Archive for August 2012

KWA NAMNA GANI MTU ANAWEZA KUMZIMISHA ROHO MTAKATIFU?

August 4, 2012

Na: Patrick Sanga

Roho Mtakatifuni Mungu, mwenye nguvu zote, maarifa yote, anayepatikana kila mahali. Yeye pia anayo nafsi na kwa hiari yake ameamua kuishi ndani ya mwili wa mwanadamu kwa kuzingatia mgawanyo wa majukumu waliyokubaliana yaani nafsi ya    Mungu Baba, Mungu Mwana(Yesu) na Mungu Roho Mtakatifu. Kazi/lengo kubwa la ujio wake ni kuwa Msaidizi wa mwanadamu kwenye ulimwengu huu wa mwili, ili kumsaidia kuishi katika mapenzi ya Mungu.

Mungu hana namna ya  kutawala kwenye ulimwengu wa kimwili bila kuwa na mwili wa damu na nyama, kwa kuwa yeye ni Roho (Yohana 4:24). Hivyo hana budi kuingia kwenye mwili wa mtu na kufanya makao yake hapo, ili kutawala na kumuongoza mwanadamu katika mapenzi yake (Yohana14:18, 23, 1Wakorinto 3:16-17, 6:19). Kwa sababu hii ni muhimu sana kwetu kutunza mahusiano yetu na Roho Mtakatifu ili tusimzimishe katika maisha yetu.

Paulo akizungumza na ndugu wa Thesalonike alisema ‘Msimzimishe Roho’ (1Wthesalonike 5:19). Paulo alitoa maonyo haya kwa kuwa alijua, Kumzimisha Roho Mtakatifu, kuna athari mbaya sana kwenye maisha ya mwamini katika kulitumikia kusudi la Mungu na hata maisha yake ya kawaida hapa duniani. Swali la msingi ni, kwa namna gani mtu anaweza kumzimisha Roho Mtakatifu? Ukisoma tafsiri za kiingereza, Biblia ya toleo la GNB katika mstari huu inasema Do not restrain the Holy Spirit’ na toleo la KJV linasema ‘Quench not the Spirit’ (1Th 5:19).

Tafsiri hizi mbili zinapanua zaidi tafsiri ya kumzimisha Roho, katika dhana mbili zifuatazo; moja kumzimisha Roho ina maana ya kumzuia Roho Mtakatifu asitawale na kuongoza maisha yako kwa kukataa msaada wake maishani mwako. Pili, kumzimisha Roho Mtakatifu ina maana ya kuishi katika mazingira ambayo yanamfanya Roho Mtakatifu ashindwe kukusaidia.

Mazingira ambayo Roho Mtakatifu anaweza kuzimishwa;

  • Kutokumpa nafasi akusaidie

Kwa mujibu wa Matahayo 14:16, Roho Mtakatifu ameletwa kwetu kama Msaidizi. Kwa tafsiri, Msaidizi ni yule atoaye msaada pale anapohitajika na kupewa nafasi ya kufanya hivyo. Vivyo hivyo na Roho Mtakatifu kama hujampa nafasi ya kukusaidia (ingawa yupo ndani yako), hawezi kufanya hivyo na kwa hiyo taratibu utakuwa unamfungia/unamzuia kukusaidia maishani mwako.

  • Kukosa upendo

Ukisoma kitabu cha 1Wakorinto sura ya 13 na 14, utagundua kwamba suala la upendo limepewa msisitizo wa kipekee kwa mtu ambaye anataka kuona utendaji wa kazi wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yake na kwa ajili ya wengine pia. Upendo kwa mtu aliyejazwa Roho Mtakatifu ni moja ya vigezo muhimu sana kwa Roho Mtakatifu kusema/kujifunua na kufanya kazi ndani yako. Hivyo kukosa upendo ni dalili ya kumzimisha Roho Mtakatifu ndani yako. Ndiyo maana Paulo anasema hata kama angekuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, pia kuwa na imani timilifu kiasi cha kuhamisha milima, kama hana upendo si kitu yeye, naam ni bure tena ni ubatili (1Wakorinto 13:1-3).

