Archive for December 2013

NAMNA MWANAMKE ANAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI ZAKE KUBADILISHA MAISHA YA NDOA YAKE (Sehemu ya mwisho)

December 29, 2013

1

Na: Patrick Sanga

Heri ya ‘Christmas’ na mwaka mpya wa 2014

Salaam nyingi kupitia jina la BWANA wetu Yesu Kristo.

Naomba nianze kwa kumshukuru Mungu ambaye leo ameniwezesha kukamilisha sehemu ya mwisho ya ujumbe huu muhimu kwa uponyaji wa ndoa za watoto wake. Kimsingi haikuwa kazi rahisi lakini kwa msaada na uongozi wake, ujumbe huu mrefu umekamilika. Katika kumalizia sehemu hii ya mwisho nitaandika mambo manne (4) ambayo mwanamke anapswa kuyazingatia ili kubadilisha maisha ya ndoa yake kwa kutumia nafasi zake ambazo ni; mwanamke kama msaidizi, mshauri, mjenzi, mlinzi na mleta kibali. Mambo hayo ni pamoja na:

 • Ndoa ni wito wa mapungufu

Mama mmoja ambaye ndoa yake ilikuwa inasumbua alinitafuta na kuniambia, Mtumishi, changamoto za ndoa yangu ni kubwa kiasi kwamba sasa ni majuto tu, sina raha kabisa hata kidogo, nimekuwa mtu wa kuumizwa na kulia kila siku kwa sababu ya ndoa yangu, naomba msaada wako. Nilimsikiliza kwa kirefu katika yote aliyonieleza kwa upana wake.

Ukweli ni kwamba mpaka leo mama huyu simfahamu hata kwa sura, lakini BWANA alinijulisha kwamba ndani yake kuna huduma kubwa, ambayo Shetani anapamba nayo kupitia mumewe. Nilipojua nafasi ya huyu mama si tu kwa muewe bali kwa mwili wa Kristo kwa ujumla ilibidi kulipa kipaumbele suala lake mpaka Mungu aingile kati. Kwa kifupi nilianza taratibu kumfundisha jambo hili, nikamuonyesha nafasi zake na namna ya kuzitumia, naam naye akaweka kwenye matendo na sasa ndoa yake, BWANA ameiponya, wanaendelea vizuri kifamilia na kihuduma pia.

Jambo ambalo nimejifunza kupitia baadhi ya wanandoa ni kwamba, ndoa ni wito wa mapungufu. Unapoingia kwenye ndoa tegemea kukutana na changamoto kadhaa kutoka mwenza wako na hivyo kuwa tayari kuzikabili na kuvumilia. Kuna mapungufu ambayo yataisha kabisa kadri unavyoendelea kukaa kwenye nafasi zako na pia yapo ambayo hayataondoka kabisa kwa kuwa hayo ndiyo sababu ya wewe kuunganishwa na mwenzi wako, na Mungu aliona katika wanawake wengi wewe ndiye unayeweza kuchukuliana na kumsaidia katika mapungufu yake.

Wapo akina mama ambao wanatamani sana waume zao wabadilike tabia zao na zifanane na za kwao kabisa, napenda kukuambia kwamba hilo haliwezekani.  Naam, ile kwamba wewe ni mwanamke na yeye ni mwanaume ni dhahiri kwamba kuna vitu hamuwezi kufanana. Licha ya tofuti za kijinsia, malezi ambayo kila mmoja amepata kwenye famila yake, hitoria zenu, tofauti ya elimu zenu, vipato vyenu, umri wenu n.k. ni dhahiri kwamba mapungufu yatakuwa ni sehemu ya maisha kwenu. Sharti mjifunze kuchukuliana na kusameheana katika madhaifu na mapungufu hayo.

