IKIWA UNAJUA UMEITWA NA MUNGU KATIKA HUDUMA JIHADHARI USIUOE AU KUOLEWA NA MWENZA WA UFALME WA GIZA

Na: Patrick Sanga

Biblia katika Waefeso 4:11-12 inasema ‘Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe’.

Mitume, Manabii, Wainjilisti, Wachungaji na Waalimu ndizo ambazo zinafahamika kama huduma kuu tano. Hawa ndio ambao BWANA amewaita na kuwaweka shambani mwake ili kuwakamilisha watakatifu na kuujenga mwili wake. Lengo hili linatujulisha mawazo ya Mungu kuhusu kanisa na watoto wake duniani na hii ina maana yoyote aliyeitwa katika huduma hizo ni wa muhimu sana kwa ajili ya ufalme wa Mungu.

Zipo falme mbili tu zinazotawala kwenye ulimwengu wa roho na ndizo zinazongoza maisha kwenye ulimwengu wa mwili pia nazo ni, ufalme wa nuru (Mungu) na ufalme wa giza (Shetani). Ikiwa ufalme wa Mungu unakusudia kuwakamilisha watakatifu na kuujenga mwili wa Kristo kupitia watu waliobeba huduma husika uwe na uhakika kwenye ufalme wa giza watu walioitwa na Mungu kwenye huduma hizo wanawindwa waangushwe kwa nguvu isiyo ya kawaida ili kuzuia kusudi la Mungu.

Shetani hapigani vita ya kijinga, yeye ni mzoefu wa vita, na ana uzoefu wa kupigana vita kuanzia mbinguni. Naam licha ya kwamba alishindwa katika vita husika, alifanikiwa kushawishi sehemu kubwa ya malaika wakamwasi Mungu wao nao wakafukuzwa pamoja naye (Ufunuo wa Yohana 12:7-12). Sasa akijua kwamba ana mda mchache na kuna adhabu kali ya umilele inamsubiri, daima huwawinda na hupigana vita isiyo ya kawaida dhidi ya wote ambao wameitwa na kuwekwa na Mungu katika nafasi mbalimbali za huduma hapa duniani.

Moja ya mbinu kubwa anayotumia kuharibu huduma za wale walioitwa na Mungu ni kuhakikisha wanaoa au kuolewa kinyume na mapenzi ya Mungu. Shetani hufanya hilo kwa kuhakikisha anamuunganisha mbeba huduma na mtu wa ufalme wa giza. Kama kijana wa kiume ndiye ambaye ndani yake kuna huduma ya uinjilisti basi Shetani atafanya jitihada kumuunganisha kijana huyo na binti ambaye ndani yake kuna huduma ya uharibifu bila kijana huyo kujua.

Hata sasa wapo watu wengi ambao bado hawajaoa au kuolewa ambao ndani yao Mungu ameweka huduma zake na anataka kuwatumia kwa namna isiyo ya kawaida katika mapambano makubwa yanayoendelea kati ya falme hizi mbili. Nami kwa nafasi yangu nimepewa kuandika ujumbe huu kwa ajili yako ili kukutahadhirisha dhidi ya hila ya Shetani kupitia ndoa katika kuharibu huduma ambazo Mungu ameweka ndani ya watu wake.

Naam, yafuatayo ni mambo matano muhimu ambayo sharti uyajue na kuwa makini ili usije ukaoa au ukaolewa na mwenza ambaye atatumiwa na Shetani kuharibu kilicho cha Mungu ndani yako:

Jambo la kwanza – Ndoa imebeba kusudi la Mungu ndani yake

Jambo muhimu kujua ni kwamba unapooa au kuolewa si kwa ajili ya kujifurahisha wewe au kutimiliza uhitaji wako wa tendo la ndoa, bali zaidi yako mambo (makusudi) ambayo Mungu anataka kufanya duniani kupitia muunganiko wenu. Sasa kama wewe ndiwe umebeba huduma husika, unahitaji mwenza ambaye atakuwa ni wa msaada katika utumishi wako na si kuharibu kusudi la Mungu (Mwanzo 1:26-31, Warumi 8:28)

Jambo la pili – suala la mwenza wako ni kipaumbele cha Mungu

Maadam wewe ni mtumishi wake fahamu kwamba suala la nani atakuwa mwenza wako kwa Mungu ni kipaumbele muhimu na hivyo hayuko tayari kuona unaoa au kuolewa nje ya mapenzi yake. Naam hii ni kwa sababu ameweka utaratibu wa kusudi lake kutimizwa kupitia wanandoa pia. Hivyo usijaribu kuzitegemea akili zako pekee katika kutafuta mwenza wako, bali mpe Mungu nafasi akuongoze maana kutokana na huduma uliyobeba uwe na uhakika Shetani atataka kuhakikisha unaoa au kuolewa na mwenza asiye sahihi ili kukwamisha kilicho cha Mungu (Mithali 19:14, Isaya 55:8).

