UPONYAJI WA NDOA ZETU

 Na: Patrick Sanga

Siku moja mama Allen (hili siyo jina lake halisi) alianza kunishirikisha mambo ya ndoa yake yanavyomtesa. Akaniambia mwanangu hizi ndoa tunapenda tu kuingia bila kujua kilichomo ndani yake. Hivi unavyoniona sina hamu kabisa ya ndoa, maana maisha tunayoishi (ingawa kwa nje watu wanaona tuko pamoja), lakini ukweli ni maisha ya taabu na majuto karibu kila siku.

Tabia ya mume wangu imefika mahali haivumiliki. Nikamuuliza tatizo ni nini hasa? Akasema ni fedha, elimu yake na kutoka nje ya ndoa. Fedha ya mume wangu wanaijua wazazi wake na si wazazi wangu, kwani mara kwa mara yeye hutuma fedha kwa wazazi wake. Inaniuma maana natamani hata mie  wazazi wangu niwatumie fedha pia.

 Mume wangu ni kweli Mungu kamjalia kuwa na elimu ya kutosha, lakini elimu yake imekuwa dharau kwangu nisiye ana elimu kama yake. Maana hunisema kwa sababu ya elimu yangu ndogo, kazi yangu na mshahara wangu mdogo ukilinganisha na wake.  Kubwa na baya Baba Allen sio mwaminifu katika ndoa, sina amani na hasa ukizingatia ugonjwa huu wa ukimwi, nina mashaka makubwa sana ndani yangu.

Nikamuuliza umefanya jitihada gani ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizi za ndoa yako? Akajibu akasema nimeamua kuishi naye kwa kuzikubali tofauti zetu (agree to differ). Kwa lugha nyingine nimekubali kuishi na hali hii, kwamba haya ndiyo maisha yangu ya ndoa chini ya jua. Hivyo imefika mahali sina jingine la kufanya ila kukubali kwamba mwenzangu yuko vile na mimi niko hivi, tutendelea kuishi kwa kutofautina hadi kifi kitutenganishe, kwani jitihada za kujaribu kurekebisha mambo haya zimekwama.

Baada ya kusikia maelezo haya niliumia sana, nikamshauri mambo kadhaa ya kufanya ili kuiponya ndoa yake. Lengo langu la msingi katika kuandika habari za mama Allen ni kujaribu kukufukirisha mwanandoa mwenzangu mambo kadhaa yatakayokusaidia kuiponya ndoa yako pia;

 • Jambo la kwanza – Ndoa ni wito wa upungufu na hivyo suala la uvumilivu ni la lazima.

Si watu wengi wanaojua kwamba ndoa ni wito wa mapungufu pia. Maandiko yanasema ‘ Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja’ (Mwanzo 2:24).

Ni dhahiri kwamba watu wanapooana wanakuwa wametoka katika asili na malezi (background) tofauti hasa kutokana na mazingira waliyokulia. Ile tu kwamba huyu anatoka katika familia hii na huyu ile, fahamu kwamba lazima kutakuwa na tofauti kadhaa katika ndoa hiyo. Naam tofauti zenu ndiyo sehemu ya  mapungufu kwenu kama  wanandoa. kwa sababu wewe ungependa mwenzako awe hivi na yeye kuna vitu ambavyo angependa vibadilike kwako.

Na wala usije ukajiona wewe upo kamili, naam kwa upande wako unaweza kuwa sawa lakini kwa mwenzako, hauko kamili. Ni vizuri ukafahamu kwamba unapoingia kwenye ndoa, utakabilana na mapungufu ya mwenzi wako. Kwa sababu hii suala la uvumilivu, kuchukuliana, kusameheana kwa wanandoa ni la msingi ili kufikia mahala pa kutengeneza tabia au mfumo mpya wa ndoa yenu.

 • Jambo la pili – Haijalishi mwenzi wako anatabia mbaya kiasi gani, Yesu anaweza kumbadilisha.

Jambo la pili ambalo nimeoana vema kusisitiza ni kwamba wewe mama au baba ambaye ndoa yako ipo kwenye misukosuko kama ya mama Allen pengine na kuzidi, usifike mahala pa kukata tamaa na kuamua kuishi kwa kuzikubali tofauti zenu kama sehemu ya maisha. Kwa kufanya hivyo utakuwa unamzuia Roho Mtakatifu kukusaidia kuiponya ndoa yako. Ni lazima kwanza ubadili fikra zako na mtazamo wako kwamba, kwa Mungu hakuna lisilowezekana na hivyo haya si maisha yangu ya ndoa ninayostahili kuyaishi.

Kwa Mungu sisi tu watoto wake. Hakuna Baba mwenye kufurahia kuona maisha ya ndoa ya watoto wake yanakuwa ya majuto. Mungu alipoleta wazo la ndoa ilikuwa ni kwa ajili ya kusudi la ufalme wake na kuwa furaha kwa watoto wake na si majuto. Nasikitika kusema leo, ndoa nyingi zimekuwa ni majuto na si kile Mungu alikiona wakati wa uumbaji hata akasema, kila kitu nilichokifanya ni chema sana (Mwanzo 1:31).

