UMEJIANDAAJE KWA TUKIO LA UNYAKUO? (Part 3)

MAENEO YA MSINGI KATIKA KUJIANDAA

Patrick & Flora Sanga

Katika sehemu hii ya tatu tutaanza kuangalia namna ya kujiandaa kwa tukio hili la unyakuo. Labda niseme suala la maandalizi ni pana sana maana kile ambacho kinaweza kukuzuia wewe usinyakuliwe kwa mwingine kinaweza kuwa sio tatizo. Ushauri wangu ni huu katika kila eneo la maandalizi ambayo nitaanza kuandika kuanzia sehemu hii ya tatu basi angalia wewe katika eneo hilo umekaaje. Katika baadhi ya maeneo ambayo nimefundisha somo hili Bwana amekuwa akinipa vitu tofauti kati ya kanisa/kundi moja na jingine, lakini yote yakilenga kuwaandaa watu wa Mungu pamoja nami tayari kwa siku ya unyakuo.

Watu wengi sana wanafikiri kwamba maadam kila wiki wao wanenda kanisani, kuwa karibu na wachungaji, manabii, mitume na zaidi kwamba wameokoka, basi hiyo ndiyo tiketi ya wao kunyakuliwa siku Bwana atakapokuja kuchukua watu wake. Naam si kweli hata kidogo, watakaonyakuliwa ni watu waliojiandaa kwa tukio hilo la ajabu. Shetani naye kwa kiwango kikubwa amefanikiwa kupumbaza watu katika hili ili wasiwe macho kukesha na kuyatunza mavazi yao hata Bwana ajapo, bali waendelee katika uchafu na dhambi hali wakidhani Bwana akija, wataenda naye.

Jambo la namna hili lilijitokeza kwa Wakristo wa kanisa la Korinto, na Paulo hali akijua tokana na mwenendo wao hawawezi kumlaki Bwana akaandika kuwaambia “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala walevi, wala watamanio, wala watukanaji, wala wanyang’anyi” (1 Wakorinto 6:9).

Sentensi hizi za Paulo kwa Wakorinto zinaonyesha baadhi yao walidhani wanaweza wakaendelea na tabia zao za kale halafu bado wakaurithi ufalme wa mbinguni. Kwa hiyo ikamlazimu Paulo kuanza kuwatajia baadhi ya sifa na vigezo vya mtu kuingia mbinguni.

Yesu mwenyewe katika kusisitiza jambo hili anasema “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21), pia katika Ufunuo 21:27 anasema “Na ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha mwana kondoo”.

 Lengo la kukuonyesha maandiko haya kadhaa ni ili kukudhihirishia kwamba watakaonyakuliwa ni watu ambao wamejiandaa kwa tukio hili kwa maana ya kuishi maisha yao katika mapenzi ya Mungu wawapo hapa duniani. Suala la kujiandaa siyo la siku moja bali ni hatua na jambo la kila siku, na ndiyo maana Mungu ameweka msisitzo kwa watumishi wengi juu ya  jambo hili, ili uweze kujifunza na kujiandaa tayari kwa tukio la unyakuo. Fuatana nami sasa ninapoanza kuelezea maeneo ya kuyafanyia kazi katika kujianda kwa tukio la unyakuo;

 Eneo la kwanzaKuwa makini na namna unavyotumia muda

Waefeso 5:15-17 “Basi angalieni sana, jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima, bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana’.

Naam, ili kupanua uelewa wetu katika jambo hili tusome pia kitabu cha Warumi 8:28 ‘Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake’.

Kila mwanadamu ambaye Mungu amemleta chini ya jua amekuja kwa kusudi maalumu la Ki-Mungu, kusudi hilo ndio sababu ya Mungu kumleta huyo mtu chini ya jua. Kwa hiyo maadam umezaliwa chini ya jua ipo sababu ya Mungu kukuleta wewe duniani, na ni mapenzi ya Mungu wewe uishi kwa kulitumikia kusudi lake katika siku zako.

Jambo hili tunaliona kwa Mfalme Daudi, maandiko yanaposema ‘Kwa maana Daudi akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu’ (Matendo 13:36). Ukisoma mstari huu katika tafsiri ya kiingereza toleo la GNB Biblia inasema “For David served God’s purposes in his own time, and then he died, was buried with his ancestors, and his body rotted in the grave”.

Kutoka kwenye mstari huu tunagundua kwamba kumbe mwanadamu anapaswa kulitumikia kusudi la Mungu katika siku za maisha yake chini ya jua. Naam kila mmoja ana jambo la ki-Mungu analopaswa kulitekeleza na halifanani na la mwingine. Ni jukumu lako kujua Mungu amekuleta duniani kufanya nini, ili usihi ukilitumikia kusudi la Mungu.

