Archive for March 2017

NAMNA YA KUSIKIA NA KUIELEWA SAUTI YA MUNGU ILI IKUSAIDE KATIKA KUFANYA MAAMUZI (Sehemu ya mwisho)

March 28, 2017

Na: Patrick Sanga

Mada – mambo ya kukusaidia kuelewa sauti ya Mungu ili kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yako

Katika sehemu ya tano ya somo hili tuliangalia njia sita ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu, ili kusoma sehemu hiyo bonyeza hapa https://sanga.wordpress.com/2017/03/16/877/ Katika sehemu hii ya sita na ya mwisho kwa somo hili nitafundisha mambo ya kukusaidia kuelewa sauti ya Mungu na hivyo kuweza kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yako.

Jambo muhimu si tu kusikia sauti ya Mungu, bali zaidi kuelewa kile anachosema . Uelewa wa sauti ya Mungu (ujumbe uliokusudiwa) imekuwa ni changamoto kwa watu wengi. Nimewasikia watu wakisema nimemwomba Mungu kwa muda mrefu lakini hajawahi kujibu au kusema nami. Naam, huwezi kumwomba Mungu aliye hai asikujibu, daima yeye huwajibu na kusema na watoto wake. Changamoto iliyopo kwa watu wengi ni kushindwa kuelewa pale Mungu anaposema nao, kiasi cha kuamini bado hawajajibiwa.

Siku za mwanzo nilipokuwa najifunza jambo hili, kufuatia wingi wa mafunuo yaliyonijia kupitia neno, maono, mazingira, ndoto, sauti nk, nilipata tabu sana, mosi kutofautisha ikiwa mafunuo hayo yalikuwa kutoka kwa Mungu au la? na pili ikiwa yalikuwa kwa ajili yangu binafsi au watu wengine nk?. Kutokana na kukosa ufahamu wa kutosha, mara nyingi nilikuwa mtu wa kutubu, kukemea au kuomba maombi mengi ambayo sehemu kubwa yake hayakuwa sahihi kwani yalihusu mimi na familia yangu tu.

Niliendelea hivyo kwa muda mrefu sana bila kujua kwamba nilikuwa nakosea, hadi pale Bwana, aliponifundisha kwamba, pamoja na kuendelea kusema kwa ajili yangu binafsi, kwa kuzingatia nafasi yangu na kusudi lake kupitia maisha yangu, mara nyingi atasema nami ajili ya watu wake ili niwaombee, kuwaonya na kuwafundisha. Bwana akaendelea kunifundiha kwamba, hata hivyo nionapo jambo lolote napaswa kutafuta kwanza maelekezo sahihi kutoka kwake’.

Naam, katika sehemu hii ya mwisho nitaandika mambo matano ya kukusaidia kuelewa sauti ya Mungu na kukuwezesha kufanya maamuzi sahihi;

Moja, jifunze kufuatilia ili kuelewa kile Mungu anasema nawe – Ukisoma Ayubu 33:14 imeandikwa ‘Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu HAJALI’. Ukienda kwenye Isaya 42:20 imeandikwa Unaona mambo mengi, lakini HUYATII MOYONI; masikio yake ya wazi, lakini hasikii’. Mistari hii inatufanya tujue kwamba, Mungu anaposema, lengo lake ni kutaka watu wake wathamini, waelewe na kuufanyia kazi ujumbe aliowapa, na si kupuuza.

 

Watu wengi Mungu anaposema nao, mosi hawana nidhamu ya kufuatilia ili kuelewa kile walichoona au kusikia na baadhi yao hata ujumbe huo ukijirudia bado hawajali hadi pale madhara yawapatapo ndipo hujuta na kukumbuka yale Mungu aliwaonya. Hivyo ni jukumu lako kuhakikisha unafuatilia hadi uelewe kile Mungu alichosema nawe maana yeye ndiye anayejua kinachokuja mbele yako na mwenye kuona usiyoyaona wewe. Naam jifunze kutopuuza ujumbe wowote ambao Mungu anauleta kwenye maisha yako kupitia njia mbalimbali.

