Archive for August 2011

NAJUTA KWA NINI NILIKUBALI KUOLEWA?

August 24, 2011

Na: Patrick Sanga

Baada ya mwaka mmoja wa ndoa, Merian asema anajuta kwa nini alikubali kuolewa. Merian na Joseph (haya siyo majina yao halisi) ni mtu na mumewe. Nikiwa katika Mkoa wao kikazi, niliamua kuwatembela wanandoa hawa. Merian alinipokea na kunikaribisha ndani kwa furaha sana. Tukaanza kuongea nami nikamuuliza, Joseph yupo? Akaniambia bado hajarudi kutoka kazini, hata hivyo kaniambia yupo njiani anakuja.

Tukaanza kuzungumuza mambo kadha wa kadha na kisha nikamuuliza mnaendeleaje na ndoa yenu changa? Baada ya kuwa nimemuliza swali hili akacheka na kisha akaanza kwa kusema, nyie maisha haya ya ndoa yaacheni tu, kwa kweli najuta kwa nini nilikubali kuolewa? Kauli hii ilinishtua sana kwa sababu kwanza sikuitegemea na pia ndoa hii ilikuwa ndio imetoka kutimiza mwaka  wa kwanza tu.

Kwa haraka kabla hajaendelea nikamzuia asiseme hayo maneno tena, maana nilijua kadri anavyosema ndivyo anavyozidi kuumba uharibifu kwenye ndoa yake. Akaniambia usinizuie, si umeuliza tunaendeleaje, subiri nimalize kukuelezea. Ndipo akaanza kuniambia kile kilichompelekea kusema anajuta kwa nini alikubali kuolewa (Kwa ufupi ni changamoto ambazo kwa ujumla naweza kusema za kawaida, hata hivyo sitaweza kuziandika hapa kwa sababu maalum).

Katika maelezo yake Merian aliniambia, vijana wengi sana walinifuata ili kunioa, mie nikawakataa, natamani ningeolewa na yoyote kati ya wale wengine, lakini si hapa nilipo na laiti likitokea lolote sasa (kwa maana ya mwenzake kufa) sitakubali kuolewa tena.

Mpenzi msomaji sijui kama unakiona ninachokushirikisha kupitia maisha ya wanandoa wenzetu hawa. Kumbuka ni mwaka mmoja tu wa ndoa, na leo tunashuhudia Merian akijutia maamuzi yake ya kuolewa na Joseph. Licha ya kwamba ni mwaka wa kwanza tu, lakini wawili hawa wameokoka pia.

Maelezo ya dada Merian yaliniletea maswali matano (5) ndani yangu ambayo ndiyo ninayotaka tujifunze kutoka kwake;

Swali la kwanza; Je! Merian, alijua nini maana ya ndoa kabla ya kuolewa?

Swali la pili: Je, Merian alijua aina ya maamuzi anayotaka kufanya kabla ya kuolewa?

Swali la tatu: Je, Merian alimuhusisha Mungu kabla ya kuolewa ili ampate mwenzi sahihi wa kuishi naye?

Swali la nne: Je, Merian alikuwa amejiandaa/andaliwa kifikra kuishi kama mke?

Swali la tano: Je, mpaka sasa, Merian anajua wajibu wake ni nini kwenye ndoa?

Kutokana na maswali haya niliwaza mambo matatu ambayo, nafikiri kama vijana wangefahamu yatawasaidia katika ndoa zao;

  • Moja, ni vema vijana wajifunze kumshirikisha Mungu awaongoze kupata mwenzi sahihi wa maisha, kabla hawajaingia kwenye hizo ndoa. 
  • Mbili, ni vema vijana wakajifunza kufikiri kimapana kabla ya kuingia kwenye ndoa. Swali la msingi katika kufungua tafakuri hii, ni kwa nini mtu aoe au kuolewa? Ni swali fupi lakini kama wewe ni mtu ambaye hufikiri kimapana swali hili litakujengea msingi mzuri wa baadaye. Naam kile kitabu cha 1 Wakorinto sura nzima ya saba kikuongoze katika tafakuri hii.
  • Tatu, ni vema vijana wangefunzwa/kuandaliwa vya kutosha kuhusu ndoa na hasa wajibu uliopo mbele yao. Endapo kama Serikali inawasomesha watumishi wake kwa lengo la kuwaongezea uwezo na maarifa ya kutekeleza majukumu yao, basi ifike mahali kanisa, wazazi, viongozi wa vijana nk makundi haya yaone umuhimu wa kuwaandaa vijana wao kuyakabili maisha ya ndoa.

