Archive for April 2010

UMEJIAANDAJE KWA TUKIO LA UNYAKUO? (Part 1)

April 19, 2010

Na: Patrick Sanga

Nakusalimu kwa jina la Yesu!

Ili uweze kuelewa somo hili mpenzi msomaji nakushauri tafuta muda usome vizuri sura ya 24 ya kitabu cha Mathayo.

Mimi nitanukuu mistari michache  kwenye sura hii;

Mathayo 24:36-44 “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala mwana, ila baba peke yake. Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adam.

 Kwa kuwa kama vile siku zile zilizovyokuwa kabla ya gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adam. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa mmoja aachwa, wanawake wawili watakuwa waskisaga; mmoja atwaliwa,mmoja aachwa.

 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamunu neon hili; kama mwenye nyumba angalijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingeliacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyoidhani mwana wa Adam yuaja”.

 Nakumbuka ilikuwa tarehe 27/03/2010, majira ya saa kumi na moja za jioni, nikiwa nimekaa chumbani kwangu, naangalia mkanda kwenye Laptop na nilikuwa na mke wangu. Ghafla nikahama katika ulimwengu huu kimawazo nikaenda kwenye eneo jingine, picha ya siku ya unyakuo ikanijia, na nikaanza kuona kwa sehemu nga kidogo jinsi unyakuo utakavyokuwa, nikaona  nguvu fulani ambayo inamnyanyua mtu na kwenda naye juu.

 Kwa ujumla si rahisi kuandika vizuri jinsi nilivyoona, lakini niliona watu wakianza kunyanyuliwa na dunia ilikuwa kama imepigwa na butwaa!. Baada ya maono haya nikaanza kutafakari na moyoni mwangu nikasikia uzito kwenye moyo kana kwamba Yesu ndiyo anarudi saa ile, ndipo nikasikia sauti kwenye ufahamu wangu ikiuliza umejiandaaje kwa ajili ya unyakuo na umewaandaaje watu wangu kwa ajili ya unyakuo?

 Wakati mambo hayo yanaendelea, mke wangu alikuwa akinisemesha lakini sikumelewa ingawa nilikuwa namsikia kwa mbali, macho yangu yalielekea kwenye mkanda lakini sikuelewa kilichokuwa kinaendelea pia. Baada ya dakika kumi hivi ndipo nikarudi kwenye ufahamu wangu wa kawaida nikaanza kutafakari na nikachukua hatua ya kwenda kuomba kwanza.

 Mara nyingi jambo hili limekuwa likinijia na Bwana ameendelea kunifundisha vitu vingi juu ya suala hili. Kutokana na yale ambayo nimejifunza na ninaendelea kujifunza katika neno lake imenilazimu kuanza kuandika mfululizo wa somo hili mpaka hapo Yesu atapokuja ikiwa atatukuta tukiwa hai au hadi pale nitakapoondoka kwa njia ya kifo. Na nimeamua kufanya hivi kwani swali la pili niliulizwa umewaandaaje watu wangu kwa tukio la unyakuo?. Nitaandelea kuweka mafundisho haya kwenye blog, ili kila mtu anayetaka kuwa tayari kwa unyakuo basi ajifunze na ajue namna ya kujiandaa.     

 Mpenzi msomaji maswali haya mawili kwangu yaliniumiza sana. Unajua wakristo wengi kwa jinsi tulivyo kila mmoja ana amini kwamba Yesu akija leo ataenda mbinguni. Hakuna mtu unaweza ukamsikia anasema siku ya unyakuo nitaachwa. Unajua ni kwa nini?. Wengi si kwa sababu Roho wa Yesu ndivyo anavyowashuhudia kwamba wataenda na Bwana, bali ni kwa sababu Shetani amepanda wazo kwenye fahamu zao kwamba Mungu hawezi kuwaacha hata kama mtu hayatendi mapenzi yake.

 Nisikilize kanisa, maadam niliulizwa nimewaandaaje watu wake, nami nina ujasiri wa kuandika na kukufundisha mambo mengi ambayo najua Shetani asingependa uyasome na kuyasikia. Nami nakuomba anza sasa kufuatilia masomo nitakayokuwa naandika kuhusu unyakuo, lakini pia fuatilia masomo ya watumishi wengine juu ya unyakuo ili uweze kuwa tayari kwa tukio hili la kushangaza na kuogofya.

