USIPOKUWA NA WAZO JIPYA HUWEZI KUTOKA MAHALI ULIPO

Na: Patrick Sanga

Mwaka 2010 nilikwenda Mbeya kwa mapumziko ya likizo na familia yangu. Wakati huo kuna mambo kadhaa nilikuwa nayapitia ambayo yalikuwa yakinipa shida rohoni mwangu na nilitamani kuvuka kutoka hapo na kwenda hatua nyingine bora ya mafanikio. Hivyo nikadumu kumwomba Mungu anifungulie mlango na kunipeleka hatua nyingine. Katika kuendelea kuomba na kutafakari neno la Mungu ndipo nikasikia sauti ndani yangu ikisema ‘usipokuwa na wazo jipya huwezi kutoka mahali ulipo’. Ingawa neno hili lilikuwa jibu kwangu, ilinichukua muda mrefu kuelewa Mungu alimaanisha nini. Ndipo nikaendelea kuomba na kujifunza kutoka kwenye Biblia kuhusu jambo hili pamoja na kusoma vitabu kadha wa kadha. Kwa sababu hii nimeona ni vema nikushirikishe uzoefu wangu ambao nina amini na wewe utakusaidia pia.

Nilijifunza kwamba maamuzi ya mtu ni matokeo ya mawazo yake, na matedo ya mtu ni matokeo ya mawazo anayowaza jumlisha maamuzi anayotekeleza. Naam hii ina maana kwamba, kumbe wazo au mawazo yana nafasi kubwa sana katika kubadilisha maisha ya mtu kwa kumtoa hatua moja na kumpeleka hatua nyingine. Ni muhimu ujifunze kutafuta mawazo mapya ili kubadili maisha yako kuwa bora zaidi ukikumbuka kwamba Mungu anakuwazia mawazo ya amani daima (Yeremia 29:11).

Wazo ni nini?
Wazo ni mpango, lengo, pendekezo, dhana au picha ambayo Mungu, Shetani huweka au kupanda ndani ya mtu (moyoni) ili mtu alifanyie kazi na hivyo kufanikisha makusudi ya ufalme wake hapa duniani. Kama umesoma mfululizo wa masomo yangu juu ya vita vya kiroho ambayo niliandika siku za nyuma nimeeleza kwa upana sana juu ya namna Mungu, Shetani kila mmoja anavyotumia mawazo kuhakikisha makusudi yao yanafanikiwa hapa duniani, na hivyo kufanya vita vya kiroho kuwa vita ya mawazo.

Ukisoma Biblia utagundua kuna vyanzo vitatu vya mawazo navyo ni; kuna mawazo kutoka kwa Mungu (Yeremia 29:11), kuna mawazo kutoka kwa Shetani (2 Wakorinto 4:4) na pia kuna mawazo kutoka kwa mtu au watu (Isaya 65:2). Mwanadamu anapita katika hatua mbalimbali za maisha kama misiba, njaa, magonjwa, dhiki, kushindwa kufikia malengo, hali ngumu kiuchumi nk. Ni furaha sana kwenye ufalme wa giza kuona watoto wa Mungu wanaishi maisha ambayo Mungu hakuwapangia, namaanisha maisha ambayo mtu anaishi nje ya mawazo ya Mungu juu yake. Naam hii ndio kazi anayokazana kuifanya Shetani ya kuwafarakanisha watu na Mungu wao.

Zifuatazo ni hatua zitakazokusaidia kupata wazo jipya la kukutoa katika hali ya maisha ambayo wewe binafsi huridhiki nayo na kukupeleka kwenye eneo bora zaidi kimafanikio;

Hatua ya kwanza – Ni muhimu kujua mahali ulipo sasa
Hili ndio jambo la msingi kabisa la kuanza nalo ili kupata wazo jipya. Kimsingi unatakiwa kujua hali yako ya sasa ya kiroho, kifamilia, kihuduma, kiuchumi, kibiashara, kifamilia, kimahusiano nk. ikoje au ni ya namna gani? Je unaridhika nayo au la? kwa nini huridhiki nayo nk. Hali yako ya sasa ni matokeo ya kuwaza kwako juu ya hilo eneo. Kwa hiyo licha ya kujua mahali ulipo jiulize ni wazo au mawazo gani ambayo yalikufikisha mahali ulipo. Kwa kugha nyingine jiulize kwa nini upo ulivyo?
Yawezekana upo ulipo kwa sababu kuna mawazo fulani yaliingia moyoni mwako nawe ukayatafakari na kisha kuyafanyia kazi na ndio maana umefika mahali ulipo. Kumbuka maisha ya mtu ni matokeo ya mawazo na maamuzi anayotekeleza maishani mwake. Mfano; kutokutoa zaka na sadaka kwa uaminifu (Malaki 3:7-10), kukosa uaminifu, uongo au kumpa ibilisi nafasi nk ni vyanzo vya laana kwenye maisha ya mtu.

