MAMBO MUHIMU KUJUA NA KUFANYA KATIKA KUUKABILI MWAKA 2014

1

Na: Patrick Sanga 

Heri ya mwaka mpya wa 2014 mpenzi msomaji, ni furaha iliyoje kuuona mwaka mwingine kwa pamoja.

Katika kitabu cha Mhubiri 3:1 imeandikwa ‘kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu’. Tafadhali soma na hili pia katika kitabu cha   1 Wakorinto 2:9 -10 linalosema “Lakini, kama ilivyoandikwa, mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchungza yote, hata mafumbo ya Mungu”.

Mhubiri kupitia andiko lake anatupa kuelewa kwamba kila mwaka mpya huwa una mambo yake ambayo hyanana budi kutokea. Zaidi maelezo ya Mtume Paulo yanatufanya tujue kwamba katika mwaka 2014 kuna mambo mazuri ambayo Mungu amewandalia watoto wake na kwa njia ya Roho Mtakatifu tunao uwezo wa kutambua nini kinakuja kwenye kila eneo la maisha yetu hata kabla hatujauingia mwaka husika. Ndio, katika mwaka 2014 kila ufalme yaani ufalme wa Mungu na ule wa Shetani kuna mambo umeyaandaa/kusudia kwa ajili yako kifamilia, ndoa, kazi, huduma, masomo, biashara, kanisa lako, taifa lako. Ni dhahiri kwamba Mungu amekusudia mema kwa ajili yako na Shetani amekusudia mabaya juu yako.

Je, unakumbuka matukio ya mwaka 2013 kwako binafsi, kifamilia, kikanisa, Kitaifa na dunia kwa ujumla?   Je, unajua katika ulimwengu wa roho matukio hayo yameacha au kuzaa kitu gani? Naam chukua muda yatafakari kibiblia na kisha jiulize laiti ungejua kabla hujaingia mwaka 2013, kwamba hayo yaliyotokea yatatokea ungechukua hatua gani?

Kumbuka lolote unaloliona katika ulimwengu wa mwili linatokea ujue, lilishatokea kwenye ulimwengu wa roho kwanza. Naam kwenye ulimwengu wa roho, ndipo una fursa ya kuona mambo yanayoenda kutokea duniani, kabla hayajatokea. Ni katika ulimwengu wa roho ndipo unaweza (a) kupambana ili kuhaikisha jema ambalo Mungu amekusudia linatimia (b) kuzuia lolote baya ambalo Shetani amekusudia juu yako, famila nk katika ulimwengu huu wa mwili.

Kutokana na umuhimu wa kuwa na ufahamu wa nini kinakuja siku za usoni yaani mwaka 2014, imenilazimu kuandaa ujumbe huu ili ukusaidie kujua angalau kwa sehemu 2014 ni mwaka wa namna gani na ndani yake kuna nini? Hii itakusaidia sana kujua ufanye nini ili kushirikiana na kuyakabili yale yanayokuja.

Kila mwaka, ndani yake kuna mambo ambayo ni LAZIMA yafanyike au yatime kulingana na nyakati ambazo zimeamriwa juu yako na Taifa pia (Rejea Mhubiri 3:1). Kwa mwaka 2014 yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu ambayo ambayo Mungu amekusudia ndani yake kwa ajili yetu;

 • Ni mwaka wa kucheka kwa kuwa BWANA anaenda kuwafurahisha watu wake

Ayubu 42:10 ‘Kisha BWANA akageuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; BWANA naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza’.  Ukisoma kitabu cha Ayubu sura 1-2 utaona habari za Ayubu na jinsi Shetani alivyoharibu maisha yake kwa ujumla. Kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa Ayubu, hata hivyo hizo ndio nyakati zilizokuwa zimeruhusiwa juu yake. Maandiko yanaonyesha kuwa baada ya Ayubu kusimama vizuri na Mungu wake katika kipindi husika, BWANA alimrejeshea Ayubu maradufu kila kilichokuwa kimeharibiwa na Shetani yaani furaha, afya, watoto na mali zake zote.

Vivyo hivyo katika mwaka 2014 BWANA amekusudia kutimiza ahadi nyingi kwa watu wake, kile kilichoharibiwa kitarejeshwa, haki zilizopotea zinaenda kurejeshwa, BWANA anaenda kurejesha uzima katika mwili wako nk. Kama ni familia yako, ndoa yako, huduma yako, kazi yako nk Shetani aliharibu na kutekwa, uwe na uhakika BWANA Yesu anaenda kuponya na kurejesha uhai tena.

