ONGEZA UFAHAMU WAKO KUHUSU NYAKATI ILI ZIKUSAIDIE KUFIKIRI KI-MUDA (Sehemu ya pili)

Na: Patrick Sanga

MaadaNamna ya kufikiri ki-Muda na matokeo yake

Shalom! Katika sehemu ya kwanza tuliangalia utangulizi juu ya umuhimu wa mtu kuwa na ufahamu kuhusu nyakati ili ziweze kumsaidia kufikiri kwa kuongozwa na muda/nyakati. Ili kusoma sehemu ya kwanza bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2012/08/04/ongeza-ufahamu-wako-kuhusu-nyakati-ili-uweze-kufikiri-ki-muda/ 

Katika sehemu hii ya pili tutaangalia namna ya kufikiri ki-muda na matokeo yake nikilenga kukuonyesha maandiko mbalimbali yanayohusu nyakati/muda na namna ambavyo maandiko haya yatakusaidia kufikiri ki – muda ili kila jambo lifanyike kwa muda uliokusudiwa maishani mwako. Kumbuka kwamba Mungu ametuwekea nyakati ili ziongoze mfumo wetu wa kufikiri na kutenda. Ni matumaini yangu kama Mwandishi kwamba ujumbe huu utakusaidia kuongeza ufahamu wako kuhusu nyakati zilizoamriwa juu yako.  

Ni muhimu sana ukafahamu kwamba siku zetu za kuishi hazifanani, kila mtu ameitwa kwa kusudi maalumu ambalo limefungwa kwenye muda. Naam muda wa kusudi la kila mmoja wetu umetofautina hata kama wote tupo kwenye kizazi hiki. Ni jukumu lako kujua nyakati zako zinataka ufanye nini ili kukamilisha kusudi la Mungu katika siku zako. Naam, Mungu ameweka majira ili yatuongoze katika kufanya na kutekeleza maamuzi mbalimbali kwa utukufu wake.

Basi sasa na tuangalie maandiko mbalimbali yanasemaje;

Mwanzo 8:22 “Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma”. Andiko hili linatuonyesha nyakati ambazo BWANA Mungu ameziamuru juu ya nchi, kwamba kuna majira ya kupanda, kuvuna, usiku, mchana nk. Ni matarajio ya Mungu kwamba mwanadamu atashirikiana na nyakati zilizoamriwa juu ya nchi kufanikisha mambo yake, muhimu zaidi kusudi la Mungu. Naam Mungu anataka watu wake wajifunze ku ‘connect’ majira yaliyopo na wajibu wetu kwake. Naam, watu wake wawaze majira yaliyopo yanataka tufanye nini kiroho, kiuchumi, kifamilia, ki-ndoa, kitaifa nk.

Ndiyo maana katika kitabu cha Mambo ya Walawi 26:4-5 Biblia inasema ‘Kama mkienda katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyafanya, ndipo nitazinyesha mvua zenu kwa nyakati zake, na nchi itazaa maongeo yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake’. Sambamba na andiko hili ukisoma pia Kumbukumbu la Torati 11:13-14 Biblia inasema ‘Tena itakuwa mtakaposikiza kwa bidii maagizo yangu niwaagizayo leo, kwa kumpenda BWANA, Mungu wenu na kumtumikia kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote, ndipo nitakapowapa mvua ya nchi yenu kwa wakati wake, mvua ya masika, na mvua ya vuli, upate kuvuna nafaka yako, na divai yako, na mafuta yako’.

Je umeona jambo hili mpendwa wangu? Ukiunganisha mawazo ya maandiko haya mawili na lile la Mwanzo 8:22 utagundua kwamba licha ya kuwepo nyakati za kupanda, kuvuna nk. lakini pia kuna nyakati za ‘mvua kunyesha’. Naam yeye apandaye hawezi kuvuna kama mvua hazijanyesha kwa nyakati zake, naam hata nchi haiwezi kuzaa maongeo na matunda mashambani.