Watu wengi hufikiri chanzo cha matatizo kwenye ndoa zao ni Shetani. Ndio hii ni sababu moja, lakini sababu nyingine kubwa, ni watu wengi kukosa ufahamu wa masuala ya ndoa kabla na baada ya kuingia kwenye hizo ndoa. Naam wakati watu wanasema Shetani anaangamiza ndoa zetu, Mungu anasema, ndoa za watoto wangu zinaangamizwa kwa kukosa maarifa (Hosea 4:6).

Ni imani yangu kwamba, kama mambo haya yatazingatiwa, sehemu kubwa ya changamoto ambazo wanandoa wanapitia, zingepata ufumbuzi wa haraka. Natoa wito kwa wadau mbalimbali wa masuala ya ndoa na hasa Wachungaji, Walimu na Viongozi wa makundi ya kiroho, kuanzisha utaratibu wa kuwa na mafunzo maalum kuhusu ndoa, kwa vijana ambao wameweka wazi dhamira zao za kuingia kwenye maisha ya ndoa.

Ni vema pia, hata kwa wale ambao wako ndani ya ndoa, wakawekewa utaratibu wa kuwa na mafunzo ya mara kwa mara, maana kwa mtazamo wangu ndoa ni shule ambayo, wahusika wanapaswa kuongeza (kujifunza) ufahamu wao kila siku, ili kulitumikia vema kusudi la Mungu. 

Bwana Yesu na utusaidie watoto wako, Amen!

MWANANGU, YULE MAMA HAKUMALIZA VIZURI SAFARI YAKE

August 10, 2011

Na: Patrick Sanga

Waraka wa Agosti

Mwanangu yule mama hakumaliza vizuri safari yake!

Hivi ndivyo Mchungaji wangu, alivyoanza kunieleza kwa habari ya kifo cha mama mmoja tuliyekuwa tukisali naye. Nilimfahamu mama huyu kuanzia mwaka 2001 nilipookoka. Kwa ufupi alikuwa ni mama mwenye kumpenda sana Mungu, aliye jali ibada mbalimbali na zaidi Mwana maombi mzuri. Alikuwa ni mama ambaye ni mfano wa kuigwa kwa mambo mengi, na kwa jinsi ya kibinadamu naweza kusema alikuwa, Mshirika mwaminifu. Mama huyu aliwahi pia kuwa mmoja wa viongozi wetu.

Kuanzia mwaka 2001 hadi 2004, nilikuwa nikiabudu pamoja na yule mama. Nilipoanza chuo ndipo nikaondoka na kwenda Mkoa mwingine kimasomo. Mwaka fulani niliporudi likizo, nikaenda kanisani kwenye ibada ya jioni, nilipofika kanisani nikaambiwa ibada ya jioni ile inafanyikia kwa mama huyu kwani amefariki. Moyoni mwangu nilihuzunika kupata taarifa ile, ila nilipata tumaini na kuamini kwamba maadam alikuwa ameokoka na endapo aliendelea kuwa mwaminifu kwa Mungu wake basi atakuwa yupo na Bwana akifurahi. Ndipo nikaenda kuungana na washirika wenzangu, kwenda kuwafariji familia ile kwa kuondokewa na ndugu yao. 

Kesho yake ndipo nilienda kwa Mchungaji wangu kumsalimu na pia kumpa pole kwa kupatwa na msiba huo. Baada ya kumpa pole kwa kuondokewa na mama huyo, ndipo alipoanza kwa kusema ‘Mwanangu, kwa kweli yule mama hakumaliza vizuri safari yake. Mungu ndiye ajuaye yuko wapi, ila nami pia kama Mchungaji wake, nasikitika kusema hakumaliza vizuri’. Kauli hii ilinishtua sana, nami nikamuuliza kwa nini unasema hivyo Pastor? Ndipo akaniambia yote ambayo yule mama alifanya miezi kadhaa kabla ya kifo chake (samahani kwa sababu maalum sitaweza kuandika yote aliyofanya yule mama).

Baada ya Mchungaji wangu kunielezea maisha yote ya yule mama katika siku zake za mwisho, ndani yangu niliumia sana. Naam niliumia kwa sababu kubwa mbili; Moja ni namna nilivyokuwa namfahamu na kumpenda yule mama kutokana na juhudi na imani yake katika Bwana. Mbili ni ufahamu nilionao kuhusu wapi mtu anakwenda kama hakufa katika Bwana. Maana imeandikwa ‘…Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao’ (Ufunuo 14:13)

Kama mtu hakufa katika Bwana (utakatifu) mahali anapokwenda panaitwa kuzimu.   Kuzimu ni mahali ambapo laiti mwanadamu angejua nini kinaendelea huko, si tu angemwamini Yesu, bali asingeleta mchezo kwenye wokovu na angeishi maisha ya utakatifu kuzidi maelezo. Jambo moja ambalo nina hakika nalo ni hili, endapo mtu atakufa katika dhambi zake, bila kutengeneza njia au mahusiano yake na Mungu akali hai, basi huyo atakuwa amemaliza safari yake vibaya, na kuzimu ndipo mahali ambapo ataenda.