Mbili, sauti ya Mungu inaendana na nyakati alizoziamuru juu yako – ukisoma katika Mhubiri 3:1 Biblia inasema ‘Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu’. Ile kusema kwa kila jambo kuna majira yake ina maana kwa kila majira kuna maelekezo yake pia. Naam kila majira yanakuja na maelekezo yake mahususi ya kufanyiwa kazi, jambo linalomaanisha ndani ya kila nyakati kuna sauti ya Mungu yenye kutoa maelekezo mahususi.

 

Ni vizuri ukaelewa kwamba Mungu anaposema amekujibu si kukupatia kile ambacho wewe ulikuwa unategemea kukipata kwa jinsi ya kibinadamu. Uwepo (uhalisia) wa kile ulichoomba ni hatua ya mwisho ya jibu lako, na kabla ya hapo, nyakati zinakutaka (demand) ufanye mambo fulani ambayo yameunganishwa na nyakati hizo ndipo uweze kupata ulichoomba. Uhalisia wa kile ulichoomba ni matokeo ya mchakato (process) wa ushirikiano kati yako na nyakati zilizoamriwa juu yako ambazo ndizo zilizobeba mambo au majibu au kusudi linalopaswa kutokea.

Tatu, unahitaji muda, utulivu na usikivu ili kuelewa kile Mungu amesema – katika Yeremia 23:18 imeandikwa Maana, ni nani aliyesimama katika baraza la Bwana, hata akalifahamu neno lake na kulisikia? Ni nani aliyelitia moyoni neno langu, na kulisikia?’ Siku zote Mungu hutafuta  utulivu na usikivu wa mwanandamu ili aweze kusema naye.

Hata hivyo moja ya gharama kubwa ya kumsikia na kumuelewa Mungu anaposema ambayo wengi wameshindwa kuilipa ni kutenga muda wa kuwa barazani pa Bwana wao (Yesu) ili aseme nao. Ndio mwanadamu anahitaji kuwa na muda na mazingira ya utulivu kama njia ya kumsaidia kufuatilia na kuelewa zaidi kile mbacho Mungu alisema naye kupitia ndoto, malaika, maono, sauti ya waziwazi, neno lake nk.

Nne, jifunze kuandika yale Mungu anasema nawe – mara nyingi Mungu husema nasi kwa habari ya mambo yajayo na anaposema kuna nyakati inakuwa si rahisi pia kuelewa kwa wakati huo. Hivyo hakikisha katika yale ambayo Mungu anasema nawe unayaandika ikiwa ni ndoto, neno, sauti au maono nk.

Kuandika kutakusaidia; (a) kufanya rejea ya yale Mungu amekuwa akisema nawe (b) kuendelea kuomba utimilifu wake ikiwa ni mambo mema au kutotokea ikiwa ni mambo mabaya (c) kuwa onyo kwako na hivyo kukuongezea umakini katika mahusiano yako na baadhi ya watu au vitu tegemeana na uliyoyona.

Tano, kuwa makini na sauti nyingine – ukirejea Yeremia 23:16 Biblia inasema Bwana wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha Bwana’. Hapa nisisitize kuhusu wale ambao hawataki kulipa gharama kumtafuta Mungu bali daima wanategemea kusikia kutoka kwa wanadamu.

Ni kweli kwamba Mungu husema kupitia wanadamu (watumishi wa kiroho), ingawa changamoto ni kwamba baadhi ya watumishi hawa si wa ufalme wa nuru, hata kama wanataja jina la Yeu, naam wamevaa ngozi ya kondoo lakini ndani ni mbwa mwitu. Kumbuka Shetani naye ana uwezo wa kusema na wanadamu kupitia njia mbalimbali. Hivyo ni muhimu sana kuwa na uelewa wa kutosha wa njia za Mungu ili ikusaidie kutofautisha na sauti ya Mungu na sauti nyingine.

Tamati – Mungu anaposema na mwanadamu kwa njia yoyote ile lengo lake ni kumsaidia mtu aishi katika njia sahihi ya kusudi lake (Zaburi 32:8). Kusikia na kuielewa sauti ya Mungu ni somo muhimu kwa mwamini kujua na kufuatilia mara kwa mara ili kuishi maisha yenye kuleta thamani kwenye maisha yake. Naamini ujumbe huu kuanzia sehemu ya kwanza hadi hii ya mwisho zitakuwa zimeweka msingi mzuri wa kuanzia.

