Archive for August 2010

UMEJIAANDAJE KWA TUKIO LA UNYAKUO? (Part 2)

August 30, 2010

Na: Patrick Sanga

Ili kusoma sehemu ya kwanza bonyeza link hii  https://sanga.wordpress.com/2010/04/19/umejiaandaje-kwa-tukio-la-unyakuo-part-1/

Katika sehemu hii ya pili nataka tuweze kuangalia jinsi baadhi ya maandiko yanavyozungumzia tukio hili la unyakuo. Lengo ni kukufanya ujue na uweze kuamini kwamba siku ya unyakuo ipo na inakuja. Kama vile unavyojua kwamba kuna siku kuzaliwa na siku ya kufa, basi amini pia kwamba kuna siku ya unyakuo. Watu wengi sana wanaamini kuna siku ya mwisho wa dunia ambayo Mungu atahukumu wanadamu wote waishio duniani walio hai na wale waliokufa (kwani watafufuliwa pia tayari kwa hukumu hiyo). Naam ni kweli siku hiyo ipo na hukumu hii itafuata mara baada ya ujio wa Yesu mara ya pili ambao utamaliza utawala wa miaka saba ya Mpinga Kristo na kuanza kwa utawala wa miaka elfu moja wa Yesu hapa duniani, kabla ya ile vita ya mwisho ya dunia ambayo Biblia inaiita Gogu na Magogu (Rejea Ufunuo wa Yohana 20:1-15, 2 Wathesalonike 2:1-8).

Hata hivyo si watu wengi pia wanaojua na kuamini kwamba kuna siku ya unyakuo ambayo ni tofauti na ile siku ya mwisho. Watu wengi huwa wanachanganya sana habari hizi za matukio ya mwisho wa dunia na hasa siku ya unyakuo na ile ya mwisho wa dunia. Lengo la kuwepo kwa siku ya mwisho ni Yesu kutoa hukumu dhidi ya watenda dhambi na wenye haki.

Katika hukumu hiyo wenye dhambi watatupwa kwenye ziwa la moto na kiberiti yaani Jehanamu pamoja na Shetani, wenye haki wataurithi uzima wa milele pamoja na Bwana Yesu (Rejea Mathayo 25:31-46, Yohana 5:22). Wakati lengo la kuwepo kwa siku ya unyakuo ni Bwana Yesu kuchukua watakatifu na kwenda nao mbinguni, tukio ambalo likishatokea, ndipo utaanza utawala wa miaka saba wa Mpinga Kristo. Hivyo fahamu kwamba, kabla ya siku hiyo ya mwisho kuna siku ya unyakuo ambayo ndiyo itakayoanza. Kwa lugha nyingine tukio la unyakuo litatangulia na kisha baadaye litafuata tukio la hukumu ya siku ya mwisho. 

Hebu tuangalie sasa baadhi ya maandiko yanavyosema juu ya siku hii;

Katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana 16:15  Yesu mwenyewe anasema “Tazama naja upesi kama mwivi. Heri akeshaye na kuyatunza mavazi yake…” na pia katika Mathayo 24:36-37 anasema “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala mwana, ila baba peke yake. Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adam’.

Paulo naye akiwafundisha wandugu wa Thesalonike anasema ‘Lakini ndugu kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku, wakati wasemapo, kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafla, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa’ (1Wathesalonike 5:1-4)

Ndugu zangu siku hii itakuwa ya ajabu sana, ya kutisha na kuogofya kwa wale watakaoachwa, lakini pia ya baraka na furaha kwa wale watakaonyakuliwa. Hii ni kwa sababu tukio hili litakuwa ni la ghafla mno tena bila taarifa kama vile Mwewe awezavyo kunyakua vifaranga vya kuku. Biblia inaweka wazi kwamba hakuna ajuaye siku wala saa na ndio maana Mtume Paulo anajaribu kulifundisha jambo hili kwa mifano kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na mwivi ajavyo usiku bila taarifa au utungu umshikavyo mama mjamzito kwa ghafla. Nasikitika kusema watu wengi wataachwa kwani si watu wengi wanaoishi leo kwa namna ambayo Bwana Yesu akija kunyakua kanisa atakwenda nao.

