Archive for November 2010

UMEJIANDAAJE KWA TUKIO LA UNYAKUO? (Part 3)

November 22, 2010

MAENEO YA MSINGI KATIKA KUJIANDAA

Patrick & Flora Sanga

Katika sehemu hii ya tatu tutaanza kuangalia namna ya kujiandaa kwa tukio hili la unyakuo. Labda niseme suala la maandalizi ni pana sana maana kile ambacho kinaweza kukuzuia wewe usinyakuliwe kwa mwingine kinaweza kuwa sio tatizo. Ushauri wangu ni huu katika kila eneo la maandalizi ambayo nitaanza kuandika kuanzia sehemu hii ya tatu basi angalia wewe katika eneo hilo umekaaje. Katika baadhi ya maeneo ambayo nimefundisha somo hili Bwana amekuwa akinipa vitu tofauti kati ya kanisa/kundi moja na jingine, lakini yote yakilenga kuwaandaa watu wa Mungu pamoja nami tayari kwa siku ya unyakuo.

Watu wengi sana wanafikiri kwamba maadam kila wiki wao wanenda kanisani, kuwa karibu na wachungaji, manabii, mitume na zaidi kwamba wameokoka, basi hiyo ndiyo tiketi ya wao kunyakuliwa siku Bwana atakapokuja kuchukua watu wake. Naam si kweli hata kidogo, watakaonyakuliwa ni watu waliojiandaa kwa tukio hilo la ajabu. Shetani naye kwa kiwango kikubwa amefanikiwa kupumbaza watu katika hili ili wasiwe macho kukesha na kuyatunza mavazi yao hata Bwana ajapo, bali waendelee katika uchafu na dhambi hali wakidhani Bwana akija, wataenda naye.

Jambo la namna hili lilijitokeza kwa Wakristo wa kanisa la Korinto, na Paulo hali akijua tokana na mwenendo wao hawawezi kumlaki Bwana akaandika kuwaambia “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala walevi, wala watamanio, wala watukanaji, wala wanyang’anyi” (1 Wakorinto 6:9).

Sentensi hizi za Paulo kwa Wakorinto zinaonyesha baadhi yao walidhani wanaweza wakaendelea na tabia zao za kale halafu bado wakaurithi ufalme wa mbinguni. Kwa hiyo ikamlazimu Paulo kuanza kuwatajia baadhi ya sifa na vigezo vya mtu kuingia mbinguni.

Yesu mwenyewe katika kusisitiza jambo hili anasema “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21), pia katika Ufunuo 21:27 anasema “Na ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha mwana kondoo”.

 Lengo la kukuonyesha maandiko haya kadhaa ni ili kukudhihirishia kwamba watakaonyakuliwa ni watu ambao wamejiandaa kwa tukio hili kwa maana ya kuishi maisha yao katika mapenzi ya Mungu wawapo hapa duniani. Suala la kujiandaa siyo la siku moja bali ni hatua na jambo la kila siku, na ndiyo maana Mungu ameweka msisitzo kwa watumishi wengi juu ya  jambo hili, ili uweze kujifunza na kujiandaa tayari kwa tukio la unyakuo. Fuatana nami sasa ninapoanza kuelezea maeneo ya kuyafanyia kazi katika kujianda kwa tukio la unyakuo;

 Eneo la kwanzaKuwa makini na namna unavyotumia muda

Waefeso 5:15-17 “Basi angalieni sana, jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima, bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana’.

Naam, ili kupanua uelewa wetu katika jambo hili tusome pia kitabu cha Warumi 8:28 ‘Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake’.

Kila mwanadamu ambaye Mungu amemleta chini ya jua amekuja kwa kusudi maalumu la Ki-Mungu, kusudi hilo ndio sababu ya Mungu kumleta huyo mtu chini ya jua. Kwa hiyo maadam umezaliwa chini ya jua ipo sababu ya Mungu kukuleta wewe duniani, na ni mapenzi ya Mungu wewe uishi kwa kulitumikia kusudi lake katika siku zako.

Jambo hili tunaliona kwa Mfalme Daudi, maandiko yanaposema ‘Kwa maana Daudi akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu’ (Matendo 13:36). Ukisoma mstari huu katika tafsiri ya kiingereza toleo la GNB Biblia inasema “For David served God’s purposes in his own time, and then he died, was buried with his ancestors, and his body rotted in the grave”.

