NAMNA YA KUSIKIA NA KUIELEWA SAUTI YA MUNGU ILI IKUSAIDE KATIKA KUFANYA MAAMUZI (Sehemu ya tano)

Na: Patrick Sanga

Mada – Njia anazotumia Mungu kusema na mwanadamu (Sehemu ya tatu)

Katika sehemu ya nne ya somo hili na pia sehemu ya pili kwa mada hii tuliangalia njia ya nne ambayo ni sauti ya wazi wazi ya Mungu, ili kusoma sehemu hiyo bonyeza hapa https://sanga.wordpress.com/2016/09/12/namna-ya-kusikia-na-kuielewa-sauti-ya-mungu-ili-ikusaide-katika-kufanya-maamuzi-sehemu-ya-nne/. Katika sehemu hii ya tano kwa somo hili na sehemu ya tatu kwa mada husika tutaangalia njia kadhaa zilizosalia. Tafadhali fuatana nami tuendelee;

Njia ya tano, amani ya Kristo – Biblia katika kitabu cha Wakolosai 3:15 inasema Na amani ya Kristo IAMUE MIOYONI mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja tena iweni watu wa shukrani’. Kwenye toleo la kiingereza la GNB mstari huu unasema The peace that Christ gives is to GUIDE YOU IN THE DECISIONS YOU MAKE; for it is to this peace that God has called you together in the one body. And be thankful’.

Mistari hii inatufanya tujue kwamba, mosi, Mungu hutumia amani ya Kristo ndani ya mtu, kama njia mojawapo ya kusema na mwanadamu, na pili, ndani ya amani ya Kristo kuna sauti ya kumwongoza mtu kufanya uamuzi sahihi. Hivyo ni muhimu kwa mwanadamu kuwa na ufahamu kuhusu namna amani ya Kristo inavyofanya kazi na kuitafuta imuongoze kufanya maamuzi. Moja ya mambo muhimu kujua ili kuona matokeo mazuri ya amani ya Kristo kama mwamuzi, ni wewe kujifunza kuomba kimaswali hususani kwenye mambo ambayo yanakuweka njia panda kimaamuzi.

Kadri unavyoendelea kuomba kwa kuuliza kwa Mungu juu ya uamuzi gani uchukue, katika wazo ambalo ndani yake utasikia kupata amani au mpenyo, utasikia uhuru au furaha au raha hiyo ni ishara kwamba jambo hilo ndio sahihi kulifanyia kazi au kulifuatilia zaidi ili uongeze ufahamu juu yake kabla ya kulitekeleza. Kumbuka amani ya Kristo ambayo tumepewa inazipita akili zote (Wafilipi 4:7), hivyo itakuongoza kwenye uamuzi sahihi zaidi hata kama akili yako mwenyewe au za watu wanaokuzunguka kwa jinsi ya kibinadamu hawakubaliani na jambo hilo.

Njia ya sita, Kupitia maono – Ukisoma katika Hesabu 12:6 inasema ‘Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika MAONO, Nitasema naye katika ndoto’. Hata hivyo ukienda kwenye kitabu cha Ayubu 33:14 imeandikwa ‘Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, KATIKA MAONO YA USIKU, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani’.

Maono ni njia ya mafumbo, picha au taswira ambayo hufunua asili, undani au ukweli wa kile kinachofunuliwa au kinachoonekana. Maono yanapomhusu Mungu yanalenga kumfanya muonaji apondeke, aongezeke kiimani na kumjua Mungu zaidi. Maono yanapomhusu mtu, watu au jambo fulani, yanalenga kutufanya tuelewe asili, undani na ukweli kuhusu watu hao au jambo hilo na hivyo kutusaidia kujua mipaka ya kushirikiana, kuhusiana na kusaidina nao.

Mara nyingi ndoto humpata aliyelala usingizi wakati maono hutokea kwa mtu aliye macho kabisa na inaweza kuwa mahali popote pale. Jambo ambalo nimejifunza na kuthibitisha ni kwamba, mara nyingi maono hutokea kwa jinsi ya rohoni, yaani mtu kuchukuliwa katika roho au kuingizwa katika ulimwengu wa roho na kuanza kuona kilichokusudiwa. Kumbuka maono si ya mchana pekee kama wengi wanavyoelewa bali hata usiku pia watu hupata maono. (Mwanzo 15:1, Isaya 6:1-6, Ezekieli 1:1-3, Ufunuo wa Yohana 1:9-10, Yoel 2:28, Habakuki 2:1-5).

Njia ya saba, Kupitia kunena kwa lugha kunakoambatana na tafsiri – Biblia katika 1Wakorinto 14:27-28 inasema ‘Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri. Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu’ (Rejea pia 1Wakorinto 12:4 & 10). Ndiyo, hususani katika mazingira ya ibada au kusanyiko la kiroho, Mungu husema na watu kupitia kunena kwa lugha ambapo kati yao wanenao kuna ambaye amepewa karama ya kufasiri kinachonenwa au yeye mwenyewe anenaye ana uwezo wa kufasiri pia.

Hata hivyo nitoe ushauri kwa viongozi wa kiroho na wasimamizi wa ibada, waongeze ufahamu wao kuhusu njia hii, maana wengi wamekuwa wakiwapiga vita na kuwazuia watu wanaotaka kunena katikati ya ibada bila kujua ikiwa kunena huko ni kwa mapenzi ya Mungu au la, jambo ambalo limepelekea kuzima sauti ya Mungu kwenye huduma zao na kuzuia ujumbe uliokuwa umekusudiwa.