Katika tukio hili la unyakuo maandiko yanaeleza wazi kwamba kwanza kutakuwa na ufufuo wa wenye haki waliolala/kufa katika Bwana, na kisha wataungana na sisi tutakaokuwa hai kunyakuliwa kwa pamoja ili kumlaki Bwana Yesu mawinguni.  

Mtume Paulo katika 1Wathesalonike 4:13-18 anasema hivi ‘Lakini ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twaambieni haya Kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi farijianeni kwa maneno hayo’.

Pia katika tukio hili Bwana Yesu hatakanyaga kwenye ardhi bali atakuwa mawinguni/hewani maana kwa mujibu wa 1 Wathesalonike 4:17 maandiko yanasema ‘Tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani’.

Katika 1 Wakorintho 15:51-53 Paulo anasema ‘Angalieni nawaambia ninyi siri; hatutalaa sote, lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda Italia na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu nasi tutabadilika. Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa

Katika fungu hili la maandiko Mtume Paulo anazidi kufafanua jambo aliloawaambia Wathesalonike juu ya siku hii, kwamba parapanda ya Bwana Italia kuashiria tukio hili la ajabu na ni imani yangu kwamba wale walioishi maisha ya utakatifu ndio watakaosikia sauti ya parapanda hii. Baada ya parapanda hii ndipo nguvu ya Bwana ya ufufuo itakapowafaufua wale waliolala katika Bwana na kisha miili yao hao na wale tutakao kuwa hai siku hizo itabadilishwa na kisha kunyakuliwa tayari kwa kumlaki Bwana hewani. Mambo haya yote yatafanyika kwa muda mfupi sana ambao ambao Paulo ameuita kufumba na kufumbua au dakika moja.

Tukio la unyakuo na Mpinga Kristo

Kama nilivyoandika awali kwamba tukio la unyakuo ndio litakalomfunua mpinga Kristo. Kwa mujibu wa maandiko hata sasa mpinga kristo yupo na anaendelea na kazi zake lakini hajadhihirika kwa kuwa kanisa kupitia Roho Mtakatifu linamzuia ashindwe kufanya kazi yake kwa udhihirisho wake halisi. Lakini punde Bwana Yesu akishanyakua watoto wake ndipo yule asi yaani mpinga Kristo atakapofunuliwa (Rejea 2 Wathesalonike 2:6-8)

Mpinga Kristo huyu kwa mujibu wa maandiko atatawala kwa muda wa miaka saba. Kwa vipindi viwili vya miezi arobaini na miwili (42) au siku elfu moja mia mbili na sitini (1260). Tambua kwamba baada ya tukio la unyakuo ndipo litafuata tukio la dhiki kuu kupitia utawala wa Mpinga Kristo.

Naam lengo langu kama mwandishi kwenye sehemu hii ya pili kukuonyesha uthibitisho wa kimaandiko juu ya uwepo wa siku au tukio la unyakuo. Hata kama hutaki kuamini usipuuzie mambo haya, ila nakushauri endelea kufuatilia mfululizo huu na pia kusoma Biblia, makala, majarida, vitabu  juu ya jambo hili na hasa matukio ya mwisho wa dunia maana Yesu alisema asomaye na afahamu.

Najua kwamba Shetani hapendi watu wafahamu ukweli kuhusu jambo hili, anachotaka ni kuwapumbaza na kuwadanya wasijue kweli, ili siku ile itakapofika waachwe waingie kwenye dhiki kuu ambayo Yesu mwenyewe alisema haijawahi kutokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu, na wala haitakuwapo kamwe (Mathayo 24:21). Usikubali ndugu yangu kutekwa ufahamu wako na fikra za Shetani, akakufanya ukapuuzia mambo haya na kisha ukaingia kwenye dhiki kuu.

