Na: Patrick Samson Sanga

6

Salaam katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

Katika waraka wa Oktoba 2016 nimeona umuhimu wa kuandika ujumbe huu maalum ambao naamini utabadilisha kufikiri kwako na kukuongoza kuishi sawasawa na mapenzi ya Mungu kwenye maisha yako.

Nakumbuka mwaka 2010 nilikuwa nikipitia changamoto (majaribu) kubwa kikazi na kifamilia pia, naam changamoto ambazo zilichukua miezi kadhaa zikiniondolea furaha yangu. Nilidumu kumuomba Mungu katika kipindi chote hicho bila kukata tamaa ili anishindie, huku nikimuuliza natokaje kwenye changamoto hizi, mbona ni muda mrefu sasa?. Siku moja nilipomaliza kusoma neno na kuomba nikaamua kujipumzisha huku nikitafakari, ndipo, nikasikia sauti ikiniambia ‘usipokuwa na wazo jipya huwezi kutoka mahali ulipo’.

Sentensi hii ya ajabu ililikuwa ni mwongozo wa kunisaidia kutafuta wazo jipya lenye kuleta ufumbuzi wa kutoka mahali nilipokuwa. Hivyo nilibadlisha maombi yangu, kutoka kwenye maombi ya kuumia na kulalamika kwenda kwenye maombi ya kupata wazo jipya la kunitoa mahali nilipo. Haikuchukua hata wiki moja nikapata wazo (neno/ufunuo) ambalo lilibadilisha kwanza fikra (mtazamo) zangu kutoka kwenye mtazamo hasi ambao nilikuwa nao juu ya yale niliyopitia na juu ya wale ambao niliamini walichangia niwe kwenye hali niliyokuwa nayo. Naam baada ya kuridhia/kutii wazo jipya la BWANA, ndipo na ufumbuzi wa changamoto ukatokeza kama vile kuwasha umeme na nuru yake ikaangaza pande zote.

2

Katika Yeremia 29:11 imeandikwa hivi ‘Maana nayajua mawazo ninayowawazia, si mabaya, bali kuwapa ninyi tumaini katika siku zenu za mwisho’.  Ukienda kwenye 1Wakorinto 2:9 imeandikwa ‘lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao’.

Mistari hii miwili inatufanya tujue kwamba Mungu ANAYO mawazo ya amani (kukufanikisha) anayotuwazia kwa kila nyanja ya maisha yetu (yako). Ukweli ni kwamba haya ni mambo ambayo hakuna jicho limeona wala sikio lililosikia, na wala hayajaingia (kama wazo) kwenye moyo wa mwanadamu yeyote.             Je unajua ni kwa nini bado hayajaingia kwenye moyo wa mwanadamu yoyote? Hii ni kwa sababu hayo ni mawazo mahususi (specific) kwa ajili yako tu na si mtu mwingine yoyote na ndiyo maana unahitaji kuyajua ili kuishi sawasawa na kusudi la Mungu kwenye maisha yako.

Sasa ukienda katika Isaya 55:8 Mungu anasema waziwazi kwamba ‘Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu…’. Fahamu kwamba katika kila unalolipitia au linalokukabili ndani yake kuna mawazo/njia za Mungu za kulikabili au kulitekeleza ambazo ni tofauti na njia zetu wanadamu. Ndio maana katika Zaburi 32:8 anasema Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama’. Hiii ina maana unahitaji KUTAFUTA KUTOKA KWA MUNGU ILI KUPATA WAZO NA NJIA SAHIHI YA KUSHUGHULIKA NA CHANGAMOTO UNAZOZIPITIA, hata hivyo uhusinao na mawasiliano mazuri kati yako na Mungu ni msingi muhimu kwenye hili.