Neema ya Bwana wetu, Yesu Kristo iwe nawe.

Utukufu na heshima, vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu.

NAMNA YA KUSIKIA NA KUIELEWA SAUTI YA MUNGU ILI IKUSAIDE KATIKA KUFANYA MAAMUZI (Sehemu ya tano)

March 16, 2017

Na: Patrick Sanga

Mada – Njia anazotumia Mungu kusema na mwanadamu (Sehemu ya tatu)

Katika sehemu ya nne ya somo hili na pia sehemu ya pili kwa mada hii tuliangalia njia ya nne ambayo ni sauti ya wazi wazi ya Mungu, ili kusoma sehemu hiyo bonyeza hapa https://sanga.wordpress.com/2016/09/12/namna-ya-kusikia-na-kuielewa-sauti-ya-mungu-ili-ikusaide-katika-kufanya-maamuzi-sehemu-ya-nne/. Katika sehemu hii ya tano kwa somo hili na sehemu ya tatu kwa mada husika tutaangalia njia kadhaa zilizosalia. Tafadhali fuatana nami tuendelee;

Njia ya tano, amani ya Kristo – Biblia katika kitabu cha Wakolosai 3:15 inasema Na amani ya Kristo IAMUE MIOYONI mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja tena iweni watu wa shukrani’. Kwenye toleo la kiingereza la GNB mstari huu unasema The peace that Christ gives is to GUIDE YOU IN THE DECISIONS YOU MAKE; for it is to this peace that God has called you together in the one body. And be thankful’.

Mistari hii inatufanya tujue kwamba, mosi, Mungu hutumia amani ya Kristo ndani ya mtu, kama njia mojawapo ya kusema na mwanadamu, na pili, ndani ya amani ya Kristo kuna sauti ya kumwongoza mtu kufanya uamuzi sahihi. Hivyo ni muhimu kwa mwanadamu kuwa na ufahamu kuhusu namna amani ya Kristo inavyofanya kazi na kuitafuta imuongoze kufanya maamuzi. Moja ya mambo muhimu kujua ili kuona matokeo mazuri ya amani ya Kristo kama mwamuzi, ni wewe kujifunza kuomba kimaswali hususani kwenye mambo ambayo yanakuweka njia panda kimaamuzi.

Kadri unavyoendelea kuomba kwa kuuliza kwa Mungu juu ya uamuzi gani uchukue, katika wazo ambalo ndani yake utasikia kupata amani au mpenyo, utasikia uhuru au furaha au raha hiyo ni ishara kwamba jambo hilo ndio sahihi kulifanyia kazi au kulifuatilia zaidi ili uongeze ufahamu juu yake kabla ya kulitekeleza. Kumbuka amani ya Kristo ambayo tumepewa inazipita akili zote (Wafilipi 4:7), hivyo itakuongoza kwenye uamuzi sahihi zaidi hata kama akili yako mwenyewe au za watu wanaokuzunguka kwa jinsi ya kibinadamu hawakubaliani na jambo hilo.

Njia ya sita, Kupitia maono – Ukisoma katika Hesabu 12:6 inasema ‘Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika MAONO, Nitasema naye katika ndoto’. Hata hivyo ukienda kwenye kitabu cha Ayubu 33:14 imeandikwa ‘Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, KATIKA MAONO YA USIKU, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani’.

Maono ni njia ya mafumbo, picha au taswira ambayo hufunua asili, undani au ukweli wa kile kinachofunuliwa au kinachoonekana. Maono yanapomhusu Mungu yanalenga kumfanya muonaji apondeke, aongezeke kiimani na kumjua Mungu zaidi. Maono yanapomhusu mtu, watu au jambo fulani, yanalenga kutufanya tuelewe asili, undani na ukweli kuhusu watu hao au jambo hilo na hivyo kutusaidia kujua mipaka ya kushirikiana, kuhusiana na kusaidina nao.

