IJUE NA KUITUMIA NAFASI YAKO KAMA MLINZI KWENYE ULIMWENGU WA ROHO (Part 4)

Na: Patrick Sanga

Maada: NAFASI/MAENEO MBALIMBALI YANAYOHITAJI MLINZI/WALINZI
Katika sehemu ya tatu tuliangalia juu ya ‘umuhimu wa taarifa na mahusiano mazuri baina ya mlinzi na watu wa eneo lake’. Ili kusoma sehemu ya tatu bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2012/02/03/ijue-na-kuitumia-nafasi-yako-kama-mlinzi-kwenye-ulimwengu-wa-roho-part-3/. Katika sehemu hii ya nne tutaangalia mifano kadhaa ndani ya Biblia ya nafasi/maeneo ambayo yalihitaji kuwa na Mlinzi au Walinzi.

Kwa nini tujifunze mambo haya?
Ni muhimu sana tuangalie maeneo/nafasi hizi kwa sababu; a) Mwandamu amepewa kuwa ‘Mlinzi’ wa kusudi la Mungu katika ulimwengu wa roho akali hapa duniani b) Mtu mmoja anaweza akapewa zaidi ya eneo moja la ulinzi katika ulimwengu wa roho c) Mungu hua anatoa taarifa kwa walinzi tegemeana na ‘nafasi zao’ pia ‘maeneo yao ya ulinzi’ d) Mwisho ni wajibu wa kila ‘Mlinzi’ kusimama kwenye nafasi yake ili kuhakikisha kusudi la Mungu linafanikiwa.

Nafasi na maeneo mbalimbali ya ulinzi;
Eneo la kwanzaNyumba ya Israeli (Mlinzi wa nyumba ya Israeli)
Biblia katika Ezekieli 33:7 inasema ‘Basi, wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli, basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu’. Hapa Mungu anaitazama Israeli kama nyumba/makazi ya watu kuishi na hivyo kuwa na umuhimu wa kuwa na Mlinzi.

Eneo la pili Mji au Taifa (Mlinzi wa mji/Taifa)
Biblia katika Isaya 62:6 inasema ‘Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani’. Hapa tunaona walinzi wa mji wa Yerusalemu ambao wapo kwenye kuta. Naam ili kuulinda mji ilibidi kuwepo na walinzi kwenye kuta za mji.

2Wafalme 9:17 inasema ‘Basi Mlinzi alikuwa anasimama juu ya Mnara wa Yezreeli, akaliona lile kundi la watu wa Yehu…’. Hapa Biblia inazungumzia Mlinzi wa mji wa Yezreeli ambaye ili kuulinda mji na wakazi wake aliwekwa juu ya Mnara. Ukisoma pia Yeremia 31:6 inasema ‘Maana kutakuwa na siku moja, ambayo walinzi watalia juu ya vilima vya Efraimu, Inukeni tukaende Sayuni, kwa BWANA Mungu wetu’. Naam hawa nao ni walinzi wa mji wa Efraimu lakini eneo lao la kazi ni juu ya vilima. Kazi yao siyo kulinda vilima, bali kulinda mji wakiwa vilimani.

Maandiko haya yanatupa kujua kwamba kumbe eneo moja linaweza pia kuwa na walinzi wengi wakiwa kwenye nafasi tofautitofauti wakitekeleza lengo moja. Kitendo cha wengine kuwa kwenye kuta, mnara, vilima ni kwa lengo la mosi kuonyesha umuhimu wa nafasi ya walinzi na pili kuhakikisha usalama wa eneo husika na hivyo kuruhusu makusudi ya Mungu kutimia.

Eneo la tatuNyakati/muda/majira (Mlinzi wa muda/nyakati)


Biblia katika Isaya21:11-12 inasema ‘… Mtu ananililia toka Seiri, Ee Mlinzi habari gani za usiku? Ee mlinzi, habari gani za usiku? Mlinzi akasema, Mchana unakuja na usiku pia; mkitaka kuuliza, ulizeni, njooni tena’. Majibu ya Mlinzi huyu yanatuonyesha kwamba si tu alikuwa akihusika na usalama wa eneo lake lakini zaidi kuhakikisaha kila kusudi linatimia ndani ya muda wake. Naam hii ina maana hata nyakati (muda) zinatakiwa kuwa na walinzi wake maalumu, naam walinzi wa kuhakikisha makusudi ya Mungu yanafanikiwa ndani ya Muda uliokusudiwa maana kila kusudi analoliachilia Mungu ndani yake limebeba muda wa kutimia.

Eneo la nnemtu au watu (Mlinzi/Walinzi wa mtu au watu)
1Samweli 14:16 ‘Nao wale walinzi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaangalia…’ pia Ezekieli 33:2 inasema ‘watu wa nchi hiyo wakimtwaa mtu mmoja miongoni mwao, na kumweka awe mlinzi wao, ikiwa aonapo upanga…
Zaidi Yeremia 6:17 ‘Nami naliweka walinzi juu yenu, wakisema, isikilizeni sauti ya tarumbeta; lakini walisema Hatutaki kusikiliza’.

Maandiko haya kadhaa yanajaribu kutonyesha kwamba kumbe hata mtu au watu kwenye ulimwengu wanapaswa kuwa na walinzi ili kuwasaidia kutekeleza wajibu wao waliopewa na Mungu vema. Mtu hapa anaweza kuwa Kiongozi (kiroho, kisiasa, kijamii nk), Mtumishi (Mchungaji, Mwalimu, Mtume nk) na yeyote aliyekaa kwenye nafasi yake ili kutimiza kusudi la Mungu.

