Archive for December 2011

MAMBO YA KUTAFAKARI KWA HABARI YA WOKOVU 2012

December 31, 2011

Patrick na Flora Sanga

Ujumbe maalum wa mwaka 2012

Awali tunamshukuru sana Mungu kwa neema yake aliyotupa katika mwaka wa 2011. Kwa msaada wake tumeweza kufanikisha mambo mbalimbali kikazi, kihuduma na mahitaji binasfi pia. Nasi tunamshukuru Mungu pia kutupa neema hii ya kuingia mwaka mpya wa 2012. Kwa heri mwaka 2011 na mambo yako, tunakukabili na kukaribisha 2012 kwa jina la Yesu.

Katika kuukaribisha na kuukabili mwaka huu mpya wa 2012, Mungu ameweka ndani yetu msukumo ili tuandike mambo ya kutakafari na kuyafanyia kazi kama ‘ulinzi wa wokovu’ kwa kila amwaminiye. Kimsingi kulikuwa na somo jingine linalohusu ‘nyakati’ ambalo tulidhamiria kulikamilisha na kuliweka katika kipindi hiki cha kuukaribisha mwaka mpya, bali kwa kuwa ndani yetu tumesukumwa kuweka ujumbe huu, ni imani yetu ujumbe huu utaongeza maarifa ya kumsaidia kila atakayeusoma. Yafuatayo ni mambo matano ya msingi kujua, kutafakari na kuyafanyia kazi katika mwaka huu wa 2012;

 • Kusudi la Yesu kuja duniani

Yohana 3:16 inasema ‘Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele’.

Ni vizuri ukafahamu na ukakumbuka kwamba Yesu alikuja kwa lengo la kurejesha uhusiano wako na Mungu, kwa njia ya wokovu. Naam wokovu huo ndiyo dhamana yako ya kuishi maisha ya ushindi hapa duniani dhidi ya Shetani na kisha baadae uzima wa milele.

 • Shetani hafurahii wokovu wako

Kwa kuwa Shetani alifukuzwa na Mungu toka mbinguni kwa sababu ya kuasi, anajua hata angefanya toba kiasi gani hawezi kusamehewa. Yeye Shetani alikuwako mbinguni kabla ya kuasi na kwa hiyo anaujua vizuri uzuri wa mbinguni. Pia anajua njia ya kuurithi uzima wa milele ni kwa mtu kumwamini Yesu sawasawa na Yohana 3:16, kwa hiyo hafurahii hata kidogo wokovu ulionao wewe. Naam Shetani anafanya kazi usiku na mchana ili ahakikishe unamuasi Mungu kama yeye alivyoasi na kisha baadae kwenda naye kwenye mateso ya milele katika Jehanamu ya moto.

 • Mazoea na kutokujali wokovu

Mpendwa msomaji, jiulize swali hili, laiti Bwana Yesu akishuka sasa kulichukua kanisa utaenda naye au utaachwa? Tafakari kwa muda… tunaamini umepata jibu. Shetani amefanikiwa kuwafanya watu wasiujali wokovu na waishi kwa mazoea, ambayo yamewafanya kupuuzia mambo mengi waliyotakiwa kuyajali. Naam amefanikwa kwa kiwango kikubwa kupofusha sheria ya Mungu ndani mioyo yao ili wasiitende na hata wakitaka kuitenda, basi waitende kinyume na mapenzi ya Mungu wao.

Wakristo wengi wanaishi maisha ambayo si ya ushuhuda wa Bwana wao. Maisha ambayo hayaonyeshi tofauti kati ya aliye mwamini Yesu na asiye mwamini. Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anauliza ‘Sisi je! Tutapataje kupona, tusipoujali wakovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia’ (Waebrania 2:3). Mpenzi msomaji, andiko hili liliandikwa kwa sababu wenzetu walikuwa hawaujali wokovu. Naam nasi tusiwe kama wenzetu hawa, sharti tuuthamini wokovu na kuulinda sana.

Mungu anataka nini kwako 2012?

 • Uishindanie imani

Biblia katika Yuda 1:3 inasema ‘Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu’. Tumekwisha kukuonya kwa habari ya lengo la Shetani, naam hakikisha siku zote unaishindania imani. Kumwamini Yesu ni kutangaza vita na ufalme wa Shetani. Shetani anafanya kila analoweza akutoe kwa Yesu, hakikisha unapambana naye ili kulinda imani uliyonayo kwa Yesu. Ili uwe mpambanaji mzuri Sharti neno la Mungu likae kwa wingi ndani yako.