Kutoka kwenye mstari huu tunagundua kwamba kumbe mwanadamu anapaswa kulitumikia kusudi la Mungu katika siku za maisha yake chini ya jua. Naam kila mmoja ana jambo la ki-Mungu analopaswa kulitekeleza na halifanani na la mwingine. Ni jukumu lako kujua Mungu amekuleta duniani kufanya nini, ili usihi ukilitumikia kusudi la Mungu.

Vita kubwa iliyopo katika ulimwengu wa roho, ni kuwafanya watu wasimjue Mungu na hivyo kushindwa kujua kwa nini wao walikuja duniani na hivyo kujikuta wanaishi maisha ambayo si ya kwao wakiacha kile ambacho Mungu aliwaiitia. Upande wa pili ni kuwafanya wale ambao tayari wanajua kwa nini wamezaliwa wakose muda wa kulitumikia kusudi la Bwana kwenye maisha yao.

Na katika kuhakikisha jambo hili linafanikiwa Shetani huwa analeta ratiba nyingi kwenye maisha ya mtu ili kuahikisha mtu anakosa muda wa kufanya lile ambalo amepewa na Bwana kulifanya katika siku zake. Siku zote vita hii inalenga kuharibu kusudi la Mungu ndani ya mtu lisifanikiwe.

Na katika kulifanikisha kusudi la Mungu la aina yoyote ile liwe la kiroho, kikazi, kiuchumi, kibishara nk ni lazima mtu wa Mungu awe na muda wa kuomba na kusoma/kulitafakari neno la Mungu. Nje ya mambo haya mawili huwezi kufanikiwa kulitumikia kusudi la Mungu katika kizazi chako. Ndani ya mambo haya mawili ndipo mtu anapoweza kupata mwongozo wa namna ya kulitumikia kusudi la Mungu katika maisha yake.

Tukuulize swali, katika masaa 24 uliyonayo kwa siku moja, ni masaa mangapi unayatumia kuomba pamoja na kusoma neno la Mungu? Kuomba na kusoma neno sio kulitumikia kusudi la Mungu bali ni nyenzo za msingi katika kukusaidia kulitumikia kusudi la Mungu. Maana yetu ni hii kama umefeli kwenye haya maeneo mawili uwe na uhakika hautakuwa na ufanisi mzuri katika wajibu wako wa kulitumikia kusudi la Mungu.

Naam ndani ya maombi na neno la Mungu utapata hekima ya kukusaidia kujua namna ya kutumia muda wako vizuri bila kuathiri kazi yako kama umeajiriwa au umejiajiri nk.

Tukuulize swali jingine, hata kama unaomba na kusoma neno je unautumia muda wako vizuri katika kutekeleza kusudi la Mungu. Si watu wengi wako makini katika kulinda na kutunza muda wa kusudi la Mungu. Huko nyuma nilishaandika juu ya muda na kusema kwamba muda na Mungu ni marafiki, ukiharibu mahusiano yako na muda kwa kuutumia vibaya ni dhahiri kwamba utakuwa umeharibu hata mahusiano yako na Mungu kwa sababu kwa Mungu muda una kipaumbele cha kwanza kuliko mtu na kwa sababu hii muda ni wa muhimu sana kwa Mungu.

Ukweli huu tunaupata kwa kusoma katika Matendo ya Mitume 17:26 Biblia inasema ‘Naye alifanaya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao”. Ulisoma pia Waefeso 1:11 inasema “na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri lamapenzi yake’.

Tunaamini umeliona lile neno akisha kuwawekea nyakati, hii ina maana alitangulia kuziweka nyakati kwanza ndipo akawaleta watu. Na sasa kwa kuzingatia kile ambacho Mungu amesema katika Muhubiri 3:1-9 naam Biblia inasema “Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu”, hii ina maana Mungu aliweka kusudi ndani ya nyakati ambazo alizifanya kwanza na ndipo akamleta mtu ili apate kulitumikia kusudi hilo.