  • Kuongozwa au kuenenda kwa mwili

Paulo aliwaambia hivi wandugu wa Galatia ‘Basi nasema, Enendeni kwa kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili’ (Wagalatia 5:16). Maneno haya alikuwa akiwaambia watu waliokoka na si wasiomjua Mungu. Kanisa la Galatia lilikuwa limeacha kuenenda kwa Roho likaanza kuenenda kwa mwili. Paulo akajua jambo hili litamzimisha Roho wa Bwana ndani yao, na kwa sababu hii hawataweza kuishi maisha ya ushindi hapa duniani na kisha kuurithi uzima wa milele, ndipo akawaonya akisema enendeni kwa Roho ili msizitimize tama za mwili.

  • Kutokutii maelekezo yake

Roho Mtakatifu kuitwa Msaidizi haina maana tunapaswa kumpamngia cha kufanya. Yeye ndiye mwenye kutuongoza katika njia itupasayo kuiendea (Zaburi 32:8). Kinachotakiwa ni mtu kuwa mtiifu kwa yale ambayo Roho Mtakatifu anakuagiza. Kukosa utiifu mara kwa mara kila anapokusemesha/kukuagiza ni kumjengea mazingira ya kutoendelea kusema na wewe na hivyo kuondoka kwako na kutafuta mtu mwingine amtumie kwa kusudi lake.  

  • Kukosa ufahamu wa utendaji wake

Mara nyingi watu wamemzimisha Roho kwa kutokujua utendaji wake ulivyo. Kuna nyakati Roho Mtakatifu anaweza akaleta msukumo ndani ya mtu wa kumtaka aombe, atulie kusoma neno n.k. Lakini kwa kutokujua namna anavyosema, wengi hujikuta badala ya kutulia na kufanya kile alichopaswa kufanya, wao hufanya mambo mengine.

Pia kuna nyakati katika ibada (sifa, maombi nk), Roho Mtakatifu anaweza akashuka juu ya mtu au watu na akataka kusema jambo, lakini viongozi wa makanisa au vikundi husika wakawazuia hao watu. Kufanya hivyo bila uongozi wa Mungu ni kumzimisha Roho. Mandiko yako wazi kabisa kwamba hatupaswi kutweza unabii (1 Wathesalonike 5:20) na wala hatupaswi kuzuia watu kunena kwa lugha (1Wakorinto 14:39). Zaidi tumeagizwa kujaribu mambo yote, na tulishike lililo jema (1 Wathesalonike 4:21).

Je tutajaribuje mambo yote ikiwa tunawazuia watu Kunena na pia tunatweza unabii? Hofu yangu ni kwamba kwa kuzuia watu kunena na pia kutweza unabii tunaweza tukajikuta tunamzimisha Roho Mtakatifu na kukataa uongozi wake kwenye maisha yetu. Ni vema tukakumbuka kile ambacho Paulo aliwaambia Wakorinto juu ya mambo haya kwamba ‘mambo yote yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu’ (1 Wakorinto 14:40). Naam na hili lina maana ni vema kwanza ujue utendaji wa Roho Mtakatifu ukoje, ili kuepuka kumzimisha kwa kutokujua utendaji wake. 

Pengine yapo mazingira mengine ambayo mtu anaweza akajikuta anamzimisha Roho Mtakatifu. Kumbuka jambo hili kwamba kumzimisha Roho Mtakatifu ni kumzuia asikusaidie, jambo ambalo tafsiri yake ni kukataa uongozi wake kwenye maisha yako. Biblia inasema katika Warumi 8:9 ‘Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo huyo si wake’. Usifanye mchezo na Roho Mungu hakikisha unatunza sana mahusiano mazuri kati yako na yeye kwa kutokumzimisha.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nawe

ONGEZA UFAHAMU WAKO KUHUSU NYAKATI ILI UWEZE KUFIKIRI KI-MUDA

August 4, 2012

Na: Patrick Sanga

Mpendwa msomaji nakusalimu kwa jina la Yesu aliye hai.

Katika waraka huu nimeona ni vema tukakumbushana kuhusu ufahamu wa nyakati tunazoishi. Hii ni kwa sababu nyakati(muda) zina mchango mkubwa sana juu ya kile ambacho kinatokea katika maisha ya mwanadamu.

Januari 30, 2011 nikiwa nimelala nilisikia sauti ya mtu ikisema ‘majira, majira, majira’. Katika kutafakari ujumbe huu ilinisumbua sana kujua majira yamefanya nini?   Baada ya kutafakari kwa muda kuhusu jambo hiili ndipo likaja wazo kuhusu, ufahamu juu ya majira/nyakati tulizonazo.