Mtume Paulo anaelezea zaidi kwa habari ya jambo hili akisema ‘Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu: la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijadhinii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele’ (Wafilipi 3: 12-13).

 • Ujikane mwenyewe kwa ajili yake

Luka 9:23 inasema ‘Akawaambia wote, Mtu yoyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate’.

Mungu anataka kama mtoto wake ujifunze kuishi kwa kuwa tayari kuruhusu matakwa yako yasitimie bali ya Mungu kwanza kwenye kila eneo. Kuishi kwa kumpa yeye nafasi ya kwanza kwenye kila eneo la maisha yakoo. Naam ujifunze kuishi kwa kutoa vipaumbele kwenye mambo ya Mungu kwanza. Ujizuie kutekeleza matakwa yako kwa kutekeleza matakwa yake nk. Katika kufafanua jambo hili Yesu alisema ‘Basi kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu’ (Luka 14:33).

Mtume Paulo akijua thamani ya wokovu alioupata na katika kufafanua jambo hili aliwaambia Wafilipi akisema ‘Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kama mavi ili niapte Kristo’. (Wafilipi 3:7–8).

 

Lengo kuu la ujumbe huu ni kukuwekea ndani yako ‘nidhamu’ itakayokutafakarisha thamani na maana ya wokovu kwako na hivyo kukufanya uwe na sababu ya kuishindania imani. Kumbuka Yesu mwenyewe alisema ‘Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake’ (Yohana 15:13). Ikiwa yeye alitupenda kiasi hiki, ni jukumu letu kuishindania imani yetu ndani yake kwa maana ya kudumu katika kumwamini yeye bila kujali tunakutana na upinzani kiasi gani katika maisha haya.

Ni imani yetu kwamba mambo haya matano yameweka msingi mzuri wa wewe kuanza nao kwa mwaka 2012, basi ndugu na tuzidi kuombeana.

Tunakutakia tena heri ya Christmas na mwaka mpya wa 2012

Neema ya Bwana Yesu Kristo na ikae nanyi daima

MAMBO YA KUTAFAKARI KATIKA KIPINDI HIKI CHA CHRISTMAS

December 24, 2011

Patrick na Flora Sanga

Heri ya Christmas mpenzi msomaji!

Mathayo 1:21 ‘Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina Yesu, maana, yeye ndiye atayewaokoa watu wake na dhambi zao’.

Hakika hii ni sherehe ya ajabu na ya kipekee sana maishani kwetu. Kila mwaka ifikapo Desemba 25, Wakristo duniani kote huadhimisha sherehe ya kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Naam kuna mambo mengi ambayo hufanyika katika siku hii au katika kipindi cha maadhimisho ya siku kuu hii. Wapo wanaojua maana ya siku hii na wapo ambao wameigeuza siku hii kuwa chukizo mbele za Mungu kutokana  na matendo yao.

Hivyo tunapoadhimisha sherehe hii katika mwaka huu, yafuatayo ni mambo ambayo tumeona ni vema tukakumbushana nayo ni;

 • Mwokozi amezaliwa

Mstari wa 21 wa kitabu cha Mathayo unatueleza kusudi la kuja kwake Bwana wetu kuwa ni kuwaokoa watu wake na dhambi zao. Naam ni upendo wa pekee sana kwa Bwana Yesu kuacha heshima na utukufu mbinguni na aje azaliwe, afe na kufufuka ili tupate waokovu. Kwa sababu hiyo kama bado hujaokoka ni vema ukafanya maamuzi ya kuokoka. Haukuwa uamuzi rahisi kwa Yesu kuacha heshima na enzi mbinguni aje kwa ajili yetu. Na wewe uliyeokoka usiendelee kuishi maisha ya dhambi kama asiyemjua Mungu.

 • Boresha uhusiano wako na Roho Mtakatifu

Biblia inasema ‘Kuzaliwa kwake Yesu kulikuwa hivi, Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana na mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu’ (Matahyo 1:17)

Mimba ya Bwana wetu ndani ya Mariamu ilikuwa ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Nasi tunajua ya kwamba, Roho Mtakatifu ni Mungu, na kwa sasa yeye ndiye ambaye yupo duniani analiandaa kanisa la Bwana na kuhakikisha kusudi la Mungu kupitia ‘mtu’ linafanikiwa. Naam ni muhimu sana kila aliye wa Kristo kuhakikisha kwamba mahusiano yake na Roho Mtakatifu yanakuwa mazuri daima. Naam tumia kipindi hiki kumshukuru Mungu kwa siku hii na kujenga msingi mzuri wa mahusiano na Roho Mtakatifu kuanzia sasa na kuendelea.

