MJUE SANA MUNGU ILI UWEZE KUZIKABILI CHANGAMOTO ZINAZOKUJA MWAKA 2011

 Patrick na Flora Sanga

Ayubu 22:21 ‘Mjue sana Mungu ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia’.

Heri ya Christmas na Mwaka Mpya wa 2011, mpenzi wetu msomaji wa blog hii.

Kwanza tukupe hongera kwa kuingia 2011, ni jambo la kumshukuru sana Mungu, kwa neema hii aliyotupa.  Mimi na familia yangu tunamshukuru sana Mungu kwa ajili ya mwaka  wa 2010 ambao tumeumaliza. Licha ya changamoto tulizokutana nazo, kwa ujumla umekuwa mwaka wa baraka na neema kwa upande wetu. Nasi tunaamini na kwako pia ndivyo ilivyokuwa japo yawezekana kuna baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki ambao umewapoteza katika mwaka uliopita. Naam wao wametangulia mbele za haki, tuliobaki Mungu ametupa neema ya kuweza kuuona tena mwaka wa 2011.

Tunajua mambo mengi yataandikwa kuhusu mwaka huu wa 2011, naam katika hayo mengi, na sisi pia tuna jambo moyoni mwetu ambalo tunaona ni vema tukakushirikisha katika kuukaribisha na kuukabili mwaka wa 2011. Jambo ambalo tunaamini Mungu ameweka moyoni mwetu kwa ajili yako, ni wewe kuongeza jitihada yako katika kumjua sana Mungu, kama ufunguo wa kukusaidia kuzikabili na kuzishinda changamoto zinazokuja mwaka 2011.

Leo, watu wengi wanaishi mbali sana na kusudi la Mungu kwenye maisha yao. Sababu mojawapo kubwa ya jambo hili ni watu hao kutokumjua Mungu vizuri na kwa mapana. Na kutokumjua Mungu kumepelekea watu wengi kuishi maisha ambayo hawakustahili kuyaishi.

Huenda katika mwaka 2010 umekutana na changamoto kubwa ambazo zimekufikisha mahali ukafikiri kwamba hakuna Mungu, Mungu hana upendo wala rehema, kama kweli ana upendo asingeruhusu lile na hili kutokea kwenye familia, ukoo, jamaa, kazi au biashara yangu nk.

Huenda imefika mahali kutokana na mapito ya mwaka 2010 unaona kama Mungu alikosea katika kuruhusu baadhi ya mambo yatokee. Pengine umetafuta dhambi ndani yako ukifikiri ndio chanzo cha mabaya lakini huoni uhusiano wa mapigo au changamoto ulizokutana nazo 2010 na maovu yako. Imefika mahala ukatamani bora ufe kuliko kuishi, au bora hata Mungu akuchukue uende ukampuzike. Naam yumkini hivi ndivyo ulivyokuwa mwaka 2010 kwako.

Katika mwaka huu wa 2011,Bwana ameweka siri nzuri ndani yetu ili tukushirikishe. Na kama ukiliweka jambo hili kwenye matendo mwaka wa 2011 utakuwa ni wa Baraka kwako. Najua unaweza kutuuliza swali tunajuaje utakuwa mzuri wakati hatujui mwisho wake? Naam uhakika wa mwaka 2011 kuwa wa Baraka tunaupata katika kitabu cha Ayubu 22:21,  maandiko yanasema ‘mjue sana Mungu ili uwe na amani, ndivyo mema yatakavyokujia’. Tunauhakika na jambo hili kwa kuwa hatuendi kwa kuuona, bali kwa imani katika neno la Mungu.

Imani yetu ni kwamba kadri unavyoongeza ufahamu wako katika kumjua Mungu ndivyo unavyoongeza maarifa ya Ki-Mungu ndani yako ya kukusaidia katika kuzikabili changamoto ambazo zipo na zinakuja katika mwaka 2011. Mungu anasema katika Hosea 4:6 ‘Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa…’ Kukosa maarifa ni matokeo ya mtu kutokumjua Mungu.

Labda tuseme hivi, mambo mengi mabaya yaliyotokea kwako mwaka 2010, laiti kama kiwango chako cha kumjua Mungu, kingekuwa kizuri au cha juu yasingekumaliza kwa kulinganisha na hali yako ya sasa.

Kutokumjua Mungu imekuwa kigezo kikubwa sana ambacho Shetani anakitumia katika kuwaonea na kuwaangamiza watoto wa Mungu. Ni wito wa Mungu leo kwamba katika mwaka 2011 ongeza ufahamu wako kuhusu Mungu ndivyo mafanikio, baraka na neema zake zitavyoenda nawe katika mwaka huu.

Kumbuka kwamba namba moja ni ufunguo wa namba nyingine, ni mwanzo wa jambo jingine, ni mwanzo wa kipindi kingine kwa hiyo hakikisha katika mwaka huu unamjua sana Mungu ili uwe na amani.

Utamjuaje Mungu?