Mpenzi msomaji katika sehemu ya tatu ndipo nitakapoanza kuzungumzia namna ya kujiandaa kwa ajili ya unyakuo kadri ninavyosikia na kujifunza kutoka kwa Bwana kupitia neno lake. Naomba sana maombi yako maana vita niliyoipata hata sasa tangu nimeweka nia ya kuanza kuandika ujumbe huu na ule wa vita vya kiroho ni kubwa sana. Ni imani yangu kwamba kwa maombi yako nitaandika mambo haya kwa wakati ili kuuandaa mwili wa Kristo yaani watu wake pamoja nami tayari kwa tukio hili la kubwa.

Tutaendelea na sehemu ya tatu…

VITA VYA KIROHO (Part 3)

August 30, 2010

Na: Patrick Sanga

Waraka wa Agosti

Ili kusoma sehemu ya pili bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2010/06/21/vita-vya-kiroho-part-2/

 SILAHA ZA USHINDI DHIDI YA SHETANI KATIKA VITA VYA KIROHO (Part 1)

Naam zipo namna nyingi sana ambazo Shetani anafanya  kazi yake hapa duniani tena kwa hila na nina amini hata sasa wewe ni shahidi juu ya namna Shetani alivyofanikiwa kuvuruga maisha, ndoa, familia, kanisa au nchi yako kwa hila zake. Katika sura hii ya tano nataka kuaandika juu ya silaha zitakazokusaidia kumshinda Shetani na hila zake katika vita vya kiroho.

Mtume Paulo alipokuwa akiwafundisha kanisa la Korinto juu ya jambo hili aliandika akisema  “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome, tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo’ (2 Wakorinto 10:3-6).

Katika nukuu ya maandiko hapo juu, Paulo anatuonyesha kwamba kuna silaha za vita vyetu ambazo si za kimwili. Na hizi silaha zimetengenezwa kwa namna ambayo zinauwezo wa kuangusha ngome kwa maana ya mawazo na fikra (hila) zinazojiinua kinyume cha elimu ya Mungu. Picha tunayoipata hapa ni kwamba vita anayopigana Shetani ni dhidi ya elimu ya Mungu kwetu. Na kwa sababu hiyo kuwa na elimu ya Mungu ni jambo la msingi katika kuvipiga vita vya kiroho.

Mtume Paulo pia katika kitabu cha Waefeso 6:10-12 anafafanua zaidi juu ya hizi silaha za vita ambazo si za kimwili akisema ‘Hatimaye mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uwezo wa nguvu zake, vaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kuzipinga hila za shetani; kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama ; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa  roho’.

Mungu, alikiwisha jua kwamba vita vya kiroho itakuwa sehemu ya maisha kwa watoto wake, hivyo akaandaa na silaha ambazo kama watoto wake watazitumia kwa hakika watakuwa ni washindi katika kila vita watakayopigana na hivyo kuhakikisha mawazo yake yanatimia kwenye maisha yao. Fahamu kwamba hizi silaha ni za Mungu, unapozivaa haimanishi wewe ndiye unapigana, bali Mungu.  Maana imeandikwa vita ni vya Bwana na kinachotafutwa ni kupinga elimu ya Mungu juu yako.

Kumbuka Mtume Paulo hakusema zitumieni, bali alisema vaeni silaha zote za Mungu. Wewe ukizivaa hizi silaha zinaingia kazini kukushindia vita iliyoinuka juu yako. Maana zenyewe zinauwezo katika Mungu hata kuangusha ngome. Kwa hiyo kitendo cha wewe kuzivaa hizi silaha za vita ni kumtengenezea Mungu mazingira ya kuzitumia hizo silaha ulizozivaa kupigana upande wako kwa ajili ya jina lake na kusudi lake kupitia wewe. Hata hivyo zipo baadhi ya silaha ambazo Mungu atawajibika kukupa wewe maelekezo juu ya namna unavyoweza kuzitumia ili kuona ushindi katika vita vya kiroho.

