KWA NINI IMANI YA MWANAMKE MKANANAYO ILIONEKANA KUWA KUBWA?

Na: Patrick Sanga

Nakusalimu kwa jina la Bwana, amani na iwe kwako.

Katika Mathayo 15:21-28 maandiko yanasema “Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akamsujudia, akisema, Bwana, unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yaka tangu saa ile

Katika zamu hii  nimeona vema kujibu swali jingine linalohusu imani ya mwanamke Mkakanayo.  Huyu Mama alikuwa mwenyeji wa nchi ya Kanaani ambayo ilikuwa karibu na pwani ya Bahari ya kati kutoka Sidoni. Kwa bahati nzuri Yesu alikuwa amekwenda katika miji ya Tiro na Sidoni kihuduma, ndipo akakutana na mama huyu ambaye alikuwa anahitaji msaada wa Yesu apate kumponya bintiye.

Haikuwa jambo rahisi kwa Yesu kuachilia uponyaji uende kwa yule binti. Lakini baada ya mvutano wa muda mrefu, Yesu alimwambia yule mama ‘Imani yako ni kubwa, na iwe kwako kama utakavyo’. Sasa swali la msingi ninalotaka kujibu ili nasi tupate kujifunza ni hili; kwa nini imani ya yule mama ilionekana kuwa kubwa kiasi cha kuamua uponyaji utoke kwa Yesu na kwenda kwa binti yake na kumponya saa ile ile?

Yafuatayo ni mambo matatu yaliyompelekea Yesu kusema, Mama, imani yako ni kubwa;

 • Kutokukata tamaa/kuchoka.

Kwa mara ya kwanza yule mama alipoeleza hitaji lake kwa Yesu, maandiko yanasema Yesu hakujibu neno. Na kwa hiyo tunaweza kusema, Yesu hakusikiliza wala kujali maombi ya yule mama. Naam mwitikio huu wa Yesu haukumvunja moyo yule mama akaendelea kuomba tena kwa kupiga kelele ili Yesu amsaidie.

 • Aliyapuuza/hakujali maneno ya wanafunzi na wale walifuatana na Yesu.

Kwa kadri yule mama alivyooendelea kumsihi Yesu amponye mwanaye, ilifika mahali wanafunzi wa Yesu waliona anapiga kelele. Hivyo wakamsihi Yesu amfukuze  ili asiendelee kuwapigia kelele. Sijui kama unaliona jambo hili kwa upana wake. Huyu mama ana  hitaji katika nyumba yake, anajieleza kwa Yesu, Yesu ana nyamaza, kama vile haitoshi Wanafunzi wa Yesu wanasema anapiga kelele. Sasa kilichomsaidia yule mama ni kupuuzia kauli zote zenye kumvunja moyo, yeye alitaka kusikia kutoka kwa Yesu na si wanadamu. Kwa hiyo hakuruhusu maneno yao yamvunje moyo/yaweke mpaka kwa kile anachoamini.

 • Alikuwa na ufahamu wa masuala ya kiroho(imani).

Ukweli huu tunaupata baada ya kuona majibu ya huyu mama pale, Yesu, alipomwambia; kwanza hakutumwa kwa watu wa taifa (kabila) lake na pili kumponya bintiye ni sawa na kuwatupia mbwa chakula cha watoto. Katika hali ya kibinadamu majibu ya Yesu na wanafunzi wake kwa huyu mama, yalitosha kumfanya huyu mama kukata tamaa na ikibidi kumtukana Yesu na wanafunzi wake pia. Lakini mwanamke huyu wa ajabu hakufanya hivyo.

Ile kuendelea kuomba kwa unyenyekevu kwa Bwana amponye bintiye na pia kujibu kwamba hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao, ilidhihirisha kwamba ni lazima huyu mama, ingawa alikuwa Mkaanani kuna namna alikuwa ana ufahamu wa mambo ya imani katika Kristo (neno la Mungu). Kwa hiyo hakikumsumbua watu (Yesu) wanasema nini, ndani yake alikuwa na ufahamu na imani kwamba hakuna jambo la kumshinda Bwana, na hivyo ndani yake akazidisha uhakika kwamba bintiye atapona tu.   

Naam ile kusema hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao, kauli hili ilimfanya Yesu kuachilia uponyaji kwenda kwa binti yake saa ile ile na ndipo akasema, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo.

Sijui kama umeliona jambo hili mpenzi msomaji, imani ya yule mama ili kuwa kubwa kiasi cha kutenda kwa kadri ya matakwa yake kuhusu binti yake. Ni imani iliyoje kutoka kwa mwanamke wa pande za Kaanani, mahali ambako kwa mujibu wa Yesu hapakuwa kipaumbele chake kuwafikia/kuwasaidia. Naam imani ya huyu mama ilivuka fikra na mipaka hiyo na kumfanya Yesu kuachilia uponyaji kawa kdari ya matakwa na muda anaotaka yule mama (Such a wonderful faith).

Tunajifunza nini?