Katika kile kitabu 1Mambo ya Nyakati 12:32 maandiko yanasema “Na wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao vilikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao” Ukisoma mstari huu kwenye tafsiri ya kiingereza toleo la BBE, Biblia inasemaAnd of the children of Issachar, there were two hundred chiefs, men who had expert knowledge of the times and what it was best for Israel to do, and all their brothers were under their orders’

Naamini umeliona jambo hili, ufahamu waliokuwa nao wana wa Isakari uliwafanya ndugu zao wote (taifa) kuwa chini ya amri (uongozi) yao. Hii ni kwa sababu kutokana na ufahamu wa nyakati waliokuwa nao wana wa Isakari waliweza kuwaongoza ndugu zao kwa kuwaelekeza nini wanapaswa kufanya kijamii, kiroho, kiuchumi, kiusalama nk katika nyakati walizokuwa wakizipitia. Naam kadri taifa la Israeli walivyokuwa wakitekeleza maagizo wanayopewa na wana wa Isakari ndivyo walivyofanikiwa pande zote.

Ufahamu huu ndio uliowasaidia kujua yawapasayo Israeli kuyatenda kwa kila majira. Ufahamu wa muda waliokuwa nao wana wa Isakari, uliwapa Israeli, kujua majira yaliyopo juu yao yanaashiria nini na nyakati zilizoko juu yao zimebeba makusudi gani ndani yake?

Naam hata sasa Mungu anataka watoto wake wawe na ufahamu wa nyakati, ili wajue yawapasayo kufanya kwa kila nyakati ambazo wanazipitia katika maisha yao. Kwa mujibu wa andiko hili katika Taifa la Israeli Mungu aliinua watu mia mbili tu, ambao ndani yao walipewa neema ya kujua nyakati na zaidi kile ambacho watu wa Taifa lao wanapswa kukitenda ndani ya nyakati husika. Hii ina maana hata sasa kuna watu ambao sababu kubwa ya wao kuletwa duniani ni kuwa na jukumu kama lile la wana wa Isakari katika familia, koo, kabila, makanisa na taifa pia.

Kwa hiyo ni jukumu lako kufuatilia jambo hili kwa undani ili kama wewe ni mmoja wao basi ukae mkao wa kuhakikisha unazjiua vyema nyakati ambazo, wewe binafsi, familia, kabila, jamaa, kanisa, Taifa  nk mnapitia, na zaidi kujua nyakati ambazo zinakujua mbele yako/yenu ili uweze  kushauri ipasavyo kwenye kila nyanya.

Katika kitabu cha Muhubiri, Biblia inasema “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu” (Muhubiri 3:1). Kwa hiyo Mungu anaposema kuhusu majira ina maana kuna wajibu/mambo ambayo mtu anapaswa  kuyafanya ndani ya majira husika. Naam Mungu anataka watoto wake wajifunze kufikiri kwa kuzingatia muda au nyakati alizowawekea.

Ni muhimu sana watu wa Mungu wakajifunza kufikiri ki-muda, naam muda/nyakati ziongoze kufikiri kwao. Biblia inasema ‘Basi anagalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu nini yaliyo mapenzi ya Bwana’ (Waefeso 5:15-17).

Ukisoma nyaraka za Mtume Paulo utagundua kwa kiwango kikubwa alijua sana umuhimu wa ‘wandugu’ kuwa na ufahamu kuhusu nyakati ili waweze kufikiri kwa kuongozwa na muda au nyakati. Paulo alilitaka kanisa la Efeso lijue kwamba liko katika nyakati za ‘uovu’, muda wao umetekwa na kuvamiwa na roho ya ‘uovu’. Hivyo ili kuzirejesha nyakati kwenye kusudi la ki – Mungu wandugu walipaswa kuenenda kwa hekima wakitafuta kujua kila siku nini ni mapenzi ya Mungu juu yao, ndoa zao, kazi zao, nchi yao nk.   

Naam ndani ya nyakati/muda kuna siri nyingi sana, katika mfululizo huu nitakuonyesha ni kwa namna gani mwanadamu anapaswa kufikiri ki muda, matokeo yake ni nini na mwisho afanye nini kushirikiana na nyakati ambazo Mungu anazileta kwenye maisha yake.

Ubarikiwe, somo litaendelea—-