Archive for December 2010

MJUE SANA MUNGU ILI UWEZE KUZIKABILI CHANGAMOTO ZINAZOKUJA MWAKA 2011

December 31, 2010

 Patrick na Flora Sanga

Ayubu 22:21 ‘Mjue sana Mungu ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia’.

Heri ya Christmas na Mwaka Mpya wa 2011, mpenzi wetu msomaji wa blog hii.

Kwanza tukupe hongera kwa kuingia 2011, ni jambo la kumshukuru sana Mungu, kwa neema hii aliyotupa.  Mimi na familia yangu tunamshukuru sana Mungu kwa ajili ya mwaka  wa 2010 ambao tumeumaliza. Licha ya changamoto tulizokutana nazo, kwa ujumla umekuwa mwaka wa baraka na neema kwa upande wetu. Nasi tunaamini na kwako pia ndivyo ilivyokuwa japo yawezekana kuna baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki ambao umewapoteza katika mwaka uliopita. Naam wao wametangulia mbele za haki, tuliobaki Mungu ametupa neema ya kuweza kuuona tena mwaka wa 2011.

Tunajua mambo mengi yataandikwa kuhusu mwaka huu wa 2011, naam katika hayo mengi, na sisi pia tuna jambo moyoni mwetu ambalo tunaona ni vema tukakushirikisha katika kuukaribisha na kuukabili mwaka wa 2011. Jambo ambalo tunaamini Mungu ameweka moyoni mwetu kwa ajili yako, ni wewe kuongeza jitihada yako katika kumjua sana Mungu, kama ufunguo wa kukusaidia kuzikabili na kuzishinda changamoto zinazokuja mwaka 2011.

Leo, watu wengi wanaishi mbali sana na kusudi la Mungu kwenye maisha yao. Sababu mojawapo kubwa ya jambo hili ni watu hao kutokumjua Mungu vizuri na kwa mapana. Na kutokumjua Mungu kumepelekea watu wengi kuishi maisha ambayo hawakustahili kuyaishi.

Huenda katika mwaka 2010 umekutana na changamoto kubwa ambazo zimekufikisha mahali ukafikiri kwamba hakuna Mungu, Mungu hana upendo wala rehema, kama kweli ana upendo asingeruhusu lile na hili kutokea kwenye familia, ukoo, jamaa, kazi au biashara yangu nk.

Huenda imefika mahali kutokana na mapito ya mwaka 2010 unaona kama Mungu alikosea katika kuruhusu baadhi ya mambo yatokee. Pengine umetafuta dhambi ndani yako ukifikiri ndio chanzo cha mabaya lakini huoni uhusiano wa mapigo au changamoto ulizokutana nazo 2010 na maovu yako. Imefika mahala ukatamani bora ufe kuliko kuishi, au bora hata Mungu akuchukue uende ukampuzike. Naam yumkini hivi ndivyo ulivyokuwa mwaka 2010 kwako.

Katika mwaka huu wa 2011,Bwana ameweka siri nzuri ndani yetu ili tukushirikishe. Na kama ukiliweka jambo hili kwenye matendo mwaka wa 2011 utakuwa ni wa Baraka kwako. Najua unaweza kutuuliza swali tunajuaje utakuwa mzuri wakati hatujui mwisho wake? Naam uhakika wa mwaka 2011 kuwa wa Baraka tunaupata katika kitabu cha Ayubu 22:21,  maandiko yanasema ‘mjue sana Mungu ili uwe na amani, ndivyo mema yatakavyokujia’. Tunauhakika na jambo hili kwa kuwa hatuendi kwa kuuona, bali kwa imani katika neno la Mungu.

Imani yetu ni kwamba kadri unavyoongeza ufahamu wako katika kumjua Mungu ndivyo unavyoongeza maarifa ya Ki-Mungu ndani yako ya kukusaidia katika kuzikabili changamoto ambazo zipo na zinakuja katika mwaka 2011. Mungu anasema katika Hosea 4:6 ‘Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa…’ Kukosa maarifa ni matokeo ya mtu kutokumjua Mungu.

Labda tuseme hivi, mambo mengi mabaya yaliyotokea kwako mwaka 2010, laiti kama kiwango chako cha kumjua Mungu, kingekuwa kizuri au cha juu yasingekumaliza kwa kulinganisha na hali yako ya sasa.

Kutokumjua Mungu imekuwa kigezo kikubwa sana ambacho Shetani anakitumia katika kuwaonea na kuwaangamiza watoto wa Mungu. Ni wito wa Mungu leo kwamba katika mwaka 2011 ongeza ufahamu wako kuhusu Mungu ndivyo mafanikio, baraka na neema zake zitavyoenda nawe katika mwaka huu.

Kumbuka kwamba namba moja ni ufunguo wa namba nyingine, ni mwanzo wa jambo jingine, ni mwanzo wa kipindi kingine kwa hiyo hakikisha katika mwaka huu unamjua sana Mungu ili uwe na amani.

