Archive for September 2009

UFUNGUO WA BARAKA ZAKO KIFEDHA

September 3, 2009

Na: Sanga, P.S.

 Malaki 3:1-12

Ule mstari wa nne na wa tano unasema “wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zintakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu wa wazinzi, na juu yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema Bwana wa majeshi”

Mpenzi msomaji sijui kama unajua kwamba neno la Mungu ni jumla ya mawazo na majibu ya Mungu kwa mwanadamu. Kuna siri nyingi sana ndani ya Biblia, ambazo si rahisi kuzielewa mpaka Roho wa Yesu akufunulie kwa utukufu wake utakapomtafuta.

Ilikuwa tarehe 31/08/2008, wakati naomba nilimuuliza Mungu maswali mawili ya kifedha.  Moja lilihusu ujenzi wa kanisa la mahali ninapoabudu na la pili lilihusu mahitaji yangu ya kifedha.  Baada ya maombi hayo ndipo Mungu aliponifunulia siri hii nami nataka nikushirikishe. Ukiweka kwenye matendo siri hii naamini maisha yako ya kiuchumi yatabadilika na kuwa bora zaidi.

Inawezekana maisha yako kiuchumi kwa sasa si mazuri, biashara zako pia hazijakaa vema, miradi yako pia haijakaa vema ni kama haisongi mbele, kuomba unaomba, yumkini na fungu la kumi unajitahidi kutoa, na sehemu ya mapato yako unapeleka kwa watumishi, bado kuna fungu jingine hata maskini unawasaidia.

Huenda pia kama ni mwajiriwa selikarini au taasisi binafsi n.k unaona hautendewi haki katika malipo mbalimbali na hata mshahara wako pia.  Huenda wewe ni yatima au mjane halafu kuna haki zako ambazo zimetekwa na yule adui, huenda ni sehemu ya mirathi yenu, huenda kama wewe ni mjane basi stahili na mali ulizotafuta na mume wako zimechukuliwa na maisha ni magumu, unaona kama Mungu amekusahau na umeenda kwenye vyombo vya sheria lakini ufumbuzi bado haujapatikana nk.

Leo nina habari njema kwako, usidhani Mungu amekusahau, isipokuwa wewe ndio umemsahau, “Naam umemsahau”.  Mungu anachotaka ni kukupigania katika haki zako.  Mungu hafurahii unayoyapitia anataka upate haki zako zote.  Sasa ili uweze kupata haki zako ni lazima ujifunze na uanze kutoa dhabihu/sadaka za haki na za kumpendeza yeye.

 Yawezekana pia baraka/haki zako  zimetekwa na wachawi, wazinzi, na watu waapao kwa uongo na wenye kukuonea. Wewe huna uwezo wa kuwashinda hawa watu kwa nguvu zako, naam  Mungu anao uwezo huo. Nguvu za Mungu za kukupigania na kurejesha baraka/haki zako zimo katika wewe kutoa sadaka za haki na za kumpendeza yeye.  i.e Kadri unavyotoa sadaka za haki ndivyo unavyomkaribisha  Mungu kukupigania na mbili ndivyo unavyowasogeza adui zako mbele za Mungu awashughulikie. Unamfanya Mungu asistarehe juu ya adui zako.

Mungu anposema  wachawi uwe na hakika anazungumzia watu ambao wanalenga kuharibu uchumi na mafanikio yako kwa ujumla katika kila nyanja  biashara,kikazi,kilimo, kiroho,kihuduma nk, na  anaposema wazinzi ana maana mbili moja ni hawa wazinzi/ makahaba wa kawaida ambao yumkini unatafuta fedha yako kwa jitihada lakini inaishia kwa hao na pili ni wale waganga wa kienyeji na watumishi/manabii wa uongo, wanaosema Bwana amesema toa hiki na kile utabarikiwa, huku mioyoni mwao wakijua hayo ni mawazo yao na si Bwana. Kibiblia huu ni  uzinifu wa rohoni. Yaani wamezini katika roho zao kwa kujifanya wana nena neno la Bwana kumbe ni mawazo yao.

