Archive for October 2012

ONGEZA UFAHAMU WAKO KUHUSU NYAKATI ILI ZIKUSAIDIE KUFIKIRI KI-MUDA (Sehemu ya pili)

October 27, 2012

Na: Patrick Sanga

MaadaNamna ya kufikiri ki-Muda na matokeo yake

Shalom! Katika sehemu ya kwanza tuliangalia utangulizi juu ya umuhimu wa mtu kuwa na ufahamu kuhusu nyakati ili ziweze kumsaidia kufikiri kwa kuongozwa na muda/nyakati. Ili kusoma sehemu ya kwanza bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2012/08/04/ongeza-ufahamu-wako-kuhusu-nyakati-ili-uweze-kufikiri-ki-muda/ 

Katika sehemu hii ya pili tutaangalia namna ya kufikiri ki-muda na matokeo yake nikilenga kukuonyesha maandiko mbalimbali yanayohusu nyakati/muda na namna ambavyo maandiko haya yatakusaidia kufikiri ki – muda ili kila jambo lifanyike kwa muda uliokusudiwa maishani mwako. Kumbuka kwamba Mungu ametuwekea nyakati ili ziongoze mfumo wetu wa kufikiri na kutenda. Ni matumaini yangu kama Mwandishi kwamba ujumbe huu utakusaidia kuongeza ufahamu wako kuhusu nyakati zilizoamriwa juu yako.  

Ni muhimu sana ukafahamu kwamba siku zetu za kuishi hazifanani, kila mtu ameitwa kwa kusudi maalumu ambalo limefungwa kwenye muda. Naam muda wa kusudi la kila mmoja wetu umetofautina hata kama wote tupo kwenye kizazi hiki. Ni jukumu lako kujua nyakati zako zinataka ufanye nini ili kukamilisha kusudi la Mungu katika siku zako. Naam, Mungu ameweka majira ili yatuongoze katika kufanya na kutekeleza maamuzi mbalimbali kwa utukufu wake.

Basi sasa na tuangalie maandiko mbalimbali yanasemaje;

Mwanzo 8:22 “Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma”. Andiko hili linatuonyesha nyakati ambazo BWANA Mungu ameziamuru juu ya nchi, kwamba kuna majira ya kupanda, kuvuna, usiku, mchana nk. Ni matarajio ya Mungu kwamba mwanadamu atashirikiana na nyakati zilizoamriwa juu ya nchi kufanikisha mambo yake, muhimu zaidi kusudi la Mungu. Naam Mungu anataka watu wake wajifunze ku ‘connect’ majira yaliyopo na wajibu wetu kwake. Naam, watu wake wawaze majira yaliyopo yanataka tufanye nini kiroho, kiuchumi, kifamilia, ki-ndoa, kitaifa nk.

Ndiyo maana katika kitabu cha Mambo ya Walawi 26:4-5 Biblia inasema ‘Kama mkienda katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyafanya, ndipo nitazinyesha mvua zenu kwa nyakati zake, na nchi itazaa maongeo yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake’. Sambamba na andiko hili ukisoma pia Kumbukumbu la Torati 11:13-14 Biblia inasema ‘Tena itakuwa mtakaposikiza kwa bidii maagizo yangu niwaagizayo leo, kwa kumpenda BWANA, Mungu wenu na kumtumikia kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote, ndipo nitakapowapa mvua ya nchi yenu kwa wakati wake, mvua ya masika, na mvua ya vuli, upate kuvuna nafaka yako, na divai yako, na mafuta yako’.

Je umeona jambo hili mpendwa wangu? Ukiunganisha mawazo ya maandiko haya mawili na lile la Mwanzo 8:22 utagundua kwamba licha ya kuwepo nyakati za kupanda, kuvuna nk. lakini pia kuna nyakati za ‘mvua kunyesha’. Naam yeye apandaye hawezi kuvuna kama mvua hazijanyesha kwa nyakati zake, naam hata nchi haiwezi kuzaa maongeo na matunda mashambani.