Utamjuaje Mungu?

Zipo njia nyingi, lakini kubwa na ya kwanza ni wewe kujijengea utaratibu wa kuwa na muda kila siku wa kusoma na kutafakari neno la Mungu, huku ukiomba upate kuelewa unachokisoma. Hakikisha unaweka muda ambao utakuwa mwaminifu katika kutekeleza jambo hili la kumjua Mungu kwa njia ya kutafakari neno lake. Naam kama tulivyosema hapo juu, sababu kubwa ya watu kuangamizwa ni wao kukosa maarifa, na ili uyapate maarifa ya Mungu sharti ulitafakari neno lake.

Jifunze jambo hili kupitia wandugu wa kanisa la huko Beroya ambao maandiko yanasema walikuwa ni waungwana. Uungwana wao ulitokana na tabia yao ya kulipokea neno la Bwana kwa uelekevu wa moyo, na kuyachunguza maandiko kila siku ili waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo. Na kutokana na tabia yao hiyo ya kutafakari neno la Bwana, watu wengi waume kwa wake, na wenye cheo miongoni mwao wakaamini (Matendo ya Mitume 17:10-12).

Kitendo cha Biblia kusema walikuwa wakiyachunguza maandiko kila siku, ina maana ilikuwa ni tabia yao, sehemu yao ya maisha. Na hii inatusaidia kujua kwamba kila siku walikuwa na muda ambao walikubaliana kwamba watakuwa wanakutana kwa lengo la kutafakari na kuchunguza maandiko. Naam jambo hili likabadilisha maisha yao binafsi, familia zao na mji wao kwa ujumla. Kama ukijenga mazoea na kuwa na nidhamu kama ya watu wa Beroya ya kutafakari neno la Mungu kila siku tegemea mambo yafutayo;

Moja ufahamu wako kuhusu Mungu utabadilika, mbili mtazamo na tafsiri yako juu ya mambo mengi utabadilika pia. Naam kuna baadhi ya mambo hata yakitokea kwenye maisha yako utajifunza kuyatazama kwa jicho la Mungu na hivyo kutoruhusu yakuharibie mahusiano yako na Mungu. Hii ni kwa sababu kwa maisha ambayo mwanadamu anaishi chini ya jua, changamoto hazikwepeki. Siku zote utaendelea kukutana na changamoto maishani mwako, ni kifo tu ndio kitakutenganisha na changamoto za hapa duniani.

Kumbuka mwanzo wa somo hili, tumeona kwamba changamoto hizi ndizo ambazo zimechangia kuharibu maisha ya watu wengi. Sasa ushindi dhidi ya changamoto zinazokuja mwaka 2011 kwako upo kwa wewe kuhakikisha unajenga msingi imara kwa kumjua sana Mungu. Anza na Roho Mtakatifu, yeye atakusaidia uwajue Mwana na Baba pia. Hawa watatu watajifunua kwenye maisha yako na kukupa amani, mafanikio na mema yote yaliyokusudiwa kwako katika mwaka 2011, kupitia Roho Mtakatifu ambaye yeye anatenda kazi duniani sasa, kulingana na magawanyo wao wa majukumu.

Kwa kadri unavyomjua sana Mungu ndivyo unavyovuta mema/mafanikio/baraka/uongozi/ulinzi kwenye maisha yako. Naam kadri unavyolitafakari neno ndivyo linavyobadili fikra zako na mtazamo wako juu ya mambo mbalilmbali. Kwa sababu hiyo changamoto au majaribu mengi ambayo Shetani alikuwa amekusudia yakupate, busara na ufahamu ulivyovipata tokana na kutafakari neno la Bwana vitakulinda na kukuhifadhi dhidi ya mabaya yote.

Naam katika mwaka 2011 weka mkakati wa kuwa na muda ambao utampa Bwana kwa lengo la kutafakari neno lake. Neno lake ni taa ya miguu yetu na ni mwanga wa njia yetu (Zaburi 119:105). Kwa hiyo haijalishi utakutana mambo mengi kiasi gani ya kukuvunja moyoukiliweka jambo , kama ukiliweka jambo hili kwenye matendo utakuwa mshindi na zaidi ya kushinda.

Kwa heri mwaka 2010, tunakukaribisha mwaka 2011 kwa imani katika jina la Yesu. Nasi tunatamka kwamba ndani yako tutamjua sana Mungu, hivyo tunaziagiza siku zako, zizalishe kumjua Mungu ndani yetu”. 

