Archive for September 2016

FURAHA YA KUTIMIZA MIAKA KUMI (10) YA BLOG HII (Ten Years Blogging Anniversary)

September 16, 2016

Na: Patrick Saga

1

Shalom mpenzi msomaji, nakusalimu kwa jina la BWANA wetu Yesu Kristo.

Leo Septemba 16, 2016 blog hii ya www.sanga.wordpress.com  imetimiza miaka kumi (10) tangu nilipoifungua na kuweka ujumbe wa kwanza tarehe 16.09.2006. Katika kuadhimisha miaka kumi ya uwepo wa Blog hii leo nimeona ni vema kuandika historia fupi kuhusu uandishi wangu na ‘blog’ hii sambamba na kutoa shukrani kwa neema ya Mungu iliyokuwa nami kwa kipindi hicho.

Historia fupi ya blog hii – Nilianza rasmi kuandaa masomo mwaka 2003 nikiwa Mkoani Mbeya, hata hivyo sikuwa na ufahamu wowote kuhusu masuala ya blog au website. Hivyo pale nilipopata fursa ya kufundisha kanisani kwetu nilifanya hivyo ingawa kuanzia mwaka 2004 nilitamani sana kama ningepata fursa ya kuwafikia watu wengi zaidi kwa masomo niliyokuwa nikiandaa.

Mwaka huo huo ndipo BWANA aliposema nami kwa mara ya kwanza kupitia kitabu cha Isaya sura nzima ya 58 na akaniwekea msisitizo na maelekezo ya pekee kwenye mstari wa 58:12 unaosema Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; UTAIINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia”.

Ilipofika mwaka 2006 nilipata fursa ya kwenda nchini Kenya kwa masuala ya kihuduma, nikiwa mpakani mwa Kenya na Somalia, mji wa Garisa, BWANA alisema nami kuhusu elimu ya kuzimu (Doctrine of Hell), naye akaniambia ‘Watu wengi sana wanaenda kuzimu baada ya kufa kwa kuwa hawanijui mimi’ na kisha akaniuliza ‘unawezaje kunyamaza ikiwa watu wengi namna hii wanapotea?

4

Mpenzi msomaji, ujumbe huu ndio uliochochea kile ambacho nilijifunza mwaka 2004 kupitia Kitabu cha Isaya sura ya 58 ambayo inaanza kwa kusema ‘Piga kelele, USIACHE, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao’ (Isaya 58:1). Hivyo baada ya kurejea jijini Nairobi BWANA alinikutanisha na Ndg. Jersey (Mwandishi wa masuala ya kijamii nchini Kenya) ambaye baada ya kumweleza nia yangu ya kuandika, aliniongoza kufungua ‘blog’ hii na rasmi nikaanza kuweka masomo.

Julai 2009, BWANA alisema nami kwa habari ya uandishi huu na akaniambia ‘bado kuna vikapu vingi vya masomo vinakungoja’. Ikiwa unataka kujua zaidi kuhusu ushuhuda huu bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2012/01/21/waandishi-tusilale-bado-kuna-wajibu-mkubwa-mbele-yetu/

5 

Kuhusu masomo na wasomaji – Tangu nimeanza kuandika masomo nimefanikiwa kuandaa zaidi ya masomo mia mbili (200) ya kiroho ingawa niliyoyaweka kwenye ‘blog’ hii mpaka sasa ni wastani wa masomo mia moja na ishirini yakiwa kwenye makundi (categories) mbalimbali kama vile vijana, wanawake, wanandoa, Roho Mtakatifu, mafundisho kwa ujumla, nyaraka mbalimbali nk. Takwimu za mtandao za hadi kufikia Septemba 2016, zinaonyesha kwamba wasomaji wa ‘blog’ hii wanapatikana kutoka zaidi ya nchi themanini (80) duniani kote.

Maboresho kadhaa yanayokuja – Si wasomaji wengi wanafahamu kwamba nimekuwa nikiandaa masomo mbalimbali ya kiroho kwa lugha ya kiingereza pia. Hivyo baada ya tafakari ya muda mrefu nimewaza kwamba kuanzia sasa nitakuwa nikiyaweka kwenye ‘blog’ hii kupitia ‘category’ yake maalum ili kulifikia na kundi jingine. Tafadhali naomba radhi kwa wasomaji wasiojua kiingereza wasijisikie vibaya, ni jambo ambalo nimelisikia ndani yangu kufanya na zaidi sitaacha kuweka masomo kwa lugha ya Kiswahili pia.

