Archive for July 2017

KIJANA AU BINTI USIJIDANGANYE, KWENYE NDOA HUTAISHI NA UMBILE WALA FEDHA

July 24, 2017

Na: Patrick Sanga

Mwaka fulani kabla sijaoa Mwinjilisti mmoja aliniambia, Sanga, ukitaka kuoa tafuta binti mwenye sura na umbile zuri ambaye kila atakayekuona naye atasema kwa kweli mwenzetu Sanga kapata mke. Nikiwa mkoa mwingine kimasomo Mzee mmoja wa kanisa aliniambia jambo la aina hiyo pia. Naam si hawa tu waliojaribu kunijengea wazo la aina hii, wapo na wengine, ila nimeamua kutaja hawa wawili kutokana na nafasi zao kama viongozi.

Wakati huo nilikuwa mbioni kutafuta mwenza wa maisha pia, hivyo mawazo ya viongozi hawa yalianza kutembea moyoni mwangu na ukweli yalitaka kuniathiri. Hata hivyo nilichagua kurudi kwenye neno la Mungu ili kuona linasemaje. Katika kujifunza ndipo niliijua kweli na hiyo kweli iliniweka huru na kuniongoza kufanya maamuzi sahihi ambayo siyajutii hadi leo, bali nadumu kumtukuza Mungu.

Hata leo vijana wengi katika kutafuta mwenza wa maisha wanaongozwa na matakwa yao binafsi ambayo mengi ni kinyume na mapenzi ya Mungu kwenye maisha yao. Ukweli ni kwamba wanaume wengi huangalia muonekano wa nje wa mwanamke hususani sura, rangi na umbile lake, hii ni kwa sababu wanaume wengi wanaamini zaidi katika mvuto na muonekano wa nje wa mwenza.

Upande wa pili wadada wengi licha ya kujali pia suala la muonekano wa nje, wao huangalia zaidi uwezo wa mtu kifedha na baadhi yao kitaaluma pia. Hii ni kwa sababu wanawake wengi wanaamini katika kupata matunzo mazuri wawapo kwenye ndoa zao. Hivyo kupata mwenza ambaye ataweza kumtunza na kumjali kwa mambo mbalimbali ya maisha ikiwa ni pamoja na mavazi, makazi mazuri, usaifiri, nk ni moja ya kipaumbele kwake, naam sijasema wote bali wengi kwa kila upande.

Mitazamo ya makundi haya mawili hapo juu nimeithibitisha kufuatia majadiliano, maswali na semina za kiroho ninazofanya na wahusika. Kimsingi vipo vigezo vingine ambayo kila upande huzingatia lakini hivi nilivyotaja ndio vikubwa kwa wengi hata kama hawatasema moja kwa moja kwako, ila kwetu watumishi wanasema, naam vijana wa kiume husema Mtumishi ‘figure ina matter’ na wadada husema ‘uhakika wa matunzo mazuri una matter’.

 

 

Ukweli ni kwamba hii ni mitazamo ambayo imegharimu na inaendelea kugharimu wanandoa wengi sana. Walioko nje ya ndoa hawajui athari zake na walioko kwenye ndoa hawataki kusema maana wanahofia kupata aibu mbele ya jamii licha ya kupitia kwenye maumivu ambayo ni siri yao ingawa kila mmoja amempata yule ambaye alimtaka.

Ukisoma Biblia katika 1Samweli 16:1-13 utaona habari ya Nabii Samweli kwenda kwenye nyumba ya Yese ili kumtia mmoja wa watoto wake mafuta kuwa mfalme wa Israeli kufuatia uasi wa mfalme Sauli. Ndani ya habari hii kuna mafunzo muhimu yanayohusu namna ya kufanya maamuzi katika maisha. Hivyo  nimeona vema kuitumia katika kufafanua somo hili kwani inauhusiano mkubwa sana na uamuzi wa kutafuta mwenza wa maisha.