Njia ya nane, kupitia malaika – Katika Biblia tunaona matukio mengi ambayo Mungu aliwatumia malaika kusema na wanadamu juu ya mapenzi yake na hivyo kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yao. Malaika ni viumbe wa Mungu na jeshi linalomsaidia Mungu kufanya kazi mbalimbali. Tunaona Mungu alivyosema na kina Musa, Ibrahimu, Yakobo, Bikira Mariam, Paulo na wengine wengi kupitia malaika.

Sauti ya Mungu kupitia malaika ni njia au ufunuo wa kiwango cha juu sana ambao Mungu anaweza kusema na wanadamu ukilinganisha na njia zingine. Ufunuo huu wa malaika unaweza kuwa kwa malaika kukutokea kupitia ndoto au malaika kutokea waziwazi kwa maumbo yao au kupitia umbile la kitu kingine kama alivyomtokea Musa katikati ya mwali wa moto uliotoka kwenye kijiti kinachowaka.

Hata hivyo kupitia wenzetu ambao malaika walisema nao tunajifunza kwamba uaminifu, kumcha Mungu na kumaanisha (commitment) kumpenda Mungu katika wito wao ni sehemu ya vigezo vilivyopelekea Mungu kusema nao kwa njia hii. Malaika waliwatokea pia watu mbalimbali pale ambapo Mungu alikuwa na kusudi maalum la kufanya kupitia wao hata kama baadhi yao hawakuwa na sifa tajwa hapo juu (Mwanzo 22:10-12, 31:11-12, Danieli 10:11, Waamuzi 2:1, 13:2, Luka 1:13,35 Mathayo 1:20, Hesabu 22:24-34, Matendo ya Mitume 27:23 -24).

Njia ya tisa, Kupitia mazingira (asili/uumbaji) – Biblia katika kitabu cha Zaburi 19:1 inasema “Mbingu zahubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake’. Pia katika Yeremia 18:2 imenadikwaOndoka, ukashuke mpaka nyumba ya mfinyanzi, na huko nitakusikizisha maneno yangu’.

Ukiunganisha mawazo ya mistari hii unajifunza kwamba Mungu anaweza kutumia uumbaji wake au mazingira ili kusema na mwanadamu kama ilivyokuwa kwa Yeremia kupitia udongo na Balaamu kupitia mnyamna Punda ili kumpinga katika nia yake ovu dhidi ya Israeli.

Unapotafakari jinsi Mungu alivyomuumba mwanadamu na viumbe wengine jinsi ya ajabu, unapoona uumbaji wa milima, bahari, miti nk uumbaji huo unaleta ujumbe wenye kukufanya ujue hakuna jambo la kumshinda BWANA. Jambo muhimu ni kwamba ndani ya uumbaji huu kuna sauti ya Mungu inayoweza kusema nawe            (Zaburi 19:2, Warumi 1:20, Hesabu 22:24-34, Yeremia 18:1-6,).

Njia ya kumi, Kupitia majaribu yako au ya wengine – katika Zaburi 119:67 Biblia inasema ‘Kabla sijateswa mimi nalipotea, Lakini sasa nimelitii neno lako’. Hii ina maana majaribu au changaoto aliyoyapitia yalikuwa sauti ya Mungu ya kumrejesha kwenye njia na utiifu. Ndiyo maana Mtume Paulo anatuambia Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi’ (2Wakorinto 12:7).

Naam mwiba ule ulikuwa sauti au ujumbe kwa Paulo katika huduma yake, kwamba pamoja na wingi wa mafunuo, vipawa na karama alizonazo bado kuna mambo yalikuwa yakimuumiza na hakuweza kuyashinda kwa sababu Mungu ndio aliridhia yawe sehemu ya maisha yake, ili kumsaidia asijivune kupita kiasi. Hata hivyo Paulo alilipokea jambo hilo kwa ukomavu mkubwa na likawa chanzo cha kuongeza usikivu na jitihada yake katika kumtafuta Mungu.

Ndio maana hata leo kupitia changamoto mbalimbali ambazo mtu binafsi au ndugu/marafiki zake wanazipitia utawasikia wakisema Mungu amenifundisha mambo mengi kupitia ugonjwa huu, misiba, adha, au mateso haya nk. Jambo hili lina maana ndani ya kila jaribu kuna sauti au fundisho, ni muhimu kujifunza siri hizi ili kuelewa shule ya Mungu kwenye maisha yako.

Mpenzi msomaji katika sehemu hii, ndio nimehitimisha njia hizi kumi ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu. Hii haina maana ziko njia kumi mahsusi, bali njia hizi zinaweza kuongezeka au kupungua kutegemeana na lengo, ufahamu, uzoefu na ufunuo wa Mwandishi.

Somo litaendelea…

Neema ya Kristo iwe nanyi

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, Wastahili BWANA wangu.

Advertisements

5 comments

      • Naam endelea kujifunza huku unamwomba Mungu. Kumbuka neno la Mungu ndio sauti yake ya wazi kwa mwanadamu, hivyo jizoeze kulisoma na kutafakari, kadri utakavyokuwa mwaminifu ndipo utaona uelewa wako hata wa njia nyingine unaongezeka. Ni hatari kwa mtu kupata mafunuo ya njia nyingine kama hana ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu.

        Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s