2

Shukrani kwa Mungu wangu – hakika nina kila sababu ya kumshukuru Mungu ambaye yeye ndiye aliyeniita kwenye jukumu hili muhimu la kuanika masomo mbalimbali ya kiroho. Haijawa kazi rahisi kuandika masomo kila mwezi/mwaka na kuyaweka humu, lakini kwa sababu mwenye kulianzisha ni Mungu hakuniacha pekee yangu ndio maana leo tunasherekea kutimiza miaka kumi ya uandishi endelevu.

Shukrani kwa wasomaji na wachangiaji – katika shukrani naomba nikushukuru wewe mpenzi msomaji kwa kutenga muda wa kujifunza na kuongeza ufahamu wako wa masuala ya kiroho kupitia blog hii, naam ninapojua kwamba masomo ninayoandaa kuna watu wanayasoma na kuwasaidia kupiga hatua fulani kwenye maisha yao linaniimarisha na kunipa nguvu mpya ya kuandika na kuandika na kuandika.

Pia nawashukuru wale ambao licha ya kusoma na kupata maarifa, wamekuwa wakiandika mawazo (comment) mbalimbali kwa lengo la kunitia moyo, kuniongezea mambo ya kuboresha na kubwa zaidi wakichangia kujibu au kuwatia moyo wasomaji mbalimbali wanaokuwa wana maswali au mahitaji ya kiroho.

Shukrani kwa wamiliki wa ‘blog’ nyingine –naomba pia kutoa shukrani zangu kwa baadhi ya wamiliki wa blog za kikristo na kijamii pia ambao wameenda mbele zaidi na kutoa fursa za baadhi ya masomo ya blog hii kuwekwa (post) kwenye blog zao na hivyo kuongeza wigo wa wasomaji wa masomo haya, nawashukuru sana wapendwa wangu, Mungu awabariki.

Shukrani kwa famila yangu – namshukuru sana Mungu kunipa mke (Flora) ambaye amefanyika msaada mkubwa kwangu katika jukumu hili la uandishi pamoja na wanangu Barnaba & Bernada ambao wamekuwa wakivumilia kunikosa siku za mapumziko (weekend) kwa kuwa, mimi hutumia siku hizo kuaandaa masomo haya. Hakika binafsi natambua mchango wao kwenye huduma hii, Mungu wangu awalinde na kuwatunza.

3

Ahsante BWANA wangu, leo tarehe 16.09.2016 ‘blog’ hii imetimiza miaka kumi (10) tangu kuanzishwa kwake, utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu.

“… Utaiinua misingi ya vizazi vingi”

NAMNA YA KUSIKIA NA KUIELEWA SAUTI YA MUNGU ILI IKUSAIDE KATIKA KUFANYA MAAMUZI (Sehemu ya nne)

September 12, 2016

Na: Patrick Sanga

1

Mada – Njia anazotumia Mungu kusema na mwanadamu (Sehemu ya pili)

Katika sehemu ya tatu ya somo hili na pia sehemu ya kwanza kwa mada hii tuliangalia njia tatu ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu, ili kusoma sehemu hiyo bonyeza hapa https://sanga.wordpress.com/2015/08/20/namna-ya-kusikia-na-kuielewa-sauti-ya-mungu-ili-ikusaide-katika-kufanya-maamuzi-sehemu-ya-tatu/ . Katika sehemu hii ya pili kwa mada husika nitaendelea na njia ya nne, naam fuatana nami tuendelee;

Njia ya nne, sauti ya wazi wazi (mdomo kwa mdomo) ya Mungu

Watu wengi wanapozungumzia kuhusu kusikia sauti ya Mungu humaanisha njia hii, naam wanataka kumsikia Mungu akisema nao wazi wazi kama vile mtu asemavyo na mwenzake, naam ni jambo linalowezekana lakini gharama yake ni kubwa ukilinganisha na nja nyingine.