Biblia katika 1Samweli 16:6-7 inasema Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake. Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo’.

Tunaona kwamba Mungu hakuwa amemtajia Samweli jina la mtoto ambaye alipaswa kumtia mafuta ila alimwambia  ‘nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako’. Hivyo Samweli alipofika alimwagiza Yese kuwaleta watoto wake wote na kuanza kuwapitisha mbele zake, akisubiri maelekezo ya BWANA kuhusu aliyekusudiwa.

Mtoto wa kwanza wa Yese aliyeitwa Eliabu ndiye alianza, kijana huyu alipopita, Samweli akasema huenda huyu ndiye napaswa kumtia mafuta. Kufuatia wazo hilo, BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi NIMEMKATAA. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo’.

Habari hii inatufanya tuelewe kwamba wazo na uamuzi wa Samweli wa kutaka kumtia mafuta Eliabu ulitokana na mwonekano  wa nje wa kijana yule kwa maana ya urefu, uzuri wa sura na umbile lake. Jambo hili linatufundisha kwamba kumbe nyuma ya sura ya mtu, umbile lake au mwonekano wake wa nje kuna nguvu au sauti inayoweza kuongoza maamuzi ya mtu au watu wengine, na hivyo ni heri kuwa makini tusiingie kwenye metego huo.

Hivyo kutokea kwenye habari hii yafuatayo ni mambo muhimu kuyajua na kuyazingatia katika suala zima la kutafuta mwenza wa maisha:

 • Usitumie mwonekano wa nje wa mtu (sura yake, kimo au umbile lake) kama kigezo kikuu cha kumchagua au kumkubali awe mwenza wako. Naam uso wake sio moyo wake, kwa sura ya nje anaweza kuwa kondoo lakini kwa sura ya ndani (moyoni) ni mbwa mwitu. Naam ndioa maana imeandikwa Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa’ (Mithali 31:30).
 • Umbile la mwenza wako halitakufanya uache kitanda chako na kulala chini, chumba kingine au hata nje ya nyumba, bali tabia ya mwenza wako inaweza kukupelekea kufanya hayo. Naam umbile la mwenza halitakufanya ufikie mahali pa kujutia ndoa yako bali tabia yake inaweza kukupelekea kufanya hayo.
 • Jifunze kumuuliza Mungu, huyu niliyemwona ambaye ninakusudia aje kuwa mke au mume wangu, je nimeona sawasawa na mapenzi yako kwangu au la? Maana wewe umesema ‘Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo’, naam nakuomba unipe macho ya kiroho nione sawasawa.
 • Usitumie mazingira ya nje ya mtu (fedha, mali au elimu) kama kigezo kikuu cha kumchagua au kumkubali awe mwenza wako wa maisha. Naam anaweza kuwa na elimu nzuri, fedha ya kutosha na mali nyingi lakini moyoni mwake hakuna upendo au hofu ya Mungu. Mali na yote yanayofanana na hayo ni vitu mnavyoweza kuvitafuta na kuvipata kwa pamoja ikiwa ndoa yenu ina amani na upendo wa kweli. Kumbuka amani ya kweli haitokani na wingi wa mali alizonazo mtu bali mahusaiano mazuri kati yenu.
 • Kumbuka unahitaji mwenza kwa ajili ya tendo la ndoa pia, sasa anaweza kuwa na umbile zuri, mali au elimu nzuri lakini asikutosheleze katika tendo husika. Bali, unapompa Mungu nafasi akuongoze uwe na uhakika anaangalia nyanja zote na hivyo atakuunganisha na mtu sahihi ambaye mtatoshelezana. Naam, endapo hutampa Mungu nafasi, huenda hata hilo tendo la ndoa unaweza ukawa unalisikia au kulipata kwa kulazimisha ingawa umo kwenye ndoa, hii ni kwa sababu tendo la ndoa halitegemei umbile, elimu au mali, bali tabia, utayari na mahusiano mazuri baina yenu.
 • Usiingie kwenye ndoa kama vile maonyesho au kwa kusikiliza watu wanasema nini, kumbuka ndoa ni ya watu wawili, naam ni wewe ndiye utakayekutana na mateso au raha na si wao. Hivyo pale unapopewa ushauri kuhusu kuoa au kuolewa rudi kwenye Biblia uone neno la Mungu linasemaje juu ya wazo hilo na zaidi mwombe Mungu akuongezee utayari wa kutii mapenzi yake kwenye maisha yako.