 Nini anachokifanya Shetani nyakati za sasa?

 Katika kipindi hiki cha dakika za mwisho Shetani anatumia hila na uongo wake kuwapumbaza watu wengi kuhusu unyakuo na habari za Yesu kwa ujumla. Anachokifanya shetani ni kuhakikisha anazuia kwa kila hali watu wasisikie habari za Yesu na hasa kuhusu matukio ya mwisho wa dunia. Na hii ni kwa sababu anajua chanzo cha imani katika Kristo ni kusikia habari za Kristo Yesu.

 Na kwa wale waliokwisha kusikia ana hakikisha hawaliweki kwenye matendo lile neno. Si hivyo tu bali, anajitahidi kuwafanya watu wasiamini kweli ya neno la Mungu. Anapofusha amri/sheria nyingi za Mungu kwenye fahamu za watu. Ananyanyua watumishi wa ufalme wa giza na kuwapa uwezo mkubwa na hao watumishi anawaagiza kutofundisha kweli yote ya neno la Mungu (kumbuka yeye hujigeuza na kujifanya malaika wa nuru). Si hivyo tu bali hata wale watumishi wa ufalme wa nuru anawapumbaza na kuwalaghai kwa hila na kuteka fahamu zao kwa njia nyingi ili wasiwafundishe wanafunzi/washirika wao kweli yote ya neno la Mungu. Shetani anawafanya watu kuwa ‘busy’ na kazi na pia mambo yasiyo ya msingi /yasiyofaa hata kama ni halali.

 Sikia kanisa, si tu kusema kwamba  umeokoka ndiyo tiketi ya kwenda mbinguni. Warumi 2:13 inasema “kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki”.

 Ndugu yangu maadam umeamua kumwamni Yesu, sharti uwe tayari kufuata sheria zinazoongoza ufalme/utawala wake, na sio tu kusema mimi ni mwanachama wa Yesu. Je, unakumbuka jinsi shetani alivyotumia hila kuwadanganya Adam na Eva pale bustanini (Mwanzo 3:1-7). Naam hata leo ndivyo anavyofanya, na kwa njia hiyo atawafanya wengi kuachwa na Bwana siku ile itakapofika.

 Je, unajua kwa nini anafanya hivyo?

 Lengo ni kuwapumbaza watu wasiwe macho kiroho/wasikeshe wakidumu kuzitenda amri za Bwana, wala kutafakari neno lake wasije wakafunguka macho yao na kugundua hila zake. Yesu alisema kama ilivyokuwa siku za Nuhu ndivyo itakavyokuwa katika kizazi hiki.

 Je kwa Nuhu ilikuwaje?

 Watu walikuwa wakiendelea na shughuri zao za kila siku kama kawaida, wakioa, wakiolewa, wakilima, kufanya biashara nk. Unisikilize ndugu hakutakuwa na matangazo kwenye vyombo vya habari kwamba watu jiandaaeni Bwana Yesu atakuja siku au mwezi fulani kulichukua Kanisa Lake. Itakuwa ni kitendo cha ghafla na bila wengi kutarajia. Ni katika saa usiyoidhani wewe ndipo Bwana atakapokuja.

 Kwa hiyo Shetani anawapumbaza watu wawe ‘busy’ na mambo mengi ili ile siku Bwana atakapokuja waachwe. Nasema usikubali, maadam umeokoka wewe si mtu wa giza, haipasi siku ile ikukute kama vile mlevi. Huu ndio wakati wa wewe kujiandaa na kuwaandaa wengine.

 Sikia ee, Kanisa, kurudi kwa Yesu kumekaribia sana. Mara nyingi kwenye ufahamu wangu wazo la unyakuo huwa linanijia na nina amini kwanza ni kwa ajili yangu kujiandaa, lakini kila likinijia huwa nafikiri na watu wengine ambao bado hawajaokoa, lakini pia na wale ambao wameokoka lakini maisha yao hayapo sawasawa na mapenzi ya Mungu tunawasaidiaje?.

 Ndugu zangu siku hiyo haisemeki, itakuwa ni siku ya aibu, huzuni isiyo na kipimo, majuto yasiyosemeka. Ni heri kama usingelizaliwa mpenzi msomaji, kuliko kuokoka halafu ukaachwa kwenye ile siku. Huruma ya Yesu itafikia mahali itakoma. Yesu anatuvumilia sana, na laiti ungelijua namna anavyokulinda usife na sababu kubwa ikiwa ni kukupa nafasi ya kutengeneza maisha yako, usingefikia mahali pa kujisifu, kuhukumu wengine, kudharau na kuishi maisha ya kienyeji kiasi hicho.