Ukirejea kwenye Biblia yapo maandiko mbalimbali yenye kuthibitisha kwamba Mungu husema kwa njia hii, lakini hata hivyo hakuna ufafanuzi wa kina juu ya namna ambavyo Mungu alisema na watumishi hao, ila mara nyingi imeandikwa ‘BWANA Mungu akasema … ‘ na jambo muhimu ni kwamba wale aliosema nao walielewa kwamba anasema nao.

Katika Hesabu 12:7-8 imeandikwa ‘Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?’

3

Katika mistari hii Mungu anatuonyesha kwamba kuna njia ambazo hutumia kusema na wanadamu ambazo ndani yake kuna mafumbo na nyingine hazina mafumbo. Katika njia hii uaminifu ndio msingi mkuu kwa mtu kumsikia Mungu akisema naye kwa sauti itokayo katika kinywa chake wala si kwa mafumbo kama ilivyo kwa njia nyingine za ndoto, maono nk (Matendo ya Mitume 22:14).

Kweli tano muhimu za kujua kuhusu njia hii ya sauti ya wazi wazi;

 • Licha ya kwamba sauti hutoka katika kinywa cha Mungu haina maana utauona uso wake (kinywa), bali kupitia Roho Mtakatifu utasikia sauti ya Mungu ikisema kama vile anakusikizisha sauti yake kwenye sikio lako au ndani ya ufahamu wako hata unaweza kugeuka utazame sauti ilikotoka. Ndiyo sauti yake inakuwa dhahiri kana kwamba anazungumza nawe ana kwa ana, isipokuwa haonekani kwa macho ya damu na nyama (Mathayo 10:18–20 Matendo ya Mitume 13:2).
 • Katika utatu wa Mungu kuna nidhamu ya ajabu kiasi kwamba si tu Roho Mtakatifu anasema anachotaka (kunena kwa shauri lake mwenyewe) bali hunena kwetu, kile anachosikia kutoka kwa Baba (Yohana 16:13).
 • Mara nyingi sauti Mungu kupitia njia hii huwa ni sauti ndogo yenye utulivu na hivyo ni muhimu kwa mwamini kuwa na usikivu na utulivu mkubwa wa rohoni kila wakati ili kusikia na kuelewa sauti ya Mungu (1Wafalme 19:11–13).

6

 • Unahitaji kuwa na ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu ndani yako ili kupima na kuelewa ujumbe wowote unaousikia. Hii ni kwa sababu, bila kujali njia gani Mungu ataitumia kusema nawe, chochote atakachosema uwe na uhakika hakiwezi kutofautiana na neno lake.
 • Unahitaji kuwa na uelewa wa ulimwengu wa roho ulivyo sambamba na namna falme zinazotawala huko zinavyofanya kazi na mawasiliano. Jambo hili litakuongezea ufahamu wako katika kuisikia sauti ya Mungu na hivyo kuitofautisha na sauti ya Shetani pia, hii ni kwa sababu licha ya Mungu kusema na Shetani (mapepo) naye husema.

Siku moja nilifanyiwa upasuaji mdogo wa uvimbe mwilini mwangu. Baada ya kumaliza nilimuuliza Daktari, hivi vitambaa (gauze) vyenye damu yangu unavipeleka wapi? Akasema upo utaratibu mzuri kukusanya, kuhifadhi na kuteketeza takataka za aina hiyo kwa pamoja kila siku kwenye tanuru maalum.

Punde baada ya Daktari kusema hivyo ndipo kwenye ulimwengu wa roho nikasikia mapepo yakisema ‘kosa kubwa sana, kabla hawajavichoma tutavichukua vitaambaa hivyo na kwa hivyo tutakuwa tumeipata damu yake’. Naam kufuatia taarifa hiyo ambayo Roho Mtakatifu aliniruhusu niijue, kwa hekima niliongea na yule Daktari njia bora zaidi ya kuviteketeza moja kwa moja bila kukusanya na taka taka nyingine, naam akanielewa.

Naomba uelewe kwamba sauti niliyoisikia siyo ya Roho Mtakatifu, bali ni ya mapepo. Roho Mtakatifu kutoka kwenye nafasi ya kuwa Mfunuaji na Mpashaji wa mambo yaliyoko mbele yetu saa ile ile alifungua masikio yangu ya rohoni nikasikia kile ambacho Shetani alikusudia kwangu. Hivyo kupitia ushuhuda huu nataka ujibiidishe kumjua sana Mungu na namna yeye anavyosema na itakuwa rahisi kwako kuelewa pale utakoposikia sauti nyingine yoyote isiyo ya Mungu.

