UMEJIAANDAAJE KWA TUKIO LA UNYAKUO?(Part 4)

 (MAENEO YA MSINGI KATIKA KUJIANDAA)

Na: Patrick Sanga

Andiko la somo: Mathayo 24:44 “Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyoidhani mwana wa Adam yuaja”.

Eneo la pili – Jifunze kusamehe na kusahau

Mpenzi msomaji heri ya Pasaka na ninakusalimu kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo; katika eneo la kwanza niliandika kwa habari ya ‘kuwa makini na matumizi yako ya muda’. Ili kusoma eneo hilo la kwanza bonyeza link ifuatayo endapo hukusoma https://sanga.wordpress.com/2010/11/22/umejiandaaje-kwa-tukio-la-unyakuo-part-3/

Naam katika eneo hili la pili Mungu ameweka msukumo ndani yangu ili tujifunze habari za kusamehe na kusahau kama sehemu yetu ya maandalizi kwa tukio la unyakuo. Biblia katika kile kitabu cha Mathayo 6:14-15 inasema “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu”.

Ukitafakari sentensi hizo utagundua kwamba, Mungu wetu, anataka na sisi kama watoto wake tuwe na tabia kama yake ya kusamehe na kusahau. Hii ni kwa sababu ya upendo wake kwetu na utayari wake juu yetu katika kutusamehe makosa na maovu yetu. Ndiyo maana maandiko yanasema kama Mungu angelihesabu maovu yetu nani angelisimama. Naam mara kwa mara Mungu, anafanya kazi ya kusamehe na kusahau makosa yetu. Yeye yupo wazi kwamba kama sisi hatutakuwa tayari kusamehe na yeye hatatusamehe makosa yetu. Fahamu kwamba kama Mungu hatatusamehe makosa yetu, hatutakuwa sehemu ya wale watakaonyakuliwa. Kwa hiyo jambo la msingi ni kujifunza kusamehe na kusahau.

Kwa nini tusamehe na kusahau? – hii ni kwa sababu katika safari ya wokovu makwazo, mambo ya kuchukiza, kukasirisha hayana budi kuja. Na mambo haya yanaletwa na adui lengo lake ni kuhakikisha tunamkosea na kumkosa Mungu kwa sisi kutokuwa na roho ya kusamehe na kusahau. Katika Luka 17:1-4 imeandikwa “Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu Yule ambaye yaja kwa sababu yake… Jilindeni; kama ndugu yako akikukosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikuosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe”.

Kwa uzoefu nilionao katika Bwana ndani ya miaka zaidi ya kumi mpaka sasa tangu nilipo okoka, nimeona, nimekutana na zaidi kusuluhisha pia kesi nyingi za wapendwa ambazo chanzo chake ni ugomvi, makwazo na mwishowe hakuna anayetaka kumsamehe mwenzake. Najua ni rahisi kusema Jifunze kusamehe na kusahau kwa maneno, lakini inapofika kwenye hali halisi ni ngumu sana. Hata hivyo tayari Mungu ameshaagiza tusamehe, hatuna namna ya kukwepa ni lazima tufanye hivyo kama tunataka kwenda kuishi naye milele. Ili uweze kujifunza kusamehe ni kusahau yafuatayo ni mambo manne ya msingi yatakayokusaidia;

  • Omba na kutafakari kimaswali kabla hujachukua uamuzi wowote endapo umekosewa.

Inapotokea  mtu yoyote kakukosea na kwa jinsi ya kibinadamu ni ngumu kwako kusamehe, ni vema ukaliombea hilo suala linalokutatiza kimaswali kabla hujachukua uamuzi wowote ule. Musa ni mfano wa kuigwa katika jambo hili. Ukisoma Bibilia katika kitabu cha Kutoka na Hesabu utaona namna Musa alivyokuwa akikutana na mambo mengi ya kumkwaza katika uongozi wake. Mara nyingi Musa hakuchukua uamuzi wa haraka bali alimuuliza Mungu kwamba sasa nifanye nini? Katika kila changamoto, Mungu alimuongoza jambo la kufanya na kazi ikaendelea. Nasisitiza kwamba uombe kwanza kwa kuwa ukimaanisha katika kuliombea jambo hilo Bwana atakufunulia kiundani lengo la huo ugomvi nawe utajua sina sababu ya kumpa Ibilisi nafasi na hivyo ni bora kumsamehe. Hii ni kwa sababu katika kila ugomvi/makwazo/kutokusamehe kuna siri/ajenda kubwa ambayo Shetani anataka itimie.

Zaidi yapo maswali kadhaa ya msingi ambayo ningependa ujiulize kila unapokutana na jambo la kukukwaza. Ni vema ujiulize chanzo cha tatizo hilo ni nini? Kwa nini mmekosana/hamna mawasiliano? Kwa namna gani wewe binafsi umechangia? Usipomsamehe aliyekukosea Mungu anakutazamaje? Mara ngapi wewe umekosea, Mungu  akakusamehe? kama asingekusamehe leo ungekuwa wapi? Naam pima uamuzi wako tokana na maombi uliyofanya na majibu ya maswali haya ndipo uchukue uamuzi wa kusamehe au kutokusamehe. Ni imani yangu kwamba kama ukiomba na kujiuliza maswali haya kwa uaminifu utaishia kwenye kusamehe tu, naam samehe ili  maombi yako pia yaweze kusikilizwa na  uweze kusamehewa pia (Luka 6:37, Marko 11:25).