Mara nyingi ndoto humpata aliyelala usingizi wakati maono hutokea kwa mtu aliye macho kabisa na inaweza kuwa mahali popote pale. Jambo ambalo nimejifunza na kuthibitisha ni kwamba, mara nyingi maono hutokea kwa jinsi ya rohoni, yaani mtu kuchukuliwa katika roho au kuingizwa katika ulimwengu wa roho na kuanza kuona kilichokusudiwa. Kumbuka maono si ya mchana pekee kama wengi wanavyoelewa bali hata usiku pia watu hupata maono. (Mwanzo 15:1, Isaya 6:1-6, Ezekieli 1:1-3, Ufunuo wa Yohana 1:9-10, Yoel 2:28, Habakuki 2:1-5).

Njia ya saba, Kupitia kunena kwa lugha kunakoambatana na tafsiri – Biblia katika 1Wakorinto 14:27-28 inasema ‘Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri. Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu’ (Rejea pia 1Wakorinto 12:4 & 10). Ndiyo, hususani katika mazingira ya ibada au kusanyiko la kiroho, Mungu husema na watu kupitia kunena kwa lugha ambapo kati yao wanenao kuna ambaye amepewa karama ya kufasiri kinachonenwa au yeye mwenyewe anenaye ana uwezo wa kufasiri pia.

Hata hivyo nitoe ushauri kwa viongozi wa kiroho na wasimamizi wa ibada, waongeze ufahamu wao kuhusu njia hii, maana wengi wamekuwa wakiwapiga vita na kuwazuia watu wanaotaka kunena katikati ya ibada bila kujua ikiwa kunena huko ni kwa mapenzi ya Mungu au la, jambo ambalo limepelekea kuzima sauti ya Mungu kwenye huduma zao na kuzuia ujumbe uliokuwa umekusudiwa.

Njia ya nane, kupitia malaika – Katika Biblia tunaona matukio mengi ambayo Mungu aliwatumia malaika kusema na wanadamu juu ya mapenzi yake na hivyo kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yao. Malaika ni viumbe wa Mungu na jeshi linalomsaidia Mungu kufanya kazi mbalimbali. Tunaona Mungu alivyosema na kina Musa, Ibrahimu, Yakobo, Bikira Mariam, Paulo na wengine wengi kupitia malaika.

Sauti ya Mungu kupitia malaika ni njia au ufunuo wa kiwango cha juu sana ambao Mungu anaweza kusema na wanadamu ukilinganisha na njia zingine. Ufunuo huu wa malaika unaweza kuwa kwa malaika kukutokea kupitia ndoto au malaika kutokea waziwazi kwa maumbo yao au kupitia umbile la kitu kingine kama alivyomtokea Musa katikati ya mwali wa moto uliotoka kwenye kijiti kinachowaka.

Hata hivyo kupitia wenzetu ambao malaika walisema nao tunajifunza kwamba uaminifu, kumcha Mungu na kumaanisha (commitment) kumpenda Mungu katika wito wao ni sehemu ya vigezo vilivyopelekea Mungu kusema nao kwa njia hii. Malaika waliwatokea pia watu mbalimbali pale ambapo Mungu alikuwa na kusudi maalum la kufanya kupitia wao hata kama baadhi yao hawakuwa na sifa tajwa hapo juu (Mwanzo 22:10-12, 31:11-12, Danieli 10:11, Waamuzi 2:1, 13:2, Luka 1:13,35 Mathayo 1:20, Hesabu 22:24-34, Matendo ya Mitume 27:23 -24).

Njia ya tisa, Kupitia mazingira (asili/uumbaji) – Biblia katika kitabu cha Zaburi 19:1 inasema “Mbingu zahubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake’. Pia katika Yeremia 18:2 imenadikwaOndoka, ukashuke mpaka nyumba ya mfinyanzi, na huko nitakusikizisha maneno yangu’.

Ukiunganisha mawazo ya mistari hii unajifunza kwamba Mungu anaweza kutumia uumbaji wake au mazingira ili kusema na mwanadamu kama ilivyokuwa kwa Yeremia kupitia udongo na Balaamu kupitia mnyamna Punda ili kumpinga katika nia yake ovu dhidi ya Israeli.

Unapotafakari jinsi Mungu alivyomuumba mwanadamu na viumbe wengine jinsi ya ajabu, unapoona uumbaji wa milima, bahari, miti nk uumbaji huo unaleta ujumbe wenye kukufanya ujue hakuna jambo la kumshinda BWANA. Jambo muhimu ni kwamba ndani ya uumbaji huu kuna sauti ya Mungu inayoweza kusema nawe            (Zaburi 19:2, Warumi 1:20, Hesabu 22:24-34, Yeremia 18:1-6,).