Jambo la muhimu zaidi tunalojifunza hapa ni kwamba kunyesha kwa mvua au kufanikiwa kwa nyakati zilizoamriwa juu ya nchi kunategemea nidhamu ya mwanadamu katika kuzishika, kuzitafakari na kuzitenda amri na sheria za BWANA. Na kwa hiyo unapofikiri nyakati zilizoko mbele yako zinakutaka ufanye nini, angalia kwanza namna unavyoenenda mbele za Mungu katika sheria zake. Unajua kwa nini? Ni kwa sababu nyakati zimeamriwa na Mungu, kutoa ushirikiano kwa mtu ambaye anazingatia maagizo ya Mungu na sheria zake. Naam, usitegemee mvua zinyeshe kwa nyakati zake, wakati wewe haujayatenda yakupasayo sawasawa na neno la BWANA. Binafsi nimejifunza kwamba ‘Kadri mtu anavyokuwa na ufahamu wa neno la Mungu na kuyatenda maagizo yake ndivyo na ufahamu wake kuhusu muda wa kila jambo unavyoongezeka ndani yake’.

Mfano wa matoleo/sadaka;

Biblia katika kitabu cha Hesabu 28:2 inasema ‘Waagize hao wana wa Israeli, uwaambie, Matoleo yangu, chakula changu cha sadaka zangu zisongezwazo kwa moto, za harufu ya kupendeza kwangu mimi, mtaangalia kuzisongeza kwangu kwa wakati wake upasao’. Pia katika Mambo ya Walawi 9:13 imeandikwa ‘Lakini mtu aliye safi, wala hakuwa katika safari, naye amekosa kuishika pasaka, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake; kwa sababu hakumtolea BWANA matoleo kwa wakati wake ulioamriwa, mtu huyo atachukua dhambi yake’.

Naamini umeona msisitizo wa Mungu juu ya kutoa sadaka/matoleo mbalimbali kwa wakati uliokubalika/amriwa. Watu wengi sana inapofika suala la matoleo hufanya kwa mazoea na vile jinsi wanavyojiskia wao kufanya. Fahamu kwamba suala la matoleo kwa Mungu ni la muhimu sana, na anataka ujifunze kutoa kwa nidhamu ya muda uliokubalika. Katika mapato/fedha ambayo Mungu anakubariki kumbuka kuna sehemu yake kwa maana ya zaka na sadaka. Naam mara uipatapo ni jukumu lako kutafuta uongozi wake juu ya wapi, lini (muda wa kutoa) na kwa kiwango (kiasi) gani unatakiwa kutoa. Kukosa nidhamu hii ni kujiingiza kwenye laana kwa kuwa yeye ameagiza watu wake wazingatie muda katika kutoa kwao (Rejea Malaki 3:9).

Tujifunze kwa watu wa kizazi cha Nabii Hagai

Katika kile kitabu cha Hagai 1:2-6 Biblia inasema ‘BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Huu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujengwa nyumba ya BWANA’ Ndipo neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? Basi sasa, BWANA wa majeshi asema, Zitafakarini njia zenu, Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka toboka’.

Maandiko yako wazi kwamba watu hawa walisema ‘huu si wakati wa kujenga nyumba ya Bwana’. Naam hivi ndivyo wao walivyofikiri ki-muda, wao waliona ule ulikuwa ni wakati wa kujenga nyumba zao kwanza. Uamuzi huu uliwagharimu sana kwani kila walilokuwa wanafanya halikufanikwa, walipanda mbegu nyingi wakavuna kidogo, kile kidogo walichovuna walikula bila kushiba, aliyepata mshahara uliisha bila kuona hata thamani yake, naam walitazamia vingi vikatokea vichache, vichahche walivyopata vikapeperushwa, na mbaya zaidi mbingu ikazuiliwa isitoe umande na nchi isitoe matunda.