Mpendwa msomaji ‘Bwana akubarikie na kukulinda, akuangazie nuru za uso wake na kukufadhili’

Hongera kwa kuingia mwaka 2011, usikate tamaa, mjue sana Mungu, atajifunua kwako kwa namna hujawahi kuona

KITABU, KITABU, KITABU( Ruhusu mapenzi ya Mungu yatimie kuhusu mwenzi wa maisha yako)

December 29, 2010

 

 

Patrick & Flora Sanga

 

Awali ya yote tunamshukuru sana Mungu, kwa kipawa cha Uandishi, alichotujalia. Mke wangu pamoja nami tumeamua kwamba tutahakikisha tunatumia kipawa hiki siku zote kwa utukufu wa Mungu, katika kuujenga mwili wa Kristo.

 

Katika mwaka huu wa 2010 tumeweza kuchapisha kitabu cha pili chenye kichwa kisemacho RUHUSU MAPENZI YA MUNGU YATIMIE KUHUSU MWENZI WA MAISHA YAKO’. Kitabu cha kwanza nalichapisha mwaka 2006 (kabla sijaoa), kilihusu ‘NJIA KUMI ZA KIBIBLIA ZA KUKUSAIDIA KUMJUA NA KUMPATA MWENZI WAKO WA MAISHA’.

 

Ndani ya mwaka wa 2010 tumeandika zaidi ya vitabu saba vya kiroho. Katika hivyo tumefanikiwa kuchapisha kitabu hiki kimoja, ingawa lengo letu ilikuwa ni kuchapisha vitabu viwili. Jambo la msingi kwetu ni kuzingatia uongozi wa Mungu katika kuvichapisha vitabu hivi, maana katika orodha ya vitabu saba, si jambo jepesi kuamua kwamba ni katbu kipi kianze na kipi kifuate. Tunaamini kwamba, ni mapenzi ya Mungu kitabu hiki kichapishwe katika majira haya, maana tulimwomba Bwana uongozi wake.

 

·        Yaliyomo

 

Kitabu kina jumla ya sura nne kama ifuatavyo;

 

Sura ya kwanza – Ni mpango wa Mungu uoe/kuolewa sawasawa na mapenzi yake.

Sura ya pili – Mungu ndiye anayewajibika kukupa mwenzi wa maisha, ni jukumu lako kuruhusu mapenzi yake yatimie.

Sura ya tatu – Jifunze uhalisia wa mambo  haya  kupitia Yakobo, Hosea na Samweli ndani ya Biblia.

Sura ya nne – Mwenzi wako ana nafasi kubwa sana katika kukusaidia kulitumikia kusudi la Mungu maishani mwako.

 

 Na katika ukurasa wa mwisho wa kitabu kuna sala ya toba.

 

·        Kwa nini kitabu hiki wakati huu?

Suala la mwenzi wa maisha limekuwa changamoto kubwa sana katika kizazi cha sasa. Kwani wapo wanandoa wengi, ambao leo wanajutia maamuzi yao ya kuoa au kuolewa. Naam moja ya sababu kubwa za majuto hayo kwa wanandoa wengi, ni kuoa au kuolewa nje ya mapenzi ya Mungu.

 

Hivyo Kitabu hiki kinaeleza kwa undani nafasi ya Mungu katika kumpa mtu mke/mume, sababu zinazomfanya Mungu afanye hivyo, kwa namna gani mtu anawajibika kuoa au kuolewa sawasawa na mapenzi ya Mungu, Dondoo za msingi kujua kuhusu mapenzi ya Mungu, nafasi ya mwenzi wako katika kulitumikia kusudi la Mungu na mwisho mifano kadhaa ndani ya Biblia itakayokusaidia kufanya maamuzi yako kwa kuzingatia mapenzi ya Mungu.

 

Lengo la kitabu hiki ni kukupa ufahamu na maarifa juu ya mapenzi ya Mungu katika suala zima la kumpata mwenzi wako wa maisha, ili kukusaidia uweze kulitumikia vema kusudi la Mungu, kwani, mwenzi wako wa maisha ana nafasi kubwa sana katika kulitumikia kusudi la Mungu.

 

·        Upatikanaji wa vitabu

Vitabu hivi vitaanza kupatikana kuanzia mwenzi Januari 2010 katika maduka   ya vitabu na wauzaji binafsi Mikoa mbalimbali. Kama pia unafahamu Bookshop/wauzaji ambao twaweza peleka vitabu hivi basi wasiliana nasi ili viweze kusambazwa na kuwafikia watu wengi kwa urahisi. Taarifa zaidi za kule vinakopatikana vitabu hivi tutawajulisheni.

 

·        Tamati

Ni imani yetu kwamba Mungu atagusa na kuponya maisha ya watu wengi ya sasa na ya baadaye, hasa kwa wale ambao wanatarajia kuja kuishi kwa pamoja kama wanandoa. Kwa wewe ambaye bado hujaoa au kuolewa ni vema ukapata nakala ya kitabu hiki, kwa hakika kitakuongezea ufahamu na maarifa ya kukusaidia kufanya maamuzi sahihi katika mapenzi ya Mungu.

 

Ubarikiwe, endelea kuombea kitabu hiki kifanyike baraka na uponyaji kwa kila atakayekisoma.