Kwa kilio kilichopo kwenye ndoa hivi sasa ni dhahiri kwamba kuna mahali kama wanandoa tumekosea na kumpa Iblisi nafasi (Waefeso 4:27) hata ameleta majuto kiasi hiki. Ushauri wangu ni kwamba ni vema kila mwanandoa akasimama kwenye nafasi zake (Mwanaume kama kichwa na Mwanamke kama Mlinzi na Msaidizi nk) kwa pamoja tumpinge Shetani naye atatukimbia. Endapo mwenzi wako hayuko tayari kwa hili au hamjui Mungu wako, basi wewe mwenye kujua siri hii kama anza, maana kwa Mungu mtu mmoja natosha kuleta uponyaji wa Taifa, je si zaidi ndoa yako? Naam usikate tamaa, Mungu wetu, ni MUNGU ASYESHINDWA.

 

Bwana Mungu na akusaidie katika kuzikabili changamoto za ndoa yako.

Advertisements

8 comments

 1. Kwa kweli tunahitaji msaada mkubwa katika ndoa zetu vinginevyo ndoa zinakuwa kifungo cha maisha katika gereza la hiari ambalo hakuna anayeweza kukuwekea dhamana isipokuwa Yesu Kristo peke yake.

  Kwa nyongeza tu ya ushauri wako kwa wanandoa, tuangalie sana kwani mambo yanayoleta matatizo makubwa katika ndoa hayaanzi yakiwa makubwa hivyo hivyo bali yanaanza kama mambo ambayo hayana madhara lakini kadri muda unavyosogea yanakuwa na kuwa matatizo makubwa. Mambo haya madogo yanatokana na mmoja kati ya wanandoa kutokaa katika nafasi yake sawasawa na kutoa mwanya kwa mwenzi wake kupata wazo la mashaka juu ya mbadiliko katika eneo la mwenzi wake. Hii inaweza kuwa hata katika kauli tu, jinsi mmoja anavyomjibu mwenzake au jinsi anavyouliza jambo fulani? Au, jinsi mmoja anavyopokea ushauri wa mwenziwe, dharau, kejeli, kutothaminiana, mambo ya kificho k.m. kuwa na account au mali za kificho, upande mmoja kuzuia upande mwingine kujua kipato na matumizi yake (mfano mke hataki mume ajue mshahara wake wala matumizi yake au kama ni biashara mwanamke/mwanamke hataki mwenzake ajue mwenendo wa biashara yake), lakini kubwa sana ni mwenzi mmoja kuwa uamuzi juu ya tendo la ndoa (hapa namaanisha labda mke siku anapoamua ndiyo mme wake atapata hiyo haki ya msingi ya ndoa na mwanaume hivyohivyo. au tendo hilo linapatikana kwa masharti ya lazima mmoja afanye jambo fulani kwa mwingine ndiyo iwezekane vinginevyo haiwezekani 1Kor 7:3-5)

  Haya yanapotokea yanaleta kutokuaminiana na mmoja kujiona hana thamani mbele ya mwenziwe. Jambo hili linashusha kwa kiwango kikubwa mapenzi ndani ya ndoa. Kutokana na kushuka kwa mapenzi ndani ya ndoa shetani anajipenyeza na kumalizia kazi yake kwa wepesi kwa kuwaonyesha suluhisho lipo nje ya ndoa zao na kuwaingiza katika uzinzi na hili linahamisha hata mawasiliano na uwajibikaji katika nyumba zao kuhamia kwenye vibanda hasara.

  Ni vema tuwe makini na mambo madogo katika ndoa zetu, unajua hata neno pole, asante, samahani vinaweza kumhamisha mwenzi wako nyumabani? Tuwe makini.

  Kosa kubwa linalofanywa mara nyingi kwa wasuluhishi wa mambo ya ndoa wanahukumu kesi za ndoa kwa kuzingatia kosa lililojitokeza mwisho ambalo ndilo lililoonekana na macho ya nje. Chumvi inatakiwa kuwekwa kwenye chanzo cha maji. 1Fal 2:21-22.

  Haya yanapotokea Mungu atupe neema tukumbuke ni wapi tulipokosea tukatengeneze. Uf 2:5(a).

  Mwisho kila mmoja akae katika nafasi ambayo Mungu alimweka. Mke kumtii mume wake na Mume kumpenda na kuishi na mke wake kwa akili.Ef 5:22-33, Kol 3:18-19, 1Pet 3:1-12.

  Mungu akubariki Mtumishi wa Mungu. Bwana ameweka chechemi kwako tunahitaji kuendelea kunywa maji yake ili tuendelee kuimarika. Barikiwa sana.

  Like

  • Brother George hakika Mungu wangu akubariki sana kwa mchango huu wa muhimu sana juu ya eneo hili la uponyaji wa ndoa zetu. Binafsi mchango huu kwangu pia ni uponyaji tosha. Ndoa ni kitu kipana sana, hivyo kadri tunavyopata input za watu mbalimbali inasaidia zaidi. Mungu akubariki tuzidi kuombeana. Asomaye na afahamu.

   Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s