Jambo la muhimu zaidi tunalojifunza hapa ni kwamba kunyesha kwa mvua au kufanikiwa kwa nyakati zilizoamriwa juu ya nchi kunategemea nidhamu ya mwanadamu katika kuzishika, kuzitafakari na kuzitenda amri na sheria za BWANA. Na kwa hiyo unapofikiri nyakati zilizoko mbele yako zinakutaka ufanye nini, angalia kwanza namna unavyoenenda mbele za Mungu katika sheria zake. Unajua kwa nini? Ni kwa sababu nyakati zimeamriwa na Mungu, kutoa ushirikiano kwa mtu ambaye anazingatia maagizo ya Mungu na sheria zake. Naam, usitegemee mvua zinyeshe kwa nyakati zake, wakati wewe haujayatenda yakupasayo sawasawa na neno la BWANA. Binafsi nimejifunza kwamba ‘Kadri mtu anavyokuwa na ufahamu wa neno la Mungu na kuyatenda maagizo yake ndivyo na ufahamu wake kuhusu muda wa kila jambo unavyoongezeka ndani yake’.

Mfano wa matoleo/sadaka;

Biblia katika kitabu cha Hesabu 28:2 inasema ‘Waagize hao wana wa Israeli, uwaambie, Matoleo yangu, chakula changu cha sadaka zangu zisongezwazo kwa moto, za harufu ya kupendeza kwangu mimi, mtaangalia kuzisongeza kwangu kwa wakati wake upasao’. Pia katika Mambo ya Walawi 9:13 imeandikwa ‘Lakini mtu aliye safi, wala hakuwa katika safari, naye amekosa kuishika pasaka, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake; kwa sababu hakumtolea BWANA matoleo kwa wakati wake ulioamriwa, mtu huyo atachukua dhambi yake’.

Naamini umeona msisitizo wa Mungu juu ya kutoa sadaka/matoleo mbalimbali kwa wakati uliokubalika/amriwa. Watu wengi sana inapofika suala la matoleo hufanya kwa mazoea na vile jinsi wanavyojiskia wao kufanya. Fahamu kwamba suala la matoleo kwa Mungu ni la muhimu sana, na anataka ujifunze kutoa kwa nidhamu ya muda uliokubalika. Katika mapato/fedha ambayo Mungu anakubariki kumbuka kuna sehemu yake kwa maana ya zaka na sadaka. Naam mara uipatapo ni jukumu lako kutafuta uongozi wake juu ya wapi, lini (muda wa kutoa) na kwa kiwango (kiasi) gani unatakiwa kutoa. Kukosa nidhamu hii ni kujiingiza kwenye laana kwa kuwa yeye ameagiza watu wake wazingatie muda katika kutoa kwao (Rejea Malaki 3:9).

Tujifunze kwa watu wa kizazi cha Nabii Hagai

Katika kile kitabu cha Hagai 1:2-6 Biblia inasema ‘BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Huu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujengwa nyumba ya BWANA’ Ndipo neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? Basi sasa, BWANA wa majeshi asema, Zitafakarini njia zenu, Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka toboka’.

Maandiko yako wazi kwamba watu hawa walisema ‘huu si wakati wa kujenga nyumba ya Bwana’. Naam hivi ndivyo wao walivyofikiri ki-muda, wao waliona ule ulikuwa ni wakati wa kujenga nyumba zao kwanza. Uamuzi huu uliwagharimu sana kwani kila walilokuwa wanafanya halikufanikwa, walipanda mbegu nyingi wakavuna kidogo, kile kidogo walichovuna walikula bila kushiba, aliyepata mshahara uliisha bila kuona hata thamani yake, naam walitazamia vingi vikatokea vichache, vichahche walivyopata vikapeperushwa, na mbaya zaidi mbingu ikazuiliwa isitoe umande na nchi isitoe matunda.

Mpenzi msomaji je umeliona kosa lao? Hawa watu walifikiri ki-muda, lakini hawakufikira matokeo ya fikra zao ki-muda yatakuwaje?. Naam kosa lao lilikuwa kwenye tafisri (interpretation) ya nyakati. Nyakati ambazo Bwana Mungu aliziweka juu yao, wao waliona ni za kujiendeleza wao na si nyumba ya BWANA.