BALI MTU HUYU NDIYE NITAKAYEMWANGALIA…

December 27, 2010

Na: Patrick & Flora Sanga.

Waraka wa Desemba

Isaya 66:1-2

Bwana asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzika ni mahali gani? Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema BWANA; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu”.

Isa 66:2All these things my hand has made, and so all these things came to be, declares the LORD. But this is the one to whom I will look: he who is humble and contrite in spirit and trembles at my word” (ESV)

Ukisoma mstari huu vizuri kuna mambo mengi unaweza kujifunza lakini kile tunachotaka tukiangaalie katika mwezi huu wa Desemba 2010 ni sifa/tabia ambazo kama mtu akiwa nazo zitamfanya Mungu amtazame/ajifunue kwake na amsikilize mtu huyo. Naam sifa ambazo zitavuta uwepo wa Bwana ukae naye daima. Ni imani yetu kwamba kama ukiliweka jambo hili kwenye matendo lazima Bwana awe upande wako.

Sifa hizo ni;

 • Mtu aliye mnyonge

Kwa tafsiri ya kawaida, Mnyonge ni mtu mwenye kustahili huruma/msaada, mtu asiyejiweza,  mnyenyekevu, aliye duni, dhaifu, mwenye upungufu, muhitaji nk. Naam kwa maana ya mafundisho ya kiroho, Mnyonge ni yule mwenye kuhitaji msaada wa Mungu siku zote za Maisha yake kwa kuwa yeye pekee hawezi jambo lolote bila Bwana. Mungu yupo tayari kumsaidia kila anayehitaji msaada wake.

Biblia inaposeama mtu aliye mnyonge maana mwenye kuhitaji msaada/huruma toka kwa Mungu. Usijaribu kufikiri mtu anaweza kufanya jambo lolote bila Bwana, jifunze kuishi maisha ambayo Bwana mwenyewe ataona na kujua kwamba mwanangu huyu ametambua kwamba mimi ndiyo nguzo yake, naam bila mimi yeye hawezi jambo lolote. Hivyo katika maisha yako yote jifunze kutafuta msada wa Mungu kwa kila jambo ulifanyalo ndivyo utakavyofanikiwa.

 • Mwenye roho iliyo pondeka

Huyu ni mtu mwenye toba au roho ya toba, naam aliye mwepesi kutubu mbele za Mungu pale anapokosea. Zaburi ya 51, ni mfano sahihi wa mtu mwenye roho ya toba. Hii ni Zaburi aliyoimba na kuomba mfalme Daudi mbele za Mungu kama toba kwa sababu ya dhambi aliyotenda kwa kulala na Bathsheba mke wa Uria na kisha kumuua Uria. Mungu aliangalia toba ya Daudi na kujua kwamba ni toba ya kumaanisha na kisha akamsamehe, maana roho yake ilidhihirisha kupondeka, hebu tusome mistari kadhaa.

V1 – Ee Mungu unirehemu sawasawa na fadhili zako, kiasi cha wingi wa rehema zako uyafute makosa yangu

V3 – Maana nimejua mimi makosa yangu, Na dhambi yangu i mbele yangu daima

V10 – Ee Mungu uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu

V11 – Usinitenge na uso wako, wala roho yako Mtakatifu usiniondolee

V17 – Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika na kupondeka, Ee Mungu hutaudharau.

Biblia imeweka wazi kwamba afichaye dhambi zake hatafanikiwa, Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema (Mithali 28:12). Angalia maisha unayoishi sasa, je ndani yako unajisikia uhuru wa kumtumikia Mungu, au unahukumiwa lakini wewe unajitia tu moyo kwa sababu ya uongozi, huduma heshima au ukaribu ulionao na watumishi wa Mungu kanisani nk. Mpendwa dawa ya dhambi si kuficha bali ni kutubu.

Ushuhuda;

Nikiwa mkoa fulani, Mungu alinisemesha kuhusu dada mmoja Mwimbaji wa nyimbo za Injili ambaye alikuwa ametengwa kanisani kwao kwa sababu ya dhambi ya uasherati. Dada huyo alipoulizwa na uongozi husika kama ametenda dhambi,   alikana kuhusika na dhambi hiyo na kudai anaonewa. Vikao vingi vilifanyika ili kumuhoji aseme ukweli lakini yeye alisema ukweli ni kwamba sijaanguka dhambini bali nasingiziwa tu.

Siku moja jioni dada huyo alinitumia sms akisema mtumishi jaribu la kutengwa limekuwa zito natamani hata kujiua. Baada ya kupata sms hiyo niliitafakari sana kimaandiko na kujua kwamba, lazima huyu dada kuna kitu ameficha kwa sababu kama kweli hakutenda dhambi roho ya kujiua ingetoka wapi? roho hiyo ilimjia kwa sababu ametenda dhambi na imeandikwa wazi kwamba mshahara wa dhambi ni mauti.

