Archive for January 2012

WAANDISHI TUSILALE, BADO KUNA WAJIBU MKUBWA MBELE YETU

January 21, 2012

Na: Patrick Sanga

Waraka wa Januari

Katika mwezi huu wa Januari nimeona vema niandike ujumbe huu kwa lengo la kuwatia moyo waandishi wengine mbalimbali wa masomo ya Biblia na yeyote ambaye ndani yake anasikia wito wa kumutumikia Mungu kwa njia hii ya uandshi. Kwa hakika namshukuru Mungu kwa neema yake ya ajabu aliyonijalia katika suala zima la uandishi wa masomo mbalimbali ya kiroho.

Binafsi nimenza kuandika masomo mbalimbali ya kiroho mwaka 2003. Ingawa kwa wakati huo sikuwa na ufahamu wa masula ya ‘blogs’ hata kidogo. Ilipofika mwaka 2004 ndipo wazo la kuweka masomo kwenye mtandao lilipoingia ndani yangu. Naam nilikaa nalo kwa miaka miwili nikitakafari nitaanzaje na hasa kwa kuwa wakati huo nilikuwa bado nasoma.

Mwaka 2006 nilikwenda Kenya kwa lengo la kujifunza mambo kadha wa kadha ya kihuduma. Tukiwa mji wa Garisa karibu na mpaka wa Somalia, Bwana kwa namna ya pekee sana alimtumia mwenyeji wangu, Mchungaji Patrick Nabwera kunifundisha habari za ukweli kuhusu kuzimu ‘The Doctrine of Hell’. Naam Bwana Yesu aliniambia ‘watu wengi sana wanaenda kuzimu baada ya kufa kwa kuwa hawanijui mimi’.

Ujumbe huu ulipenya ndani yangu kwa uzito wa kipekee mno, ndipo nikaazimia kwamba nitafanya kila ninaloweza kuhakikisha watu wanamjua Mungu. Baada ya kurudi Nairobi (Mji Mkuu wa Kenya), nikakutana na kaka mmoja aitwaye ‘Jersey’ nikamweleza nia yangu ya kuandaa masomo na kuweka masomo kwenye mtandao. Ndipo Jersey akanieleza kwa habari ya blog, akanielekeza namna ya kufanya  na kisha akanifungulia blog hii.

Tangu wakati huo nimeendelea kuandaa masomo na kuyaweka kwenye blog zangu (Kiswahili na kiingereza). Mpaka sasa nimefanikiwa kuweka kwenye blog hizi wastani wa masomo mia moja na ishirini. Hata hivyo yapo masomo mengine mengi ambayo nimeshaandaa lakini sijweka kwenye blog hizi kwa kuwa mengine ni kwa ajili yangu na mengine muda wake bado.

Suala zima la unadishi kwangu halijawa jepesi kama vile mtu asiyejua wajibu huu anavyoweza kudhani. Nimekuwa nikikutana na changamoto (upinzani) nyingi sana zenye kunifanya nikate tamaa.  Mara kadhaa huko nyuma niltamani kuacha kabisa kuaanda masomo, kwani adui alikuwa akileta upinzani na mawazo kwamba hakuna faida yoyote ya kuandika masomo haya, ni kupoteza muda wangu ambao ningetumia kufanya mambo mengine. Jambo hili lilinitesa kwa muda lakini nikakumbuka kile ambacho Paulo alimwambia Timotheo kusema ‘ Mambo hayo uyaagize na kuyafundisha’ — hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma, na kuonya na kufundisha (1 Timotheo 4:11, 13). Kwa hakika neno hili lilinipa nguvu ya kuendelea kuandika masomo.

Ili kuthibitisha kwamba Bwana Yesu anaithamini kazi yetu, Mungu alisema nami kwa njia ya ndoto kupitia ushuhuda ufuatao.  Julai 2009, miaka miwili baada ya kufungua blog hii, siku ya Jumamosi nilitulia nyumbani kwangu kwa muda wa saa nane mfululizo nikiaandaa masomo mbalimbali. Usiku wa siku hiyo nilipolala nikaota ndoto nimechkuliwa hadi mbinguni. Nilipofika, Malaika mmoja akanichukua na kunipeleka kwenye chumba kimoja kizuri umbile lake kwa ndani ni kama duara (mviringo). Ndani ya chumba hiki kulikuwa na mfano wa makabati ya chuma yenye milango miwili ambayo yamejengwa kwenye ukuta kufuata ule mzunguko. Ndipo yule Malaika akaenda na kufungua kabati mojawapo na kuanza kutoa mfano wa karatasi ambazo zimeandikwa na kunipa.