Na kwa mujibu wa Waefeso hii ina maana kusudi ndilo lilitangulia na kisha mtu akafuata/akafanywa kwa ajili ya lile kusudi la Mungu. Naam, kabla ya kusudi muda ulitangulia ndipo kusudi likafuata, na hivyo kusudi lile limebanwa kwenye muda.  Hivyo, Mungu anapokupa kusudi sharti ulitekeleze kwa muda uliokusudiwa, kinyume chake utakuwa umekwamisha lengo la Mungu kukuleta duniani, usitegemee kumuona maana muda wake uliutumia kufanya/kutekeleza kusudi jingine ambalo si lake.

 Huenda sentensi hii itakuwa imekushangaza lakini neno hili Yesu aliwaonya wanafunzi wake kwa mfano akisema ‘Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu, mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya. Amini, nawaambieni atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini mtumwa Yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi, bwana wake mtumwa huyo atakuja saa asiyoidhani na siku asiyoijua, atamkata vipande viwili, na kumweke fungu lake pamoja na wanafiki; ndipo kutakuwapo kilio na kusaga meno” (Mathayo 24:45-51).

Katika huu mfano ‘kuwapa watu chakula kwa wakati wake’ umetolewa kama mfano wa kusudi la Mungu kwa huyu ndugu anayezungumziwa hapa. Na msisitizo upo kwenye kutoa chakula kwa wakati ule uliokubalika/amuriwa. Maandiko yanasema heri siku akirudi bwana wake amkute anafanya hivyo, si tu kutoa chakula, bali anakitoa kwa wakati wake. Lakini mtumwa Yule akisema bwana wake anakawia na akatumia ule wakati kufanya mambo mengine tofauti na kusudi la bwana wake, bwana huyo atarudi saa na siku asiyo ijua na kumwekea kwenye fungu la wanafiki.

 Hii ni picha kamili ya ujio wa Yesu kuchukua watoto wake, Yesu atakapokuja kuchukua kanisa lake moja ya vigezo vya msingi kwa mtu kunyakuliwa ni namna mtu alivyolitumikia kusudi la Mungu ndani ya muda ule mtu aliopewa.

 Hatujui mpaka sasa tunapoandika jambo hili wewe una umri gani, je unafikiri Mungu akipima kusudi lake na muda ulioishi kwa mizani yake anaona nini? umekuwa mtumwa mwema au mbaya. Kumbuka unaposhindwa kuutumia vizuri muda kwa kufanya kile ambacho ni cha Mungu basi umetoa fursa ya Shetani kukutumia kufanya cha kwake, kwa sababu katika ulimwengu wa roho hakuna muda unaopotea, kama mtu hajautumia muda upande wa ufalme wa Mungu basi ujue ameutumia muda huo upande wa ufalme wa giza.

 Je nani anafaidi matunda ya muda wako? Kumbuka kwa kila muda unaopita katika mikono yako kuna kitu kinazaliwa chenye kuweka alama ama kwenye ufalme wa Mungu au ule wa giza. Sikia kanisa muda uliopewa na Mungu siku moja utakushitaki kwa sababu hukuutumia vizuri. Moja ya mambo ya msingi ambayo tumethibitisha kwa Bwana ni kwamba siku zote Mungu anapomuita mtu wake ili alitumikie kusudi lake katika mambo ya kwanza ya msingi ambayo Mungu atamsisitiza mtu huyo ni kujifunza kuwa na nidhamu ya matumizi mazuri ya muda. Jambo la muda litaendelea kupiga kelele ndani yake siku zote maanda kusudi la Mungu limefungwa ndani ya muda.

 Ushuhuda;

Mwaka 2006 nikiwa Dar es Salaam, tulikuwa tunaomba na baadhi ya wanafunzi wenzangu juu ya huduma tuliyokuwa tunataka kwenda kufanya kwenye mkoa wa Lindi wakati wa Likizo. Nakumbuka ilikuwa muda wa saa moja za jioni, ghafla nikiwa nimefumbua macho mbele yangu mita kama mbili naliona kiganja cha mkono unaong’aa sana, na kwenye ule mkono kuna saa ya dhahabu na majira (mishale) ya ile saa yalikuwa yanakimbia/yanazunguka kwa spidi kubwa sana. Wakati naona jambo lile ndipo nikasikia sauti ikisema ‘lolote ninalowaagiza kulifanya lifanyeni kwa muda ulioamriwa, maana muda hamsubiri mtu, sharti mtu atumike sambamba na muda wa kusudi’. Kile kiganja kikapotea, ndipo nikawashirikisha jambo hili waombaji wenzangu, tukamshukuru Mungu wetu.