2

Nimalize kwa kukutia moyo kwamba, usiumie endapo hujawahi kuisikia sauti ya Mungu wazi wazi kama alivyo sema na akina Musa. Jambo muhimu ni kwamba Mungu ana njia nyingi za kusema na wanadamu, na yeye anachotafuta ni utiifu wao kwenye maagizo yake ili kutenda mapenzi yake. Ukweli ni kwamba ipo tofauti kubwa sana ya kumsikia Mungu akisema kwa njia hii (wazi wazi) na kupitia njia nyingine.

Habari njema ni kwamba, Mungu hajaweka mipaka ya kusema na watoto wake, bali katusaidia kujua vigezo vya yeye kusema nasi kwa njia hii. Ikiwa unatamani kumsikia Mungu akisema nawe wazi wazi hakikisha unakuwa mwaminifu kwa yale ambayo anasema nawe kwa njia za kawaida na kudumu kuimarisha uhusiano mzuri na Roho Mtakatifu(Yohana 14:26). Ukidumu kufanya hivyo utaiingizwa kwenye hatua nyingine kubwa ya mahusiano na mawasiliano kati yako na Mungu na kusikia akisema nawe kwa njia hii.

Naam mpenzi msomaji leo naishia hapa, katika mfululizo ujao nitaendelea na njia nyingine, neema ya BWANA wetu Yesu Kristo iwe nawe. Somo litaendelea…

 

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, unastahili BWANA wangu.

‘… Utaiinua misingi ya vizazi vingi’

USIKATE TAMAA

September 10, 2016

Na: Patrick na Flora Sanga

1

Shalom, katika kufundisha ujumbe huu andiko letu kuu la somo ni 1 Samweli 30:1-20. Hii ni habari ya Daudi ambayo inaeleza namna ambavyo Daudi akiwa ameenda vitani, adui zake walikuja wakateka familia na mali zao walizoziacha na kuondoka navyo. Hivyo Daudi aliporejea kutoka vitani na askari wake mia sita ndipo akakuta mji wao umechomwa moto na familia zao wote wametekwa.

Licha ya wanaume hao kulia hadi kuishiwa nguvu, Biblia inasema kwenye inasema hivi Naye Daudi akafadhaika sana; kwa sababu watu walikuwa wakisema kwamba apigwe kwa mawe, kwa maana nafsi za hao watu wote walisononeka, kila mtu kwa ajili ya wanawe na binti zake; lakini Daudi alijitia nguvu katika Bwana, Mungu wake’ (1 Samweli 30:6).

Hadi leo Shetani hutumia roho ya kukatisha tamaa kuwafanya waamini wengi kushindwa kufikia tamati ambayo Mungu ameikusudia kwenye kila eneo la maisha yao. Kumbuka roho ya kukata tamaa inafanya kazi kwa karibu na roho ya hofu. Roho ya hofu na kukatisha tamaa huelekezwa kwa mtu ambaye anatia bidii au amedhamiria kufanya na kufikia hatua hatua kubwa mbeleni.

Katika kuachilia roho ya kukata tamaa zipo njia nyingi ambazo adui hutumia, mojawapo ikiwa ni kutumia maneno ambao ndio mkakati wake mkubwa. Sambamba na maneno, adui hutumia na vitendo pia kuhakikisha anatimiza dhamira yake. Kumbuka lengo la Shetani kuleta roho ya kukatisha tamaa si tu kukufanya ushindwe kufikia malengo bali zaidi ni kukufarakanisha na Mungu ili uone kwamba ahadi zake si za kweli na wala si mwaminifu.

4

Katika kitabu cha 2 Samweli 17:1-2 Biblia inasema Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu; nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, NAMI NITAMTIA HOFU; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake’. Mpenzi msomaji, hivi ndivyo adui anavyowaza hata leo juu ya watoto wa Mungu katika kuhakikisha anawakatisha tamaa na kuwavunja mioyo yao, naam unapaswa kuwa makini na silaha hii ya giza ya maneno.