 • ‘Christmas’ siyo siku ya kufanya uovu

Ni vema watu wote wakatambua kwamba siku hii siyo siku ya kufanya kila namna ya uchafu na dhambi ambazo wanadamu wamezoea kufanya katika siku hii. Ni vema siku hii ikaheshimika sana, maana ndiyo siku ambayo dunia ilipokea mwokozi wa ulimwengu. Naam siku ambayo ufumbuzi wa dhambi ulikuja kwa wanadamu duniani. Shetani amekuwa akijaribu kuharibu sifa/ picha (image) ya siku hii, kwa kuwafanya wanadamu wapange kufanya kila namna ya machikizo mbele za Mungu wetu. Ole kwao wafanyao hayo, naam tulio wa Kristo Yesu tunajua maana ya siku hii na tunaona fahari kwa ajili ya siku hii, utukuzwe Baba kumtoa mwanao, utukuzwe mwana kwa kukubali kuja ili tupate kuwa warithi wa ufalme wako tungali dunani na kisha uzima wa milele.

 • Fanya tathmini ya wokovu wako

Kwa kawaida wanadamu hufanya tathimini ya mambo mbalimbali katika maisha yao. Ni wachache sana ambao hufanya tathmini juu ya maisha yao ya wokovu ndani ya Kristo. Katika mwaka 2011, je umekuwa Balozi wa kweli wa Kristo katika nyumba, ofisi, mji au Taifa lako na kwa wale wanaokuzunguka kila siku? vipi kuhusu uaminifu, je umekuwa muaminifu kwa kiasi gani mbele za Mungu, je unaweza kusema umeishi maisha ya ushuhuda katika Kristo Yesu nk.

Vipi kuhusu mahusiano yako na wenzako, je kuna amani, vipi kuhusu zaka na dhabihu? Kwa kifupi katika vigezo vyote vya wokovu alama zako zikoje, ingekuwa unajiwekea alama katika mia moja ungejiwekea ngapi? na Bwana naye angekuwekea ngapi? Naam pale unapoona hukufanya vema, omba toba na kuomba nguvu mpya ya kukusaidia kipindi kinachofuata baada ya siku hii na mwaka ujao wa 2012.

Mpenzi msomaji unapomalizia ujumbe huu hebu sema maneno yafuatayo ya shukrani;

“Bwana Yesu hongera kwa siku hii ya pekee ya kuzaliwa kwako, ambayo ulifanya maamuzi magumu sana kwa sababu ya upendo wako kwetu. Watoto wako tunajua maana ya siku hii na tunaona fahari sana kwa ajili ya siku hii, ahsante sana kwa kutuchagua na kutufanya warithi wa neema yako. Kwa imani tunaungana na jeshi lote la mbinguni katika kusherekea siku hii ya pekee, tunatamani tungekuwa na wewe kwa jinsi ya mwili ili tufurahi kwa pamoja. Nasi tunaoomba uwepo wako na furaha (tabasamu) yako vidhihirike ndani yetu, kwa namna ya pekee, maana furaha yako ndiyo nguvu zetu. 

Mpenzi msomaji, familia yangu inakutakia heri ya ‘Christmas’ na maisha yenye kumuja Mungu zaidi.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu! Wastahili Bwana wetu.

UHURU WAKO KATIKA KUMTUMIKIA MUNGU, UNATEGEMEA UHUSIANO WAKO NA MWENZI WAKO

December 22, 2011

Na: Patrick Sanga

Biblia katika kitabu cha Mwanzo 2:18 inasema ‘Bwana Mungu akasema, si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye’. Ni kusudi na mpango wa Mungu watu waoe na kuoana. Hii ni kwa sababu kufanikiwa kwa kusudi la Mungu duniani kunategemea ndoa au wanandoa pia. Naam kwa Mungu ni muhimu sana kujua nani anakuwa mwenzi wako wa maisha tegemeana na kusudi lake la kukuumba.