Naam hata leo kuna sababu kubwa tatu zinazofanya watu washindwe kupokea majibu ya mahitaji yao au yale wanayoamini kwamba Mungu atawafanyia;

 • Kukata tamaa

Utasikia mtu anasema huu ni mwaka wa tatu, tano au saba namuomba Mungu sioni majibu, nimechoka, bora kwenda kwa waganga wa kienyeji au kuacha wokovu. Haajalishi kwa jinsi ya kibinadamu majibu yako yamechelewa kwa kiasi gani, usikate tamaa. Si lengo la Yesu kukutesa au kukuhuzunisha maana, Bwana hapendi kuwatesa wala kuwahuzunisha wanadamu (Maombolezo3:33). Hivyo usikubali kukata tamaa kwa sababu iwayo yote, mruhusu Yesu akusaidie, usijaribu kutegemea akilia zako. Zidisha imani yako kwake, atafanya tu, mpendwa.

 • Maneno ya kusikia

Kwa mujibu wa Yakobo 3:1-12 Ulimi ni kiungo kidogo lakini chenye madhara makubwa. Ulimi ni moto, uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti na hakuna awezaye kuufuga. Kwa huo twamuhimidi Bwana na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mafano wa Mungu nk. Jambo ninalotaka kusisitiza hapa ni kwamba usikubali maneno ya kusikia yakakusababishia ugonjwa wa nafsi yako na hivyo kuharibu imani yako. Kazi ya kinywa ni kusema, huwezi kuzuia watu wasiseme, ila unaweza kuzuia wanayosema kama ni mabaya yasitimie kwenye maisha yako. Naam ni kwa kutumia damu ya Yesu kuyafuta na kwa kutumia neno la Mungu kuumba kile unachotaka.

 • Kukosa ufahamu wa neno la Mungu kuhusu imani

Maandiko yanasema neno la Kristo likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote… (Wakolosai 3:16). Kwa nini likae kwa wingi? Mwimbaji wa Zaburi anajibu ni kwa sababu neno la Mungu ni taa ya miguu yetu, mwanga wa njia zetu(Zab 119:105). Hivyo litakusaidia kushinda vikwazo vya imani yako, maana kila imani sharti ijaribiwe. Yesu mwenyewe alijaribiwa alipokuwa jangwani lakini kwa sababu ya ufahamu wa neno la Mungu alimshinda Shetani. Hakikisha unakuwa na nidhamu ya kujisomea neno la Mungu kila leo.

Kwa sababu imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo, tena bayana ya yale yasiyoonekana (Waebrania 11:1), tunaweza kusema kwamba ukubwa wa imani ya huyu Mama ulitokana na uhakika aliokuwa nao kwamba Yesu atamponya mwanawe licha ya upinzani aliokutana nao kuhusu imani yake. Si tu kwamba yule mama alikuwa ana amini Yesu atamponya bintiye, bali yeye alishaona kwa imani kwamba Yesu amemponya mwanawe na hivyo alikuwa anang’ang’ania utimilifu wa kile alichoona kwa imani. Naam alikiona alichokiamini, hivyo alikijua anachokiamini, akakipata alichokiona.

Naam hakikisha unaongeza imani yako kila siku, ili ifikie na kuzidi ile ya Mwanamke Mkananayo na hivyo iweze kuamua majibu kwa kadri ya matakwa na muda wako kutoka kwa Yesu.

Mungu akubariki.

Advertisements

2 comments

 1. Jambo moja muhimu ambalo ni budi kulisema juu ya mama huyu ni kuona kwake mbali ya lile lilombele yake. Alitambukile kuwa makombo ya chakula cha mfalme bado ni chakula cha mfalme-yaani ni kile alichopikiwa kwa hiyo hakibadiliki kwa sababu tu ni mabaki. Ni hakika pia kuwa mbwa wa mfalme katika hali ya kawaida hupata chakula kizuri kwa kukuwa ni mabaki. Kumbuka pia kuwa masazo sio chakula kilichotupwa jalalani ni kile kilichobaki baada ya waliotakiwa kula kushiba. Kwa mantiki ya imani, mama huyo alitarajia yasioonekana kwa macho, yasiyosikizwa, yasiyoguswa, yasiyonuswa bali yale yatarajiwayo. Alitaraji kupata uponyaji na daktari wake alikuwa ni Yesu pekee. Hakumwona Yesu kama tabibu bali kama mleta uhai. Na kwa hivyo hakuyaona majibu ya Yesu wala kutojaliwa na wanafunzi kama kikwazo. Aliona busara katika majibu yaliyotolewa. Alitambua nafasi yake kama Mkanaani ambaye kwa hakika na kwa mujibu wa Yesu hakuwa sababu ya yeye kuja duniani. Na mama yule alitumia mwanya ulikuwapo kutoa mahitaji yake. Hakutaka nafasi imponyoke!

  Wakati mwingine Yesu aweza kuja na fursa finyu anayoitoa isitumiwe vyema. Kuona fursa nako ni kufunuliwa! Kuona fursa katika wokovu kunataka imani iliyokomaa! Kumbuka kufunuliwa sio jambo shitukizi linatokana na Imani!

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s