Archive for May 2012

NAMNA MWANAMKE ANAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI ZAKE KUBADILISHA MAISHA YA NDOA YAKE (Part 2)

May 20, 2012

Na: Patrick Sanga

Maada: Nafasi ya Msaidizi, Mshauri na Mleta kibali  

Ili kusoma sehemu ya kwanza bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2012/03/01/namna-mwanamke-anavyoweza-kutumia-nafasi-zake-kubadilisha-maisha-ya-ndoa-yake/

Mpenzi msomaji, Mungu akubariki kwa kufuatilia mfululizo wa somo hili. Ni imani na maombi yangu kwamba masomo haya yatafanyika msaada kwenye maisha yako na ndoa yako kwa ujumla. Katika sehemu hii ya pili nitaandika kuhusu nafasi tatu ambazo ni nafasi ya Mwanamke kama Msaidizi, Mshauri na Mleta kibali.

Mwanamke kama Msaidizi

Mwanzo 2:18 ‘BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye’.  Ukisoma mstari huu katika toleo la GNB Biblia inasema ‘Then the LORD God said, “It is not good for the man to live alone. I will make a suitable companion to help him.” Biblia inatueleza kwamba Adam ndiye aliyetangulia kwanza kudhihirishwa kabla ya Mwanamke. Kabla ya Hawa kuletwa, Mungu alimpa Adam majukumu mengi ambayo alipaswa kuyatekeleza.

Katika kutekeleza majukumu yake Adam aliona kwamba amepungukiwa mwenza wa kufafanana naye na ndani yake akatamani angepata mtu wa kuwa naye karibu kwa kila afanyalo. Ukweli huu tunaupata tukisoma Mwanzo 2:20 kwamba ‘Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. Naam kutokana na upweke wa Adam ndipo Mungu akamfanya Hawa mkewe kama msaidizi. Kitendo cha Mungu kumfanya mwanamke kama msaidizi ni ishara kwamba Mungu alijua kuwa Adam hawezi kuwa na ufanisi mzuri katika kutekeleza majukumu (Kusudi) aliyopewa bila mwenza wa kufanana naye.

Maandiko yanasema kwamba ‘Maana mwanaume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke katika mwanaume. Wala mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanaume’ (1Wakorinto 11:8-9).  Ile kwamba mwanamke aliumbwa kutoka kwa mwanaume na kwa ajili ya mwanaume ni kuonyesha kwamba wajibu au nafasi mojawapo ya mwanamke ni kuwa msaidizi wa mumewe. Hata hivyo neno msaidizi halipaswi kutafsiriwa vibaya na kuonyesha kwamba mwanamke hana thamani.

Mwanamke ni msaidizi wa mume katika kulitumikia kusudi la Mungu isipokuwa kinacho watofautisha ni utendaji wao tu. Mume hapaswi kumdharau mkewe wala mke kumdharau mumewe kwa kuwa mume si mume bila mke na mke si mke bila mume, wao ni mwili mmoja, kusudi lao ni moja na BWANA wao ni mmoja.   Maandiko yafuatayo yanaonyesha baadhi ya mambo ambayo mwanamke anapokuwa katika nafasi ya Msaidizi anapaswa kuyafanya;

Tito 2:4 inasema ‘Ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao, na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe’.

1 Timotheo 5: 14 ‘Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu’. Ukisoma pia katika 1 Wakorinto7:4a kwa habari ya tendo la ndoa Biblia inasema ‘Mke hana amri juu ya mwili wake…’ na mstari wa 5a unasema’ Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda…, Naam hii ina maana kama mke ataweka amri kwa habari ya tendo la ndoa kwa mumewe ajue kabisa ameshindwa kumsaidia mumewe na kuna hatari ya kuanguka kwenye zinaa. Naam Mungu anataka akina mama walioko kwenye ndoa wajifunze kuwasaida waume zao wasiingie kwenye zinaa.