Na tangu siku hiyo suala la kutumika ndani ya muda wa kusudi halijatoka kwenye ufahamu wangu, gharama yake ni kubwa sana, kwani ili kuutumia muda sawasawa na mapenzi ya Mungu lazima ujifunze kukaa mkao wa kuruhusu mapenzi ya Mungu na si ya kwako juu ya muda wako yatimie. Uwe tayari kuruhusu uhuru wako utumiwe na Mungu na si unavyotaka. Uwe tayari kukosa kwenda kustarehe mahali siku za weekend, kutumia muda mrefu kuongea, kutazama TV, Internet, uwe tayari pia kukosa muda wa kuwa na marafiki zako, uwe tayari hata kutumia muda wa kuwa na familia yako kwa ajili ya Bwana nk. Kwa kifupi uwe tayari kuongozwa na Bwana kuhusu matumizi ya muda wako.

Sina maana hayo mambo mengine hayafai, maana ndani ya muda wa kusudi, Mungu ameweka pia muda wa kupumzika ambao unaweza kuutumia kwa mambo kama hayo, tatizo watu wengi wanaona muda huo hautoshi na hivyo wanaamua kutumia muda wote kufanya mambo yao. Naam, uamuzi ni wako lakini kumbuka kusudi liko ndani ya muda, na majira yake yanaenda haraka, siku moja utaulizwa muda wako uliutumia kufanikisha kusudi la nani na kwa kiwango gani, naam utalipwa sawasawa na matendo yako katika kuutumia muda, maana kila unachokifanya, kinafanyika ndani ya MUDA uliopewa.

Ni lazima ujifunze kuunganisha sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwezi na mwaka. Ukitaka kutumika ndani ya muda wa kusudi ni lazima ujifunze kufikiri kwa mtiririko huo hapo juu wa muda, sekunda zinatengeneza dakika, dakika zinatengeneza saa, saa zinatengeneza siku nk, jiulize wakati sekunde zinatengeneza dakika, na dakika zinatengeneza saa, na saa kutengeneza siku, wewe umetengeneza nini kwenye kusudi la Mungu katika maisha yako? Ni matarajiao ya Mungu kwamba kama dakika zinavyozunguka ili kutengeneza saa, na wewe tumia muda huo kutengeneza kitu katika ulimwengu wa roho. Kutokana na mzunguko wa majira, ilianza sekunde, kisha dakika, kisha saa, siku nk, kwa hiyo unaona namna kimoja kinavyozalisha jina jipya, naam ukitumika ndani ya muda kwa kila sekunde, dakika, saa nk utazalisha jambo jipya katika ulimwengu wa roho (asomaye na afahamu).

Naam, tungeweza kuandika mengi juu ya muda, jambo la msingi hakikisha unakuwa makini katika matumizi yako ya muda kwa kujua nini ni mapenzi ya Mungu kwa kila hatua unayopitia, na mbinu kubwa ya kukusaidia katika hili ni kuomba na kusoma ukilitafakari neno la Mungu.

 Mungu akubariki

MWANAMKE, SIMAMA KWENYE NAFASI YAKO ILI UWEZE KUIPONYA NDOA YAKO

November 1, 2010

Na: Patrick Sanga

Namshukuru Mungu ambaye anazidi kunipa neema ya kuandika na kuandika masomo mbalimbali na pia yale yanayohusu akina mama hasa wao kuwa kwenye nafasi zao.

Mnamo Novemba, 2009 mama mmoja alinitumia email akinieleza kwa jinsi ambavyo ndoa yake imekuwa ikimsumbua na kufika mahali pa yeye kujutia hata kwa nini alikubali kuolewa. Baada ya kupata ujumbe wake nilichukua hatua ya kufanya maombi kwa ajili ya huyu mama na wengine wenye shida kama yake kwenye ndoa zao. Katika kuomba, Mungu alinisemesha na kunifundisha kupitia Biblia mambo ya msingi ambayo sasa nimeona ni vema nikayaandaa kama somo na kuweka kwenye blog ili kila nafsi ya mwanamke yenye kuhitaji haya maarifa iweze kuyapata, maana imeandikwa katika Mithali 19:2 kwamba ‘si vema nafsi ya mtu ikakosa maarifa’.

