Archive for October 2011

UMEJIAANDAAJE KWA TUKIO LA UNYAKUO? (Part 5)

October 28, 2011

(MAENEO YA MSINGI KATIKA KUJIANDAA)

Na : Patrick Sanga

Eneo la tatu – Usimzimishe Roho Mtakatifu.

Andiko la somo – Mathayo 24:44 “Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyoidhani mwana wa Adam yuaja”.

Katika eneo la pili naliandika kwa habari ya kujifunza kusamehe na kusahau kuwa sehemu yako ya maisha na hivyo kujiweka katika mazingira ya kuwa tayari kwa unyakuo. Ili kusoma sehemu ya pili tafadhali boneza link hii https://sanga.wordpress.com/2011/04/30/umejiaandaaje-kwa-tukio-la-unyakuopart-4/

Katika sehemu hii ya tatu nimeona ni vema tuangalie umuhimu wa kutunza mahusiano yetu na Roho Mtakatifu ili tusimzimishe katika maisha yetu. Labda niseme kumzimisha Roho Mtakatifu ni kikwazo kwa mtu kumuona Mungu katika maisha yake ya kawaida hapa duniani lakini pia kunyakuliwa.

Katika kitabu cha 1Wthesalonike 5:19 Biblia inasema ‘Msimzimishe Roho’. Kuanzia ule mstari wa kwanza wa sura hii, Paulo alianza kwa kuwaeleza ndugu wa Thesalonike namna unyakuo utakavyokuwa na pia akaeleza  baadhi ya mambo ya msingi kwa watu hawa kuzingatia ili wasiachwe katika unyakuo huo. Moja ya mambo aliyowaambia ni wao ‘kutokumzimisha Roho Mtakatifu’.

Swali la msingi linalokuja ni kwa namna gani mtu anaweza kumzimisha Roho Mtakatifu? Ukisoma Biblia ya toleo la GNB katika mstari huu inasema Do not restrain the Holy Spirit’ na toleo la KJV linasema ‘Quench not the Spirit’ (1Th 5:19).

Tafsiri hizi mbili zinapanua zaidi tafsiri ya kumzimisha Roho katika dhana mbili tofauti zifuatazo; moja kumzimisha Roho ina maana ya kumzuia Roho Mtakatifu asitawale na kuongoza maisha yako kwa kukataa msaada wake maishani mwako. Pili, kumzimisha Roho Mtakatifu ina maana ya kuishi katika mazingira ambayo yanamfanya Roho Mtakatifu ashindwe kukusaidia.

Mazingira ambayo Roho Mtakatifu anaweza kuzimishwa; 

  • Kutokumpa nafasi akusaidie

Kwa mujibu wa Matahayo 14:16, Roho Mtakatifu ameletwa kwetu kama Msaidizi. Kwa tafsiri Msaidizi ni yule atoaye msaada pale anapohitajika na kupewa nafasi ya kufanya hivyo. Vivyo na hivyo na Roho Mtakatifu kama hujampa nafasi ya kukusaidia (ingawa yupo ndani yako), hawezi kufanya hivyo na kwa hiyo taratibu utakuwa unamfungia/unamzuia kukusaidia maishani mwako.

  • Kukosa upendo

Ukisoma kitabu cha 1 Wakorinto sura ya 13 na 14, utagundua kwamba suala la upendo limepewa msisitizo wa kipekee kwa mtu ambaye anataka kuona utendaji wa kazi wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yake na kwa ajili ya wengine pia. Upendo kwa mtu aliyejazwa Roho Mtakatifu ni moja ya vigezo muhimu sana kwa Roho Mtakatifu kusema/kujifunua na kufanya kazi ndani yako. Hivyo kukosa upendo ni dalili ya kumzimisha Roho Mtakatifu ndani yako. Ndiyo maana Paulo anasema hata kama angekuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, pia kuwa na imani timilifu kiasi cha kuhamisha milima, kama hana upendo si kitu yeye, naam ni
bure tena ni ubatili (1Wakorinto 13:1-3).

  • Kuongozwa au kuenenda kwa mwili

Paulo aliwambia hivi wandugu wa Galatia ‘Basi nasema, Enendeni kwa kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili’ (Wagalatia 5:16). Maneno haya alikuwa akiwaambia watu waliokoka na si wasiomjua Mungu. Kanisa la Galatia lilikuwa limeacha kuenenda kwa Roho likaanza kwenda kwa mwili. Paulo akajua jambo hili litamzimisha Roho wa Bwana ndani yao, na kwa sababu hii hawatweza kuurithi uzima wa milele na pia kunyakuliwa kama Bwana angekuja kwa nyakati zile. Ndipo akawaonya akisema enendeni kwa Roho ili msizitimize tama za mwili.

