IJUE NA KUITUMIA NAFASI YAKO KAMA MLINZI KWENYE ULIMWENGU WA ROHO (Part 2)

Waraka wa Desemba

Na: Patrick Sanga

Mambo matano ya muhimu kujua na kuzingatia kuhusu nafasi ya Ulinzi katika ulimwengu wa roho;

 • Mwandamu amepewa kuwa ‘Mlinzi’ wa kusudi la Mungu katika ulimwengu wa roho akali hapa duniani.

Maadam umeokoka tambua kwamba wewe ni ‘mlinzi’ wa kusudi la Bwana. Na hilo kusudi ambalo umepewa kulinda lina muunganiko na maisha ya kiroho ya watoto wa Mungu, ama wa nyumbani kwako, kanisani kwako, kazini kwako nk. Kwa lugha nyingine kila aliyeokoka ni mlinzi wa mtu au watu wengine katika eneo ulilopo/ nchi yako nk, kwa jinsi ya rohoni.  Je wewe uko macho kufanya kazi ya ulinzi kwa hao watu na maeneo uliyopo? Na je hata ulipoona hatari umetoa taarifa kama mlinzi ili watu/taifa lisije angamia?  Watu/ndoa/familia ngapi leo zimeingia kwenye shida na wewe kama ‘mlinzi wao’ unaanza kuwasema vibaya na kusahau kwamba Mungu ameweka ‘future’ ya hao watu mikononi mwako. 

 •  Ni wajibu wa kila ‘Mlinzi’ kusimama kwenye nafasi yake ili kuhakikisha kusudi la Mungu linafanikiwa.

Sehemu kubwa ya maafa/majanga/matatizo ambayo yanawapata watoto wa Mungu leo ni kwa sababu kuna ‘walinzi’ ambao hawakusimama vema kwenye nafasi zao. Watu wengi leo wamekufa kiroho na kukwama kufikia makusudi ya Mungu kwao kwa kuwa wewe kama walinzi umelala na kusahau kazi yako ya ‘ulinzi’.  

Kuwa mlinzi ina maana ya kuwajibika katika nafasi ile ambayo Mungu amekuitia katika kuujenga mwili wake. Naam kumbuka sisi ni viungo katika mwili wa Kristo. Kadri unavyowajibika katika nafasi yako, ndivyo unavyotoa fursa kwa viungo vingine kuwajibika katika nafasi zao.

Mungu anakutaka ujifunze kuwajibika katika lile ambalo amekuitia na hivyo kukufanya kuwa mlinzi katika ulimwengu wa roho. Hakikisha unatekeleza wajibu wako kama Bwana Mungu alivyokusudia. Naam kufanya kwa kadri ya maagizo ya Bwana katika siku za maisha yako chini ya jua.

 • Mungu hua anatoa taarifa kwa walinzi tegemeana na ‘nafasi zao’ na pia ‘maeneo yao ya ulinzi’.

Siku zote Mungu anapotoa taarifa kuhusu mambo yanayokuja juu ya watoto wake ambayo kama hawatajipanaga yatawamaliza, huwa anatoa taarifa kwa walinzi kwa kuzingatia nafasi walizonazo kwenye ulimwengu wa roho. Na ndiyo maana nasisitiza jifunze kusimama katika nafasi yako ya ulinzi, ili Mungu anapotafuta mtu wa kumpa taarifa kwenye eneo lako akuone. Naam ukishaipata usisite kuwajulisha wale ambao wapo chini ya himaya/mlango/eneo lako la ulinzi ili kwa pamoja mjipage kukabliana na hatari husika.

