WAANDISHI TUSILALE, BADO KUNA WAJIBU MKUBWA MBELE YETU

Na: Patrick Sanga

Waraka wa Januari

Katika mwezi huu wa Januari nimeona vema niandike ujumbe huu kwa lengo la kuwatia moyo waandishi wengine mbalimbali wa masomo ya Biblia na yeyote ambaye ndani yake anasikia wito wa kumutumikia Mungu kwa njia hii ya uandshi. Kwa hakika namshukuru Mungu kwa neema yake ya ajabu aliyonijalia katika suala zima la uandishi wa masomo mbalimbali ya kiroho.

Binafsi nimenza kuandika masomo mbalimbali ya kiroho mwaka 2003. Ingawa kwa wakati huo sikuwa na ufahamu wa masula ya ‘blogs’ hata kidogo. Ilipofika mwaka 2004 ndipo wazo la kuweka masomo kwenye mtandao lilipoingia ndani yangu. Naam nilikaa nalo kwa miaka miwili nikitakafari nitaanzaje na hasa kwa kuwa wakati huo nilikuwa bado nasoma.

Mwaka 2006 nilikwenda Kenya kwa lengo la kujifunza mambo kadha wa kadha ya kihuduma. Tukiwa mji wa Garisa karibu na mpaka wa Somalia, Bwana kwa namna ya pekee sana alimtumia mwenyeji wangu, Mchungaji Patrick Nabwera kunifundisha habari za ukweli kuhusu kuzimu ‘The Doctrine of Hell’. Naam Bwana Yesu aliniambia ‘watu wengi sana wanaenda kuzimu baada ya kufa kwa kuwa hawanijui mimi’.

Ujumbe huu ulipenya ndani yangu kwa uzito wa kipekee mno, ndipo nikaazimia kwamba nitafanya kila ninaloweza kuhakikisha watu wanamjua Mungu. Baada ya kurudi Nairobi (Mji Mkuu wa Kenya), nikakutana na kaka mmoja aitwaye ‘Jersey’ nikamweleza nia yangu ya kuandaa masomo na kuweka masomo kwenye mtandao. Ndipo Jersey akanieleza kwa habari ya blog, akanielekeza namna ya kufanya  na kisha akanifungulia blog hii.

Tangu wakati huo nimeendelea kuandaa masomo na kuyaweka kwenye blog zangu (Kiswahili na kiingereza). Mpaka sasa nimefanikiwa kuweka kwenye blog hizi wastani wa masomo mia moja na ishirini. Hata hivyo yapo masomo mengine mengi ambayo nimeshaandaa lakini sijweka kwenye blog hizi kwa kuwa mengine ni kwa ajili yangu na mengine muda wake bado.

Suala zima la unadishi kwangu halijawa jepesi kama vile mtu asiyejua wajibu huu anavyoweza kudhani. Nimekuwa nikikutana na changamoto (upinzani) nyingi sana zenye kunifanya nikate tamaa.  Mara kadhaa huko nyuma niltamani kuacha kabisa kuaanda masomo, kwani adui alikuwa akileta upinzani na mawazo kwamba hakuna faida yoyote ya kuandika masomo haya, ni kupoteza muda wangu ambao ningetumia kufanya mambo mengine. Jambo hili lilinitesa kwa muda lakini nikakumbuka kile ambacho Paulo alimwambia Timotheo kusema ‘ Mambo hayo uyaagize na kuyafundisha’ — hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma, na kuonya na kufundisha (1 Timotheo 4:11, 13). Kwa hakika neno hili lilinipa nguvu ya kuendelea kuandika masomo.

Ili kuthibitisha kwamba Bwana Yesu anaithamini kazi yetu, Mungu alisema nami kwa njia ya ndoto kupitia ushuhuda ufuatao.  Julai 2009, miaka miwili baada ya kufungua blog hii, siku ya Jumamosi nilitulia nyumbani kwangu kwa muda wa saa nane mfululizo nikiaandaa masomo mbalimbali. Usiku wa siku hiyo nilipolala nikaota ndoto nimechkuliwa hadi mbinguni. Nilipofika, Malaika mmoja akanichukua na kunipeleka kwenye chumba kimoja kizuri umbile lake kwa ndani ni kama duara (mviringo). Ndani ya chumba hiki kulikuwa na mfano wa makabati ya chuma yenye milango miwili ambayo yamejengwa kwenye ukuta kufuata ule mzunguko. Ndipo yule Malaika akaenda na kufungua kabati mojawapo na kuanza kutoa mfano wa karatasi ambazo zimeandikwa na kunipa.