Mpenzi msomaji je umeliona kosa lao? Hawa watu walifikiri ki-muda, lakini hawakufikira matokeo ya fikra zao ki-muda yatakuwaje?. Naam kosa lao lilikuwa kwenye tafisri (interpretation) ya nyakati. Nyakati ambazo Bwana Mungu aliziweka juu yao, wao waliona ni za kujiendeleza wao na si nyumba ya BWANA.

Walipowaza kwa nini mabaya haya yamewakuta? Ndipo BWANA akawajibu akisema ‘Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake’ (Hagai 1:9). Ili kuwasaidia watu wake Nabii Hagai akawambia mkitaka kuona tena Baraka za Mungu juu yenu ‘Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijengue nyumba ya BWANA’. Kwa lugha nyingine alikuwa akiwaambia Baraka ambazo Mungu alizileta juu yenu mlitakiwa kuzielekeza katika kuijenga nyumba ya BWANA na si za kwenu. Na ndiyo maana nimekueleza, jifunze kutafuta uongozi wa Mungu juu ya matoleo yako kwa habari ya muda wa kutoa, wapi pa kutoa na kwa kiasi cha kutoa.

Mara kwa mara nimewasikia watu wakisema nimelazimika kutumia fedha yote niliyoipata ikiwa ni pamoja na zaka/sadaka, kufanya mambo yangu, maana sikuwa na namna nyingine kwa kuwa hitaji langu lilihitaji zaidi ya fedha niliyoipata. Maandiko yapo wazi kabisa kwamba zaka ni ya BWANA, hivyo kitendo cha kutumia sadaka/zaka ya BWANA kufanya mambo yako, ni kuzuia mvua zisinyeshe kwa nyakati zake, na hivyo kuharibu majira ya kupanda na kuvuna kwenye maisha yako.

Mfano wa Ibrahimu

Biblia katika Mwanzo 18:14 inasema ‘Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati uu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume’. Toleo la ESV kwenye mstari uuu linasema ‘Is anything too hard for the LORD? At the appointed time I will return to you, about this time next year, and Sarah shall have a son.

Huyu ni baba yetu wa Imani Ibrahimu ambaye alikuwa amefadhaika kwa kukosa uzao kupitia Sarai mkewe. Mungu akamtokea na kumweleza kwamba hakuna jambo gumu la kmushinda yeye, bali Mungu alitaka Ibrahimu ajue endapo anaona ahadi ya Mungu haijatimia, ajue kwamba nyakati (appointed time) zilizobeba ahadi/kusudi husika hazijawadia na hivyo aendelee kuwa mvumilivu.Naam ndio maana Paulo aliwambia Wandugu wa Galatia   akisema ‘Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho’ (Wagalatia 6:9). Naam wewe upandaye panda ukijua kwamba kuna nyakati za kuvuna.

Kumbuka kwamba kwa kila jambo kuna majira yake, naam Mungu ameziweka nyakati zituongoze kujua nini tunapaswa kufanya, maana kinachoamua nini kifanyike ni nyakati. Naam ni jukumu lako kujifunza kufikiri ki-muda ili kukamilisha yale ambayo Mungu ameyakusudia kufanya kupitia wewe kwenye familia yako, ndoa, kabila, Ofisi na Taifa lako kwa ujumla.

Ubarikiwe, tutaendelea na sehemu ya tatu…

Neema ya BWANA iwe nawe daima

NAMNA MWANAMKE ANAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI ZAKE KUBADILISHA MAISHA YA NDOA YAKE (Sehemu ya 3)

October 26, 2012

Na: Patrick Sanga

Nafasi ya nne – Mwanamke kama Mlinzi

Katika sehemu ya pili tuliangalia nafasi tatu za awali ambazo ni nafasi ya Msaidizi, Mshauri na Mleta kibali. Ili  kusoma sehemu ya pili bonyeza link hii  https://sanga.wordpress.com/2012/05/20/namna-mwanamke-anavyoweza-kutumia-nafasi-zake-kubadilisha-maisha-ya-ndoa-yake-2/ Kumbuka kwamba lengo la ujumbe ni kuangalia ni kwa namna gani Mwanamke aliyeolewa anaweza kutumia nafasi zake kubadilisha/kuiponya ndoa yake. Katika sehemu hii ya tatu tutaangalia nafasi ya mwanamke kama Mlinzi. Naam kwa rejea kumbuka kwamba, msingi wa somo hili ni maneno ambayo Octoba 2009 BWANA aliniambia akisema ‘Waambie wanawake wasimame kwenye nafasi zao ndipo wataona uponyaji kwenye ndoa zao’.

