USIPOKUWA NA WAZO JIPYA HUWEZI KUTOKA MAHALI ULIPO

Na: Patrick Samson Sanga

6

Salaam katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

Katika waraka wa Oktoba 2016 nimeona umuhimu wa kuandika ujumbe huu maalum ambao naamini utabadilisha kufikiri kwako na kukuongoza kuishi sawasawa na mapenzi ya Mungu kwenye maisha yako.

Nakumbuka mwaka 2010 nilikuwa nikipitia changamoto (majaribu) kubwa kikazi na kifamilia pia, naam changamoto ambazo zilichukua miezi kadhaa zikiniondolea furaha yangu. Nilidumu kumuomba Mungu katika kipindi chote hicho bila kukata tamaa ili anishindie, huku nikimuuliza natokaje kwenye changamoto hizi, mbona ni muda mrefu sasa?. Siku moja nilipomaliza kusoma neno na kuomba nikaamua kujipumzisha huku nikitafakari, ndipo, nikasikia sauti ikiniambia ‘usipokuwa na wazo jipya huwezi kutoka mahali ulipo’.

Sentensi hii ya ajabu ililikuwa ni mwongozo wa kunisaidia kutafuta wazo jipya lenye kuleta ufumbuzi wa kutoka mahali nilipokuwa. Hivyo nilibadlisha maombi yangu, kutoka kwenye maombi ya kuumia na kulalamika kwenda kwenye maombi ya kupata wazo jipya la kunitoa mahali nilipo. Haikuchukua hata wiki moja nikapata wazo (neno/ufunuo) ambalo lilibadilisha kwanza fikra (mtazamo) zangu kutoka kwenye mtazamo hasi ambao nilikuwa nao juu ya yale niliyopitia na juu ya wale ambao niliamini walichangia niwe kwenye hali niliyokuwa nayo. Naam baada ya kuridhia/kutii wazo jipya la BWANA, ndipo na ufumbuzi wa changamoto ukatokeza kama vile kuwasha umeme na nuru yake ikaangaza pande zote.

2

Katika Yeremia 29:11 imeandikwa hivi ‘Maana nayajua mawazo ninayowawazia, si mabaya, bali kuwapa ninyi tumaini katika siku zenu za mwisho’.  Ukienda kwenye 1Wakorinto 2:9 imeandikwa ‘lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao’.

Mistari hii miwili inatufanya tujue kwamba Mungu ANAYO mawazo ya amani (kukufanikisha) anayotuwazia kwa kila nyanja ya maisha yetu (yako). Ukweli ni kwamba haya ni mambo ambayo hakuna jicho limeona wala sikio lililosikia, na wala hayajaingia (kama wazo) kwenye moyo wa mwanadamu yeyote.             Je unajua ni kwa nini bado hayajaingia kwenye moyo wa mwanadamu yoyote? Hii ni kwa sababu hayo ni mawazo mahususi (specific) kwa ajili yako tu na si mtu mwingine yoyote na ndiyo maana unahitaji kuyajua ili kuishi sawasawa na kusudi la Mungu kwenye maisha yako.

Sasa ukienda katika Isaya 55:8 Mungu anasema waziwazi kwamba ‘Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu…’. Fahamu kwamba katika kila unalolipitia au linalokukabili ndani yake kuna mawazo/njia za Mungu za kulikabili au kulitekeleza ambazo ni tofauti na njia zetu wanadamu. Ndio maana katika Zaburi 32:8 anasema Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama’. Hiii ina maana unahitaji KUTAFUTA KUTOKA KWA MUNGU ILI KUPATA WAZO NA NJIA SAHIHI YA KUSHUGHULIKA NA CHANGAMOTO UNAZOZIPITIA, hata hivyo uhusinao na mawasiliano mazuri kati yako na Mungu ni msingi muhimu kwenye hili.

 Je unalipataje wazo jipya?

hy

Rejea ya mistari husika hapo juu inatupa kujua kwamba kwa Mungu ndiko kwenye mawazo sahihi na muafaka ya kututoa mahali tulipo. Hivyo unahitaji kulitafuta wazo jipya toka kwa Mungu kwa njia ya maombi ukiongozwa na neno lake. Kadri utakavyokuwa mwaminifu kutaka kujua kutoka kwake wazo jipya uwe na uhakika utajibiwa maana yeye ni mwaminifu katika ahadi zake.

Katika Wafilipi 4:6-7 imeandikwa Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu’.  Kwenye toleo la kiingereza la ESV mstari ule wa saba  umeandikwa ‘And the peace of God, which surpasses all understanding, will GUARD your hearts and your minds in Christ Jesus’.

af

Katika kufanya maombi ya kutafuta wazo jipya unahitaji kuongozwa na neno la Mungu kwa sababu ndani ya neno ndipo kuna elimu (maarifa au hekima au ufahamu) ya Mungu ipitayo akili zote. Mtume Paulo aliijua siri hii ndio maana akawaambia Wafilipi, msijisumbue, hivyo akawataka wamweleze Mungu mahitaji na changamoto zao. Kisha akawafunulia siri ya kile kitakachotokea akiwaambia, kwa Mungu kuna amani ipitayo akili zote, na kazi ya hiyo amani ni KUWAONGOZA (GUARD) KWENYE NIA NA MAAMUZI SAHIHI JUU YA YALE MNAYOYAPITIA. Amani ya Kristo hapa inawakilisha wazo lililo bora kuzidi mawazo mengine, ndiyo maana imeandikwa ipitayo akili zote, na kazi ya mojawapo ya amani ni kumsaidia mtu kufanya maamuzi sahihi, naam mtu hawezi kufanya uamuzi sahihi kama hajapata wazo sahihi toka kwa Mungu.