Tunapoenda kufunga mwaka nimesikia ndani kuweka ujumbe huu kwenye blog hii nikiamini utawafaa wengi. Jambo la msingi ambalo nataka ulipate ni kuhusu uhusiano uliopo kati ya ‘uhuru’ wa kumtumikia Mungu na ndoa yako. Pengine si wengi wanaojua umuhimu wa mahusiano mzuri baina yao kama wanandoa na kumtumikia Mungu. Naam ndiyo maana kuna ujumbe huu kwa ajili yako.

Watumishi wengi katika nyakati za leo hawajawapa heshima na nafasi ambayo wenzi wao wanaistahili. Baadhi ya wanaume wameona kupata mke ni sehemu ya kukamilisha sifa za utumishi wao kama wanandoa bila kujua kwa nini ameunganishwa na huyo mwenzi wake. Wengine wamekuwa wakiwapuuza wake au waume zao na bado madhabahuni wanalihubiri neno. Na kuna baadhi yao hawana upendo kwa wake zao, wake nao  si watiifu kwa waume zao, ni watu wa kugombana, wenye uchungu ndani yao nk, naam bila kutengeneza au kumaliza tofauti zao hizo  utawakuta madhabahuni wakihudumu kwa raha kabisa. Je, jambo hili ni sahihi kweli? Je ni jambo la kumpendeza Bwana?

Fahamu kwamba ‘uhuru wako katika kumtumikia Mungu kwenye nafasi aliyokupa katika mwili wake, ipo kwa mwenzi wako wa maisha’. Ilikuwa Desemba 28, 2010, Bwana Yesu aliponifundisha jambo hili. Naam uhuru wako wa kumtumikia Mungu upo kwa mke/mume wako. Hivyo kama mahusiano yako na mwenzi wako si mazuri huwezi kutumika katika mapenzi yake. Naam uhuru wa wewe kusikia na kupokea kutoka kwa Mungu unategemea sana mahusiano yako na mwenzi wako.

Nilipofuatilia tafsiri ya neno hili uhuru (freedom) niligundua zipo tafsiri nyingi lakini nikachukua hizi tatu kwa kuwa zinaendana na ujumbe huu.  Tafsiri moja wapo ya ‘Oxford dictionary’ inasema uhuru ina maana ya ‘special privilege or right of access’.  Na tafsiri ya neno hilo kutoka katika ‘Encarta dictionary’ ni ‘right to use or occupy a space’ na pia tafsiri nyingine ni ‘ease of movement’.

Naam mahusiano yako na mwenzi wako yanapokwa mazuri jambo hili linakupa haki, kibali, nafasi na mpenyo wa kumtumika Mungu katika kiwango alichokusudia na zaidi katika mapenzi yake. Jambo hili linakupa mpenyo wa kusikia, kuhoji na kusemezana na Mungu juu ya kile ambacho anataka uwafundishe watoto wake ama ukiwa madhabahuni, au kwa njia ya kuandika, kushuhudia nk. Naam kwa hiyo mahusiano mazuri kati yako na mwenzi wako ni ufunguo wa wewe kumtumika Mungu.

Si hivyo tu bali mahusiano yako na mwenza wako yanapokuwa mazuri utapata wepesi wa kutembea na kutumika katika kusudi la Mungu. Naam ndivyo unavyopata haki ya kutumia kila ambacho Mungu ameweka ndani yako kwa utukufu wake, naam ndivyo unavyokuwa na nguvu ya utawala kwenye nafasi na eneo lako la utumishi katika ulimwengu wa roho.

Biblia inasema katika 1Petro 3:7 ‘Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe’.

Naamini umeona kile kipengele cha mwisho kinavyosema. Hii ina maana kama mwanaume atashindwa kukaa na mke wake kwa akili na kumpa heshima, maombi yake yatazuiliwa. Sasa fikiri mwanaume huyu ni mtumishi yaani Mchungaji, Mwalimu, Nabii nk nini kitatokea kwa wale anaowachunga au kuwahudumia? Naam mahusiano yako na mwenzi wako ni ya maana sana kama unataka kutumika katika mapenzi ya Mungu. Mahusiano mazuri baina yenu yanaleta mawasiliano mazuri baina yako kama Mtumishi na Mungu wako. Hivyo msingi wa mawasiliano mazuri na Mungu wako, upo kwa mwenzi wako.

