IJUE NA KUITUMIA NAFASI YAKO KAMA MLINZI KWENYE ULIMWENGU WA ROHO (Part 5)

Na: Patrick Sanga

Maada: Tafsiri ya kuwa Mlinzi katika ulimwengu wa roho

Katika sehemu ya nne tuliangalia baadhi yanafasi/maeneo yanayohitaji kuwa na mlinzi/walinzi katika ulimwengu wa roho. Ili kusoma sehemu ya nne bonyeza link hii
https://sanga.wordpress.com/2012/06/01/ijue-na-kuitumia-nafasi-yako-kama-mlinzi-kwenye-ulimwengu-wa-roho-part-4/

Yapo maswali mawili muhimu ambayo tukipata majibu yake yatatuongezea ufahamu mzuri zaidi wa masuala ya ulinzi katika ulimwengu wa roho. Maswali hayo ni, Je, Mungu anaposema nimekuweka kuwa mlinzi wa eneo fulani, maana yake nini? Na swali la pili ni Je mwanadamu anawezaje kujua kwamba amewekwa kuwa Mlinzi wa eneo fulani katika ulimwengu wa roho?

Katika sehemu hii ya tano tutaangalia swali kwanza linalosema, Mungu anaposema nimekuweka kuwa Mlinzi wa eneo fulani maana yake nini? Basi fuatana nami tuendelee;

Ni vizuri ukafahamu kwamba suala la kuweka walinzi katika maeneo mbalimbali ni utaratibu ambao Mungu amejiwekea mwenyewe ili kufanikisha makusudi yake hapa duniani kupitia mtu/watu. Na kwa sababu hiyo yeye hana namna ya kufanya kazi hapa duniani bila kumtumia mwanadamu katika nafasi hii ya ulinzi. Mungu anapokuweka kuwa Mlinzi katika ulimwengu wa roho tafsiri yake ni;

Moja – umewekwa kuwa kiongozi wa eneo lako la ulinzi

Kuwa Mlinzi wa eneo fulani katika ulimwengu wa roho maana yake ni kuwa kiongozi wa hilo eneo katika mambo au masula mbalimbali yanayohusiana na hilo eneo. Kwa dhana hii kiongozi ni yule afanyaye maamuzi kwa niaba ya watu wa eneo lake. Hii ni kwa sababu Mlinzi aliyekaa vema kwenye nafasi yake ndiye mwenye uwezo wa kuona jambo lolote linalotaka kuja kwenye eneo lake, na kwa kutumia nafasi yake ana uwezo wa kuruhusu litokee au kuzuia lisitokee. Na kama ni sharti litokee basi anayo fursa ya kuwaonya watu wake wajipange kukabiliana na jambo husika linalokuja.

Mbili – Umewekwa kuwa mwombaji wa eneo lako la ulinzi

Ukirejea Isaya 62:6 Biblia inasema ‘Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani’. Naam jambo hili liko wazi kwamba Mungu anapokuweka kuwa Mlinzi sharti ujue sababu za kuwa Mlinzi kwenye hilo eneo,   ni makusudi gani anataka kuyatimiliza kwenye hilo eneo lako nk. Ukishajua kazi yako kama Mlinzi ni kudumu kuomba, ili kuhakikisha yale ambayo Mungu anayo moyoni mwake juu ya eneo lako yanatimia bila kukwama.

Tatu – Umewekwa kuwa mwonyaji/mtoa taarifa wa eneo lako la ulinzi Biblia katika Ezekieli 33:7 inasema ‘Basi, wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli, basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu’. Siku zote taarifa inalenga kumpa mtu fursa ya kujiandaa kukabiliana na jambo linalokuja mbele yake. Mfano Ndoto, mara nyingi Mungu hutumia ndoto ili kuwaonya watoto wake juu ya mambo ambayo yanataka kuja juu yao.

Naam hata katika ulimwengu wa roho wewe mlinzi una nafasi kubwa ya kutoa taarifa za msingi kwa watu wa eneo lako ili kuhakikisha wanakuwa salama. Naam kadri Mungu anavyokupa taarifa za eneo lako nawe fanya hima kuzitoa kwa nyakati zilizoamriwa ili kufanikisha shauri la BWANA, ukikumbuka yeye anakutazama kama msemaji wake na mwonyaji wa watu wake kwenye eneo lako.

Ukisoma Yeremia 6:17 Biblia inasema ‘Nami naliweka walinzi juu yenu, wakisema, isikilizeni sauti ya tarumbeta; lakini walisema Hatutaki kusikiliza’. Walinzi hawa ambao BWANA aliwaweka walikuwa na jukumu la kuwaonya watu kusikiliza sauti ya tarumbeta na kuwapa watu tafsiri ya ujumbe wa tarumbeta husika. Kwa bahati mbaya wapewa taarifa wa eneo lao hawakutaka kusikiliza sauti yao, na ndio maana katika sehemu  ya tatu niliandika kwamba ni muhimu sana kuwe na mahusiano mazuri kati ya  Mlinzi na watu wa eneo lake/wapewa taarifa.