Ukweli wa jambo hili tunauona tunapounganisha mawazo ya mistari hii maana imeandkwa‘Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu’ (Mithali 4:7) na hii ni kwa sababu ‘Mtu mwenye hekima ana NGUVU; Naam, mtu wa maarifa huongeza UWEZO’(Mithali 24:5) naam na uwezo na nguvu zake ni huu ‘Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; MIMI NI UFAHAMU, mimi nina nguvu. Kwa msaada wangu wafalme humiliki, NA WAKUU WANAHUKUMU haki. Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, WAAMUZI wote wa dunia’ (Mithali 8:14-16).

10

Mpenzi msomaji maneno haya yakutie nguvu usiwe mtu wa kulia lia au kulalamika hata kumuwazia Mungu vibaya, naam haijalishi unapita kwenye changamoto za aina gani fahamu kwamba kwa Mungu liko wazo lililo bora na lenye nguvu kushinda mawazo (sauti)  mengine yoyote ya wanadamu, Shetani nk, naam litafute wazo hilo kutoka kwa Mungu litakusaidia nawe utachukua maamuzi sahihi kwa msaada wa AMANI YA KRISTO IPITAYO AKILI ZOTE, KUMBUKA AKILI ZOTE.

Hebu nikuonyeshe mawazo mapya kadhaa wakati namalizia ujumbe huu;

 • Kama hivi sasa kuna wazo la mauti limekuzunguka, wazo jipya la BWANA LINASEMA hutakufa bali utaishi upate kuyasimulia matendo makuu ya BWANA (Zaburi 118:17)
 • Kama umezungukwa na wazo la hatari/hofu, wazo la Mungu siku ya leo LINAKUAMBIA kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa (Isaya 54:17)
 • Kama unapita kwenye mateso mengi na uonevu/kutotendewa haki, wazo jipya la BWANA linasema ‘Mateso ya mwenye haki ni mengi lakini Bwana humponya nayo yote’ (Zaburi 34:19) na tena linakuambia ‘utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia’ (Isaya 54:17).
 • Kama unapita kwenye hatia ya dhambi na umeijutia na kuitubia dhambi uliyoitenda wazo la Mungu siku ya leo linasema ‘Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako’ (Isaya 43:25).

Kumbuka kwamba katika kuleta wazo jipya Mungu anaweza kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusema nawe moja kwa moja, kupitia watumishi (watu) wengine, kupitia mahubiri au mafundisho ya kiroho kwenye vitabu, luninga, mitandao ya kijamii, blogs au website nk.

9

Mpenzi msomaji, kulia, kujisumbua, kulalamika au kulaumu wengine siyo njia ya kupata ufumbuzi. TAMBUA KWAMBA KWA MUNGU WETU LIKO WAZO JIPYA LA KUKUTOA MAHALI ULIPO, LITAFUTE NAWE UTALIONA NALO LITAKUSIADIA. Ikiwa haujaokoka na unapenda kuokoka bonyeza ‘link’ hii  https://sanga.wordpress.com/wokovu/  utapata mwongozo muafaka.

Utukufu na Heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA

… Utaiinua misingi ya vizazi vingi (Isaya 58:12)

Advertisements

10 comments

   • Amen Mungu aliyeianzisha kazi hiyo ndani yako aikamilishe. Naomba uwe unanitumia masomo zaidi kwenye e-mail yangu. Pia masomo ya kujitambua kama kijana na kuishi maisha ya kuendelea kudumu katika kumpendeza MUNGU. Barikiwa.

    Like

   • Amina Edna, changamoo kwangu ni muda, ushauri wangu, unaweza kuji subscribe kwenye blog hii, ili kila niwekapo somo jipya linakuja kwako pia moja kwa moja.

    Like

 1. Mtumishi (Patrick Snga) zidi kutufundisha pasipo kukata tamaa. Napenda sana kufatilia masomo yako mahali hapa tangu mwaka 2011. Umekuwa kimya sana. Kuna kitu kikubwa sana ulichonacho kwa ajili ya kanisa la leo, tunahitaji walimu wa kulisaidia kanisa. Nakuombea sana Mungu azidi kukuinua. Je, una page yoyote ya facebook? Naitwa Mtumishi Wilfred Tarimo Mmiliki wa http://www.ishindotoyako.com

  Like

 2. Mtumishi kwa kweli masomo yako yamenibadilisha sana kutoka nilipokua na kuniweka mahala pazuri na penye hofu ya Mungu pia nilipenda nipate masomo ya akina mama au jinsi ya kuishi katika ndoa. ubarikiwe sana

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s