Jambo la tatu – Shetani anajua kile ambacho Mungu ameweka ndani yako

Jambo kubwa ambalo watu wengi hawajui ni kwamba Shetani anauwezo wa kuona maisha na matokeo ya mtu ya baadae tangu kuzaliwa kwake. Ndio ni ajabu kwamba Shetani anajua huduma uliyobeba na athari yake kwenye ufalme wake kuliko wewe mwenyewe unavyojua. Hivyo kwa kuzingatia ufahamu alionao wa kule unakokwenda Shetani hupambana kuhakikisha ndoto, maono na malengo uliyotakiwa kukamilisha vinakufa ndani yako (Mwanzo 3:1-5, Waamuzi 16:5).

Jambo la nne – Uwepo wa maajenti wa Shetani kanisani

Shetani ameingiza kwa siri makanisani wanaume na wanawake (maajenti) ambao bado hawajaoa au kuolewa. Maajenti hao wapo kwa ajili ya kuanzisha na kushawishi mahusiano yenye kupelekea ndoa kwa vijana au mabinti waliobeba huduma ndani yao. Maajenti hao ni watu wenye juhudi katika baadhi ya mambo ya Mungu na ibada pia. Kufuatia hila yao, vijana au mambinti wanapowaona huwatamani na kuvutwa kuanzisha mahusiano na kisha kufunga ndoa, wasijue huo ndio mlango wa uharibifu wa kusudi la Mungu aliloweka ndani yao (Waamuzi 16:4, 2Wakorintho 11:3,14-15).

Namna anavyoingiza fikra za uharibifu – katika kukutanisha au kukuletea fikra za mwenza wa ufalme wa giza, Shetani anaweza; (a) kukusemesha kwa sauti au kuleta ndoto ya huyo mtu kwamba unafunga naye ndoa, unatoa mahali, unamtambulisha nk (b) kumleta mtu mwenyewe akaja akakwambia BWANA amesema naye wewe ndiwe mwenza wa maisha yake sambamba na maneno mengi yenye kuonyesha muunganiko wenu utafaa kwa ajili ya kusudi la Bwana (c) kuwatumia viongozi wa kiroho, wazazi, marafiki ili kukushawishi uoe au uolewe na mwenza wa ufalme wa giza.

Jambo hatari ni kwamba katika kupandikiza fikra hizo Shetani hutumia hila. Shetani ni baba wa uongo, hivyo hutumia uongo kupitia ushawishi au ubembelezi ambao nyuma yake una nguvu za kipepo. Nguvu hizo zinaweza kuwa kwenye macho, mdomo, kifua, mavazi, zawadi au vitu mbalimbali nk ili kuhakikisha anakupata na hatimaye kufanikisha ndoa kati yako na mtu wa ufalme wake wa giza. Ndoa inayofungwa kanisani ni matokeo ya agano lililokwisha fanyika kwenye ulimwengu wa roho, nani amehusika kuunganisha ndoa hiyo kwenye ulimwengu wa roho linabaki kuwa swali la msingi lenye kuamua kufanikiwa au kufeli kwako katika utumishi wako (Asomaye na afahamu).

 Jambo la tano – Unahitaji kumuuliza Mungu kuhusu mwenza wa maisha yako

Haijalishi Shetani atatumia mbinu gani ili kuhakikisha nia yake ovu inafanikiwa, bali wewe, fanya mambo yafuatayo; (a) Hakikisha daima umezivaa silaha zote za nuru ili silaha zake giza zisikupate (b) Hakikisha kabla hujasema hujamkubalia mtu yoyote kwa habari ya kuwa mwenza wako unamuuliza Mungu kwanza ikiwa mtu huyo ni wa mapenzi yake kwako kwa ajili ya kusudi lile alilioweka ndani yako. Ukizingatia haya hakuna namna Shetani atafanikiwa katika kukuunganisha na mwenza wa ufalme wake.