Mambo manne yafuatayo kama ukiyaweka kwenye matendo nina uhakika yataleta mabadiliko/uponyaji na pia kujenga msingi imara wa ndoa yako. Mambo hayo ni kama ifuatavyo;

  • Sharti wanawake wasimame kwenye nafasi zao ndipo wataona uponyaji kwenye ndoa zao.

Hili lilikuwa jambo la kwanza Bwana kunijulisha, ili niwakumbushe tena akina mama. Nimeshaandika kuhusu nafasi za Mwanamke huko nyuma, kwa ufafanuzi zaidi bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2006/10/23/wanawake/. Kwa kifupi niseme uponyaji wa wa ndoa yako upo kwa wewe kuwa kwenye nafasi yako. Mungu hana namna ya kukusaidia kama hauko kwenye nafasi yako.

Ni lazima uzijue nafasi ambazo Mungu amekupa na kisha kusimama vema ukiwajibika kwenye hizo nafasi. Kinamama wengi leo wanalia sana Mungu aponye ndoa zao na matokeo yake yanakuwa tofauti na matarajio yao. Endapo kama na ndoa yako ipo kwenye eneo kama hili, angalia kama umekaa vizuri kwenye nafsi ambazo Mungu amkupa katika ulimwengu wa roho. Nina uhakika unaweza ukawa kuna maeneo ulijisahau hivyo tengeneza, maana uponyaji na uharibifu wa ndoa yako kimaandiko upo katika uwezo wako mama.

Ni maombi yangu kwamba Roho Mtakatifu akujulishe jambo hili, uponyaji wa ndoa yako haupo kwa Mungu, bali Mungu ameweka uwezo huo ndani yako. Ili uwezo huo uweze kufanya kazi sawasawa ni jukumu lako kuwa kwenye nafasi zako.  

  • Unahitaji hekima ya Mungu ili kujenga ndoa yako

Ukisoma kitabu cha Mithali 14:1 Biblia inasema “Kila mwanamke aliye na hekima huijenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe”. Biblia imeshaweka wazi kwamba wewe unaweza kuijenga au kuibomoa nyumba yako. Uwezo wa kufanya jambo hili unategemea kiwango cha hekima ya Mungu ambayo ipo ndani yako na juu yako pia. Hekima ya kuponya ndoa yako ambayo sasa unajua iko mashakani, ipo kwenye neno la Mungu na si kwa waganga wa kienyeji.

Unaipataje hekima ya Mungu?

Katika Mithali 8:1 Biblia inasema ‘Je! Hekima halii? Ufahamu hatoi sauti yake?’ mstari wa 10 unasema ‘Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi’. Ule mstari wa 14 unasema ‘Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu, mimi ni nguvu’. Na ule wa 16 unasema ‘Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia’.

Siku zote kama unataka hekima ya Mungu ya kukusaidia kwenye eneo lolote la maisha yako utaipata kwenye neno la Mungu au kwa Mungu.  Imeandikwa katika Mithali 12:1a “Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa’. Hekima ya Mungu kwa mtu ni matokeo ya kiwango cha neno la Mungu ambalo mtu ameliweka na kulitafakari kwa wingi moyoni mwake. Kwa hiyo kwa Watawala, hekima ya Mungu kwa Mtawala inategemea kiwango cha neno la Mungu kuhusu utawala ambalo Mtawala amekiweka ndani yake. Naam hekima ya Mungu kwa Mwanamke itategema kiwango cha neno la Mungu kuhusu nafasi zako ambacho umekiweka ndani yao nk.

Sharti neno la Mungu kuhusu nafasi zako, wajibu wako nk liwe kwa wingi ndani yako ndipo hekima ya Mungu ya  kujenga nyumba/ndoa/familia yako itakapokaa ndani yako na juu yako. Na kwa kuwa hekima ni ufahamu, maarifa, shauri na nguvu, itakusaidia katika kuijenga ndoa yako, kama inavyowasaidia watawala, waung’wana na waamuzi katika majukumu yao (Mithali 8:16). Naam hekima hiyo itaongoza kinywa chako kuleta uponyaji wa ndoa na nyumba yako, kama Biblia inavyosema katika Mithali 31:26 “Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake”.