Ngoja nimalizie kwa sentensi hii, siku moja nikiwa natembea kwenda kanisani Bwana aliniambia “watu wengi ninawapigania na kuwalinda wasikutwe na mauti, maana najua wakifa kwa kuwa hawako tayari hawawezi kuja kwangu, inaniuma sana hao watu wanapotafsiri vibaya ulinzi wangu kwao, wao wanafikiri ni kwa sababu wana haki ya kuishi tokana na elimu, fedha, madaraka yao, kumbe sivyo. Na mbaya zaidi licha ya kuwatengenezea watu hao fursa nyingi za kutubu/kutengeneza njia zao, wao hawakubali kutii/kubadilika. Sina namna ya kumsaidia mtu ambaye hayuko tayari kunitii”.

 Mpendwa wangu uvumilivu wa Mungu kwako na kwangu kwanza ni ili tutengeneze njia zetu, ukiendelea kufanya shingo ngumu, huruma yake itafika mahali na kukoma. Watu wengi ambao wako kuzimu hivi sasa, ujue sehemu kubwa walipuuzia nafasi/fursa ambazo Mungu aliwapa za wao kutengeneza njia zao.

 Ujumbe huu unakuja kwa lengo la kukuonyesha mambo ya msingi unayotakiwa kufanya kama sehemu ya maandalizi tayari kwa siku ya unyakuo.

 Tutaendelea na sehemu ya pili…

KUFANIKIWA KWA KUSUDI LA MUNGU KUNATEGEMEA NAMNA UNAVYOTUMIA FURSA ULIZOPEWA (Part1)

April 8, 2010

Na: Patrick Sanga

Waraka wa Aprili

Heri ya Pasaka mpenzi msomaji!

“ Naam jifunze kutumia vizuri fursa anazokupa Mungu maishani mwako, ili usiathiri/usikwamishe kusudi la Mungu kwako na kwa wengine”

 Isaya 53:3-6

Kwetu Wakristo majira ya Pasaka ni kipindi cha muhimu maana lengo la Mungu kumtuma Yesu ndiyo lilitimia hapa. Kupitia kifo cha Yesu tumeupata wokovu na ushindi dhidi ya nguvu zote za Shetani. Katika kipindi hiki nimeona ni vema nika-kutafakarisha mstari huu wa Isaya 53:5 unaosema “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu, Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”.

 Katika fungu hili la maneno nataka tutazame zaidi sentensi hii inayosema ‘adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake’. Je, umeshawahi kutafakari sentensi hii ina maana gani? Huenda zipo tafsiri nyingi tegemeana na namna unavyotazama na pia unalenga nini katika kujifunza. Baada ya kutafakari sana niligundua mambo mawili yafuatayo;

Jambo la kwanza;

  • Ilimlazimiu Yesu  kuteseka ili sisi tupate amani

Mpenzi msomaji wangu ukweli ni kwamba kwa dhambi zetu ilibidi sisi (wanadamu) kuadhibiwa. Lakini kutokana na upendo wake alikubali kubeba adhabu yetu ili sisi tupate amani.  Yohana 15:3 “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake”. Na ni matarajio yake kwamba gharama kubwa ya kifo chake ni kwa ajili yetu tupate amani, na anatarajia tuitumie vizuri amani aliyotuletea tokana na kifo chake.

Wakolosai 1:20 ‘Na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake’…

Wakolosai1:20 ‘Kwa njia yake Mungu alivipatanisha naye vitu vyote naam, viumbe vyote mbinguni na duniani; alileta amani kwa damu ya Kristo msalabani” (Tafsiri nyingine).

 Jambo la pili;

  • Adhabu yake ilitokana na mwanadamu kutumia vibaya amani aliyopewa/iliyokuwepo.

Moja ya kazi au faida kubwa ya kifo cha Yesu pale msalabani ni “kurejesha/kuleta amani duniani na pili ni kuukomboa wakati ambao ulikuwa umetekwa”. Hii ni kwa sababu mwanadamu alitumia vibaya amani   aliyopewa. Sasa naamini unajua palipo na amani ndipo penye maendeleo. Hivyo tunapoendelea na somo hili naomba itazame amani kama fursa (opportunities) za mtu kufanya vitu/mambo mbalimbali ili afanikiwe. Ili kufanikisha kusudi lake Mungu amemuwekea mwanadamu fursa tofautitofauti ili  azitumie. Ni jikumu la mwanadamu kuzitumia vizuri na akifanya hivyo kusudi la Mungu litatimia kwake na kwa wengine.

