FURAHA YA KUTIMIZA MIAKA KUMI (10) YA BLOG HII (Ten Years Blogging Anniversary)

Na: Patrick Saga

1

Shalom mpenzi msomaji, nakusalimu kwa jina la BWANA wetu Yesu Kristo.

Leo Septemba 16, 2016 blog hii ya www.sanga.wordpress.com  imetimiza miaka kumi (10) tangu nilipoifungua na kuweka ujumbe wa kwanza tarehe 16.09.2006. Katika kuadhimisha miaka kumi ya uwepo wa Blog hii leo nimeona ni vema kuandika historia fupi kuhusu uandishi wangu na ‘blog’ hii sambamba na kutoa shukrani kwa neema ya Mungu iliyokuwa nami kwa kipindi hicho.

Historia fupi ya blog hii – Nilianza rasmi kuandaa masomo mwaka 2003 nikiwa Mkoani Mbeya, hata hivyo sikuwa na ufahamu wowote kuhusu masuala ya blog au website. Hivyo pale nilipopata fursa ya kufundisha kanisani kwetu nilifanya hivyo ingawa kuanzia mwaka 2004 nilitamani sana kama ningepata fursa ya kuwafikia watu wengi zaidi kwa masomo niliyokuwa nikiandaa.

Mwaka huo huo ndipo BWANA aliposema nami kwa mara ya kwanza kupitia kitabu cha Isaya sura nzima ya 58 na akaniwekea msisitizo na maelekezo ya pekee kwenye mstari wa 58:12 unaosema Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; UTAIINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia”.

Ilipofika mwaka 2006 nilipata fursa ya kwenda nchini Kenya kwa masuala ya kihuduma, nikiwa mpakani mwa Kenya na Somalia, mji wa Garisa, BWANA alisema nami kuhusu elimu ya kuzimu (Doctrine of Hell), naye akaniambia ‘Watu wengi sana wanaenda kuzimu baada ya kufa kwa kuwa hawanijui mimi’ na kisha akaniuliza ‘unawezaje kunyamaza ikiwa watu wengi namna hii wanapotea?

4

Mpenzi msomaji, ujumbe huu ndio uliochochea kile ambacho nilijifunza mwaka 2004 kupitia Kitabu cha Isaya sura ya 58 ambayo inaanza kwa kusema ‘Piga kelele, USIACHE, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao’ (Isaya 58:1). Hivyo baada ya kurejea jijini Nairobi BWANA alinikutanisha na Ndg. Jersey (Mwandishi wa masuala ya kijamii nchini Kenya) ambaye baada ya kumweleza nia yangu ya kuandika, aliniongoza kufungua ‘blog’ hii na rasmi nikaanza kuweka masomo.

Julai 2009, BWANA alisema nami kwa habari ya uandishi huu na akaniambia ‘bado kuna vikapu vingi vya masomo vinakungoja’. Ikiwa unataka kujua zaidi kuhusu ushuhuda huu bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2012/01/21/waandishi-tusilale-bado-kuna-wajibu-mkubwa-mbele-yetu/

5 

Kuhusu masomo na wasomaji – Tangu nimeanza kuandika masomo nimefanikiwa kuandaa zaidi ya masomo mia mbili (200) ya kiroho ingawa niliyoyaweka kwenye ‘blog’ hii mpaka sasa ni wastani wa masomo mia moja na ishirini yakiwa kwenye makundi (categories) mbalimbali kama vile vijana, wanawake, wanandoa, Roho Mtakatifu, mafundisho kwa ujumla, nyaraka mbalimbali nk. Takwimu za mtandao za hadi kufikia Septemba 2016, zinaonyesha kwamba wasomaji wa ‘blog’ hii wanapatikana kutoka zaidi ya nchi themanini (80) duniani kote.

Maboresho kadhaa yanayokuja – Si wasomaji wengi wanafahamu kwamba nimekuwa nikiandaa masomo mbalimbali ya kiroho kwa lugha ya kiingereza pia. Hivyo baada ya tafakari ya muda mrefu nimewaza kwamba kuanzia sasa nitakuwa nikiyaweka kwenye ‘blog’ hii kupitia ‘category’ yake maalum ili kulifikia na kundi jingine. Tafadhali naomba radhi kwa wasomaji wasiojua kiingereza wasijisikie vibaya, ni jambo ambalo nimelisikia ndani yangu kufanya na zaidi sitaacha kuweka masomo kwa lugha ya Kiswahili pia.

2

Shukrani kwa Mungu wangu – hakika nina kila sababu ya kumshukuru Mungu ambaye yeye ndiye aliyeniita kwenye jukumu hili muhimu la kuanika masomo mbalimbali ya kiroho. Haijawa kazi rahisi kuandika masomo kila mwezi/mwaka na kuyaweka humu, lakini kwa sababu mwenye kulianzisha ni Mungu hakuniacha pekee yangu ndio maana leo tunasherekea kutimiza miaka kumi ya uandishi endelevu.

Shukrani kwa wasomaji na wachangiaji – katika shukrani naomba nikushukuru wewe mpenzi msomaji kwa kutenga muda wa kujifunza na kuongeza ufahamu wako wa masuala ya kiroho kupitia blog hii, naam ninapojua kwamba masomo ninayoandaa kuna watu wanayasoma na kuwasaidia kupiga hatua fulani kwenye maisha yao linaniimarisha na kunipa nguvu mpya ya kuandika na kuandika na kuandika.