 Je unalipataje wazo jipya?

hy

Rejea ya mistari husika hapo juu inatupa kujua kwamba kwa Mungu ndiko kwenye mawazo sahihi na muafaka ya kututoa mahali tulipo. Hivyo unahitaji kulitafuta wazo jipya toka kwa Mungu kwa njia ya maombi ukiongozwa na neno lake. Kadri utakavyokuwa mwaminifu kutaka kujua kutoka kwake wazo jipya uwe na uhakika utajibiwa maana yeye ni mwaminifu katika ahadi zake.

Katika Wafilipi 4:6-7 imeandikwa Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu’.  Kwenye toleo la kiingereza la ESV mstari ule wa saba  umeandikwa ‘And the peace of God, which surpasses all understanding, will GUARD your hearts and your minds in Christ Jesus’.

af

Katika kufanya maombi ya kutafuta wazo jipya unahitaji kuongozwa na neno la Mungu kwa sababu ndani ya neno ndipo kuna elimu (maarifa au hekima au ufahamu) ya Mungu ipitayo akili zote. Mtume Paulo aliijua siri hii ndio maana akawaambia Wafilipi, msijisumbue, hivyo akawataka wamweleze Mungu mahitaji na changamoto zao. Kisha akawafunulia siri ya kile kitakachotokea akiwaambia, kwa Mungu kuna amani ipitayo akili zote, na kazi ya hiyo amani ni KUWAONGOZA (GUARD) KWENYE NIA NA MAAMUZI SAHIHI JUU YA YALE MNAYOYAPITIA. Amani ya Kristo hapa inawakilisha wazo lililo bora kuzidi mawazo mengine, ndiyo maana imeandikwa ipitayo akili zote, na kazi ya mojawapo ya amani ni kumsaidia mtu kufanya maamuzi sahihi, naam mtu hawezi kufanya uamuzi sahihi kama hajapata wazo sahihi toka kwa Mungu.

Ukweli wa jambo hili tunauona tunapounganisha mawazo ya mistari hii maana imeandkwa‘Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu’ (Mithali 4:7) na hii ni kwa sababu ‘Mtu mwenye hekima ana NGUVU; Naam, mtu wa maarifa huongeza UWEZO’(Mithali 24:5) naam na uwezo na nguvu zake ni huu ‘Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; MIMI NI UFAHAMU, mimi nina nguvu. Kwa msaada wangu wafalme humiliki, NA WAKUU WANAHUKUMU haki. Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, WAAMUZI wote wa dunia’ (Mithali 8:14-16).

10

Mpenzi msomaji maneno haya yakutie nguvu usiwe mtu wa kulia lia au kulalamika hata kumuwazia Mungu vibaya, naam haijalishi unapita kwenye changamoto za aina gani fahamu kwamba kwa Mungu liko wazo lililo bora na lenye nguvu kushinda mawazo (sauti)  mengine yoyote ya wanadamu, Shetani nk, naam litafute wazo hilo kutoka kwa Mungu litakusaidia nawe utachukua maamuzi sahihi kwa msaada wa AMANI YA KRISTO IPITAYO AKILI ZOTE, KUMBUKA AKILI ZOTE.

Hebu nikuonyeshe mawazo mapya kadhaa wakati namalizia ujumbe huu;

 • Kama hivi sasa kuna wazo la mauti limekuzunguka, wazo jipya la BWANA LINASEMA hutakufa bali utaishi upate kuyasimulia matendo makuu ya BWANA (Zaburi 118:17)
 • Kama umezungukwa na wazo la hatari/hofu, wazo la Mungu siku ya leo LINAKUAMBIA kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa (Isaya 54:17)
 • Kama unapita kwenye mateso mengi na uonevu/kutotendewa haki, wazo jipya la BWANA linasema ‘Mateso ya mwenye haki ni mengi lakini Bwana humponya nayo yote’ (Zaburi 34:19) na tena linakuambia ‘utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia’ (Isaya 54:17).
 • Kama unapita kwenye hatia ya dhambi na umeijutia na kuitubia dhambi uliyoitenda wazo la Mungu siku ya leo linasema ‘Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako’ (Isaya 43:25).

