JE, UNAJUA HIYO NDOA UNAYOTAKA KUINGIA INAKUPELEKA WAPI?

Na: Patrick Sanga

Mtumishi, ninachohitaji sasa ni mume tu, umri unazidi kwenda na nimeomba ila sioni nikijibiwa, waliojitokeza kutaka kunioa hawamaanishi na sasa nimechoka kusubiri. Hivyo kuanzia sasa mwanaume yoyote atakayekuja haijalishi ameokoka au hajaokoka na hata akiwa mpagani nitakubali kuolewa naye ili na mimi niwe na mume. Hivi ndivyo dada Agnes (siyo jina lake halisi) alivyonieleza baada ya kunipigia simu.

Kimsingi kila ninapotafakari changamoto zilizoko kwenye ndoa, hususani ndoa ambazo zilifungwa bila wahusika kumpa Mungu nafasi awaongoze kupata wenza sahihi, huwa napata mzigo wa kuwaombea vijana (kiume/kike), Mungu awape uvumilivu na kuwaongoza ili wasiingie kwenye ndoa kinyume na mapenzi yake juu yao.

Najua hata sasa wapo vijana wengi wanaopitia changamoto inayofanana na ile ya Agnes. Vijana ambao wamekuwa wakiwaza kukubali kuoa au kuolewa na mtu yoyote atakayekuja bila kujali kwamba mwenza husika ni wa mapenzi ya Mungu au la, na zaidi bila kujua ndoa wanayotaka kuingia itawapeleka wapi.

Hoja ya dada Agnes ilinifanya nitafakari kwa upana sana juu ya pito lake, kisha nikamshauri mambo kadhaa ya kufikiri kabla ya kuchukua uamuzi wake alioukusudia. Ujumbe huu unakuja ili kusaidia kubadilisha mtazamo wako na kukuongoza katika njia ya Bwana unapokutana na changamoto ya aina hii, tafadhali jifunze na kuzingatia mambo yafuatayo;

Huhitaji kuoa yoyote au kuolewa na yoyote – ukisoma Biblia yako vizuri utagundua kwamba mbele za Mungu wewe ni mtu wa thamani na upo duniani kwa kusudi maalum ufalme wake. Hii ina maanisha hauhitaji kupata mwenza yoyote, bali unahitaji kupata mwenza sahihi kwako kati ya wengi waliopo, naam, mwenza ambaye ni wa mapenzi ya Mungu kwako (Zaburi 8:4-6, Yeremia 29:11)

Kinadharia mtu yoyote anaweza kuwa mwenza wako, lakini kinafasi na utumishi wa kusudi la Mungu uliloitiwa, si kila mtu anafaa kuwa mume wako au mke wako, yuko mmoja aliyewazidi wote, ndiye aliyekusudiwa kwa ajili ya nafasi hiyo. Naam kwa Mungu, suala la nani atakuwa mwenza wako wa maisha ni kipaumbele, yeye hutaka kuona unampa nafasi akuongoze kumpata mwenza ambaye kwa huyo mtalitumikia vema kusudi lake (Warumi 8:27, Mithali 19:14, Zaburi 32:8).

Ndoa ni wito unaoleta wajibu na changamoto – kuingia kwenye ndoa ni kuingia kwenye majukumu ambayo yanahitaji uwe na mwenza sahihi mtakayesaidiana naye katika kuyakabili na kuyatatua. Ndoa inafungua milango ya majukumu na changamoto mbalimbali ambazo zinaongeza zile ulizokuwa nazo kabla ya kuoa au kuolewa (Mwanzo 2:20).

Baadhi ya majukumu na changamoto utakazokutana nazo ni za kifamilia, kiuchumi, kimakazi, kihuduma, kikazi, kijamii, kimahusiano na watu wengine nk, naam changamoto ambazo kama huna mwenza sahihi mwenye uwezo wa  kukuvumilia na kuchukuliana nawe katika mapungufu yako, changamoto hizo zitawafikisheni pabaya.