Naam hata sasa ni muhimu sana wewe mama ukajua Mungu amewaunganisha ili kufanya nini hapa duniani kwa ajili ya ufalme wake. Changamoto kubwa iliyipo leo ni kwamba wanandoa wengi wameingia kwenye ndoa kwa sababu ni desturi ya wanadamu kuoa na kuolewa. Wengi wameshindwa kuunganisaha suala la kuoa au kuolewa na kumtumikia Mungu kupitia ndoa yao. Mungu anapokuunganisha na mumeo maana yake anakupeleka kwenye wajibu wa kuwa msaidizi kwa mumeo. Naam hakikisha kwamba unafanyika msaada kwa mumeo kwa namna ambayo kile ambacho mnajua kwamba Mungu amewapa kukifanya hapa duniani kinafanikiwa. Zaidi unaweza soma Mithali 31:10-31 ili kuongeza ufahamu zaidi kuhusu nafasi ya mwanamke kama Msaidizi.

Mwanamke kama Mshauri

Katika hali ya kawaida watu wengi hutafsiri mshauri kuwa msiaidizi. Kwa kuzingatia dhana ya nafasi katika ulimwengu wa roho imenilazimu kutenganisha ili kukuonyesha umuhimu wa nafasi ya mwanamke kama Mshauri. Biblia katika Mithali 31:26 inasema ‘Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake’.

Naam andiko hili linatupa kujua kwamba Mke ndiye mshauri mkuu wa mumewe. Siri moja ya mwanamke kuwa mshauri mzuri ni kuwa na ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu. Hivyo kama Mke hana hekima itokanayo na neno la Mungu kwa wingi ndani yake, hawezi kuwa mshauri mzuri. Ushauri unategemea nguvu za ufahamu alizonazo Mwanamke, kadri anavyokuwa na ufahamu wa kutosha wa neno ndivyo anavyokuwa kwenye nafasi ya kutoa ushauri bora kwa mumewe.

Biblia katika kitabu cha Mithali 8: 14-16 inasema ‘Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu na mimi nina nguvu. Kwa masada wangu wafalme humiliki, Na wakuu wanahukumu haki. Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia’. Fahamu kwamba hekima ndani yako mama itakupa maarifa na ufahamu wa kumshauri mumeo ili kufanya maamuzi sahihi katika kila atendalo. Hekima ni sawasawa na   shauri/maarifa/ufahamu/nguvu. Ukiona kiongozi yoyote anatawala/anaongoza watu vizuri ujue washauri wake wanamshauri vizuri au ujue ana wahsauri wazuri. Vivyo hivyo mwanaume anafanya kazi zake vema na kufanikiwa katika yale atendayo ujue nyuma yake kuna mwanamke mwenye nguvu za ufahamu anayemshauri vema.

Naam chanagmoto au matatizo mengi yaliyopo kwenye ndoa leo ni matokeo ya akina mama kukosa hekima itokanayo na neno la Mungu ya kuwashauri waume zao. Wengi wanategemea akili zao, au ushauri wa rafiki zao nk. katika kuangalia ndoa zao na mambo yao yaendaje. Kutegemea ushauri wa watu wengine bila wewe mwenyewe mama kutafuta hekima itokanyo na Mungu kwanza inaweza kukufikisha kupata ushauri wa kipepo kama ilivyomtokea Hawa pale Bustanini. Kumbuka Mshauri ni mtoa taarifa, mtoa pendekezo juu ya nini mume wake aweza fanya au kutofanya.

Mwanamke kama mleta kibali.