 • Tumia muda mwingi kuomba na si kuongea (Mithali 10:19,17:27, 18:21)

Maneno ni moja ya vyanzo vikubwa vinavyochangia kuharibu ndoa nyingi leo. Biblia katika kitabu cha Mitahli 10:19 inasema ‘Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili’. Wapo baadhi ya akina mama ambao kueleza wengine mambo ya ndoa yao ni kawaida yao. Jambo baya zaidi ni kwamba wanawasema waume zao vibaya hata kwa watu ambao hawakustahili kuelezwa hayo. Kumbuka imeandikwa pia ‘Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi, Na wao waupendao watakula matunda yake’ (Mithali 18:21)

Je unatumia muda kiasi gani kuomba kwa ajili ya mumeo? Na unatumia muda kiasi gani kuzungumza na watu wengine kwa siku? Naam nakushauri jifunze kutumia muda mwingi kuomba kwa ajili ya ndoa yako na kwa hakika BWANA Mungu atakufunulia mambo mengi sana kwa habari ya nyumba yako.

Biblia katika kitabu cha Ayubu 13:5 inasema “Laiti mngenyamaza kabisa, hilo lingekuwa hekima kwenu’. Sikia mwanamke, licha ya matendo, hekima kwa sehemu kubwa inadhihirika kwa njia ya kinywa, naam kunyamaza ni bora kuliko kunena, na hasa unapokuwa na hasira, chunga sana usinene maana hekima haifanyi kazi na hasira bali upole.

Katika Mithali 17:27) imeandikwa “azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; Na mwenye roho ya utulivu ana busara”. Hivyo nakushauri tumia muda wako mwingi kuomba kwa jili ya ndoa yako na si kuongea mambo yasiyojenga, ukijua kwamba maneno ni moja ya silaha kubwa ambayo Shetani anatumia kubomoa ndoa nying sana hata leo.

 • Usiwaze mabaya juu ya mume wako

  Nilipotembelea mkoa fulani kikazi, baba mmoja aliniomba nikazungumze na mke wake, ambaye aliamua kuondoka nyumbani kwa zaidi ya miezi sita na kwenda kuishi kwa wazazi wake. Baada ya kuzungumza na huyu baba kwa upana nilikubali na kisha nikapanga muda wa kuonana na mke wake. Tulipoonana alinieleza kile kilichomuumiza na kumpelekea kuondoka kwa mumewe. Katika kuzungumza kuna wakati yule mama alisema ‘natamani huyu mwanaume angekufa kabisa’.

  Binafsi nilifikiri amekosea nikamuuliza umesemaje? Akarudia tena kusema natamani afe naamini nitapata amani zaidi kwa maisha yangu yaliyosalia. Nilipomuuliza kwa nini unafikiri afe? akajibu yeye si mtu sahihi aliyepaswa kunioa, kwani walikuja wengi sana, kunichumbia, sijui kwa nini nilimkubali huyu na ndio maana leo naumia hivi.

  Nami nikamwoji je unajua athari ya hayo unayosema? Hujui kwamba akifa nje ya muda na mapenzi ya Mungu, damu yake itadaiwa mikononi mwako?  Kuwaza hivyo ni kukosea sana, tayari mlishafunga ndoa, na sasa unapaswa kufikiri namna ya kubadilisha maisha ya ndoa yako kuwa kwenye hali bora zaidi na si kuendelea kubomoa. Ndipo nikamwambia ‘kama hutazijua na kuzitumia nafasi ulizopewa na Mungu, kamwe amani haiwezi kuja kwenye ndoa yako’. Ilichukua miezi yule mama kuelewa na kurejea kwenye nafasi zake, lakini ashukuriwe Mungu naye alifanyia kazi na sasa amerudi kwa mumewe wanaendelea vema.

Sikia mwanamke unayesoma ujumbe huu, madaam ulikubali kuolewa, usimpe ibilisi nafasi kwa kuwaza mabaya juu ya mume wako, ukihoji, kwa nini nilikubali kuolewa na huyu baba, au kusema najuta kuolewa na huyu baba, au laiti wangekuwa wanabadilisha wanaume ningebadilisha haraka wa kwangu nk. Kumbuka kutengemaa kwa ndoa yako ni kufanikiwa kwa makusudi ya ufalme wa Mungu hapa duniani. Changamoto mnazozipitia kama wanandoa lengo lake ni kuwatoa kwenye nafasi yenu ya kufanya kile chenye kuujenga ufalme wa Mungu.