Usiku nikamuomba Mungu anijulishe ukweli juu ya hali ya yule dada, ndipo nikasikia sauti ikisema ‘afichaye dhambi zake hatafanikiwa’. Nikaelewa kwamba yule dada kuna dhambi amefanya na yeye ameficha. Ndipo nikamuita na kisha kumuelezea picha yote na baadaye akakiri kwamba kweli alianguka dhambini  na hakutaka watu wajue kwa sababu ingemuondolea heshima aliyonayo. Nikamsaidia kiriho na sasa anaendelea vema katika Bwana.

Fundisho tunalotaka ujue katika ushuhuda huu ni; kwa ile miezi karibu mitano ambayo yule dada alikuwa ametengwa, maisha yake yalikuwa kama ya mtumwa, kila alichojaribu kufanya hakikuweza kufanikiwa, maisha yake yalijaa huzuni muda wote, akamuona Mungu kuwa dhalimu, kumbe yeye ndiye alikuwa dhalimu. Naam usifiche dhambi, bali tubu, Mungu yuko tayari kukusamehe usjijaribu kujitia moyo tokana na heshima au kibali ulichonacho kwa watu, mbele za Bwana ni machukizo  makubwa, kuficha dhambi halafu ukaendelea kutumika. Naam tubu kabla roho ya kutokufanikiwa haijakuvamia na laana zake.

 • Atetemekaye asikiapo neno langu

Huyu ni mtu mwenye kulipokea neno la Mungu kwa hofu na si mazoea. Mungu anataka watu wake wasilizoee neno lake, bali iwepo tofauti kati ya neno lake na kauli za watu wengine, watu wasilipokee neno lake kama vile taarifa ya habari za kila siku. Jifunze kutoka kwa wandugu wa Beroya, ambao walikaa chini na kuchunguza kile walichokisikia na kisha kukiweka kwenye Matendo                (Matendo 17:10-12). kwenye ule mstari wa 11 Biblia inasema ‘Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo’. Je nini matokeo ya jambo hili? Ule mstari wa 13 unasema ‘Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini, na wanawake wa kiyunani wenye cheo na wanaume si wachache’.

Maandiko haya yanatusaidia kujua kwamba mtu atetemekaye asikiapo neno la Mungu ni yule ambaye anapolisikia neno la Mungu moja halipuuzii, pili analipokeea kwa uelekevu wa moyo, tatu analichunguza(kwa kutafakari) na kisha anachukua hatua ya kuliweka kwenye matendo. Naam fanya hivyo nawe utaishi.

Ni imani yetu kwamba ukiyaweka mambo haya matatu kwenye matendo basi utavuta uwepo wa Mungu kwenye maisha yako siku zote.

Mungu akubariki

MAMBO YA KUKUSAIDIA UNAPOWEKA MALENGO YA MWAKA 2011

December 24, 2010

Na: Patrick Sanga

Heri ya Christmas!

Katika kuumalizia mwaka huu wa 2010 nataka nikutafakarishe kwa kukuuliza swali hili, je malengo yako uliyojiwekea katika mwaka 2010 katika nyanja mbalimbali kama vile kiroho, kihuduma, kifamilia, kikazi, kibiashara, kiuchumi nk yamefanikiwa kwa kiwango gani? Na kama hujafanikiwa je umejiuliza kwa nini hujafanikiwa kwa kiwango ambacho unaamini ulitakiwa kufanikiwa? Je, umegundua nini ni vikwazo vya wewe kufikia malengo yako?

Kama ukiyatafakari maswali hayo hapo juu utagundua kwamba najaribu kutaka kujua kama kwanza huwa una tabia ya kuwa na malenngo, na kisha kuweka mikakati inayotekelezeka ili kufikia hayo malengo, na mwisho kufanya tathimini   mara kwa mara ili kupima malengo yako yanafanikiwa kwa kiwango gani kadri siku zinavyozidi kwenda.

Naam najua si watu wengi sana wenye tabia ya kujiwekea malengo na hasa wapendwa. Ukiwauliza kwa nini huna malengo? atakuambia naenda kwa imani. Ukimuuliza imani maana yake nini? Atakujibu, kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo tena bayana ya yale yasiyoonekana (Waebrania 11:1).

Tatizo la wapendwa wengi ni kutokujua uhusiano uliopo kati ya imani na mtu mwenye malengo. Kulingana na tafsiri ya imani ni dhahiri kwamba, kuwa na malengo ni namna mojawapo ya kuwa na imani, kwani ili imani iwepo ni lazima kuwe na matarajio. Hivyo unapoweka malengo maana yake unaifanya imani yako kuwa na uelekeo, kwa kujua mahali unapotaka kufika.