Naam kama Mlinzi ni muhimu sana kuwa makini na uhakika na taarifa unazozipata kutoka kwa Mungu kuhusu watu wa eneo lako. Hakikisha kwamba kweli zimetoka kwa Mungu na si mawazo yako au za Shetani. Ukishajua zifanyie kazi kwa kadri ya maelekezo unayoyapokea kutoka kwa Mungu. Ukiambiwa mwonye mtu fulani fanya hivyo bila kuogopa cheo chake, elimu yake nk. Kwa kutii kwako huenda utaikoa roho ya mtu huyo na uharibifu, naam hata asipotii damu yake haitadaiwa kwako bali itakiwa juu yake, lakini kutokutii ni kuharibu mahusiano yako na Mungu.

Nne – Umewekwa kuwa mshauri na rafiki wa Mungu kwenye eneo lako la ulinzi

Katika nafasi ambazo Mungu ametupa heshima ya pekee sana ni pamoja na hii ya kuwa Walinzi wa kusudi lake kwenye maeneo mbalimbali. Mlinzi katika ulimwengu wa roho ni mshauri wa Mungu wa masuala ya kiroho kwenye eneo lake. Naam kwa nafasi hii Mlinzi anaweza kwenda mbele za Mungu na kuzungumza naye juu ya kile ambacho anataka kifanyike au kisifanyike kwenye eneo lake au kwa watu wa eneo lake.

Hebu tujifunze kutoka kwa Musa jinsi  alivyoijua na kuitumia nafasi yake ulinzi vema. Biblia katika kitabu cha Kutoka 32:9 -14 inasema ‘Tena BWANA akamwambia Musa, mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu; Basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize; nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. Musa akamsihi sana BWANA, Mungu wake na kusema, BWANA kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu na kwa mkono wenye nguvu?… Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulionao juu ya watu wako. Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka na Israeli, watumishi wako, uliowaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni … Ukisoma ule mstari wa kumi na nne Biblia inasema ‘Na BWANA akaghairi ule uovu aliosema atawatenda watu wake’.

Ndugu yangu, kama wewe ni msomaji mzuri wa Biblia utakuwa unaijua habari hii. Kutokana na wana wa Israeli kujifanyia ndama na kuiabudu kama Mungu, hasira za BWANA ziliwaka juu yao na akakusudia kuangamiza Taifa zima isipokuwa Musa na nyumba yake tu. Naam Musa kama Mlinzi tena rafiki na mshauri wa Mungu alitumia nafasi yake vema kumshauri Mungu ipasavyo juu ya hatua stahiki zinazopaswa kuchukuliwa kwa watu walio chini ya eneo lake. Mungu naye kwa kuzingatia ushauri wa Mlinzi wa kusudi lake, alighairi mabaya aliyokusudia kuwatenda watu wake.

Unajua kwa nini Mungu alighairi? Sio tu kwa sababu Musa aliomba Mungu awasamehe, bali kwa sababu Musa kutoka katika nafasi yake ya ulinzi wa kusudi la Mungu, alimkumbusha Mungu kusudi lake la kuwatoa wana wa Israeli utumwani sambamba na kukumbusha agano alilowaapia Ibrahimu, Iasaka na Yakobo. Ndiyo maana ninasisitiza kwamba ni muhimu sana kwako kama Mlinzi kujua nini ni mapenzi ya Mungu kwenye eneo lako na watu wake.

Mpenzi msomaji kabla sijamalizia sehemu hii ya tano, hebu nikuonyeshe jambo lingine tamu sana kutoka habari hii ya Musa. Biblia kwenye ule mstari wa kumi inasema BWANA akamwambia Musa ‘Basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize; nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu’. Je umeliona lile neno linalosema ‘niache’. Kitendo cha Mungu kumwambia Musa ‘basi sasa niache’ kinatuonyesha kwamba, si tu Musa alikuwa kiongozi wa wana wa Israeli, bali, zaidi aliwekwa na Mungu kuwa ‘MLINZI WAO’ na kwa sababu hiyo hakuna ambaye angeweza kufanya jambo juu yao bila ridhaa yake.

Naam huenda wana wa Israeli hawakuijua vema nafasi ya Musa kwao, bali Musa akiijua thamani ya nafasi yake kwa Mungu na watu wa eneo lake, alishauri vema na BWANA akaghairi hasira zake juu yao. Sasa hebu fikiri kama walinzi wote kwenye maeneo yao, wangezijua na kuzitumia nafasi zao vema kama Musa, kusudi la Mungu lingefanikiwa kwa kiwango gani? Binafsi nimejifunza kwamba kufanikiwa kwa kusudi la Mungu hapa duniani si tu kunategemea utiifu wa watu wake bali zaidi kunategemea namna Walinzi wake wanavyozitumia nafasi zao katika ulimwengu wa roho.

Ndugu zangu, nafasi ya ulinzi katika ulimwengu wa roho, ni nafasi ya pekee sana ambayo Mungu ametupa watoto wake. Ni matarajio ya Mungu kuona kwamba tunazijua vema nafasi zetu na kuzitumia kama viongozi, waombaji, waonyaji/watoa taarifa na washauri wake juu ya masuala mbalimbali ya kiroho kwenye maeneo yetu ya ulinzi. Bwana Yesu alisema ‘Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga’ (Mathayo 10:25). Naam sisi tuliopewa ufunuo huu, na tuutumie kwa utukufu wake.

Tutaendelea na sehemu ya sita…

Utukufu na heshima vina wewe Yesu! Wastahili Bwana wangu.

Advertisements

14 comments

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s