Labda nianze kwa kuuliza, je una fahamu kwamba wajibu wa kumlinda mumeo ni wako? Naam Mungu amejiwekea utaratibu mpya kwamba Mwanamke amlinde mwanaume. Je ni ulinzi wa namna gani? Ni ulinzi wa kiroho ndio ambao mwanaume anahitaji kutoka kwa mkewe. Mke anatakiwa kuwa makini ‘sensitive’ katika ulimwengu wa roho kuangalia ni mashambulizi gani Shetani amekusudia kuyaleta kwa mume/ndoa yake. Naam akishajua aweke ulinzi ili mawazo ya Shetani yasitimie kwenye ndoa yake.

Kuwa Mke wa fulani, ni nafasi ya ulinzi katika ulimwengu wa roho ambayo Mungu anaitoa. Kwa hiyo fahamu kwamba unapoingia kwenye ndoa, Mungu anakupa wajibu wa kumlinda mumeo. Biblia katika Yeremia 31:22 inasema ‘Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanaume. Nafasi ya ulinzi ni nafasi ya pekee sana ambayo Mwanamke amepewa na endapo ataitumia vizuri itamsaidia kweli kweli kuiponya ndoa yake. Hii ni kwa sababu mlinzi ndiye anayeona mambo yanayotaka kuja kwenye ndoa yake akali kwenye ulimwengu wa roho, kabla hayajadhihirika kwenye ulimwengu wa mwili.

Ukisoma Mstari huu wa Yeremia 31:22 katika toleo la kiingereza la ESV unasema ‘How long will you waver, O faithless daughter? For the LORD has created a new thing on the earth: a woman encircles a man’ na pia katika toleo la KJV imeandikwa ‘How long wilt thou go about, O thou backsliding daughter? for the LORD hath created a new thing in the earth, A woman shall compass a man’. Maneno ‘Mwanamke atamlinda mumewe’ kwenye ESV imeandikwa ‘a woman encircles a man’ na kwenye KJV imeandikwa ‘A woman shall compass a man’. Maneno haya yana maana ya zingira, zunguka au fanya duara.

Hapa Biblia inajaribu kutueleza jambo la mwanamke ambaye yamkini kutokana na changamoto za ndoa yake/mume wake alijikuta amekuwa mtu wa kuasi/kufanya mabaya. Sasa ili kumsaidia ndipo BWANA akamtuma Yeremia kumweleza ‘acha kutanga tanga, Mungu ameumba jambo jipya nalo ni ‘wewe mwanamke, umepewa wajibu wa kumlinda/kumzingira mwanaume/mumeo’. Naam ulinzi huu ni kwa jinsi ya rohoni. Mwanamke anaweza kumwekea/kumfanyia mume wake ulinzi dhidi ya makahaba, malaya, wenye hila, wala rushwa au chochote ambacho ni chanzo cha uharibifu wa ndoa nk.

Katika nafasi hii ya ulinzi Mke una wajibu wa kujua kwa nini Mungu amekuunganisha na mume uliye naye sasa. Naam lipo kusudi la ufalme wake, hivyo ni jukumu lako   kuhakikisha linatimia katika siku zenu za kuwepo hapa duniani kama wanandoa. Naam msaidie Mume wako kama Mlinzi kwa namna ambayo kusudi la Mungu halitakwama kwenye maisha yenu. Fahamu kazi ya Mlinzi ni kumsaidia Bwana wake kufanikisha majukumu yake. Endapo Mlinzi hatakuwa makini kwenye nafasi yake basi majukumu ya Bwana wake hayatafanikiwa, si kwa sababu ametaka bali ni kwa sababu Mlinzi/Walinzi wake hawakumpa usaidizi wa kutosha kiulinzi.