Hivyo haijalishi mume wako kakosea nini, wewe mtwike Mungu fadhaa zako zote, na uwe tayari kusamehe na kusahau, wala usiawaze mabaya juu yake, kwa kuwa kadri unavyowaza mabaya ndivyo unavyoiingiza ndoa yako kwenye uharibifu, ndivyo unavyoyaumba na kuyaita mabaya zaidi yaje kwenye ndoa.

 • Nafasi yako ni ya thamani sana kwa mumeo

  Katika kusoma kwangu Biblia na kufuatilia sana kuhusu nafasi ambazo Mungu amempa mwanamke, nimegundua kwamba nafasi ya mke kwa mume ni ya muhimu sana. Pengine kwa kiasi fulani inafanana na nafasi ya Kristo kwa kanisa, maana ikiwa katika ulimwengu wa roho mwanamke amepewa kuwa Msaidizi, Mshauri, Mlinzi, Mjenzi na Mleta kibali, je haya si sehemu tu ya majukumu ambayo Yesu anayo kwa kanisa lake kwa ujumla?

  Nafasi ulizopewa na Mungu katika ulimwengu wa roho, ni ishara kwamba kufanikiwa kwa kusudi la Mungu kupitia ndoa yenu kunategemea sana namna ambavyo mwanamke anazitumia nafasi zake. Naam zaidi kukubalika, kustawi na kufanikiwa kila mume wako atendalo kunategemea pia namna ambavyo wewe (mke) utazitumia nafasi zako. Hivyo kuchelea kwako kutumia vizuri nafasi zako ni kukwamisha kusudi la Mungu kwenye ndoa yako, familia yako, jamii yako na taifa lako.

Ukweli ni kwamba ‘Mume wako anakuhitaji sana hata kama maneno na matendo yake hayaonyeshi kwamba anakuhitaji”. Naam, mumeo anakuhitaji kuliko unavyofikiri, kadri wewe unavyokaa kwenye nafasi yako ndivyo unavyosaidia familia yako, kijiji chako, kanisa lako na taifa lako. Naam mume wako anahitaji sana upendo wako,kumbuka upendo ndio uliomsukuma Kristo aje afe kwa ajili yetu (Yohana 3:16), ingawa hata leo wapo watu wasiomwamini, wenye kumtukana lakini yeye bado anawapenda.  Upendo wa Kristo ndani yako ukukumbushe kusimama kwenye nafasi zako kwa ajili ya mumeo.

Naam bado ningeweza kuandika mambo mengine mengi zaidi, lakini fahamu jambo hili,  laiti mwanamke akisimama na kuzitumia nafasi zake vema, mabadiliko na uponyaji mkubwa kwenye ndoa yake ni matokeo halisi ya kutarajia. Nafasi hizi tano zinampa fursa mwanamke ya kuruhusu mawazo ya Mungu kupitia ndoa yake kutimia na kuzuia mawazo ya Ibilisi kupitia ndoa yake yasitimie. Naam nafasi ya mwanamke katika ndoa ndiyo inayoamua uzima au mauti ya ndoa yake, nafasi ndizo zinazoamua kufanikiwa au kufeli kwa ndoa yake.

Hivyo endapo utayaweka mafundisho haya kuanzia sehemu ya kwanza kwenye matendo si tu ndoa yako itaponywa, bali, maombi yenu yatasikilizwa, mume wako atapata kibali mbele za BWANA, naam atakuwa mume bora katika jamii na kufanikiwa katika kila atendalo. Mahusiano na mawasiliano mazuri yatakuwa sehemu ya maisha yenu na hivyo kurahisisha kutekelezwa kwa kusudi la Mungu. Ninapomalizia ujumbe huu muhimu nakushauri usijitazame kama mwanamke wa kawaida bali jifunze kujitazama kutoka kwenye nafasi zako kama Msaidizi, Mshauri, Mlinzi, Mjenzi na Mleta kibali, naam na maisha ya ndoa yako yatabadilika.

Mungu wangu akubariki na kuiponya kabisa ndoa yako, kupitia damu na jina la Yesu, amen.

 

Utukufu na heshima vina wewe Yesu! Wastahili BWANA wangu.