Zifuatazo ni silaha za kukusaidia kushinda katika kuvipiga vita vya kiroho kama ukizivaa na kuzitumia pia sawasawa na malekezo yake kwako;

  • Kujifunga kweli katika kiuno chako (Wafeso 6:14a)

Kujifunga kweli maana yake ni kusema na kuitenda kweli yote kama ambavyo neno la Mungu linaagiza. Kwa mujibu wa Yohana 17:17 neno la Mungu ndiyo kweli. Biblia inasema kwenye mstari wa 17 ‘Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndiyo kweli’. Kujifunga kweli maana yake ni kuwa mtu ambaye siku zote unazungumza ukweli na si uongo. Na ujasiri wa kunena kweli utaupata kwa njia ya kuwa na neno la Mungu ndani yako. Shetani ndiye baba wa uongo, kwa hiyo kwake kutumia uongo katika kufanikisha kazi zake ni jambo la kawaida.

Ili Shetani afanikiwe kuharibu mahusiano yako na Mungu atakufundisha kutumia uongo kama njia ya wewe kufanikiwa kimaisha. Wewe mwenyewe ni shahidi, jinsi watu wengi wanavyofanikisha mambo yao kwa kutumia uongo. Fahamu kwamba kwenye kila wazo la Shetani kuna uongo ndani yake. Huwezi kumshinda kama hutajifunza kusema kweli. Jifunze siku zote kusema kweli bila kujali ukweli au uaminifu huo utakugharimu kiasi gani.

Lengo lako liwe kumpendeza Mungu na si wanadamu, kama unajua kusema na kuitenda kwako kweli ndiyo mapenzi ya Mungu basi zungumza kweli yote blia kuficha. Kwa Mungu ukisema kweli unavuta ulinzi wake kwako na ukisema uongo unaoundoa ulinzi wake kwako. Jifunze jambo hili kupitia maisha ya Danieli na Yusufu katika Biblia. Kusema kweli ni kuharibu kazi nyingi za Shetani, maana msingi wa kazi za Shetani ni uongo. Na kwa sababu hii usifikiri mtu anayesema kweli watapatana na Shetani. Hata hivyo usiogope kwani kwa kuwa Mungu ni kweli atakulinda na hila zote za yule mwovu. Kama unataka kufanikiwa kimaisha jifunze kusema, kuitenda na kuitetea kweli.

  • Kuvaa dirii ya haki kifuani (Waefeso 6:14b)

Ukisoma kitabu cha Warumi 2:13 Biblia inasema “kwa sababu si wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki”.

Na pia katika Isaya 32:17 Biblia inasema ‘Na kazi ya haki itakuwa amani; na mazao ya haki yatakuwa ni utulivu na matumaini daima’.

Zaburi 37:28 “Kwa kuwa BWANA hupenda haki, wala hawaachi watauawa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa”.

Kila moja ya hizi silaha ambazo Paulo aliwafundisha kanisa la Efeso ina maeneo maalum ambayo unapaswa kuitumia ili kuona ushindi katika vita vya kiroho. Silaha ya haki sio silaha ya mashambulizi bali ni silaha ya kinga. Silaha ya haki unapaswa kuitumia au imekusudiwa kutumika hasa pale unapopita au kukutana na vita yenye kukuletea maudhi, hasira, gadhabu, chuki nk na hasa kwa njia ya maneno, mawazo na matendo. Yaani Shetani anapanda maneno/wazo ndani ya mtu, kisha huyo mtu anakuja kukuletea hayo maneno au anatenda jambo ambalo kwa namna moja au nyingine unajikuta hasira na chuki imeingia ndani yako.