Kuna tafsiri nyingi za malengo na hasa kwa kutegemeana na kile unachotaka kukipata au kukifikia, lakini tafsiri rahisi zaidi ni hii. Malengo ni hatua fulani katika maisha ya mtu ambayo hajaifikia na hivyo anataka kuifikia. Na jambo la msingi, unapaswa kufafanua vizuri lengo husika ambalo unataka kulifikia. Ufafanuzi mzuri wa lengo au malengo yako utakusaidia katika kujiwekea mikakati mizuri yenye kutekelezeka.  

Katika ujumbe huu mfupi wa  funga mwaka ya 2010 nataka tu kukumbusha mambo kadhaa ya msingi yatakayokusaidia unapoanza kuweka  malengo ya mwaka 2011.

Jambo la kwanza; Weka malengo yako mapema, kwa kuzingatia vipaumbele vyako.

Ni vema ukaweka malengo ya mwaka unaofuata kabla mwaka huo haujaingia. Mfano, kama mpaka sasa bado hujaweka malengo unayotaka kuyafikia katika mwaka 2011 basi tumia muda huu uliobaki kufanya kazi hiyo. Kwa nini nasema jambo hili, hii ni kwa sababu utekelezaji wa malengo yako unapaswa kuanza tarehe 01.01.2011 kama tukifika kwa neema yake Kristo.

Kwa hiyo kama tarehe hiyo ikifika hujapanga malengo yako jua kwamba tayari umeanza vibaya na kuna uwezekeano mkubwa wa kutokufikia malengo yako. Ikiwa ulishaweka malengo kwa kipindi cha mika mtatu, mtano au zaidi, bado pia unalazimika, kuyafafanua vizuri hayo malengo yako kwa kuzingatia mazingira yaliyopo na rasilimali utakazohitaji. Naam unapoweka malengo kumbuka kuyawekea  muda wa hilo lengo kufikiwa.

Mfano;

Moja ya malengo yangu kila mwaka kihuduma, ni kuandaa masomo yasiyopungua hamsini(50) na kuyaweka kwenye blog. Ukichukua 50 ukagawanya kwa miezi kumi na mbili unapata wastani wa masomo manne kila mwezi. Na hii ina maana kila wiki ni lazima niandae somo moja. Kwa hiyo ikipita wiki sijaandaa somo, ni dhahiri kwamba nitakwama katika kufikia malengo yangu. Nimekupa mfano huu rahisi ili uone umuhimu wa kuweka malengo mapema tena kwa kuyafunga kwenye muda.

Kwa uzoefu wangu katika kuweka malengo kikazi,kihuduma,kiuchumi, kifamilia, nk, nimejifunza na kugundua kwamba malengo ni muda, malengo ni mikakati na kisha malengo ni nidhamu uliyonayo katika kutekeleza mikakati na hasa ile inayohusu fedha. Muda ni ufunguo mkubwa wa kukusaidia kufikia malengo yako. Ukicheza na muda, huwezi kufikia malengo yako. Na kwa sababu hii ni lazima ujifunze kufikiri kimuda na kim-kakati kwa kila lengo unaloliweka.  

Naam kufanikiwa kwa malengo ya Mtu binafsi, Shirika, Serikali nk kutategemea namna mtu/watendaji wa Serikali au Shirika husika wanavyotumia muda walionao, mikakati iliyopo na mwisho nidhamu yao katika utendaji wao.  Naam, mambo haya matatu yakizingatiwa yatafanyika funguo za kufikia malengo yako au ya Shirika lako.  

 Jambo la pili: Weka mikakati ya kutekeleza malengo yako 

Ili malengo yako yaweze kutekelezeka, sharti uwe na mikakati inayotekelezeka, vinginevyo huwezi kuyafikia malengo yako. Mikakati ni mbinu, njia utakazotumia katika kutekeleza malengo yako. Naam kwa kuwa malengo yako yanakuwa ndani ya muda fulani ni lazima na mikakati nayo iwe kimuda. Katika kuweka mikakati, kuna baadhi ya malengo yatakutaka ushirikiane na baadhi ya watu, sasa kuwa makini na nani unashirikana naye katika kuyafikia malengo yako.

Jambo la tatu: Fanya tathmini ya utekelezaji wako wa malengo

Watu wengi sana, huwa wanasahau sana hiki kipengele katika utekelezaji wa malengo yao, na ndio maana si wengi wanaofikia malengo yao. Tathmini unaweza ukafanya kwa vipindi viwili au vitatu kwa mwaka. Maana yangu ni kwamba unaweza uka-ugawa mwaka mara mbili na hivyo kuamua kwamba utakuwa ukifanya tathmini zako mwezi wa sita na kumi na mbili. Naam huu ndio mfumo ambao mimi binafsi huutumia. Hata hivyo kuna baadhi ya malengo huwa nayafanyia tathmini yake kila mwezi, ingawa tathmini kubwa huwa nafanya Juni na Desemba. Katika kufanya tahmini jambo kubwa ni kuangalia mikakati yako imekusaidia kwa kiwango gani kufikia malengo yako.   