Hebu tuone mifano kadhaa ndani ya Biblia;

 • Kukatishwa tamaa kwa Jairo wakati anamuomba Yesu amponye mwananwe mgonjwa (Rejea Marko 5:22-23, 35-36). Mstari wa 35 na 36 inasema ‘Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu’.
 • Kukatishwa tamaa kwa Nehemia wakati ameamua kuujenga ukuta uliobomoka (Rejea Nehemia 2:19, 4:1-3, 7-8). Kwenye ile Nehemia 4:1-3 imeandikwa ‘Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto? Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe’.

Je unaona nguvu ya maneno katika kukatisha tamaa. Naam kila unapopiga hatua ya kutaka kufanikiwa na kufikia hatua nyingine, Shetani naye anaandaa jeshi la kukukatisha tamaa usifikie malengo yaliyokusudiwa. Hata sasa Shetani yuko kazini akitumia roho ya hofu kukatisha watu wengi tamaa wasipige hatua. Ndiyo maana ujumbe huu unakuja kwako kukuhakikishia kwamba huna sababu ya kukata tamaa.

Kwa nini usikate tamaa?

3

Ukweli zipo sababu nyingi ndani ya Biblia lakini kwa mtazamo wangu sababu kubwa inayozibeba zote ni hii Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, KWA SABABU YEYE ALIYE NDANI YENU NI MKUU KULIKO YEYE ALIYE KATIKA DUNIA (1 Yohana 4:4). Haleluya, ukiijua kweli hii na maadam unaenenda kwa uaminifu mbele za Mungu HAKUNA sababu ya kukata tamaa kwa sababu aliye NDANI yako ambaye ni Mkuu (mweza wa yote) anasema;

 • Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu (Isaya 41:10)
 • Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza (Isaya 43:2).
 • Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana (Isaya 54:17).
 • Tazama, mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza? (Yeremia 32:27)

5

Mfalme Daudi naye kwa kuthibitisha kweli hii anatuambia ‘nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji (Zaburi 23:4). Mtume PAULO anakazia kwa kusema Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu’ (Wafilipi 4:13). Tena zaidi ya yote BWANA Wetu Yesu anasema ‘… MIMI NIPO PAMOJA NANYI SIKU ZOTE, HATA UKAMILIFU WA DAHARI’.

Naam tukirejea kwenye andiko letu la somo, tunaona kwamba Mfalme Daudi licha ya kukatishwa tamaa si tu na adui zake bali hata askari na rafiki zake hakukubali kukata tamaa, bali BWANA ambaye Daudi alimtegemea, alimtia nguvu mpya hata maandiko yanasema ‘Naye Daudi akawapiga tangu ukungu wa jioni hata jioni ya siku ya pili; hakuna aliyeokoka, ila vijana mia nne waliopanda ngamia na kukimbia. Wala hawakupotewa na kitu, mdogo wala mkubwa, wana wala binti, nyara wala cho chote walichojitwalia hao; Daudi akavirudisha vyote’ (1 Samweli 30:17&19).

Mpenzi msomaji tunaamini ujumbe huu umekuongezea imani ndani yako, NAAM USIKATE TAMAA MTETEZI WETU YU HAI, NI MUNGU MWENYE NGUVU TENA MSHAURI WA AJABU, mpe leo nafasi akusaidie.

…Utaiinua misingi ya vizazi vingi… (Isaya 58:12)

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, Wastahili BWANA wetu

JIHADHARI USIANGUKE TENA ILI USITENGWE NA MUNGU

September 8, 2016

Na: Patrick & Bernada Sanga

1

Shalom, neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Kwa mwanangu Bernada Sanga ambaye BWANA alipokuwa akinifundisha ujumbe huu alimtumia binti huyu na ndio maana ninatambua ushiriki wake katika kukamilisha ujumbe huu, naam fuatana nami tuendelee…

Katika waraka huu wa mwezi Septemba 2016 imenilazimu kuandika ujumbe huu muhimu ambao lengo lake ni (a) kuwasaidia viongozi kutimiza majukumu ya nafasi zao ipasavyo ili wasipatwe na anguko (kutengwa) na Mungu (b) kuwapa ufahamu wa kweli hii viongozi ili wasije wakarudia au kufanya makosa yatakayopelekea anguko lao kutokana na nafasi zao kwenye ulimwengu wa roho na mwili pia.