Njia ya kumi, Kupitia majaribu yako au ya wengine – katika Zaburi 119:67 Biblia inasema ‘Kabla sijateswa mimi nalipotea, Lakini sasa nimelitii neno lako’. Hii ina maana majaribu au changaoto aliyoyapitia yalikuwa sauti ya Mungu ya kumrejesha kwenye njia na utiifu. Ndiyo maana Mtume Paulo anatuambia Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi’ (2Wakorinto 12:7).

Naam mwiba ule ulikuwa sauti au ujumbe kwa Paulo katika huduma yake, kwamba pamoja na wingi wa mafunuo, vipawa na karama alizonazo bado kuna mambo yalikuwa yakimuumiza na hakuweza kuyashinda kwa sababu Mungu ndio aliridhia yawe sehemu ya maisha yake, ili kumsaidia asijivune kupita kiasi. Hata hivyo Paulo alilipokea jambo hilo kwa ukomavu mkubwa na likawa chanzo cha kuongeza usikivu na jitihada yake katika kumtafuta Mungu.

Ndio maana hata leo kupitia changamoto mbalimbali ambazo mtu binafsi au ndugu/marafiki zake wanazipitia utawasikia wakisema Mungu amenifundisha mambo mengi kupitia ugonjwa huu, misiba, adha, au mateso haya nk. Jambo hili lina maana ndani ya kila jaribu kuna sauti au fundisho, ni muhimu kujifunza siri hizi ili kuelewa shule ya Mungu kwenye maisha yako.

Mpenzi msomaji katika sehemu hii, ndio nimehitimisha njia hizi kumi ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu. Hii haina maana ziko njia kumi mahsusi, bali njia hizi zinaweza kuongezeka au kupungua kutegemeana na lengo, ufahamu, uzoefu na ufunuo wa Mwandishi.

Somo litaendelea…

Neema ya Kristo iwe nanyi

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, Wastahili BWANA wangu.

FAHAMU UMUHIMU WA NAFASI YA MTU AU WATU WENGINE KWENYE MAISHA YAKO KIBIBLIA (Sehemu ya kwanza)

March 9, 2017

Na: Patrick Sanga

Mada: Mambo muhimu kujua kuhusu nafasi ya watu wengine kwenye maisha yako

Katika dunia tunayoishi kuna watu ambao ni fursa na wengine ni kikwazo katika kutekeleza kusudi la Mungu kwenye maisha yako. Unaweza ukawa nao lakini usijue kwamba wapo katikati yako, upande wako au kinyume chako. Katika kufanikisha kusudi lake hapa duniani Mungu hutumia watu, na kufanikiwa kwa kusudi lake kunategemea utiifu wa watu (mtu) hao kwenye wajibu waliopewa.

Biblia katika Warumi 8:28 inasema Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake’. Sasa ukienda kwenye Mithali 16:4 imeandikwa ‘Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya’. Biblia imetumia maneno mawili hapa ‘wampendao’ na ‘wabaya’. Kupitia maandiko haya tunajua kwamba Mungu anahitaji makundi yote mawili yaani wenye haki na wabaya ili kufanikisha kusudi lake.

Hivyo ni muhimu ufahamu kwamba kuna watu ambao Mungu amewaweka kwenye kila ngazi ya maisha yako ambao inabidi uunganishwe nao ili kufanikiwa na kuiendea njia sahihi. Watu wanaohusika na maisha yako wanaweza kuwa watoto, wazazi/walezi, viongozi wa kiroho na kijamii/kiserikali, marafiki, wafanyakazi wenzako nk. Sambamba na kundi hilo, pia usisahau kwamba wapo wale ambao ni kikwazo kwenye hatua unazopiga. Katika ufalme wa giza lengo la kundi hili la wabaya ni kukuondoa kwenye njia ya Mungu kabisa, lakini katika ufalme wa nuru lengo la kundi la pili ni kukufanya uimarike katika kumtafuta, kumtegemea na kumjua Mungu zaidi (Waamuzi 3:1-4)

w

 

Kumbuka kama siyo changamoto walizokutana nazo wana wa Israeli na baba zetu kina Ibrahimu, Isaka, Yakobo, Daudi, Paulo nk wasingemjua Mungu kwa kiwango walichomjua, naam wasingemtafuta na kupata mafunuo yaliyowawezesha kupiga hatua bila kukata tamaa. Hii inamaanisha kwamba mwanadamu pia anahitaji kuishi katikati ya makundi yote ili kufikia mwisho uliokusudiwa huku akiongeza umakini, utulivu na usikivu kwa Mungu katika kila hatua anayopiga (2Wakorinto 11:24-29).