Jambo la nne: Boresha malengo kadri muda unavyokwenda, kwa kuzingatia tathmini unayoifanya.

Kama katika tathmini unayofanya mara kwa mara umegundua kwamba kuna lengo au malengo haya tekelezeki, basi kwanza litazame hilo lengo tena vizuri, kisha mikakati yake. Lazima kama siyo lengo, basi mikakati unayotumia haijakaa vizuri, na kwa hiyo unaweza kuliboresha lengo lako vizuri na hvyo mikakati yake pia. Mimi hutumia tathmini ya mwezi wa sita kurekebisha baadhi ya malengo na kisha kuboresha mikakati yake. Na kisha baada ya tathmini kubwa ya Desemba ndipo pamoja na mke wangu tunaweka malengo yetu ya mwaka unaofuta. Jambo la msingi hapa ni kuhakikisha kwamba malengo tunayoweka kila mwaka yanalenga kutufikisha kwenye malengo yetu ya miaka mitano mbele, tuliyokwisha kuyaweka tangu mwanzo.

Jambo la tano: Jenga mazoea ya kuyasoma na kutafakari malengo yako mara kwa mara.

Jambo hili litakuwekea msukumo wa kuhakikisha unatekeleza mikakati yako ili kuyafikia malengo yako. Mfano unaweza kuweka malengo yako kwenye Laptop/Computer yako,  unaweza ukaweka malengo yako kwenye meza yako ya kusomea au unaweza ukaweka ‘Remainder” kwenye simu yako iwe inakukumbusha kila wiki kupitia malengo yako nk. Hata hivyo ni vema ukaweka, malengo/mikakati yako, mahali ambapo ni salama kwa maana ambayo haitakuwa rahisi kwa mtu au watu wengine kuona, Shetani asije akawatumia hao katika kukwamisha malengo yako.

Kutokana somo hili, hebu angalia katika mwaka wa 2010 kama uliweka malengo, umeyafikia kwa kiwango gani? Naam kama haujafanikiwa vizuri, basi naamni somo hili litakusaidia katika kujipanga kwa mwaka 2011 ili kama kwa neema ya Mungu tukifika Desemba 2011 unapofanya tathmini ya mwisho wa mwaka uwe na sababu ya kumshukuru Mungu kwa namna alivyokusaidia kuyafikia malengo yako.

Mungu akubariki, mimi na familia yangu, tunakutakia heri ya ‘Christmas’ na Mwaka mpya wa 2011.

Neema ya Kristo na iwe nawe daima.

NAMNA YA KUMTUMIA ROHO MTAKATIFU KAMA MSAIDIZI KUPITIA KAZI ZAKE

December 20, 2010

Na:Patrick Sanga

Yohana 14:16-18 … Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni, wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu”.

Katika somo hili nataka kuandika juu ya kazi za Roho Mtakatifu na kukuonyesha namna unavyoweza kumtumia Roho Mtakataifu kama Msaidizi kupitia kazi zake. Labda niseme kwa lugha hii, kama unataka kuona msaada wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yako, ni lazima kwanza uzijue kazi zake, maana kazi zake ndizo zinazotuonyuesha maeneo ya msaada wake, kazi zake ndizo zinazofafanua kwa namna gani Roho Mtakatifu ni Msaidizi.

Roho Mtakatifu ni nani?

Roho Mtakatifu ni Mungu, mwenye nguvu zote, maarifa yote, anayepatikana kila mahali. Yeye anayo nafsi na ameamua kuishi ndani ya mwili wa mwanadamu. Kusudi kubwa la ujio wake ni kuwa Msaidizi wa mwanadamu kwenye ulimwengu huu wa mwili, ili kumsaidia kuishi katika mapenzi ya Mungu.

Roho Mtakatifu amemamua kuishi ndani ya mwili wa mtu kwa sababu, Mungu hana namna ya  kutawala kwenye ulimwengu wa kimwili bila kuwa na mwili wa damu na nyama, kwa kuwa yeye ni Roho (Yohana 4:24). Hivyo hana budi kuingia kwenye mwili wa mtu na kufanya makao yake hapo, ili kutawala na kumuongoza mwanadamu katika mapenzi yake. (Yohana 14:23, Yohana 14:18, Ufunuo 3:20, 1Wakorinto 3:16-17, 6:19).

Kinachotusaidia kujua kwamba Roho Mtakatifu ana nafsi, ni tabia zake, maana kwenye kila nafsi kuna hisia, nia, kumbukumbu, akili nk. Baadhi ya sifa na tabia za Roho Mtakatifu ni; anapatikana kila mahali (Omnipresence), Zaburi 139:7, ana maarifa/anajua yote (Omniscient, Intelligence), 1 Wakorinto 2:10-11, ni mwenye nguvu zote/wa umilele (Omnipotent), Mwanzo 1:2, ni Mtakatifu, Luka 11:13, ana hisia (Waefeso 4:30, Mwanzo 6:3) – Wala msimuhuzunishe Roho wa Mungu…, Roho yangu haitashindana na Mwanadamu milele, ana nia (will), 1Wakorinto 12:11 – Hutenda kazi kama apendavyo.