 • Ni mwaka wa amani utakaokupa fursa ya kujijenga na kutimiliza mapenzi ya Mungu kwa mwaka husika

  1 Waflme 5: 3-6, ukisoma ule mstari wa nne hadi tano Biblia inasema ‘Ila leo BWANA, Mungu wangu, amenipa amani kila upande, hakuna adui wala tukio baya. Nami tazama, nakusudia kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wangu, kama BWANA alivyomwambia Daudi baba yangu, akisema, Mwana wako, nitakayemweka katika kiti chake cha enzi mahali pako, ndiye atayeijenga nyumba kwa jina langu’.

  Maneno haya yalisemwa na Sulemani baada ya kutawazwa kuwa mfalme kufuatia kifo cha baba yake Daudi. Ukisoma Biblia yako vema utagundua kwamba utawala wa Daudi ulikuwa na vita sana, na kwa sababu ya vita na damu nyingi iliyomwagika katika kipindi chake BWANA alimzuia Daudi asimjengee Hakalu. Hekalu lilijengwa kipindi cha mwanawe Sulemani.  Naam ili Sulemani aweze kujenga hekalu vema, BWANA akampa amani pande zote na kazuia baya lolote lisitokee.

  Vivyo hivyo Mungu anaenda kuleta amani juu yako kila upande katika mwaka 2014 ili utumie fursa si kujijenga wewe binafsi bali kuujenga ufalme wake kwa mwaka husika kwa kutimiza yale anataka kufanya juu ya Taifa, Kanisa, familia, ndoa kupitia wewe. Hii haina maana kwamba Shetani hajapanga mabaya, tunafahamu kwamba yeye ni baba wa uongo, lengo lake kubwa ni kuiba, kuchinja na kuharibu.

  Amini kwamba kabla Shetani hajatekeleza mipango yake BWANA ataizuia na kupigana kwa ajili yako ili kutoathiri kusudi lake kupitia wewe kama alivyofanya  siku za Mfalme Yehoshafati, aliposema “Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa BWANA ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao, kwa BWANA yu pamoja nanyi” (2Nyakati 20:1-25), naam hivi ndivyo BWANA anavyoenda kuwashindia watoto wake katika mwaka huu.

Hakika huu ni mwaka wako wa kujijenga kiuchumi, kibiashara, kifamilia, kikazi, kwa kilimo nk. Ndio BWANA anaenda kuruhusu majira mazuri juu ya nchi yetu na kuzuia kila uharibifu uliokusudiwa juu yetu.

 • Ni mwaka wa kuwekeza na kukusanya (kuweka akiba) kwa kuwa kuna mabadiliko ya kiuchumi yanakuja

  Biblia katika kitabu cha Mwanzo 41:35-36 inasema ‘Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mikononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa’. Maelezo haya ya Yusufu ni matokeo ya fasili ya ndoto ya Farao kiongozi wa Misri.  Baada ya kupata tafsiri yake ilibidi Taifa la Misri watumie miaka saba ya mwanzo kukusanya chakula kwa ajili ya miaka mingine saba ya njaa iliyokuwa inakuja mbele yao.

  Usiogope, binafsi, sikuelezi kwamba pia katika Taifa letu kuna miaka saba ya njaa inakuja. Hata hivyo jambo ambalo nina uhakika linaenda kutokea ni mabadiliko muhimu ya kiuchumi si tu wa nchi yetu bali dunia nzima kuanzia mwaka 2015 ambayo yataleta athari si tu kwa uchumi wa Taifa bali mpaka mtu mmoja mmoja. Mabadiliko hayo kama yatakukuta haujajipanga vizuri kwa kuwekeza katika sekta na nyanja mbalimbali za kiuchumi itakugharimu sana. Naam mabadiliko haya yatakayoanza mwaka 2015 yaatakuwa mazuri kwa wale waliojiandaa kuyakabili, na si vinginevyo (asomaye na afahamu).

  Hivyo nikushauri katika mwaka 2014 fanya kila jitihada kuwekeza fedha, muda na nguvu katika kuimarisha biashara zako, kazi zako, mifugo na zaidi kuongeza vyanzo vingine vya mapato. Naam tia bidii sana katika kila utakalofanya kwa mwaka 2014 ukimtanguliza Mungu. Katika Kumbukumbu la Torati 8:18 imeandikwa ‘Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, mana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake hata hivi leo’. Hivyo tarajia kupata mawazo mapya na yaliyo bora zaidi yatakayokusaidia kupata utajiri katika mwaka 2014 kutoka kwa BWANA Yesu, naam tegemea akili zako kutakaswa na hivyo kuwa na mawazo ya ubunifu na ufumbuzi zaidi katika mwaka 2014 yatakayopelekea kukubalika na kuinuliwa kwako zaidi kushinda wengine kazini kwako.