Mpenzi msomaji, najua watu wengi hawapendi kuambiwa ukweli huu, lakini ni vema uujue kabla hujafa, ili ujifunze kuishi maisha ya kumpendeza Mungu wako. Biblia inasema ‘Na kama vile watu walivyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu’ (Waebrania 9:27). Je wewe utamalizaje safari yako hapa duniani? Je unajua kwamba kifo chako ndio mwanzo wa maisha mapya ya umilele? Naam maisha hayo ni ama ya mateso milele (kuzimu kisha Jehanamu) au raha milele (mbinguni kisha Jerusalemu mpya).

Wapi mtu atataka kwenda baada ya kufa anapaswa kufanya maamuzi akiwa hai. Naam si tu kuokoka bali kuishi maisha matakatifu, maana wapo wengi ambao waliokoka lakini baada ya kufa kwao wakajikuta kuzimu, na hii ni kwa sababu hawakuwa waaminifu kwa Mungu wao katika kutii amri zake. Kama unafikiri kuwa Mkristo ni tiketi ya kukupeleka mbinguni siku ukifa, badilisha fikra zako mapema, maana, mbinguni hawaendi Wakristo, bali watakatifu, naam wale wayafanayao mapenzi ya Mungu hapa duniani (Mathayo 7:21). Naam ili kuongeza ufahamu wako pia kuhusu wapi mtu huenda baada ya kufa katika dhambi bonyeza link hii http://www.spiritlessons.com/Mary_K_Baxter_A_Divine_Revelation_of_Hell.htm

Kwa maelezo ya Mchungaji wangu yule mama katika siku zake za mwisho alifika mahala pa kwenda kwa waganga wa kienyeji ili kupata msaada. Nami moyoni mwangu nilijiuliza maswali mengi kwamba, kwa nini alienda kwa waganga wa kienyeji kutafuta msaada? Je, ni kweli Mungu wake aliyemwamini siku zote alishindwa kumsaidia? Kwa nini aliruhusu Shetani amdanganye kiasi hiki, kama Hawa alivyodanganywa?      (Mwanzo 3:1-19). Ndipo nikajua kuna mahali yule mama alimpa Ibilisi nafasi (Waefeso 4:27) na Shetani akatumia nafasi hiyo ili kuhakikisha mama yule anamaliza vibaya.

Nilipozidi kutafkari juu ya jambo hili, ndipo nikakumbuka kile ambacho Mtume Paulo aliwaambia Wagalatia akisema ‘Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambaye Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulubiwa? Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Je mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho mnataka kukamilishwa katika mwili? (Wagalatia 3:1-3).

Ukisoma vizuri sentensi za Paulo ambazo nyingi zipo katika mfumo wa maswali ni ishara kwamba Paulo mwenyewe alikuwa haamini kile ambacho anakiona kinatokea kwa Wagalatia. Kwani alijua walivyoanza vizuri na Bwana, lakini hali yao ya mwisho ilikuwa ni mbaya tena ya mwilini. Kwa sababu hii Paulo akaugua sana rohoni, ndipo ikamlazimu kutumia lugha ngumu (kali) sana ili kuwasaidia. Naam kwa andiko hili tunajua kwamba mtu anaweza akaanza safari yake vizuri na kisha akamaliza vibaya, ndiyo maana Mhubiri 7:8a naye anasema ‘Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake…’

Ni huzuni kubwa sana kwa mtu aliyemjua Mungu halafu akarudi nyuma na kumaliza katika mwili. Mpendwa wangu jifunze kuchunga na kutunza mguu wako katika Bwana ukiwa makini wapi unakanyaga. Ni vema tumruhusu Roho Mtakatifu atuongoze na kutufundisha njia itupasayo kuiendea, huku tukiwa watiifu na waaminifu kwake (Zaburi 32:8). Neno la Bwana na liongoze hatua zetu ndani yake kwa kuwa imeandikwa ‘Neno la Bwana ni taa ya miguu yangu’ (Zaburi 119:105). 

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nawe kukusaidia.