Ni vizuri ukafahamu kwamba ili Shetani ammalize mumeo, njia kuu kwake ni kupitia kwa mkewe. Angalia leo ndoa ngapi zimeharibika na ukifuatilia chanzo utagundua Mke amechangia kwa sehemu kubwa. Hebu taunaglie mifano kadhaa ndani ya Biblia;

 Ndoa ya Anania na Safira (Matendo ya Mitume 5:1-11).

Ule msitari wa 1-2 maandiko yanasema ‘Lakini Mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume’.  Ukisoma fungu zima hapo juu utagundua kwamba kutokana na wizi wao wote wawili, walikufa siku moja. Jambo ninalotaka tulione hapa ni ile kusema ‘mkewe naye akijua haya’. Maneno haya yameandikwa ili kuonyesha namna ambavyo Safira hakutumia nafasi yake kuiponya ndoa yake. Kutokana na kutokumshauri mumewe vizuri na kumlinda dhidi ya hatari iliyokuwa mbele yao, wote wawili walikufa. Nani ajuae kwamba pengine Safira angemwonya mumewe, mumewe angemsikiliza. Naam kwa kuwa alinyamaza, na Mungu alinyamaza, mauti ikawajia.

Ndoa Ahabu na Yezebeli (1Wafalme 21:1-23)

Ukisoma andiko hili utaona namna Yezebeli mke wa Ahabu alivyotumia vibaya nafasi zake, kwa kumuua Nabothi ili amrithishe mumewe shamba la Nabothi. Biblia katika mstari wa 9 -10 inasema Yezebeli ‘ Akaandika katika zile nyaraka, akasema, pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki na kumshuhudia, kunena, umemtukana Mungu na mfalme, kisha mchukueni nje mkampige kwa mawe, ili afe’. Watu wa mji walifanya kama Yezebeli alivyoagiza. Naam Yezebeli hakujua huo ndio ulikuwa mwisho wa utawala wao kwa kosa lile, kwani mahali pale ambapo mbwa waliramba damu ya Nabothi ndipo na damu ya Ahabu ilipomwagika wakairamba pia. Naam angekuwa na ufahamu huu, angetumia nafasi zake vizuri kuponya ndoa yake na utawala wao juu ya nchi.

Ndoa ya Abramu na Sarai (Mwanzo 16:1- 6) nk.

Kutokana na Sarai kutokupata mtoto kwa miaka mingi alimshauri Abramu mumewe atembee na mjakazi wake aliyeitwa Hajiri pengine angepata mtoto. Maandiko yanasema Abramu akaingia kwa Hajiri naye akashika mimba. Kitendo cha Hajiri kushika mimba kikamfanya Sarai aonekane duni/asiyefaa mbele za Hajiri. Ndipo Sarai akamwambia mumewe kusema ‘ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe’. Maandiko hayatuelezi endapo Abramu aliwahi kumwambia mkewe kwamba unipe mjakazi wako nimwingie ili kukuzalia mtoto. Lilikuwa ni wazo la Sarai, naam akalitekeleza, bila kujua matokezo ya mawazo yake ni nini. Ukiendelea kusoma Biblia utagundua kwamba jambo hili liliwakosanisha Sarai na Hajiri, si hivyo tu lakini hata ndoa yake iliathirika. Laiti angedumu kwenye ahadi ya Mungu, fedheha aliyoipata isingemtokea.