Shetani hupambana kuhakikisha watu wanaoana kinyume na mapenzi ya Mungu – Ndoa inayofungwa katika mapenzi ya Mungu ni pigo kwenye ufalme wa giza maana kupitia ndoa za aina hiyo makusudi ya Mungu hutimilizwa endapo wanandoa hao watasimama kwenye njia ya Bwana. Shetani kwa kujua hilo hupambana kuhakikisha watu wanaoana kinyume na mapenzi ya Mungu kwenye maisha yao.

Sasa jiulize unapofika mahali ukasema yoyote atakayekuja nitamkubali, unajuaje kwamba huyo atakayekuja ni wazo la ufalme wa giza au la? Kumbuka haji kama mbwa mbwitu bali atakuja akiwa amevaa vazi la kondoo. Naam usitafute mwenza wa maisha kwa akili zako au usiwaze kutaka kuoa au kuolewa na yeyote atakayekuja maana itakugharimu sana.

Ndoa hiyo itakupeleka wapi – Kumbuka ndoa ni wito unaokutaka kuwaacha baba na mama yako na kisha kuanzisha maisha mapya (Mwanzo 2:24). Sasa jiulize hiyo ndoa unayotaka kuingia itakupeleka wapi? Je ni maisha ya furaha au majuto? Usisahau kwamba ni mke au mume mmoja tu na hakuna fursa ya kuoa au kuolewa tena hadi kifo kiwatenganishe (Soma biblia vizuri huku ukimuuliza Roho Mtakatifu pale usipoelewa, usidanganywe na wale wanaotafsiri maandiko kwa matakwa yao binafsi).

Tafadhali jiulize, kwenye hiyo ndoa unayotaka kuingia utaishi kwa amani au la? Je unajua mtaishi na huyo mtu kwa muda gani? Je unajua kwamba ndoa inaweza kukuondoa kabisa kwa Mungu hata kukufanya uache huduma/wokovu wako na kuishia pabaya? Je unajua kwamba ndoa ni wito wa mapungufu? Je utaweza kuyabeba mapungufu ya mtu ambaye unataka kufunga naye ndoa bila kujua ni wa mapenzi ya Mungu au la? Wewe unayafahamu mapungufu yako binafsi, je unafikiri huyo mwenza wako ataweza kuchukuliana na mapungufu yako kama si wa mapenzi ya Mungu kwako?

Ni maombi yangu, ujumbe huu ukufikirishe kutafuta uongozi wa Mungu kuhusu mwenza sahihi kwako na si kuamua unavyotaka. Suala sio kuitwa mke au mume wa fulani, ni heri kuchelewa kuoa au kuolewa, kuliko kuingia kwenye ndoa ambayo itakuwa ni tanzi na maumivu kwako. Kumbuka wewe ni thamani, usikubali kuoa yeyote au kuolewa na mwanaume yoyote bali yule wa mapenzi ya Mungu kwako (Asomaye na afahahamu).

 ‘Utukufu na Heshima vina wewe Yesu, Wastahili BWANA’

Advertisements

7 comments

 1. Tumsifu Yesu Kristo Mtumishi, Barikiwa sana kwa mafundisho yako. Roho Mtakatifu aendelee kukuongoza sawasawa na mapenzi yake. Zab 32:8

  Like

 2. Naomb unitumie somo hili nilidownloard katika mfumo wa PDF On Jun 16, 2017 2:34 PM, “…UTAIINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI… (Isaya 58:12)” wrote:

  > sanga posted: “Na: Patrick Sanga Mtumishi, ninachohitaji sasa ni mume tu, > umri unazidi kwenda na nimeomba ila sioni nikijibiwa, waliojitokeza kutaka > kunioa hawamaanishi na sasa nimechoka kusubiri. Hivyo kuanzia sasa mwanaume > yoyote atakayekuja haijalishi ameokoka au ” >

  Like

  • Shalom, mazingira hayaniruhusu kufanya hivyo kwa sasa, ila naweza kukutumia kupitia kwenye email yako kwa mfumo wa word, hivyo ikiwa uatataka kwa format hiyo nitume email yako.

   Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s