Kibiblia lazima ujue kwamba kuna mabaya mengi ambayo yamekusudiwa juu yako kama mtoto wa Mungu kutoka kwa Shetani. Salama yako ni wewe kuivaa dirii ya haki kama mojawapo ya silaha ya vita. Kuivaa dirii ya haki maana yake ni kuitenda sheria ya Bwana, kuwa na utulivu, kutafuta amani na kuweka tumaini lako kwa Mungu licha ya mazingira ya hatari/maudhi unayoyapitia. Kadri unavyotenda mambo haya ndivyo unavyomfanya Bwana kuwa mlinzi na ngome kwako wakati wa taabu na mabaya. Si hivyo tu bali unakuwa umetengeneza mazingira ya Mungu kutokukuacha na hivyo kupigana upande wako dhidi ya adui zako.  

Moja ya mbinu kubwa anazozitumia Shetani kuwaangamiza watu wengi leo ni kuwafarakanisha wao na Mungu wao au wao kwa wao. Ninaposema kufarakanisha namanisha kukosanisha, kuondoa amani, kuwafanya wachukiane, wasiaminiane, kuleta maudhi kati yao na hivyo kupelekea wasemane vibaya, mmoja amwone mwingine hafai nk.

Silaha ya haki ina uwezo wa kukutengeneza mazingira ya amani, utulivu na matumaini endapo unapita kwenye mzingira ya mafarakano, kuumiza, maudhi nk. Watu wengi wanapokuwa wamekosana kwa jambo lolote lile wengi huishia kugombana, kutengana, kukata mawasilano nk. Inapofika mahali pa namna hii unatakiwa kuvaa dirii ya haki kifuani mwako kwa maana ya kuweka kwenye matendo kile ambacho sheria ya neno la Mungu inasema. Si hivyo tu bali pia unatakiwa kuwa na imani juu ya kile ambacho sheria imeonyesha. Kumbuka haki haiji kama mtu sio mtenda sheria, yule mwenye kuitenda sheria ndiye mwenye kuhesabiwa haki. (Warumi 2:13).

Mfano; Waebrania 12:14 inasema “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atkayemwona Bwana asipokuwa nao”.

Mpaka Roho Mtakatifu anaagiza jambo hili liandikwe ina maana hawa ndugu walikuwa wamefarakana na kati yao hakuna amani wala utakatifu. Na huu ulikuwa ni makakati wa Shetani kuhakikisha hawa watu wanakosa kuona uwepo/uongozi wa Bwana kwenye maisha yao ya sasa na pia washindwe kuurithi uzima wa milele.

Hivyo ikalazimu Roho Mtakatifu kupitia mwandishi kuwaagiza kusema sharti matafute tena amani  na huo utakatifu vinginevyo hamtaweza kumwona Bwana akijifunua kwa kiwango cha juu kwenye maisha yenu. Kitendo cha wao kutafuta tena amani ambayo Shetani alifanikiwa kuipoteza kati yao ndiko kuivaa dirii ya haki yaani kuweka kwenye matendo kile ambacho sheria ya Roho wa uzima imeagiza.

Kumbuka kazi ya haki ni amani na mazao yake ni utulivu na matumaini daima. Hii ina maana ukiivaa haki, itakuletea amani, utulivu na matumaini daima. Utulivu na matumaini vinahitajika hasa wakati wa adha au vita inayolenga kuondoa amani kati yako na mtu au watu wengine. Usikubali Shetani akuondolee amani yako kwa sababu iwayo yote, jifunze kuvaa dirii ya haki kifuani mwako kwa kiuitenda sheria ya Bwana. Zaburi ile sura nzima ya 37 ni mfano halisi wa namna ya kuitumia haki kama silaha ya vita, hakikisha unaisoma hiyo sura nzima.

  • Kuwa na shauku/utayari wa kuhubiri Injili ya amani (Waefeso 6:15)

 Injili ni habari njema za Yesu Kristo ziletazo amani. Kwa mujibu wa Mathayo 28:19-20 “Yesu aliwaambia wanafunzi wake “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nami siku zote, hata ukamilifu wa dahari”.