Walipowaza kwa nini mabaya haya yamewakuta? Ndipo BWANA akawajibu akisema ‘Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake’ (Hagai 1:9). Ili kuwasaidia watu wake Nabii Hagai akawambia mkitaka kuona tena Baraka za Mungu juu yenu ‘Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijengue nyumba ya BWANA’. Kwa lugha nyingine alikuwa akiwaambia Baraka ambazo Mungu alizileta juu yenu mlitakiwa kuzielekeza katika kuijenga nyumba ya BWANA na si za kwenu. Na ndiyo maana nimekueleza, jifunze kutafuta uongozi wa Mungu juu ya matoleo yako kwa habari ya muda wa kutoa, wapi pa kutoa na kwa kiasi cha kutoa.

Mara kwa mara nimewasikia watu wakisema nimelazimika kutumia fedha yote niliyoipata ikiwa ni pamoja na zaka/sadaka, kufanya mambo yangu, maana sikuwa na namna nyingine kwa kuwa hitaji langu lilihitaji zaidi ya fedha niliyoipata. Maandiko yapo wazi kabisa kwamba zaka ni ya BWANA, hivyo kitendo cha kutumia sadaka/zaka ya BWANA kufanya mambo yako, ni kuzuia mvua zisinyeshe kwa nyakati zake, na hivyo kuharibu majira ya kupanda na kuvuna kwenye maisha yako.

Mfano wa Ibrahimu

Biblia katika Mwanzo 18:14 inasema ‘Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati uu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume’. Toleo la ESV kwenye mstari uuu linasema ‘Is anything too hard for the LORD? At the appointed time I will return to you, about this time next year, and Sarah shall have a son.

Huyu ni baba yetu wa Imani Ibrahimu ambaye alikuwa amefadhaika kwa kukosa uzao kupitia Sarai mkewe. Mungu akamtokea na kumweleza kwamba hakuna jambo gumu la kmushinda yeye, bali Mungu alitaka Ibrahimu ajue endapo anaona ahadi ya Mungu haijatimia, ajue kwamba nyakati (appointed time) zilizobeba ahadi/kusudi husika hazijawadia na hivyo aendelee kuwa mvumilivu.Naam ndio maana Paulo aliwambia Wandugu wa Galatia   akisema ‘Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho’ (Wagalatia 6:9). Naam wewe upandaye panda ukijua kwamba kuna nyakati za kuvuna.

Kumbuka kwamba kwa kila jambo kuna majira yake, naam Mungu ameziweka nyakati zituongoze kujua nini tunapaswa kufanya, maana kinachoamua nini kifanyike ni nyakati. Naam ni jukumu lako kujifunza kufikiri ki-muda ili kukamilisha yale ambayo Mungu ameyakusudia kufanya kupitia wewe kwenye familia yako, ndoa, kabila, Ofisi na Taifa lako kwa ujumla.

Ubarikiwe, tutaendelea na sehemu ya tatu…

Neema ya BWANA iwe nawe daima

Advertisements

17 comments

 1. Shalom Mtumishi….
  Na ashukuriwe Mungu kwani binafsi nimepata ufunuo juu ya somo hili. Lakini nina swali nataka unifafanulie na ikibidi kwa kutumia mistari…. Fungu la kumi au zaka ni lazima itolewe ktk madhabahu ninakohudumu au hata madhabahu zingine au mahali pengine ninaposhuhudiwa na Roho Mt.?

  Like

 2. Asante mtumishi kwa mafundisho mazuri na yenye afya kiroho,ila shida yangu na hitaji langu ni kutaka kujua namna ya kuandaa mahubiri kulingana na nyakati, mazingira na rika mbalimbali, nitashukuru kwa msaada wako mtumishi wa Bwana. Asante na Mungu azidi kukutia nguvu.

  Like

  • Utukufu kwa Yesu na ahsante kwa maombi yako pia. Kuhusu hitaji lako swali bado ni pana kwani naona mambo mawili, je unalenga kuaandaa ujumbe wa kuhubiri pale unapotaka kuhudumu au kuandaa masomo kama hivi nifanyavyo? Sasa endapo hoja ya kwanza ni sahihi nakushauri jifunze kumpa nafasi Roho Mtakatifu ndio akuoongoze kupata ujumbe sahihi maana kanisa ni la Kristo na yeye ndiye anayejua mahitaji ya watu na aina ya watu watakaokuja ibadani kwa siku husika, hivyo unapomuuliza nini uhubiri atakuongoza kwenye ujumbe sahihi utakaofanyika msaada kwa watu hao. Sasa endapo unataka kujua zaidi basi tuawasiliane Brother.

   Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s