NAFASI YAKO NI MUHIMU SANA KATIKA KUUJENGA MWILI WA KRISTO

Na: Patrick Sanga

Biblia katika 1 Wakorinto 12:11-14,18 imeandikwa ‘Lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, AKIMGAWIA kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni VINGI. Bali Mungu AMEVITIA viungo kila kimoja katika mwili kama ALIVYOTAKA’ (1Wakorintho 12:1-31, Warumi 12:4-8)

Kanisa ni mwili wa Kristo wenye viungo vingi, naam, kila kiungo kinao wajibu (unique) wa kufanya ili kuujenga mwili wa Kristo na kuusaidia kufikia malengo yake ipasavyo. Naam ili kutekeleza wajibu huo, kila kiungo kimepewa uwezo na kimewekewa namna (mipaka) yake ya utendaji kazi ambayo matokeo yake yanaathari kwa mwili mzima. Kumbuka mwenye kugawa wajibu kwa kila kiungo ikiwa ni karama, vipawa au huduma sambamba utendaji kazi wake ni Mungu.

Hii ina maana sisi kama viungo katika mwili wa Kristo, kila mmoja anamuhitaji mwenzake maana anacho kitu cha kuufaa mwili mzima. Wapo watu ambao katika ulimwengu wa  roho ni mikono, moyo, ubongo, mapafu, midomo, macho (wanaona tusivyoona), masikio, miguu, pua, maziwa, viungo vya uzazi, viungo vya kutoa uchafu nk. Jambo muhimu ni kwamba, kila mmoja lazima afanye wajibu wake huku akishirikiana, kutia moyo na kuombea viungo vingine kila kimoja kifanye kazi yake pia, ipasavyo.

Ndio maana katika 1Wakorinto 12:17,21-24 imeandikwa Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa? Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi. Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana. Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri HAVINA UHITAJI; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa’.

Watu (viungo) wanaoonekana kuwa wanyonge, wadhaifu, hawana heshima au wana upungufu, katika ulimwengu wa roho wamepewa uwezo mkubwa zaidi katika utendaji wa mwili wa Kristo. ikiwa sisi tunaona havina uzuri, tambua uzuri wao ni ule usioonekana kwa macho ya damu na nyama, bali macho ya kiroho pekee.

Rejea mstari wa 24 ‘viungo vizuri havina uhitaji’, kwa sababu havioni haja ya kumtafuta Mungu kwani vinaamini vinajitosheleza au vimekamilika. Fikra hii ndiyo inayovifanya viungo hivi kudharau au kutotambua umuhimu (nafasi) wa viungo vingine katika utendaji wa mwili wa Kristo. Naam, Mungu kwa kulijua hilo akaweka utaratibu wa kujifunua kupitia udhaifu au upungufu wa mtu. Naam hii ni kwa sababu uweza wa Mungu unatimilika katika madhaifu, umefichwa na unakaa juu ya vinavyoonekana kuwa vinyonge, vidhaifu    (2Wakorntho 12:7-10).

Kutokana na upungufu au unyonge wao wanapokea mafunuo zaidi na hii ni kwa sababu ya utaratibu wa Mungu kujidhirisha (kujifunua) kupitia mdahaifu au mapungufu ya mtu. Madhaifu, masumbufu, adha au shida walizonazo zinawafanya wawe karibu zaidi na Mungu. Na kwa kwa sababu Mungu haonekana kwao wamtafutao, anapowajibu si tu atasema kwa ajili yao pekee bali zaidi kwa ajili ya mwili wa Kristo.

Usidharau wengine kwa kuwa huwezi kujua nani anahusika moja kwa moja na maisha yako ya kila siku. Naam anaweza kuwa yule ambaye kwa jinsi ya kibinadamu haumpi heshima au umuhimu unaostahili, au unaona hana msaada kwako. Hawa ni watu ambao wanashughulika na maisha yako bila wewe kujua (viungo vya ndani, undercover agents). Naam wameitwa hivyo na wamepewa maelekezo ya aina hiyo na Mungu wao, jambo muhimu wewe waombee na si kuwasema vibaya.