Punde tu baada ya kufungua ile kabati, ghafla nikaanza kuona picha ya jinsi nilivyokuwa pale nyumbani naandaa masomo, mchana wa siku hiyo. Naam kadri nilivyokuwa nikiandaa masomo na kumaliza, yule Malaika alikuwa alikuwa akitoa somo kwenye kabati na kunipa. Kwa hiyo nikawa naona maeneo yote mawili, yaani kile mimi ninachofanya duniani na kile Malaika anachofanya huku mbinguni. Naam uaminifu na uharaka wangu katika kuandaa masomo ndio uliomfanya yule Malaika kuyatoa kwenye kabati uharaka na wakati pia.

Kitu cha kushangaza ni kwamba kila baada ya idadi kadhaa ya masomo kutimia, niliona yule Malaika anatoa ‘kikapu’ kitupu anaweka pembeni na kisha anasogeza kingine na zoezi la kutoa masomo likaendelea. Kwa hakika nilishangaa sana kujua kwamba kumbe kuna uhusiano kati ya kile ninchofanya na mbinguni. Nilipokuwa katika kutafakari neno hili, ndipo yule Malaika akaniambia ‘bado kuna vikapu vingi vya masomo vinakungoja’. Nami nikashtuka na kujua kwamba Mungu amesema nami kwa njia ya ndoto na kuonyesha namna anavyothamini kile ninchofanya. Kwa hakika mbinguni kuna ‘store’ kubwa ya masomo ambayo Mungu amekusudia kuyateremsha kwa watoto wake duniani kupitia waandishi. Ndoto hii ilinifanya nikakumbuka maneno ya Yesu aliposema ‘… Kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale (Mathayo 13:52’.

Kwa hakika maono haya na kile ambacho sasa naona Mungu anafanya kwa watu wake kupitia masomo haya, siku zote hunitia nguvu za kuandika na kuandika na kuandika masomo kwa ajili ya kuujenga mwili wa Kristo.

Waandishi wenzangu na kila mwenye kuandaa masomo kwa ajili ya kuulisha mwili wa Kristo yafuatayo ni mambo kadhaa ambayo ni muhimu kujua na kuzingatia kadri tunavyoendelea kufanya kazi hii;

 • Mungu anaithamini kazi yetu. Najua kazi hii ilivyo na changamoto nyingi, lakini changamoto hizo zisikufanye ushindwe kuandika masomo kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Usikate tama, vumilia na endelea kufanya kazi ya Mungu maadam ni mchana ukitumia kipawa hiki cha pekee kwa utukufu wa Mungu na kwa uongozi wake.
 • Kile tunachoandika katika mapenzi ya Mungu kwa hakika kinafanyika msaada na uponyaji wa watu wake aliowakusudia. Usije ukafikiri unapoteza muda kwa kuandika, hapana. Maadam unaandika kwa uongozi wa Mungu uwe na uhakika kuna uponyaji mkubwa sana unatembea kupitia ujumbe huo.
 • Mungu anataka tujifunze kuwa na muda maalum wa kutulia kufanya kazi hii, na sio kufanya kwa mazoea. Kulingana na ratiba zangu za kazi mimi hutumia vema siku za mapumziko kuandaa masomo. Fahamu kwamba endapo Mungu amekuita umtumikie kwa njia hii, ‘kutoandika masomo kwa wakati ni kosa kubwa sana na ni kumpa adui nafasi ya kuharibu watoto wa Mungu kwa mafundisho ya uongo’. Mungu anataka tuipe kazi hii umuhimu kama tunavyofanya kwenye kazi nyingine.