 Kazi za Roho Mtakatifu

 • Kufundisha, Mwalimu (Yohana 14:26) … Atawafundisha yote…
 • Kuongoza, Kiongozi (Warumi 8:14, Yohana 16:13) – Atawaongoza awatie kwenye kweli yote, wote wanaoongozwa na Roho hao ndio … Mfano (Matendo ya Mitume 13:4, Acts 8:29)
 • Ni mfunuaji wa mambo/mafumbo/siri za Mungu (1Wakorinto 2:10) – Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote. Usipoteze muda kumtaka Mungu akufunulie siri zake, wewe mwambi Roho Mtakatifu hiyo ndiyo kazi yake.
 • Muombezi (Warumi 8:26) – Roho hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.
 • Mtoa/mpasha habari za mambo yajayo (Yohana 16:13f) – Na mambo yajayo atawapasha habari yake.
 • Ni msemaji wa mambo ya Mungu/Yesu (Yohana 15:26, 2 Petro 1:21) – Yeye atanishuhudia (he will speak about me), Wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.
 • Ni mtetezi/msemaji wa mambo yetu (Marko 13:11) – Kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu.
 • Ni mkumbushaji wa yale uliyojifunza au uliyoagizwa na Mungu (Yohana 14:26)… Atawakumbusha yote niliyowaambia.
 • Kutia/kuwapa nguvu watu wake nguvu/uwezo (Matendo1:8) – Lakini mtapokea nguvu akisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu…
 • Kuuhakikisha (convict, make aware, sadikisha) ulimwengu kwa habari ya dhambi, haki na hukumu (Yohana 16:8) e.g unajuaje kwamba kuna hukumu? Warumi 8:16

Naam kazi hizi za Roho Mtakatifu zinatufikisha mahali pa kujua kwamba jukumu lake kubwa ni kuwa Msaidizi wa mwanadamu. Kufanyika msaada wa mwanadamu katika mambo hayo hapo juu pale mwanadamu atakapohitaji msaada huo.  Hivyo ni jukumu lako kumpa nafasi kwa kuboresha mahusiano yako na yeye ili akusaidie. Hata hivyo Roho Mtakatifu kuitwa Msaidizi haina maana kwamba ndio umvunjie heshima, bali fahamu kwamba, Roho Mtakatifu ni Msaidizi kwa namna ambayo bila yeye mimi na wewe hatuwezi kutenda neno lolote.

Kazi hizi zinatupa kujua kwamba Roho Mtakatifu yupo tayari kutusaidia katika kila eneo la maisha yetu. Ni jukumu letu kumpa  nafasi hiyo na kutambua kwamba bila msaada wake sisi hatuwezi lolote. Watu wengi leo hawaoni msaada wa Mungu kwao kwa sababu ya kutokumpa Roho Mtakatifu nafasi ya kuwasaidia katika maisha yao na pia kwa kutokujua maeneo ya kumtumia Roho Mtakatifu kama Msaidizi.

Je, unahitaji msaada wa Roho Mtakatifu eneo gani la maisha yako?, ni ndoa, kazi, madeni, huduma, kanisa, utawala nk mpe nafasi akusaidie, akufundishe na kukuongoza katika kweli yote. Kumbuka yeye ni Mungu ambaye ni Mwalimu na Kiongozi pasina yeye mimi na wewe hatuwezi neno lolote. Unataka kumjua Mungu, kuwa na maombi yenye matokeo mazuri na kufanikiwa katika maisha yako kiroho na kimwili pia mwambie Roho Mtakatifu akusaidie.

Msaada wa Roho Mtakatifu hauna mipaka maadam unahitaji msaada katika yale ambayo ni mapenzi ya Mungu. Hivyo haijalishi unapita katika jambo gani mpe nafasi Roho Mtakatifu akusaidie. Na ili uweze kuthamini msaada wa Roho Mtakatifu jifunze siku zote kufikiri kwa dhana kwamba bila msaada wake wewe huwezi lolote, na kwa sababu hiyo utaona umuhimu wa yeye kukusaidia katika maisha yako.

Usisubiri mambo yako yaharibike au usiachague mambo unayofikiri magumu ndio umshirikishe akusaidie, yeye anataka kuwa Bwana wa maisha yako, akusaidie kwa kila kitu hata mambo madogo kabisa kwenye maisha yako. Kina-muumiza Mungu kuona watoto wake chini ya jua wanahangaika katika maisha yao, wakati yeye amemleta Roho Mtakatifu ili awasaidie katika maisha hayo. Tumia vizuri fursa ya Roho Mtakatifu sasa maadam anapatikana, kuna wakati hatapatikana.

 Neema ya Kristo iwe nawe