Ni vizuri ukafahamu kwamba bila kuwa na mahusinao mazuri na mwenzi wako wa maisha, utumishi wako ni bure. Naam uhuru wako katika kumtumika Mungu unategemea uhusiano wako na mwenzi wako. Si rahisi kwa Mungu kusema na wewe kama mahusiano yako na mwenzi wako si mazuri, matokeo yake utawasikizisha/hubiri/fundisha watu mawazo yako na pengine ya adui, zaidi utahudumu kwa mazoea bila uwepo wa Bwana, au chini ya kiwango cha upako uliokusudiwa, tena ni kwa sababu Mungu anawaonea huruma watu wake.

Jifunze kufanya tathimini ya mahusiano yako na mwenzi wako mara kwa mara, na kuhakikisha unayaboresha, naam jambo hili ni muhimu sana kwenu binafsi na zaidi kwa Mungu ili kupata uhuru wa kusikia kutoka kwake kila wakati kwa ajili yenu na  wale ambao amekupa kuwahudumia.

Nakutakia utumishi mwema katika nafasi yako pamoja na mwenzi wako, mwenzi wako ni wa muhimu sana, mpe nafasi yake, utaona mabadiliko kwenye utumishi wako.

IJUE NA KUITUMIA NAFASI YAKO KAMA MLINZI KWENYE ULIMWENGU WA ROHO (Part 2)

December 7, 2011

Waraka wa Desemba

Na: Patrick Sanga

Mambo matano ya muhimu kujua na kuzingatia kuhusu nafasi ya Ulinzi katika ulimwengu wa roho;

 • Mwandamu amepewa kuwa ‘Mlinzi’ wa kusudi la Mungu katika ulimwengu wa roho akali hapa duniani.

Maadam umeokoka tambua kwamba wewe ni ‘mlinzi’ wa kusudi la Bwana. Na hilo kusudi ambalo umepewa kulinda lina muunganiko na maisha ya kiroho ya watoto wa Mungu, ama wa nyumbani kwako, kanisani kwako, kazini kwako nk. Kwa lugha nyingine kila aliyeokoka ni mlinzi wa mtu au watu wengine katika eneo ulilopo/ nchi yako nk, kwa jinsi ya rohoni.  Je wewe uko macho kufanya kazi ya ulinzi kwa hao watu na maeneo uliyopo? Na je hata ulipoona hatari umetoa taarifa kama mlinzi ili watu/taifa lisije angamia?  Watu/ndoa/familia ngapi leo zimeingia kwenye shida na wewe kama ‘mlinzi wao’ unaanza kuwasema vibaya na kusahau kwamba Mungu ameweka ‘future’ ya hao watu mikononi mwako. 

 •  Ni wajibu wa kila ‘Mlinzi’ kusimama kwenye nafasi yake ili kuhakikisha kusudi la Mungu linafanikiwa.

Sehemu kubwa ya maafa/majanga/matatizo ambayo yanawapata watoto wa Mungu leo ni kwa sababu kuna ‘walinzi’ ambao hawakusimama vema kwenye nafasi zao. Watu wengi leo wamekufa kiroho na kukwama kufikia makusudi ya Mungu kwao kwa kuwa wewe kama walinzi umelala na kusahau kazi yako ya ‘ulinzi’.  

Kuwa mlinzi ina maana ya kuwajibika katika nafasi ile ambayo Mungu amekuitia katika kuujenga mwili wake. Naam kumbuka sisi ni viungo katika mwili wa Kristo. Kadri unavyowajibika katika nafasi yako, ndivyo unavyotoa fursa kwa viungo vingine kuwajibika katika nafasi zao.

Mungu anakutaka ujifunze kuwajibika katika lile ambalo amekuitia na hivyo kukufanya kuwa mlinzi katika ulimwengu wa roho. Hakikisha unatekeleza wajibu wako kama Bwana Mungu alivyokusudia. Naam kufanya kwa kadri ya maagizo ya Bwana katika siku za maisha yako chini ya jua.

 • Mungu hua anatoa taarifa kwa walinzi tegemeana na ‘nafasi zao’ na pia ‘maeneo yao ya ulinzi’.

Siku zote Mungu anapotoa taarifa kuhusu mambo yanayokuja juu ya watoto wake ambayo kama hawatajipanaga yatawamaliza, huwa anatoa taarifa kwa walinzi kwa kuzingatia nafasi walizonazo kwenye ulimwengu wa roho. Na ndiyo maana nasisitiza jifunze kusimama katika nafasi yako ya ulinzi, ili Mungu anapotafuta mtu wa kumpa taarifa kwenye eneo lako akuone. Naam ukishaipata usisite kuwajulisha wale ambao wapo chini ya himaya/mlango/eneo lako la ulinzi ili kwa pamoja mjipage kukabliana na hatari husika.