Mithali 8:17 inasema ‘nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona’. Naam siku zote, hekima inawasiaidia wale wanaoitafuta na wakaipata’. Na njia kubwa ya kupata hekima hiyo ni kwa njia ya kusoma na kuatafakari neno la Mungu kila siku na kuomba kama nilivyokufundisha hapo juu.

  • Uwe makini kufuatilia maisha ya mume wako/watu wa nyumbani mwako

Mithali 31: 27 “Huangalaia sana njia za watu wa nyumbani mwake; wala hali chakula cha uvivu”. Tafsiri ya kiingereza ya BBE inasemaShe gives attention to the ways of her family; she does not take her food without working for it”. Moja ya nafasi za mwanamke ambayo nilishaandika huko nyuma ni kuwa mlinzi wa mwanaume, hii ikiwa ni pamoja na mume wake.

Naam jukumu la ulinzi ni kubwa sana ambalo Mwanamke umepewa, siku zote mlinzi ana wajibu wa kufuatilia kwa karibu sana maisha/nyendo za yule  anayemlinda. Kwa dhana ya ndoa yako, ni jukumu lako kama mlinzi kufuatilia maisha ya mume wako na kujua kama anaishi katika mapenzi ya Mungu. Naam ukijua anaishi nje ya mapenzi ya Mungu simama kwenye nafasi zako uendelee kuomba huku ukiamini Mungu atambadilisha na kumsaidia kuishi katika mapenzi yake.

Kuwa makini kufuatilia maisha na njia za mume wako, itakusaidia kujua hali yake, na hatari ambayo inataka kumpata, hivyo kama mumeo ameokoka au ni mcha Mungu utakuwa na jukumu la kumtahadharisha kwamba awe makini na baadhi ya vitu ambavyo umeona asipokuwa makini navyo ataanguka. Naam kama hajaokoka na ni mtu ambaye hamjui wala kumjali Mungu, usikate tamaa na isikufanye ukaondoka kwenye nafasi yako, dumu hapo ukijua kwamba Mungu ni mwaminifu atafanya kwa kuzingtia maagizo yako kama mlinzi.

  • Usisubiri hadi tatizo litokee ndipo uanze kutafuta msaada wa Mungu

 Jifunze kutumia wakati wa amani kuweka msingi mzuri wa ulinzi kwenye ndoa yako. Usisubiri wakati wa hatari ndipo ujipange kwa mapambano. Ki Mungu kila siku kwako ni siku ya kujenga au kuongeza ukuta wa ulinzi kwa nyumba yako.   Sehemu kubwa ya maombi ambayo akina mama wanapeleka kwa Mungu ni ili apate kuziponya ndoa zao kwa sababu zimeingia kwenye matatizo. Sijui kama unaona jambo hili, wengi wanaomba kwa sababu ndoa zao zipo kwenye shida. Naam Mungu anataka ujifunze kuomba ulinzi wa ndoa yako wakati ndoa yako ina amani, tumia vizuri wakati wa amani kujenga kuta za ulinzi kwa ndoa na nyumba yako kwa ujumla.

 Ni imani yangu kwamba ujumbe huu, umekuongezea kwa kiasi fulani maarifa ya kukusaidia katika kuijenga ndoa yako. Jambo la msingi kujua ni kwamba, Katika kubadilisha maisha ya mume wako na kuiponya ndoa yako, Mungu anaangalia kwanza kama umesiamama kwenye nafasi zako na unatekeleza wajibu wako.

 Neema ya Kristo iwe nawe

VITA VYA KIROHO (Part 4)

November 1, 2010

 

Na: Patrick Sanga

Waraka wa Septemba, 2010

SILAHA ZA USHINDI DHIDI YA SHETANI KATIKA VITA VYA KIROHO (Part 2)

 Katika sehemu ya tatu tuliishia kwa kuangalia silaha ya imani sasa fuatana nami tuendele…

  • Chapeo ya wokovu, Waefeso 6:17ª Biblia inasema ‘Tena ipokeeni chapeo ya wokovu

Ukisoma kamusi ya kiebrania na kigiriki neno ‘wokovu’ limetafsiriwa kama ulinzi au kinga. Wokovu unapatikana kwa njia ya kukiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na Mwokozi (Warumi 10:10). Wokovu huu ni kuokolewa kutoka kwenye nguvu ya dhambi, utawala wa Shetani na mapepo yake. Kwa hiyo kama hujaokoka fanya maamuzi ya kuokoka kwa kuwa wokovu ni ulinzi dhidi ya nguvu za giza na kazi zote za Shetani. Maana mara nyingi watu wasiookoka Shetani anawaonea na kuwatesa sana.