Shetani naye anapoandaa vita anakuwa amelenga mahali/eneo maalumu la kupiga (walengwa). Mungu akijua hilo lazima atafute mlinzi anayehusika na mtu, watu, eneo, kijiji husika nk ili ampe taarifa juu ya kile ambacho kinataka kuja kwenye eneo lake la ulinzi. Jambo hili ndilo linalotupa picha ya uwepo wa nafasi tofauti za ulinzi kwa watoto wa Mungu, naam ni sharti kila ‘mlinzi’ asimame kwa uaminifu kwenye nafasi yake, ili kupata taarifa kutoka kwa Mungu juu ya eneo/maeneo yake ya ulinzi.

 •   Jifunze kuitazama ‘taarifa’ unayopewa na Mungu kama ‘fursa’ ya uponyaji kwako binafsi na kwa wale walioko chini ya lindo lako.

Katika sehemu ya kwanza tiliona madhara ambayo yatampata mlinzi binafsi kama hatatoa taarifa kwa anaowalinda. Taarifa ambayo mlinzi huyu alikuwa anaitoa ilikuwa ni fursa kwa wapewa taarifa kuchukua hatua za utekelezaji. Ilikuwa ni nafasi ya wao kujiaandaa kwa jambo linaloweza kuja mbele yao. Naam uzima na mauti kwa wale wanaolindwa ulikuwa kinywani kwa Mlinzi.

Jambo la msingi ninalotaka ulijue hapa ni kwamba, mlinzi huyu aliwapa watu taarifa ambayo na yeye amepewa (ameonyeshwa) na Mungu kwa sababu yupo kwenye nafasi yake. Kwa hiyo ni muhimu sana kwako kama mlinzi kuhakikisha unakuwa makini kusikia taarifa sahihi kutoka kwa Bwana na kisha kuwajulisha walengwa kwa kuwa taarifa ya mlinzi katika ulimwengu wa roho ni ‘fursa’ ya uponyaji.

 •  Mtu mmoja anaweza akapewa zaidi ya eneo moja la ulinzi katika ulimwengu wa roho.

Ndani ya Biblia kuna mifano kadhaa ya watumishi ambao walipewa jukumu la kuwa walinzi kwenye eneo zaidi ya moja (nitaeleza kwa upana katika sehemu ya tatu na kuendelea). Na hii inatupa picha kwamba hata sasa mtu mmoja anaweza kuwa na eneo zaidi ya moja la ulinzi kwenye ulimwengu wa roho.

Kusudi la uumbaji na utiifu wa ‘Mlinzi’ katika maagizo anayopewa na Mungu, ndivyo vinavyoamua wingi wa maeneo ya ‘ulinzi’ na mamlaka yake juu ya maeneo hayo katika ulimwengu wa roho. Kumbuka katika sehemu ya kwanza tumejifunza kwamba ‘kufanikiwa kwa kusudi la Mungu duniani kunategemea utiifu wa ‘walinzi’ wake waliopo duniani kwenye nafasi ambazo amewapa katika ulimwengu wa roho’. Naam kwa mlinzi lililo muhimu zaidi ni utii katika maagizo ya Bwana wake.

Katika sehemu hii ya pili nimeandika mambo haya matano ili kuweka msisitizo juu ya nafasi ya ulinzi ambayo unayo katika ulimwengu wa roho. Mambo mengi mabaya ambayo yanawakuta watoto wa Mungu, ndugu zetu, miji yetu na nchi zetu yasingetokea kwa kiwango tunachokishuhudia kama kila “Mlinzi” angesimama kwenye nafasi yake.

Mungu amejiwekea utaratibu wa kutoa taarifa kupitia ‘Walinzi’ juu ya kile ambacho Shetani amekusudia kukifanya hapa duniani. Ni heshima iliyoje kupewa nafasi kubwa kiasi. Naam Mungu anataka ‘walinzi’ katika ngazi ya familia, kanisa, ardhi, uchumi, mahusiano ya kimataifa, jamii, mji, mkoa, Taifa nk wasimame kwenye nafasi zao.

Katika sehemu ya tatu nitaanza sasa kuelezea nafasi mbalimbali za ulinzi na kwa kutumia mifano. Endelea kuombea ujumbe huu, ni imani yangu umekuja kwa wakati muafaka.