Hatua ya pili – Fahamu mahali unapotakiwa au unapotaka kwenda.
Kama huridhiki na hali yako ya sasa ya maisha, hii ina maanisha kuna hali nyingine bora zaidi ambayo unatamani kuifikia. Kwa sababu hii unahitaji kuanza kufikiri au kuwaza ni wapi unataka kwenda/kufika kwa maana ya mafanikio, ni hatua gani ya mafanikio kiroho, kihuduma, kifamilia, kibiashara nk unataka kuifikia maishani mwako? Naam unatakiwa kutoridhika na mazingira uliyonayo ili kuweka kiu ya wazo la kukutoa mahali ulipo.

Hatua ya tatu – Tumia Biblia kama msingi wa kupata mawazo/wazo jipya
Biblia inasema katika Yeremia 29:11 ‘Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho’. Ni muhimu ukafahamu kwamba neno la Mungu ni jumla ya mawazo ya Mungu juu ya namna gani watoto wake wanapaswa kuishi ili kufanikisha maisha yao na kusudi lake hapa duaniani.
Biblia imejaa mawazo mapya toka kwa Mungu (Mithali 16:20, Joshua 1:8, Mithali 20:5). Naam bila kuwa na wazo jipya huwezi kutoka mahali ulipo. Soma kwa kulitafakari neno la Mungu, ndivyo utakavyojua kwa hakika Mungu anakuwazia mawazo ya amani kwenye kila eneo la maisha yako kuliko ulivyokuwa unafikiri.

Hatua ya nne – Jifunze kuwa na muda wa kuwaza
Hili ni jambo ambalo Shetani amefanikiwa kuwafunga watu wengi sana wasiliweke kwenye matendo. Mungu amemuumba mtu kwa namna ambayo kama mtu atakuwa na nidhamu ya kutenga muda kwa ajili ya kuwaza kile ambacho Mungu anaweka kwenye moyo wa mtu, basi maisha ya mwanadamu yangekuwa bora sana licha ya changamoto nyingi zinazomkabili.

Ni muhimu sana kwako kama mtoto wa Mungu kuwa na muda wa KUWAZA. Tafadhali nieleweke vema sijasema muda wa kuomba au kusoma neno, bali muda wa KUWAZA/KUFIKIRI kile Mungu anataka ukifanye hapa duniani kupitia mawazo anayotelemsha moyoni mwako. Jijengee nidhamu hii utaona mabadiliko makubwa sana kwenye kila eneo la maisha yako, anza hata kuwa na dakika kumi na tano, nusu saa, saa moja nk. (Zaburi1:1-2)

Hatua ya tano – Jifunze kufikiri kwa nyakati au ki-muda (1 Nyakati 12:32, Kumbukumbu 32:29, Luka 19:41-45).
Biblia iko wazi katika kitabu cha Mhubiri 3:1 ikisema ‘Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu’. Hii ina maana kila kusudi ambalo mwanadamu amepewa limefungwa kwenye muda na hivyo mwanadamu lazima ajifunze kushirikiana na kuukomboa muda/wakati (Waefeso 5:16) ili maisha yake binafsi yawe na mafanikio lakini pia kusudi la BWANA.
Hivyo tunajifunza kwamba kwa mujibu wa (Mhubiri 3: 1) ili mwanadamu aweze kushirikiana vema na muda, ni lazima ndani yake ajifunze kufikiri ki- muda (thinking in terms of time). Naam kila wazo au kusudi linalokuja moyoni mwake toka kwa Mungu, basi mosi atafute kujua muda wa hilo wazo kutimia ni lini , na pili ajifunze kuweka muda kwa kila mikakati au mipango ambayo anaiweka kwa ajili ya kutekeleza wazo husika. Mfano: Ni imani yangu kwamba Nuhu alipoambiwa tengeneza Safina, ndani yake alipiga mahesbu ya muda unaohitajika kwa ujumla na hivyo kila hatua ya ujenzi akaiwekea muda mpka Safina ilipokamilika.

Naam unahitaji wazo jipya kutoka kwa Mungu ili kutoka mahali ulipo kiroho, kiuchumi, kibiashara nk. Tafuta wazo jipya toka kwa Mungu, naam Kwa mapato yako yote jipatie ufahamu (Mithali 4:7)

Neema ya Kristo iwe nawe daima

Advertisements

15 comments

 1. Ama hakika Mungu ni mwema ketu sote,kwani ni mara ya kwanza kupata somo hili tena kwa intarnet.mungu azidi kukutia nguvu na maarifa katika kutufundisha sisi kondoo wake Amen

  Like

 2. Nimebarikiwa na mafundisho ya wazo jipya kilichobaki niutekelezaji tu, Mungu akubarki mtumishi katika huduma Mungu aliyokuitia.

  Like

 3. Nashukuru kwa ufahamu unaoendelea kuutoa, Roho Mtakatifu azidi kukuongoza na Mungu akupe ujuzi wa rohoni wa kulisha wana wa Mungu. kikubwa Mungu atupe utii.

  Like

 4. Mungu akubariki sana mtumishi wa Mungu.nimefarijika kupata blog yako kwani nimejifunza hapa jambo kubwa ktk maisha

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s