Biblia inaeleza wazi kwamba wapo watu wazuri kwa sura na maumbile, hivyo siyo kosa kuwa na mwenza wa aina hiyo na ukifanikiwa kumpata aliyetulia hongera sana. Hata hivyo ni muhimu utambue sio wewe peke yako unayemuona ni mzuri, mpo wengi. Mbaya zaidi ni endapo mwenza wako atakuwa na tabia ya kujiona au kujisika kweli yeye ni mzuri hususani kufuatia sifa anazopewa na watu wa nje. Hivyo ni muhimu ujifunze namna ya kuomba na kuishi na mtu wa aina hiyo, vinginevyo ndoa yako haiwezi kuwa na utulivu.

Hakika ni rahisi kumpenda mtu Kwa kuangalia sura yake, umbile lake au uwezo wake, bali wewe, hakikisha kabla hujaamua kuishi naye unatafuta kujua ikiwa ni wa mapenzi ya Mungu kwako au la. Binafsi kabla sijaoa kuna dada nilimpenda na nilitamani sana aje kuwa mke wangu kwa sababu ya uzuri na upole wa sura yake. Kabla sijamuambia chochote, nilimuliza Mungu kwanza kuhusu dada huyo, BWANA akaniambia huyo si mtu wa mapenzi yangu kwako, wala hautafika naye mbali, mwache, maana najua mawazo ninayokuwazia, naam nikatii na kumwacha ingawa nilimpenda sana.

 Mpenzi msomaji, kwenye ndoa hutaishi na umbile wala sura ya mtu pekee, bali zaidi tabia ya mwenza wako, naam tabia ndiyo inayoamua aina ya maisha ya ndoa yako yatakavyokuwa.  Tabia ya mtu ndiyo inayopelekea wanandoa kulala vyumba tofauti ndani ya nyumba moja, au mmoja kulala chini na mwingine kitandani ndani ya chumba kimoja, tabia ndiyo inayopelekea wanandoa kupigana ilihali wameokoka nk.

Hii ni kwa sababu maisha ya mtu yamefichwa ndani ya moyo wake na si umbile lake wala sura yake wala mali zake. Kumbuka imeandikwa Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? (Yeremia 17:9). Naam huwezi kumjua mtu kwa kumwangalia kwa nje ndiyo maana unahitaji kumhusisha Mungu anayeona sura ya ndani (moyo wa mtu) akusaidie. 

Naam kwa kalamu ya mwandishi, nakuhimiza, mpe Mungu nafasi akusaidie na kukuongoza kupata mwenza sahihi wa maisha na si kuangalia umbile la mtu, uzuri wa sura yake, uwezo wake kifedha au kielimu kama vigezo vikuu vya kufanya maamuzi. Siandiki masomo haya kwa sababu naweza kuandika, bali naandika kwa sababu nimeagizwa kuandika ili kuwaepusha wengi na kile ambacho Mtume Paulo alikiita ‘shida iliyopo kwenye ndoa’ na zaidi ili kuwasaidia wengi kulitumikia ipsasvyo kusudi la Mungu kwenye maisha yao, kupitia ndoa zao (asomaye na fahamu).

Utukufu na Heshima vina wewe Yesu, Wastahili BWANA wangu.