Vita kubwa iliyopo katika ulimwengu wa roho, ni kuwafanya watu wasimjue Mungu na hivyo kushindwa kujua kwa nini wao walikuja duniani na hivyo kujikuta wanaishi maisha ambayo si ya kwao wakiacha kile ambacho Mungu aliwaiitia. Upande wa pili ni kuwafanya wale ambao tayari wanajua kwa nini wamezaliwa wakose muda wa kulitumikia kusudi la Bwana kwenye maisha yao.

Na katika kuhakikisha jambo hili linafanikiwa Shetani huwa analeta ratiba nyingi kwenye maisha ya mtu ili kuahikisha mtu anakosa muda wa kufanya lile ambalo amepewa na Bwana kulifanya katika siku zake. Siku zote vita hii inalenga kuharibu kusudi la Mungu ndani ya mtu lisifanikiwe.

Na katika kulifanikisha kusudi la Mungu la aina yoyote ile liwe la kiroho, kikazi, kiuchumi, kibishara nk ni lazima mtu wa Mungu awe na muda wa kuomba na kusoma/kulitafakari neno la Mungu. Nje ya mambo haya mawili huwezi kufanikiwa kulitumikia kusudi la Mungu katika kizazi chako. Ndani ya mambo haya mawili ndipo mtu anapoweza kupata mwongozo wa namna ya kulitumikia kusudi la Mungu katika maisha yake.

Tukuulize swali, katika masaa 24 uliyonayo kwa siku moja, ni masaa mangapi unayatumia kuomba pamoja na kusoma neno la Mungu? Kuomba na kusoma neno sio kulitumikia kusudi la Mungu bali ni nyenzo za msingi katika kukusaidia kulitumikia kusudi la Mungu. Maana yetu ni hii kama umefeli kwenye haya maeneo mawili uwe na uhakika hautakuwa na ufanisi mzuri katika wajibu wako wa kulitumikia kusudi la Mungu.

Naam ndani ya maombi na neno la Mungu utapata hekima ya kukusaidia kujua namna ya kutumia muda wako vizuri bila kuathiri kazi yako kama umeajiriwa au umejiajiri nk.

Tukuulize swali jingine, hata kama unaomba na kusoma neno je unautumia muda wako vizuri katika kutekeleza kusudi la Mungu. Si watu wengi wako makini katika kulinda na kutunza muda wa kusudi la Mungu. Huko nyuma nilishaandika juu ya muda na kusema kwamba muda na Mungu ni marafiki, ukiharibu mahusiano yako na muda kwa kuutumia vibaya ni dhahiri kwamba utakuwa umeharibu hata mahusiano yako na Mungu kwa sababu kwa Mungu muda una kipaumbele cha kwanza kuliko mtu na kwa sababu hii muda ni wa muhimu sana kwa Mungu.

Ukweli huu tunaupata kwa kusoma katika Matendo ya Mitume 17:26 Biblia inasema ‘Naye alifanaya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao”. Ulisoma pia Waefeso 1:11 inasema “na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri lamapenzi yake’.

Tunaamini umeliona lile neno akisha kuwawekea nyakati, hii ina maana alitangulia kuziweka nyakati kwanza ndipo akawaleta watu. Na sasa kwa kuzingatia kile ambacho Mungu amesema katika Muhubiri 3:1-9 naam Biblia inasema “Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu”, hii ina maana Mungu aliweka kusudi ndani ya nyakati ambazo alizifanya kwanza na ndipo akamleta mtu ili apate kulitumikia kusudi hilo.

Na kwa mujibu wa Waefeso hii ina maana kusudi ndilo lilitangulia na kisha mtu akafuata/akafanywa kwa ajili ya lile kusudi la Mungu. Naam, kabla ya kusudi muda ulitangulia ndipo kusudi likafuata, na hivyo kusudi lile limebanwa kwenye muda.  Hivyo, Mungu anapokupa kusudi sharti ulitekeleze kwa muda uliokusudiwa, kinyume chake utakuwa umekwamisha lengo la Mungu kukuleta duniani, usitegemee kumuona maana muda wake uliutumia kufanya/kutekeleza kusudi jingine ambalo si lake.

 Huenda sentensi hii itakuwa imekushangaza lakini neno hili Yesu aliwaonya wanafunzi wake kwa mfano akisema ‘Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu, mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya. Amini, nawaambieni atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini mtumwa Yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi, bwana wake mtumwa huyo atakuja saa asiyoidhani na siku asiyoijua, atamkata vipande viwili, na kumweke fungu lake pamoja na wanafiki; ndipo kutakuwapo kilio na kusaga meno” (Mathayo 24:45-51).

