Archive for December 2012

SALAMU ZA MWAKA MPYA WA 2013

December 31, 2012

Na: Patrick Sanga

Sanga

 

Bwana Yesu asifiwe sana mpenzi msomaji.

Ni furaha na neema iliyoje kwa Mungu wetu kutupa tena fursa ya kuwasiliana katika siku hii ya leo ya kumalizia mwaka wa 2012. Mimi pamoja na familia yangu tunamshukuru sana Mungu kwa uzima na afya njema aliyotujalia katika mwaka mzima wa 2012.

Naam kwa kifupi nimeona ni vema nikaandika ukurasa huu kwa ajili ya kueleza/kufafanua mambo kadhaa kuhusu blog hii katika tarehe hii.

Mosi, kwa namna ya pekee namshukuru sana Mungu kwa neema yake aliyonijalia na kunifanya kuwa mmoja wapo wa Waandishi wenye elimu ya ufalme wa mbinguni. Naam ahsante sana Yesu kwa masomo yote ambayo uliniwezesha kuyaandika katika mwaka mwaka wa 2012.

Pili, natumia fursa hii kukushukuru wewe Mpenzi msomaji wangu kwa namna ambavyo umesimama nami kwa mwaka mzima wa 2012. Kwa hakika namshukuru sana Mungu kwa ajili yako na hasa kwa wewe ambaye licha ya kutenga muda wa kusoma mafundisho haya, ulitenga pia muda wa kuweka ‘comment’ zako kwenye masomo mbalimbali ya blog hii. Binafsi ninathamini sana muda uliotumia kusoma na kujifunza kupitia blog hii. Ukweli ni kwamba kadri wewe msomaji ulivyokuwa uki – ‘comment’ na kuonyesha kwamba masomo haya yamefanyika msaada kwako na wengine pia, ndivyo nami nilivyopata nguvu ya kuandika na kuandika na kuandika. Naam Mungu wangu akubariki sana.

Greetings

Tatu, katika mwaka wa 2012 kuna wasomaji kadhaa ambao waliomba niweze kuandaa masomo maalum na kuyaweka hapa au kuwatumia kwenye email zao. Pia lipo kundi jingine la wasomaji ambao waliuliza masawli mbalimbali ya kiroho. Nachukua fursa hii kuomba radhi kwa masomo na maswali ambayo sikuweza kuandika na kuyajibu ndani ya mwaka huu. Naam naendelea kuyafanyia kazi ni imani yangu kwamba sehemu kubwa ya masomo husika nitayakamilisha katika mwaka wa 2013.    

Pia katika mwaka 2012 kuna wasomaji wengi walitamani sana niwatumie masomo haya kwenye ‘email’ zao moja kwa moja. Kwa asilimia kubwa sikuweza kufanya hivyo kikwazo kikiwa ni muda. Naomba radhi pia kwa kushindwa kufanya hivyo, njia rahisi ambayo wewe msomaji unaweza kufanya ni kuji – ‘subscribe’ kwenye blog hii ili kila mara niwekapo ujumbe kwenye blog hii nawe upate moja kwa moja kwenye ‘email’ yako.

Nne, kipekee kabisa naomba kuwashukru “Christian bloggers’ wote ambao katika mwaka wa 2012 walioona vema kuweka masomo haya kwenye blog zao ili kuwafikia wasomaji wengi ambao hawaijui blog hii. Naam Mungu awabariki sana wapendwa kwa huduma hii. Jambo hili limepelekea kuwe na ongezeko kubwa sana la wasomaji wa blog hii kutoka katika nchi zaidi ya 80 duniani kote, hii ni kwa mujibu wa taarifa ya wordpress ya mwaka 2012.  

Nini kinakuja mwaka 2013 katika blog hii?

Katika kufanya kwangu tathmini ya mwaka huu, nimeangalia mapungufu yaliyojitokeza nami nitaboresha ili kuendelea kuujenga mwili wa Kristo. Hata hivyo ukweli si kazi rahisi kuandaa masomo kwa mfumo huu maana ni kazi inayohitaji muda wa kutosha wa maandalizi. Ahsante Yesu maana tayari ndani yangu kuna masomo mengi kwa ajili yako mpenzi msomaji kwa mwaka wa 2013. Maombi yako ni muhimu sana ili kila wazo la Mungu kupitia masomo haya lisitupite.  Kwa mara nyingine tena ahsante sana kwa namna ulivyokuwa pamoja nami katika mwaka wa 2012. Nakutakia heri ya Christmas na mwaka mpya wa 2013.

Mwandishi

Naam kwa heri mwaka wa 2012, karibu sana mwaka wa 2013, ndani yako tunatamka kumjua sana Mungu kupitia mafundisho ya neno la Mungu. Waandishi wenzangu ‘Maadam ni mchana na tuifanye kazi hii kwa bidii, maana kwa njia ya kalamu yako BWANA anaujenga mwili wake’.

Ahsante Yesu kwa fursa hii ya uandishi,

Utukufu na heshima vina wewe BWANA! Wastahili Yesu.