NAMNA UNAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI YA MLINZI KWENYE ULIMWENGU WA ROHO KUFANYA MAOMBI YENYE MATOKEO MAZURI ZAIDI (Sehemu ya 1)

July 5, 2017

Na: Patrick Sanga

 

Mada: Tafsiri ya kuwa Mlinzi katika ulimwengu wa roho

Shalom, tunapoanza mwezi huu wa Julai 2017, nimeona ni vema kuanza pia mfululizo wa somo hili muhimu ambalo naamini si tu litabadilisha maisha yako bali litabadilisha na kuomba kwako. Lengo la somo hili ni (a) kuongeza ufahamu wako kuhusu nafasi ya Mlinzi kama Mwombaji (Mwombezi) na mwisho ni (b) Kuboresha mfumo wako wa kuomba uwe na matokeo mazuri zaidi.

Mambo mengi mabaya yanayotokea leo ni matokeo ya walinzi kutojua na kutofanya wajibu wao ipasavyo kwenye nafasi zao katika ulimwengu wa roho. Ukisoma Biblia utaona Mwanadamu amepewa nafasi ya kuwa ‘Mlinzi’ katika nyanja mbalimbali za maisha ili kufanikisha makusudi ya Mungu hapa duniani. Rejea ya Ufunuo wa Yohana 5:10 inatufanya tujue kwamba kila aliyeokoka ni Mlinzi, kinachotutofautisha ni nafasi au maeneo ya ulinzi ambayo tumepewa kuwajibika.

Suala la kuweka ‘walinzi’ katika maeneo mbalimbali ni utaratibu ambao Mungu ameuweka na unatoa uhalali na fursa ya pekee kwa pande zote kuwa karibu kimawasiliano. Naam, kufanikiwa kwa kusudi lake duniani kunategemea nidhamu na utiifu wa ‘walinzi’ wake kwenye nafasi alizowaweka.

Biblia katika Ezekieli 33:7 inasema ‘Basi, wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli, basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu’. Pia ukienda kwenye Isaya 62:6-7 imeandikwa ‘Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Eee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani’.

Maandiko haya yanatufanya tujue kwamba yako makusudi au mambo ambayo Mungu anahitaji kufanya juu ya nchi, miji, kanisa, ofisi, ndoa, mtu au watu nk. Naam ili kuyafanikisha anahitaji ‘Mlinzi au Walinzi’ atakaowatumia kufanikisha makusudi yake. Swali muhimu kujiuliza ni, Je, Mungu anaposema nimekuweka kuwa ‘MLINZI’ wa eneo fulani maana yake nini? Naam katika ulimwengu wa roho, unapowekwa kuwa Mlinzi wa eneo fulani maana yake ni;

 • Umewekwa kuwa Kiongozi wa eneo husika (Waebrania 13:17, Ufunuo 5:10)

Kuwa Mlinzi wa eneo fulani katika ulimwengu wa roho ni kuwa kiongozi wa eneo husika katika mambo au masula mbalimbali ya eneo lako la ulinzi. Huu ni wajibu wa kufanya maamuzi kwa niaba ya watu wa eneo lako sambamba na kuleta ufumbuzi wa changamoto zenye kuwakabaili.

Kumbuka mlinzi ndiye mwenye uwezo wa kuona jambo lolote linalotaka kuja kwenye eneo lake na ki-nafasi ana uwezo wa kuruhusu litokee au kuzuia lisitokee. Ikiwa ni jambo ambalo halina budi kutokea basi anayo fursa ya kuwaonya watu wake wajipange kukabiliana na jambo husika (Wimbo Ulio Bora 3:3, 2Samweli 12:14-19).