Ee Mwanamke, Je umeona jinsi wanandoa hawa yaani Safira, Yezebeli na Sarai walivyotumia vibaya nafasi zao? Ni Wake wangapi leo wanafanya mambo yanayofanana na haya kwa kujua au kutokujua? Ndoa ngapi leo zipo kwenye matatizo kwa kuwa Wake wanawadharau waume zao? Ndoa ngapi leo zimeharibika kwa sababu Wake hawawashauri vema waume zao juu ya Zaka na Sadaka? Ndoa ngapi leo zimeharibika kwa kuwa Wake hawataki kuwapa waume zao haki ya tendo la ndoa? Ndoa ngapi leo zinaharibika kwa sababu Wake wanawaunga mkono waume zao kufanya yaliyo maovu? Naam imefika mahala Wake wanakubali kufanya zinaa kinyume na maumbile na waume zao? Naam ndoa ngapi leo zimeharibika kwa kuwa wanawake hawapo kwenye nafasi zao kama Wasaidizi, Washauri, Waleta kibali na Walinzi, na hivyo Shetani anatumia uzembe wao kuharibu ndoa zao? Naam baadhi ya akina mama wanafanya mambo mabaya kwa lengo la kuwapendeza waume zao, wasijue kadri wanavyotoka nje ya nafasi zao kiroho, ndivyo adui anavyopanda uharibifu kwenye ndoa zao ili kukwamisha kusudi la Mungu kupitia ndoa zao.

Mambo ya muhimu kwa mwanamke kujua kuhusiana na nafsi ya kuwa mlinzi ni a) Mke amepewa/amefanywa  kuwa ‘Mlinzi’ wa ‘Mume’ katika ulimwengu wa roho akali hapa duniani b) Ni wajibu wa Mke kama ‘Mlinzi’ kusimama kwenye nafasi yake ili kuhakikisha kusudi la Mungu linafanikiwa kupitia ndoa yake c) Ili Mungu ampe Mke taarifa kuhusu mumewe na nyumba yake, Mke sharti awe kwenye nafasi yake maana Mungu hua anatoa taarifa kwa walinzi tegemeana na ‘nafasi zao’ d)Mke anapsawa kuitumia ‘taarifa’ anayopewa na Mungu kama ‘fursa’ ya uponyaji wa ndoa yake.

Wake wengi leo wamebaki kuwalaumu waume zao kutokana na mambo wanayoyafanya ili hali wao hawafanyi pia wajibu wao. Je mara ngapi kwa siku unamuombea mumeo kwa kumaanisha? Ni ulinzi kiasi gani umemuwekea mumeo? Je unafafamu kwamba suala la usalama wa mume wako, Mungu ameliweka kwako? Naam usipofanya na Yesu hafanyi? Ukinyamaza na yeye ananyamaza? Unajua kwa nini? Ni kwa sababu Mungu hawezi kuweka ulinzi juu ya mji, kama Mlinzi wa mji hajasema ‘BWANA linda mji huu’ (Isaya 62:6-7). Naam Jenga nidhamu ya kuomba kila siku kwa ajili ya mumeo ili Mungu aachilie ulinzi wake juu ya mumeo kwa kuwa wewe, kama Mlinzi uliyeko kwenye nafasi, umeshauri na umeelekeza kufanya hivyo. Naam ni wajibu wako pia kutumia damu ya Yesu kumwekea mumeo ulinzi kwenye kila eneo la misha yake na hivyo kuiponya ndoa yako (Asomaye na afahamu).

Tutaendelea na sehemu ya nne…

Utukufu na heshima vina wewe Yesu! Wastahili BWANA.

KUISHINDANIA IMANI

October 13, 2012

                                Na: Patrick Sanga

Mwandishi wa kitabu cha Yuda ameanza kwa kusisitiza akisema, Wapenzi nilipokuwa nikifanya bidii sana, kuwaandikia kwa habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu (Yuda 1:3)

Imani ni nini? Biblia inasema ‘Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana’ (Webrania 11:1). Chanzo cha imani ni nini? Paulo kwa Warumi anafafanua akisema ‘Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo’ (Warumi 10:17). Hivyo imani ambayo tunapaswa kuishindani ni uhakika tulionao juu ya neno la Mungu, msingi ukiwa Yohana 3:16 inayosema ‘Kwa maana jinsi hii Mungu, aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele’.

Kwa nini tuishindanie imani?