  • Jenga na kuboresha mahusiano yako na Roho Mtakatifu

Roho Mtakatifu ndiye Msaidizi wetu katika kukabiliana na mambo mbalimbali hapa dunuani. Si watu wengi wanaotambua nafasi ya Roho Mtakatifu kwenye maisha yao na kumpa nafasi awasaidie. Unapokutana na jambo lolote la kukukwaza iwe kazini, kanisani, nyumbani nk, jifunze kumwambia Roho Mtakatifu jambo hili ni zito kwangu, naomba unipe neema na nguvu ya kusamehe na kusahau, yeye ni mwaminifu atakusaidia. Kwa lugha nyepesi, mshirikishe Roho Mtakatifu kila kwazo unalolipitia akusaidie, hawezi kushindwa.Kama aliweza kumsaidia Yesu Kristo pale msalabani ili kusamehe dhambi zetu tena dunia nzima kwa nini ashindwe kwenye suala lako, naam mtumie atakusaidia (Luka 23:34).

  • Tafuta kupatana na ndugu yako hata kama yeye ndiye kakukosea

Katika maeneo magumu sana kwa wapendwa wengi ni hili la kuanzisha mchakato wa mapatano na mtu aliye kukosea. Hata hivyo hili nalo ni agizo la Bwana Yesu kwamba endapo kama ndugu yako amekukosea msamehe, halafu tafuta kupatana naye tena. Usilipe mabaya, bali wewe tenda wema kama vile Yusufu alivyotenda kwa ndugu zake ambao walimuuza kwa Wamisri (Mwanzo 50: 17-21).

Biblia katika Warumi 12:14,17-21 maandiko yanasema ‘Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani. Msilimlipe mtu uovu kwa uovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama yamkini kwa upande wenu, make katika amani na watu wote. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema’.

Naamini maandiko haya yanajifafanua vya kutosha, tenda nawe utaishi. Jenga mazoea ya kuomba msamaha kwa ajili ya yule aliyekukosea kwani kwa makosa yake anampa Ibilisi nafasi bila yeye kujua (Waefeso 4:26-27).

  • Weka ndani yako sheria ya Bwana na kuitenda

Katika Zaburi 119:165 imeandikwa ‘wana amani nyingi sana waishikao sheria ya Bwana, wala hapana la kuwakwaza’. Pia katika Zaburi 119:105 maandiko yanasema ‘Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu’

Ndani ya neno la Mungu kuna uweza wa kukuongoza wewe kushinda dhambi ikiwa ni pamoja na hali ya kutokusamehe. Jenga mazoea ya kusoma na kulitafakari neno la Mungu kila siku litakujengea uweza ndani wa kuwaza, kutafsiri na kuyatazama mambo mengi ki – Mungu na hivyo hata katika yale ambayo ni magumu kusamehe kibinadamu, utasamehe kwa sababu ya uweza uliopo kwenye neno lake.

Ninapomalizia eneo hili la pili katika kujiandaa na tukio la unyakuo, nakushauri jifunze kusamehe na kusahau, mimi ninayeandika ujumbe huu nimepita katika mazingira ambayo ni magumu kusamehe kwa jinsi ya kibinadamu. Nilipoenda mbele za Mungu kwa njia hizo nilizoandika hapo juu, Bwana mwenyewe aliniongoza kusamehe ikiwa ni pamoja na kuanzisha mchakato wa mapatano na wale ambao wamenikosea.

Mpendwa wangu muda tulionao hapa duniani ni kidogo sana, haipaswi uishi wakati ndani yako kuna mtu au watu ambao hujawasamehe haijalishi wamekutendea nini. Jifunze kusamehe kwa kuwa anayekukosea hajui alifanyalo,laiti angejua makwazo yake na kiburi chake cha kutokuwa tayari kusamehe kina athari gani sasa na wakati ujao asingefanya hayo.

Ni vizuri ukafahamu kwamba unapomsamehe mtu kosa lake maana yake umemuondolea mtu huyo dhambi yake na usipomsamehe maana yake umemfungia mtu huyo dhambi yake. Ukweli huu tunaupata baada ya kusoma Yohana 20:23 inayosema “Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa”. Ukisoma mstari huu katika toleo la GNB Biblia inasema ‘If you forgive people’s sins, they are forgiven; if you do not forgive them, they are not forgiven’.

Mpendwa msomaji ikiwa maandiko yanasemaBWANA ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa…” (Hesabu 14:18), mimi na wewe tu nani hata tushindwe kusamehe? Petro alimuuliza Yesu, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia,sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini (Mathayo 18:21-22). Naam samehe bila kujali ndugu yako amekukosa mara ngapi, samehe tu.

 Hata sasa kuna kundi kubwa la watu wanaokwenda kuzimu kwa sababu ya kutokusamehe, Bwana amekuwa akisema nawe mara nyingi kuhusu kusmehe, lakini hutaki kusikia. Nakusihi fanya haraka kabla ya siku hiyo, kama hausamehi wanaokukosea usitegemee kwenda na Bwana siku ya unyakuo endapo utakuwa hai. Naam utaachwa na kuingia kwenye utawala wa Mpinga Kristo, utawala ambao ndani yake utajaa mateso na huzuni isiyopimika. Jiulize kwa nini uachwe au kwenda kuzimu kwa sababu ya kutokusamehe?. Naam tengeneza upande wako kwa kusamehe kama Bwana wetu alivyotufundisha.

 Ni imani yangu kwamba ujumbe huu utakusaidia na kubadilisha maisha yako ili na wewe ujifunze kusamehe na kusahau.

Mungu akubariki

Advertisements

5 comments

  1. Asante Mungu kwa kutupatia watu kama huyu mtoto wa Sanga kwa maana anatukumbusha kuishi katika utatu wako mtakatifu ili tuje kuurithi ufalme wa mbinguni amina.

    Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s