 Tafsiri pana zaidi tunayoipata katika silaha hii ya chapeo ya wokovu ni kuwa na matumizi mazuri ya kinywa chako. Watu wengi leo wameingia kwenye uonevu mkubwa wa Shetani kutokana na yale wanayokiri kwa vinywa vyao. Sasa ili uwe salama tumia vizuri kinywa chako kwa kukiri yale ambayo yapo sawasawa na neno la Mungu kwenye maisha yako. Kadri unavyokiri mabaya unayaumba kwenye maisha yako, unavyokiri sawasawa na neno la Mungu unaumba ulinzi/kinga ya ki-Mungu dhidi ya mabaya ya Shetani kwenye maisha yako.

  • Upanga wa roho yaani neno la Mungu, Waefeso 6:17b inasema “Na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu”                                            

Hosea 4:6, Mithali 8: 8-15,  Acts 17: 11

Katika Hosea 4:6a Biblia inasema ‘watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa…’ na Mithali 12:1a anasema ‘Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa’. Kukosa neno la Kristo kwa wingi ndani yako ni kujiweka kwenye mazingira ambayo ni rahisi kupigwa na adui katika vita vya kiroho. Neno la Mungu linapokaa kwa wingi ndani yako ni ulinzi dhidi ya majaribu na dhambi. Zaburi 119:11 ‘Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi’.

Na ndiyo maana kuna vita kubwa kweli inayozuia watu wasipende kuwa na muda wa kusoma neno la Mungu, maana Shetani anajua ili aendelee kuwaangamiza watu, dawa ni kuwazuia wasisome neno la Mungu, kwa kuwafanya wabakie kusoma na kutazama vitu visivyojenga roho zao.

Mungu pia alimwagiza Joshua kusema ‘Kitabu hiki cha Torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako’ (Joshua 1:8).

Paulo naye akiongozwa na Roho wa Yesu aliwaambia wandugu wa Kolosai akisema Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote … (Wakolosai 3:16). Neno la Mungu linaitwa Upanga wa Roho kwa kuwa Roho Mtakatifu na Neno la Mungu lao ni moja, hawapingani. Kumbuka kadri unavyoliweka neno kwa wingi moyoni mwako na kulitafakari ndivyo unavyokuwa kwenye mazingira mazuri kiroho ya kumshinda Shetani na ndivyo unavyomjengea Roho Mtakatifu maingira mazuri ya kukusaidia.

  • Kusali na kuomba katika roho (Waefeso 6:18)

Biblia katika kile kitabu cha 1Yohana 5:14 inasema “Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake,atusikia”.

Kwa kifupi niseme kwamba jifunze kumtumia Roho Mtakatifu kama msaidizi kwenye eneo la maombi pia. Maana yake jifunze kuomba kwa roho au katika roho. Kuomba katika roho sio kuomba kwa kunena kwa lugha tu, bali kuomba sawasawa na uongozi wa Roho Mtakatifu ndani yako na huku ndiko kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu kwenye maisha yako. Unaomba si kulenga ajenda zako tu bali za Mungu kwa kila wakati wa maisha yako.

Ukiwa na nidhamu ya kuomba kwa mfumo huu wa kuomba katika roho, yeye Bwana ni mwaminifu mahali popote utakapokuwa kama kuna hatari saa hiyo au wakati unaokuja Roho mwenyewe atakupa taarifa mapema na zaidi atakuongoza hata namna ya kuomba ili uweze kupangua vita ambayo Shetani alikuwa amekusudia juu yako.

Naam kwa kifupi ndani ya hizi silaha saba ambazo Paulo aliwafundisha kanisa la Efeso kuna kila aina ya ushindi ambao watoto wa Mungu kama wakizivaa na kuzitumia kwa uongozi wa Mungu mwenyewe basi Shetani hawezi kuwashinda kwenye maisha yao kwa namna yoyote ile. Katika sehemu ijayo ya somo hili nitahitimisha kwa kuandika dondoo za msingi kukumbuka na kujua kuhusu vita vya kiroho.

 Bwana Mungu akubariki sana.