Somo litaendelea —

Advertisements

15 comments

 1. mtumishi BWANA YESU asifiwe!

  nimebarikiwa sana na somo lako hapo juu,na nimejifunza sana.nashukuru Mungu kwa kukufunulia na naomba pia azidi kukufundisha.kinachoniuma mimi ni kwamba walinzi wapo wanajitahidi kutoa meseji walizopewa na Mungu lakini watu wanaopewa hizo meseji hawazipokei au hata wakizipokea hawazifanyii kazi.yaani kumekuwa na kaubishi fulani hivi kwamba kwani yeye nani kamuambia,na kama ni Mungu kwanini Mungu aseme naye asiseme na sisi.Jamani hili ni tatizo kubwa sana miongoni mwa binadamu.naona kuna haja ya kuwafundisha watu pia kwamba wanapopata unabii au mtumishi akipewa ujumbe na Mungu kwaajili au kuhusu yeye afanye nini ili unabii ule utimie au Mungu aghairi.mfano mzuri ni wa Yona na ninawi,ninawi walipopata ule ujumbe walitubu kwa dhati na Mungu alighairi kuwaangamiza.mfano mwingine ni wa Nuhu alipokuwa anajenga safina walimdhiaki na mwisho wake ikawa ni maangamizo yao.

  Naomba Mungu somo linalofuata litufundishe mlindwaji anatakiwa afanyeje nini anapopewa taarifa za hatari na mlinzi wake.ubarikiwe sana mtumishi.

  mithali 29:18 Mahali pasipo na maono, watu huangamia,
  bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.
  mithali 29:18 pasipo maono watu huacha kujizuia;bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.
  Proverbs 29:18
  Where there is no vision, the people perish: but he that keepeth the law, happy is he.

  Like

  • Otaru Mrs, Mungu akubariki sana kwa mchango wako huu, binafsi umenibariki sana. Kwa hakika wewe ni Mlinzi, maana umejua kule ujumbe huu unakoelekea mapema kiasi hiki, Bwana azidi kusema nawe, nawe uwe mwaminifu kufanyia kazi ujumbe wake. Ni kweli hicho unachosema kipo na kukosekana kwa mawasiliano na mahusiano mazuri baina ya Mlinzi na watu wa eneo lake kumeleta matokeo ambayo hayakukusudiwa. Naam naweza nikasema ndio maana Mungu ameweka somo hili ndani yangu tena nilifundishe kwa mfululizo, naamini kadri nitakavyoendelea kuandika, majibu ya changamoto hizi yatapatiwa ufumbuzi na kila upande utajua wajibu wake.Ubarikiwe sana.

   Like

 2. Ubarkiwe mtumishi usife moyo kwa wito huu mimi nakufuatilia sana ktk masomo yko,kwenye swala la taarifa nmejifunza kitu…Kwakua hata mimi nmekwisha letewa taarifa kwakua mwenendo wngu ulikuwa unaelekea pabaya,maana kuna kitu Mungu aliniahidi na kilipochelewa nikafanya maaamuzi yakuacha kile Mungu amesema nakufuata mawazo yngu,na ndipo Mungu alipotumia mtu kuniletea taarifa nami nilipoipata nikageuka nikafunga na kutubu..

  Like

  • Ahsante kwa ujumbe wako ndg. Leonard, furaha ya mwandishi ni pale anapoona kile anachoandika kinafanyika msaada wa wasomaji, utukufu kwa Yesu, tuzidi kuombeana. Haijalishi jawabu la Mungu litachelewa kiasi gani, usikate tamaa, yeye hujibu kwa wakati muafaka. Barikiwa sana.

   Like

 3. Bwana Yesu asifiwe sana.

  Mtumishi namshukuru sana Mungu aliyekupa mafunuo ya kuandika ujumbe huu katika mtandao huu katika nyakati hizi ili tupone.