Pia nawashukuru wale ambao licha ya kusoma na kupata maarifa, wamekuwa wakiandika mawazo (comment) mbalimbali kwa lengo la kunitia moyo, kuniongezea mambo ya kuboresha na kubwa zaidi wakichangia kujibu au kuwatia moyo wasomaji mbalimbali wanaokuwa wana maswali au mahitaji ya kiroho.

Shukrani kwa wamiliki wa ‘blog’ nyingine –naomba pia kutoa shukrani zangu kwa baadhi ya wamiliki wa blog za kikristo na kijamii pia ambao wameenda mbele zaidi na kutoa fursa za baadhi ya masomo ya blog hii kuwekwa (post) kwenye blog zao na hivyo kuongeza wigo wa wasomaji wa masomo haya, nawashukuru sana wapendwa wangu, Mungu awabariki.

Shukrani kwa famila yangu – namshukuru sana Mungu kunipa mke (Flora) ambaye amefanyika msaada mkubwa kwangu katika jukumu hili la uandishi pamoja na wanangu Barnaba & Bernada ambao wamekuwa wakivumilia kunikosa siku za mapumziko (weekend) kwa kuwa, mimi hutumia siku hizo kuaandaa masomo haya. Hakika binafsi natambua mchango wao kwenye huduma hii, Mungu wangu awalinde na kuwatunza.

3

Ahsante BWANA wangu, leo tarehe 16.09.2016 ‘blog’ hii imetimiza miaka kumi (10) tangu kuanzishwa kwake, utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu.

“… Utaiinua misingi ya vizazi vingi”

Advertisements

8 comments

 1. “Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule. 6 Akatazama, kumbe! Pana mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena. 7 Malaika wa BWANA akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako. 8 Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku h…”
  Mungu akubariki mno kaka, Na Mungu akatende kwako kama kwa wajina wangu Eliya.
  barikiwa

  Like

 2. Hongera sana Patrick kwa kutimiza muongo (decade) mmoja wa huduma katika blog yako. Binafsi nimenufaka sana kwa mafundisho yaliyo kwenye blog yako ingawa sijawahi kupitia nikasoma somo moja baada ya lingine ila mengi nimeyasoma. Huwa nikijifunza ujumbe fulani kwenye biblia nina-google kuona walimu wamefundisha namna gani kuhusu hilo jambo na katika kufanya hivyo nimekuwa nakutana na mada nyingi ulizofundisha. Na baadaye nili-subscribe kwenye blog yako hivyo nikawa napata kila post unayoweka kwenye blog yako.

  Kiukweli blog yako imeniimarisha sana katika wokovu na huduma yangu. Huwa nikijifunza jambo ninapenda sana kufahamu “what”, “how” na “why” kuhusu hilo jambo na kwako nimekuwa nikipata hivyo vyote. Pia mafundisho ninayoyapata kwako yameniongezea uwezo wa kuhudumia kundi alilonipa Bwana kulihudumia nyumbani kwangu na kwenye faragha ninayoshiriki. Katika miaka ya awali nilipookoka, faragha za awali nilizipata kwa walimu wa kwenye mitandao na wewe ukiwa miongoni mwao, ninamshukuru sana Mungu kwa ajili yako. Na wakati huo sikuwa hata na upenyo wa kushiriki faragha kanisani ninakoabudu kutokana na ufinyu wa muda. Hivyo huduma ninayoipata kwenye blog yako imefanyika baraka kubwa katika maisha yangu.Yale niliyojifunza kwako nimekuwa nikiwafundisha wengine nilioweza kuwafikia. Mungu akubariki sana Patrick na wote wa malangoni mwako, azidi sana kuimarisha huduma yako, awape na afya njema na nguvu zaidi ya kuifanya kazi yake.

  Like

  • Amen, amen, amen Martha, utukufu katika mambo yote apewe Mungu, naam ahsante pia kwa kuwa na muda wa kujifunza kupitia blog hii, na kuwafundisha wengine, Mungu wangu akubariki na kukumbuka katika mahitaji yako pia.Naam tuzidi kuombeana.

   Like

 3. Hongera Kaka Sanga na Mungu atukuzwe kwa kazi unayofanya kwa ajili ya ufalme wa Mungu.

  Blog hii imekuwa kwangu sehemu ya kumsikia Mungu kupitia Neno lake.

  Mungu azidi kukuimairsha, mana kwa njia hii ya blog,Mungu anasema na kutubadilisha wengi.

  Bwana Yesu apewe sifa.

  Like

 4. barikiwa sana kaka. masomo yamenisaidia sana.
  na mengi nimekuwa naprint nawapatia watu wanasoma sasa sijui kama ni kosa. kama nikosa utanisamehe ila naprint sana na kuwapa wengine wasome.

  Mungu aendelee kukupa ufunuo zaidi.

  Like

  • Amen Gift, Mungu akubariki kwa huduma njema uifanyayo maadam hakuna kinachoongezwa wala kupunguzwa katika niliyoyaandika. Uwe na amani, huduma yako ni njema pia endelea nayo.

   Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s