Na anaposema waapao kwa uongo maana yake anazungumzia waongo kwa ujumla wanaweza kuwa washirika wako kibiashara, kikazi, kihuduma n.k watu wanaotumia uongo kukuibia pesa yako, muda wako, maendeleo yako wanaokopa wasilipe n.k Je kwa nini hayo yote yanakukuta wewe? . Ni kwa sababu bado hujatoa dhabihu za haki na za kumpendeza Mungu, naam bado hujatoa.

Je, Kutoa dhabihu za haki na za kumpendeza Mungu ndio kukoje?

Ni kutoa kwa muda na uongozi wa Mungu matoleo yako mbalimbali.  Si watu wengi wenye nidhamu hii. Pesa na utajiri ambao Mungu anakupa mkononi mwako ni kwa ajili ya kuimarisha agano lake pia.  Yaani kuhakikisha makusudi yake hapa duniani yanafanikiwa kwa kutumia watu anaowabariki.  Kumbuka kufanikiwa kwa makusudi ya Mungu duniani kunategemea utiifu wa watu wake duniani.  Sasa hii ni pamoja na wewe kama mtu wa Mungu kutoa fedha yako kwa ajili kazi ya Mungu hapa duniani.

Suala sio kutoa tu, bali ni kutoa kwa kufuata muongozo wa Roho Mtakatifu ndani yako kwa maana ya wapi upeleke sadaka yako na pili kutoa kwa muda unaotakiwa kutoa kwa maana ya lini/wakati gani unatakiwa kutoa.

Jambo hili linaweza kuonekana gumu kwa jinsi ya kibinadamu, lakini huku ndiko kuongozwa na Roho Mtakatifu katika utoaji.  Kama ukiweka mahusiano yako na Roho Mtakatifu kuwa mazuri ni rahisi sana kuona uongozi wake juu ya matoleo yako.  Fahamu kwamba baraka za mtaoaji zimefungwa katika muda na eneo/mahali anapotoa.  Hii ina maana kila sadaka unayotoa ina baraka zake.  Sasa baraka hizo zinategemeana na namna unavyotoa kwa maana ya muda na eneo.

Kwa hiyo jifunze kutoa kwa uongozi wa Mungu, kabla hujatoa sadaka yako, jifunze kumuuliza Mungu je sadaka hii napeleka wapi na kwa muda gani?     Kwa kufanya hivyo utakuwa umetengeneza mazingira ya Mungu kufungua baraza zako kifedha/kiuchumi n.k. Kama huoni baraka za Mungu kifedha kwako huenda ni kwa sababu umezizuia kwa kutotoa dhabihu (sadaka) za haki na za kumpendeza Mungu. Neno kumpendeza Mungu linawakilisha kiasi/kiwango na muda. Maana yake toa kwa kiwango anachotaka yeye kwa ajili ya kazi yake na si kwa kiwango unachotaka wewe na pili toa kwa muda anaotaka yeye na si wewe. Kinachosisitizwa hapa pia ni uaminifu katika kutoa na si kumuibia Mungu (Malaki 3:8).

Ikumbukwe kwamba hapa sizungumzii sadaka yako ya kawida uliyopanga kutoa kanisani wakati wa Ibada.  Bali nazungumzia sadaka maalumu ambayo unataka kutoa kwa ajili ya wahitaji, wajane, yatima, zaka/fungu la kumi, kwenye huduma mbalimbali, watumishi nje ya eneo unaloabudu nk. Hii ni sadaka ambayo Mungu anakubariki na ndani yako kabisa unasikia msukumo wa kutoa kwa ajili ya kazi yake.  Naam naamini huwa kuna nyakati unakutana hali kama hii.

Sasa unapotaka kutoa sadaka ya aina hii ndipo unapopaswa kumuliza Mungu vizuri juu ya wapi, lini na kwa kiwango gani utoe. Japo wakati mwingine Mungu huwa anasema na mtu au watu moja kwa moja kwamba pesa hii peleka mahali fulani. Sasa wengi wanapinga kwa kuwa huenda kanisani mwao mafundisho waliyopewa wameambiwa sadaka yoyote inapaswa kutolewa kanisani tena wanapoabudu tu kitu ambacho Kibiblia si kweli.  