Hii ni nafasi ya ajabu sana ambayo Mungu amempa mwanamke. Mwanamke anapokuwa kwenye hii nafasi mambo matatu yanafanyika; 1) Mume anaingia kwenye ngazi ya kushirikishwa siri/mambo/majukumu mengi kutoka kwa BWANA. 2) Kukubalika kwa mume wake katika jamiii/kazi/kanisa nk kunaongezeka 3) Na mwisho maombi ya mume wake yanasikilizwa. Mambo haya yanathibitishwa na Biblia katika  Mithali 18:22 inayosema ‘Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA’, pia   Mithali 31: 23 inayosema ‘Mume wake hujulikana malangoni; Aketipo pamoja na wazee wa nchi’

Zaidi kwa habari ya maombi ya mume kusikilizwa au kutokusikilizwa Biblia katika      1 Petro 3:7 inasema ‘Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe’. Naam hii ni ishara kwamba mke anaweza kusababisha maombi ya mumewe yakasikilizwa au yasisikilzwe. Unaweza ukafikiri hili andiko linawahusu akina baba pekee, lakini ukilitafakari kwa upana utagundua kwamba linawahusu akina mama pia ili wajue kwamba kuwa mke ni nafasi ambayo inaweza kuzuia maombi/baraka/majibu au kukwamisha mafanikio ya waume zao kama hawatukuwa makini katika kuwasaidia waume zao kuishi nao kwa akili.

Si wengi wanaojua kwamba kuna maombi mengi ya familia/waume zao hayajibiwi kwa sababu maombi ya mume ambaye ndiye kichwa hayasikilizwi na Mungu. Na chanzo cha kutokusikilizwa ni kuharibika kwa uhusiano kati ya mume na ‘mleta kibali’ wake yaani mke. Hivyo wewe mama mwenye ufahamu huu jifunze kwenda mbele za Mungu na kuomba toba kwa ajili ya mumeo mara kwa mara. Kwa sababu kuna vitu au maamuzi anayoweza kufanya nay eye akaona yuko sahihi lakini kumbe ni uamuzi ambao unajenga ukuta kati ya maombi yake na Mungu wako.

Hakikisha unasimama vema kwenye hii nafasi ili Mungu alete uponyaji kwa mume wako na maombi yake yaweze kusikilizwa. Naam simama kwenye nafasi yako ili kumjengea mazingira mazuri mumeo ya kuishi na wewe, ndivyo na maombi yake yatakavyosikilizwa, ndivyo atakavyopata kibali mbele za BWANA, naam atakuwa mume bora katika jamii na kufanikiwa katika kila atendalo.

Tamati endapo mwanamke atakaa vizuri kwenye nafasi hizi haijalishi mume wake ni mgumu kiasi gani, mama akizungumza kwa maana ya maonyo au ushauri lazima mwanaume asikilize au kufuata kile ambacho msaidizi, mlinzi, mleta kibali wake nk anamweleza, na kama akikataa uharibifu ni haki yake. Mungu ameweka sauti ndani ya mwanamke ambayo inaweza kuleta uponyaji kwa mumewe endapo mwanamke atakaa vizuri kwenye hizi nafasi.

Ubarikiwe, tutaendelea na sehemu ya tatu…

Asomaye na afahamu!

 

USIPOKUWA NA WAZO JIPYA HUWEZI KUTOKA MAHALI ULIPO

May 17, 2012

Na: Patrick Sanga

Mwaka 2010 nilikwenda Mbeya kwa mapumziko ya likizo na familia yangu. Wakati huo kuna mambo kadhaa nilikuwa nayapitia ambayo yalikuwa yakinipa shida rohoni mwangu na nilitamani kuvuka kutoka hapo na kwenda hatua nyingine bora ya mafanikio. Hivyo nikadumu kumwomba Mungu anifungulie mlango na kunipeleka hatua nyingine. Katika kuendelea kuomba na kutafakari neno la Mungu ndipo nikasikia sauti ndani yangu ikisema ‘usipokuwa na wazo jipya huwezi kutoka mahali ulipo’. Ingawa neno hili lilikuwa jibu kwangu, ilinichukua muda mrefu kuelewa Mungu alimaanisha nini. Ndipo nikaendelea kuomba na kujifunza kutoka kwenye Biblia kuhusu jambo hili pamoja na kusoma vitabu kadha wa kadha. Kwa sababu hii nimeona ni vema nikushirikishe uzoefu wangu ambao nina amini na wewe utakusaidia pia.