Mwandishi mwenzangu, kuna vikapu vya masomo vinakusubiri. Katika nyumba ya Mungu kuna hazina ya kutosha ya masomo kwa ajili ya watoto wake hapa duniani. Ili aweze kuyateremsha, Mungu anakuhitaji wewe Mwandishi, ukae kwenye nafasi yako maana ndani yako ameweka kipawa cha uandishi. Jambo moja ambalo nimelithibitisha ni kwamba hakuna mwisho wa kuandika, ila kila mwandishi ana vikapu vyake, ana fungu lake, ana masomo yake ambayo anapswa kushirikiana na Roho Mtakatifu ili yaachiliwe katika nyakati zilizokubaliwa na yatunzwe kama kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili Bwana.

Advertisements

13 comments

 1. Bwana Yesu Asifiwe.
  Kipekee namshukuru Mungu sana kwa Ujumbe huu kwa waandishi.
  Ukweli ni kwamba kupitia waandishi tunabarikiwa sana kwa ujumbe ambao
  Mungu ametuma kupitia kwenu, hakika zinatujenga na kutubadilisha. Tunafunguliwa ufahamu wetu na roho zetu zinauhishwa kwa upya.
  Changamoto zipo ila zisiwakatishe tamaa. Kazi ya Mungu lazima isonge mbele.
  Mungu awabariki na azidi kuwatumia katika kazi yake kama yeye apendavyo.
  Amina.

  Like

  • Ahsante sana dada Stella kututia moyo katika kazi hii, tunahitaji maombi yenu ili tuandike kwa kadri ya uongozi wa Mungu mwenyewe. Mungu akubariki kwa kupenda kusoma na kufuatilia yale ambayo tunaandika, kwetu tunapata nguvu ya kuandika tunapoona masomo haya yanafanyika msaada kwa wasomaji.

   Like

 2. Ubarikiwe sana Patrick kwa mafundisho mazuri. Binafsi mafundisho ninayoyapata kwako na kwa waandishi wengine kwa njia hii ya mtandao yamekuwa msaada mkubwa sana kupata maarifa ya ki-Mungu. Si hilo tu mafundisho haya yamekuwa pia msaada kwa familia yangu na kwa watu wengine wa karibu ninaoweza kuwashikisha kujifunza. Nimekuwa nikiwaprintia wenzangu ambao hawana access na mtandao, nami pamoja nao tumekuwa tukijifunza na kubarikiwa.

  Nawatia moyo waandishi kuwa mwendelee kusonga mbele licha ya changamoto kadha wa kadha mnazokumbana nazo, Mungu mwenyewe atawawezesha kuzikabili. Neno la Mungu linasema kuwa tunayaweza mambo yote katika YEYE atutuiaye nguvu (Wafilipi 4:13). Kisha mkitambua kuwa shetani anateseka na hapendi watu wa Mungu wanapopewa maarifa kwa kuwa anashindwa kuwaangamiza. Yesu mwenyewe aliwahi kusema kuwa watu wanapotea kwa kuwa hawajui maandiko wala uweza wa Mungu.

  Ndugu yangu Patrick endelea kuvaa silaha zote za MUNGU ili uweze kuzipinga hila la shetani. MUNGU atakuwezesha kuzikabili changamoto zote na huduma yako itasimama (Efeso 6:10-13) na utaendelea kufanyika baraka.

  Like

  • Amina dada Martha kwa hakika ubarikiwe kwa huduma yako ya kuhakikisha kwamba hata wale wasio na access ya mtandao wanayapata masomo haya, naam kwa hakika Mungu anaithamini kazi yetu Waandishi, ahsante kwa maombi yako juu yetu Waandishi, usiache kutuombea, nasi kwa msaada wa Mungu hatutaacha kuandika, ila maombi yenu ni muhimu sana ili tuandike kwa kadri ya uongozi wa Roho wa Mungu.

   Like

 3. Mtumishi, TYK wa Nazareti aliye hai.

  Mimi namshukuru Mungu katika Kristo Yesu. Tafadhali sana Mtumishi wa Mungu ninaomba somo lisemalo IJUE NGUVU YA MSALABA.

  Ahsante,

  Mariam. Udsm.