Katika ujumbe huu anguko lina maana ya kutengwa na kusudi la Mungu kunakosababishwa na mwanadamu kukosa utiifu. Naam, anayehusika kutenga ni Mungu mwenyewe kwa sababu ya uasi au kukosa utii kwa mwanadamu na hivyo kupelekea Mungu kuamua KUTOENDELEA tena na mtu huyo katika kulitekeleza kusudi lake hapa duniani.

Hebu na tuangalie mifano kadhaa kutoka kwenye Biblia kuhusu jambo hili:

 • Anguko la Adam (Mwanzo 3:9-24), mstari wa 23 unasema kwa hiyo Bwana Mungu AKAMTOA katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. Kutoa hapa lina maana ya kumfukuza kutoka kwenye eneo ambalo kimsingi alikusudiwa kuwepo.
 • Anguko la Musa (Hesabu 20:2-12), ule mstari wa 12 unasema ‘Bwana akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, HAMTAWAINGIZA kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa’. Naam si tu kina Musa walitengwa na kusudi husika, bali pia walipoteza heshima ya kuwa sehemu ya utekelezaji wa kusudi la Mungu kamili.
 • Anguko la Sauli (1 Samweli 15:10-26, 16:1), naam ule mstari wa 26 unasema, Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, BWANA NAYE AMEKUKATAA WEWE, USIWE MFALME WA ISRAELI. Na kisha Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi NIMEMKATAA asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe (1Samweli 16:1).
 • Anguko la familia ya Eli (1 Samweli 2:27-33), ule mstari wa 30 unasema ‘Kwa sababu hiyo, Bwana, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa Bwana asema, JAMBO HILI NA LIWE MBALI NAMI; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa si kitu’.

3

MAMBO MUHIMU KUJUA YATAKAYOKUSAIDIA USIANGUKE NA HIVYO KUTENGWA NA KUSUDI LA MUNGU KAMA WALIOTUTANGULIA

 • Maelekezo mahususi (specific instrunctions) kutoka kwa Mungu ndiyo msingi wa mafanikio au anguko kwa mwamini (kiongozi). Maelekezo hayo hutolewa kwa kuzingatia nafasi aliyo nayo mtu katika ulimwengu wa roho na mwili pia. Na kwa maana hiyo anguko nalo linategemea nafasi aliyo nayo mtu katika ulimwengu wa roho na wa mwili pia.
 • Maagizo mahususi yamefungwa kwenye muda wa kila kusudi, hivyo kukosa utiifu ni kuchelewesha au kukwamisha kusudi hilo kwa muda ulioamriwa.
 • Maelekezo mahususi yameunganishwa na heshima au utukufu kwa Mungu. Yanapotekelezwa ipasavyo jina la Mungu linatukuzwa, yasipotekelewa ipasavyo yanatoa fursa kwa adui za Mungu kukufuru na jina lake kuchafuliwa (Hesabu 20:12, 1 Samweli 2:17, 29-30).
 • Hivyo Jifunze kuwa makini na maelekezo unayopewa na Mungu kwa kuzingatia nafasi yako na muda wa maelekezo hayo kutekelezwa.
 • Kutoka kwenye nafasi yako, jihadari usije ukafanya maamuzi au kuruhusu mazingira yatakayopelekea dharau kwenye jina la BWANA.

Kumbuka kwamba ishara mojawapo ya anguko ni kifo, naam kifo hapa ni kwa namna mbili, kifo cha kiroho ambacho kinazuia ufunuo wa Mungu uliokuwa ukileta maelekezo mahususi juu yako (1Samweli 3:1) na pili ni kifo cha kibinadamu kabisa  (1Samweli 2:34, 2Samweli 3:33).

3

Anguko lako si tu litakugharimu wewe binafsi bali zaidi huduma yako, familia yako na vizazi vijavyo, hivyo kuwa makini na maelekezo mahsusi yanayoendana na wito na nafasi yako, naam jihadhiri usianguke kwa kukosa utiifu ili usitengwe na Mungu na kupoteza heshima ambayo amekupa kupitia nafasi ulizonazo, heshima ya jina lake kutukuzwa hapa duniani kupitia wewe.

‘… Utaiinua misingi ya vizazi vingi’.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu wastahili Bwana wangu.