  • Kutokutii maelekezo yake

Roho Mtakatifu kuitwa Msaidizi haina maana tunapaswa kumpamngia cha kufanya. Yeye ndiye mwenye kutuongoza katika njia itupasayo kuiendea. Kinachotakiwa ni mtu kuwa mtiifu kwa yale ambayo Roho Mtakatifu anakuagiza. Kukosa utiifu mara kwa mara kila anapokusemesha/kukuagiza ni kumjengea mazingira ya kutoendelea kusema na wewe na hivyo kuondoka kwako na kutafuta mtu mwingine amtumie kwa kusudi lake. Je, unategemea nini Roho wa Bwana akiondoka
ndani yako?

  • Kukosa ufahamu wa utendaji wake

Mara nyingi watu wamemzimisha Roho kwa kutokujua utendaji wake ulivyo. Kuna nyakati Roho Mtakatifu anaweza akaleta msukumo ndani ya mtu wa kumtaka
aombe, atulie kusoma neno n.k. lakini kwa kutokujua namna anavyosema wengi hujikuta badala ya kutulia na kufanya kile alichopaswa kufanya, wao hufanya
mambo mengine.

Pia kuna nyakati katika ibada (sifa, maombi nk), Roho Mtakatifu anaweza akashuka juu ya mtu au watu na akataka kusema jambo, lakini viongozi wa
makanisa au vikundi husika wakawazuia hao watu. Kufanya hivyo bila uongozi wa Mungu ni kumzimisha Roho. Mandiko yako wazi kabisa kwamba hatupaswi kutweza unabii (1 Wathesalonike 5:20) na wala hatupaswi kuzuia watu kunena kwa lugha (1Wakorinto 14:39). Zaidi tumeagizwa kujaribu mambo yote, na tulishike lililo jema (1 Wathesalonike 4:21).

Je tutajaribuje mambo yote ikiwa tunawazuia watu Kunena na pia tunatweza unabii? Hofu yangu ni kwamba kwa kuzuia watu kunena na pia kutweza unabii tunaweza tukajikuta tunamzimisha Roho Mtakatifu na kukataa uongozi wake kwenye maisha yetu. Ni vema tukakumbuka kile ambacho Paulo aliwaambia Wakorinto juu ya mambo haya kwamba  ‘mambo yote yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu’ (1 Wakorinto 14:40). Naam na hili lina maana ni vema kwanza ujue utendaji wa Roho Mtakatifu ukoje ili usije ukajikuta unamzimisha kwa kutokujua.

Pengine yapo mazingira mengine ambayo mtu anaweza akajikuta anamzimisha Roho Mtakatifu. Kumbuka jambo hili kwamba kumzimisha Roho Mtakatifu ni kumzuia asikusaidie, jambo  ambalo tafsiri yake ni kukataa uongozi wake kwenye maisha yako. Biblia inasema katika Warumi 8:9 ‘Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo huyo si wake’. Usifanye mchezo na Roho Mungu hakikisha unatunza sana mahusiano mazuri kati yako na yeye kwa kutokumzimisha.

Naam asomaye na afahamu, nawe usimzimishe Roho Mtakatifu.

UPONYAJI WA NDOA ZETU

October 28, 2011

 Na: Patrick Sanga

Siku moja mama Allen (hili siyo jina lake halisi) alianza kunishirikisha mambo ya ndoa yake yanavyomtesa. Akaniambia mwanangu hizi ndoa tunapenda tu kuingia bila kujua kilichomo ndani yake. Hivi unavyoniona sina hamu kabisa ya ndoa, maana maisha tunayoishi (ingawa kwa nje watu wanaona tuko pamoja), lakini ukweli ni maisha ya taabu na majuto karibu kila siku.

Tabia ya mume wangu imefika mahali haivumiliki. Nikamuuliza tatizo ni nini hasa? Akasema ni fedha, elimu yake na kutoka nje ya ndoa. Fedha ya mume wangu wanaijua wazazi wake na si wazazi wangu, kwani mara kwa mara yeye hutuma fedha kwa wazazi wake. Inaniuma maana natamani hata mie  wazazi wangu niwatumie fedha pia.

 Mume wangu ni kweli Mungu kamjalia kuwa na elimu ya kutosha, lakini elimu yake imekuwa dharau kwangu nisiye ana elimu kama yake. Maana hunisema kwa sababu ya elimu yangu ndogo, kazi yangu na mshahara wangu mdogo ukilinganisha na wake.  Kubwa na baya Baba Allen sio mwaminifu katika ndoa, sina amani na hasa ukizingatia ugonjwa huu wa ukimwi, nina mashaka makubwa sana ndani yangu.