 Kwa hiyo ukikuta ndani yako msukumo wa Mungu unakuongoza kutoa eneo tofauti na lile ulilozoea usiogpe. Jambo la kufanya ni kuuliza tu vizuri kwa Mungu tena ili kuthibitisha maana huo ni utaratibu wa Mungu ili kufanikisha kazi yake , kuwatunza watumishi wake na wahitaji kupitia baraka anazoachilia kwa watu wake.

Ni vizuri nikatoa angalizo hili, kwenye masuala ya fedha makanisa mengi yameweka utaratibu wao na sheria zao kuhusu matoleo mbalimbali ikiwemo  sadaka na mafungu ya kumi. Na mara nyingi makanisa yanataka utaratibu huo ufuatwe na uheshimiwe. Zipo taratibu ambazo hakika hata Mungu zinambariki lakini pia zipo taratibu ambazo kweli si za Kibiblia. Kama wewe ni msomaji wa Biblia naamini bila shaka utakubaliana na kile nimeandika kwenye ujumbe huu kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Yesu alisema ninyi mkikaa katika neno langu mmekuwa wanafunzi wangu kwelilkweli, tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru  (Yohana 8 :31-32). Mfano kanisani ni mojawapo ya maeneo ambayo mtu anaweza kutoa fungu la kumi. Yapo na maeneo mengine mengi kama wahitaji, watumishi/watakatifu,  huduma mbalimbali nk. Kwa hiyo ni suala la kumsikiliza Mungu anakuongoza kutoa wapi na kwa kiwango gani. Unaweza pia kuwa na sadaka au fungu la kumi na Bwana akakuongoza kuligawa kwenye mafungu kadhaa tegemeana na maeneo na kiasi anachotaka upeleke.

 Siku hiyo 31/08/2008 Mungu alinifundisha kama nataka kuona mabadiliko kwenye masuala ya kifedha katika maisha yangu basi nifanye hayo niliyoandika hapa. Naam mwaka umepita tangu aliponijulisha hili na nimelifanyia kazi na kuthibitisha kuwa Mungu si mtu hata aseme uongo, maneno yake na ahadi zake ni kweli na amina.

 Maana haki zangu na baraka zangu ambazo Shetani aliziiba zimerejeshwa. Lakini nimegundua kwa kutendea kazi neno hili kumbe hata baraka zangu za mbele ambazo Bwana Mungu amekusudia nizipate nazo zinakuja kwa wakati na kwa kiwango kilichokusudia nizipate. Na hivyo nimejifunza kwamba kutoa sadaka kwa nidhamu ya eneo, muda na kiwango ni kinga dhidi ya baraka zangu za kiuchumi katika siku za mbele/zijazo.

 Lengo langu ni kufundisha kweli ya neno la Mungu ili watu wabadilike katika maisha yao ya kiuchumi. Naam anza sasa kwa kuwa na nidhamu katika matoleo yako. Hakika utaona baraka za Mungu katika kila nyanja ya maisha yako. Hata kama kuna haki/baraka zako ziliibiwa zitarejeshwa. Vitarejeshwa maana Mungu si mtu aseme uongo na  analiangalia neno lake apate kulitimiza.

Asomaye na afahamu.

JIONYESHE KUWA UMEKUBALIWA NA BWANA.

September 3, 2009

 Na :Sanga, P.S

 Waraka wa Septemba

Nawasalimu kwa jina la Bwanakatika mwezi huu wa Septemba, 2009. Katika mwezi huu nakuja na changamoto fupi, inayohusu mwenendo wetu katika Kristo kama vijana tuliokoka. Biblia katika 2Timotheo 2;15a Paulo alimwambia Timotheo akisema “jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Bwana

Kama unafuatilia mwenendo wa sasa wa watu nitumie wanaosema wameokoka utagundua kwamba matendo yao ni tofauti na ukiri wao. Ndugu zangu nimeshuhudia watu wengi sana wanaosema wameokoka lakini kupitia wao Mungu wetu na wokovu kwa ujumla umekuwa ukitukanwa na imepelekea watu wengine kusema hakuna kuokoka duniani. Hebu tujiulize kwa nini wafikie mahali waseme kauli hizi kama si kwa sababu ya matendo yetu kufanana na ya kwao.Je si kwa sababu wanaona tunapokea na kutoa rushwa kama wao,je si kwa sababu na sisi tunakunywa pombe,kutoa mimba, zinaa,uasherati nk. kama wao?