  Like

 4. Nimesikia ndani yangu kutoa machozi kwa ujumbe ulioandika nimejiona kama ulikuwa unaongea na mimi binafsi kupitia ujumbe huu, nakumbuka nami pia hivi kalibuni nilikuwa napata mafundisho na kupewa msukumo fulani wa Roho Mtakatifu, ila nikakatishwa tamaa sio ya kawaida, nilivunjika moyo mno mno ila najisikia kuamka tena na kuinuka na kuendelea na safari hii pamoja na Roho Mtakatifu. Mungu Akubariki Mtumishi wa Mungu.

  Like

  • Ndugu Twaha namshukuru Mungu kwa ujumbe wako huu, binafsi nimeelewa vema kile unachomaanisha kwani uandishi ni sehemu ya maisha yangu,nakusihi kwa sababu iwayo yote usikate tamaa, hakikisha kila ambacho Mungu anakuletea ndani yako unakiandika na kukitunza vizuri ukisubiri maelekezo ya Mungu zaidi kuhusu ujumbe huo. Mungu akubariki, narudia tena usikate tamaa.

   Like

 5. Hello! Patrick,

  Ubarikiwe sana kwa huduma yako hii. Ni ukweli usiopingika kuwa huduma ya kuwafikia watu kwa njia ya maadishi (kuandika vitabu…) ni muhimu sana na yenye mguso. Sisi (nami pia ni mwandishi wa vitabu) kama waandishi tunapaswa tuwaombee watu wasome vitabu. Kuna roho fulani ya kishetani inayowafunga watu wasione umuhimu wa kusoma vitabu na hivyo kutununua. Tuombe Bwana awafungue na wayapate maarifa haya ‘wasiangamizwe’. Nakutia moyo songa mbele with time mambo yatzidi kubadilika kuwa mazuri zaidi kwa walengwa.

  Bless you so much!

  Noel Kihoza!

  Like

  • Ndugu Noel, Mungu akubariki kwa kutembelea blog hii na kutoa comment zako, maana najua kazi yetu ni moja katika mwili wa Kristo, ahsante kwa maombi yako na kunitia moyo. Ni wazi kwamba adui hapendi watu wapate maarifa kwa njia ya kusoma maana anajua ‘apendaye mafundisho hupenda maarifa’. Ni imani yangu kwamba Mungu ataendelea kufungua watu na kuwasaidia wapende kusoma yale ambayo waandishi wanaandika kwa lengo la kuujenga mwili wa Kristo.

   Like

 6. Asante Mtumishi wa Bwana Sanga kwa ujumbe wako mzuri wa kunitia moyo nitafanya kama ulivyonishauri nitaendelea kuandika na kusubiri maelekezo zaidi kutoka kwa Mungu, pia nashukuru Mungu kwa kuikamata channel tena ilikuwa imenipotea nimeipata tena ila ilinighalimu, anayejidhania kuwa amesimama na aangalie ASIANGUKE, watumishi tuko vitani tusijisahau adui yetu akati tamaa anarusha vikombora vyake ili atupate, Mungu aliye mlinzi wa Israel yupo pamoja nasi. Mungu ibariki Blog yetu hii ionekane kila mahali Duniani ili adui asipate mtu ikiwezekana aende peke yake MOTONI.

  Like

  • Hizi ni habari njema sana ndugu Emmanueli kwa Bwana Mungu kukuwezesha na wewe kukubali na kuamua kuendelea kuandika na kuandaa masomo kwa ajili ya kuujenga mwili wa Kristo. Naam ndugu yangu na tufanye kazi ya Bwana wetu maadam ni mchana, tena kwa bidii ili hata tutakapofika mbinguni, Bwana atuambie mlifanya kazi nzuri sana ‘Package’ ya masomo iliyokuwa kwenye vikapu vyenu mmeimaliza kwa wakati wenu wa duniani, njooni mpumzike pamoja na watakatifu wenzenu na waandishi wenzenu, naamini itakuwa njema sana kuonana na kina Musa, Daudi, Paulo, Yohana nk. Utukufu na heshima vina Mungu Roho Mtakatifu mwenye kutuongoza kuandika kwa kadri ya mapenzi yake. Tuzidi kuombeana.

   Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s