 Ndoa, familia, na watu wengi leo hawana amani kwa sababu Yesu si Bwana/mtawala kwenye maisha yao. Wapo ambao hawajamuani kabisa lakini pia hata wale wanaokiri kumuanini bado hawajampa kuyaongoza na kuyatawala maisha yao kwa asilimia mia moja. Ni jukumu lako sasa kuwaambia watu hao  uzuri wa huyu Yesu uliyemwamini wewe katika kuponya, kulinda, kubariki, kuwakomboa kutoka katika dhambi na hukumu ijayo nk ili na wao wamuamini.

Ngoja nikupe siri hii nzuri, zipo baraka nyingi sana za kiulinzi kutoka kwa Bwana zinazoambatana na wewe kumtumikia Mungu kwa njia ya kuwaambia wengine habari za huyu Yesu. Na jambo hili halikuhitaji uwe Mchungaji, Mwalimu au Mwinjilisti bali utayari/shauku ya kuwaambia au kuwafundisha wengine habari za Yesu uliyemwamini.

Kile kipengele cha mwisho cha Mathayo 28:20 Yesu aliwaahidi wanafunzi wake kwamba yeye atakuwa pamoja nao siku zote, hata ukamilifu wa dahari. Kuwa pamoja nao ni pamoja na kuwalinda dhidi ya kila hila na uharibifu kutoka kwa Shetani. Jambo hili Mtume Petro aliandika akisema tunalindwa na nguvu za Mungu kwa imani. Imani ipi? Imani ya kulindwa kunakotokana na kumtumikia Mungu. Yapo mengi mabaya ambayo Shetani amekusudia juu yako ambayo huyaoni ila kwa wewe kuwa mwaminifu kufanya kazi hii ya Mungu ya kumfanya yeye ajulikane itakupa kibali mbele zake cha kumfanya adumu kukulinda maana una thamani kwenye ufalme wake. Mimi binafsi ni shahidi wa jambo hili. Binafsi nimelithibitisha jambo hili katika Bwana, maana nimeona Mungu akinipigania kwa namna ya ajabu dhidi ya hila za Shetani za kunimaliza kiroho na kimwili, sababu ikiwa kumtumikia yeye kwa kuwafundisha wengine habari zake.

  • Kuwa na imani kwamba Mungu atatenda yale aliyoahidi katika neno lake (Waefeso 6:16)

Waefeso 6:16 inasema ‘zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu’.

Waebrania 11: 1 inatueleza kwamba ‘Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyoonekana’.

Ndani ya Biblia zipo ahadi nyingi za Mungu kwako ambazo zinagusa kila eneo la maisha yako kiulinzi, baraka, uponyaji, afya njema, uzima, uzao, mafanikio nk. Ni jukumu lako kuzisoma na kuifunga imani yako hapo. Maana mara nyingi Shetani huwawekea watu mashaka juu ya Mungu wao na ahadi zake kwamba hatazitimiza. Kwa hiyo kama huzijui hizo ahadi ni rahisi sana kutekwa na fikra za Shetani. Hivyo ni jukumu lako kuhakikisha unaweka imani thabiti kwenye ahadi za Mungu katika maisha yako.

Siku zote Shetani hutumia mashaka/kukosa imani na hofu kama zilaha zake za kukuondoa kwa Mungu. Hii ikiwa ni pamoja na kukujengea mawazo kwamba neno la Mungu si kweli na ahadi zake ni uongo na hasa hufanya jambo hili kwa njia ya mawazo kama nilivyoeleza kwenye sehemu ya kwanza ya somo hili kwamba vita huanzia kwenye mawazo. Mawazo haya ya uharibifu, Mtume Paulo anayaita mishale yenye moto ya yule mwovu. Ili uweze kuizima hii mishale lazima uitwae ngao ya Imani, yaani uwe na uhakika juu ya ahadi za Mungu kwenye maisha yako kwamba atazitimiliza.

Naamini unapata mambo ya kukusaidia, kwa leo naishia hapa tutaendelea na hizi silaha katika sehemu ya nne…