 • Umewekwa kuwa Mwonyaji wa eneo lako la ulinzi (Ezekieli 33:1-9)

Daima Shetani hupambana kuhakikisha watoto wa Mungu, wanaishi nje ya mapenzi ya Mungu kwenye maisha yako, yeye huja ili aibe na kuchinja na kuharibu. Hivyo ili watoto wa Mungu waweze kuepushwa na mabaya hayo, wanahitaji Mlinzi ambaye anajukumu la kuwaonya watu wa eneo lake kadri naye anavyopokea maonyo husika toka kwa Mungu. Naam, haya ni maonyo ambayo yana gharama kubwa kwa kila upande kama yatapuuzwa (Eze 3:26-27)

 • Umewekwa kuwa Mtoa taarifa wa eneo lako la ulinzi (Isa 21:6, 11 & Yer 6:17)

Siku zote taarifa inalenga kumpa mtu ufahamu wa nini kipo au kinakuja na hivyo kuwa fursa ya kujiandaa kukabiliana na jambo husika. Mwanadamu kama mlinzi una nafasi kubwa ya kutoa taarifa za msingi kwa watu wa eneo lako ili zifanyiwe kazi kwa wakati. Naam kadri Mungu anavyokupa taarifa za eneo lako nawe fanya hima kuzitoa kwa nyakati zilizoamriwa ili kufanikisha malengo.

 • Umewekwa kuwa Mshauri wa Mungu kwenye eneo lako la ulinzi

Mlinzi katika ulimwengu wa roho ni mshauri wa Mungu wa masuala ya kiroho kwenye eneo lake. Naam kwa nafasi hii Mlinzi anaweza kwenda mbele za Mungu na kuzungumza naye juu ya kile ambacho anataka kifanyike au kisifanyike kwenye eneo lake au kwa watu wa eneo lake (Kutoka 32:9-14)

Kutoka 39:10 inasema BWANA akamwambia Musa ‘Basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize… Je umeliona lile neno linalosema‘niache’. Kitendo cha Mungu kumwambia Musa ‘basi sasa niache’ kinatuonyesha kwamba,si tu Musa alikuwa kiongozi wa wana wa Israeli, bali, zaidi alikuwa ‘MLINZI wao’ na kwa sababu hiyo hakuna ambaye angeweza kufanya jambo juu yao bila ridhaa yake. Nafasi yako kama mlinzi ina thamani kubwa sana hivyo itumie ipasavyo kwa manufaa yako na watu wa eneo lako binafsi kama Musa alivyoitumia.

 • Umewekwa kuwa Mwombaji wa eneo lako la ulinzi (Isaya 62:6)

Kuomba ni wajibu mkubwa zaidi ambao Mlinzi amepewa kwenye eneo lake la ulinzi, wajibu huu ndio unaowezesha majukumu yake mengine kufanyika ipasavyo. Mlinzi wa eneo anapswa kujua sababu na makusudi ya yeye kuwa mlinzi kwenye eneo husika ndipo atakuwa kwenye nafasi ya kudumu kuomba, ili kuhakikisha yale ambayo Mungu anayo moyoni mwake, kuhusu eneo lake la ulinzi yanatimia. Huu ni wajibu unaokutaka kuomba na kufikiri kama Mlinzi wa eneo husika tena bila kukata tamaa (Luka 18:1).

Ndugu zangu, nafasi ya ulinzi katika ulimwengu wa roho, ni nafasi ya pekee sana ambayo Mungu ametupa watoto wake. Haya matano ndio majukumu ambayo Mlinzi anapaswa kuyafanya kutokana na nafasi yake. Hata hivyo kwa kuwa somo hili linahusu maombi, kuanzia sehemu ya pili ya ujumbe huu nitaaingia ndani kufundisha kuhusu nafasi ya mlinzi kama  mwombaji wa eneo lake la ulinzi. Naam binafsi nimejifunza kwamba kufanikiwa kwa kusudi la Mungu hapa duniani si tu kunategemea utiifu wa watu wake ,bali zaidi, kunategemea namna Walinzi aliowaweka wanavyozitumia nafasi zao katika ulimwengu wa roho na hivyo kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwenye ulimwengu wa mwili. Fuatilia mfululizo wa somo hili, utaelewa siri iliyoko ndani ya ujumbe huu muhimu kwa nyakati tulizonazo.

Tutaendelea na sehemu ya pili …

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, Wastahili BWANA.