NAMNA YA KUSIKIA NA KUIELEWA SAUTI YA MUNGU ILI IKUSAIDE KATIKA KUFANYA MAAMUZI (Sehemu ya nne)

Na: Patrick Sanga

1

Mada – Njia anazotumia Mungu kusema na mwanadamu (Sehemu ya pili)

Katika sehemu ya tatu ya somo hili na pia sehemu ya kwanza kwa mada hii tuliangalia njia tatu ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu, ili kusoma sehemu hiyo bonyeza hapa https://sanga.wordpress.com/2015/08/20/namna-ya-kusikia-na-kuielewa-sauti-ya-mungu-ili-ikusaide-katika-kufanya-maamuzi-sehemu-ya-tatu/ . Katika sehemu hii ya pili kwa mada husika nitaendelea na njia ya nne, naam fuatana nami tuendelee;

Njia ya nne, sauti ya wazi wazi (mdomo kwa mdomo) ya Mungu

Watu wengi wanapozungumzia kuhusu kusikia sauti ya Mungu humaanisha njia hii, naam wanataka kumsikia Mungu akisema nao wazi wazi kama vile mtu asemavyo na mwenzake, naam ni jambo linalowezekana lakini gharama yake ni kubwa ukilinganisha na nja nyingine.

Ukirejea kwenye Biblia yapo maandiko mbalimbali yenye kuthibitisha kwamba Mungu husema kwa njia hii, lakini hata hivyo hakuna ufafanuzi wa kina juu ya namna ambavyo Mungu alisema na watumishi hao, ila mara nyingi imeandikwa ‘BWANA Mungu akasema … ‘ na jambo muhimu ni kwamba wale aliosema nao walielewa kwamba anasema nao.

Katika Hesabu 12:7-8 imeandikwa ‘Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?’

3

Katika mistari hii Mungu anatuonyesha kwamba kuna njia ambazo hutumia kusema na wanadamu ambazo ndani yake kuna mafumbo na nyingine hazina mafumbo. Katika njia hii uaminifu ndio msingi mkuu kwa mtu kumsikia Mungu akisema naye kwa sauti itokayo katika kinywa chake wala si kwa mafumbo kama ilivyo kwa njia nyingine za ndoto, maono nk (Matendo ya Mitume 22:14).

Kweli tano muhimu za kujua kuhusu njia hii ya sauti ya wazi wazi;

  • Licha ya kwamba sauti hutoka katika kinywa cha Mungu haina maana utauona uso wake (kinywa), bali kupitia Roho Mtakatifu utasikia sauti ya Mungu ikisema kama vile anakusikizisha sauti yake kwenye sikio lako au ndani ya ufahamu wako hata unaweza kugeuka utazame sauti ilikotoka. Ndiyo sauti yake inakuwa dhahiri kana kwamba anazungumza nawe ana kwa ana, isipokuwa haonekani kwa macho ya damu na nyama (Mathayo 10:18–20 Matendo ya Mitume 13:2).
  • Katika utatu wa Mungu kuna nidhamu ya ajabu kiasi kwamba si tu Roho Mtakatifu anasema anachotaka (kunena kwa shauri lake mwenyewe) bali hunena kwetu, kile anachosikia kutoka kwa Baba (Yohana 16:13).
  • Mara nyingi sauti Mungu kupitia njia hii huwa ni sauti ndogo yenye utulivu na hivyo ni muhimu kwa mwamini kuwa na usikivu na utulivu mkubwa wa rohoni kila wakati ili kusikia na kuelewa sauti ya Mungu (1Wafalme 19:11–13).

6

  • Unahitaji kuwa na ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu ndani yako ili kupima na kuelewa ujumbe wowote unaousikia. Hii ni kwa sababu, bila kujali njia gani Mungu ataitumia kusema nawe, chochote atakachosema uwe na uhakika hakiwezi kutofautiana na neno lake.
  • Unahitaji kuwa na uelewa wa ulimwengu wa roho ulivyo sambamba na namna falme zinazotawala huko zinavyofanya kazi na mawasiliano. Jambo hili litakuongezea ufahamu wako katika kuisikia sauti ya Mungu na hivyo kuitofautisha na sauti ya Shetani pia, hii ni kwa sababu licha ya Mungu kusema na Shetani (mapepo) naye husema.

Siku moja nilifanyiwa upasuaji mdogo wa uvimbe mwilini mwangu. Baada ya kumaliza nilimuuliza Daktari, hivi vitambaa (gauze) vyenye damu yangu unavipeleka wapi? Akasema upo utaratibu mzuri kukusanya, kuhifadhi na kuteketeza takataka za aina hiyo kwa pamoja kila siku kwenye tanuru maalum.

Punde baada ya Daktari kusema hivyo ndipo kwenye ulimwengu wa roho nikasikia mapepo yakisema ‘kosa kubwa sana, kabla hawajavichoma tutavichukua vitaambaa hivyo na kwa hivyo tutakuwa tumeipata damu yake’. Naam kufuatia taarifa hiyo ambayo Roho Mtakatifu aliniruhusu niijue, kwa hekima niliongea na yule Daktari njia bora zaidi ya kuviteketeza moja kwa moja bila kukusanya na taka taka nyingine, naam akanielewa.

Naomba uelewe kwamba sauti niliyoisikia siyo ya Roho Mtakatifu, bali ni ya mapepo. Roho Mtakatifu kutoka kwenye nafasi ya kuwa Mfunuaji na Mpashaji wa mambo yaliyoko mbele yetu saa ile ile alifungua masikio yangu ya rohoni nikasikia kile ambacho Shetani alikusudia kwangu. Hivyo kupitia ushuhuda huu nataka ujibiidishe kumjua sana Mungu na namna yeye anavyosema na itakuwa rahisi kwako kuelewa pale utakoposikia sauti nyingine yoyote isiyo ya Mungu.

2

Nimalize kwa kukutia moyo kwamba, usiumie endapo hujawahi kuisikia sauti ya Mungu wazi wazi kama alivyo sema na akina Musa. Jambo muhimu ni kwamba Mungu ana njia nyingi za kusema na wanadamu, na yeye anachotafuta ni utiifu wao kwenye maagizo yake ili kutenda mapenzi yake. Ukweli ni kwamba ipo tofauti kubwa sana ya kumsikia Mungu akisema kwa njia hii (wazi wazi) na kupitia njia nyingine.

Habari njema ni kwamba, Mungu hajaweka mipaka ya kusema na watoto wake, bali katusaidia kujua vigezo vya yeye kusema nasi kwa njia hii. Ikiwa unatamani kumsikia Mungu akisema nawe wazi wazi hakikisha unakuwa mwaminifu kwa yale ambayo anasema nawe kwa njia za kawaida na kudumu kuimarisha uhusiano mzuri na Roho Mtakatifu(Yohana 14:26). Ukidumu kufanya hivyo utaiingizwa kwenye hatua nyingine kubwa ya mahusiano na mawasiliano kati yako na Mungu na kusikia akisema nawe kwa njia hii.

Naam mpenzi msomaji leo naishia hapa, katika mfululizo ujao nitaendelea na njia nyingine, neema ya BWANA wetu Yesu Kristo iwe nawe. Somo litaendelea…

 

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, unastahili BWANA wangu.

‘… Utaiinua misingi ya vizazi vingi’

Advertisements

3 comments

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s