Kumbuka kwamba katika kuleta wazo jipya Mungu anaweza kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusema nawe moja kwa moja, kupitia watumishi (watu) wengine, kupitia mahubiri au mafundisho ya kiroho kwenye vitabu, luninga, mitandao ya kijamii, blogs au website nk.

9

Mpenzi msomaji, kulia, kujisumbua, kulalamika au kulaumu wengine siyo njia ya kupata ufumbuzi. TAMBUA KWAMBA KWA MUNGU WETU LIKO WAZO JIPYA LA KUKUTOA MAHALI ULIPO, LITAFUTE NAWE UTALIONA NALO LITAKUSIADIA. Ikiwa haujaokoka na unapenda kuokoka bonyeza ‘link’ hii  https://sanga.wordpress.com/wokovu/  utapata mwongozo muafaka.

Utukufu na Heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA

… Utaiinua misingi ya vizazi vingi (Isaya 58:12)

FURAHA YA KUTIMIZA MIAKA KUMI (10) YA BLOG HII (Ten Years Blogging Anniversary)

September 16, 2016

Na: Patrick Saga

1

Shalom mpenzi msomaji, nakusalimu kwa jina la BWANA wetu Yesu Kristo.

Leo Septemba 16, 2016 blog hii ya www.sanga.wordpress.com  imetimiza miaka kumi (10) tangu nilipoifungua na kuweka ujumbe wa kwanza tarehe 16.09.2006. Katika kuadhimisha miaka kumi ya uwepo wa Blog hii leo nimeona ni vema kuandika historia fupi kuhusu uandishi wangu na ‘blog’ hii sambamba na kutoa shukrani kwa neema ya Mungu iliyokuwa nami kwa kipindi hicho.

Historia fupi ya blog hii – Nilianza rasmi kuandaa masomo mwaka 2003 nikiwa Mkoani Mbeya, hata hivyo sikuwa na ufahamu wowote kuhusu masuala ya blog au website. Hivyo pale nilipopata fursa ya kufundisha kanisani kwetu nilifanya hivyo ingawa kuanzia mwaka 2004 nilitamani sana kama ningepata fursa ya kuwafikia watu wengi zaidi kwa masomo niliyokuwa nikiandaa.

Mwaka huo huo ndipo BWANA aliposema nami kwa mara ya kwanza kupitia kitabu cha Isaya sura nzima ya 58 na akaniwekea msisitizo na maelekezo ya pekee kwenye mstari wa 58:12 unaosema Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; UTAIINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia”.

Ilipofika mwaka 2006 nilipata fursa ya kwenda nchini Kenya kwa masuala ya kihuduma, nikiwa mpakani mwa Kenya na Somalia, mji wa Garisa, BWANA alisema nami kuhusu elimu ya kuzimu (Doctrine of Hell), naye akaniambia ‘Watu wengi sana wanaenda kuzimu baada ya kufa kwa kuwa hawanijui mimi’ na kisha akaniuliza ‘unawezaje kunyamaza ikiwa watu wengi namna hii wanapotea?

4

Mpenzi msomaji, ujumbe huu ndio uliochochea kile ambacho nilijifunza mwaka 2004 kupitia Kitabu cha Isaya sura ya 58 ambayo inaanza kwa kusema ‘Piga kelele, USIACHE, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao’ (Isaya 58:1). Hivyo baada ya kurejea jijini Nairobi BWANA alinikutanisha na Ndg. Jersey (Mwandishi wa masuala ya kijamii nchini Kenya) ambaye baada ya kumweleza nia yangu ya kuandika, aliniongoza kufungua ‘blog’ hii na rasmi nikaanza kuweka masomo.