  Sijui niseme nini lakini wana wa Mungu tuliopewa dhamana ya ulinzi tutajibu nini mbele za Mungu kwani yapo maswali mengi yanayotusubiri kujibu kama hatujabadili staili yetu ya ulinzi na kurudi kila mmoja pale Bwana alipomweka na kuanza kujipanga upya kwa ajili ya ulinzi. Katika hali ya kawaida huwezi kupewa kazi ya ulinzi katika godown halafu wizi ukatokea wewe useme huna habari na wizi huo halafu ubakie kuwa mlinzi katika godown hilo. Ndivyo ilivyo kwetu walinzi wa leo. Uhalifu na wizi mwingi umefanyika katika malindo yetu nasi tunaendelea kusema Bwana asifiwe na kucheka.

  Leo maafa mengi yanatokea katika nchi k.m. rushwa, ufisadi, viongozi wabovu wasio na hofu ya Mungu wanapata madaraka, mafuriko yanatokea yanamaliza watu, njaa, uchumi kuporomoka, ndoa kukosa amani na kuvunjika, familia zisizo na amani, watoto wasio na utii, uvutaji wa bangi na madawa ya kulevya, mafundisho ya uongo ya Neno la Mungu n.k. Katika kila eneo nililolitaja kuna walinzi ambao Mungu amewaweka ili jambo lolote likitaka kutokea watoe taarifa ili hatua za tahadhari ziweze kuchukuliwa. Je haya yote yametokea na yanaendelea kutokea, walinzi tuko wapiiiiii? Mungu utuhurumie. Oooh Bwana Yesu tutajiteteaje?

  Ni wakati wetu wa kujitambua na kutubu pale ambapo hatukusimama sawasawa au tulihama lindo na kuacha lindo wazi na adui akapata nafasi. Kwa sababu inawezekana kabisa tatizo kuwa tumeshindwa kuwa walinzi kuanzia katika ngazi ya mlinzi mwenyewe na hasa katika ngazi ya familia. Tumesahau ulinzi wa familia zetu jambo ambalo shetani amelitumia kulipiga kanisa na hata taifa kwa ujumla. Mungu atusaidie sana katika hili, tufunguke macho tuone na tuanze kwa upya.

  Mungu akubariki sana mtumishi wa Mungu endelea kutufunulia yale Bwana anayokufunulia ili tupone, kanisa lipone na nchi iweze kupona.

  Like

  • Hello ndg. George kwanza Mungu akubariki kwa mchango wako muhimu katika eneo hili la ulinzi, kwa hakika wewe ni Mlinzi maana hata kufikiri kwako kunaonyesha wewe ni Mlinzi. jambo la msingi kwa kila Mlinzi ni kuanza kwa toba kama ulivyosema maana mambo mengi yanaharibika leo na walinzi wamelala hawako kwenye nafasi zao. Naam tujipange ili tusihukumiwe kwa kutokuwa kwenye nafasi zetu, bali kwa tukapewe taji kwa kuwa tulitumika kwa uaminifu katika nafasi zetu.
   Mungu akubariki, tuzidi kuombeana.

   Like

 4. Ni maombi yangu kwamba Mungu azidi kukubariki sana katika
  unyenyekevu ili azidi kukupa maarifa ya Yesu yaliyofichwa ndani
  yake ili UKOMBOZI WA NAFSI za wateule uwe wa mafanikio ya kutisha zaidi(MITHALI 1:7,HOSEA 4:6).Somo hili limeitikisa dunia yangu ya ujinga
  na upumbavu kiasi cha kuniacha uchi kabisa ili Yesu anivike vazi la Maarifa yake.Naomba unitumie full package ya somo hili kupitia upendouliohai@gmail.com.Ubarikiwe sana.

  Like

 5. Mpendwa mwalimu Patrick
  samahani kwa usumbufu bado nasubiri ile full package ya somo hili.
  Natanguliza shukurani na Mungu akubariki sana.

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s