Kumbuka kwamba kanisa lolote linaundwa na familia, hivyo sharti dhana hii ya kutambua nafasi ya mtu mwingine lianzie kwenye ngazi ya familia, ndoa zetu pia. Ukitambua nafasi ya mweza wako, walezi au watoto wako utawapa umuhimu waostahili kwani ndio viungo vya mwili wa Kristo. Kuna watu wanashindwa kumtumikia Mungu ipasavyo kwa sababu ya changamoto ya ndoa zao (Waefeso 5:22-27 vs 1Wakorintho 7:25-28)

Je unaitumiaje nafasi na uwepo wako katika kuujenga mwili wa Kristo? – Biblia katika Mtahayo 24:45-46 inasema Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo’.

Ukienda kwenye Luka 12:47-48 imeandikwa ‘Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi’ (Rejea Luka 12:42-48).

Mambo muhimu kuzingtia kama kiungo cha mwili wa Kristo:

  • Uwe mwaminifu kwenye eneo la wito wako kama kiungo katika mwili wa Kristo. Dumu kuwaombea na kuwatia moyo watu (viungo) wengine kwa sababu kadri wanavyofanya wajibu wao pia ipasavyo, ndivyo na mwili wa Kristo unavyoongezeka. Usiwe chanzo cha mwili kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo au kukwamisha viungo vingine vishindwe kufanya kazi kwa maneno au matendo yako. Ikiwa hujui wajibu wako ni nini, uliza kwa Mungu ili uwe na uhakika kitu gani umepewa kufanya katika mwili wake, kutokujua sio uetetezi, utahukumiwa kwa kutokujua kwako?
  • Fanya sehemu yako, usione wivu wala usijaribu kujilinganisha na mtu au watu wengine kwa sababu kila mmoja ameitwa na kupewa uwezo (vipawa) kama Mungu apendavyo. Naam tumeitwa tofauti wapo waliopewa vingi, wapo waliopewa kidogo, na kila mmoja atawajibika kwa nafasi yake.

  • Usiruhusu mapito, maneno ya watu au changamoto unazopitia zikuzuie kutekeleza wajibu wako kwa sababu mbele zake Bwana huo sio utetezi. Tena wala usiruhusu Shetani kupitia uongo (roho zidanganyazo) wake akuondoe kwenye kuyatenda mapenzi ya Mungu. Kumbuka vipo viungo vionekanavyo na visivyonekana.
  • Ongeza na kudumisha upendo wako kwa wengine, maana, upendo haupungui neno wakati wowote. Kumbuka imeandikwa ‘Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo’ (1Wakorinto 13:1-2,13)

Hitimisho: Tambua kwamba haupo ulipo kwa bahati mbaya, bali umewekwa hapo kama kiungo muhimu katika uendeshaji na utendaji wa mwili wa Kristo. Kila mmoja amepewa (entrusted) wajibu wa kufanya katika kuujenga mwili wa Kristo. Pale unapolala (kutowajibika) unaugharimu mwili wote kwa kutoa nafasi ambayo Shetani anaitumia kuleta athari kwa mwili mzima. Usisahau kwamba muda wa kutoa hesabu kwa Bwana aliyekupa wajibu huo unakuja (Mathayo 25:14-29).

Utukufu na Heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA

Advertisements

7 comments

  1. Mtumishi Bwana Yesu Asifiwe Huwa Nasoma Post Zako Mara Kadhaa Nashukuru Mungu Huwa Zinanisaidia Sana Asante Yesu Kuna Masomo Hata Nikiyasahau Huwa Nayaludia Napata Uelewa Zaidi , Ubalikiwe Ila Naomba No Yako Ya Simu Kuna Mambo Huwa Nataka Kukueleza Ila Si Hapa Yangu Ni 0769901199 , samahan kwa usumbufu

    Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s