Eneo la tanoKanisa/nyumba ya Bwana/Malango (Mlinzi wa kanisa/lango)
2 Wafalme 11:18 ‘Na Yehoyada kuhani akaweka maakida (Walinzi) juu ya nyumba ya Bwana’. Katika 2Nyakati 23:18 -19 Biblia inasema ‘Akawasimamisha walinzi malangoni pa nyumba ya Bwana’… Maandiko yote haya yanatuonyesha kwamba hawa wote walikuwa ni walinzi wa nyumba ya Bwana isipokuwa kwenye maeneo tofauti. Kundi la kwanza ni walinzi juu ya nyumba ya Bwana na kundi la pili ni walinzi walikokuwa kwenye malango ya nyumba ya Bwana. Kumbuka ninapozungumzia habari za Mlinzi/Walinzi naaminsha katika ulimwengu wa roho, kwa hiyo kwa sasa ni walinzi kanisa/malango kutokea kwenye ulimwengu wa roho na si majengo.

Naam huenda yapo maeneo mengine mengi ya ulinzi ndani ya Biblia lakini nimejitahidi kukuonyesha maeneo haya kadhaa ili upate kujua suala la ulinzi ni ajenda muhimu sana kwa Mungu katika kutekeleza kusudi lake hapa duniani.

Hivyo kutokana na maeneo haya tunaelewa kwamba hata leo yapo maeneo mbalimbali ambayo yanahitaji kuwa na walinzi katika ulimwengu wa roho sambamba na haya tuliyojifunza hapa juu. Baadhi ya maeneo mengine yanayohitaji kuwa na walinzi wa kiroho ni; vijiji, familia, kabila, koo, makampuni, mipaka, ndoa, huduma, ardhi (mazao + chakula), maji (vyanzo) bahari, maziwa, mito) nk.

Jambo la msingi – Biblia inasema katika Zaburi127:1b ‘BWANA asipoulinda mji, Yeye aulindaye akesha bure’. Hivyo ili kazi ya mlinzi iwe ya thamani anahitaji kuhakikisha BWANA yupo pamoja naye katika kulinda eneo lake. Naam mlinzi anapaswa kuhakikisha mahusiano yake na BWANA muda wote ni mazuri ili kuruhusu mawasiliano mazuri kati yao. Naam ili kudumisha mawasiliano haya Mlinzi (Walinzi) anapaswa kuzuia chochote ambacho kitaharibu mahusiano yake na BWANA wake vinginevyo kitaondoa uwepo wa BWANA wake kwenye mji wake au eneo lake la ulinzi (asomaye na afahamu).

Tutaendelea na sehemu ya tano…
Katika sehemu inayofuata nitajibu maswali mawili ambayo ni 1) Je Mwanadamu anawezaje kujua kwamba amewekwa kuwa mlinzi wa eneo fulani katika ulimwengu wa roho? 2) Mungu anaposema nimeweka au nimekuweka kuwa mlinzi wa eneo fulani maana yake nini? Majibu ya maswali naamini yataongeza zaidi ufahamu wako juu ya nafasi ya Ulinzi lakini la muhimu zaidi kukusaidia kuelewa nafasi yako ya ulinzi ni ipi na nini ufanye.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu! Wastahili Bwana.

Advertisements

12 comments

 1. Kaka BWANA azidi kukufunulia mengi zaidi ili uzidi kuwa msaada kwa wengine kama kusudi lako la Isaya 58:12 Bwana alivyoliweka ndani yako.

  Like

  • Hello Mercy ubarikiwe sana kwa kufuatilia mfululizo wa somo hili. Kwa wiki kadhaa nilikuwa najiandaa na kufanya mitihani. Namshukuru Mungu nimemaliza na sasa niko huru kufanya kazi hii ya uandishi kwa ajili ya kuujenga mwili wa Kristo. Naamini kabla ya mwisho wa mwezi huu sehemu ya tano itakuwa tayari. Tuzidi kuombeana.

   Like

 2. Mtumishi nakufatilia kila siku ktk mtandao wako. Unanibariki sana kwa mafundisho yako unayoyatoa ktk mtandao wako. Kuna Mafundisho mengine uliyoyatoa hapo nyuma ungefanya yabaki ktk mtandao wako,kwani kuna wakati mtu unakumbuka somo fulani ukitaka kulisoma unakuta hakuna.kama ya vijana uliyofundisha hapo nyuma. Mungu akutie nguvu. NAKULA NA KUKUA KIROHO. Mtumishi: wilfred Tarimo

  Like

  • Hello Wilfred, Mungu akubariki sana kwa kuamua kujifunza kupitia blog hii, nami kadri ninavyoona watu wanaendelea kumjua Mungu kupitia masomo haya ndivyo ninavyopata nguvu za kuandika nikijua kazi yangu si bure. Kwa habari ya masomo hakuna ambayo huwa nayaondoa, yote yapo kwenye blog tangu somo la kwanza nilipoingiza Septemba 2006. Ukiwa kwenye home page ya blog yangu upande wa kushoto kuna categories, unachotakiwa kufanya ingia kwenye category husika kwa mfano ‘Vijana’ itakuletea masomo ambayo nimeyaingiza huko, scroll mpaka chini utaona kuna mshare umeandikwa ‘previous’ entries ukibonyeza hapo itakupeleka kwenye masomo mengine ya nyuma zaidi kwenye category hiyohiyo ya vijana. Barikiwa sana na karibu.

   Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s