Nilijifunza kwamba maamuzi ya mtu ni matokeo ya mawazo yake, na matedo ya mtu ni matokeo ya mawazo anayowaza jumlisha maamuzi anayotekeleza. Naam hii ina maana kwamba, kumbe wazo au mawazo yana nafasi kubwa sana katika kubadilisha maisha ya mtu kwa kumtoa hatua moja na kumpeleka hatua nyingine. Ni muhimu ujifunze kutafuta mawazo mapya ili kubadili maisha yako kuwa bora zaidi ukikumbuka kwamba Mungu anakuwazia mawazo ya amani daima (Yeremia 29:11).

Wazo ni nini?
Wazo ni mpango, lengo, pendekezo, dhana au picha ambayo Mungu, Shetani huweka au kupanda ndani ya mtu (moyoni) ili mtu alifanyie kazi na hivyo kufanikisha makusudi ya ufalme wake hapa duniani. Kama umesoma mfululizo wa masomo yangu juu ya vita vya kiroho ambayo niliandika siku za nyuma nimeeleza kwa upana sana juu ya namna Mungu, Shetani kila mmoja anavyotumia mawazo kuhakikisha makusudi yao yanafanikiwa hapa duniani, na hivyo kufanya vita vya kiroho kuwa vita ya mawazo.

Ukisoma Biblia utagundua kuna vyanzo vitatu vya mawazo navyo ni; kuna mawazo kutoka kwa Mungu (Yeremia 29:11), kuna mawazo kutoka kwa Shetani (2 Wakorinto 4:4) na pia kuna mawazo kutoka kwa mtu au watu (Isaya 65:2). Mwanadamu anapita katika hatua mbalimbali za maisha kama misiba, njaa, magonjwa, dhiki, kushindwa kufikia malengo, hali ngumu kiuchumi nk. Ni furaha sana kwenye ufalme wa giza kuona watoto wa Mungu wanaishi maisha ambayo Mungu hakuwapangia, namaanisha maisha ambayo mtu anaishi nje ya mawazo ya Mungu juu yake. Naam hii ndio kazi anayokazana kuifanya Shetani ya kuwafarakanisha watu na Mungu wao.

Zifuatazo ni hatua zitakazokusaidia kupata wazo jipya la kukutoa katika hali ya maisha ambayo wewe binafsi huridhiki nayo na kukupeleka kwenye eneo bora zaidi kimafanikio;

Hatua ya kwanza – Ni muhimu kujua mahali ulipo sasa
Hili ndio jambo la msingi kabisa la kuanza nalo ili kupata wazo jipya. Kimsingi unatakiwa kujua hali yako ya sasa ya kiroho, kifamilia, kihuduma, kiuchumi, kibiashara, kifamilia, kimahusiano nk. ikoje au ni ya namna gani? Je unaridhika nayo au la? kwa nini huridhiki nayo nk. Hali yako ya sasa ni matokeo ya kuwaza kwako juu ya hilo eneo. Kwa hiyo licha ya kujua mahali ulipo jiulize ni wazo au mawazo gani ambayo yalikufikisha mahali ulipo. Kwa kugha nyingine jiulize kwa nini upo ulivyo?
Yawezekana upo ulipo kwa sababu kuna mawazo fulani yaliingia moyoni mwako nawe ukayatafakari na kisha kuyafanyia kazi na ndio maana umefika mahali ulipo. Kumbuka maisha ya mtu ni matokeo ya mawazo na maamuzi anayotekeleza maishani mwake. Mfano; kutokutoa zaka na sadaka kwa uaminifu (Malaki 3:7-10), kukosa uaminifu, uongo au kumpa ibilisi nafasi nk ni vyanzo vya laana kwenye maisha ya mtu.