Katika huu mfano ‘kuwapa watu chakula kwa wakati wake’ umetolewa kama mfano wa kusudi la Mungu kwa huyu ndugu anayezungumziwa hapa. Na msisitizo upo kwenye kutoa chakula kwa wakati ule uliokubalika/amuriwa. Maandiko yanasema heri siku akirudi bwana wake amkute anafanya hivyo, si tu kutoa chakula, bali anakitoa kwa wakati wake. Lakini mtumwa Yule akisema bwana wake anakawia na akatumia ule wakati kufanya mambo mengine tofauti na kusudi la bwana wake, bwana huyo atarudi saa na siku asiyo ijua na kumwekea kwenye fungu la wanafiki.

 Hii ni picha kamili ya ujio wa Yesu kuchukua watoto wake, Yesu atakapokuja kuchukua kanisa lake moja ya vigezo vya msingi kwa mtu kunyakuliwa ni namna mtu alivyolitumikia kusudi la Mungu ndani ya muda ule mtu aliopewa.

 Hatujui mpaka sasa tunapoandika jambo hili wewe una umri gani, je unafikiri Mungu akipima kusudi lake na muda ulioishi kwa mizani yake anaona nini? umekuwa mtumwa mwema au mbaya. Kumbuka unaposhindwa kuutumia vizuri muda kwa kufanya kile ambacho ni cha Mungu basi umetoa fursa ya Shetani kukutumia kufanya cha kwake, kwa sababu katika ulimwengu wa roho hakuna muda unaopotea, kama mtu hajautumia muda upande wa ufalme wa Mungu basi ujue ameutumia muda huo upande wa ufalme wa giza.

 Je nani anafaidi matunda ya muda wako? Kumbuka kwa kila muda unaopita katika mikono yako kuna kitu kinazaliwa chenye kuweka alama ama kwenye ufalme wa Mungu au ule wa giza. Sikia kanisa muda uliopewa na Mungu siku moja utakushitaki kwa sababu hukuutumia vizuri. Moja ya mambo ya msingi ambayo tumethibitisha kwa Bwana ni kwamba siku zote Mungu anapomuita mtu wake ili alitumikie kusudi lake katika mambo ya kwanza ya msingi ambayo Mungu atamsisitiza mtu huyo ni kujifunza kuwa na nidhamu ya matumizi mazuri ya muda. Jambo la muda litaendelea kupiga kelele ndani yake siku zote maanda kusudi la Mungu limefungwa ndani ya muda.

 Ushuhuda;

Mwaka 2006 nikiwa Dar es Salaam, tulikuwa tunaomba na baadhi ya wanafunzi wenzangu juu ya huduma tuliyokuwa tunataka kwenda kufanya kwenye mkoa wa Lindi wakati wa Likizo. Nakumbuka ilikuwa muda wa saa moja za jioni, ghafla nikiwa nimefumbua macho mbele yangu mita kama mbili naliona kiganja cha mkono unaong’aa sana, na kwenye ule mkono kuna saa ya dhahabu na majira (mishale) ya ile saa yalikuwa yanakimbia/yanazunguka kwa spidi kubwa sana. Wakati naona jambo lile ndipo nikasikia sauti ikisema ‘lolote ninalowaagiza kulifanya lifanyeni kwa muda ulioamriwa, maana muda hamsubiri mtu, sharti mtu atumike sambamba na muda wa kusudi’. Kile kiganja kikapotea, ndipo nikawashirikisha jambo hili waombaji wenzangu, tukamshukuru Mungu wetu.

Na tangu siku hiyo suala la kutumika ndani ya muda wa kusudi halijatoka kwenye ufahamu wangu, gharama yake ni kubwa sana, kwani ili kuutumia muda sawasawa na mapenzi ya Mungu lazima ujifunze kukaa mkao wa kuruhusu mapenzi ya Mungu na si ya kwako juu ya muda wako yatimie. Uwe tayari kuruhusu uhuru wako utumiwe na Mungu na si unavyotaka. Uwe tayari kukosa kwenda kustarehe mahali siku za weekend, kutumia muda mrefu kuongea, kutazama TV, Internet, uwe tayari pia kukosa muda wa kuwa na marafiki zako, uwe tayari hata kutumia muda wa kuwa na familia yako kwa ajili ya Bwana nk. Kwa kifupi uwe tayari kuongozwa na Bwana kuhusu matumizi ya muda wako.