Shetani naye anapoandaa vita anakuwa amelenga mahali/eneo maalumu la kupiga (walengwa). Mungu akijua hilo lazima atafute mlinzi anayehusika na mtu, watu, eneo, kijiji husika nk ili ampe taarifa juu ya kile ambacho kinataka kuja kwenye eneo lake la ulinzi. Jambo hili ndilo linalotupa picha ya uwepo wa nafasi tofauti za ulinzi kwa watoto wa Mungu, naam ni sharti kila ‘mlinzi’ asimame kwa uaminifu kwenye nafasi yake, ili kupata taarifa kutoka kwa Mungu juu ya eneo/maeneo yake ya ulinzi.

 •   Jifunze kuitazama ‘taarifa’ unayopewa na Mungu kama ‘fursa’ ya uponyaji kwako binafsi na kwa wale walioko chini ya lindo lako.

Katika sehemu ya kwanza tiliona madhara ambayo yatampata mlinzi binafsi kama hatatoa taarifa kwa anaowalinda. Taarifa ambayo mlinzi huyu alikuwa anaitoa ilikuwa ni fursa kwa wapewa taarifa kuchukua hatua za utekelezaji. Ilikuwa ni nafasi ya wao kujiaandaa kwa jambo linaloweza kuja mbele yao. Naam uzima na mauti kwa wale wanaolindwa ulikuwa kinywani kwa Mlinzi.

Jambo la msingi ninalotaka ulijue hapa ni kwamba, mlinzi huyu aliwapa watu taarifa ambayo na yeye amepewa (ameonyeshwa) na Mungu kwa sababu yupo kwenye nafasi yake. Kwa hiyo ni muhimu sana kwako kama mlinzi kuhakikisha unakuwa makini kusikia taarifa sahihi kutoka kwa Bwana na kisha kuwajulisha walengwa kwa kuwa taarifa ya mlinzi katika ulimwengu wa roho ni ‘fursa’ ya uponyaji.

 •  Mtu mmoja anaweza akapewa zaidi ya eneo moja la ulinzi katika ulimwengu wa roho.

Ndani ya Biblia kuna mifano kadhaa ya watumishi ambao walipewa jukumu la kuwa walinzi kwenye eneo zaidi ya moja (nitaeleza kwa upana katika sehemu ya tatu na kuendelea). Na hii inatupa picha kwamba hata sasa mtu mmoja anaweza kuwa na eneo zaidi ya moja la ulinzi kwenye ulimwengu wa roho.

Kusudi la uumbaji na utiifu wa ‘Mlinzi’ katika maagizo anayopewa na Mungu, ndivyo vinavyoamua wingi wa maeneo ya ‘ulinzi’ na mamlaka yake juu ya maeneo hayo katika ulimwengu wa roho. Kumbuka katika sehemu ya kwanza tumejifunza kwamba ‘kufanikiwa kwa kusudi la Mungu duniani kunategemea utiifu wa ‘walinzi’ wake waliopo duniani kwenye nafasi ambazo amewapa katika ulimwengu wa roho’. Naam kwa mlinzi lililo muhimu zaidi ni utii katika maagizo ya Bwana wake.

Katika sehemu hii ya pili nimeandika mambo haya matano ili kuweka msisitizo juu ya nafasi ya ulinzi ambayo unayo katika ulimwengu wa roho. Mambo mengi mabaya ambayo yanawakuta watoto wa Mungu, ndugu zetu, miji yetu na nchi zetu yasingetokea kwa kiwango tunachokishuhudia kama kila “Mlinzi” angesimama kwenye nafasi yake.

Mungu amejiwekea utaratibu wa kutoa taarifa kupitia ‘Walinzi’ juu ya kile ambacho Shetani amekusudia kukifanya hapa duniani. Ni heshima iliyoje kupewa nafasi kubwa kiasi. Naam Mungu anataka ‘walinzi’ katika ngazi ya familia, kanisa, ardhi, uchumi, mahusiano ya kimataifa, jamii, mji, mkoa, Taifa nk wasimame kwenye nafasi zao.

Katika sehemu ya tatu nitaanza sasa kuelezea nafasi mbalimbali za ulinzi na kwa kutumia mifano. Endelea kuombea ujumbe huu, ni imani yangu umekuja kwa wakati muafaka.

Somo litaendelea —