UMUHIMU WA KUWA NA MUNGU MAISHANI (Sehemu ya mwisho)

Na: Patrick S. Sanga

Mada: Nini matarajio ya Mungu kwako au kwetu?

Katika sehemu ya kwanza naliandika sababu kuu mbili za umuhimu wa kuwa na Mungu maishani kwako. Ili kusoma sehemu hiyo tafadhali bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2017/10/28/umuhimu-wa-kuwa-na-mungu-maishani-mwako-sehemu-ya-1/ . Karibu sasa tuendelea na sehemu ya pili ambayo ni ya mwisho pia.

Ni ajabu kwamba wakati sisi tunafikiri umuhimu wa kuwa na Mungu katika maisha yetu, yeye anataka tujue nini matarajio yake kwetu ukizingatia kwamba yeye ndiye muumbaji wetu na mwokozi wetu. Hivyo swali muhimu kujiuliza na kupata majibu yake ni, nini matarajio ya Mungu kutoka kwangu (kwetu)? Naam yafuatayo ni matarajio muhimu ya Mungu kwako ambayo yanakamilisha dhana ya umuhimu wa kuwa na Mungu maishani:

  • Uwe na ufahamu wa lipi ni kusudi lake kwenye maisha yako – Tafuta kujua nini Mungu ameweka moyoni mwangu kufanya niwapo duniani (Why do I exist?), kwa nini nimeumbwa? Tafuta kutoka kwa Mungu majibu ya maswali husika ili uwe na uhakika wa sababu za uwepo wako na hivyo kuishi maisha uliyokusuidwa

Unalijuaje kusudi? – kwa njia ya kumuuliza Roho Mtakatifu (1Wakorintho 2:9-10, Matendo ya Mitume 13:1-3), kupitia viongozi wa kiroho au watu ambao umeunganishwa kwao kiroho, Wazazi/walezi (Waamuzi 14:1-9), Vipawa mbalimbali (Warumi 12:6-8). Naam ufahamu wa kwa nini upo utakusaidia kusimama imara kwenye kusudi husika bila kuyumbishwa.

  • Hakikisha unadumu kumpenda Mungu maishani mwako – Biblia katika Mathayo 22:37 inasema ‘Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote’ (Ona pia Kumbukumbu la Torati 6:5). Lazima ujizuie kuipenda na kuifuatisha namna ya dunia hii kwa sababu Shetani anajua kwamba akifanikiwa kumfanya mtu akaipenda dunia atakuwa ameondoa hali ya kumpenda na kumtumika Mungu moyoni mwake (Warumi 12:1, 1Yohana 2:14, 1Wakorintho 6:12).

  • Hakikisha unadumu kuutafuta ufalme wa Mungu – Biblia katika Mathayo 6:33 inasema Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa’.

 Ufalme wa Mungu ni nini?Ni utawala wa Mungu mwenyewe ambao msingi wake ni haki, amani na furaha. Katika Warumi 14:17 imeandikwa ‘Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu’ (Mathayo 13:44-46).

 Kwa nini tuutafute? – kwa sababu ndani ya ufalme wa Mungu: (a) kuna elimu ya ufalme husika (Mathayo 13:52) kuna mapenzi ya ufalme husika (Mathayo 6:10) na (c) kwa kuutafuta ndivyo tutakavyompendeza Mungu maana ufalme wa Mungu unakuja ili kuachilia (release) mapenzi ya Mungu yatendeke kwenye eneo lako na kuleta utukufu kwa jina la Yesu (Warumi 14:17-19).

Kwa nini usije wenyewe hadi tuutafute? – kwa sababu ya dhambi ya mwanadamu pale bustanini, dhambi iliondoa ufalme wa Mungu duniani na ikampa Shetani uhalali wa kuwa mungu wa dunia hii (Mathayo 4:8-9). Naam tangu wakati huo Mungu alijiwekea utaratibu wa kuonekana pale anapotafutwa isipokuwa pale tu anapoamua kujidhihirisha kwa kusudi maalum (Mithali 8:17).

Kadri mtu anavyoongeza jitihada ya kumtafuta Mungu ndivyo Mungu anavyoleta ufunuo wa kumsaidia mtu husika namna ya kuishi na kuzikabili changamoto mbalimbali katika kutekeleza kusudi lake hapa duniani.

  • Ufalme wa Mungu uko wapi? – Luka 17:20-21 Na alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani (midst) yenu’.
  • Ufalme wa Mungu unatafutwaje?Kwa njia ya; (a) toba yaani kubadili mwenendo yaani mawazo na matendo (Mathayo 4:17) (b) kuruhusu utawala wa Roho Mtakatifu (2Wakorinto 3:17) (c) kuhakikisha haki, amani na furaha vinatawala (Warumi 14:17-19) (d) kwa njia ya maombi (Mathayo 6:8-10).

Naam kuutafuta ufalme wa Mungu ni kuhakikisha jambo au wazo lililo la Mungu linakuwa na utawala kwenye eneo husika. Biblia katika Zaburi 34:14 inasema ‘Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie’. Amani hapa inawakilisha jambo au wazo lililo sahihi/ jema.

Mpenzi msomaji endapo Mungu akiona yupo mtu au watu ambao wanadumu kuhakikisha ufalme wake unatawala na mapenzi ya ufalme wake yanatimizlwa kwa nini ashindwe kushughulika na kula yao, vaa yao na malazi yao?. Naam fahamu kwamba namna ya kuishi ya mtu ipo ndani ya ufalme wa Mungu, kadri unavyojibiidisha kuutafuta ndivyo Mungu anavyojishughulisha na mahitaji yako ya kila siku.

Mungu amejiwekea utaratibu wa kuwapenda wanaompenda, Mithali 8:17a, Zaburi 91:14, Warumi 14:17-19 – Kwa kuwa yeye amtumikiaye Kristo katika mambo hayo HUMPENDEZA Mungu…  Kumpenda Mungu kunapimwa kwa utayari wa mtu kuyatenda mapenzi ya Mungu katikati ya mazingira yenye kumfanya amkosee au amchukie Mungu wake (Mathayo 6:24).

Hitimisho – Mpenzi msomaji ukweli ni kwamba Mungu anayo mambo mengi sana ya kutushirikisha au kutujulisha kuliko yale ambayo tunayo ili kumwomba au kumshirikisha yeye. Kwa lugha rahisi matarajio na mategemeo ya Mungu kwetu ni makubwa kuzidi yale ambayo sisi tunayo kwake na ndiyo maana hapa nimekuonyesha mambo muhimu kama matarajio yake kwetu.

Kumbuka kwamba unamuhitaji Mungu ili akuongoze kuishi sawasawa na kusudi lake maishani mwako. Naam ili kukuongoza katika kusudi lake sharti akuongoze katika njia yake. Hivyo basi kwa kila hatua unayotaka kupiga katika maisha yako mpe Mungu nafasi ya kwanza akusaidie maana huo ndiyo wajibu wake mkuu na ndio umuhimu wa kuwa na Mungu katika maisha yetu unaotutofautisha na wengine.

Utukufu na Heshima, Vina wewe Yesu, Watshaili BWANA.

Advertisements

4 comments

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s