Julai 2009, BWANA alisema nami kwa habari ya uandishi huu na akaniambia ‘bado kuna vikapu vingi vya masomo vinakungoja’. Ikiwa unataka kujua zaidi kuhusu ushuhuda huu bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2012/01/21/waandishi-tusilale-bado-kuna-wajibu-mkubwa-mbele-yetu/

5 

Kuhusu masomo na wasomaji – Tangu nimeanza kuandika masomo nimefanikiwa kuandaa zaidi ya masomo mia mbili (200) ya kiroho ingawa niliyoyaweka kwenye ‘blog’ hii mpaka sasa ni wastani wa masomo mia moja na ishirini yakiwa kwenye makundi (categories) mbalimbali kama vile vijana, wanawake, wanandoa, Roho Mtakatifu, mafundisho kwa ujumla, nyaraka mbalimbali nk. Takwimu za mtandao za hadi kufikia Septemba 2016, zinaonyesha kwamba wasomaji wa ‘blog’ hii wanapatikana kutoka zaidi ya nchi themanini (80) duniani kote.

Maboresho kadhaa yanayokuja – Si wasomaji wengi wanafahamu kwamba nimekuwa nikiandaa masomo mbalimbali ya kiroho kwa lugha ya kiingereza pia. Hivyo baada ya tafakari ya muda mrefu nimewaza kwamba kuanzia sasa nitakuwa nikiyaweka kwenye ‘blog’ hii kupitia ‘category’ yake maalum ili kulifikia na kundi jingine. Tafadhali naomba radhi kwa wasomaji wasiojua kiingereza wasijisikie vibaya, ni jambo ambalo nimelisikia ndani yangu kufanya na zaidi sitaacha kuweka masomo kwa lugha ya Kiswahili pia.

2

Shukrani kwa Mungu wangu – hakika nina kila sababu ya kumshukuru Mungu ambaye yeye ndiye aliyeniita kwenye jukumu hili muhimu la kuanika masomo mbalimbali ya kiroho. Haijawa kazi rahisi kuandika masomo kila mwezi/mwaka na kuyaweka humu, lakini kwa sababu mwenye kulianzisha ni Mungu hakuniacha pekee yangu ndio maana leo tunasherekea kutimiza miaka kumi ya uandishi endelevu.

Shukrani kwa wasomaji na wachangiaji – katika shukrani naomba nikushukuru wewe mpenzi msomaji kwa kutenga muda wa kujifunza na kuongeza ufahamu wako wa masuala ya kiroho kupitia blog hii, naam ninapojua kwamba masomo ninayoandaa kuna watu wanayasoma na kuwasaidia kupiga hatua fulani kwenye maisha yao linaniimarisha na kunipa nguvu mpya ya kuandika na kuandika na kuandika.

Pia nawashukuru wale ambao licha ya kusoma na kupata maarifa, wamekuwa wakiandika mawazo (comment) mbalimbali kwa lengo la kunitia moyo, kuniongezea mambo ya kuboresha na kubwa zaidi wakichangia kujibu au kuwatia moyo wasomaji mbalimbali wanaokuwa wana maswali au mahitaji ya kiroho.

Shukrani kwa wamiliki wa ‘blog’ nyingine –naomba pia kutoa shukrani zangu kwa baadhi ya wamiliki wa blog za kikristo na kijamii pia ambao wameenda mbele zaidi na kutoa fursa za baadhi ya masomo ya blog hii kuwekwa (post) kwenye blog zao na hivyo kuongeza wigo wa wasomaji wa masomo haya, nawashukuru sana wapendwa wangu, Mungu awabariki.

Shukrani kwa famila yangu – namshukuru sana Mungu kunipa mke (Flora) ambaye amefanyika msaada mkubwa kwangu katika jukumu hili la uandishi pamoja na wanangu Barnaba & Bernada ambao wamekuwa wakivumilia kunikosa siku za mapumziko (weekend) kwa kuwa, mimi hutumia siku hizo kuaandaa masomo haya. Hakika binafsi natambua mchango wao kwenye huduma hii, Mungu wangu awalinde na kuwatunza.

3

Ahsante BWANA wangu, leo tarehe 16.09.2016 ‘blog’ hii imetimiza miaka kumi (10) tangu kuanzishwa kwake, utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu.

“… Utaiinua misingi ya vizazi vingi”