 Hebu tutazame  na kujifunza kutoka katika habari hii ya Luka;

  Luka 19:41-44 inasema“Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua hata wewe ,katika siku hii yapasayo amani, lakini sasa yamefichwa machoni pako, kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke, watakuzingira na kukuhusuru pande zote, watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako”.

 Tafsiri nyingine ya Kiswahili inasema “Luka 19:42 inasema: “Laiti ungelijua leo hii yale yaletayo amani... na pia mstari wa 44 inasema …kwa sababu huku-utambua wakati Mungu alipokujia kukuokoa…”

Toleo la ASV mstari wa 42  inasema “If thou hadst known in this day, even thou, the things which belong unto peace! but now they are hid from thine eyes”.                                                                                                      Toleo la DARBY kwenye mstari huo linasemaIf thou hadst known, even thou, even at least in this thy day, the things that are for thy peace: but now they are hid from thine eyes”.

 Sasa kutoka kwenye tafsiri hizi nne utagundua;

 Kilichowaingiza kwenye shida hawa ndugu (mji) ni kutokujua yapasayo/yaletayo amani na pia kutotambua majira ya kujiliwa kwao. Hii ina maana hawakujua amani yao imeshikilwa/inaletwa/inatokana/ inategemea nini?. Kutokujua kwao kuliwafanya washindwe kuidumisha amani iliyokuwepo.  Kwa kifupi Yesu alimaanisha amani yenu imeshikiliwa na vitu fulani ambavyo mnatakiwa kuvilinda, kuvitunza nna kuvizingatia vinginevyo uharibifu mkubwa utawajia. Yesu alitaka wajue amani haiji yenyewe, bali kuna vitu vinavyoileta amani, kuna vitu vimeishikila amani, au hadi amani ije inategemea vitu fulani. Kwa hiyo ni mpaka mvitafute/mvitazame/mvizingatie vinavyoleta au vinavyshikilia amani.

 Hebu soma mstari huu Waebrania 12:114 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote…”. Amani yako na watu wengine inategemea vitu fulani, mojawapo ya hivyo vitu au nguzo ni fursa, namna unavyotumia fursa ulizopewa zitaamua amani au mafarakano. 

 Sikia kanisa, hawa ndugu hawakujua kwamba amani yao imeshikiliwa na ‘namna wanavyotumia fursa walizopewa’. Wakitumia vizuri amani yao itadumu na wakitumia vibaya amani yao itaondoka. Na hivyo kufanikiwa kwa kusudi la Mungu katika maisha yao kulitegemea namna wanavyotumia fursa walizopewa na Mungu.

 Hata leo, ni kwa sababu ya wanadamu kutokutumia vizuri fursa ambazo Mungu amewapa katika maisha yao ndio maana wanatahiri kusudi la Mungu kwenye maisha yao na kwa wengine. Fursa ambazo Mungu angetegemea zitumike vizuri, watoto wake wanazitumia vibaya na hivyo kukwamisha kazi yake. Kanisa sikia  hakuna kitu Kinamuuma Mungu kama watu kushindwa kutumia vizuri fursa alizowapa”. Jambo hili linamuumiza kiasi cha kumrudisha msalabani mara ya pili. Amani aliyokupa kama fursa kwa wewe kuitumia vibaya inamuingiza kwenye gharama kubwa na kumuumiza sana.

 Tutaendelea na sehemu ya pili…

Ubarikiwe.

VITA VYA KIROHO (Part 1)

April 8, 2010

 

Na: Patrick Sanga

 Yohana 10:10 ‘Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu…

 Waefeso 6:10-18 ‘Hatimaye mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uwezo wa nguvu zake, vaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kuzipinga hila za shetani 12 kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama ; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwngu wa  roho’.

 2 Wakorinto 10: 3-5 ‘Maana ingawa tunaenenda kaitka mwili hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili 4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili,bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome); 5 tukiangusha mawazo na kila kkitu kilichoinuka kijiinuacho kinyume cha elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii kristo.

