JIFUNZE KUENENDA KWA ROHO ILI USIMHUZUNISHE ROHO MTAKATIFU

Na: Patrick Sanga

9

Shalom, hakuna namna mwamini anaweza kuishi maisha ya kumpendeza Mungu hapa duniani bila kuenenda au kuongozwa na Roho Mtakatifu kwani yeye ndiye aliyepewa jukumu la kutufundisha na kutuonyesha njia itupasayo kuiendea. Hivyo basi suala la kujifunza kuenenda kwa Roho ni la LAZIMA kwa kila mwamini ili aishi maisha aliyokusudiwa awapo duaniani na kuepuka matokeo ya kumhuzunisha Roho Mtakatifu maana gharama yake ni kubwa sana.

Biblia kwenye Waefeso 4:30 inasema ‘Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi’ na tena imeandikwa Msimzimishe Roho’ (1Wathesalonike 5:19). Roho Mtakatifu ni Mungu, anayo nafsi ambapo ndani yake kuna hisia na kwa jinsi hiyo anaweza kufurahi au  kuhuzunishwa pia (1Wathesalonike 5:6). Matokeo ya kumhuzunisha Roho Mtakatifu ni mabaya sana kwa mwanadamu na Mungu pia, ingawa mwenye kuathirika zaidi ni mwanadamu na ndio maana tunaonywa tusimuhuzunishe.

 Kumhuzunisha Roho Mtakatifu ni kufanya au kusema jambo lolote lile ambalo litakatisha, kusimamisha au kuzuia kabisa utendaji au uongozi wake kwenye maisha yako. Naam kwa lugha nyingine kumuhuzunisha Roho Mtakatifu ni kumuwekea mpaka katika utendaji wake kwa kukataa uongozi, maonyo au ushauri wake  unaolenga kuwezesha utekelezwaji wa kusudi la Mungu kupitia mwanadamu.

b

 Je ni kwa namna gani mtu naweza kumhuzunisha Roho Mtakatifu?

Kwenye Isaya 63:9-10 imeandikwa Katika mateso yao yote yeye aliteswa, na malaika wa uso wake akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake, aliwakomboa mwenyewe; akawainua, AKAWACHUKUA siku zote za kale. Lakini WAKAASI, wakamhuzunisha Roho yake Mtakatifu; kwa hiyo akawageukia, akawa adui, akapigana nao’.

Matendo ya Mitume 7:51 inasema ‘Enyi wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote MNAMPINGA Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo’. Pia Zaburi 78:40-41 inasema Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani! Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; WAKAMPA MPAKA Mtakatifu wa Israeli’.

Maandiko haya yanatufanya tujue kwamba Roho Mtakatifu anaweza kuhuzunishwa kupitia UASI wa mwanadamu. Neno uasi lina maana ya kupinga maelekezo au kukataa kuwa chini ya mamlaka au utawala wa Mungu na kwa jinsi hiyo ni kupingana na mamlaka husika. Kadri mtu anavyomwasi Mungu kwa njia yoyote ile ndivyo anavyomhuzunisha Roho Mtakatifu, naam ndivyo anavyotengeneza mpaka na hivyo kukata mawasiliano kati yao.

4

Uasi wa mwanadamu ni kikwazo au kizuizi kwa Roho Mtakatifu kumsaidia na kumuongoza katika mapenzi kamili ya Mungu. Ndio ile kusema ‘ siku zote mnampinga Roho Mtakatifu’ (Matendo ya Mitume 7:51) ina maana kuna namna alitaka kuwasiaida, wao wakakataa usaidizi wake. Uasi unaweza kuwa kwenye neno la Mungu au maelekezo mahususi ambayo Roho Mtakatifu anampa mtu katika hatua mbalimbali za utendaji au utekelezaji wa kusudi la Mungu kwenye maisha yake.

Katika Zaburi 32:8 imeandikwa ‘Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama’. Kwenye Yohana 14: 26 imeandikwa ‘Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia’ na Yohana 16:13 imeandikwa ‘Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake’.

Hii ni kutonyesha kwamba Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu amekusudia kuyaongoza maisha ya mwanandamu katika kusudi lake na hivyo mwanadamu hanabudi kuishi kwa kufuata uongozi wake. Sasa uasi mbaya zaidi ambao mwanandamu huufanya ni ule wa kutenda au kwenda kinyume na mapenzi au maelekezo ya Mungu kwenye maisha yake na kuamua kuyafanya yale yampendezayo yeye asijue kwamba ipo tofauti kubwa ya kiathari kati ya uasi unaohusisha mfumo rasmi wa utaratibu (procedure) na ule usiohusisha mfumo rasmi utaratibu (non-procedure).