Nikamuuliza umefanya jitihada gani ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizi za ndoa yako? Akajibu akasema nimeamua kuishi naye kwa kuzikubali tofauti zetu (agree to differ). Kwa lugha nyingine nimekubali kuishi na hali hii, kwamba haya ndiyo maisha yangu ya ndoa chini ya jua. Hivyo imefika mahali sina jingine la kufanya ila kukubali kwamba mwenzangu yuko vile na mimi niko hivi, tutendelea kuishi kwa kutofautina hadi kifi kitutenganishe, kwani jitihada za kujaribu kurekebisha mambo haya zimekwama.

Baada ya kusikia maelezo haya niliumia sana, nikamshauri mambo kadhaa ya kufanya ili kuiponya ndoa yake. Lengo langu la msingi katika kuandika habari za mama Allen ni kujaribu kukufukirisha mwanandoa mwenzangu mambo kadhaa yatakayokusaidia kuiponya ndoa yako pia;

  • Jambo la kwanza – Ndoa ni wito wa upungufu na hivyo suala la uvumilivu ni la lazima.

Si watu wengi wanaojua kwamba ndoa ni wito wa mapungufu pia. Maandiko yanasema ‘ Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja’ (Mwanzo 2:24).

Ni dhahiri kwamba watu wanapooana wanakuwa wametoka katika asili na malezi (background) tofauti hasa kutokana na mazingira waliyokulia. Ile tu kwamba huyu anatoka katika familia hii na huyu ile, fahamu kwamba lazima kutakuwa na tofauti kadhaa katika ndoa hiyo. Naam tofauti zenu ndiyo sehemu ya  mapungufu kwenu kama  wanandoa. kwa sababu wewe ungependa mwenzako awe hivi na yeye kuna vitu ambavyo angependa vibadilike kwako.

Na wala usije ukajiona wewe upo kamili, naam kwa upande wako unaweza kuwa sawa lakini kwa mwenzako, hauko kamili. Ni vizuri ukafahamu kwamba unapoingia kwenye ndoa, utakabilana na mapungufu ya mwenzi wako. Kwa sababu hii suala la uvumilivu, kuchukuliana, kusameheana kwa wanandoa ni la msingi ili kufikia mahala pa kutengeneza tabia au mfumo mpya wa ndoa yenu.

  • Jambo la pili – Haijalishi mwenzi wako anatabia mbaya kiasi gani, Yesu anaweza kumbadilisha.

Jambo la pili ambalo nimeoana vema kusisitiza ni kwamba wewe mama au baba ambaye ndoa yako ipo kwenye misukosuko kama ya mama Allen pengine na kuzidi, usifike mahala pa kukata tamaa na kuamua kuishi kwa kuzikubali tofauti zenu kama sehemu ya maisha. Kwa kufanya hivyo utakuwa unamzuia Roho Mtakatifu kukusaidia kuiponya ndoa yako. Ni lazima kwanza ubadili fikra zako na mtazamo wako kwamba, kwa Mungu hakuna lisilowezekana na hivyo haya si maisha yangu ya ndoa ninayostahili kuyaishi.

Kwa Mungu sisi tu watoto wake. Hakuna Baba mwenye kufurahia kuona maisha ya ndoa ya watoto wake yanakuwa ya majuto. Mungu alipoleta wazo la ndoa ilikuwa ni kwa ajili ya kusudi la ufalme wake na kuwa furaha kwa watoto wake na si majuto. Nasikitika kusema leo, ndoa nyingi zimekuwa ni majuto na si kile Mungu alikiona wakati wa uumbaji hata akasema, kila kitu nilichokifanya ni chema sana (Mwanzo 1:31).

Kwa kilio kilichopo kwenye ndoa hivi sasa ni dhahiri kwamba kuna mahali kama wanandoa tumekosea na kumpa Iblisi nafasi (Waefeso 4:27) hata ameleta majuto kiasi hiki. Ushauri wangu ni kwamba ni vema kila mwanandoa akasimama kwenye nafasi zake (Mwanaume kama kichwa na Mwanamke kama Mlinzi na Msaidizi nk) kwa pamoja tumpinge Shetani naye atatukimbia. Endapo mwenzi wako hayuko tayari kwa hili au hamjui Mungu wako, basi wewe mwenye kujua siri hii kama anza, maana kwa Mungu mtu mmoja natosha kuleta uponyaji wa Taifa, je si zaidi ndoa yako? Naam usikate tamaa, Mungu wetu, ni MUNGU ASYESHINDWA.

 

Bwana Mungu na akusaidie katika kuzikabili changamoto za ndoa yako.