Sina maana hayo mambo mengine hayafai, maana ndani ya muda wa kusudi, Mungu ameweka pia muda wa kupumzika ambao unaweza kuutumia kwa mambo kama hayo, tatizo watu wengi wanaona muda huo hautoshi na hivyo wanaamua kutumia muda wote kufanya mambo yao. Naam, uamuzi ni wako lakini kumbuka kusudi liko ndani ya muda, na majira yake yanaenda haraka, siku moja utaulizwa muda wako uliutumia kufanikisha kusudi la nani na kwa kiwango gani, naam utalipwa sawasawa na matendo yako katika kuutumia muda, maana kila unachokifanya, kinafanyika ndani ya MUDA uliopewa.

Ni lazima ujifunze kuunganisha sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwezi na mwaka. Ukitaka kutumika ndani ya muda wa kusudi ni lazima ujifunze kufikiri kwa mtiririko huo hapo juu wa muda, sekunda zinatengeneza dakika, dakika zinatengeneza saa, saa zinatengeneza siku nk, jiulize wakati sekunde zinatengeneza dakika, na dakika zinatengeneza saa, na saa kutengeneza siku, wewe umetengeneza nini kwenye kusudi la Mungu katika maisha yako? Ni matarajiao ya Mungu kwamba kama dakika zinavyozunguka ili kutengeneza saa, na wewe tumia muda huo kutengeneza kitu katika ulimwengu wa roho. Kutokana na mzunguko wa majira, ilianza sekunde, kisha dakika, kisha saa, siku nk, kwa hiyo unaona namna kimoja kinavyozalisha jina jipya, naam ukitumika ndani ya muda kwa kila sekunde, dakika, saa nk utazalisha jambo jipya katika ulimwengu wa roho (asomaye na afahamu).

Naam, tungeweza kuandika mengi juu ya muda, jambo la msingi hakikisha unakuwa makini katika matumizi yako ya muda kwa kujua nini ni mapenzi ya Mungu kwa kila hatua unayopitia, na mbinu kubwa ya kukusaidia katika hili ni kuomba na kusoma ukilitafakari neno la Mungu.

 Mungu akubariki

Advertisements

10 comments

 1. KWAKWELI NAMSHUKURU MUNGU KWA UJUMBE WAKE. NAAMINI MUNGU WETU NI MUNGU WA ALTENATIVE, YAKWAMBA ANAWEZA KUSEMA NA MTU WAKE KWA NAMNA YA AJABU. MTUMISHI MUNGU AMESEMA NAMI JUU YA MUDA. NIKO KIPINDI KIGUMU LAKINI MUNGU ALICHONIAMBIA LEO NIKWAMBA NINIKWAMISHWA NA MUDA NA KUTO KUFANYA KUSUDI LA MUNGU KWA WAKATI ULIOAMLIWA. NA KUJIULIZA KILA DAKIKA INAYOPITA NIMEFANYA NINI AMBACHO NI KUSUDI LA MUNGU!

  MUNGU AKUBARIKI NA AKUPE TENA UJUMBE WAKE KWA WAKATI ULIOAMLIWA.

  NIMEOKOKA NA NAMPENDA SANA YESU KWAKUWA YEYE NI BWANA NA MWAKOZI WA MAISHA YANGU.

  AMINA

  Like

 2. Shalom mtumishi wa Mungu kwa kweli nashukuru sana kwa ujumbe wako wenye nguvu za Mungu ndani yaske ni dhairi kabisa Mungu siku zote anatupenda ndio maana huwa anatumia watumishi wake kwa jinsi ya tofauti sana kwa kusema na kanisa ushauri wangu kwa kanisa la leo ni kwamba tusipende kumzoelea Mungu mwenyezi na kuzoelea mambo ya kale yatatupeleka sahemu mbaya pasipo sisi kutambua maana ibilisi tutakua tumempa nafasi naye atatutia giza macho yetu na kuangukia pua jeanamu ya moto.
  Jaman kuzimu kunamateso na kunatisha jaman tujitaidi kumtafuta Mungu siku zote ili siku akirudi tuondoke pamoja nae na kuepuka azabu isio na mwisho Mungu wa Ibraim,Isaka na Yakobo awabariki na tuzidi kuwa na hofu na Mungu wetu.

  Like

 3. Mungu Akubariki Na Kukutumia Zaidi Hata Ya Hivi Mtumishi,imenigusa Sana,je!Kama Nilikuwa Sina Au Nimelegea Ktk Hayo Yote Ninaanzaje Kutengeneza Ktk Kuukomboa Wakati?Pia Je! Roho Anachokushuhudia Ndio Kusudi La Mungu Lenyewe Au?

  Like

 4. Bwana Akubariki Na Kukutumia Mno,imenigusa Sana.Lakini Naomba Ushauri Je! Kama Sijagawa Mda Kwa Kusudi La Mungu,nifanyaje?Alafu Je! Kusudi La Mungu Ndo Lile Jema Ambalo Roho Mtk Anakutuma Ufanye?

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s