5

Hebu tuone mifano kadhaa ndani ya Biblia – Dhambi ya Haruni na Miriam vs dhambi ya Haruni kutengeneza sanamu ya ndama (Hesabu 12:1-14, Kutoka 32:1-35). Pia uasi wa Ibrahimu na Sara (Mwanzo 16:1-6, Wagalatia 4:22-31). Pia unaweza ukajifunza jambo hili kupitia uasi wa Musa na Haruni (Hesabu 20:12, 27:14), Uasi wa Daudi (2Samweli 11:1-27), Uasi wa Sauli (1Samweli 15:1-35) nk.

Je upi ni ufumbuzi utakaomsaidia mwanadamu asimuhuzunishe Roho Mtakatifu?Ndugu zangu, kiwa matokeo na athari za uasi ni kubwa kiasi hicho kwa mwanadamu, basi ni lazima mwanadamu ajifunze kuenenda kwa Roho ili asimhuzunishe Roho Mtakatifu. Katika Wagalatia 5:16-18 imendikwa ‘Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria’.

Kuenenda kwa Roho maana yake kuishi kwa kuongozwa na utaratibu wa Roho Mtakatifu. Biblia katika Yeremia 31:33 inasema Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu’. Warumi 8:1-2 imeandikwa ‘Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti’.

Zipo sheria kuu mbili zinazotaka kuongoza maisha na mwelekeo wa kila mtu dunaini. Moja ni sheria ya Roho wa uzima na ya pili ni sheria ya dhambi na mauti. Hizi ni sheria ambazo daima zinapingana na haziwezi kuja kupatana na hivyo ni uamuzi wa mwanadamu kuachagua sheria anayotaka iyaongoze maisha yake kwani mtu anapoishi kwa mojawapo ya sheria hizi sheria husika inamtenga mbali na sheria nyingine.

2

Kabla ya kifo cha Yesu msalabani, sheria ya dhambi na mauti inayofanya kazi kupitia mwili ilikuwa na nguvu dhidi ya torati (sheria). Torati ilikuwa ni dhaifu juu ya mwili na kwa hiyo maagizo (mahitaji) ya torati yasingeweza kutimizwa ndani ya mwanadamu. Hivyo Yesu alikuja ili aihukumu dhambi katika mwili wake, naam ili kwa njia hiyo wale waendao kwa Roho waweze kutimiza mahitaji ya sheria (Warumi 8:3-4).

Roho Mtakatifu anapokuwa ndani ya mtu kuna vitu (mafuta, hekima, nguvu, neema)  anaachilia ndani au juu ya mtu husika ili kumsaidia namna ya kuenenda awapo duniani. Nasikitika kusema kwamba ‘bila kujifunza na kuwa na nidhamu ya kuenenda kwa Roho, waamini wataendelea kuwa watu wenye kulalamika kila siku huku wakipoteza fursa nyingi za mafanikio sambamba na kushindwa kuishi maisha ya ushindi hapa duniani’ (Wagalatia 5:18, Luka 4:18, 1Yohana 2:27).

Kumbuka Roho Mtakatifu anao utaratibu (sheria) ambao sharti tuujue na kuufuata ndipo tutaweza kutembea naye au kueneneda kwa Roho. Mtu anapochagua kuenenda kwa Roho, Roho Mtakatifu kutokana na nafasi yake wa wajibu wake kwetu atamuongoza mtu husika katika shauri sahihi. Naam, hata hivyo ili mtu aenende kwa Roho ni lazima; kwanza atambue nafasi ya Roho Mtakatifu (Yohana 14:17), pili ampe kibali cha kuyaongoza maisha yake (1Petro 1:21) na mwisho ajue namna ya kuhusiana na kuwasiliana na Roho Mtakatifu.

1

Naam, nidhamu ya kujifunza na kudumu kuenenda kwa Roho itakusaidia usiseme au kufanya mambo unayotaka wewe wala kuyatafuta yakupendezayo, bali uishi sawasawa na mapenzi ya Mungu. Chagua leo kuenenda kwa Roho, nawe hutajutia maamuzi yako ya kuokoka bali ndivyo utakavyojua upendo na uweza wa Mungu katika kuwaongoza watoto wake kwenye shauri lake wawapo duniani.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA.

Advertisements

5 comments

  1. Mungu akubariki sana .

    On Sun, 15 Apr 2018 1:13 pm …UTAIINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI… (Isaya 58:12), wrote:

    > Sanga posted: “Na: Patrick Sanga Shalom, hakuna namna mwamini anaweza > kuishi maisha ya kumpendeza Mungu hapa duniani bila kuenenda au kuongozwa > na Roho Mtakatifu kwani yeye ndiye aliyepewa jukumu la kutufundisha na > kutuonyesha njia itupasayo kuiendea. Hivyo basi suala ” >

    Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s