Ushuhuda wa kwanza – Mwanamke mmoja aliyeolewa akiwa mtu mzima kidogo, kabla ya kuolewa alinishirikisha kwa habari ya mwenza wake na akaniambia Mungu amesema naye kwa habari ya mwanaume huyo na hivyo wanategemea kufunga ndoa yao hivi karibuni. Kiroho alikuwa ni mwanamke mwenye kumjua Mungu vizuri, hivyo hakuwa ananishirikisha ili nimshauri bali alikuwa ananipa taarifa juu ya uamuzi wake huo. Binafsi nilimwonya na kumweleza kwamba wewe ni mtumishi mkubwa wa Mungu kuliko mimi, lakini katika hili sioni kama uko sawa, najua una upweke wa kuishi peke yako, lakini katika hili sidhani kama ni mapenzi ya Mungu, omba vizuri.

Naye akasisitiza kwamba kuna mambo makubwa Mungu anaenda kufanya kupitia uwepo wao kama wanandoa, hivyo wakatambulishana kwa wazazi na viongozi wao, maisha yakaendelea na wakaanza huduma kwenye mji ambao walisema Bwana amewaita. Nasikitika kusema kwamba walitumika kwenye huduma na ndoa yao kwa miaka isiyozidi mitatu tu yule mama akafariki bila uzao kwa huyo mwanaume. Mbaya zaidi ni kwamba wakati yule mama anaenda kwa yule mwanaume alikuwa na watoto wadogo, baada ya kifo chake yule mwanaume aliwatelekeza wale watoto.

Fundisho muhimu ni kwamba – Yule mama alikuwa na huduma kubwa sana yenye kuujenga ufalme wa Mungu ipasavyo, lakini huduma yake ilifia kupitia ndoa yake kama huduma ya Samsoni ilivyofia mikononi mwa Delila. Hata kama huenda katika dakika zake za mwisho alitubu na kutengeneza na Mungu wake, ile kwamba alikufa ina maana na utumishi wake katika huduma aliyoitiwa ulikufa pia. Naam hicho ndio ufalme wa giza unataka, kuwaondoa watumishi katika nafasi zao kwa kila mbinu.

Ushuhuda wa pili – Mwanaume mmoja aliniuliza hivi Mwl. Sanga, wewe mwenzetu umepewa neema ya kuweza kuzijua siri nyingi za Mungu kupitia neno lake, je hakuna maandiko kwenye Biblia ambayo ukiyaunganisha yanampa mtu uhalali wa kuoa mke wa pili? Ukweli nilishangaa sana kusikia swali hili kutoka kwake, hivyo nami ilibidi nimuulize kwa nini wewe kwa nafasi yako unaniuliza swali la aina hii? akasema Mtumishi naomba unijibu tu maana hapa nilipoingiia hapakaliki.

Naam kwa neema ya Mungu nilikaa na yule baba tukazungumza juu ya changamoto yake na nini cha kufanya ili kuhakikisha kwamba kile alichokusudia Mungu kupitia maisha yake kinafanikiwa hata kama yuko na mwenza ambaye ni changamoto sana kwa huduma yake.

Fundisho muhimu ni kwamba – ili na wewe usifikie kuuliza au kutafuta endapo kuna njia mbadala (alternative) ya kupata mke wa pili au mume wa pili, unapaswa kwanza kumtafuta Mungu ili akuongoze kuingia mahali ambapo patakalika na kazi ya huduma uliyopewa na Mungu itendeke. Usisubiri hadi uingie kwenye shimo ndipo umtafute Mungu akusaidie, bali mtafute Mungu akuongoze kupitia kwenye njia ambayo anajua haina shimo la uharibifu.

Hitimisho – Hata leo tuna watumishi ambao huduma zao zimekufa, baadhi yao zimepoa, baadhi yao zimebadilishwa, baadhi yao zimezikwa na baadhi yao walishakufa kiroho na wengine kimwili kabisa, sababu ya msingi ikiwa ni kuoa au kuolewa na watu ambao walipandikizwa na ufalme wa giza bila wao kujua. Naam hatuna budi kujifunza kutokana na makosa yao, bali wewe, jihadhari usioe au kuolewa na mwenza wa ufalme wa giza ikiwa unajua umeitwa na Mungu katika huduma yoyote ile maana athari yake ni kubwa sana (Asomaye na afahamu).

Utukufu na Heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA.

Advertisements

8 comments

  1. Barikiwa sana kaka Sanga, hakika umenifungua kitu. Yanipasa nipige magoti na kumuomba Mungu vyema ili mapenzi yake yatimizwe kwangu. AMINA

    Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s