Punde tu baada ya kufungua ile kabati, ghafla nikaanza kuona picha ya jinsi nilivyokuwa pale nyumbani naandaa masomo, mchana wa siku hiyo. Naam kadri nilivyokuwa nikiandaa masomo na kumaliza, yule Malaika alikuwa alikuwa akitoa somo kwenye kabati na kunipa. Kwa hiyo nikawa naona maeneo yote mawili, yaani kile mimi ninachofanya duniani na kile Malaika anachofanya huku mbinguni. Naam uaminifu na uharaka wangu katika kuandaa masomo ndio uliomfanya yule Malaika kuyatoa kwenye kabati uharaka na wakati pia.

Kitu cha kushangaza ni kwamba kila baada ya idadi kadhaa ya masomo kutimia, niliona yule Malaika anatoa ‘kikapu’ kitupu anaweka pembeni na kisha anasogeza kingine na zoezi la kutoa masomo likaendelea. Kwa hakika nilishangaa sana kujua kwamba kumbe kuna uhusiano kati ya kile ninchofanya na mbinguni. Nilipokuwa katika kutafakari neno hili, ndipo yule Malaika akaniambia ‘bado kuna vikapu vingi vya masomo vinakungoja’. Nami nikashtuka na kujua kwamba Mungu amesema nami kwa njia ya ndoto na kuonyesha namna anavyothamini kile ninchofanya. Kwa hakika mbinguni kuna ‘store’ kubwa ya masomo ambayo Mungu amekusudia kuyateremsha kwa watoto wake duniani kupitia waandishi. Ndoto hii ilinifanya nikakumbuka maneno ya Yesu aliposema ‘… Kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale (Mathayo 13:52’.

Kwa hakika maono haya na kile ambacho sasa naona Mungu anafanya kwa watu wake kupitia masomo haya, siku zote hunitia nguvu za kuandika na kuandika na kuandika masomo kwa ajili ya kuujenga mwili wa Kristo.

Waandishi wenzangu na kila mwenye kuandaa masomo kwa ajili ya kuulisha mwili wa Kristo yafuatayo ni mambo kadhaa ambayo ni muhimu kujua na kuzingatia kadri tunavyoendelea kufanya kazi hii;

  • Mungu anaithamini kazi yetu. Najua kazi hii ilivyo na changamoto nyingi, lakini changamoto hizo zisikufanye ushindwe kuandika masomo kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Usikate tama, vumilia na endelea kufanya kazi ya Mungu maadam ni mchana ukitumia kipawa hiki cha pekee kwa utukufu wa Mungu na kwa uongozi wake.
  • Kile tunachoandika katika mapenzi ya Mungu kwa hakika kinafanyika msaada na uponyaji wa watu wake aliowakusudia. Usije ukafikiri unapoteza muda kwa kuandika, hapana. Maadam unaandika kwa uongozi wa Mungu uwe na uhakika kuna uponyaji mkubwa sana unatembea kupitia ujumbe huo.
  • Mungu anataka tujifunze kuwa na muda maalum wa kutulia kufanya kazi hii, na sio kufanya kwa mazoea. Kulingana na ratiba zangu za kazi mimi hutumia vema siku za mapumziko kuandaa masomo. Fahamu kwamba endapo Mungu amekuita umtumikie kwa njia hii, ‘kutoandika masomo kwa wakati ni kosa kubwa sana na ni kumpa adui nafasi ya kuharibu watoto wa Mungu kwa mafundisho ya uongo’. Mungu anataka tuipe kazi hii umuhimu kama tunavyofanya kwenye kazi nyingine.

Mwandishi mwenzangu, kuna vikapu vya masomo vinakusubiri. Katika nyumba ya Mungu kuna hazina ya kutosha ya masomo kwa ajili ya watoto wake hapa duniani. Ili aweze kuyateremsha, Mungu anakuhitaji wewe Mwandishi, ukae kwenye nafasi yako maana ndani yako ameweka kipawa cha uandishi. Jambo moja ambalo nimelithibitisha ni kwamba hakuna mwisho wa kuandika, ila kila mwandishi ana vikapu vyake, ana fungu lake, ana masomo yake ambayo anapswa kushirikiana na Roho Mtakatifu ili yaachiliwe katika nyakati zilizokubaliwa na yatunzwe kama kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili Bwana.