  Kama una mradi wako yaani duka au biashara yoyote usiridhike nayo ipanue zaidi au kuongeza nyingine mpya, naam chukua hata mkopo upanue wigo wako ni muhimu sana kwa kule tunakokwenda.  Sambamba na hayo anza sasa kuweka akiba ya fedha (endapo hufanyi hivyo) ambayo ni muhimu sana kwa huko tunakokwenda, ni muhimu sana ukaweka akiba yako kwenye mifuko mbalimbali ya kutunza akiba ya kijamii au ukawa na akaunti maalum kwa ajili ya akiba.

Mpenzi msomaji sijajua kama una ufahamu kiasi gani juu ya namna ambavyo Mungu huwa anasema kuhusu mambo yanayokuja siku za usoni. Nataka ufahamu kwamba mambo matatu niliyokueleza hapo juu ndio mawazo ya Mungu kuhusu watu wake kwa mwaka 2014. Naam daima mawazo ya Mungu ni mawazo ya amani (Yeremia 29:11), haya ambayo amesema nawe kuhusu 2014 unapaswa kuhakikisha unayafuatilia mpaka yatimie juu yako na Taifa letu pia. Namna mojawapo ya kuhakikisha haya yanatimia ni kujiwekea malengo ambayo yatatoa fursa kwa imani yako kuwa na mahali pa rejea kadri unavyozidi kuukabili mwaka 2014.

Biblia katika kitabu cha Waebrania 12:1 inasema ‘Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana’. Ni muhimu sana ukajiwekea utaratibu wa kuwa na malengo ili yakusaidie kujua hatua zilizoko mbele yako ambazo unapaswa kuzifikia. Naam si suala tu la kuweka malengo bali kuyaweka kwa kuzingatia kile kinachokuja katika mwaka 2014. Natambua liko kundi kubwa la watu ambao wanaweza kuwa walishaweka malengo yao hata hivyo bado una fursa ya kuyaboresha (adjust) kwa kuzingatia hiki ambacho umejifunza katika ujumbe huu. Malengo yako yatakusaidia kujua hatua unazopiga endapo zinakufikisha kule ambako Mungu anataka ufike katika mwaka 2014.

Maandiko yanasema katika Isaya 60: 1 ‘Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa BWANA umekuzukia’. Ukisoma msatri huu katika toleo la kiingereza la ESV unasema Arise, shine, for your light has come, and the glory of the LORD has risen upon you’ (Isaiah 60:1). Neno ondoka ambalo kwa kiingereza ni ‘arise’ kwa fasiri ya diktionari ya kiebrania na kigiriki lina maana ya timiliza (accomplish), maliza (complete), fikia lengo (achieve) au fanikiwa (succeed).

Kwa tafsiri hii ina maana kwamba, Mungu anayo mambo (mipango) ambayo katika mwaka 2014 anataka ufanikiwe katika kuyatimiliza na kuyafikia. Naam na ili uweze kuyafikiwa yeye anaenda kukulinda kwa kufanyika ukuta wa moto utakaokuzunguka pande zote sawasawa na Zekaria 2:5 ‘Kwa maana mimi, asema BWANA, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa huo utukufu ndani yake’.  

Zaidi katika Mitahli 8:17 imeandikwa ‘Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona’. Ni imani yangu kama (a) ukidumu katika kumpenda Mungu kwa kuzishika amri zake (b) ukadumu katika kumtafuta (c) ukasimama vema kwenye nafasi yako kama mlinzi basi uwe na uhakika haya ambayo leo Mungu ameyafunua kwako kuhusu mwaka 2014 yatakuwa dhahiri na mwaka huu utakuwa wa baraka za pekee kuliko yote iliyotangulia.

Nimeona vema kusisitiza jambo hili kwani imeandikwa ‘wakati wasemapo kuna amani ndipo uharibifu uwajiapo’.  Hivyo ni muhimu sana ukazingatia kumpenda Mungu na kuwa makini na maisha yako kwa kila hatua ili kutumia vizuri mazingira bora ambayo Mungu anaenda kuyaruhusu kwako katika mwaka wa 2014.  

2

Heri ya mwaka mpya wa 2014

Utukufu na heshima vina wewe Yesu! Wastahili BWANA.

 

Advertisements

18 comments

  • Ahsante Tumaini, kazana kuniombea kama nilivyosema kuna masomo mengi ambayo Mungu ameweka ndani yangu hakika kwa neema yake kupitia maombi yenu, nitaweza kuyaandika kwa wakati na kuyaweka kwenye blogu hii kwa wakati.

   Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s