 Siku zote jambo lolote lile linalotokea kwenye maisha ya mtu katika ulimwengu wa kimwili ujue lilianzia kwenye ulimwengu wa kiroho. Mfano ukiona wanandoa wanatengana ujue walishatengana kwanza katika ulimwengu wa roho ndipo sasa inadhihirika kwenye ulimwengu wa kimwili.  Kwa hiyo siku zote vita kati ya Mkristo na Shetani inapigwa katika ulimwengu wa roho kwanza.   

 Mtu akimshinda shetani na mapepo yake kwenye ulimwengu wa roho ujue hata kwenye ulimwengu wa mwili atashinda. Naam ni katika ulimwengu wa roho ndipo Mungu anapotaka watoto wake tuliokoka tujue namna ya kuvipiga vita dhidi ya shetani. Naam tukishindwa kwenye ulimwengu wa roho na kwenye ulimwengu wa kimwili tutashindwa na tukishinda kwenye ulimwengu wa  roho na kwenye ule wa mwili tutashinda.

 Ukweli huu tunaupata kutoka kwenye andiko la 2Wakorinto 10:3-5, maana Biblia inasema silaha zetu si za mwili, ina maana ni za kiroho, sasa huwezi kutumia silaha za kiroho kupigana vita ya kimwili. Na kwa hiyo mapambano ni katika ulimwengu wa roho sawasawa na Waefeso 6:12.

 Watu wengi huwa wanasubiri hadi jambo litokee kwenye ulimwengu wa mwili ndipo na wao utaona wanapanga mikakati mizito ya maombi tena ya kufunga. Sio kitu kibaya lakini kibiblia ni makosa kwa sababu tunakuwa watu tunaoongozwa na matukio katika ulimwengu wa mwili wakati Mungu alikusudia tushughulike na hilo jambo tangu lilipojitokeza kama wazo katika ulimwengu wa roho. 

 Unapoona watu wanafanya maandamano katika ulimwengu wa mwili ujue tayari hayo maandamano yalishafanyika kwenye ulimwengu wa roho. Kwa hiyo kama hukutaka hayo maandamano yafanyike, ulitakiwa kuwa macho kwenye ulimwengu wa roho ili punde utakapoliona wazo la kuandamana kwenye ulizuie kule kule na kisha ungesikia hata kwenye ulimwengu wa kimwili maandamano yameahirishwa.

 Ikumbukwe kwamba chanzo cha vita/ugomvi/vurugu zozote zile kwa wanandoa, viongozi, watumishi, marafiki nk ni Shetani. Shetani ndiye anayepanda wazo la ugomvi, kusengenya ndani ya mtu nk kupitia mapepo. Mapepo ni watenda kazi wa shetani, ambao wanafanya kazi kwa amri yake. Mfano ili kuvuruga ndoa Shetani anaweza kutuma pepo la kutozaa kwa wanandoa, na vita ikaanzia hapo nk.

 Na ndiyo maana Paulo kwa kainsa hili la Efeso aliomba akisema “Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru…” (Waefeso 1:18). Hii ni kwa sababu vita yoyote ile huanzia kwenye ulimwengu wa roho tena kwa mfumo wa wazo. Shetani hutafuta nani ampatie wazo lenye kuleta uharibifu. Na akimpata ndipo huteremsha wazo hilo kwenye moyo wake. Ezekieli 38:10 inasema “Bwana Mungu asema, itakuwa katika siku hiyo mawazo yataingia moyoni mwako, nawe utakusudia kusudi baya”.

 Vita yoyote ambayo Shetani anaipiga inalenga kuharibu maisha ya mtu. Mfano Adam na Eva (Mwanzo 3), Mfalme Daudi (2 Samwel 11). Hata siku moja shetani huwa hafanyi vita bila lengo. Kama Mungu anayo mawazo ya amani anayo kuwazia, na shetani naye anayo mawazo ya uharibifu anayokuwazia.

 Mwenye kuvileta vita hivi ni shetani. Kwa hiyo usije ukamchukia ndugu yako kama unaona anakuchukia wakati mlikuwa manapatana. Ukiona ndugu yako anakuchukia ujue siyo yeye ni wazo alilopewa kwenye ulimwengu wa roho. Sasa badala ya kulifanyia kazi huko, yeye akazembea na ndio maana hata kimwili anakuchukia.

 Tutaendelea na sehemu ya pili…