 Ndugu zangu wokovu ni mfumo wa maisha ambao una taratibu zake za kuishi Endapo ulifanya maamuzi ya kuokoka basi sharti uishi kwa mfumo wa wokovu. Naamini haukulazimishwa kuokoka lakini uliamua kwa hiari yako.Unapoamua kuokoka unatangaza vita katika ufalme wa shetani. Hii ni kwa kuwa awali ulikuwa haki yake. Kuokoka ni kuleta nuru ulimwenguni,  yaani ni kuwasha taa mahali penye giza.

   Mungu anasema mtakuwa watakatifu kama mimi nilivyo mtakatifu,Waebrania 12;14 anasema “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo UTAKATIFU kwa maana hakuna mtu atakaye muona Mungu asipokuwa nao”. Zaburi 16: 3 anasema “Watakatifu walioko duniani ndio walio bora, na hao ndio   ninao pendezwa nao”.Nimekupa hii mistari ili uone kuwa INAWEZEKANA mtu kuishi maisha ya utakatifu akiwa hapa duniani.

   Mungu anatutaka tuwe watakatifu kwa kuwa yeye ni mtakatifu. Mungu hawezi kutoa agizo ambalo anajua halitekelezeki. Yeye angekuwa mzinzi tulikuwa na haki ya kuwa wazinzi,walevi,wachawi nk, lakini kwa kuwa yeye ni mtakatifu LAZIMA na sisi watoto wake tuwe watakatifu.

    Paulo alimweleza Timotheo ajitahidi kujionyesha kuwa amekubaliwa na Bwana. Kwani alijua kwamba inawezekana kuishi maisha ya utakatifu tungalipo vijana. Paulo anataka ujana wetu usitukanwe kwa namna yoyote ile bali tuwe kielelezo. Ndugu zangu kama umeamua kuokoka lazima uazimie kuishi maisha ya mfumo wa wokovu. Kila kambi inapigania upande wake ufanikiwe, sasa kama upo kambi ya Yesu unatakiwa kuishi kama yeye anavyo taka uishi ili tuwe na ushindi dhidi ya kambi ya Shetani na mapepo yake. Suala ni kujizuia katika yale mambo ambayo hayampendezi Mungu wetu kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

 Pengine nitumie fursa hii pia kukualika wewe Mkristo ambaye unapenda na unataka kwenda mbinguni kwamba tafuta kitabu kilichoandikwa “Kweli mbingu ipo” cha Choo Thomas usome. Ni kitabu cha kweli na cha muhimu kwa kila Mkristo kukisoma. Nukuu mojawapo kwenye ile sura ya 24 ukurasa wa 211 inasema “ kuzaliwa mara ya pili kunamaanisha ni kuachana na mambo yasiyo ya Kimungu ambayo hapo awali uliyatamani na unachohitaji ni kumpendeza Mungu tu”. Zaidi unaweza kusoma mengi zaidi kuhusu kitabu hiki na mwandishi huyo kupitia anuani hii ya website yake http://www.choothomas.com

       Maadam tupo katka dunia hii vikwazo/changamoto za kututoa kwa  Yesu ni nyingi, lakini tunatakiwa kujua nafasi zetu kwenye ufalme wa Mungu, na kuishi maisha ya kifalme.Vitu vyote ni halali lakini kumbuka kwetu sisi tulio okoka si vyote vifaavyo. Kwa hiyo suala la kujizuia katika yale mambo ambayo hayaleti utukufu kwa Mungu wetu ni la LAZIMA. “Tunawajibika kuishi maisha matakatifu kwani inawezekana kwake yeye aaminiye

 

Neema ya Kristo iwe nawe.