Zipo njia nyingi, lakini kubwa na ya kwanza ni wewe kujijengea utaratibu wa kuwa na muda kila siku wa kusoma na kutafakari neno la Mungu, huku ukiomba upate kuelewa unachokisoma. Hakikisha unaweka muda ambao utakuwa mwaminifu katika kutekeleza jambo hili la kumjua Mungu kwa njia ya kutafakari neno lake. Naam kama tulivyosema hapo juu, sababu kubwa ya watu kuangamizwa ni wao kukosa maarifa, na ili uyapate maarifa ya Mungu sharti ulitafakari neno lake.

Jifunze jambo hili kupitia wandugu wa kanisa la huko Beroya ambao maandiko yanasema walikuwa ni waungwana. Uungwana wao ulitokana na tabia yao ya kulipokea neno la Bwana kwa uelekevu wa moyo, na kuyachunguza maandiko kila siku ili waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo. Na kutokana na tabia yao hiyo ya kutafakari neno la Bwana, watu wengi waume kwa wake, na wenye cheo miongoni mwao wakaamini (Matendo ya Mitume 17:10-12).

Kitendo cha Biblia kusema walikuwa wakiyachunguza maandiko kila siku, ina maana ilikuwa ni tabia yao, sehemu yao ya maisha. Na hii inatusaidia kujua kwamba kila siku walikuwa na muda ambao walikubaliana kwamba watakuwa wanakutana kwa lengo la kutafakari na kuchunguza maandiko. Naam jambo hili likabadilisha maisha yao binafsi, familia zao na mji wao kwa ujumla. Kama ukijenga mazoea na kuwa na nidhamu kama ya watu wa Beroya ya kutafakari neno la Mungu kila siku tegemea mambo yafutayo;

Moja ufahamu wako kuhusu Mungu utabadilika, mbili mtazamo na tafsiri yako juu ya mambo mengi utabadilika pia. Naam kuna baadhi ya mambo hata yakitokea kwenye maisha yako utajifunza kuyatazama kwa jicho la Mungu na hivyo kutoruhusu yakuharibie mahusiano yako na Mungu. Hii ni kwa sababu kwa maisha ambayo mwanadamu anaishi chini ya jua, changamoto hazikwepeki. Siku zote utaendelea kukutana na changamoto maishani mwako, ni kifo tu ndio kitakutenganisha na changamoto za hapa duniani.

Kumbuka mwanzo wa somo hili, tumeona kwamba changamoto hizi ndizo ambazo zimechangia kuharibu maisha ya watu wengi. Sasa ushindi dhidi ya changamoto zinazokuja mwaka 2011 kwako upo kwa wewe kuhakikisha unajenga msingi imara kwa kumjua sana Mungu. Anza na Roho Mtakatifu, yeye atakusaidia uwajue Mwana na Baba pia. Hawa watatu watajifunua kwenye maisha yako na kukupa amani, mafanikio na mema yote yaliyokusudiwa kwako katika mwaka 2011, kupitia Roho Mtakatifu ambaye yeye anatenda kazi duniani sasa, kulingana na magawanyo wao wa majukumu.

Kwa kadri unavyomjua sana Mungu ndivyo unavyovuta mema/mafanikio/baraka/uongozi/ulinzi kwenye maisha yako. Naam kadri unavyolitafakari neno ndivyo linavyobadili fikra zako na mtazamo wako juu ya mambo mbalilmbali. Kwa sababu hiyo changamoto au majaribu mengi ambayo Shetani alikuwa amekusudia yakupate, busara na ufahamu ulivyovipata tokana na kutafakari neno la Bwana vitakulinda na kukuhifadhi dhidi ya mabaya yote.

Naam katika mwaka 2011 weka mkakati wa kuwa na muda ambao utampa Bwana kwa lengo la kutafakari neno lake. Neno lake ni taa ya miguu yetu na ni mwanga wa njia yetu (Zaburi 119:105). Kwa hiyo haijalishi utakutana mambo mengi kiasi gani ya kukuvunja moyoukiliweka jambo , kama ukiliweka jambo hili kwenye matendo utakuwa mshindi na zaidi ya kushinda.

Kwa heri mwaka 2010, tunakukaribisha mwaka 2011 kwa imani katika jina la Yesu. Nasi tunatamka kwamba ndani yako tutamjua sana Mungu, hivyo tunaziagiza siku zako, zizalishe kumjua Mungu ndani yetu”. 

Mpendwa msomaji ‘Bwana akubarikie na kukulinda, akuangazie nuru za uso wake na kukufadhili’

Hongera kwa kuingia mwaka 2011, usikate tamaa, mjue sana Mungu, atajifunua kwako kwa namna hujawahi kuona

Advertisements

4 comments

  1. MBARIKIWE SANA WATUMISHI WA MUNGU, Ingawa nimesoma ujumbe huu mwaka ukiwa unaelekea ukingoni lakini nimepokea sehemu yangu. Nimebarikiwa kwa Jina la Yesu Napokea kumjua sana Mungu.

    Mbarikiwe ktk Jina la Yesu.

    Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s