Hatua ya pili – Fahamu mahali unapotakiwa au unapotaka kwenda.
Kama huridhiki na hali yako ya sasa ya maisha, hii ina maanisha kuna hali nyingine bora zaidi ambayo unatamani kuifikia. Kwa sababu hii unahitaji kuanza kufikiri au kuwaza ni wapi unataka kwenda/kufika kwa maana ya mafanikio, ni hatua gani ya mafanikio kiroho, kihuduma, kifamilia, kibiashara nk unataka kuifikia maishani mwako? Naam unatakiwa kutoridhika na mazingira uliyonayo ili kuweka kiu ya wazo la kukutoa mahali ulipo.

Hatua ya tatu – Tumia Biblia kama msingi wa kupata mawazo/wazo jipya
Biblia inasema katika Yeremia 29:11 ‘Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho’. Ni muhimu ukafahamu kwamba neno la Mungu ni jumla ya mawazo ya Mungu juu ya namna gani watoto wake wanapaswa kuishi ili kufanikisha maisha yao na kusudi lake hapa duaniani.
Biblia imejaa mawazo mapya toka kwa Mungu (Mithali 16:20, Joshua 1:8, Mithali 20:5). Naam bila kuwa na wazo jipya huwezi kutoka mahali ulipo. Soma kwa kulitafakari neno la Mungu, ndivyo utakavyojua kwa hakika Mungu anakuwazia mawazo ya amani kwenye kila eneo la maisha yako kuliko ulivyokuwa unafikiri.

Hatua ya nne – Jifunze kuwa na muda wa kuwaza
Hili ni jambo ambalo Shetani amefanikiwa kuwafunga watu wengi sana wasiliweke kwenye matendo. Mungu amemuumba mtu kwa namna ambayo kama mtu atakuwa na nidhamu ya kutenga muda kwa ajili ya kuwaza kile ambacho Mungu anaweka kwenye moyo wa mtu, basi maisha ya mwanadamu yangekuwa bora sana licha ya changamoto nyingi zinazomkabili.

Ni muhimu sana kwako kama mtoto wa Mungu kuwa na muda wa KUWAZA. Tafadhali nieleweke vema sijasema muda wa kuomba au kusoma neno, bali muda wa KUWAZA/KUFIKIRI kile Mungu anataka ukifanye hapa duniani kupitia mawazo anayotelemsha moyoni mwako. Jijengee nidhamu hii utaona mabadiliko makubwa sana kwenye kila eneo la maisha yako, anza hata kuwa na dakika kumi na tano, nusu saa, saa moja nk. (Zaburi1:1-2)

Hatua ya tano – Jifunze kufikiri kwa nyakati au ki-muda (1 Nyakati 12:32, Kumbukumbu 32:29, Luka 19:41-45).
Biblia iko wazi katika kitabu cha Mhubiri 3:1 ikisema ‘Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu’. Hii ina maana kila kusudi ambalo mwanadamu amepewa limefungwa kwenye muda na hivyo mwanadamu lazima ajifunze kushirikiana na kuukomboa muda/wakati (Waefeso 5:16) ili maisha yake binafsi yawe na mafanikio lakini pia kusudi la BWANA.
Hivyo tunajifunza kwamba kwa mujibu wa (Mhubiri 3: 1) ili mwanadamu aweze kushirikiana vema na muda, ni lazima ndani yake ajifunze kufikiri ki- muda (thinking in terms of time). Naam kila wazo au kusudi linalokuja moyoni mwake toka kwa Mungu, basi mosi atafute kujua muda wa hilo wazo kutimia ni lini , na pili ajifunze kuweka muda kwa kila mikakati au mipango ambayo anaiweka kwa ajili ya kutekeleza wazo husika. Mfano: Ni imani yangu kwamba Nuhu alipoambiwa tengeneza Safina, ndani yake alipiga mahesbu ya muda unaohitajika kwa ujumla na hivyo kila hatua ya ujenzi akaiwekea muda mpka Safina ilipokamilika.

Naam unahitaji wazo jipya kutoka kwa Mungu ili kutoka mahali ulipo kiroho, kiuchumi, kibiashara nk. Tafuta wazo jipya toka kwa Mungu, naam Kwa mapato yako yote jipatie ufahamu (Mithali 4:7)

Neema ya Kristo iwe nawe daima