  • Vita iliyopo kwenye ulimwengu wa roho kati ya Mungu na Shetani. Katika Waefeso 6:12 Biblia inasema ‘Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho’
  • Kuna watu wamejiingiza kwa siri ili kuivuruga imani yetu katika Kristo, Biblia inasema katika  Yuda 1:4 ‘Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo’
  • Wapo walioangamizwa kwa sababu ya kushindwa kuishindania imani Biblia inasema katika Yuda 1:5 ‘…Bwana, akiisha kuwaokoa watu katika nchi ya Misri, aliwaangamiza baadaye wale wasioamini,
  • Bila imani hatuwezi kumependeza Mungu. Imeandikwa ‘Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao’ (Waebrania 11:6)

Kwa namna gani mtu unaweza  kuishindania imani?

  • Kuendelea kuongeza imani yako (Rejea Luka 17:5, Warumi 10:17 na Mathayo 17:21) Kutokana na upungufu wa imani ambao wanafunzi walikuwa nao kwa mujibu wa Mathayo 17:21 ndipo katika Luka 17:5 wakamwomba Bwana awaongezee imani. Ili kuongeza imani sharti ujifunze ‘kusikia’ neno la Mungu kila siku. Naam ujenge nidhamu ya kusoma neno la Mungu, kujali ibada na pia kuwa na utaratibu wa kuwa na ibada hata nyumbani kwako.
  • Kwa kulinda nafasi uliyopewa/ulizopewa na Mungu (Rejea Yuda 1:6, Wimbo Ulio Bora 1:6, Mathayo 22:8). Maadam umeokoka wewe ni Mlinzi wa kusudi la Mungu katika ulimwengu wa roho kwenye eneo ulilopo. Zaidi kiroho, kiuchumi, kijamii, kifamilia, kiknisa nk kuna nafasi ambazo Mungu ametupa sit u katika ulimwengu wa mwili zaidi ni katika ule wa kiroho, hivyo ni jukumu letu kuzilinda. Je upo makini kiasi gani kulinda nafasi uliyopewa na Mungu katika ulimwengu wa roh na ule wa mwili.
  • Kwa kuwa na ufahamu wa nyakati unazoishi. Mungu ameziweka nyakati ili zituongoze kufanikisha kusudi lake kwa kufanya kile kinachotakiwa kufanyika kwa wakati husika. Naam ni jukumu lako kuwazanyakati ulizopo zinataka nini kutoka kwako. Naam jifunze kutoka kwa wana wa Isakari maandiko yanasema ‘Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Isareli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao’ 1Nyakati 12:32.  Kwa ufahamu zaidi juu ya nyakati rejea maandiko yafuatayo (Muhubiri 3:1-8, Mwanzo 8:22, Waefeso 5:15-17, 1Wathesalonike 5:1-4, Luka 19:41).  
  • Endelea kuwa mwaminifu hata kama huoni matokeo yake sasa. Uaminifu wako ndio utakaodhihirisha kwamba wewe unaishindania imani. Imeandikwa ‘Mtu mwaminifu atakuwa na Baraka tele (Mithali 28:20a). Mungu hawezi kukuacha uabike mpendwa wangu, usijiingize kufanya mambo yanayokuondolea uaminifu wako kwa Mungu, maana kwa kufanya hivyo utapelekea wokovu wetu katika Kristo kutukanwa.

Shetani anajua kwamba ameabikiwa na muda mchache wa kufanya kazi zake hapa duniani. Lengo lake ni kuhakikisha anadanganya watu wengi wa kwenda nao kwenye ziwa la moto ambalo kimsingi liliandaliwa kwa jili yake na Malaika walioasi. Usiruhusu hila yake, roho ya kuchoka na kukata tamaa vikumalize na kuharibu mahusaino yako na Mungu. Hakikisha unadumu katika kuishindania imani hata ajapo Mwana wa Adamu, maana pasipo Imani haiwezekani kumpendeza.

Mungu akubariki, na tuzidi kuombeana.