Hivyo basi pamoja na utangulizi huu, yafuatayo ni mambo matano muhimu kujua na kuyafanyia kazi ili watu hao wahusike ipasavyo na yote ambayo Mungu ameweka ndani yao kwa jili yako;

  • Omba Mungu akuunganishe na watu husika – kama nilivyosema awali, unaweza kuwa unaishi katikati ya watu hawa usiwajue na hata wao wasijue kwamba wanahusika na maisha yako, hivyo omba Mungu akuunganishe nao. Kumbuka kila mtu ambaye Mungu anamleta kwenye maisha yako ni wazo jipya. Hivyo kadri unavyoomba ndivyo ufunuo wa nini huyo mtu amebeba kinachokusu unavyoongezeka na ndivyo naye anavyowajibika ipasavyo kwenye nafasi yake.

5

  • Omba wakae na kudumu kwenye nafasi zao – Wengi katika watu hawa hawako kwenye nafasi zao kiwajibu, hivyo ni jukumu lako kuomba Mungu awaweke na awadumishe kwenye nafasi ambazo uwepo wao ni fursa ya kufanikiwa kwako. Kadri unavyoomba ndivyo watu hao watakavyokaa kwenye nafasi husika kwa majira (nyakati) ambayo wanahitajika kuwepo ili kuwa dalaja la mafanikio yako.
  • Omba ulinzi wa Mungu juu yao – Kumbuka Shetani anafahamu siri hii, hivyo daima yeye (Shetani) huandaa mikakati (vikwazo/majaribu) ya kuwafanya watu hao wasikae kwenye nafasi zao na hivyo washindwe kufanya wajibu wao unaokuhusu. Hivyo kumbuka kuwaombea ulinzi wa kila kinachowahusu familia, watoto, kazi, ndoa nk maana uwepo na usalama wao ni mafaniko yako.

  • Dumisha mahusiano mazuri pamoja nao – mahusiano na mawasiliano mazuri kati yako na wale ambao Mungu amewaweka kuhusika na maisha yako ni wa lazima ili kufikia mafanikio yako. Naam jifunze kuombea amani yao maana kadri kunavyokuwa na amani kati yenu ndivyo na wao wanavyokuwa kwenye nafasi nzuri ya kushughulika na yale yanayokuhusu pia.
  • Watu hawa wapo kwa kila nyanja ya maisha – ni vizuri ukaelewa kwamba watu hawa wapo kwa kila nyanja ya maisha yako ikiwa ni pamoja na kikazi, kibiashara, kihuduma, kielimu, kiuchumi, kifamilia, ndoa, kilimo, ufugaji nk. Hivyo sio lazima watu hawa wakufahamu ana kwa ana au hata kwa jina lako, bali kupitia maisha yao, kazi zao, mahubiri au mafundisho yao, huduma zao, malezi yao na mwenendo wao kwa ujumla kuna vitu ambavyo wanaviachilia mahususi kwa ajili ya kukusaidia kupiga hatua ya kutekeleza kusudi la Mungu kwenye maisha yako.

r

 

Kwa nini uwaombee? –  hii ni kwa sababu watu hawa wameunganishwa moja kwa moja na mafaniko yako na hivyo unawahitaji ili kupiga hatua ya kwenda mbele, na si kila mtu anaweza kusimama kwenye nafasi yao kwa ajili yako. Watu hawa ni mfano wa mwili (viungo) wako, hata kama una moyo wenye nguvu na uwezo mkubwa sana kifikra na kimaauzi, bado unahitaji mwili unaofanya kazi ipasavyo ili kufikia yale unayowaza.

Tuteandelea na sehemu ya pili…

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili Bwana wangu.